Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, June 14, 2013

WEMA HAUOZI-21



Sikuweza kuamini mjukuu wangu,….ulikuwa mkoba ule ule niliokuwa nikiuona kwenye zile ndoto nilizokuwa nikiota kule hospitalini….ni miujuiza ya mungu…’babu akarejea maneno hayo.

‘Unautafuta huu mkoba?’ akaniuliza huku akinitizama huku akijaribu kila iwezekanavyo nisimuone zaidi ya ya macho yake, amabyo pia yalikuwa hayaonekani vizuri kwa vile ile nguo aliyojifunika ilikuwa inacheza cheza kutoka na upepo.

‘Nafikiri ndio huo….’nikasema nikinyosha mkono kuuchukua, ili niweze kuutambua,lakini yule mtu hakunikabidhi akaurudisha na kuuweka pale alipouchukulia, na akasogea na kukaa pale alipokuwa amekaa, na taratibu akajifunua zile nguo alizokuwa amejifunika usoni…..na kugeuka kuniangalia…’ 

Hapo ndipo babu alipoishia, lakini akili yangu ikavutiwa na maelezo ya mama ambaye lishafika akitaka kuendelea kuelezea nini kilitokea, kwani siku ya kesi ilishafika.

*******

Ilikuwa ni asubuhi ambapo tulipanga iwe siku ya kikao kwa ajili ya maandalizi ya kesi yetu, ambayo ilitarajiwa kufanyika kesho yake, kwahiyo wale wote waliotakiwa kuwa mashahidi walitarajiwa kuwepo kwenye hicho kikao.

Mimi nikiwa na wazazi wangu, tukiwa tunawasubiri hawa wageni, tukawa tunaongea hili na lile katika kupoteza muda, kwa ujumla hatukuwa na matumaini sana japokuwa watu mbali mbali walishakubali kutoa ushahidi akiwemo mjumbe, na mafundi waliojenga hiyo nyumba, japokuwa tulifahamu kuwa ushahidi wao hautakuwa na nguvu sana.

‘Sisi tusikate tamaa, hao hao mashahidi watatosha,na nina imani kwa vile tunachotetea ni haki yetu, watakachoongea huenda kikasaidia kumshawishi hakimu…’akasema baba.

‘Ushahidi muhimu ni huo wa malipo ya hiyo pesa, kuwa kweli ulilipwa na hiyo kampuni, na hapo kunahitajika stakabadhi ya kulipa hiyo hundi, …’akasema mmoja wa mashahidi ambaye alikuwa kafika mapema nay eye alikuwa akifahamu sheria kidogo.

‘Lakini hebu niulize….sasa yule mwanamke aliyekuja siku ile na kusema kuwa yeye ni mwanasheria na akasema anatafuta njia ya kukusaidia akadai kuwa mtakutana mahakamani alikuwa na maana gani?’ akauliza mama.

‘Mama yule ni mchumba wa huyo wanayemuita mwanasheria wao wa familia, ….kweli kwa hali halisi anaweza akamsaliti mchumba wake…akaisaliti familia ambayo anatarajia kuolewa na kuishi nao?’ nikauliza.

‘Inavyoonekana kuna kutokuelewana kati yake na huyu mchumba wake..’akasema baba.

‘Kama ni hivyo, basi tunaweza kumtumia , hata kupata huo ushahidi unaohitajika mahakamani,ambao nahisi wanao wao, kama kweli hawajauharibu..’akasema mama.

‘Mimi bado sijamuamini,…..ukiangalia kwa makini, inaonyesha yule mwanamke alifika siku ile kuchunguza, …jambo, na mimi nahisi kuwa alitaka kujua kuwa kweli wewe upo tayari kurithiwa na huyo mchumba wake, akionyesha wivu, nyie hamulioni hilo,….yule anampenda sana mchumba wake, lakini huyo mchumba wake, anatamaa…na nahisi siku ile alipogundua kuwa huna nia hiyo akaona arejee kwa mchumba wake….’akasema baba.

Mara mlango ukagongwa, na wote tulikaa kimiya , na mimi nikainuka nikijua kuwa huenda ni hawo wageni wetu, tuliowatrajia, na nikaenda kufungua mlango, na malngo ulipokuwa wazi, nikajikutwa nimeshikwa na butwaa, na kwa sekunde chache nilibakia nimeduwaa, halafu kwa sauti isiyo na nguvu nikasema ;

‘Karibu..’nikageuka kuangalai ndani huku nikiwa nimekunja uso.

