Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, May 30, 2013

WEMA HAUOZI-14


Mjumbe alipokuja kwangu, alianza kwa kunisihi kuwa ni bora nikaondoka hapo kwenye hiyo nyumba, ili wahusika waweze kukamilisha mambo yao ya kuweka mali za marehemu kwenye umiliki wa kifamilia kwa muda, hadi hapo mirathi na taratibu nyingine za kisheria zitakapotangazwa na kama kuna lolote jingine, nilifikishe kwa wanafamilia, ili taratibu zote zifuatwe ikiwemo haki ya mjane, na mimi hapo hapo nikamuuliza;

‘Mjumbe wewe ni kiongozi wetu wa eneo hili, sawa si sawa?’nikamuuliza huku tukiwa tumesimama, sikutaka hata kumkaribisha kiti, na mkononi nilikuwa nimeshikilia panga. Silaha yangu kubwa ilikuwa panga, na panga langu lilikuwa refu na zito, likiwa na makali.

‘Ni sawa….’akanijibu huku akionyesha kuwa na wasiwasi,… sijui ni kwasababu ya hilo swali, au panga nililoshika au alikuwa na wasi wasi wa jambo jingine ambalo huenda hakulitaka litokee, na alikuwa akichelea likitokea kunaweza kuharibu amani. Nilijua kabisa kaja na kundi la watu ,…japokuwa wao hawakuonekana, walikuwa wanasubiria sehemu nyingine, mimi nilishajiandaa kwa lolote lile, na nisingelikubali kutoka humo, labda wanitoe nikiwa sijitambui, au maiti…’babu akawa anaongea kwa ujasiri.

‘Mjukuu wangu, mimi najiamini, inapofikia sehemu ya kudai haki yangu siogopi kitu…, huwa siogopi, nafahamu kabisa yule anayefanya jambo la dhuluma, moyo wake umetekwa na wasiwasi,..na hilo linamweka katika udhaifu wa kujiamini, na hapo unapata mwanya wa kumshinda. 

'Unajua mkuu wangu hata haya majambazi yanayokuja kupora watu kwa silaha, wasingeliweza kufanya hivyo, kama tungelikuwa tunajiamini, wao kwanza wanachofanya ni kuwaondolea hiyo hali ya kujiamini, na kuwajengea hofu, na kwa udhaifu wetu, tunaogopa…japokuwa, kiubinadamu inahitaji moyo, na ujasiri, kitu ambacho ni adimu kwa bina-adamu….’akasema babu.

`Mjukuu wangu, katika maisha yako, kumbuka mambo hayo, kwanza kuhakikishia unasimama kwenye haki, na kuitenda haki, …uwe mkweli na utende yaliyo kweli…usiwe mzembe, mvivu, kuwa wa kwanza kujituma kwa kila jambo, ili upate baraka ya mwanzio, hayo yatakupa ufahamu wa kujiamini,…ni lazima utajiamini, maana hutakuwa na wasiwasi,…

Nikamwangalai mjumbe kwa kumkazia macho, na kuendelea kumuuliza maswali nikitaka kwanza kujue lengo lao, pili kujaribu kumuelimisha, ili alainike na kuondokana na dhamira yao hiyo, nikamuuliza swali;
‘Kwahiyo wewe kama mjumbe, mambo yote ya eneo lako hili yakitendeka unayaona, sawa si sawa?’ nikamuuliza mjumbe na yeye akanijibu huku akinikazia macho kujionyesha kuwa haniogopi, na yeye kama mjumba ana mamlaka yake.

‘Ni sawa kwa yale yaliyopo wazi, ambayo yanaonekana kwa upeo wa macho na kusikia, kama yanafanyika ndani ya nyumba za watu, na kwa siri, mimi sio mchawi, au mtalaamu wa kugundua mambo yaliyo siri kiasi hicho,…. siwezi kusema naweza kuyaona yote’akasema.

