Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, June 10, 2013

WEMA HAUOZI-19



                      Mama aliendelea kunihadithia maisha yake kwa kusema

Mgeni aliyegonga mlango alipoingia tulitupiana macho na wazazi wangu tukikumbuka maongezi yetu yaliyopita, na baba hakusita kuonyesha hisia zake kwa kunionyeshea ishara kuwa niwe makini, na mimi nikageuka kumwangalia mgeni nikichelea asije akamuona baba yangu alipokuwa akinionyesha hiyo ishara…

‘Karibu mgeni,….’nikasema nikimuonyeshea huyo mgeni kukaa kwenye  kiti, nikitarajia kuwa atasema kuwa hatakaa ana haraka, lakini haikuwa hivyo, kwani mgeni, alisogea pale kwenye kiti na kukaa na kabla hajafanya hivyo, aliwageukia wazazi kwa adabu, na kuanza kuwasiliama mmoja mmoja nikatulia hadi walipomaliza kusalimiana, na baadaye nikamuuliza mgeni nimpe chochote, ikiwa ni sehemu ya kumchokoza ili nisikie akisema amekuja mara moja anaondoka….

‘Hapana nashukuru sana, mimi nimepitia tu hapa, kwani sikuwepo kwenye kesi, na niliyoyasikia kwa wenzangu yaliniuma sana, na yamezidi kunitonesha moyo wangu…nikaona nije tuongee, na tuone ni jinsi gani tutaweza kusaidiana,kama tulivyoongea siku ile…’akasema na mama akanionyesha ishara kuwa niwe makini.

‘Ndivyo ilivyo, yote namwachia mungu….’nikasema nikisita kuongea sana.

‘Mimi nilijua mapema, kuwa itakuwa hivyo kama nilivyongea na wewe siku ile, ni hii sio kwmba labda unaonewa, hapana, yote ni kwa vile huna ushahidi wowote wa kulinda hoja yako, itamuwia vigumu hakimu kukupatia haki yako kwa hali kama hiyo, na ukiangalia wenzako walikuwa wamejiandaa kwa kila kitu..’akasema.

‘Lakini haki ya mtu haiendi bure, hata  kama watashinikiza na kupata mali ya dhuluma, ipo siku itawatokea puani, mimi nina imani kuwa haki ya mtu haiendi bure….’akasema baba.

‘Mzazi wangu, hizo ni imani za kujipa moyo, na bora kuwa na imani hiyo ila wenzako hawayaangalii hayo….na imani kama hiyo hata wao wanayo, kuwa kila mtu akipata kapata kwa uwezo wa mungu na ni haki yake kupata, hata kama kadhulumu, wanakuambia kwanza kupata, mengine ni majaliwa…kwahiyo ukiomba omba ukiwa na wewe unajituma na kujisaidia, usilale huku unaomba upate chakula, …kweli utakipata, hapana ni mpaka utoke, ukitafute…ukiomba wakati mwenzako keshapata, inakuwa kama dua la  kuku kwa mwewe….’akasema.

‘Sasa kama tutakuwa tunafanya hivyo, yaani dunia ikiwa ni ya kudhulumiana, kuwa yule mjanja ndiye mshindi hata kama sio haki yake, unafikiri kutakuwa na amani kweli, maana kama mimi nimeshindwa na nina uhakika kuwa hiyo ni mali yangu..kwa vile tu sina huo unaoitwa ushahidi kutokana na uchakachuaji wa ujanja, huoni kuwa ninaweza kufanya lolote….’akasema mama.

‘Mama,….wenzako wamesimamia kwenye sheria, ina maana lolote utakalolifanya litakuja kukuleta matatizo baadaye, maana sheria itawalinda, …cha muhimu wewe ni kujipanga, na kuhangaika kutafuta ushahidi, maana upo, haiwezekani ufanya jambo, kusiwepo na ushahidi, cha muhimu ni kujaribu kutafuta wale wanaojua sheria, …wao mawakili, hawa ukiwaeleze ajinsi ilivyokuwa, watajua jinsi ganii ya kusaidia.’akasema.

