Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, May 7, 2013

WEMA HAUZI-4‘Siku ya kwanza ilikuwa ngumu kwetu mwanangu, maana ilibidi tutafute sehemu ya kujibanza, ili angalau tupate usingizi, mbu, wakawa wageni wetu, baridi lilikuwa kali kweli …ukumbuke mimi ndio nilitoka kujifungua kwahiyo bado nilikuwa na maumivu ya kujifungua.

Kama nilivyokuambia kuwa yule mtu niliyekuwa naye alikuwa kava kofia pana, na mawani makubwa na alikuwa na mandevu mengi, kwahiyo sikuweza kumgundua haraka kuwa ni nani, …lakini yeye nilihisi kuwa alishanigundua hasa pale tulipoanza kuongea;

‘Unasema umejifungua mtoto,…mtoto gani ?’ akaniuliza.

‘Mtoto mwanaume….’nikamwambia.

‘Baba yake ni nani?’ akaniuliza huku akionyesha kuwa makini sana, lakini alikuwa haniangilii moja kwa moja, kama vile anaona aibu kuniangalia machoni.

‘Baba yake kamkataa, kasema hiyo mimba siyo yake…kwahiyo …ndivyo ilivyokuwa,…’sikutaka kumuelezea zaidi, lakini alizidi kunidadisi

‘Unahisi ni kwanini aliikataa hiyo mimba ?’ akauliza.

‘Sijui,..labda aliogopa kuwajibika, maana mimi simjui mwanaume yoyote zaidi yak wake yeye, na mungu wangu ni sahidi..’nikasema.

‘Oh, lakini kila mtu anapenda kusema hivyo, hata mwizi akikamatwa, anaapa na kuapa kuwa mungu wak ni shahidi, huenda anahisi una mahusiano na mtu mwingine..’akasema.

‘Hiyo ni shauri lake, ahisi anavyotaka yeye, lakini mimi nina uhakika huo, kwasababu sikuwahi kuwa na mwanaume mwingine zaidi yake, yeye ndiye aliyenifundisha hayo yote, sikuwa nayajua…’akasema mama

‘Sasa ukikutana naye tena utasemaje, …?’ akaniuliza.

‘Sina haja naye tena, …tatizo ni kuwa, nimemtelekeza mwanangu,…sasa sijui itakuwaje?’ mama akaanza kulia.

‘Huo ni uzembe wako….utaondakaje umuache mtoto mchanga peke yake, …sijawahi kusikia mama aliyejifungua karibuni akimuacha mtoto wake, wewe ndio wa kwanza…..huna huruma na kichanga, hapana, lawama zote zitakushukia wewe…’akasema huyo mwaname akionyesha kinilaumu kupita kiasi.

‘Sasa ndio unanilaumu mimi, ..isingelikuwa kuahangaika kukuokoa wewe, nisingelifikwa na haya yote…lakini kweli ni kosa langu, sijui kilisnishiak kitu gani, hadi nikaondoka pale, na kumuacha mwanangu, …nitajilaumu sana, kama mwanangu atazurika kwa lolote lile..’akasema.

‘Nasikia mwanamke akijifungua anatakiwa kukandwa na maji ya moto, sasa ni nani atakukanda?’ nikashangaa akiniuliza hivyo.

‘Sijui, na wala sijali tena…mimi hapa nilipo nataka nipate nauli nirudi huko nilipomuacha mwanangu..’nikamwambia huyo jamaa.

‘Sawa ngoja kupambazuke tuone kazi gani tunaweza kuifanya ili tupate nauli…’akasema. Hata hivyo nauli haikupatikana kirahisi hivyo, wiki ikapita, mwezi ukaingia, na miezi ikawa inahesabika.

‘Ina maana hukuweza kumgundua kuwa ni nani?’ nikamuuliza mama

********

‘Kila nilichokiona ni cha ajabu ni kwa huyu mwanaume , alikuwa akijaribu sana kutokuwa karibu na mimi au kuniangalia machoni;

‘Mbona unaonekana kunikwepa,….nakuona kama unaniogopa vile?’ nikamuuliza.

