Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, June 7, 2013

WEMA HAUOZI-18


Kama ilivyotarajiwa na wengi kesi hiyo haikuwa nzuri kwangu, na wanasema wahenga, siku njema huonekana kuanzia asubuhi, na mimi siku hiyo nilishaanza kuiona kuwa haitakuwa na jema kwangu. Akili yangu ilikuwa haitulii, na moyoni nilikuwa na wasiwasi,…

Nilipokuwa tayari nimeshajiandaa mara simu yangu ikaita, ….nikashituka utafikiri sijawahi kusikia huo mlio kabla, nikaitoa hiyo simu kwenye mkoba wangu, na kuangalia mpigaji ni nani, alikuwa ni nesi, huyu nesi nilimuomba awe karibu na baba yangu wa kufikia, nilimuomba awe akimhudumia baba yangu huyo,na kama kuna tatizo lolote aweza kuniarifu kwa haraka,…

Baba yangu huyo wa kufikia bado alikuwa kalazwa, mkono wake ulikuwa umefungwa mhogo(POP),na sehemu ile aliyochomwa kisu, ilikuwa imeshonwa, lakini alikuwa akidai ubavuni, alikuwa akipata maumivu makali, kwahiyo wakawa wamempiga picha ya X-ray, na walikuwa wakisubiria matokeao yeka, na kutokana na hiyo hali, bado alikuwa amelazwa hapo hospitalini. Tulitarajia kuwa huenda wiki hii angeliruhusiwa, lakini dakitari akashauri kuwa abakia siku mbili zaidi akisuburia majibu ya vipimo alivyochukuliwa.

Nikaichukua simu yangu kwenye mkoba, kwani nilishaiweka ndani ya mkobwa wangu, tayari kwa safari ya kuelekea mahamani. Nikasubiri kama huyo nesi anabipu, au anapiga, na nilipoona simu inaendelea kuita,nikaamua kuipokea, nilihisi mapigo ya moyo yakiongezeka, kwa wasiwasi, nikaanza kuhisi vinginevyo, …na hisioo hizo zikanifanya nikae kwenye kiti wakati naiweka hiyo simu hewani.

‘Halooh,…’nikasema kwa sauti ya mashaka.

‘Ni mimi nesi hapa napiga simu kutoka hospitali ya mkoa,….’akasema.
 Huyo nesi alisema jana usiku mgonjwa hali yake haikuwa nzuri, ..lakini leo asubuhi kidogo mgonjwa ana nafuu, ila kaagiza kuwa ananihitaji mimi niende tukaonane naye kwa haraka sana.

‘Nesi ningelikuja maana sijui kwanini ananihtajia hivyo , lakini nahitajika mahakamani, leo ndio siku yetu ya kesi yangu..’nikasema na Nesi akasema atajaribu kumweka sana.

‘Kwani unamuonaje…yupo katika hali mbaya kiasi gani?’ nikamuuliza.

‘Usiku ndio ilikuwa na hali mbaya sana, joto lilikuwa kali sana mwilini, na kwa vile tulishachukua vipimo vya damu, na picha ya x-ray tutaangalia tatizo nini, huenda ni malaria au inawezekana ni athari za ndani kwa ndani, kwa hivi sasa joto halipo tena, na halalamiki kusikia maumivu tena, sasa hivi anasema vyote vimatulia…kwahiyo hali yake sio mbaya sana, lakini ilibidi nifikishe ujumbe wake kwako maana kasisitiza kweli…’akasema

‘Basi tutaangalia jinsi gani tutakavyojipanga, na nashukuru sana nesi….’nikasema.

‘Usijali, tupo pamoja, nakutakia kilalaheri…’akasema huyo nezi.

Baadaye niliongea na wazazi wangu, ikabidi tugawane, nikamwambia baba yangu mzazi ni bora yeye apitie huko kwa mgonjwa akaone kuna tatizo gani, halafu yeye akitoka huko tukutane mahakamani, kwani na yeye anaweza kuhitajika kama shahidi. Kwakweli moyo wangu haukuwa na amani tena, kila mara nilikuwa nikijiuliza kwanini baba yangu huyo ananihtaji kwa haraka kiasi hicho, kuna nini, je ni kutokana na kuumwa kwake, au kuna jambo jingine ….