‘Shemeji samahani nilikuwa nataka tuongee mimi na wewe faragha…’akasema huyo mgeni huku akiwa kasogea na kuwa karibu na pale niliposimama, na kwa hali hiyo akawa anaonekana na wazazi wangu waliokuwa ndani.

‘Mimi sina kitu cha kuongea na wewe faragha, nakumbuka kwa mara ya mwisho niliweka wazi msimamo wangu, …sasa sioni kwanini bado unanifuata fuata, kama umeamua kunidhulumu haki yangu, basi fanyeni hivyo….lakini mimi siwezi kujizalilisha kwenu, na nakuomba unielewe hivyo…’nikamwambia.

‘Shameji siku ya kesi imekaribia…, na ukiangalia kiukweli wewe huna ushahidi wowote utakaokusaidia, na mimi nisingelipenda kukuona wewe ukienda kuumbuka mahakamani, na pili mimi sina haja ya kukudhulumu, ninachokifanya ni kusaidia pale ndugu yangu alipoishia na kuhakikisha kuwa mali yake inakuwa salama, na kwa jinsi alivyotaka yeye..kuwa niiweke kwenye mikono salama na wewe uwe na mimi…kama familia yangu…’akasema

‘Hayo ni maneno yenu na hiyo ni mipango yenu, sisi hatuwezi kuwaiingilia,….endeleeni hivyo hivyo na mipango yenu ya uwongo wa kutunga, mimi nina imani kabisa kuwa mume wangu hakuwahi kusema hayo, na kama alisema, ilikuwa ni kipindi kile alichokuwa kachanganyikiwa na ulevi, lakini baadaye alitulia….. , mimi nina imani kabisa kuwa alikuwa keshafahamu ukweli kuwa nyumba na duka  nilijenga kwa pesa yangu…na tuliongea naye hadi akasisitiza kuwa tukabadili hiyo hati ya nyumba iwe kwa jina langu…’nikasema.

‘Shemu, mbona unarudia hayo hayo….kama ni kweli ushahidi upo wapi,…tusaidieni kwa hilo, nionyeshe huo ushahidi ili nijirishe nafsi yangu, hujui ni kiasi gani ninavyotaabika kiakili, nikisikia hivyo, wakati kaka yangu alianiambia tofauti na hayo unayoyaongea….?’ akauliza.

‘Kwani wewe ni hakimu, ….mpaka uhitaji huo ushahidi wetu, huo ushahidi wetu unautakia nini, hili swala kwa sasa lipo mahakamani, na kama kuna ushaidi basi utakutana nao huko mahakamani, wasi wasi wako ni nini?’ akauliza baba kuingilia mazungumzo yetu.

‘Wazee wangu shikamooni, samahani sana kwa kutokuwaslimia,…..’akasema  huku akiweka mikono kifuani kuonyesha kuwa ana adabu kwao, na wazee waakmuitikia, na baadaye akasema;

‘Mzee…, mimi ndio maana nimefika hapa kwa nia njema kabisa ya kumsaidia shemeji yangu huyu, ..huyu ni shemeji yangu, na nimejaribu kuwa wazi kwake, kuwa nipo tayari, kufuata taratibu zote za kimila,…ikiwemo hiyo ya kumrithi mjane…., na labda hilo neno sio sahihi kwake, linaleta hisia mbaya, lakini ni ukweli usiopingika kuwa mtu akifiwa, na mumewe, sio kwamba ni adhabu kwake, ….kuwa basi yeye hawezi kuishi na mume mwingine tena…..na kama ikibidi, labda sihitajiki kuliongea hapa kwenu, kama mtoto, ila nitataka kufuata taratibu zote zinazohitajika, ili , kama hilo kurithi linaleta hisia mbaya, tusiseme hivyo……mimi nipo tayari kufuata taratibu nyingine, …’akasema na kutulia.

‘Taratibu gani hizo….?’ akauliza mama kwa mshangao.

‘Mimi naweza kuja kumposa binti huyu kwenu, ili awe mke wangu..nazungumza hili kwa nia njema kabisa, nafanya hivi kwa ajili yake na  mtoto, kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mke aliyeachwa na ndugu yangu hapati shida, na juhudi zake hazipotei bure…’akasema huku akiwa kaweka mikono kifuani kwake na wazazi wangu wakawa wanamwangalia kwa makini.

‘Nani kakuambia kuwa mimi nahitaji mume…..sina haja ya ndoa na mtu yoyote, ….nilishawaamba wazi, na msifikirie kuwa mimi nitakubali kwa kutumia mitego yenu hiyo..kamwe sitakubali kwa hilo, hata kama mtachukua kila kitu changu…bado nitabakia kwenye msimamo wangu….’nikasema.

