Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, June 4, 2013

WEMA HAUOZI-16Baada ya kumaliza maelezo yangu, ya awali nikaingia kwenye hoja yangu, ambayo nilianzia pale tulipofika Dar, na mume wangu alipogundua kuwa kaibiwa pesa zote alizokuwa nazo, na jinsi gani tulivyohangaika na maisha magumu, maana hatukuwa na pesa, tukaanza kuomba vibarua huku na kule na tulipopata pesa kidogo, tukaanza kufanya biashara ndogo ndogo za kuuza karanga, na ubuyu…

‘Kama hizo pesa mnazodai zingelikuwepo, kwanini tungeishi maisha hayo ya taabu, ….sio maisha rahisi kama mnavyohisi, ….’nikawaambia
Nikaendelea kuwaelezea jinsi tulivyofikia hatua ya kufunga ndoa, na tukio zima la kukamatwa kwa mume wangu, ambalo lilitokea pindi tu tulipotoka kufunga ndoa, nikawaelezea jinsi gani alivyoniacha katika hali ngumu…..

‘Hata hivyo sikukata tamaa,nikaanza kuhangaika nikiwa peke yangu, kwa kuendeleza zile biashara nilizokuwa nikizifanya alipokuwepo mume wangu. Nilihangaika, na kukutana na mitihani mingi, ikiwemo ya kupambana na wanaume walitoka kunibaka…..yalikuwa maisha ya shida …taabu na hatari’nikaendelea kuwahadithia, na watu walikuwa kimiya, na wengi waliona kama kisa cha kufikirika.

‘Kuna muda nilifanikiwa nikaweza kupata pesa za kuniwezesha kupata nauli ya kurejea nyumbani, na siku hiyo nikajiandaa kabisa kuwa kesho yake naondoka, wezi wakaniingilia na kuzichukua pesa zote, nikabakia mikono mitupu,….hebu fikirieni hiyo, pesa yenyewe ya kuingiliwa na majambazi ilikuwa pesa gani, na kama hiyo pesa ingelikuwepo, kweli majambazi wangeiacha,….walitafuta na kukuta hizo pesa kidogo wakaondoka zao….hapo ina maana nilitakiwa kuanza maisha upya, na je ningelianzaje wakati pesa zote wameshazichukua…

‘Haya ninayowahadithia ndio maisha niliyokutana nayo Dar, sio rahisi kama watu mnavyokisia kuwa ukifika pale utaweza kupata kazi kirahisi na kujiwezesha,..sio rahisi kihivyo, maana hata kazi za ufanyakazi wa  ndani wa kulea watoto na kuosha vyombo….haipatikani kirahisi, japokuwa mnasikia kila sikuwa watu wanakuja huku kuulizia wafanyakazi wa ndani, inakuwa vigumu ukiwepo pale, kwani watakuaminije kuwa wewe sio hawo matapeli wa mjini..’nikainua uso kuwaangalia, na wote walikuwa wamenikodolea macho wakisikiliza maelezo yangu.

‘Kwahiyo mimi pale nikaanzia na biashara ndogo ya zile karanga zilizobakia, …bahati nzuri walipokosa pesa , hawakuhangaika kuchukua karanga kidogo nilizokuwa nazo na ubuyu, na ndizo hizo nilianza nazo,japokuwa zilikuwa kidogo sana, nahazingeliweza kunisaidia kitu, ukumbuke nilikuwa naishi kwenye nyumba ya kupanga, chumba …na siku za kulipia kodi zilikaribia, na mwenye nyumba akija, kama huna kodi unaondoka, ….anaingiza mtu mwingine siku hiyo hiyo…

‘Ili niishi hapo, ilibidi kwanza nihangaike ipate hiyo kodi, kwahiyo nikaanza kuhangaika mitaani, kuuza hizo karanga, na kujichanganya kwa mama Ntilie, ambao waliweza kunipa kazi ya usafi, na hata kubeba mizigo ambayo niliweza kuibeba, ya wale wanaonunua vitu sokoni, na wanahitajia kubebewa hadi kwenye magari yao au hata nyumbani kwao….’nikatulia kidogo.