Au kuna jambo jingine linalohusiana na hiyo kesi, kwani alikuwa anafahamu fika kuwa siku hiyo ndio siku ya kesi yangu, na alishanipa baraka zake,…..sasa kuna nini…. nikawa najiuliza maswali mengi bila kupata majibu.

*********

Tuliingia mahakamani na kesi ikaanza, kwasababu sikuwa na wakili, ilibidi nisimame mwenyewe kujielezea, na niliposimama watu walikuwa wametulia, wakinitizama kwa shauku, nilishangaa kuona watu wengi hapo mahakamani, sikujua ni kwasababu ya kesi yangu au wamekuja kwa kesi nyingine, sikujali hilo, nikajipa moyo na kuanza kutoa maelezo yangu, na baada ya kumaliza maelezo yangu, sikutaka kuongea mengi sana, nilifupisha kadri ya uwezo wangu,…

Hakimu akauliza kuwa nina uthibitisho wowote au shahidi yoyote, kuthibitisha maelezo yangu, nikasema kwasasa sina……

Nikafikia mwisho wa maelezo yangu na hakimu akaruhusu maswali, na aliyeanza kuja kuniuliza maswali alikuwa yule yule mwanasheria wa familia ya mume wangu.

Kwakweli maswali yake yalinifanya watu wanione mimi ni tapeli, niliyejitungia mwenyewe mbinu za kupata nyumba, na duka,….na baadaye nikahitajika kutoa mashahidi na ushahidi nikawa sina. Zamu yangu ikaisha, na ikaja zamu ya washitakiwa,…kwakweli walikuwa wamejiandaa na kwa vile walikuwa na mtu anayefahamu ni nini anachokifanya, nikaishiwa nguvu na kukata tamaa kabisa.

Huyo mwanasheria wa familia, ambaye alisimama kwa niaba ya familia, alianzia mbali, na kwa kujiamini, na akafikia sehemu akasema;

‘Muheshimiwa hakimu, mimi ni ndugu wa marehemu, na nilikuwa nikifika mara kwa mara nyumbani, na kipindi alipofungwa, nilikuwa masomoni nje ya nchi, kwahiyo sikuweza kuja kuona ni nini hasa kilitokea, na kama ningelikuwepo, natumai ukweli halisi ungejulikana mapema, kwani ukweli huo ulikuja kujulikana wakati keshatumikia kifungo…...’akatulia na kumwangalia hakimu ambaye alikwa akindika kitu kwenye makabrasha yake.

‘Ndugu hakimu, ndugu yangu huyo alipotoka kifungoni, alikuwa mgonjwa, na baada ya uchunguzi akapatikana kuwa kaambukizwa kifua kikuu, …na akaanza matibabu, lakini hali yake ilizidi kuzorota, kama unavyojua kuwa ugonjwa huo ili dawa zifanye kazi vyema unahitajika kufuata masharti , ikiwemo kutokunywa pombe na kuvuta sigara. Lakini kutokana na hali ya msongo wa mawazo,na kukosa mshauri wa karibu, akawa anavunja hayo masharti, na dawa zikawa hazifanyi kazi yake ipasavyo. Mimi kipindi hicho nilikuwa nimesharudi, kwahiyo nikafika kuonana naye….

‘Kwakweli hali yake ilikuwa ya kusikitisha, maana inavyoonekana, pamoja  na kuwa alishagunduliwa tatizo ni nini, lakini kuna mambo mengi alihitajika kutendewa, kama vile kupewa ushauri nasaha, kupata lishe bora na ukarimu,…..kwa udadisi wa haraka, sisi kama wnafamilia tuligundua kuwa hakuwa akipata mambo hayo ipaavyo, maana unaweza ukakaa na mgonjwa usijue kumliwaza, na badala yake ukatumia lugha ya ukali, shuruti na kukatisha tamaa. Ndugu yangu huyo kwa ahli aliyokuwa nayo, na kutokana na mitihani aliyokuwa nayo, alihitaji ushauri nasaha ikiwemo lishe ….’akatulia.