‘Lakini hayo yanahitaji pesa,….huwezi kumtafuta wakili, aje ajitoee, , yeye kwake hiyo ni ajira, ….na ukiangalai kesi hii ilivyokaa, inawezekana kabisa, wameshauharibu ushaidi uliopo wa kutusaidia , mimi naona sheria hizo zimewekwa ili kuwasaidia wenye nacho ni sheria za kutetea dhuluma, kama sheria ndio hivyo, basi haina haja ya kwenda mahakamani…’akasema baba.

‘Tatizo sio mahakama, tatizo ni wewe unayedai haki yako, je una viambatishi vya kuhakikisha kuwa hiyo ni haki yako,…nakupa mfano mdogo tu wa maisha yetu, wengi tunapokwenda kununua vitu madukani, hadai kupata stakabadhi , kitu ambacho ni haki yako, kwahiyo hata likitokea tatizo huwezi kwenda kulalamika kuthibitisha kuwa wewe ndiye uliyenunua hicho kifaa mahali  hapo…lakini kama ungelikuwa na stakabadhi, huwezi kudhulumiwa, huo unakuwa ni ushahidi wako,….ni vitu unaviona ni vidogo, kama hakuna tatizo, lakini kukitokea tatizo utauona umuhimu wake….’akasema.

‘Kwahiyo una maana nikinunua majani sukari, hivi vitu vidogo vidogo tunavyonunua kila siku nahitajika kupewa stakabadhi, ..huoni ni kupoteza muda, na hata hivyo hawo wenye maduka nao watakuwa na muda gani wa kukuandikia hiyo staakbadhi, pipi, stakabadhi, majani, stakabadhi….watu wenyewe hata kuandika ni shida…..’akasema mama.

‘Ni muhimu kufanya hivyo, kama umenunua vitu vidogo vidogo vingi, vyote hivyo vinaandikwa kweney staakbadhi moja, ndivyo ilivyo, maana hiyo pia inawasaidia watu wa ushuru, wakija kwenye maduka, wanahitaji kuangalia hizo stakabadhi, kwa ajili ya malipo ya kodi, kwahiyo, kitu kama hicho kina manufaa sio kwako tu, lakini pia kwa maendelea ya taifa letu….ni taratibu ambazo tunazizarau kwa vile labda hatujakuwa na utaratibu mzuri na tabia hiyo ya kuweka kumbukumbuku, lakini kukiwepo na utaratibu mnzuri, na sisi wateja, walaji tukawa makini kwa hilo,….kutakuwa hakuna matatizo tena, na wote tutakuwa tunaijenga nchi yetu….’akasema.

‘Sasa sisi watu wa chini, watu wa huku kijijini tutajuaje hayo,na elimu yetu ni ya chini ya mwembe, ukiangalia hata hizo stakabadhi wameandika kwa kiingereza…wakati sisi lugha yetu ni ya Kiswahili, wengine hata hicho Kiswahili ni shida kwao wanajua lugha zao za asili,…..huonio kuwa hayo mambo yamewekwa kuwalinda wajanja…?’ akasema baba.

‘Ni kweli tatizo ni elimu, na huenda hilo la ukosefu wa elimu limefanywa makusidi ili werevu wapate kufaidika na wasio soma wapate kudhulumiwa,….unafikiri kama tungekuwa na wakili, kweli kesi kama hiii tungelishindwa, n kwakuwa hatuna wakili, hatuna pesa za kumpata wakili, na elimu yetu ya kutambua ni nini tufenye ..basi tena..’akasema mama.

‘Wazazi wangu,….mimi sijakubali kushindwa, hata kama sina hiyo elimu inayotakiwa, lakini nina elimu yangu ya asili ya kutambua kuwa hili ni jema au hili ni baya, nina elimu ya kutambua kuwa hii ni haki au hii sio haki yangu, tatizo ni jinis gani ya kumshawishi mtu mwingine kuwa ninachodai ni haki yangu, kwa vile nafsi za wengi zimejaa ubinafsi na dhuluma….’nikasema na huyu mgeni wangu akawa anatuangalia kila mmoja akitoa maoni yake na kama kawaida yake macho yake yalijaa huruma,….inaonekana hiyo ndio tabia yake.