‘Sio hivyo, wewe umetoka kujifungua karibuni, na tunaishi pamoja, lililo jema, ni kuhakikisha naishi na wewe kama vile inavyotakiwa, tusije tukaingie kwenye mahusiano mengine…ilihali hatujakubaliana na hilo….’akasema na mimi nikaona lina msingi, na nikakubaliana naye.

‘Lakini hata hivyo, hayo madevu yako huoni kuwa yanatisha,….hata sura haijulini vyema, kwanini huyanyoi, au kuyaounguza, ….na hiyo miwani, mbona ni ya jua, sijawahi kukuona ukiiondoa machoni, nahisi kuna jambo ndani yake….’nikamwambia.

‘Hapana sitaki kunyoa hiz ndevu kwasababu….mwenyewe unafahamu kuwa ninatafutwa na polisi, sipendi kabisa wanifahamu mimi ni nani, huwezi kujua, hawa watu wanaweza wakawa wametumwa huku……najua kabisa nikinyoa hizi ndevu, polisi wakiniona watanitambua, ….’akasema, lakini nikamsisitiza kuwa angalau ayapunguze, maana yalikuwa mengi sana, kiasi kwamba yalikuwa yakimziba hata mdomo.

Kwa kumuonyesha kuwa nilikuwa nalifuatilia hilo, nikanunua mashine ya kunyolea na wembe wake,…yeye akasema kwa wasiwasi

‘Nitayapunguza mwenyewe….’akasema, na kweli siku hiyo akapunguza hizo ndevu kidogo, kiasi kwamba sura yake ilikuwa vile vile ya kificho. Mimi akilini mwangu nilijua kabisa anafanya hivyo kwa ajili ya kujilinda, ili asitambulikane, kwahiyo sikupenda kumshawishi zaidi, japokuwa nilikuwa siyapendi yale madevu yake…alikuwa anatisha.

Siku moja alikunywa pombe akalewa sana,…na huwa akilewa hivyo, anaishia kulala fofofo, …. mimi nikaona hapo ndio sehemu ya kumpatia…nitampunuza hizo ndevu, angalau kidogo, , …nilipohakikisha kuwa kalala, nikachukua ile mashine na kuanza kumnyoa kwasababu ya haraka haraka, na kwa vile nilifanya hivyo kwa haraka bila kuwa na mpangilia maalumu, nikajikuta nimemnyoa vibaya, sehemu nyingine ndevu zikawa zimekwesha kabisa,….ilikuwa kama mtu aliyenyofolewa.

Alipoamuka asubuhi na kujiona alivyokuwa kanyofolewa ndevu zake, na kuonekana kioja, ikabidi achukue ile mashine na kujinyoa mwenyewe vizuri zaidi huku akilaani kweli kweli...

‘Hivi ni nani kanifanya hivyo, ni wewe tu najua umenifanya hivi kwanini umenifanya hivi, ina maana hukunielewa, sasa itabisi niwe makini zaidi,….sijui nitafanya nini wakiniona hawa maaskari’ akawa analaalmika kwa hasira.

‘Wewe hukumbuki ulipogombana na yule mtu, ….akakupiga na kukuzidi nguvu, alichukua sijui chupa ile, na akawa anakukwangua nayo kwenye midevu yako….…’nikamdanganya.

‘Sio kweli….ni wewe umenifanya hivi, na ole wake polisi wanikamate, tutaenda wote jela…’akasema huku akimaliza kujinyoa, na alipogeuka kuniangalia, , nikajikuta nikipigwa na bumbuwazi. Yeye akageuka kwa haraka na kuchukua mawani yake ni kuivaa, lakini alikuwa kachelewa.

‘Hivi kumbe ni wewe…’nikamwambia.

‘Ndio ni mimi kwani nimekuwa nani tena, ….’akasema huku akitaka kuondoka.

‘Yaani kujificha kwako kote no kudai kuwa unajificha na polisi…kumbe ni wewe…oh..’nikajikuta nikisema huku mwili mzima ukinisisimuka kwa hasira.