‘Basi tulishauriana jinsi gani ya kumsaidia, na tukaonana naye ili kumpa ushauri wetu, lakini mwenzetu huyo hakukubaliana na wazo letu moja kwa moja, kama mume alihitaji kuongea na mkewe…lakini tulipokutana naye baadaye, tulishangaa akisema hawezi kuondoka kwake na kuitelekeza familia yake. Lakini hata hivyo sisi kama ndugu ilibidi tupate njia nyingine mabadala, tukashauriana kuwa mmojawetu awe pale nyumbani kwa marehemu,ili kutoa msaada wa karibu, na hapo tukamchagua mmoja wa ndugu zetu, …..mdogo wetu wa kike, ili awe anafika na kutoa huduma zinastahili.

‘Siku moja, nilifika tena kuja kuwaona, mara nyingi ninapofika yeye huja kwenye makao ya familia yetu, kwa kaka yetu mkubwa, siku hiyo aliniambia kuwa anahitaji msaada wangu, nikamuuliza msaada wa nini, akasema kuwa wao sasa hivi wana nyumba na duka, na amejitahidi hadi hivyo vimemilikishwa kwa jina lake, lakini bado hana uhakika na usalama wa mali hizo kwa baadaye..

‘Kwa baadaye kwa vipi, bro, maana umeshamilikisha, hapo huhitajii kuingiwa na wasi wasi tena…’nikamwambia, na yeye akasema;

‘Kama unavyoona hali yangu, sitarajii kuishi muda mrefu tena,….maisha yangu yalimalizikia jela, na yaliyotokea yamenivunja nguvu na sina raha….kwahiyo naona kuna haja ya kufanya jambo kwa ajili ya mtoto wangu…’akasema hivyo

‘Nikajaribu kumliwaza, maana alivyokuwa akiongea, ilionyesha kuwa keshakata tamaa ya kuishi, kwani alikuwa kama anatoa usia, wa jinsi gani mali yake itakavyogawanywa, na alitaka hayo niyaweke kisheria, basi mimi nikamwambia kama ni hilo halina shida, kwanza inabidi yeye mwenyewe aandike kwa mkono wake, aweke na sahihi, halafu nitamtafuta mwanasheria kuja kusimamia, sikutaka mimi nifanya kila kitu

‘Siki hiyo sikulichukulia maanani, nikaondoka, na siku kadhaa,akanipigia simu kuwa keshaandika kila kitu, nimlete huyo mwanasheria, na sikutaka kumvunja nguvu, nikamtafuta mwanasheria, tukafika naye, akatuonesha hiyo barua aliyoandika, ambayo ilielezea jinsi gani anataka mali yake iwe kama akifariki.

‘Ndugu hakimu, mimi niliona ajabu kubwa, maana mali yote aliindikisha kwangu, na msaidizi wake awe ni mdogo wangu wa kike,  nikamuuliza, kwanini anafanya hivyo, wakati ana mke na mtoto…..’akasema;

‘Mila zetu mume akifariki, ndugu anaruhusiwa kumrithi mjane, na wewe nimekuona unafaa kumrithi mke wangu,…kwa vile wewe hujaoa, na pia mke wangu bado kijana, mtaweza kuishi naye bila wasiwasi, kwahiyo wewe utasimama badaa yangu,….sihitaji kumwandikisha mke wangu, ….ni kama mimi nilivyo, mbona kila kitu nimeandikisha kwa jina langu,…mke sijamuandikisha, kwahiyo itakuwa hivyo hivyo kwako, na nakuomba usije ukamtupa mke wangu,….na pili wewe ni mwanasheria, unaweza ukazilinda mali zetu…kwa ajili ya familia yangu, nakuamini sana ndugu yangu’akasema huku akimwangalia hakimu.

‘Ndugu yangu haya uliyoyaandika na mambo mazito, je uliwahi kuongea na mke wako?’ nikamuuliza.

‘Mke wangu sijaongea naye kiundani, hata hivyo, nimjuavyo mimi hatakubali , najua yeye ana msimamo wake, na nikimwambia haya anaweza akachanganyikiwa akashindwa kufanya shughuli zake, ambazo zinatusaidia kuishi, kwahiyo akasema kama litatokea lolote,..hatuombei hivyo, lakini mimi mwenyewe najiona, kila siku nakufa….nakuomba wewe ndugu yangu uwe ni msimamizi wa mali yangu, na sio msimamizi tu, lakini uwe m- miliki kwa niaba yangu, maana wewe ndio mimi….’akasema

‘Kwakweli muheshimiwa wakili, nilikataa mbele yake, sikukubali kubeba mzigo huo mnzito, ..kwasababu hayo yalikuwa msimamo wake, hajamshirikisha mkewe….’akasema na kutulia.

