Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, May 2, 2013

WEMA HAUOZI-2



Baada ya baba yako kunifukuza siku ile na mapanga sikutarajia kuwa nitakuja kuishi naye tena, sikutarajia kuwa tutakuja hadi kufunga ndoa naye, …’akaendelea kuongea mama, wakati huo akilini mwangu nikilikuwa nikiwazia yale aliyokwisha nisimulia babu, …nikiyahakiki na haya anayonismulia mama ambayo kweli yote yalikuwa ni ya ukweli…..

Nikakumbuka swali nililomuuliza babu, kutaka kujua kuwa huyo baba yangu wanayemzungumiza ni baba yupi, ambaye aliwahi kuishi na mama ambaye  siku moja alimuokoa mama akitaka kubakwa na wahuni wa mitaani,…na huyo baba aliyemkataa ni baba yupi, kwani nakumbuka babu yeye alisema hivi;

‘Baba yako aliyempa mama yako uja uzito…na kufikia kumfukuza mama yako kwa panga, alipotea hapa kijijini, na haikujulikana wapi alipokwenda, lakini mama yako atakuja kukuelezea vyema ,…… baadaye,

‘Baba aliyekuja kuishi na mama yako, alikuja baadaye akafariki…., familia yao ilikuja kulete kasheshe, kwani waliposikia ndugu yaoo huyo keshafariki, walikuja wakadai mali yote  ya ndugu yao huyo bila kujali kuwa mali hiyo ilichuma kwa ushirika kati ya mama yako na huyu marehemu,,…hayo mama yako atakuelezea mwenyewe zaidi ..’akasema babu

‘Babu kwanini usiendelee kunielezea wewe mwenyewe, unakimbilia kusema mama atanielezea mwenyewe zaidi,…babu nilihsawahi kumuulizia mama kuhusu maisha yangu, aliktaa kabisa kunielezea, najua kabisa hataweza kunisimulia maisha yake yalivyokuwa…sijui kwanini hataki…’nikamwambia babu naye akaendelea kusema;

‘Mama yako alipofukuwa hapo nyumbani kwao, na alipofika kwa huyo mwanaume na kufukuzwa, alishindwa sasa aende wapi….

Kiukweli Mama yako hakuwa mhangaikaji, kama walivyokuja kudai watu baadaye …..zaidi ya huyo mwanaume aliyempa mimba,, hakuwa na rafiki yoyote mwingine mwanaume, na hata alipofukuzwa kwao aliogopa kabisa kwenda kwa ndugu zao wengine, akiona aibu, na alihis kuwa huenda wao watamfukuza pia, wakijua ni nini kilichotokea, na wakiogopa kukosana na baba yako.

‘Mama akaanza kuhangaika huku na kule …’ babu alipofika hapo akajinyosha na kujiweka kwenye kiti chake vyema, halafu akasema;

‘Basi mama yako akawa anaishi porini….na kwa vile wanandugu walimuogopa baba yako wakashindwa kumchukua, wapo waliokuwa na uwezo huo, na walitamani kukuchukua, lakini kwa jinsi baba yako alivyokuwa….hapatani na watu kwa tabia zake mbaya za ulevi….na kujigamba kuwa yeye mtoto wake wa kumzaa hawezi kuzalishwa nyumbani,…watu wakawa kama wameungana kwa pamoja, na kumsusia yeye na maisha yake, hakuna aliyekubali kubeba lawama.

Mama yako akawa anaishi maisha ya kudandia, leo hapa kesho hapa, akawa mama wa mitaani. Na ili aishi, akajikuta anajiingiza kwenye biashara za hapa na pale , na hata zile zisizo faa, ili mradi siku iende, na wewe uweze kukua tumboni kwake…

Hauchi hauchi kukapambazuka, mama yako akafikia muda wa kujifungua…lakini hakuwa makini na tarehe hizo

Siku alipofikwa na machungu alikuwa, akifanya kazi ya kibarua kwa jamaa mmoja wa kihindi kama mfanyakazi wa ndani, na kwa vila alihitajika kufanya kazi hiyo ili apate chochote, na kuwekeza kwa ajili ya uzazi wake, akawa anajitahidi tu,  kwa shida, masimango, na kudharauliwa, na hata kunyanyapaliwa, hakujali,… hata pale  dalili za machungu ya kujifungua yalipojitokeza, hakujali….hakujua…maana dalili kama hizo zilikuwa zikimjia na kuondoka kabla...

