Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, May 3, 2013

WEMA HAUOZI-3



`Bibi yako alipoamuka asubuhi akaenda chumba alicholala huyo mzazi, akiwa na mpangilia wa kumsaidia kuoga na kumkanda na maji ya moto,…..akafika kwenye chumba cha huyo mzazi na kugonga mlango, lakini kulikuwa kimiya, ….basi akaamua kuingia, na kumkuta mtoto mchanga yupo peke yake kitandani, akiwa bado amelala.

Kipindi hicho nyumba yangu ilikuwa ya miti, iliyokandikwa kwa udongo, na kuezekwa kwa majanii sio hii, hii ilikuja kujengwa baadaye na mama yako….’akasema babu, na tukawa wote tunaiangalia hiyo nyumba kwa macho. Babu akaendelea kuhadithia ….

‘Huyu mtu atakuwa amekwenda wapi asubuhi hii…’bibi yako akawa anauliza kwa sauti na mimi nikamsikia na nilipoona anaendelea kujiuliza hivyo, ikabidi na mimi nimuulize kwa sauti, toka kwenye chumba chetu;.

‘Ina maana huyo mzazi hayupo huko ndani kwake?’ nikauliza

‘Hayupo…hata huko nje, haonekani,….sijui atakuwa kaenda wapi asubuhi hii, na ile hali alitakiwa asitoke nje, kwani ubaridi ni mkali sana. …’akasema bibi.

‘Kaondoka na kitoto?’ akauliza babu.

‘Aheri angeliondoka naye, nisingelikuwa na wasi wasi kiasi hicho, lakini mtoto kaachwa peke yake hapo kitandani, na bado kamelala…’bibi yako akasema na mimi nikatoka kule chumbani na kuja kuungana naye kuhakikisha hayo anayozungumza bibi yako, na kweli huyo mzazi hakuonekana.

Masaa yanakwenda, mzazi haonekani, na mtoto anaanza kulia njaa, hapo ikabidi tuanze kuhangaika, …kutafuta maziwa, na uzuri ni kuwa tulikuwa na ng’ombe wa maziwa, kwahiyo hatukupata shida sana ya kumlea huyo mtoto…kichanga kikaanza kutumia maziwa ya ngombe.

Masaa yalivyozidi kwenda bila ya kuonekana huyo mzazi, tukaanza kuingiwa na wasiwasi, kwani, hakukuwa na dalili yoyote ya mzazi, na hata tulipofanya utafiti, hatukuweza kugundua kuwa huyo mzazi alielekea wapi. Hakuna hata jirani mmoja aliyemuona huyo mzazi. Na badala ya majirani kutusaidia wakawa wanatuangalia kwa jicho baya…na hata wale wasio na subira, wakaanza kusema;

‘Kaanza …mambo yake….’

Mimi nilivyosikia hivyo, nikasema ‘Mke wangi ni vyema tukamfahamisha mjumbe, maana hili linaweza kuwa tatizo, unakumbuka lile tatizo la mwanzo lilivyotuletea matatizo, hili linaweza likatupeleka pabaya….’nikamwambia bibi yako.

‘Maneno ya watu unayajali, mimi sijali, kwa vile sijawahi kufanya lolote baya kama wanavyodai wao,….kama nimepangiwa kuwawa kwa mikono yao,….siwezi kuzuia hilo, waache waje waniue….’akasema bibi yako.

Na kweli kwa tabia ya bibi yako alikuwa hajali, kwani maneno waliyokuwa wakiongea watu, kama angelikuwa na roho nyepesi angelishikwa na shinikizo la damu, lakini sio bibi yako. Bibi yako alikuwa jasiri, na hasa pale alipoona kuwa analolifanya lipo kwenye haki…atalisimamia hadi hatua ya mwisho.

Mimi sikutulia, nikamuacha bibi yako akimuhangaikia huyo kichanga, nikaenda kuongea na mjumbe, na mjumbe akasema kiutaratibu inatakiwa yapite masaa ishirini na manne, ndio taarifa zifikishwe kwenye vyombo vya usalama.