‘Kwakweli ilikuwa kazi nzito, na nilikuwa nachoka kupita maelezio, ilifikia muda sasa, nikaona sitaweza …nikaanza kuingiwa na tamaa, kuwa labda na mimi nijiingize kwenye biashara haramu za ukahaba, lakini moyo wangu ulikataa kata kata…

‘Nikajiuliza nitawezaje kuishi, nitapata wapi kodi ya nyumba, na siku zinakaribia za kulipa hiyo kodi, nikasema nitajitahidi hivyo hivyo, na sitakata tamaa, nikadunduliza, hadi siku ya kulipa kodi ilipofikia nikawa na kiasi hicho taslimu…..

Siku hiyo niliyoweza kulipia kodi ya mwezi mmoja, na kubakiwa bila hata senti moja ya akiba zaidi ya karanga na ubuyu ambazo nilizinuunua kwa ajili ya kuuza kesho yake, nilikuwa sina hata pesa ya kununulia maji ya kunywa na sikujua nitakula nini…san asana nilitafuta punje chache za karanga, ilimradi siku iweze kwenda….na hutaamini, kuna muda na mimi nilichakura majalalani , ili angalau nipata masalia….na hili nililifanya wakati natafuta chupa za plastiki, kwa ajili ya kuuza. Nilichopata, nilikwenda kukipasha moto, …siku ikaenda…’nikasema na nilipogeuka kumwangalia mama yangu nikamuona machozi yanatiririka usoni.

‘Siku hiyo baada ya kulipa kodi na kubakiwa bila senti moja, nilijilaumu kwanini ile pesa nisingeliitumia kama nauli….lakini moyoni,nilijiuliza , kama ningeliitumia kama nauli na kurejea huku, bado ningelikuwa sina kitu, na sikutaka kuja kuwasumbua wazazi wangu ,…na mtoto wangu nitamlea vipi, nikaona kilicho bora nikuhangaika, nipate chochote, angalau pesa ya maziwa …..’hapo nikatulia.

‘Nikajipa moyo kuwa mimi kama mzazi, sina jinsi, lazima nihangaike,….ili nipate pesa ya kumlea mwanangu, na ikibidi niweze kufuatilia kesi ya mume wangu, kwani nilijua nina dhima kwake. Kwakeli siku ile sitaweza kuisahau maishani….’nikakohoa kulainisha koo.

‘Siku ambayo nilianza kuhisi hali ilivyo kuwa ngumu mbele yangu, na kweli hapo nilianza kuona umuhimu wa kuwa na mwenzangu, yeye alikuwa ni mwanaume na ilikuwa rahisi kwake kujichanganya kwenye kazi ngumu, na kupambana na wanaume wenzake, na akitoka hapo sio haba, tuliweza kupata visenti kidogo tukaongezea mtaji wetu. Lakini hakuwepo tena, ..na sikuwa an ndugu anayenifahamu, majirani zangu, ambao ni wapangaji wenzangu, walikuwa na shughuli zao…na maisha yao hayakuwa tofauti nay a kwangu….hapo nilimkumbuka sana mume wangu na kuanza hata kulia ….

‘Lakini nikajiuliza hata nikikesha kwa kulia, itasaidia nini, cha muhimu ni kujituma, ili nipate nauli,kwahiyo hapo lengo likawa kutafuta nauli, ikifikia tu, naondoka, ….’nikajipa moyo

`Usiku ule ulikuwa mgumu sana kwangu sikuweza kulala, nikaona muda huo baada ya kumaliza kuzifunga zile karanga na ubuyu, niutumie pia kumuomba mungu…siku zote nilikuwa namuomba mungu, lakini siku ile ilikuwa tofauti,….niliomba nikijua kuwa sasa hali yangu imefikia kubaya….’hapo nikajikuta machozi yakinilenga lenga, nikiikumbuka hiyo siku.

