Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, July 2, 2013

WEMA HAUOZI-28


‘Usiwasikilize hawa watu, wote lao moja, …..angalia ni kitu gani walichonifanyia mimi, waulize mke wangu yupo wapi,….walimchoma moto wakidai eti ni mchawi,…wakachoma na nyumba yangu..’ Sauti iliyotoka nyuma ya hawa watu, iliwafanya agande kwa muda kabla hawajageuka kuangalia ni nani huyu anayeongea. Wengine walishagundua ni sauti ya nani, lakini kwa uhakika zaidi iliwabidi wageuke.

‘Binti yangu nikuambie ukweli,  yote haya wamesababisha na hwa watu, waliovaa ngozi ya kondoo kumbe ni chui,…. na sasa wanakunyanyasa na mali yako, nia na lengo lao ni kutaka kukudhulumu…’ile sauti ikaendelea.

‘Nakuonya, ole wako uingie kwenye mtego wao,ukifanya tu wanavyotaka, ujue huna lako, nia na lengo lao ni moja, kutaka kukudhulumu, kwa visingizio vya mila na desturi,….ni nani mgeni wa hizo mila, sio kweli kuwa mila zetu zinawakandamiza akina mama, hata kwa kile chao walichokipata kwa jasho lao, …sio kweli, mimi sio mgeni wa hizo mila….usiwasikilize, na ukiwasikiliza, sio tu umepoteza jasho lako, lakini pia utakuwa umewadhulumu wengine, kwani watu kama hawa wameshaonja asli,  wataendelea kuwadhulumu wengine, tunataka hii dhuluma ikome,…’ wale watu wakawa wanamuangalia huyo msemaji huku wakiwa wamekodoa macho yao, kama hawaamini kumuona tena huyu mzee, na wale wasio na simile, wakaanza kunong’ona kimiya kimiya….

‘Huyu mtu katokea wapi?’ wa kwanza kunong’ona alikuwa ni mjumbe.

‘Mimi nilijua keshakufa…’akasema mzee mwingine.

‘Hawa ndio wanga wa hiki kijiji….hawafi haraka….’akasema mzee mwingine.
Na wakati huo huyo mzungumzaji akawa keshawakaribia, na bila kuwaogopa, akaja kusimama karibu nao, kama vile alikuwa miongoni wa hilo kundi la wageni, na kuwaangalia mmoja baada ya mwingine huku akisema;

‘Ongeeni kwa sauti, tuwasikie, nyie si ndio wababe wa hapa kijijini,….kwanini mnanong’ona nong’ona ongeeni kwa sauti kama kweli mnajiamini, si nyie mnaiona sheria ipo juu yenu mnafanya mnavyotaka, sasa yamewafika shingoni…au sio, mumejikunyata kama paka aliyelowana, hata aibu hamna…sasa, mnaanza kupita majumbani na kurubuni watu, haya niambieni  ni kitu gani mlichomfanya huyu binti yangu, na sasa mnakuja kuomba msamaha kwake?’ akauliza.

‘Hayakuhusu haya mzee mwenzangu, tunaomba usiingilie haya mambo, ni mambo yanayohitaji hekima, na tusipofanya hivi, kijiji hiki kitaharibika , ….’akasema mjumbe.

‘Mimi sio mzee mwenzako..futa hiyo kauli, kama ningelikuwa mzee mwenzako, siku ile ulipoamrisha vijana wako wanipiga hadi kutaka kuniua, ungenihurumia ukifahamu kuwa mimi ni mzee, lakini hukujali, lengo lako lilikuwa nipigwe hadi nife, ili haya yanayotokea, yaweze kufanikiwa….hujafanikiwa,..nakuambai ukweli hujafanikiwa, na hutafanikiwa…usitamke tena hilo neno eti mzee mwenzangu…. hawo ulio nao ndio wazee wenzako, na kundi lenu la muaji’akasema baba yangu huyo wa kufikia na watu wakaguna.