Nikarejea nyumbani na kumkukuta bibi yako akiwa analea kichanga, na siku hiyo ikapita, sikuwahi kukumbuka tena kwenda kwa mjumbe, tukawa tunakilea hicho kichanga kama mjukuu wetu, maziwa yapo, tuna shida gani. Waache watu wasema wakichoka watalala…kumbe wenzetu walikuwa na yao moyoni….

‘Walimwengu ni watu wabaya sana mjukuu wangu, sijui huo uvumi ulianzia wapi, maana kuna kisa cha kwanza kilikuwa hivi hivi, ….wema wa bibi yako ukawa umegeuka kuwa shubiri kwake. Kama nilivyokuambia kuwa bibi yako alikuwa mkunga, kwahiyo wasichana waliofikia kujifungua, ambao walishindwa kwenda mahospitalini, walikuwa wakimuita bibi yako kwenda kusaidia kuwazalisha. Na hata wengine kufika hapa nyumbani

‘Kazi hii ya ukunga  sio mchezo, na wengi walikuwa wakimuita bibi yako wakiwa kwenye hali mbaya, bibi yako alikuwa akijitahidi kadri ya ujuzi wake kuwasaidia, lakini kuna mengine yalikuwa juu ya uwezo wake, na kwasabbu hiyo, ilifikia wakati mwingine mtoto kupoteza uhai, au hata mzazi mwenyewe…hayo yakitokea ilikuwa ni shida kwa bibi, watu walikuwa wakimshutumu…

‘Hutaamini mjukuu wangu, ….ilifikia hatua sasa watu wanaanza kugeuza maneno kuwa bibi yako ndiye aliyekuwa akiwaua….hawo wazazi walishikwa na uchungu na kwasababu mbali mbali wakaweza kupoteza uhai, au watoto wao kufariki….’akasema babu na kutulia kwa uchungu.

‘Mimi nilimshauri bibi yako aachane na kazi hiyo, maana haina faida kwake, ukizingatia kuwa kazi kubwa aliyokuwa akiifanya hakuwa akipata malipo ya maana, inakuwa kama kujitolea tu, na yule aliyeweza kumlipa chochote, alipokea, lakini wengi walikuwa hawana cha kumlipa bibi yako, …nay eye hakujali, akarizika,…lakini wema wake huo haukuonekana….

Siku moja usiku alikuja msichana mmoja, akiwa mja mzito, msichana huyo, alisema kuwa hana pesa, na wazazi wake, wameshindwa kumsaidia…na hospitali ni mbali,….na mwanaume wake aliyempa huo uja uzito, ni jamaa ambaye naye hana mbele wala nyuma…kwahiyo akaona aje akae hapa nyumbani , kwani anahisi dalili za machungu….

‘Hilo halitawezekana, …umeshasikia watu wakiongea vibaya kuhusu mke wangu..mimi sikubalianai na hilo….nakushauri uende kwa mjumbe atajua jinsi gani ya kukusaidia’nikasema

‘Basi kwa vile ni usiku nitalala hapa, na kukipambazuka nitaondoka…’akasema huyo binti, na hatukuwa na 
jinsi, tukakubali, kwani hakuwa ameonyesha dalili zozote mbaya, …lakini ninajuta kwanini tulimkubalia..

‘Mjukuu wangu  ilipofikia usiku wa manane huyo binti akazidiwa,akaanza kupiga kelele, akidai tumbo linamuuma sana, na hapo bibi yako akamchunguza akasema ….anakaribia kujifungua na hakuna muda wa kupoteza, ina maana alitakiwa kusaidiwa kwa haraka, ili ajifungue, na usiku kama ule, tusingeliweza kwenda kwa mjumbe….