‘ Kweli sikujua muda gani usingizi ulinishika, maana nilikuwa nikimuomba mungu kwa hali niliyoifahamu, na nilikumbuka wazazi wangu walivyonifundisha, wazazi wangu wa kunizaa, na wazazi wangu wa kufikia ambao siku zote walikuwa wakiniambia kuwa, kumbuka kumuomba mungu wako, kwanza kwa kutubu madhambi yako, maana kila siku sisi ni watendani wa mdhambi, mengine hayakwepeki,….na waliniambia kuwa kila ikifika usiku omba msamaha kwa yale mabaya uliyoyafanya, halfu baadaye unaomba kwa kuyakumbuka mema yote uliyoyafanya…hayo mema, ndio yatakupa baraka….

‘Nakumbuka sana wazazi wangu walivyoniambia kuwa yale mema uliyoyafanya yatakuwa ndio kiyoo chako cha kukumulikia njia ya mfanikio,..ndio maana inatakiwa katika maisha yako kujitahidi kutenda mema, na ujibidishe kuytafuta matendo mema, hata ikibidi kujitolea, ….ndio maana inapotokea jambo la kufanya usitegee, uwe wa kwanza kujituma, kujitolea, ili uweza kuyapata hayo mema..

‘Kujituma kwa kutenda mema hakuji hivihivi, hii tabia huanzia toka utotoni, na hili nisingelifanya na kufanikiwa kama nisingelipata msingi mwema kutoka kwa wazazi wangu wa kunizaa na huyo wa kufikia ambaye nashangaa kusikia kuwa mnamuona kama mtu mwema mbaya, …..mimi kama ndugu yenu nawahakikishia kuwa huyo mzee ni mtu mwema sana na muadilifu wa kweli,…na kama mngelimsikiliza msingalifika hapo na kusigishana na yeye, nasikia kuwa mumefikia hadi kupigana na yeye, na sijui hali yake kwa hivi sasa  ipoje….masikini baba wa watu…’nikasema na kushika shavu.

‘Ndugu zanguni, ninachotaka kuwambia ni kuwa, isingelikuwa hawa wazazi kujitolea kunilea katika maadili mema, kunifundisha kujituma, nisingeliweza kuishi maisha maisha niliyokutana nayo Dar, huenda ningejiingiza kwenye biashara ya ukahaba, maana nilifikia hatua siku inapita bila kuonja kitu zaidi ya kutafuta tembe chache za karanga, huku natembea umbali mrefu kutafuta wateja wa karanga,…wengine wananunua, wengine wananiibia wengine wananisimanga,…lakini yote hayo hayakunikatisha tamaa….’nilirejea kuwaelezea maelezo hayo kwa msisitizo.


`Siku nyingine nilikuwa nikununua ndizi Kariakoo za kuiva, kwa wale wanaouza nje, na mimi natembea mitaani nikiwa nimeongeza faida yangu, …sikuchagua biashara tena, iwe ndizi au embe …ilimradi napaat faida kidogo…

 ‘Mola hamtupi mja wake, maombi yangu yalikubaliwa, na sikuamini siku nilipopigiwa simu kuwa nimeshinda katika moja ya promosheni za matangazo ya kampuni za simu, …na waliponitajia hicho kiwango nilichoshinda niliona kama wananitania, lakini kweli nilishinda na kukabidhiwa kitita cha pesa,…na ndicho hicho kilichoniwezesha kuja huku na kujenga nyumba na hilo duka …..’hapo nikasikia watu wakiguna.

‘Kwahiyo nduguzanguni samahanini sana kwa maelezo hayo marefu, lakini nia na lengo langu ni-ili muwe na ufahamu kwa kina, …..najua wengine hawaamini haya, hata mimi sikuwa naamini kuwa mtu anaweza kushinda na kulipwa pesa zote hizo. Ni bahati, na bahati ilikuwa yangu siku ile, na yote haya yalitokea kwa kudra za mungu…’nikatulia na nilimuona mwenyekiti akitabasamu, tabasamu la dharau, na nikamuona akiinuka na kumsogelea yule mdogo wake mwanasheria na kumnobg’oneza kitu

Mimi nikawa nimetulia sikuwa na la kuongea zaidi, nikasubiri, mwenyekiti atasema nini, na baada ya wao kuteta kwa muda, nikamuona mwenyekiti akisimama, na kuelekea pale alipokuwa kakaa mzee, yaani baba yao mdogo, yule aliyeonga mwanzoni, na wakateta kwa muda, halafu akareeja pale alipokuwa amekaa , akakohoa;