‘Oh kwani vipi….nimebadilika ehe, nimekuwa kijana….mrembo au sio…?’  akageuka na kuniangalia huku akicheka….akiwa na mawani yake usoni, sijui ni kweli kuwa hakufahamu nina maana gani kumwambia vile. 

Yeye , akageuka kwa haraka na kwenda mezani kulipokuwa na karanga na kuanza kazi ya kufungwa karanga kwenye vimfuko, kwa ajili ya kwenda kuuza, huo ulikuwa ni mmoja wa miradi yetu tuliokuwa tukiufanya.

‘Una urembo gani wewe, mnyama mkubwa wewe…mzandiki, msaliti mkubwa wewe….’nikasema kwa hasira na hapo, akageuka na kuniangalia aliposikia sauti yangu ya hasira na matusi ambayo hakuyatarajia kutoka kwangu.

‘Kwanini unanitukana?’ akaniuliza huku akiendelea kufunga karanga. Kwa maisha tuliyokuwa tukiishi lugha kama hizo zilikuwa ni kitu cha kawaida, nay eye alishazoea hizo lugha hiyo japokuwa mwanzoni alikuwa akigombana na watu karibu kila siku…, kwani akatika kuhangaika kwetu, tulikuwa tukikutana na matusi ya kila aina, kwahiyo matusi na kejeli ilikuwa sehemu ya maisha yetu, tulijuja tukazoea. Naona pale aliposikia nkiyaporomsha matusi, alijifanya hakujali, …..

‘Leo umegauka kuwa hao wauza unga,…ambao kila siku wanajifunzia matusi kwangu,…mimi sasa sijali, waache watukane wanavyotaka, lakini najua ni nini ninachokifanya…, mimi sijali, hayo ndio maisha yetu, walalahoi, kinachonishanga ni kutukanwa na mtu ninayemthamini kama wewe…nimekukosea nini mpenzi…’akasema.

‘Ningelikuwa mpenzi wako usingelinitelekeza kipindi kile….., na kunisusia uja ujazito na kudai kuwa mimba sio ya kwako…’nikamwambia na hapo akajikuta akidondosha kile kimfuko cha karanga alichokuwa kakishika mkononi na kunikodolea macho.

‘Oh, ina maana umeshanigundua….sasa nimekwisha, ….maana kama wewe umenigundua, hao polisi nitawakwepaje….umeshaniweka ndani wewe….’akasema akinigeukia huku akiwa kashika kidevu chake na kuivaa miwani yake haraka.

‘Ningeligundua kuwa ni wewe nisingelikuokoa kwenye ule mto , ningelikuachia ukafa na maji,…una bahati sana wewe, lakini hata hivyoo siwezi kukusamehe kamwe kwa hayo uliyonitendea…kamwe sitaweza kukusamehe….’akasema mama akinihadithia kisa cha maisha yake na huyo mwanaume.

‘Mimi nina uhakika umeshanisamehe,….. na ninashukuru kuwa tumekutana tena, na mungu akijalia tutaishi pamoja kama mke na mume….hiyo ndio ahadi yangu toka siku nyingi…..’akasema na kuniacha nibakie mdomo wazi,sikuamini maneno yake, niliona ni kwa vile nimemfanyia mambo makubwa ambayo yalistahili kutendewa watu wema, lakini sio mtu kama yeye…tulitulia kwa muda kila mmoja akijifanya yuko bize na kufunga karanga.

‘Mama nanihii, natumai umenisamehe au sio…?’ akauliza, tangu siku alipogundua kuwa nina mtoto alikuwa kazoea kuniita hivyo; mama nanihii.

‘Kwa hayo uliyonitendea, siwezi kamwe kukusamehe, …..hakuna ambaye angeliweza kukusamehe kwa ujeuri na unyama kama ule,…..wewe sio mtu wa kusamehewa, ulichonifanyia ni unyama uliopitiliza….huoni kuwa wewe umekuwa chanzo cha kuharibika maisha yangu, na sasa wewe umekuwa chanzo cha kunifanya nimtelekeze mwanangu..’akasema akionyesha hasira usoni.