Hapo kukawa hakuna jinsi, bibi yako akafanya kazi hiyo ya ukunga bila kupenda. Lakini kumbe yule binti alikuwa na matatizo kabla, kumbe hakuwa na damu ya kutosha, na hata alipojifungua alipoteza damu nyingi sana, ….’ Akatulia babu akikohoa.

‘Kwanza huyo binti alijifungua salama, na bibi yako akajaribu kumpa dawa, na majani ya kuongeza damu, lakini haikusaidia, ilipokaribia asubuhi, hali ya huyo binti ikawa mbaya, mimi nikakimbilia kwa mjumbe, ntuliporejea na mjumbe na watu wengine wawili, tukamkuta huyo binti keshapoteza uhai…..’ Babu alipofika hapo akatulia, akionyesha wasiwasi, utafikiria ndio hiyo siku tukio lilipotokea….

‘Ilikuwa kesi kubwa sana, ikishinikizwa na huo umbea uliokuwa umezagaa, basi ikawa ndio sababu, ..bibi akashikiliwa na polisi, na akajikuta analala kituo cha polisi kwa siku mbili, na hata alipotoka hakuwa na amani, watu wakawa wanamnyoshea vidole, wakimuita majina mbaya….akawa sasa hana amani tena…na ujasiri wa bibi ukaanza kupungua, na yeye sasa akaanza kuogopa.

‘Jamani hivi hawa watu wana akili kweli…mimi sijamtuma mtu kunichukua kama mkunga na kila mara nawashauri kuwa ni vyema wakaenda hospitalini, lakini hawasikii, ….sasa mimi nimefanya kosa gani,…mimi naufahamu ukunga vyema, lakini kuna mambo ambayo yanahitaji utaalamu zaidi,…na mimi nimejitahidi kadri ya uwezo wangu,yameshindika, kama hayo ya kupungukiwa na damu, mimi siwezi kuwaongezea damu kwa haraka, sina vifaa….’akawa analalamika bibi yako.

‘Huo ndio mtihani wa kutenda wema,….mimi nilikushauri mapema kuwa achana na kazi hiyo, lakini hukutaka kunisikia….’nikamwambia bibi yako yeye alisema

‘Mimi natenda hayo kwani ni wajibu wangu,… kwa hali zote zilizotokea, kama ulivyoona, sikuwa na jinsi , nisingeliweza kuwatelekeza hawo watu, na mahospitali yetu yapo mbali na huku kijijini, ..’akasema.

‘Hilo ndio tatizo, na hata ungeliwaamusha watu usiku kama ule….wangechukua muda kufika, ilibidi ujitaidi kwa kadri unavyojua,….siwezi kukulaumu mke wangu, lakini watu hawajui, na inavyoonyesha kuna watu kwa makusudi wamepandikiza huo uwongo….’nikasema.

‘Haya tumuachie mungu,….najua ipo siku wema wangu utazaa matunda, hata kama sio kwangu, lakini kwa yoyote yule atakayekuwa upande wangu, …kwani kwa uhakika, hata siku moja wema hauozi…’huo ndio ulikuwa usemi wa bibi yako.

‘Bibi yako alikuwa na tabia moja, kuwa hapendi kutegea, anapenda sana kujitolea, kwa kazi yoyote yeye yupo mstari wa mbele…kama ilivyo mimi, ….ndio maana nawaasa mara kwa mara kuwa mjenge tabia ya kujituma,…usiwe na tabia ay kutegea,..wewe uwe msitari wa mbele kwa kila jambo linalohitaji kujitolea, kuna faida kubwa sana….’akasema babu

‘Kwa imani yangu mimi, niliyofundishwa na babu yangu….aliniambia kuwa kila jambo, mwanzo wake ndip kwenye baraka, kwahiyo kama likitokea jambo, ukawa wa kwanza kujitolea, zile baraka zinakushukia wewe..na zinazobakia kidogo, zitachukuliwa na hawo watakaokuja baadaye. Na pia hata kwenye tukio la masikitiko, au ajali, ile halai ya kwanza ya tukio, inatakiwa uonyeshe ujali wako kwa mungu wako…kuwa mungu ndiye kawezesha hayo….’babu akatulia akiwaza jambo.

