Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, May 14, 2013

WEMA HAUOZI-7



Wakati mama anaendelea kunithibitishia yale aliyonihadithia babu , kila mara akili yangu ilikuwa ikiyakumbuka maelezo ya babu, jinsi alivyokutwa siku hiyo baada ya kupoteza fahamu, akasema;

`Mama yako alinikuta nimepoteza fahamu, na walinihangaikia hadi nikazindukana, na nilipozindukana, nikawa sijiamini, kwani niliyoyaona hadi nikapoteza fahamu, yalikuwa yakiniandama kichwani;

‘Baba kulitokea nini…’akaniuliza mama yako.

‘Hata sijui, ….nahisi ni mauza uza ya kuondoka kwa mke wangu, …’nikamwambai nikiogopa kuongea kile nilichokiona.

‘Baba mbona inaonekana kama ulikuwa ukipigana na mtu , maana vitu humu ndani vimetawanyika, ….?’ Nikamuuliza babu yako na mume akaulia hivyo hivyo.

Nikawa najiuliza mengi, je ina maana ni kweli hayo yaliyonitokea ni kweli sio ndoto, maana kama vitu vimetawanyika, ina maana kweli nilikuwa nikipambana na mtu, nikaanza kukumbuka yaliyotokea ;

********

Babu aliendelea kuelezea na ukumbuke kuwa hizi zilikuwa kumbukumbu nikiwa nipo na mama

Siku hiyo nilipanga kwenda milimani, huko kuna jamaa mmoja ninaye mfahamu, jamaa huyo ana utaalmu wa kupambana na wachawi, na huwa mkimuita kijijini, anawafichua wale wote wenye vitendo hivyo. Nilikuwa nimefikia uamuzi huu baada ya kuona nashikwa na majinamizi ya kila siku.

Basi nilipoamuka asubuhi , nikawa najiandaa, niliamua kuondoka pale tu hawo watoto wakiondoka sikutaka kuwaambia wapi nilipokusudia kwenda, kwani wasingelinikubalia. Nikaweka vitu vyangu tayari, na nikiwa nasubiri, nikajilaza kwenye kitanda change, na mara kausingizi kamang’amu ng’amu kakanijia.

Niliona kitu kama kivuli cha mtu, kikinijia, na huwa kinanitokea mara kwa mara, baada ya kipindi hicho cha kufariki mke wangu. Na nilijua kikinijia kinachofuata ni kukabwa, na nisipojitahidi ninakuwa kama napoteza fahamu kabisa, safari hii sikukubali, nikajitutumua

‘Leo nimekuja rasmi kukumaliza, maana nimekukuanya hunisikii, …’sauti ya kufifia ikasema
Mimi sikumjibu, ikawa kama kwenye ndoto, nikainuka na kujiandaa kwa mapambano. Kile kivuli ambacho sasa kilionekana kam mtu, ambaye sikuweza kumuona sura yake ikacheka kwa dharau;

‘Ndio unataka kufanya nini wewe…’ikasema

‘Nitajilinda na wewe mwanga mkubwa….’nikasema na sauti ya kicheko ya dharau ikasikika, na kilichofuata hapo ni dhoruba, maana hilo lijamaa, lililokuwa na umbao kubwa lilinizoa zoa na kunirusha hewani.

Nilihisi nikidonoka kwenye viti, na maumivu yakajaa mwilini kuonyesha kuwa nimeumia, sikukubali, nikainuka na huku nikikumbuka dua nlizofudishwa za kujilinda na watu hawa. Tatizo ni kuwa japokuwa nilikuwa nazifahamu hizo dua, lakini kila nilipokuwa nikitaka kuzitaja, ilikuwa kama kumbukumbu zimepotea.

‘Nitahakikisha kuwa leo unasalimu amri kwangu….’hilo jitu likasema.

‘Mimi siwezi kukubali kuwa mtumwa wako, kamwe…’nikasema na sikujua kwanini nilisema hivyo, ila inavyoonyesha hilo jitu lilitaka nifanye yale ambayo sikukubaliana nayo.