‘Shemeji, hakuna mtu atakayechukua kitu chako…hili nakuhakikishia…kama kuna kitu chako kama chako, hakuna atakyekigusa….hilo nakuthibitishia, sisi tunachokilinda ni mali ya ndugu yetu,.na kauli yake,….na nafahamu kuwa kwa aslimia kubwa huenda mlichuma wote, ni sawa, …ndio mama sisi kama wanafamilia tuliliona hili, ..wewe bado utaendelea kuchuma na kufaidikia na kile mlichokianza na kaka marehemu,… ila sisi kama wanafamilia tunachokikataa ni wewe kumiliki, na kudai kuwa ni mali yako binafsi, na ulijenga hiyi nyumba kwa pesa zako ….wakati hilo sio sahihi..’akasema.

‘Sio sahihi kwa vile mumechukua ushahidi wote,…sio sahihi kwa vile mumejenga hiyo hoja kinafiki mbele ya hakimu…, lakini mkumbuke kuwa kamwe jasho la mtu na haki ya mtu haipotei bure, ..hiyo haki ni yangu, na nina uhakika kuwa nimejenga kwa pesa zangu,….mungu wangu ni shahidi hata kama nyie mtalipinga, hata kama nitakosa shahidi wa kidunia, ila mungu wangu anatosha kuwa shahidi yangu…’nikasema.

‘Shemeji, kama kungelikuwa na namna yoyote ya kunishawishi,…nisingelifanya haya, maana mimi siwezi nikaamini hayo unayoniambia,…..nitaaminije,….wakati ndugu yangu mwenyewe alinitamkia , na hata kuniomba nikaandikishe….hati miliki kwa jina langu kwa vile alitaka mimi na wewe tuwe familia moja…..’akasema huku akiniangalia, halafua akawageuka wazazi wangu kama vile anaomba msaada wa

‘Shemeji….hapana shemeji,…mimi bado sijaamini,..nionyesheni ushahidi kama mnao, na kama nikiuona, nakuhakikishaia kuwa ni kweli,…shemeji, wazazi wangu,…mimi nitakwenda kuiambia mahakama kuwa kweli hiyo ni mali yake, na sitasubiri familia itoe uamuzi,…’akasema.

‘Hayo ni maneno ya mfa maji,…naona mumehisi kuwa tumeshaupata huo ushahidi na mtakuja kuumbuka mahakamani, ..ndio maana mnajaribu kutafuta upenyo wa hadaa…..sisi tutakutana huko huko mahakamani…’akasema baba akijiamini, huku nikiwaza jinsi gani ya kuupata huo ushahidi.
Huyu jamaa aliposikia maeneo hayo toka kwa wazazi wangu, akaonekana kutulia, na baadaye akanigeukia na kusema;

‘Shemeji,..bado nasisitiza kuwa nina mazungumzo kati yangu mimi na wewe ya faragha, hili ni muhimu tuongee tukiwa wawili,…sina nia mbaya yoyote juu yako,…mimi kama mtu niliyekabidhiwa wewe na mtoto nina wajibu wa kuhakikisha mnaishi kwa amani na salama….’akasema.

‘Nashukuru kwa hilo…., tupo salama na amani, hamna shida, unaweza kwenda …’nikasema.

‘Shemeji tafadhali, nakuomba…’akasisitiza na wazazi wangu wakaingilia kati na kuniambia nikamsikilize kuwa anataka kusema nini.

********

‘Haya niambie unanitakia nini kwa faragha..?’ nikamuuliza pale tulipoingia kwenye chumba kingine.

‘Ni hivi shemeji,…sina uhakika kuwa yule mchumba wangu amewahi kuja hapa na mkakutana naye au vipi, ila nahisi hivyo kuwa huenda amefika akaongea na wewe….cha muhimu ninachotaka kukuambia ni kuwa, yule anatapatapa…kuna mambo ambayo tunasigishana, likiwemo hili la kutimiza wajibu wangu nilioachiwa na ndugu yangu….’akatulia na kuniangalia , na machoni alionekana hana raha.

‘Kwahiyo unahitaji ushauri wangu au..?’ nikamuuliza.

‘Shemeji, nikuambie ukweli, huenda hilo ulikuwa hulijuia kwasababu sikuwahi kuoanana na wewe uso kwa uso, lakini mimi nakufahamu muda mrefu tu….na kiukweli moyo wangu ulikuwa umevutika na wewe, kwa vile ulikuwa mke wa ndugu yangu, niliheshimu hilo, japokuwa moyoni, nilitamani nipate mtu kama wewe…’akasema huku akiwa anaonyesha huzuni, au sikumuelewa.