‘Samahanini kidogo kwa kuwapotezea muda, nilikuwa nateta kidogo…shemeji sijui kama umemaliza maelezo yao, au bado….naona umenyamza, endelea, tunakusikiliza ..mimi nilikuwa nateta na wazangu, maana kuna mambo mengine unaogoa kuyaongea mpaka usikie wenzako wanasema nini, hekima ina masharti yake, usijione wewe ni kiongozi, ukazani kila utakaloongea lina hekima….na kwa vile nina wenzangu, nilihitajia hekima zao kidogo…’ Akasema na kuniangaliai na mimi nilikuwa nimetulia kimiya.
‘Natumai  umemaliza ….’akasema mwenyekiti, na mimi nikasema kwa sauti ya kinyonge ;

‘Nimemaliza ndugu zangu, nawasikiliza nyie mtasemaje kuhusiana na hilo kosa lililofanyika, siwezi kuwalaumu, maana sio jambo rahisi kukubalika mpaka ujione umeshinda,…..ni kweli nilishinda na nikazipata hizo pesa , na ndizo zilizojenga hiyo nyumba na duka…..natumai mumenielewa, ….na kama kosa lilifanyika, basi tulirekebishe, …..’nikasema na kutulia.

‘Sawa shemeji tumekusikia na ombi lako limefika mbele ya kikao, na mimi kama mwenyekiti siwezi nikasema lolote kwasasa, mimi ni kama kiongozi wa kusimamia hiki kikao, na ni vyema kila mmoja akachangia kuhusiana na hoja hii, na kabla sijamkaribisha mzee wetu atoe ufafanuzi kidogo, ningeliomba, mwanasheria wetu akuhoji kidogo, kutokana na maelezi yako hayo…’akasema mwenyekiti na yule shemeji, mwanasheria, akasimama …

‘Mimi ni kijana naomba nisimame, na kutokana na nilivyozoea huko mahakamani, huwa tukiongea tunakuwa tumesimama, …’akasema na baadaye akanigeukia na kuniangalia usoni, akatabasamu na kugeuka kumwangalia mwenyekiti….

‘Ndugu mwenyekiti, ….kwanza nilitaka kujua,hili ni ombi toka kwa ndugu yetu, mwanafamilia, au ni lalamiko?’ akauliza huku akishika kichwa.

‘Naomba umuulize muhusika mwenyewe..’akasema mwenyekiti.

‘Ninalalamika..kuwa nimetendewa isivyo haki…sio ombi, huwezi kuomba haki yako’nikasema kwa sauti.

‘Haya kama ni hivyo,naomba nikuulize swali moja, ili kuweza kuweka maelezo yako sawa, je ulipopewa hizo pesa, ulitangazwa kwenye vyombo vya habari, maana mimi nijuavyo, hawa watu wakitoa mashandano kama hayo wanayoyaita promosheni, wanatangaza kwenye vyombo vya habari, …’akasema na kutoa ufafanuzi.

‘Ni kweli waliniambia ndivyo kuwa watanikabidhi hizo pesa kwenye shughuli waliyoiandaa, lakini mimi niliwaomba, kutokana na dharura niliyo nayo, kuwa nahitajika kuja kusimamia kesi ya mume wangu, na nikawaambia kuwa kuna wagonjwa, kuna mtoto wangu, ananihtaji,…na hali ngumu niliyo nayo,….ningeliomba nisiwepo kwenye hiyo shughuli…. pia nikawaambai kuwa wakinitangaza kwa hali ninavyoijua hizo pesa zitaishia mikononi mwa watu…’nikasema na mwenyekiti akacheka, na kunyosha mikono yakuonyesha kuwa hakuna kitu.