‘Ndugu yangu, wazazi wangu, kama nilivyowaambia kuwa huenda sisi wenyewe ndio tunachangia haya yote, na hii itawafanya hawo werevu kuwachukulia haki zenu. Kwasababu watu wengi hawataki kujua kuwa haki japokuwa ipo, lakini inahitjia kuipigania, sio kila kitu kinakuja kama mvua, na hata mvua ukiwa umeharibu vyanzo vyake, itaadimika. Kwanini hatujiuliza kuwa, kuna tatizo gani tukifuata utaratibu, ….’akatulia akiwa kaangalia chini.

‘Ni  kwanini tunazarau kufuata utaratibu wa mambo mengine ambayo yapo wazi, mimi sioni kwanini mtu usidai kitu kama stakabadhi….au upo ndani ya daladala unalipa nauli hudai tiketi yako,…baadaye linatokea tatizo unashindwa kudai haki yako..haya ni mambo mdogo tu yasiyohitajia elimu kubwaa…jamani hali ilivyo sasa,tunahitaji tubadilike. ….’akasema huyo wakili sote mle ndani tukawa tumetulia kumsikiliza.

‘Sasa mimi nimekuja, pamoja na hayo, lakini kama nilivyoongea na ndugu yangu huyu, nilimuelezea kuwa nitajitahidi kutafuta uwezekano wa kumsaidia, lakini kama ujuavyo, mimi nipo ndani ya hiyo familia, hata hivyo, mimi ni mwanasheria, kama mwanasheria nihitajika kutumia ujuzi wangu huo kuhakikisha sheria inatekelezwa, kwa haki, ……….’akatulia kidogo.

‘Mimi niliporudi Dar, nlijaribu kufuatilia tena kule kwenye hiyo kampuni, nilihangaiak sana, nia na lengoo langu, lilikuwa kama inawezekana kumpata huyo aliyekuwa mkuu wa hicho kitengo wakati huo, na japokuwa waliweza kumpata, …lakini ikawa vigumu kwa huyo mtu, kusema lolote, kwa vile kumbukumbu zote zilibakia humo humo kwenye hiyo kampuni, hakuondoka nazo…hata hivyo, nilimuomba afanye kila iwezekanavyo, awaombe wenye hiyo kampuni, atoe msaada wake…’akatulia.

‘Tatizo ni kuwa mtu anapoondoka kwenye kampuni husika , haruhusiwi tena kufanya lolote kwenye hiyo kampuni, na ukizingatia kuwa huyo mtu alikuwa ameshaajiriwa kwenye kampuni nyingi, asimu kibiashara na hiyo kampuni tunayoizungumzia….’akatulia

‘Ndio maana narudi pale pale, kuwa unapofanya jambo la kibiashara, kulipa pesa au kupokea pesa, huwa mara nyingi unahitajika kuwa na stakabadhi na kampunii kubwa kama hiyo , isingeliweza kutoa pesa nyingi kama hizi bila kuwa na kumbukumbu za malipo….na hilo ndilo limenipa hamasa ya kufuatilia…’akatulia.

‘Sasa cha ajabu…..nilichokiona ni kuwa kwenye kumbukumbu hizo jina lako halikuwepo….ni kwanini?’ akauliza.

‘Kama nilivyokuambia,…nilihitaji nipate hizo pesa, kwa haraka, na niliwaomba, wafanye iwezekanavyo, ili nipata hizo pesa, hata kwa kusimamiwa na mtu mwingine…sikujali mambo ya stakabadhi..na hata nilipopewa hiyo stakabadhi, sikujali kuangalia ni nini kilichonadikwa….mawazo hayo sikuwa nayo…sasa hivi ndio wazo hilo linanijia,….kwakweli sikumbuki, kuangalia jina kwenye hiyo stakabadhi kama kweli liliandikwa langu au….sikumbuki kabisa…’nikasema.

‘Lakini ulipewa stakabadhi ya kuonyesha kuwa umepoeka pesa….?’ Akauliza.

‘Ndio nilipata….na nikaja nayo, na hiyo pamoja na kumbukumbu nyingine walizonipa nilihifadhi kwenye mkoba wangu, ambao ni mkuukuu…niliuweka kwenye kabati, na vitambulisho vyangu vya kupigia kura…lakini havipo tena,…’nikasema.