‘Lakini pia nilikuwa an sababu nyingine kubwa ya msingi ya kukataa…, kwasababu nilishasikia uvumi kuwa mali hiyo , yaani nyumba na duka, vilijengwa na mkewe, na mkewe aliwahi kusema kuwa alijenga na pesa aliyopata kutokana na ushindi wa promosheni ya moja ya kampuni za simu. Hilo nililiona linaweza kuleta utata baadaye.

‘Uvumi huo tuliwahi kuongea naye kabla, na aliniomba nifuatilie huko mjini, nione kuwa kweli aliwahi kupata hizo pesa, na nilijaribu kufanya hivyo, na muda alioniita, nilikuwa sijafanikisha huo uchunguzi, kwahiyo ombi lake, nikaliweka pembeni kwanza, ….Nilimwambia wazi, kwasasa sitaweza kukubali hadi hapo nitakapokamilisha uchunguzi wangu kuhakikisha kuwa kweli hayo anayozungumza mkewe ni ya kweli.

Niliporudi Dar, ikabidi nilifanyie kazi hilo swala, na nikawa nafika ofisi za kampuni hiyo, ambayo shemeji yangu, yaani mke wa marahemu anadai kuwa ndipo aliposhidia hiyo proimosheni. Ofisi hiyo haikuwepo hapo tena, na hata jina la kampuni hiyo halikuwepo tena, ila kwa vile nilifahamu kuwa kampuni hiyo zamani ilikuwa naitwa hivyo na baadaye ilikuja kuabdili jina na kuitwa kampuni nyingine, na ilikuwa na wamiliki wengine kabisa na hata wafanyakazi waliokuwepo kipindi hicho hawapo tena.

Ilikuwa kazi kweli kutafuta ukweli wa hilo …kuwa kweli shemeji aliwahi kushinda, na je kulikuwa na kumbukumbu zozote zinazothibitisha hilo…nikafuatilia..kwakeli muheshimiwa hakimu , sikuweza kuona ushahidi wowote kuwa yeye aliwahi kupata huo ushindi, ….na hata jina alke halikuwepo katika orodha ya watu walioshinda kwa tarehe hizo alizozitaja,….’akatulia.

‘Mimi kuona hivyo, nikawa na mashaka na shemeji, kuwa kama ameweza kutunga uwongo kama huo, inawezekana pia akafanya lolote kwa ndugu yetu, kwahiyo nikarudi , na kuonega na familia, na sikuongea na ndugu yangu huyo marehemu kuhusiana na hilo, maana ningelimwambia huenda ingelisababisha ugomvi kwenye hiyo familia,….mimi na kaka zangu tukajadiliana kama wanafamilia, inabidi tumsaidie ndugu yetu, ili kuona usalama wake na afya yake pia.

‘Kwa upande wa afya yake hatukuwa na wasiwasi tena, kwani ndugu yetu tuliyemtuma awe anamsaidia, alikuwa akifanya hivyo kwa karibu sana, na dawa na matunzo mengi tuliyatoa kwa kupitia kwake, na ilifikia hadi akaonyesha mafanikio mazuri,…

Lakini tatizo ilikuwa , pamoja na kuwa ndugu yetu yupo pale, lakini hawezi kuingilia maisha ya ndani ya wanandoa, na aliona kabisa, jinsi gani kaka yetu huyo marehemu alivyokuwa akigombana mara kwa mara na mkewe,…na ikitokea hivyo, yeye, yaani marehemu anakimbilia kunywa pombe na kuvuta sigara, vitu ambavyo ni sumu kwake….’akatulia na kumwangalia hakimu.

‘Hapo tukawa na mtihani mkubwa, je tufanyeje,…maana hatuwezi kumchukua ndugu yetu tukaishi naye, ikabidi tuwe tunamuelelekeza ndugu yetu, yaani mdogo wetu jinsi gani ya kufanya, kuwa kwa mfano akiona kuna ugomvi, ajaribu kuingilia kati, na kumuondoa ndugu yetu mbali, ili asizidi kuchanganyikiwa..