Kuna kundi la watu wasiotaka kisiwapite, walishaanza kujitokeza na kuskiliza ni nini kulikoni.

‘Chunga mdomo wako mzee mwenzetu, kauli yako itakuponza,….’akasema mzee mwingine.

‘Sijali lolote kwa sasa, mumebakiza nini kwangu, kama mnataka  kunimalizia haya waiteni hawo vijana wenu waje wanimalizie, maana nina uhakika, nyie hakuna mweney ubavu wa kupambana na mimi, kama yupo ajitokeze,…msione nachechemea nah ii fimbo mkafikiria mumeshanimaliza,…bado….kama mnabisha,  njooni mnimalizie,..nyie si ndio mnajifanya wababe wa hiki kijiji, njooni sasa mnimalizie, ….na msipofanya hivyo, nitahakikisha kundi lenu lote linawajibika kisheria,….’akasema baba huyo wa kufikia.

‘Mzee mwenzetu, tunashukuru umefika tulikuwa mbioni kuja kwako, nia na lengo letu ni kuweka maafikiano na matengamano ya hiki kijiji,nafahamu mengi yametokea na wengi wameumia , lakini ifike sehemu tuseme basi, imetosha,…..mimi kama kiongozi wa hiki kijiji, nimegundua kuwa kuna dalili za kinyongo, uadui na fitina katika kijiji chetu, sasa hiyo sio dalili nzuri, …tukae tuongee, tuyamalize kihekima kama wazee, tuonyeshe mfano’akasema mjumbe.

‘Hayo ndio maneno yako ya kinafiki…na yanajitokeza pale mabwana zako wanapojikuta hawana njia nyingine….mimi hunadanganyi kwa maneno yak o hayo, ….utawajibika na utaumbuka kiukweli…’akasema huyo mzee, na wote wakageuka kumwangalia huyo mzee kwa kauli yake hiyo, maana wote wanamuheshimu sana huyo kiongozi wa kijiji, na kusikia shutuma kama hizo zikielekezwa juju yake, wakahisi kuna jambo nzito sana, na wengine wakakimbia kuwaita watu wengine, na kundi likazidi kuongezeka.

‘Mjumbe leo kapatikana…’mmoja akawa ananong’ona kwa mwenzake.

‘Mwache apashwe, anafikiria wote ni watu wakudanganywa kwa maneno yake ya kisiasa, ….mimi simuoni huruma…’akasema mama mmoja.

‘Lakini kwani kafanya nini…?’ akauliza baba mmoja.

‘Sikiliza hayo maneno ya huyo mzee, unakumbuka walichomfanya huyo mzee, wamemuua mke wake kwa kumchoma moto, na kuchoma nyumba yake, na hawakutosheka na hilo, wakampiga mzee wa watu akimtetea huyo binti mjane….’akasema huyo mama.

‘Kwani hiyo nyumba ni ya nani, kwasababu nijuavyo, tatizo kubwa, ni kuwa hizo familia zinagombea urithi wa mali…baada ya mume wa huyo binto kufariki?’ akauliza jamaa mwingine.

‘Inasemakena, hiyi nyumba ilijengwa na pesa za huyo binti,…’akasema mama mmoja.

‘Nyie,…hiyo sio kweli, huyo binti alipata wapi pesa za kujenga nyumba kubwa kama hiyo….’akasema baba mwingine.

‘Alipata pesa baada ya kushinda ile michezo inayochezeshwa na makapuni ya simu…’akasema dada mmoja.

‘Hivi kweli mnayaamini hayo…wale ni wajanja tu, hawawezi kutoa pesa nyingi kwa watu,..wanpeana wenyewe kwa wenyewe…uliwahi kusikia mtu mwingine wa hapa kijijini kashinda,…hamna kitu kama hicho, akishindi labda awe na udugu na hawo wafanyakazi wa kampuni hizo, ili baadaye wagawane..huo ni uwongo….’akasema jamaa mmoja.