‘Hapo ndipo nahisi kuna jambo limejificha ndani yake….maana hata nilipokutana na huyo jamaa, na nilipomwelezea hilo, nilimuona akisita, na hata alipokumbuka, alikuwa hapendi kabisa kunisaidia,…nahisi kuna kitu kimefanyika,….lakini sijakata tamaa, kwani baada ya kuona hivyo, ikanibidi niwasiliane na vyombo vya usalama, ili wafanya uchunguzi…’huyo mwanadada akatulia.

‘Oh, wanaweza kukubali kufanya uchunguzi kwa tukio kama hilo?’ baba akauliza.

‘Ndio kazi yao….lakini unahitajika uonyeshe dhamira ya kweli kwao,…mimi ni wakili, na mawakili wanakuwa na dhamana kisheria, kwahiyo nilipowaambia , waliona kuwa lina umuhimu, hata hivyo yupo mwanausalama mmoja naelewana naye, amekubali kulivalia njuga…’akasema.

‘Oh,ndugu yangu nitashukuru sana, lakini nitawalipa nini, maana hali yenyewe unavyoiona, sina mbele wala nyuma, hata duka ambalo nililitegemea, siwezi kufanya lolote tena, …..limefungwa eti kwa vile lipo kwenye migogoro, …’nikasema.

‘Hiyo haiwezi kukuzuia kufanya biashara yako, kwa vile ndio sehemu inayokupatia riziki, ….kwa vile nimeamua kukusaidia kutokana na jinsi mambo yalivyojitokeza, nitajitahidi upewe kiabli cha kufanya biashara…’akasema.

‘Huoni ukifanya hivyo, utakuwa umeisaliti familia yako?’ nikumuuliza.

‘Usijali….imebidi iwe hivyo, maana mwenzangu hanielewi, yeye kaweka ufamilia mbele, na kuiweka sheria nyuma…hilo tumeshindwa kukubaliana , na hata uchumba wetu umeshaingia doa…sijui kwanini…labda, akini hilo tuliache kwanza.’akasema na kuonyesha uchungu fulani kwa kukunja uso..

‘Ina maana wewe na mchumba wako hamuelewani tena?’ nikamuuliza.
Akainama na kuangalia chini, baadaye akawa kama kajishitukia na kuniangalia machoni, na hapo akaniuliza ;

‘Nikuulize swali, na naomba unijibu kwa usahihi, maana nimeshaamua kukusaidia, na kwa ajili hiyo, huenda uchumba wangu na mwenzangu ukaisha…japokuwa oh,…., lakini niliyoyasikia yamenikera sana, sijawa na uhakika wa moja kwa moja, ila sikio halina kizuizi, ….napenda nikuulize swali muhimu sana…’akatulia huku akiwa ameniangalia machoni.

‘Uliza tu mpendwa…’ aliyesema hivyo alikuwa ni mama, mimi nilikuwa nimeduwa, uwoga ulikuwa umeshaanza kuniingia sijui kwanini...

‘Je kama ni lazima ili tuweze kufanikiwa kwa hili, kama kutakosekana huo ushahidi ninaoutafuta ambao ni muhimu sana….na ikabidi tutafute njia nyingine, na njia zipo nyingi za kutafuta haki yako, na nyingine sio za moja kwa moja, lakini lengo ni kutafauta njia ya kupata haki yako.

Mimi niliwaza sana wazo hili, nikaona nisiwe machoyo, maana hata hivyo, naona mambo yameshaharibika,….kuna njia moja iliyobakia ambayo ni kujitoa muhanga , hata kama hupendi, lakini inabidi, ili tuweze kushinda, …..’akatulia huku akionyesha ujasiri fulani.