‘Lakini mume na mkewe,….huwezi kuwatenganisha, …na kilichokuja kutushangaza ni kuona ndugu yetu anakuwa kama kachanganyikiwa maana alifikia hatua sasa akifanya kila anachoambiwa na mke wake, …na tunaweza tukamshauri jambo, akakubali, lakini akifika kwa mke wake, anabadilika, na ilionyesha wazi kuwa kuna tatizo kubwa sana, na huenda limefanywa hivyo kwa malengo fulani….na kila ndugu yetu huyo alionekana mwingi wa mawazo, na yeye mwenyewe alidai kuwa ili kuondokana na hayo mawazo, ndio maana alikuwa akikimbilia kulewa, na kuvuta sigara, kitu ambacho kilizidi kumathiri kiafya…

‘Alipozidiwa sana, tuliamua kama wanafamilia kufanya kila iwezekanavyo tumchukue tukae naye, ili tuweze kumuhudumia wenyewe na kuhakikisha anafuata masharti yote, na matibabu muhimu kwakweli hali yake ilikuwa mbaya sana, na tunasikitika kuwa uamuzi huo ulifika kipindi tumeshachelewa….

‘Na utaona ajabu, siku huyo ambayo tuliamua kwenda kumchukua kwa nguvu,hata mke wake hakuwepo nyumbani, fikiria mgonjwa kama huyo, wewe kama mke, kama kweli unamjali mwenzako, usingeliweza kuondoka na kumuacha kitandani, hajala, hajasaidia kuogoshwa, maana ilifikia hatua kila kitu kinafanyika hapo hapo kitandani, ,……hali yake ilikuwa ya kusikitisha, na alipofika kwetu, haikuchukua muda akafariki ….tukampoteza ndugu yetu…’akasema kwa uchungu.

******

Mimi pale nilipokuwa nimekaa, huku nasikiliza maelezo ya huyo mwanafamilia, niliingiwa na hasira, machungu na kama isingelikuwa kuheshimu sheria za mahakama, ningelifika pale mbele nimzabe kibao huyo mtu na kumshushua kuwa ni mwongo mkubwa,... Sikuamini kuwa msomi kama huyo angeliweza kunitunga uwongo kiasi hicho,…sikuamini, yaani ina maana wema wangu wote niliufanya kwa mume wangu haukutambulikana…wangelijua jinsi gani nilivyokuwa nikiteseka na mume wangu, wasingelisema hayo, lakini ni nani atathibistiha hayo…

Nilijikuta nikitoa machozi kama maji,…. na hata muda wa maswali ulipofika sikujua niulize nini, hata hivyo nikajitahidi na kusimama na kwa hasira nikamuuliza;

‘Kama unadai hizo pesa sio za ushindi wa shindano hilo la promosheni, je pesa hizo zilipatikana wapi, na ni nani alijenga hiyo nyumba?’ nikamuuliza kwa hasira.

‘Ndugu yetu alituambia kuwa katika shughuli zake mbalimbali, aliweza kupata pesa nyingi, kwani walikuwa wakihangaika hadi huko milimani kutafuta madini, kwahiyo…kama ni biashara ya madini, huwa inatokea mtu akapata bahati na kupata pesa nyingi tu, yeye sio wa kwanza, wapo wengi hapa kijijini wamefanikiwa kwa hilo.

‘Yeye akawa miongoni mwa waliofanikiwa, na alipopata pesa,aliamua kwenda kuwekeza Dar, na alisema siku alipopata hizo pesa marafiki zake wakawa wanamundama wakitaka kumpora hizo pesa, basi akawa anaishi kwa mashaka kwa kujificha,…hakuwa na usalama. Na siku alipoamua kuondoka hapo kijijini ndio siku mliokutana naye na mkaondoka kwa siri,…….