‘Ili uhakikishe kuwa sio uwongo, ..huyo binti alishinda, na ushahidi umeshaonyeshwa mahakamani, sasa hivi imebakia kutoa hukumu, lakini ujuavyo, mnyinge hana haki, tarehe zinaanza kupigwa, ili hata huo ushahidi uyeyuke….’akasema mama mmoja.

‘Hizo ni hisia zako, kama ushahidi umeshafikishwa mahakamani, hakuna ujanaj hapo, ..hata wapige tarehe vipi, jamii, imeshathibitisha hilo, haki ya huyo mwanamke haitapotea, na sisi wanawake, tupo nyuma yake, ikitokea kubatilishwa…wakaharibu huo ushahidi, tutaandamana…’akasema mwanamke mmoja.

‘Hayo unaongea tu, …siku ikifika utakuwa umejificha chumbani kwako, kama hukuwepo, nyie ndio waoga wakutupwa, mangapi mnafanyiwa, lakini hamlalamiki, japo tu kulalamika…usitudanganye hapo….’akasema jamaa mmoja.

‘Hebu tulieni tusikie nini mjumbe anapashwa…’akasema jamaa mmoja akitaka kusikia ni nini kimetokea.

********

‘Mimi nimekuwa mnafiki mzee mwenzangu…?’ mjumbe akawa anamuuliza huyo mzee aliyekuwa akiongea kwa sauti kama anahutubia jamii, na alijitahidi kuongea kwa sauti ya chini ili watu wasisikie. Mzee huyu alikuwa anafahamu jinsi gani ya kuongea na watu kutegemeana na hali ilivyo, na ndio maana wakamchagua kiongozi wa kijiji, lakini sasa …

‘Ndio wewe ni mnafiki mkubwa,..wewe ni ndumila kuwili, …ukifika kwa hawo unaowaona ni matajiri, unasema hivi, ukija kwetu, unatudanganya hivi….mimi wewe  nimeshakufahamu fika,…hasa siku ile ulipokuja hapa na vijana wako na kuwaamrisha wanipiga karibu ya kuniua, imefuatilia mambo yako, na hatimaye nimekugundua, wewe ni mnafiki,….mnzandiki mkubwa, muongozaji wa kundi la wauawaji, na nitahakikisha unakwenda jela…’akasema huyo mzee, na wale wazee wengine aliongozana naye wakainamisha vichwa vya chini kama vile wanaona aibu.

‘Hapa hapakaliki mjumbe, fanya jambo, tuondoke, vinginevyo, watu watajazana hapa na mwishowe ataropoka mengi na utashindwa la kufanya….’akasema mzee mmoja.

‘Tunakushukuru mzee mwenzetu, lakini tunakuomba utupishe kwani tuna maongezi na huyu binti, kwa ajili ya usalama wa hiki kijiji….’akasema mjumbe akimsogelea huyo mzee, na huyo mzee, akamnyoshea fimbo kuwa asimkaribie.

‘Naomba usinikaribie, hasira nilizo nazo juu yako, hazipimiki…kwanza siondoki hapa, mpaka nyie muondoke, mtambue kuwa mimi ni mzazi wake, aliyenitambua hivyo,…na  kwa vile ninajau ni nini lengo lenu, la kutaka kumrubu huyu binti , sitaondoka kamwe, …nyie hamna jipa, nia yenu ni kumshawishi, huyu binti ili afute kesi, hilo la kwanza, lakini kubwa lao, ni kuwa mnataka akamtete huyo mnayemuita jemedari wenu, wakudhulumu hata mali ya mayatima….’akasema huku akitembea kuelekea pale aliposimama huyo binti.

‘Huyu binti, hatafanya hivyo kamwe, na kifanya hivyo, basi mimi sio baba yake tena….’akasema huyo mzee, na wale wazee  wakageuka wakiangaliana na mmoja akamwambia mjumbe.

‘Tuondokeni….hapa, hapa hapakaliki tena, hatutaweza kuongea lolote …..’wakasema na kweli wakaanza kuondoka,na baadhi ya watu wakaanza kuzomea.