‘Nasema hivyo, kwa vile nimeamua kukusaidia na hii ni njia nyingine mbadala ya kupata ushahidi na kupata haki yako,..hii ni njia ya kupitia kukubali kurithiwa….nazungumza hili kwa vile nina ushidi kuwa kama utakubali, tunaweza kuvipata hivyo vitu…na ikibidi, itakuwa njia nyingina ya kupata ushaidi tunaouhitajia, unaweza kukubaliana na wazo hili?’ akauliza na kunifanya nishituke, yeye akawa nusu anatabasamu, nusu haeleweki, lakini alionyesha kuniangalia kwa shauku

Sauti yake ilionyesha udhabiti, kuashiria kuwa alikuwa na uhakika na alichokisema, …na kwasaabbu hiyo nikawa na wasiwasi kuwa huenda wazo hili likawa na uzito mkubwa,….sikutarajia kuwa hata huyu mwanadada mwanasheria angelikuja na wazo kama hili…kichwani nikawa namuomba mungu anipe wasaa wa kutoa jibu, litakalokidhi haja, na isiwe jibu linataliniweka kubaya. Nikawageukiwa wazazi wangu, ambao na wao mwanzoni walinipa wazo hilo…

Baba na mama wakaniangalia, kila mmoja akiwa shauku ya kusikia kauli yangu, sikurizika na macho yao, nikaona wao wanaweza wakakubalina na wazo hili hata kunishinikiza nikubali kurithiwa, ….na hapo nikajaribu kumvuta huyo anayehitahika kunirithi, je niatweza kishi naye, je nafsi yangu  ipo razi naye,….je kweli nampenda..

‘Nilishangaa kwanini kila ninapokutana na huyo jamaa, nafsi yangu inakuwa kwenye hisia zisizo za kawaida, siwezi kuziita kuwa ni kupenda, hapana, sijawazia jamboo kama hilo, ila kila nilipobahatika kuonana naye moyo wangu ulikuwa ukienda mbio….lakini baada ya siku ya ile kesi, moyo wangu ulishaingia kutu, ila hali ya ya moyo kwenda mbio ilibadilika na kuwa chuki,…..na kama ningelikuwa na uwezo wa kufanya jambo, baya, basi nisingelisita kufanya hivyo kwa mtu kama huyu.

‘Nikageuza macho yangu na kumwangalia huyo mwanadada, ambaye alikuwa kaniangalia moja kwa moja machoni, ….lakini cha ajabu macho yetu yalipokutana kwa sasa nilichokiona machoni kwake ni ukungu wa machozi, yaliyokuwa yakitaka kutoka,…na alipoona hivyo, akachukua leso yake na kujifanya anajifuta usoni, kumbe alikuwa na nia ya kuiondoa ile hali machoni mwake, mimi bia kujijua zaidi nikajikuta niongea hivi ….

‘Hapana , siwezi kukubali kurithiwa, kamwe, hata kama kwa kufanya hivyo, kungesaidia kufanikiwa kupata haki yangu, ..kamwe….sitaweza kudai haki kwa kuuza utu wangu…..’nikasema na upande wa pili wa wazazi wangu , nikawasikia wakipumua,lakini sikupenda kuwageukiwa, macho yangu yalikuwa yanamtizama huyo mwanadada, na akacheka kidogo, kicheko cha kuonyesha kushangaa, halafu akawa kama hataki kuniangalia machoni, akasema;

‘Ahsante sana,…..’ Sikuelewa kwanini kasema Ahsante…nilijaribu kumwanmgalia machoni, lakini hakunipa mwanya huo, akainuka na kuanza kuondoka, bila kusema kwaheri, na alipofika mlangoni, akawageukiwa wazazi wangu akasema;

‘Hongera wazazi wangu,……kweli mnajua kulea, ….’halafu akanigeukia na kusema;

‘Tutakutana mahakamani..’akasema huku akianiangalia kwa macho makavu, ambayo usingeliweza kujua ana nia gani, ya amani au ya shari…akaondoka.

NB: Ndivyo ilivyokuwa je, itakuwaje..?


WAZO LA LEO: Hali jinsi inavyozidi kuwa ngumu, kila mmoja anajaribu kupata, kwa njia nyingi, na nyingine zisizo za halali. Na kwa hali hii , ule utofauti wa walionacho na wasio kuwa-nacho unazidi kuwa mkubwa, ubinadamu unakuwa ni jambo adimu, watu wapo tayari kudhulumu, kudanganya, kuhonga, ilimradi wapate, na wakipata wanatafuta mwanya wa kuhalalisha kipato chao hata kwa kutumia maandiko matakatifu, swali langu ni kuwa je tunamdanganya nani….
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Justin Kasyome said...

duh!leo nimepata kkitu baada ya kusoma kisa hiki..big up sana...