‘Shemeji…hili nakuambia toka moyoni, siliongei leo kwa vile kuna jambo lolote jingine, hapana, shemeji, nimeamua leo nikuambie ukweli, wa kutoka moyoni kwangu….’akatulia na kuniangalia usoni, mimi nilikuwa nimeinama chini.

‘Mara nyingi nilikuwa nafika hapa na kaka yangu, lakini nilikuwa siingi ndani, ….na moja ya saabbu ni hiyo, kuto….siunajua shemeji, mtu unampenda na ni mke wa kaka yako, utafanyaje….inabidi uheshimu na uumie kiundani ndani, na niliona jambo jema ni kuwa mbali na wewe kadiri ilivyowezekana….’akatulia kidogo.

‘Yaani nasema hayo kutoka kwenye moyo wangu,…nilikuwa najaribu kukuangalia kwa mbali, wewe nafikiri hukuwa na umakini na mimi, kama ungelikuwa mdadisi ungeligundua hilo, lakini hilo halina maana kwa sasa…ila nilitaka tu kutoa lile lilokuwa moyoni kwangu, kuwa sio kwamba nayafanya haya kwa vile unahitajika kurithiwa….silipendi hilo neno, lakini inabidi iwe hivyo, nayafanya haya kwanza kwa ajili ya kutimiza yale niyoyaahidi kwa ndugu yangu, lakini kubwa zaidi ni kwa vile nakupenda……..’akasema.

‘Nakusikiliza shemeji….naomba ufanye haraka kutoa maana kma ulivyoona sisi tuna kikao, na wageni ndio hao wanaanza kuingia….’nikasema niliposkia mlango ukigongwa.

‘Oh, shemeji huna habari…ina maana hujaambiwa, haiwezekani, kesi imeahirishwa ni mpaka kesho kuwa asubuhi…’akasema na mara tukasikia hodi nyingine,….na baaadaye nikasikia mtu akisema kuwa kaleta barua.

‘Inawezekana ndio barua hiyo ya kukuarifu kuwa kesi ni kesho kutwa asububuhi sio kesho tena…na kama unataka, mimi ninaweza hata hiyo kesho kesi ikaahirishwa na hata kufutwa kabisa….’akasema.

‘Ufute hiyo kesi kwani wewe ndio umeshitaki…..?’ nikamuliza nikimwangalia kwa zarau.

‘Nafahamu hilo, ….ila tukikubaliana , mimi nitakwenda kuongea na hakimu, na kesi ikafutwa kabisa…’akasema.

‘Utafutaje kesi ambayo wewe sio uliyeshitaki…?’ nikamuuliza huku nikiwa nimekunja uso kwa hasira.

‘Unisikilize kwa makini shemeji, nasema `tu-ki-ku-baliana’, na tukasema hili swala tutalimaliza nyumbani, ….basi wewe na mimi tunakwenda pale mahakamani, tunamwambia muheshimiwa hakimu kuwa tumeshakubaliana,…sioni kwanini tufikie hapa,shemeji mimi nakupenda sana, nahitaji nishike ile nafasi ya ndugu yangu, …..’akasema.

‘Shemeji, nimekusiliza kwa makini…kwakweli jisini unavyofanya nazidi kukuona kuwa hufai….Hivi wewe una akili kweli, una ubinadamu kweli, wewe una mchumba, unafikiri huyo mchumba wako atakuelewa vipi, au ulikuwa unampotezea muda wake bure..usiwe na roho ya kinyama…jaribuni kuwafikiria na wengine, …’nikamwambia.

‘Hilo shemeji lisikuumize kichwa, mimi na huyo mchumba wangu tunajuana,….na uchumba wetu ulikuwa na msharti, kadhaa…ambayo kama hayakutimia, au hatukukubaliana, basi uchumba huo unavunjika, na hayo tumeshayaongea,…sina unyama wa anmna hiyo, …..yeye mwenyewe karizia hilo, iwe hivyo, na kakubali kama utakubali wewe uwe mke wangu, basi yeye atakaa pembeni….’akasema.