Walipoondoka  akabakia yule mwanasheria akiwa kainama hakutaka kusema neno, akatulia hadi pale mzee aliposema.

‘Na wewe unasubiri nini?’ akauliza huyo mzee

‘Mimi nimekuja kwa mengine….’akasema akisita.

‘Hamna linguine hapa, wewe ndiye uliyekutana na hawo wazee mkapanga mje kumbembeleza huyu binti, ili akaseme mahakamani kuwa kaka yako hakufanya hilo aliloshitakiwa nalo,….kweli wewe unataka kupindisha sheri, eti, ni kweli huyo binti hakutaka kunyongwa na huyo kaka yako..?’ akawa kama anauliza.

‘Karibuni ndani, nashkuru baba, umefika na kuniokoa maana nilishaingiwa na wasiwasi sikujua kabisa nitakuja kusema nini, maana sikuwa nimetambua huo ujio wao na lengo lao, naombe tusiongelee hapa nje, maana watu wanatuskiliza, na wengine hawana nie njema…..’nikasema kukatisha malumbano mengine kati yam zee na huyo mwanasheria.

‘Sawa, lakini huyu mtu aondoke…mimi sijamuamini kamwe…kama anashindwa kukutetea wewe na mali yako, halafu anajfanay kuwa yeye ndiye aliyeachiwa kukurithi wewe…kweli ni mtu huyu..’akasema akimnyoshea huyo mwanasheria fimbo,na huyo mwanasheria akarudi nyuma kuikwepa hiyo fimbo.

‘Mzee samahani huko unakwenda mbali…’akasema huyo mwanasheria.

‘Haya sema ni kitu gani kimekuleta hapa,?’ akauliza huyo mzee

‘Nilikuwa na mazungumzo na shemeji…’akasema.

‘Unalotaka kuzungumza, zungumza mbele yangu, kwani unataka kumuoa, unataka kumtongoza, au ni maswala haya haya ya huyo kaka yako?’ akauliza huyo mzee.

‘Ni maswala hayo hayo ya kaka mzee wangu…’akasema huyo mwanasheria kwa unyenyekevu.

‘Kama ni hayo, ongea tuone jinsi gani tutakusaidia, sina neno na wewe kijana, usiogope, hapa ilibidi nipandishe hasira maana nina usongo na hawa watu,…na wewe kama utakuwa upande wao, ujue, umepotea…na sijui kwanini familia yenu imebadilika kiasi hicho,…kaka yako yupo pabaya, ….’akasema huyo mzee.

‘Lakini mzee….’akataka kujitetea huyo mwanasheria, na huyo mzee, akawa kama hakusikia huko kujitetea akaendelea kuongea;

‘Hawa watu nawafutilia kila hatua, na kikao chao cha kuja hapo  kilifanyika mapema kabla hata ya huyu kijana hajakwenda kuonana na hawo wazee, walikuwa na ajenda moja, ya kutaka kuhakikisha wanaiharibu hiyo kesi yako…’akasema akimwangalia binti, na baadaye aakmgeukia huyo mwanasheria na kusema;

‘Na pia kujaribu kujifanya wanamtetea huyo kaka yako…na hivyo vikao vilifanyika kwanza kwa uficho na abadaye kikao cha mwisho ambayo na wewe ulikuwepo kilifanyika kwa mjumbe, yote hayo mimi nayafahamu….wewe ulipofika kuwapa hiyo taarifa ya kukamatwa kwa kaka yako, wenzako walishajua na walikuwa kwenye mikakati ya kwenda kumtetea, ha hata kumuwekea dhamana…’akasema huyo mzee.
‘Sasa mzee, utatusaidiaje maana yote haya ni hasira za kaka, hataki kutuliza hasira zake…sizani kama ni mbaya kiasi hicho, cha kuhusika kwenye mauaji yaliyowahi kutokea haap kijijini.’akasema mwanasheria.