‘Wewe utakubali tu, wenzako walikuwa wakaidi kama wewe sasa hivi wahaonekani tena, …’likasema hilo dude, na mimi hapo nikakumbuka baadhi ya maneno ya hiyo dua, na kila nilipotamka neno moja lile dua likawa kama linaumia.

‘Oh, ..kumbe ..oh…’likawa linasema huku likionyesha kupepesuka, na kila hatua nikawa naingiwa na kumbukumbu. Nilipoona limeishiwa nguvu, nikainuka, na kuchukua kiti. Huwezi amini, kitu ambacho nilikuwa sikuwezi kukiinua kirahisi, niliweza kukiinua kama chombo kidogo tu, nikambamiza huyo jamaa.

‘Oh, unajifanya kuwa uan nguvu sio…’likasema hilo dubushwa na mimi nikawa nimekumbuka ile dua niliyofundishwa na lile lidubwana likatoweka. Nikayumba na kudondoka chini. Na ndivyo walivyonikuta wazazi wako.

‘Je huyo alikuwa ni nani ananichezea’nikajiuliza pale walipoondoka wazazi wako, na hapo hapo, nikaamua kwenda huko milimani.

*****

Safari ya milimani haikuwa rahisi, maana ilionekana kuwa huyo adui yangu alikuwa akijua kuwa safari hiyo ni ya kumwangamiza, basi akawa ananiandama, kwa kunikabili kwa maajabu ya kila namna, lakini kwa vile nilishazamiria kupambana naye sikuogopa. Na kila aliponitokea nilikumbua hiyo dua, na kila nilipoisoma jitu hilo hutoweka.

Nilifika sehemu yanye mto, na hapo nikataka kunywa maji na wakati naima, nikashitukia nimepigwa na kitu nyuma ya kisogo, kilikuwa kigumu kama chuma, na nikadondokea kwenye maji, na nilipoamuaka nilijikuta nipe kwenye chumba kidogo, huku nikiwa nimefungwa kamba za ngozi ya wanyama mikono na miguu.

Nikiwa nimening’inizwa              hewani na chini kuna mijoka ya kila namna imelala, na mingine ikiwa imeinua vichwa ikiniangalia, kwa uchu, na kila mara kamba ile niliyofungwa ilikuwa ikiisha nguvu, na kuonekana kunisogeza karibu na ile mijoka.

‘Sisi hatuna zaidi ni wewe kukubalina na matakwa yetu..’nikasikia sauti ikisema.

‘Matakwa gani…..hayo. mbona mimi siwaelewi…’nikawauliza.

‘Kwanza achana na huo mpango wako wa kwenda huko milimani kwa huyo muhuni anayeingilia kazi zetu, sio kwamba tunamuogopa sana, …..ila hatutaki kuharibiana katika shughuli zatu, na pili tunakuhitajia uungane na sisi ….’ile sauti ikasema.

‘Na kama nisipokubalina na hayo …?’ nikauliza.

‘Basi hatuna budi, …hawo nyoka wanakuhitaji kwa hamu….na kesho utakutwa ukiwa umeungua kama mishikaki…je umesahau yaliyotokea kwa mkeo, hebu mwangalia kule akiwa katikati ya mto...’ile sauti ikasema na mara nikamuona mke wangu akiwa kati kati ya moto akionekana kupiga kelele ya kuomba msaada.....'hapo moyo wa uwoga, hasira....ukaniingia

Wakati natafakari hayo, akili ikanijia kuwa nikubali kwa kudanganya, lakini mara akili nyngina ikanijia, na nikakumbuka yale maneno ya ile dua, nikaanza kuiomba, na mara nilihisi uvumi mkali ukienea mle ndani ndani, vumbi, na hilo vumbi likawa linazitawanya zile nyoka, na moja moja ikaanza kukimbia.

‘Muueni haraka, msimuachie…’sauti ikasema na mimi sikuacah kuiomba ile dua, huku moyoni nkikumbuka yale mema niliyowahi kuyatenda kwa watu, maana moja ya amsharto ya hiyo dua ni kuwa wakati unaisoma unatakiwa ukumbuke yale mema uliyowahi kuyatenda, na mimi mema yalikuwa mengi hata sikuweza kuyamaliza, na mara nikawa nimesimama peke yangu.