‘Kwasababu alikuwa akikuamini sana, hakuwa na shaka na wewe, na uliweza kuona wapi alipokuwa kaweka peza zake, aliweka pesa hizo kwenye mkoba ambao alikuwa habanduki nao mkononi, na mtu pekee aliyekuwa anajua kuwa ana pesa ni wewe. Aliniambia kuwa mlipofika Dar, zile pesa zikawa hazionekani…na aliniambia akiwa na uhakika akisema;

Ndugu yangu sio rahisi mtu kuja kuzichukua hizo pesa, kwani nilikuwa nimezifunga vyema, kama nguo, na kuziweka kwenye mkoba, na huyu mtu aliyefanya hivyo, atakuwa anafahamu kuwa hapo niliweka pesa, na hakuna mwingine zaidi ya mke wangu…..’

‘Pesa zangu hizo nimezipata kwa shida, ..na nikikumbuka hilo, akili yangu haikai vyema, inanisikitisha sana, kwani ndio ulikuwa mtaji wangu wa maisha, na sasa wamenifunga, sina maisha tena, …..pesa zangu zimeibiwa, sitaki hata kuishi…’ndivyo alivyokuwa akiniambia akiw keshakata tamaa.

‘Kwa maneno haya unaweza kuona jinsi gani kuibiwa kwa hizo pesa kulivyomtesa ndugu yangu, na ana uhakika mtu pekee ambaye angeliweza kumuibia hizo pesa kwa jinsi alivyokuwa kazificha ni mke wake….’akasema na kumgeukia hakimu, na huku akiendelea kusema;

‘ Ndio maana tunaamini kuwa pesa ulizojengea nyumba ni hizo pesa ulizochukua kutoka kwa ndugu yangu…’akasema.

‘Mimi nilijua wasomi sio waongo, …..na sitakuamini tena katika maisha yangu….’sina cha kuuliza tena muheshimiwa hakimu…’nikasema na kuanza kulia, sikuwa na nguvu ya kuongea, sikuamini kuwa huyo mtu anaweza kunifanyia hivyo nikarudi na kukaa.

**********

Hakimu alipouliza ushahidi kwa upande wao,wakawa nao, kila kitu kikiwa kimejitosheleza kuthibitisha maelezo yake, hakimu alionekana kuniangalia kwa mshaka sana, ndivyo nilivyokuwa nikiwaza hivyo, kuwa hata hakimu aliniona mimi kama tapeli, basi baadaye hakimu alisema kuwa mimi mshitakiwa anhitajika kuleta ushahidi na vithibitisho kwenye siku iliyopangwa kusikilizwa tena hiyo kesi, na baada ya hapo, itasubiriwa siku ya hukumu

 Siku hiyo,… kila mtu pale ndani alioniona mimi kama tapeli fulani, hata sikuweza kuwaangali watu machoni, maana wengi, nilihisi walikuwa wakiniangalia kwa jicho baya, na hisia mbaya dhidi yangu, nikainama na kutoka nje, huku wakinifuatilia kwa akribu wazazi wangu.

Tulipotoka nje ya mahakama, yule mwanasheria wa familia akaja kuongea namimi, kwanza sikutaka hata kumwangalia, lakini baadaye niliona sio ubinadamu, nikataka kujua anahitaji nini kutoka kwangu, nikamskiliza;

‘Shemeji usituone kuwa labda hatukupendi,….sisi tunakupenda sana na hili tuliona lifanyike ili ujirizishe mwenyewe, kiukweli kama ulivyoona, hukuwa na hoja ya kudai hiyo nyumba kuwa ni yako, na mimi niliongea wazi yale aliyoniambia ndugu yangu, je unafikiria mimi ningelifanya nini kama ndugu yangu kaniambia haya yote, nikae kimiya, ndio huenda ningelikaa kimiya kama ungelitulia tukakubaliana. Lakini wewe hutaki, hutaki hata kunisikiliza….’akasema

‘Nyumba ni ya kwangu, duka ni la kwangu nimejenga kwa jasho langu, kama mumeamua kunidhulumu, sawa,..lakini bado nitaendelea kuvipigania hadi hatua ya mwisho…’nikamwambia.

‘Shameji kwanini unasema hivyo, …usijihangaishe kwa kupoteza muda wako bure, kwa kukata rufaa, ujue ukishindwa huko mbele, kuna gharama utahitajika kuzilipa, na pia kwanini tufike huko, mimi naona kwa vile umeshaona uhakika wa jambo lenyewe lilivyo, tuongee tukubaliane……kwasababu huna ushahidi wowote, ni nani atakuamini kwa hayo unayoyasema wakati huna hata kitu kimoja cha kuthibitisha hivyo….shemeji achana nayo, tushirikiane tu,….’akasema akiniangalia moja kwa moja usoni.