‘Kaka yako ana hasira na kuburi, kama huheshimu wazee wa wenzako, ukaona wewe ndiwe mwenye mamlaka kwenye familia na unataka mamlka hayo yavuke mpaka hadi kwa familai za wenzako, unafikiria mwisho wake utakuwaje…hebu niambie wewe uliyesomea sheria, ni mamlka gani aliyopewa kaka yako, ya kuingilia familia za wenzake?’ akaulizwa na kabla hajajibiwa huyo mzee akaendelea kuongea’

‘Ufahamu kijana, kila familia, kila jamii ina utaratibu wake, huwezi ukalazimisha utaratibu wa familia fulani ukawa sawa na familia yako eti kwasabbau wewe ni kiongozi wa familia yako, kama wewe ni kiongozi wa famila yako na mna utaratibu wenu, basi heshimuni na taratibu za familia nyingine…ni muhimu sana hilo, muwe makini sana, msijifanye kuwa eti nyie mna taraibu nzuri, mna kiongozi, mpo pamoja, na mnaonyesha mfano, kwahiyo kila family hapa iwe ianwasikiliza nyie….mnakosea.’akasema mzee.

‘Mimi nakubaliana na wewe mzee, lakini tukumbuke kuwa mawazo, akili, na utashi wa maamuzi unatofautiana kati ya mtu na mtu, wengine wameshajijengea  hali fulani kuwa wao wakati wote wapo sahihi, na kwa vile ni viongozi wa jamii zao, na wanajua kuwa wamepewa mamlaka na jamii hizo, wanafanya kila wawezavyo kulinda kile walichokabidhiwa….kwao masilahi ya familia zao wanayaweka mbele kuliko kitu chochote….’akasema.

‘Mimi sikukatilii kijana….ni sahihi kwa mtizamo huo, lakini kama kweli wanavyofanya  ni sahihi na kwa haki , kama ni sahihi na haki, isingelikuwa ni neno,hakuna ambaye angeliwanyoshea vidole, lakini sivyo hivyo, wenzenu wana ajenda ya siri…..ndio maana nikamuita mjumbe wetu ni mnafiki, maana yeye kama mjumbe ana takiwa kufuata sheria, lakini sheria kwake ina sura mbili, wakikosa wakubwa, au watu wake, hawo watatafutiwa sababu za kusamehewa,…utasikia lugha kama bahati mbaya,…kakosea tu…. Tuongee, tuitishe vikao, kamati zitaundwa eti kufuatilia,…ujanja ujanja tu….

'Lakini wakikosa wanyonge watu wa upande wa kushoto kwao, wanasakamwa na kwanza wanachokifanya wao ni kuwaita hawo wanyonge majina mbaya, walalahoi, waongo, wafitinashaji, wachochezi,…siasa kali,…sijui nini kali….ilimradi waonekane hawo wanyonge ni wabaya…tufika kweli kwa utaratibu huo…?’

‘Lakini mzee, kukosea kupo, na kusameheana kupo, tukiishi kwa kuadhibiana kwa kila kosa, huoni mwisho wa siku watu wote watakuwa na majeraha kwenye mioyo yao, na kinyongo kitakuwa hakiondoki kwa vile kila mmoja atataka mawnezake afanyiwe hivyo hivyo….

‘Mzee mimi ninafikiri, wakati mwingine inabidi tufika mahali tusema sasa basi tukae tuongee tuelewane, na tusameheane, na wale waliokosewa, wataangaliwa jinsi gani ya kutibiwa majeraha yao….mimi mwenyewe imeniuma sana kusikia hayo uliyofanyiwa, sikujua kuwa ilifikia hatua hii, hayo nilifichwa kabisa,…mimi kama mwanasheria wa familia nisingelikubaliana na hilo…na jingine ni kuwa kama kuna wakosaji, watawajibika kinamna ambayo itakubalika, bila na wao kuumizwa zaidi,…’akasema mwanasheria.