Nikaanza safari ya kupanda milima na ambonde, hadi nikafika nyika, ambayo ndio makazi ya huko ninapokwenda, na hapo, nikahisi nipo kwenye dunia nyingine, maana watu wa huko kwetu wandai kuwa eneo hilo wanaishi watu wasio na dhambi,…ndio maana eneo hilo muda wote lina rutuba, majani yake ni kijani, matunda ya kila namna yalionekana kila kona.

Nilisimama kwa muda nikishangaa eneo hilo, na hapo nikakumbuka zile duwa na nikazisoma na nikaiona ile njia iliyonipeleka hadi kwa huyo mtu niliyemuhitaji, Nikafika kwake, na alioniona alinikaribisha na hata kabla sijamaliza kuongea akasema;

‘Rudi, huko kwenu matatizo yako yamesikilizwa,….ila watu wa kijiji chako wataandamwa na misuko suko, kwa yale waliyoyafanya, wewe utaokoka, kwa maendo yako mema, na kila ukumbuke kuomba na kuyakumbuka matendo yako mema, kwani ndiyo yatakayo kulinda…nenda haraka…

Basi nikareeja huku kwetu, na nilipofika nilisikia taarifa ya moto mkali uliozuka, na kuteketeza nyumba ya yule wanayemuita mtalaamu, na yeye hajulikani wapi alipo, na wengine walidai huenda aliteketea kama alivyokuwa akiwaamrisha watu kuwatekeza wale aliowaita ni wachawi…

*******

Kumbukumbu za babu zikanitoka, na sasa nikawa namsikiliza mama anavyoelezea jinsi ilivyotokea walipokwenda hospitalini

Kilichonishangaza ni jinsi mtoto wetu alivyopona kwa haraka, hata madakitari wenyewe walishikwa na mshangao, kwani tulipofika hapo hospitalini alikuwa na hali mbaya sana, alikuwa amelegea na macho yalishaanza kugeuka meupe kama mtu  asiyekuwa na damu. Alikuwa katapika sana, na joto la homa lilikuwa kali sana.

‘Kwanza inabidi tumpunguze joto la homa….’akasema docta na wakataka kumpiga sindano ya kushusha homa, akatuelekeza kwenda wodini, ambapo matibabu hayo yatafanyika, kwani kwa jinsi walivyomuona waliona ni bora alazwe…wakachukua vipimo vya kwanza lakini cha ajabu hawakuona tatizo lolote, na mtoto akawa amezidiwa, na wakaona ni vyema alazwe kwanza, huku akiendelea na matibabu …

‘Sasa tutafanyaje, …kwani mmoja ni lazima abakie na mtoto,….’nikamwambia mume wangu.

‘Mimi mwenyewe ni mgonjwa, kwahiyo ni vyema nikabakia na mtoto huku nikiendelea kutibiwa…’akapendekeza mume wangu, lakini sikulipenda wazo, kwani matatizo yake yanaweza yakamuambukiza mgonjwa, kwani tulishahisi kuwa huenda ana kifua kikuu.

‘Mgonjwa kweli ataweza kumhudumia mgonjwa….ngoja tuskilizie matibabu yako kuwa watasemaje, ….nikasema na mume wangu akaelekea kwenye matibabu yake. Ni kipindi hicho wakati mume anakwenda chukuliwa vipimo, nikabakia na mttoto, akiwa kalegea, kalala kwenye kitanda cha wodi, na mimi nikajikuta mwili haina nguvu..

Nilishangaa jinsi gani nilivyojisikia vile kwa ghafla, nikawa kama nipo kwenye ulevi wa mdawa, nikawa najitahidi kuizuia ile hali, nikashika macho kuondoa giza lilokuwa liktanda usoni, na hapo nikakumbuka dua aliyonifundisha babu yako, kuwa nikijis vibaya noisome, ….nikaanza kuisoma huku nimeweka vidoke kwenye macho, mtoto akiwa kalala kitandani, nikimsubiria docta aje pale kitandani, kwani alikuwa akiendelea kuhudumia wenzangu na zamu yangu ilikuwa haijafikia.