Siku hiyo ilikuwa tofauti, machungu yalikuwa makubwa sana….hakuweza kuvumilia,…na akajikuta kizunguzungu kikimtanda machoni na ghafula akaanguka…. na bosi wake aliyekuwa karibu naye akamsogelea na kuanza kumtimba mateke huku akimsimanga;

‘Vewe mvivu sana, yaani sijui kwanini mume wangu amekung’ang’ania uendelee kufanya kazi hapa kwangu akijua Vewe ni mja mzito….hebu amuka huko….’akasema huyo mama.

Mama yako alijaribu kuinuka lakini hakuweza, kiuona kilikuwa kimekaza kweli kweli, maumivu yalikuwa sio ya kawaida, …hakuweza kuamuka, na alipojitahidi akajikuta akizidiwa na kudondoka, akatulia kimiya…..yule mama alipoona hivyo akajua mama yako amekwishakufa, akamuita mlinzi wake na kumuamrisha mama yako atolewe humo ndani.

‘Mama Bosi, sasa nitampeleka wapi,….huyu mtu, naona kama keshakufa?’ akauliza yule mlinzi.

‘Kamtupeni Popote pale lakini isiwe hapa nyumbani kwangu, kamtupe huko majalalani alipokuwa akiishi, ….’akasema huyo mama.

Basi yule mlinzi, akamuita mwenzake wakambeba huyo mama, na wazo lao kubwa likawa kwenda kumpeleka hospitalini, lakini wakiwa njiani wakakumbuka jambo.

‘Unamfahamu huyu mwanamke, je unawakumbuka ndugu zake, maana huu ni msala,…?’ akauliza.

‘Huyu mwanamke, nasikia aliwahi kufukuzwa kwao,….kwahiyo hatuwezi kumrejesha kwao au kwa jamaa yao yoyote, ….tunachotakiwa ni kufanya kama alivyosema bosi..tukamtupe maporini…’akasema mwenzake.

‘Hapana huo sio ubinadamu….mimi nina wazo, twende kwenye nyumba yoyote yenye mwanamke mtu mzima. Natumai yeye atajua la kufanya …’akasema na wote wakakubaliana na wazo hilo, wakaenda hadi kwenye nyumba moja wanayoifahamu kuwa anaishi mwanamke mtu mzima, na kumweka hapo kwenye kibaraza, na kuondoka zao.

Bahati nzuri, siku huyo bibi yako, alikuwa kaenda kwa jirani, kulikuwa na shughuli, na alichelewa kurudi mimi, nilikuwa nimejipumzikia ndani, nikapitiwa na usingizi, sikuwa najua kuwa kuna mtu katupwa hapo nje, kwenye kibaraza cha nyumba.

Bibi yako wakati anarudi ndio akamuona mtu kalala hapo kibarazani kwake…. Kwanza aliogopa akijua kuwa ni maiti, ……akapita hadi ndani na kuniamusha…na mimi kwa haraka nikatoka nje kuangalia.

‘Nilimkagua huyo mtu, yaani mama yako, na nikagundua kuwa hajafa, …

‘Huyu mtu hajafa,…..sasa tufanyeje….?’ Nikamuuliza.

‘Inabidi tuwaite majirani na mjumbe….maana hapa tunaweza tukazua kesi..’akasema bibi yako, na mara mama yako akazindukana, na kutaka kuinuka, na sisi tukamsaidia akaweza kukaa vyema. Tukamhoji ni kitu gani kimemsibu, na wakati anajaribu kuelezea, uchungu ukamshika,…

‘Huo sasa ni uchungu,…na hospitali hapa ni mbali, mpaka kukodi baiskeli….’akasema bibi.
Tuwaite majirani watusaidie…’nikasema na wakati naondoka, bibi yako akawa anamsaidia mama yako.

Nilipita kwa majiani, lakini wengi wa akina mama walikuwa bado kwenye hiyo shughuli, sana sana niliowakuta ni akina baba, ambao wasingeliweza kumsaidia bibi yako kwenye mambo ya kumzalisha mama yako…kama ikibidi, kwani bibi yako alikuwa anafahamu mambo ya ukunga.