‘Tatizo lako unaongea hivyo kwa vile unamtetea kaka yako, kama angalikuwa ni mtu mwingine, nina uhakika ungelisema sheria kali itumike dhidi yake, ili iwe fundisho kwa wengine ni kweli si kweli…, si ndivyo mnavyopenda kusema mkiwa mahakamani, sasa wakati umefika hawo watu waliokosa na kusababisha kijiji hiki kiwe hakikaliki kwa amani, waadhibiwe ili iwe fundisho kwa wengine….’akasema mzee.

‘Sio hivyo mzee….nazungumza hivyo kwa vile namfahamu vyema kaka yangu. Kaka ni mtu mwema sana, na kinachomponza ni kuwa yeye kama kiongozi, anataka kila lililosemwa au kuwepo kwenye mila, lifuatwe kama lilivyo, na atajitahidi kuhakikisha kila mwanafamilia analindiwa haki zake kwa taratibu za kimila na desturi,…, na bila kujali kuwa ndani ya jamii kuna wanaojificha wenye maovu, …’akasema mwanasheria huku akiwa kainama chini.

‘Mzee, ninafahamu kuwa kuna …kwa mfano hawa kina mama walioolewa ndani ya familia, wenye haki zao,…ambazo wamekuja nazo , ni kweli kuna wengine walijaliwa wakaja na mali zao, hizo huwezi kuzilamisha kuwa ni mali ya familia yote, labda mwenyewe apende kuwa hivyo….na vitu kama hivyo,…lakini bay zaidi kaka yupo tayari kuwabeba  hata wakosaji ndani ya familia, kwa vile ni mwenzetu,….mwisho wa siku yeye ndio anaonekana kuwa ni kiongozi wa wahalifu….’akasema.

‘Kijana, sikiliza, hayo unayoongea mimi nayaelewa sana,…na mimi ninamfahamu sana kaka yako kuliko unavyomfahamu wewe…kaka yako, kinachomuharibu ni kuwa kajiunga na kundi hilo la watu wanajifanya wao ni mashuhuri wa hiki kijiji, waheshimiwa, mabwana wakubwa….’akatulia kuonyesha uchungu .

‘Kijana mimi nimeapa kuwa nitakula nao sahani moja, wakitaka kuniua waniue, sijali tena. Kundi hilo, ndilo limewaua wazee,…wewe sijui kama unafahamu hilo, ila hilo limetokea hapa kijijini na limetia doa kubwa sana hapa kwetu, wazee wasio na hatia wameuliwa, kwa shutuma, imani za kinafiki, eti wazee hawo ni wachawi,….hivi kuwa mzee ni kosa, watu wameshahu kabisa kuwa isingelikwua ni hawo wazee wao wasingelikuwepo hapa….

'Jamani vijana , mnataka nini, ....mnasahau kabisa mlipotoka, au niambieni mnataka dunia hii iende wapi,…kama mnawaua wazee...kwani nyie mtaendelea kuwa vijana milele,kesho na kesho  kutwa utelekea huko huko....hiyo ni laana, ndio maana baraza zinapotea hakuna neema tena….kwa mtindo huo nawaambia kamwe hamtafanikiwa… sijui kama wewe hilo umejaribu kulifuatilia, au la…kama bado utambue hilo…lipo na kuna watu wanakinyongo na hilo…msipolitatua hilo, bado kuna kisasi moyoni…’akasema huku akijinyosha mgongo.

‘Angalia walivyonifanya mimi, karibu waniue, kisa kwa vile natetea haki za huyu binti, na kama isingelikuwa huyu binti kunisaidia matibabu, na kuniwekea walinzi kule hospitalini sasa hivi mngelikuwa mananiita marehemu…nap engine kunivika makosa kuwa mimi ni mmoja wa wachawi wa kijiji, kama walivyomvika mke wangu makosa ambayo hana…hana kabisa, mungu mwenyewe ndiye anajua.’akatulia kidogo huku akikunja uso kwa huzuni.