`Mhhh…’ halafu nikamnyaa, nikaangalai pembeni, huku nimeweka mkono kiunoni, utafikiri nimeshashinda kesi, na yeye akawa bado ananiangalia, halafu akasema;

‘ Shemeji mimi nakuhakikishia kama kweli ungelikuwa na kitu cha kunishawishi kuwa hivyo vitu ni vyako, nisingelichukua hiyo hatua niliyoichukua,…nilifanya hivyo baada ya kujirizisha, na kuona kuwa kweli hayo aliyoniambia ndugu yangu yana ukweli…..sasa kama unayo ushahidi wowote, au kuna njia yoyote ya kukuamini, kuwa hayo unayoyasema ni kweli, nionyeshe, mimi mwenyewe nitahakikisha kuwa vyote hivyo vinaandikishwa kwa jina lako, …’akaniambia.

‘Usitake kujitakasa hapa kwangu mnafiki mkbwa wewe, ….huna lolote, mwongo mkubwa wewe, nyie ndio mnaotumia elimu yenu vibaya, umefanya hivyo, kwa vile ulifahamu kuwa ushahidi niliokuwa nao, haupo tena…..mtu una elimu yako badala ya kujitahidi upate vya jasho lako mnakimbilia mbali za wenzenu,….hamtafanikia abadani’nikasema kwa hasira na kanza kuondoka.

‘Shameji tafadhali nisikilize kidogo, mimi nipo tayari kukusaidia, na hata kama hiyo nyumba na duka utahitajia niandikishe kwa jina lako ninaweza kuwashawishi ndugu zangu, tukafanya hivyo,lakini hilo sio rahisi kihivyo, ….nikupe siri moja, ili ufanikiwe hilo kwanza unahitajika ukubali kuwa mwanafamilia,…na ufuate kama alivyoagiza na ndugu yangu….mimi nipo tayari…..shemeji…’akasema na niligeuka na kumwangalia kwa macho yaliyojaa hasira.

‘Hilo la kujizalilisha kwenu,…ndivyo mnavyotaka,…?’ nikamuuliza, lakini sikumpa nafasi ya kutoa jibu nikasema;

‘Hata siku moja sitafanya hivyo…..kama ndio lengo lenu, mumenoa, tutapambana huko huko mahakamani…..’nikasema na yeye akaniangalia huku akitabasamu, hakuonyesha wasiwasi, ….alikuwa akijiamini kupita maelezo, na mimi nikageuka na kuondoka zangu
Tulipofika nyumbani, wazazi wangu wakaniuliza tufanyeje, kwani ilivyo, japokuwa hukumu bado,lakini inaonyesha wazo kuwa kesi tumeshindwa, kwahiyo tutafute jinsi gani ya kufanya…..na hapo nikawaambia, kama tutashindwa hapo inabidi tukate rufaa, kwasababu ninachodai ni haki yangu…

‘Hata kama tukikata rufaa, tutapatia wapi huo ushahidi, ….huoni kuwa huko tutakwenda kupoteza muda bure, na tutahitajika kulipa gharama?’ Akauliza mama.

‘Inabidi kwanza kuhangaike kutafuta huo ushahidi, kama kuna nyaraka zozote, …na kama tunaweza kumtumia mtu akajaribu kuzitafuta hizo nyaraka kwenye hiyo familia, nahisi kama waliiziba wao, na huenda ni huyo wifi yako, mliyekuwa mkiishi naye …’akasema baba.

‘Sina uhakika sana na hilo, nahisi waliziiba kipindi hicho nilipokuwa kwenye msiba, lakini wote hawo lao moja, hata huyu mchumba wa huyo mwanasheria wao, simuamini, na yeye alifika hapa jana, akajifanya kuwa anataka kunisaidia, nahisi hawa watu wanakuja kwa lengo la kupata taarifa, mwisho wa siku wanatuangamiza….’nikasema.