‘Nawaombeni tu, mnisaidie tukampeleke hospitali….’nikawaambia hawo majirani akina baba, na wakafika wawili, lakini tulikuwa tumechelewa, kwani tulipofika tulimkuta bibi yako akiwa kakashika kachanga.

‘Oh, amejifungua salama….’akasema bibi yako.

‘Hivyo ndivyo ulivyozaliwa mjukuu wangu, ….’akasema babu huku akitabasamu.

********

Babu alipofika hapo kwenye akili yangu, nikawa namsikiliza mama aendelee kuanzia hapo, ili kuthibitisha hayo, na ukumbuke kuwa wakatii huo mama alikuwa akiendelea kuongea, mama akasema;.

‘Mwanangu hata sijui jinsi gani nilivyokuzaa ninachokumbuka ni machungu,….machungu ambayo nilitamani roho itoke nikapumzike,…nilikumbuka siku nilipowahi kufika kiliniki , ilikuwa mara moja tu, na yule nesi alinielekeza mambo mengi, ya kufuata, lakini sikuwahi kuyafuata kabisa…sikuwa na muda huo, muda wote ulikuwa wa kuganga njaa, kuilea mimba…..oh.

Basi, hata uchungu uliponifika sikujua ndio muda umefika wa kukuzaa, …ulikuwa uachungu ambao sikuwahi kuupata kabla…. kitu cha mwisho kukisikia ni sauti yako ukilia, nikajua kweli sasa nimekuzaa na upo salama, na hapo hapo, nikapoteza fahamu.

Nilipoamuka ilikuwa ni usiku, niligeuka na kukuona umelezwa karibu yangu, ikiwa ni giza, …unajua tena nyumba za kwetu, hakuna umeme, taa ni kibatali, na taa ilishazimika kwa kukosa mafuta, nikainuka na kukuangalia kwenye giza,..sikuweza kuiona sura yako ya uchanga…

Nikahisi vikono vyako vidogo vikinishika…., hapo akili haikuwa yangu tena…..nilijikuta nikipandwa na hasira za machungu, hasira za kutelekezwa, hasira za kunyanyaswa na matajiri,…lakini vile vimkono vyako, vikanifanya moyoo uone huruma, nikalala vyema na kukunyonyesha na kuhakikisha kuwa umeshiba,…

Halafi kitu kikawa kimenizinga akilini, maana sikujua nini ninachokifanya kwa wakati ule, nikainuka kitandani, kwa shida,maumivu, kuchoka,..yaliniandama, lakini sikujali hayo, nikajikakamua na kutoka nje.

Nikatoka, nje, na kupata kibaridi cha usiku, sikujua naenda wapi, …miguu yangu ikawa anatembea tu, kwa kunyata….nikiyumba, ..nikatembea , nikatambea, hadi karibu na mto. Nilipofika hapo, nikahisi kiu, nikaamua kuinama na kupata maji..

Mara macho yangu yakahisi mtu amelala, ufukweni, nusu ndani ya maji, mwanzoni nilizania ni mamba, lakini huu mto haujawahi kuwa na mamba, nikajikuta nikimsogelea, na nilipomfikia, nikainama….alikuwa ni mwanaume…nashangaa sikuogopa, nikaweka kidole kwenye shingo ya huyo mtu kuangalia mapigo ya moyo, nikakuta bado yupo hai.

Nikajikakamua nikamvua nje ya maji, …..na hapo nilikuwa hoi, kwasababu ya kutumia nguvu nyingi kumtoa huyo mtu, …nikakaa pembeni yake, na kwasababu ya kuchoka, maumivu,…nikajikuta nimeshikwa na usingizi, ….na mwili wangu ukawa umelalia kifuani mwa huyu jamaa…..

‘Wewe amuka haraka,….tuondoke hapa, polisi wananitafuta…’ilikuwa sauti iliyoniamusha. Kulikuwa bado na kiza, lakini ilionyesha kuwa ni alifajiri.

‘Kwani wewe ni nani?’ nikamuuliza huku nikiingiwa na wasiwasi.