‘Mzee….nakuomba unisikilize kidogo..’akasema huyo mwanasheria, lakini mzee hakumsikiliza akaendelea kuongea.

‘Katika hilo kundi kuna wazee wanajiona kuwa wao ni watu wa mila na desturi, wanafahamu mila zote na wanataka zifuatwe, …wapo wazee wanajiita wao ni watabiri, waanjimui,..sijui watu gani, nashindwa hata kutaja majina yao…eti wao wanawafahamu wachawi, …kwahiyo atakayebainika kuwa ana dalili hizo, anatungiwa uwongo, hadi anauwawa…’akatulia.

‘Je ni nani kweli anafahamu kuwa huyu ni mchawi, au yule sio mchawi, ?’ akauliza.

‘Mara nyingi wanaofanya hivyo kutabiri, ni waganga wa kienyeji…’akasema mwanasheria.

‘Sasa humo kwenye kundi lao, kuna waganga wa kienyeji wanaotambulikana, na hawo wanalindwa hata wakikosea hawachukuliwi hatua yoyote…mwenzao mmoja katoweka kiajabu, hajulikani wapi alipo, na huyo ndiye alikuwa kinara wao…lakini hata hivyo, kuna watu wapo nyuma ya hilo kundi, wafadhili wakuu wa hayo yote, wanaolinda huo uchafu, na wana majukumu ya serikali….sasa bila sisi wananchi kusimama bega kwa bega na kulalamika, …hata kuwachukuli hatua hatutaweza kumaliza huu uozo hapa kwenye kijiji….’akasema.

‘Sawa mzee nimekuelewa….’akasema mwanasheria huku akiangalia saa, lakini mzee hakumpa nafasi akaendelea kuongea.

‘Yaliyotoea kwa mke wangu, nisingelipenda tena yajirudie, na ….ndio maana nimeipeleka hiyo kesi mahakamani, kama kwei ipo sheria kwa wanyonge, basi, …..hawa watu lazima waadhibiwe.. ili iwe fundisho kwa wengine….ndio maana nasema kama kweli huyu binti ananijali, na kujali yaliyotokea kwa mke wangu, basi asije akarubuniwa na nyie na kundi lenu, akakubali kwenda kumtetea ndugu yako…’akageuka kumwangalia binti yake.

‘Mzee nakuomba…taafdhali, usimkataze shemeji yangu kwa hilo,nakuomba wanza hebu nipe nafasi niongee kidogo, maana ninawahi …kuhusu maswala ya kaka, na tulikuwa tunataka tuondoke na shemeji..’mwanasheria akaanza kujitetea huku akimwangalia huyo binti, kwa wakati mmoja na huku akimwangalai huyo mzee.

‘Hilo halitawezekana, binti yangu haendi popote…….’akasema mzee na kwenda kusimama mlangoni,
Yule mwanasheria akamwangalai shemeji yake, halafu akamwangalia huyo mzee…

NB: Je ni hayo tu, tutaonana sehemu ijayo mungu akijalia.

WAZO LA LEO: Maafikiano ya kweli yatafanikiwa kwanza kwa kuangalia pande zote mbili, ili kuleta mlinganyo wa sawa sawa, ili kujaribu kutibu majeraha ya waliokosewa. Usuluhishi wa kweli hautafanikiwa kama waliojeruhiwa na kuonewa, hawajatambulikana na kutetewa haki zao. Tuwape wenye haki zao haki wanazostahiki kupata, ili kutokuleta manung’uniko, na maumivu ya chini kwa chini.
  
Ni mimi: emu-three

2 comments :

Unknown said...

kweli mwisho wa ubaya ni aibu, na sasa wamekaribia kujitambua wanako kwenda. nzuri sana

Unknown said...

Jamani,jamani huyu dada asikubali kwani kasahau aliyofanyiwa EE mungu hembu muongoze huyu mja wako. Hongera sana ndugu yng kwn kila cku twapata fundisho jipya.