‘Samhani sana shemeji, ….nikisema hivyo, kuwa nina mashaka na maelezo yako hayo sizani kisheria kama yanaweza kukubaliwa, maana ilivyo,wao wana msharti yao, na huwa wanatoa hizo promosheni kwa nia ya kujitangaza,…kwenye mashandano yao kuna maneno wanasema, `na msharti kuzingatiwa…’ yana maana yake kisheria,..sasa shemeji yetu, iweje wewe wa kufanyie tofauti na wengine, ..?’ akaniuliza.

‘Ni kweli walinikatalia kata kata kuwa hawataweza kunipa hizo pesa hadi kwenye hiyo shughuli waliyoiandaa….mimi nikawaambia kama ni hivyo, basi sihitaji pesa zao maana najua sitaweza kuzitumia kama wakinitangaza….’nikasema, watu wakaguna kuonyesha kuwa nilichoongea ni uwongo wa kujitungia.

‘Kwani kitu gani ulichokuwa ukikiogopa kuwa ukitangazwa kitatokea, utaibiwa au….?’ Akauliza huyo mwanasheria.

‘Mume wangu alikuwa jela kwasababu ya kushitakiwa kwa kuiba pesa, wewe huoni mimi kama mke wake, wangelinihisi kuwa hizo pesa ni hizo alizokuwa kaiba mume wangu, wangelikuja kudai hizo pesa na sikuwa na muda wa kuanza kupambana na hawo watu, lengo na nia yangu ni kumpigania mume wangu atoke,…,na hata hivyo, mtu akiumwa na nyoka, akiguswa na unyasi ni lazima atashituka, mimi nilishaibiwa,, kwahiyo nilikuwa na uwoga wa kuibiwa….’nikasema.

‘Hiyo shemeji sio sababu ya msingi ya kuweza kuwaabdili hawo watu wakufanyie tofauti, kwasbabu hayo mashindano ya lengo maalumu, hawatoi kama sadaka…..sizani…hebu tuambie ilikuwaje mpaja wao wakufanyie tofauti, haiingii akilini, ailikuwaje shemeji?’ akauliza.

‘Niliwaomba mtu mwingine asimame badili yangu na mimi nitamlipa…’nikasema na watu wakacheka, na huyo shemeji mwanasheria akasema;

‘Hiyo sasa mpya, ….shemeji mimi nafahamu sana hizo promosheni na lengo lao kubwa ni kujitangaza, na pesa hizo ni yingi, wasingeliweza kukubali kufanya kama ulivyotaka wewe….ina maana basi ulihinga, kwa lugha rahisi, kitu ambacho hakiwezekani..’akasema.

‘Kama hamuamini basi…..kama mnataka basi ,naomba twende huko Dar, nina imani watathibitsha hilo….’nikasema.

‘Shemeji, sio kwamba nakupinga kwa nia ya kukupinga, hilo nililisikia, na nikalifanyia uchunguzi, ..kiukweli sikuweza kuliona jina lako kwenye hiyo promosheni, kweli kulikuwa na mshindi wa namna hiyo, lakini jina lako halipo pale, na bahati mbaya, mitambo yao ya kipindi hicho iliharibiwa na virusi,….lakini hata hivyo, bado walikuwa na namna nyingine za kupata hiyo taarifa, kuna picha za tukio hilo, mawasiliano  ya simu….,wewe haupo ‘akasema na mimi nikamkatisha.

‘Nimekuambia, niliwaomba kwa hiyo dharura, sasa picha yangu ingelionekana vipi….kama hamuniamini kuwa kweli nishinda mimi sijali,…lakini kwanza kwanini hamjiulizi kuwa wale waliokuja kudai mwanzoni kuwa hizo pesa nilizojengea ni za wizi, mbona walishindwa kunipeleka mahakamani, wao wenyewe walikuja kufutilia na baadaye wakaona ni kweli na kuachana na hayo madai yao…?’ nikawauliza.

‘Shameji, ….hayo yote nilifuatilia,….niliwauliza….wakasema waliona hakuna haja tena ya kuhangaika, …kwani walipofika huko kwenye ofisi za simu uliposema ulishinda, walijikuta wakipewa tarehe, njoo kesho njoo kesho, na ukumbuke kuwa kampuni hiyo ilishabadilika mara nyingi, leo inaitwa jina hili kesho lile,...kwahiyo waliokuwepo awali hawapo tena….hata hivyo. Kumbukumbu muhimu hazipotei….hakuna jina lako…kabisaa’akasema huyo wakili.