‘Cha mhumi ni kukata kabisa mguu nao kwa kutokuwa na mawasiliano nao, kama wakija ni wageni wakaribishe lakini chunga ulimi wako, usiwe na maongezi yanayohusiana nah ii kesi, na kama ikiwezekana usiwakaribishe ndani, achana nao kabisa….wote lao ni moja..’akasema mama.

‘Mimi nina wazo jingine, unajua kuna usemi usemao, adui yako mpende, …usemi huu una hekima kubwa sana, sisi hawa tuwe nao pamoja, na hao hao ndio tutawatumia kupata taarifa. Na nina wazo ambalo sijui kama binti yangu utakubaliana nalo…’akasema na kuniangalia kwa mashaka.

‘Wazo gani?’ nikamuuliza.

‘Huyo mwanasheria wao, anaonyesha kabisa kuwa amekupenda, sasa unaweza kumtumia huyo huyo ukayamaliza haya yote, kwa njia kubwa mbili, kwanza kwa kukubali kweli yeye akurithi uwe mume wake, na hapo utakuwa umekipata kila kitu…ni akili kichwani mwako, lakini pia kuna njia ya pili, ambapo unaweza kujifanya wewe ni mpenzi wake, na ukaweza kumshawishi hadi akabadili hati za nyumba na duka….sikufundishi vibaya mwanangu, lakini hizo njia pia zinaweza kutumika, kwa wakati kama huu ambapo, tupo vitani….au wenzangu mnasemaje?’ akasema baba.

‘Baba….hapana, mimi njia zote  hizo kwangu zisiziafiki maana ni za kuhadaa, ….kwanza baba mimi sipendi kuolewa kwenye hiyo familia tena, kama ni lazima ifanyika hivyo, na baba moyo wangu hautaki tena kuolewa, kabisaa…nataka niishi na mwanangu tu……hata hivyo, mimi ninachodai ni haki yangu , na ninataka haki yangu niipate kwa halali, sio kwa mbinu za kuhadaa….’nikasema.

‘Mimi kihalali nakubalina na hiyo hali, kihalali,…akini kwa hali kama hii, najiuliza kwa vipi, maana mahamani wanahitaji ushahidi, ..na sisi hatuna aina yoyote ya ushahidi, wala amshahidi ambao ni muhumi…na tunavyohisi ni kuwa ushahidi upo kwa hawo hawo maadui zetu….’akasema baba.

‘Mwanangu,…wakati mwingine unahitajika kutumia mbinu za kiujanja kama hizo, …mimi siwezi kuiona ni hadaa, ni medali za kivita,…ilimradi tu, usiwe na nia mbaya…vinginevyo, basi tena mwanangu sisi wazazi wako tupo, na sasa tupo tayari kuishi na wewe bila shaka…’akasema baba na kabla hajamaliza mlango ukagongwa na hodi ikasikika.

Ilikuwa ni sauti ya kike, …ya yule mchumba wa wakili…

NB: Je itakuwaje? Ndio hivyo, …..tunajikongoja, ipo siku tutaweza….wengi wananishauri nikamilishe vitabu,….mambo magumu! Hata hivyo tupo pamoja,


WAZO LA LEO: Hivi ni lazima kudanganya ili kupata haki yako, haki ni haki haipatikani kwa ujanja, kwa kufanya hivyo ni sawa na kufua shati jeupe kwa maji machafu.
Ni mimi: emu-three

5 comments :

Justin Kasyome said...

lol! kaz kweli kweli! haya ngoja tuone itakuwaje il akweli haki haipatikani kwa ujanja ujanja lazima kuwa straigth!

Yasinta Ngonyani said...

kisa kinakolea na kusisimua safi sana...nasubiri

Anonymous said...

Hello! I could have sworn I've been to this blog before but after looking at many of the articles I realized it's
new to me. Regardless, I'm certainly delighted I found it and I'll be book-marking it and checking back often!



my blog post ... how much is an e cig

Anonymous said...

Thanks designed for sharing such a fastidious idea, article is pleasant,
thats why i have read it entirely

My web-site :: electronic cigarrettes

Anonymous said...

fantastic put up, very informative. I ponder why the other experts of this sector don't realize this. You must continue your writing. I am confident, you've a great readers' base already!

Look at my page e cig brands