‘Usijali,..ilimradi wewe umeniokoa …basi utakuwa rafiki yangu…tuondoke haraka, hapa nilipo nina pesa nyingi,….lakini natafutwa na polisi, siwezi kuwapa hizi pesa, tumehangaiak pamoja, lakini wenzangu wanataka kunidhulumu, sikubali….najua hawo wenzangu wakinikamata wataniua, nab ado polisi nao wanatutafuta….sikubali kwenda jela….’akasema huyo jamaa. Ilikuwa bado giza, na sikuweza kumtambua vyema ni nani huyo mtu…alikuwa kiongea kuonyesha kuwa bado amelewa.

Bila kufikiria zaidi nikamfuata, …..tukawa tunakimbia kidogo kidogo, hadi tukafikia kituo cha mabasi yanayokwenda Dar, akakata tiketi za watu wawili, tukaingia ndani ya hilo basi na mimi nikamfuata, tukakaa kwenye kiti…. Wakati wote huyo jamaa alikuwa kavaa kofia pana, na mawani, ambayo sijui aliyapatia wapi, maana wakati namtoa kwenye ule mto sikuyaona hayo mawani, zaidi ya begi, chafu chafu alilokuwa kalikumbatia. ..Alikuwa na madevu mengi

‘Tunakwenda wapi?’ nikamuuliza.

‘Dar….huko tutaanza maisha..’akasema nakuinama,….kulalia mikono yake na mara nikamsikia akikoroma kuashiria kuwa keshalala…..alikuwa kalikumbatia hilo begi lake utafikiria ni mtoto wake. Na kwa vile kulishaanza kupambazuka,akili sasa ikawa anaanza kunirejea, nikakumbuka,…nikamkumbuka mwanangu, nikasimama, nikitaka kushuka…

‘Unakwenda wapi..?’ akaniuliza huyo jamaa akiwa kanishika mkono wangu

‘Mwanangu….namtaka mwanangu….’nikaanza kulalamika.

‘Huwezi kurudi tena, hapa tupo mbali sana, kama ni mwanao, utakuja kumrejea baadaye, kumbe una mtoto, sasa ilikuwaje ukamuacha mtoto wako…. kwasasa huna jinsi,….subiri fufike Dar….’akasema huyo jamaa na kuendelea kulala.

Kwakweli niliumia sana,..sikujua ni kitu gani kilichonifanya nifanye hivyo, na sikuweza kutuliza akili yangu hadi ulipofika Dar, na tukawa tunashuka kwenye basi, na hapo balaa jingine likatkuta, ..

‘Ule mkoba wangu umeuona?’ akaniuliza huyo mtu.

‘Ulikuwa umeushikilia mkononi wakati wote, …’nikasema.

‘Haiwezekani,….pesa zote zilikuwa ndani ya huo mkoba, mungu wangu..tumekwisha,…..’akasema huku akiwa kashikilia kichwa, na baada ya kuhangaika huku na kule kuutafuta huo mkoba wake bila mafanikio na kuhakikisha kuwa keshaibiwa, akaangua kilio kama mtoto mdogo.

‘Nimeumbuka…oh, juhudi yote ile, hata kukaribia kutolewa roho, imeishia patupu..oh, sasa tutakwenda wapi,…’akawa analalamika.

‘Turudi nyumbani..’nikasema

‘Kwa nauli gani?’ akauliza.

‘Mimi hata sijui, wewe ndiye uliyenileta huku, na wala sikuwa na lengo, hilo nimemuacha mtoto wangu mchanga , na sijui ataishije….’nikasema na yule jamaa akawa anaondoka, na mimi nikawa namfuatilia nyuma.

NB: JE ni nini kitafuata? Tuwe pamoja!

WAZO LA LEO: Kuzaa au kutokuzaa ni majaliwa ya muumba. Ukijaliwa kupata watoto, mshukuru mola wako, na kama hujajaliwa mshukuru pia. Mkiwa kwenye ndoa mkakutana na mitihani ya namna hiyo, msikate tamaa, na wala msinyanyapaliane…

Lakini hapa kuna tatizo, kwani kuna watu, wengine wanapata watoto, na kuishia kuwatelekeza au hata kuwaua, kwa sababu zao mbali mbali, huo ni unyama. Tukumbuke kuwa kuna ambao wanatafuta watoto, na kuomba usiku na mchana ili mola awajalie angalau wapate hata mtoto mmoja, lakini uzazi, hawana, au hata kama wanacho kizazi, lakini mola hajawajalia. Wewe unaua….hiyo 
Ni mimi: emu-three

No comments :