‘Mimi nimeshawaambia kama hamuniamni, sijali, mimi sitakubali kwa hilo, kwani nyumba na duka vyote hivyo nimejenga kwa pesa zangu, …nitavipigania hadi hatua ya mwisho,…’nikasema kwa hasira. Na mwenyekiti aliposikia hivyo akaingilia kati.

‘Shemeji, nilitaka usikie sheria inasemaje juu ya hilo, maana hata mimi niliposikia hivyo niliingiwa na mashaka,….hatukuwahi kusikia jina lako likitajwa kuwa wewe umeshinda pesa kama hizo, ina maana wote siku hiyo hatujaliwa kusikiliza redio na kuangalia runinga….hilo ndilo lililotufanya tusiamini kuwa pesa hizo ulizipata kwa bahati nasibu, ni jingine ni kauli ya mume wako na maandishi yake mwenyewe, …kama unayahitaji tutakuonyesha, ….’akasema mwenyekiti.

‘Hiyo sio kweli, maandishi mumeyatunga wenyewe….hakuna kitu kama hicho..,nawafahamu sana huenda mlimuhadaa, ili mwisho wa siku ionekane hivyo…na hapa mtakuwa mkimsingizia marehemu kwa vile hayupo…’nikasema kwa hasira.

‘Mimi niliongea na ,mume wako akiwa bado mzima, na alisema hizo pesa huenda wewe ndiye uliyemuibia wakati mnafika Dar, ukazificha,….maana muda wote mlikuwa wote wawili, haiwezekani ule mkoba umtoke mikononi, na wakati yeye alikuwa kaushikilia mikononi….’

Aliniambia mpaka leo hajui jinsi gani huo mkoba ulivyomtoka hadi hizo pesa zikachukuliwa, mtu ambaye angeliweza kufanya hivyo ni wewe….maana mlikuwa pamoja, na alikuamini….kwahiyo wewe ulipopata huo mwanya, ukaziiba, na alipokamatwa, na ukaona umepata nafasi ya kudanganya,….’akasema mwenyekiti kwa kujiamini, na nilipotaka kujitetea akaonyesha mkono wa kunituliza, kuwa hajamaliza, akasema;

‘Ndio maana ukasingizia kuwa ulishinda kwenye hiyo bahati nasibu…na ndugu yetu, alisema kuwa kwa vile wewe ndio umezichukua na kuzifanyia jambo la maana, bsi haina shida, ila akasema ni lazima ahakikishe kuwa nyumba na hilo duka zinakuwa katika jina lake, ndio maana akapigania hadi ukakubali kuandikisha jina lake ….’akasema mwenyekiti, na kunifanya nibakie siamini maneno haya, kwani niliwahi kukorofishana na mume wangu akayazungumza hayo, lakini baadaye nilimuelewesha mume wangu hadi akakubali…

‘Nahisi mliongea naye kipindi kile alichokuwa akilewa sana,….tukawa hatuelewani, na kipindi hicho tulikuwa hatuelewani kwsaabau ya ulevu wake, na nahisi ndipo mlipomshawishio hadi akanishawishi nikakubali kuandikisha jina lake….mimi nilikubali kwasababu ni mume wangu, na huenda ndipo mlipomrubuni hadi akakubali kuwaandikia hayo maandishi mnayodai kuwa aliyaandika yeye na kuweka sahihi yake…..’nikasema.

‘Kama ulijenga kwa pesa yako tunavyokujuwa wewe, usingelikubali kuandikisha jina la mume wako kwenye hati ya nyumba an duka, …..kwanini usingesema kuwa muandikishe kuwa mumejenga kwa kushirikiana, ina maana kwako hakuwa na uzito, kwani pesa zilikuwa ni za kwake…?’ akasema mwenyekiti.