Ni wakati huo  tunasubiria matibabu ya mume wangu, na nikiwa namsubiria docta afike kwenye kitanda chetu mara nikamuona mtoto akiinuka na kutaka kutoka nje,

‘Unataka kwenda wapi?’ tukamuuliza tukiwa tumeshikwa na mshangao, na wakati huo dakitari wa kumpiga sindano ya kupunguza homa, alikuwa anakaribia kitanda nilipokuwa nimemlaza mtoto. Nikahisi huenda mtoto anaogopa sindano

‘Kwenda cheza….’akawa anaongea kitoto.

Docta akafika na kumshika shavuni, akatugeukia na kutuangalia, na kusema;

‘Mbona hana homa tena..home imeshuka, haina haja, ya kupigwa sindano, ila chukueni vidonge hivi, mumnyweshe, na kama anataka kucheza, tokeni naye nje, halafu baadaye mrejee , ili tumchukue vipimo vingine….’akasema na sisi tukamshika mtoto mkono na kumshusha kitandani, alikuwa amekonda kweli na mwili ulikuwa mdhaifu lakini alijitahidi na kusimama

Basi tukamshusha kutoka kitandani, kwani alishaanza kutembea, na akawa anatoka nje, na sisi tukawa tunamfuatilia kwa nyuma, na alipofika nje,kweli akaanza kucheza, anakimbia huku na kule, na docta alipokuja wodini ambapo tulishapangiwa, akatukuta hatujarudi , akatufuatilia nje, na kutukuta katika hiyo hali.

‘Vipi mgonjwa amepona?’ akauliza huku akimwangalia anavyocheza.

‘Ndio…naona imekuwa hivyo, hata sisi tunashangaa….’tukasema

‘Kuna vipimo nataka kumchukua, mnaonaje tukarudi ndani, huenda dawa alizokunywa zimefanya kazi yake….’akasema docta.

‘Lakini bado, tulikuwa hatujamnywesha hizo dawa….’nikasema na docta akamwangalia yule mtoto kwa mshangao, hata hivyo akasema twende ndani tukachukue vipimo vingine. Na hata vipimo vilivyochukuliwa tena havikuonyesha tatizo lolote.

Docta akatugeukia na kusema;

‘Kama isingelikuwa ni mimi nimempokea awali, ningewaambia kuwa mumemleta mtoto, akiwa hana tatizo lolote, labda kama mlitaka kumchunguza hali yake kwa vile amekonda, lakini mimi mwenyewe ndiye niliyempokea, na niliona hali yake ilivyokuwa mbaya…nashangaa sasa anaonekana mzima kabisa, na hata vipimo vinaonyesha hivyo, je hali kama hii inatoka mara kwa mara?’ akauliza

‘Hapana,…hii ni mara ya kwanza kuonekana kupona, siku zote amekuwa na hali mbaya, joto la homa halishuki, kutapika , hapendi kula kabisa….’nikamwamba docta.

‘Basi huenda ugonjwa umeogopa umekimbia, baada ya mtoto kufika hapa hospitalini…’akasema docta kwa mzaha.

‘Kwahiyo docta, unasema hana tatizo lolote,..na hajapata dawa yoyote…?’ akauliza mume wangu

‘Mimi kwa hali ninayoiona kwasasa kwa mgonjwa, sioni kama kuna haja ya kubakia hapa hospitalini, ….hana tatizo lolote kwa sasa, na kwa jinsi mnavyomuona, …..ondokeni naye, na kama hali itarejea kuwa mbaya, basi mrejesheni….’akasema docta.

‘Sawa docta….’nikasema na docta akamgeukia mume wangu na kusema;

‘Ila kwa baba yake inabidi arudi kesho kuja kuchukua majibu yake…sioni kama kuna haja ya kumlaza, au mnasemaje?.’akasema dakitari kama anauliza.