‘Nina uhakika mtoto yupo salama huko alipo….na nina uhakika kuwa tutarudi tutamkuta akiwa salama….hilo nakuhakikishia, na nitafurahi sana nikimuona mtoto wangu…ahsante sana kwa wema wako na kuvumilia mengi….’akasema na kuinuka, akajinyosha huku akiwa kashika kiuno, alionekana kuchoka maana alikuwa akifanya kazi nyingi za nguvu.

‘Sasa hivi unamuita mtoto wako,..hahahaha, eti nikimuona mtoto wangu….kweli nyie wanaume mna visa, …wakati nina mimba ulinikana, sasa una uhakika mtoto yupo, na unajua analelewa na watu wengine, huna majukumu naye,….unajigamba, ….`mtoto wangu’….huna mtoto wewe, mtoto ni wa huyo unayemjua kuwa alinipa ule uja uzito…sio wa kwako wewe umeshasahau kunifukuza na panga…eehe’mama akasema kwa hasira.

Yule mwanaume, kuona vile, akageuka na kusogea pembeni, akachukua mfuko aliokuwa kaweka nguo zake na kutafuta kitu, baadaye akatoa kiboksi, akakifungua, kilikuwa kiboksi kizuri, …kiboksi kidogo, akanisogelea na kukifungua, na ndani yake kulikuwa na pete nzuri sana.

Akanisogelea hadi tukawa tumeangalia machoni, halafu akapiga magoti, na huku amekifungua kile kiboski, akainua kichwa na kuniangalai machoni, akasema;

‘Mama nanihii, naomba unikubalie ombi langu, nataka uwe mke wangu…wa hii shida tunayoipata kwasasa na raha tutakayokuja kuipata baadaye nina uhakika kuwa raha ipo mbele yetu,….’akasema huku akiniangalia kwa macho ya huruma. Sikumjibu kitu, macho yangu yalikuwa kwenye ile pete, ilikuwa nzuri ya bei mbaya, sikujua wapi alipoipatia….

‘Najua nilikukosea sana…….na nikuambie ukweli, siku ile ulipoondoka pale, niliingiwa na huzuni kubwa sana, nilijuta sana kwa tendo lile, nikawa ninalia kila siku ya mungu,….na nikuambie ukweli, kuwa kila siku, kutoka siku ile. Nilikuwa nikikutafuta kila kona..na nikawa nalewa kupita kiasi, kila nikikumbuka….na hata nilipopata zile pesa cha kwanza nilichofanya ni kwenda kununua hii pete ya bei mbaya, kwa ajili yako….’akasema.

‘Siwezi kuamini hayo maneno yako’mama akamwambia huku akigeuka pembeni kutaka kuondoka, lakini miguu ilikuwa minzito, akajikuta amesimama pale pale, huku akiwa kageuka upande kuangalia sehemu nyingine.

‘Siku tukirudi jaribu kuulizia watu wanaonofahamu,….watakuambia kila kitu, jinsi gani nilivyokuwa nikikuulizia,nikikutafuta kila kona, amini hayo ninayokuambia …….nilifika hadi kwenu kukuulizia, kama unabisha waulizie wazazi wako…...na cha ajabu nilimkuta mama yako akisikitika sana…na yeye alikuwa akikutafuta…ilikuwa ni hasira tu waliyokuwa nayo hawakuwa na dhamira ya kukufukuza moja kwa moja….’akasema.

‘Walinikataa wenyewe…kama walikuwa na dhamira hiyo au la….mimi sijui…, ila lawama zangu hadi mwisho ni kwako wewe….kwenu nyie wanaume mnaopenda kuwahadaa wanawake na mwisho wa siku mnakimbilia kuwatelekeza…eti hamjui hio mimba, wakati kabisa, ulikuja kupanda mbegu kwangu….hiyo ni laana….’nikamwambia huyo mwanaume.

‘Pole sana….kwangu mimi nakiri kosa, na ninaomba msamhana nipo chini ya miguu yako, ila kwa wazazi wako,….ilikuwa ni wajibu wao kukasirika, ….na kosa ni la kwangu mimi..nitajitahidi sana kwenda kuwaomba msamaha….’akasema huyu mwanaume akionyesha kujuta kiukweli..