‘Nyie mnadai kuwa pesa hizo zilizojenga hiyo nyumba ni za wizi , kama kweli alindika hizo nyaraka za kuhalalisha kuwa nyumba hiyo ni yake kutokana na hizo pesa mnazodai kuwa ni hizo za wizi, na kama ni kweli mbona hamkuwaambia wenyewe, walioibiwa ili waje wataifishe hiyo nyumba na duka..?’ nikawauliza na watu wakacheka.

‘Hilo lipo kwenye ajenda yetu ya mwisho, ajenda ya kukushukuru kwa kuweza kumfichia mume wako, …na juhudu za ziada ulizozifanya hadi ukaweza kujenga hiyo nyumba, …..ni dhuluma ndio lakini kwa namna nyingine imewezesha kuwepo na nyumba nzuri kwenye familia yetu , hilo tulitaka baadaye tukupongeze, na kama ikibidi tungelitafuta njia ya kuliweka sana, na …hatua iliyofanyika ya kuiandikisha kwa jina la mtu mwingine ni moja ya kuhakikisha kuwa mali hizo hazichukuliwi tena….’akasema mwenyekiti.

‘Haya mengine hatukutaka kuyasema ni siri zetu za ndani….maana kama tumefanikiwa kwa kiasi hicho, tukapata nyumba na duka, hatuwezi kuanza kuchunguza kuku kala nini,….eti,…’ akawa kama anauliza na baadaye akasema

‘Sisi tunachoangalia ni nyama…au sio…! Nyama ni hiyo nyumba na duka, na iliyobakia kwetu ni kusaidia juhudi za mwenzetu, aliyefanikiwa hadi ikapatikana hiyo nyumba, tusikubali ichukuliwe tena, itakuwa ni aibu kwetu…’ akawa anapunguza sauti, kwani huwa akiongea sauti yake ni nzito na kusikika.

‘Kwahiyo sisi tuliliongelea hili , tukaona ili lisilete utata, tulinyamazie hivi hivi, …wasije wakasikia wenyewe na kuanza kuleta balaa, ingawaje mwanasheria wa familia keshaliweka sawa,…katu hataweza kudai kuwa pesa iliyojenga hiyo nyumba na duka imetokana na pesa ya wizi, ushahidi upo wapi….hatutakubali hilo abadani,….’akawa anaongea kwa sauti ya chinichini ili eti asisikiwe.

‘Hizi zilizojenga hiyo nyumba, hazikutokana na pesa mnayodai ni ya wizi,….nyumba hiyo nimejenga kwa pesa yangu,nieleweni ndugu zanguni ….’ Nikasema kwa sauti, hadi mwenyekiti akaniangalia kwa mshangao. Sikumjali, nikasema;

‘Mbona hamunielewi ndugu zanguni,….kama ni hivyo, kwakweli mimi sitakubali,….hiyo nyumba ni yangu, na kama mlipanga kufanya hivyo, mkifikiria kuwa nyumba hiyo imejengwa kwa pesa za urithi, mlikosea, na nawaambi, msiwe na haja ya kuogopa, kuwa hawo watu watakuja kudai eti hizo pesa zilikuwa zao zilizoibiwa, hizo pesa ni za kwangu, zilitokana na huo ushindi wa promosheni ….’nikasema kwa sauti kubwa.

‘Hebu punguza sauti shemeji, hatupo kwenye ugomvi hapa…tumekusikia hayo maelezo yako, kiukweli, siyo ya kweli, umejitungia, ili kuhalalisha hilo…tunashukuru sana kuwa ulionyesha juhudi za kuweza kujenga hiyo nyumba, ….kweli tunashukuru sana, ….’akasema mwenyekiti.

‘Naona sasa mnanitafuta ubaya,…mimi sikubaliani kabisa,…na kama mumeshikilia maamuzi yenu hayo mimi nitachukua hatua nyingine,… nitafika mahakamani kudai haki yangu…’nikasema na hapo yule mwanasheria akanyosha mkono, na mwenyekiti akamruhusu.

‘Shemeji hapo kazungumza la maana sana, …kama mtu anaona katendewa kinyume na sheria, na anahitaji haki yake, sehemu muhimu ni mahakamani..mimi nashauri, ili aweze kuitetea haki yake vyema, tumpe nafasi hiyo ya kwenda mahakami, na kama atathibistiha hivyo, basi tutabadilisha kila kitu, na kuweka jina lake….’akasema huyo mwanasheria.