‘Kwahiyo babu ilikuwaje kwa bibi…?’ mimi nikauliza, nikiwa na hamasa ya kujau ni nini kilimkuta bibi na hapo babu akaniangalia kwa muda bila kusema neno, na baadaye akasema;

‘Unajua watu walifikia hadi kuandamana kuja hapa nyumbani kumzuru bibi yako,…’akasema babu

‘Kwasababu gani lakini ….’ikabidi niulize maana niliona kama vile babu alikuwa hataki kusemi wazi kwanini bibi alikuwa akiandamwa na watu kiasi hicho, mpaka hapo sikuwa nimeona ubaya alioufanya bibi hadi watu wamchukie kiasi hicho.

‘Watu walimzushia bibi yako kuwa ni mwanga…eti bibi yako ni mchawi…hahaha’babu akawa kama anaigiza kucheka, na kusema;

‘Bibi yako hajui hata chembe moja la uchawi….zaidi ya huo utaalamu wa ukunga alioupta toka kwa bibi yake,….mimi ni shahidi na mungu pekee ndiye anajua….lakini watu hawakuniskia, wakawa wamezingirwa na imani hiyo, ….inasikitisha sana….’Akasema babu kwa uchungu, na alipotamka maneno haya, nikajikuta nikishituka na kumkazia babu macho

‘Eti nini….mbona sioni ukweli wa hayo, mtu kujitolea kusaidia watu,…ndio iligeuka kuwa hivyo,…?’ nikauliza.

‘Ndio ilivyokuwa kwa bibi,…na hata mjumbe alipoingilia kati haikusaidia kitu, ilibidi bibi yako ahame mji kwa muda…na watu wakaahidi kuwa wakimuona tena hapa kijijini watamuua,….’akatulia babu.

‘Lakini mtu kwao, bibi yako hakujali, alikaa kidogo huko alipokwenda na baadaye akarejea na walipomuona wakawa wananong’onezana kuwa eti ikitokea jambo jingine….linalofanana na hilo, eti bibi yako akiua mtu mwingine, watahakikisha na yeye wanamuua…..’akasema babu kwa uchungu.

‘Na kweli walifanya hivyo…?’ nikamuuliza babu, na hapo akainamisha kichwa akionyesha masikitiko, na alikaa hivyo kwa muda, nikajua alikuwa akilia kimoyo moyo, maana wanaume wengine hawalii kwa sauti,….wanalia ndani kwa ndani…na ndivyo alivyofanya babu

Alipoinua kichwa kuniangalia, niliona macho yake yakiwa yamejaa ukungu, ….na mara machozi yakaanza kumtoka.

NB: Inasikitisha, lakini ndivyo wanadamu tulivyo…..tutazidi kupashana kuhusu kilichotokea kwa bibi huyu..

WAZO LA LEO: Tusiwe na tabia za kuamini mambo ya kishirikina, ..….kwani hizo ni imani zisizo na ushahidi wa kitaalamu, …tunaweza tukajikuta tukigombana ndugu kwa ndugu, majirani kwa majirani kutokana na uzaifu huo.

Swali ni kuwa Je una uhakika gani kuwa mtu fulani ni mchawi?....Kama una uhakika huo, basi ufikisheni huo ushahidi kwenye sheria, ili haki itendeke,….tukichukulia sheria mkononi, tunaweza tukahukumu mtu asiye na hatia, na wenye hatia wakaendelea kutenda makosa hayo.

Ni mimi: emu-three

2 comments :

Anonymous said...

Thanks for sharing your info. I truly appreciate your efforts and I am waiting for your next write
ups thanks once again.

Check out my web site - galaxy s4

Anonymous said...

I'm gone to convey my little brother, that he should also pay a visit this web site on regular basis to take updated from hottest news update.

Feel free to visit my blog post :: hcg diet direct
Also see my website > hgc diet