‘Sisi tunakusikiliza wewe…..’akasema mume wangu ambaye mwili wake ulikuwa umepungua sana, na alikuwa kikohoa mfululizo, na tulijua kabisa, kuwa huenda kaathirika na kifua kikuu.

‘Haina haja ya kumlaza, hali yake sio mbaya sana, ila atakunywa hivi vidonge, ….vitamsaidia huku tukisubiria majibu ya vipimo vyake. Halafu akamgeukia mtoto na kumwangalia kwa makini, alikuwa akionyesha mshangao mkubwa usoni jinsi mtoto alivyobadilika kwa haraka kiasi kile.

Basi mimi na mume wangu tukakubaliana yeye atafute sehemu abakie hapo akisubiria hayo majibu ya vipimo vyake, na mimi na mtoto tukarudi nyumbani.

Niliporudi nyumbani babu yako alikuwa hayupo, na nikawa na wasiwasi sana tukikumbuka kuwa tulimuacha akiwa mgonjwa, kwahiyo huenda kazidiwa kapelekwa hospitali, lakini  hata tulipouliza watu , hakuna hata mmoja aliyefamu kuwa kaenda wapi, tulihangaika huku na kule, lakini hatukupata maelezo yoyote,sisi tukaona tusubiri, kwani hatukuwa na la kufanya.

Ghafla tukasikia mayowe ya watu, na watu wakawa wanakimbilia huko mayowe yalipotokea, na kwa mawazo yangu ya haraka, nikamuwazia babu yako, huenda wamemkuta akiwa kafariki au lolote limetokea ….ikabidi nifuatilie huko mayowe aylipotokea.

Ilikuwa ni maeneo ya yule wanayemuita mtaalamu, nyumba yake ilikuwa inateketea, na moto ulikuwa mkubwa sana….

NB: Je ni nini kilimtokea `mtaalamu..'

WAZO LA LEO : Ni kweli yote yawezekana, wapo walipoona kwa njia hizo, kwa kile tunachoweza kukiita ni miujiza, wapo waliopona kwa imani zao, hata bila kutumia dawa. Na hapo ndipo tunapoamini kuwa mungu yupo na akitaka liwe litakuwa.

 Imani hizi hotofautiana, kutegemeana na dini za watu mbali mbali. Kutofautiana huku kwa imani kusiwe kigezo cha kujenga uhasama uadui na chuki, ….kwani sote ni waja wake muumba, sote ni watoto wa   
Adamu na Hawa, kwanini tusjione hivyo, kuwa sisis ni ndugu wa baba na mama mmoja, kwanini tusipendane, kwanini tusioneane huruma, kwanini tunapenda kutafuta vyanzo vya kufarakana, ambavyo hata havipo kwenye imani za dini, bali ni hisia za uchoyo wetu….vyovyote tutakavyofanya au kujisikia, katu hatubadili hilo, kuwa sote ni wana-wa-Adamu.



Ni mimi: emu-three

7 comments :

Anonymous said...

Tumekupata mkuu kazi yako ni hazina kubwa

Anonymous said...

Je huwezi kufomati tukaweza kusoma kwenye simu. Inatupa shida sana ukifungua kwenye simu hata hivyo kazi nzuri huna mpinzani kiukweli

Anonymous said...

Je huwezi kufomati tukaweza kusoma kwenye simu. Inatupa shida sana ukifungua kwenye simu hata hivyo kazi nzuri huna mpinzani kiukweli

Anonymous said...

Je huwezi kufomati tukaweza kusoma kwenye simu. Inatupa shida sana ukifungua kwenye simu hata hivyo kazi nzuri huna mpinzani kiukweli

Anonymous said...

Je huwezi kufomati tukaweza kusoma kwenye simu. Inatupa shida sana ukifungua kwenye simu hata hivyo kazi nzuri huna mpinzani kiukweli

Anonymous said...

Hii ni zaidi ya mtandao wa kijamii ni bora uifanye iwe e-book

Anonymous said...

I used to be able to find good information from your blog articles.


Also visit my blog - Cyclepress.Co.Jp