‘Na kama utafanya hivyo,basi atakuwa umeisaliti familia….maana kama familia haya tulitakiwa tuyaongea humu ndani na kuyamaliza, lakini yakitoka nje, na kwenda mhakamani,…hapo wewe sio mwenzetu….hebu tujiulize hapo unamshitaki nani,?’ akauliza mwenyekiti akionyesha kukasirika.

‘Mimi nimetoa malalamiko yangu kwenu, mumeyapinga, na nyote mpo kitu kimoja, sasa unafikiria haki yangu nitaipata wapi….mnataka nitulie wakati najua kabisa kuwa hiyo ni haki yangu,…hapana, mimi nitaipigania haki yangu hadi hatua ya mwisho, …na nawaambia ukweli,…nyumba na duka ni mali yangu, sikubaliani na chochote, hata kama udugu utavunjika kwa hilo, kwa vile najua ninachokitetea ni haki yangu…’nikasema na hapo kikao kikaanza kuvurugika.

‘Sikiliza wewe mwanamke….nimekuvumilia sana…na nimekuambia haina haja ya kupandisha sauti juu, na sikiliza kwa makini, sisi tunajua nini tulikifanya, na tulitarajia kuwa ungelikuwa na ushahidi mpya, ambao ungetusaidia, lakini kumbe ni hayo maelezo yako…sasa sikiliza kwa makini, nyumba ile sio mali yako, na duka ..huo ndio uamuzi wa kikao hiki,….kama una jingine, sema, kama una ushaidi mwingine tunauhitajia,..vinginevyo, tunakuomba uheshimu kikao na viongozi wako, maana wao walifanya haya kwa nia 
njema,…’akasema mwenyekiti, na watu wakamshangilia.

‘Mwenyekiti, mimi sitakubaliana na hilo..’nikasema na mwenyekiti akaniamurisha ninyamaze.
Wazazi wangu waliomba waongee kidogo, lakini hawakuruhusiwa, na walipoona kikao kinakwenda hali ya kutokuelewana, wakanishauri tuondoke, na wazee wakutane walijadili hilo swala kwa undani, lakini wao kama familia walishikilia msimamo wao kuwa kamwe hawatakubali kuachia mali ya mtoto wao kuandikishwa kwa mtu mwingine,

‘Kama ni hivyo mimi nitachukua hatua nyingine, nitakwenda mahakamani…’nikasema.

‘Ukifanya hivyo, ….ujue kuwa umejitenga na familia hii, na sio kwamba tunaogopa kwa hatua hiyo, lakini kwa hatua kama hiyo ya kuishitaki familia, inaonyesha kuwa haupo ndani ya familia….’akasema mwenyekiti .


‘Sawa, mimi nifanya hivyo kwa nia njema, ili haki yangu ipatikane…na kama itafanya niachane na familia kwa ajili ya hilo, samahanini sana, mtanisamehe kwa hilo,…’nikasema na kuinuka kuondoka, na wazazi wangu wakainuka na kunifuata nyuma na yule mwanasheria, akasema;,

‘Basi hakuna shida, tutakutana mahakamani…’.

NB: Haya je mnasemaje kuhusu maamuzi ya huyu mwanamama?


WAZO LA LEO: Wakati mwingine haki inaweza ikawa ngumu kupatikana kwa majadiliano ya kifamilia, na wakati mwingine wanafamilia wanaweza wakawa hawamtendei haki mwanafamilia mwenzao, kwasababu ya mila na desturi, na mila nyingi na desturi zinawatenga akina mama, kuwa wao kama wanawake hawana haki ya kutetea haki zao, na utakuta haki hzi ni za msingi na za kweli.  Zipo haki zao zinajulikana kisheria na kidini, lakini wanashindwa kuzitetea,au kupewa nafasi ya kuzitetea . Kitu cha kufahamu ni kuwa haki ni kwa kila mtu awe mwanamke au mwanaume kila mmoja anastahili apewe haki yake. 
Ni mimi: emu-three

No comments :