‘Hata sikumoja, usije ukaota hilo…kwa ufupi nakuomba, ukamrejee mchumba wako umwambia kuwa mimi sitaki kuolewa na wewe…sitaki kuolewa kwenye hiyo familia yenu tena…ni bora niishi  hivi hivi hadi kufa kwangu kuliko kuolewa kwenye hiyo familia yenu…’nikasema

‘Kwanini shemeji unasema hivyo,…tumekukosea nini,familia yetu imefanya nini kibaya kwako …?’ akauliza kwa uchungu

‘Wewe haya mliyoyafanya mnafikiri ni mazuri….hamjui ni kiasi gani mlivyoniumiza, na bora haya yangelikuwa kati yangu na nyie, lakini mumefikia hadi ya kumuumiza yule baba yangu wa kufikia, kwa ajili ya mali ambayo sio halali yenu..sitawasamehe kwa hilo….kamwe.nakuomba uondoke…na sitaki kuongea na wewe kuhusiana na hilo ombi lako…natumai umenisikia…mengine tutakutana mahakamani’nikasema.

‘Kwa hilo shemeji, sitaacha kukuomba…, iwe itakavyokuwa, lakini mimi kila siku nitakuja kwa ajili ya hilo, kwa vile nafanya hivyo sio tu kwa matakwa ya ndugu yangu, lakini pia ni kwa vile nakupeda…’akasema

‘Lakini mimi sikupendi, kwahiyo huwezi kulazimisha mapenzi,….wewe ni msomi naomba ulielewe hilo, ….sikupendi na sitatokea kupenda mtu yoyote kwenye hiyo familia yenu, na ipo siku mtaumbuka, kwa tabia hiyo ya kutaka dhuluma, ..ipo siku mtaumbuka….’nikasema kwa sauti.

Na mara ghafla huyu shemeji akapiga magoti mbele yangu, na huku akiwa katoa kiboksi kikionyesha kuwa ni cha pete….na akawa anakifungua huku kapiga magoti mbele yangu…nikawa nimetahayari kwa kitendo chake hicho, na hata kabla sijaweza kusema neno, huku nimekunja uso kwa hasira, mara mlango ukafunguliwa, ….

`Shemeji….nakuomba ukubali uwe mke……’akaanza kuongea, na ndip hapo mlango ukafunguliwa na aliyekuwa kasimama kati kai ya mlango alikuwa yule mchumba wake, akaniangalia huku akionyesha tabasamu kidogo, lakini lilifia pale alipomuona huyu jamaa akiwa kanipigia magoti na mkononi kashika pete…..mimi nikiwa bado nimetahayari , nikamwangalia shemeji yangu huyo aliyekuwa bado kapiga magoti, na aliposikia mlengo ukifunguliwa akageuza kichwa na kuangalia huko mlangoni, alimuona mchumba wake, akiwa anatuangalia na tabasamu lililojaa huzuni machoni

Yule shemeji yangu alipoona huyo aliyeingia ni nani, kwa haraka akasimama, huku akifuta futa kwenye magoti yake kuondoa vumbi kwenye suruali yake.

‘Wewe umefuata nini huku…?’ akauliza , na sauti yake ilionyesha unyinge fulani, sio ile sauti ya kujiamini aliyozoea kuiongea.

‘Samahani…kidogo, nataka kuongea na mteja wangu…’akasema huyo mchumba wake.

‘Mteja wako…?’ akauliza huyo shemeji yangu kwa uso uliosawajika, alikuwa kama kaishiwa nguvu,….

NB: itakuwaje?


WAZO LA LEO: Tuwe makini na kauli zetu, tuwe makini na mtendo yetu, ambayo tukiyaongea au kuyafanya yanaathiri hisia zetu. Hili ni kwa wale waliotokea kupendana, na kuotokana na misigishano kukawa na kutokuelewana, ni vyema kuwa makini kutokuumizana zaidi  na kujenga chuki zaidi. Pendaneni kwa wema, na kama ikibidi kuachana achaneni kwa wema.
Ni mimi: emu-three

5 comments :

Justin Kasyome said...

kweli, ni muhimu kuwa makini na kauli zetu...

Yasinta Ngonyani said...

Visa kama hivi vinafunza sana nakusihi andika kitabu kitawasaidia wengi maana wengi hawana nafasi/uwezo wa mtandao kama wengine ila kununua kitabu najua wengi wana uwezo..Bonge la shule hapa....amani kwa wote.

Unknown said...

Mbona haiendelei mnatunyima uhondo bhana

Unknown said...

Mbona haiendelei mnatunyima uhondo bhana

emuthree said...

Niliadimika kidogo kutokana na mitihani ya hapa na pale...tuendelee sehemu inayofuata, nawashukuru sana @Justine Kasyome, dada wangu @Yasinta, ndugu yangu @Nancy Msangi na wale wote wa Kimiya kimiya. Tupo pamoja