‘Wazazi wangu, wanalawama….wangelinipa muda, niweze kuwaelezea vyema, maana ilibidi nifanye hivyo, kwani nilikuwa sijaongea na wewe….wao walikimbilia kunifukuza….sasa sioni kwanini wahangaike kunitafuta tena….shauri lao..na hata wewe ulinikataa, sasa kwa vile umesikia nina mtoto, na mtoto mwenyewe mwanaume, unajifanya sasa unanipenda,…sizani kama nitaweza kulisahau hilo…’akasema mama.

‘Najua hilo…lakini nakupenda sana mama Nanihii..nisamehe, na pokea hii pete yangu ya uchumba, na ukitaka kesho tunakwenda kufunga ndoa,….’akasema na mama akamgeukia huku akimwangalia kwa mashangao, hakuamini hilo….

Nilifikiria sana na niliona hakuna jinsi, kwani hata hivyo, nilikuwa nampenda sana huyo mwanaume, na siku aliponikataa, niliumia sana, na moyoni nilikuwa nimeapa kutokuwa na mahusiano na mwanaume mwingine yoyote….

Na kweli kesho yake tukaenda kufunga ndoa,…..’akasema mama huku akionyesha uso wa furaha…lakini baadaye ile furaha ikayeyuka na kubadilisha sura yake na kuwa ya huzuni.

‘Tulipotoka kufunga ndoa ….tukawa tupo mitaani tumeshikana mikono kwa raha zetu…tulijihisi tupo duniani nyingine, dunia ya wependanao,…..hatukujua, kumbe kulikuwa na watu wanatufuatilia kwa nyuma, hatukujua hilo kabisa..na mwenzangu alishajisahau.., mara hawo watu wakatupita, na walipokuwa mbele yetu, wakatugeukia, na kipindi hicho jamaa yangu alishajisahau na kuvua miwani yake.

Wale watu wakasimama mbele yetu na mmoja akatoa kitambulisho na kujitambulisha kuwa wao ni askari kanzu.

‘Mnataka nini ….?’ Akauliza mwenzangu akionyesha wasiwasi

‘Wewe ndiye Mtumwa…au sio?’ akauliza huyo askari, na kabla mume wangu hajajibu kitu mwingine akatoa pingu,..

‘Ndiye yeye mkuu…..tulirejeshe home, rikajibu mashitaka…’akasema huyo askari mwingine na wakaanza kumpiga mume wangu pale alipokataa kutii amri, na baadaye likaja gari aina ya landrover, wakambeba mume wangu juu kwa juu ….na kumuingiza kwenye hilo gari, wakaondoka naye.

Nilijaribu kufuatilia wapi walipompeleka, lakini kwa siku hiyo sikufanikiwa na kesho yake, nikaenda kituo ambacho nilihisi kitaweza kuwa na taarifa naye, kama walivyoniahidi, na hapo wakanimbia kuwa mume wangu karudishwa huko nyumbani, kwenda kujibu mashitaka ya wizi, wa mamilioni ya pesa.

‘Nikabakia peke yangu……’ akasema mama akionyesha masikitiko.

NB: Haya ndio hivyo, kwa shida tutafika….

WAZO LA LEO: Linapotokea jambo hasa la misiba, au majanga, ajali nk, ambalo ni la kusikitisha, kwanza tuliweke mikononi mwa muumba, kuwa yeye ndiye mweza wa yote, na pili, tusikimbilie kunyosheana vidole, kabla hatujakuwa na ushahidi wa chanzo cha janga hilo. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunaonyesha hisia zetu, zilizojificha…na kumbe huenda hata huyo tunayemnyoshea kidole hahusiki. Chuki ni tabia ya ibilisi.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Very nice post. I simply stumbled upon your weblog and wanted to say that I've truly enjoyed surfing around your weblog posts. In any case I will be subscribing in your rss feed and I am hoping you write once more very soon!

Here is my website ... home Loans fresno