‘Na mimi nimeuliza hilo kwa yale mambo ambayo yapo wazi, sijalenga mambo ya ndani ya nyumba, …na hatuzungumzii maswala ya gizani mjumbe…’nikamwambia na yeye akasema;

‘Mimi najitahidi sana kuwa makini kwa kadri ya uwezo wangu, na ikiwa ni pamoja na kuwapitia watu wangu, na pia kuhakikisha kuwa kila kinachotendeka kwenye eneo langu nakifahamu….kwa ajili ya usalama na matakwa ya eneo letu, ilimradi yapo ndani ya sheria, na kama yanakiuka sheria, sitasita kuyafikisha kunakostahili, kama yanazidi uwezo wetu…’akasema.

Mjumbe wetu huyu namfahamu sana, huwa wakati mwingine ana maneno mengi yasiyo na vitendo, na kujisifia kusiko na sababu, ni mwanasiasa mwenye lugha ya kushawishi, lakini udhaifu wake ni kuwabeba wale wenye uwezo, ….nikamuuliza;

‘Na hata kukiwa na ujenzi wa nyumba, au maduka unakuwa makini kufuatilia kuwa ni nani amejenga sawa au si sawa?’ nikamuuliza na hapo, akatulia kama swali hilo limemgusa.

‘Ni sawa,…naweza kusema hivyo, kuwa kama kuna nyumba mpya inajengwa naifuatilia, kwasababu ni sehemu ya nyumba zangu, kama ujuavyo mimi ni mjumbe wa nyumba kumi, zikizidi nina haki ya kufahamu, ili serikali za mitaa ijue hilo, japokuwa kisheria hilo lilihitajika kuwa mkazi wowote akijenga nyumba, au muhusika ni lazima kuifahamisha serikali za mitaa kupitia kwa mjumbe wake, lakini wengine hawafanyi hivyo, …ila kwa vile ni eneo langu, hata kama atakuwa hakufuata sheria za kujitambulisha, nitafahamu kwani ujenzi haujifichi…’akasema.

‘Kwahiyo ilipojengwa hii nyumba, na duka, wewe uliiona kama mjumbe na ulifahamishwa kisheria au sio?’ nikamuuliza.

‘Niliiona, japokuwa sikufahamishwa kisheria,…lakini kwa vile nafahamu udhaifu wa watu wangu, nilijitahidi kukutana na huyu mwanamama, …na nilifika hapa mara kwa mara kuingalia ikiendelea kujengwa na kama unavyojua ni moja ya nyumba zilizojengwa kwa haraka na kwa kisasa zaidi….’akasema.

‘Na ulimfahamu vyema anayejenga hii nyumba ni nani, sawa si sawa?’ nikamuuliza.

‘Nilimfahamu ndio…’akasema akionyeshwa kukerwa na maswali yangu, na yeye kama kiongozi, alijiona kama namshushia hadhi yake, na hapo alikuwa kwa dhamira yake nyingine na huenda hakuhitajia  maelezo zaidi.

‘Ni nani aliyekuwa mjenzi wa hii nyumba?’ nikamuuliza na hapo akaangalia nje kwa kupitia mlangoni, maana pale aliposimama, alikuwa akiona nje, mimi sikuwa naona huko nje, kwani nilikuwa sehemu inayozuiwa na mlango kwa ndani…na alivyoangalia nje ilikuwa, kama vile anataka kuhakikisha kuwa hayo anayoongea hayasikiki.

‘Maswali yako bwana, mjenzi si fundi nani hii, aah, jina lake nani vile, …’akasema akionyesha kwa hakuelewa hilo swali nilikuwa na maana gani.

‘Sijaulizia fundi, …naulizia aliyejenga hiyo nyumba, ….ni nani?’ nikauliza sikutaka kumfafanulia vyema nikiwa na maana yangu

‘Ohoo, tatizo lako unauliza maswali mengi kama polisi, au wakili mahakamani, ….au wazee wa baraza, haya, kama ulikuwa na maana hiyo, aliyejenga hiyo nyumba alikuwa Mama wa hii nyumba…’akasema.

‘Ukisema mama wa hii nyumba una maana gani?’ nikamuuliza ili niwe na uhakika, japokuwa nilifahamu ana maana gani.

‘Unajua hapa hatutaki kuangalia kumbukumbu zilizopita, tunachohitajia hapa kwa sasa ni sheria na taratibu zote za kimila…mimi nafahamu kabisa lengo lako ni nini, hayo maswali yote, nafahamu msingi wake ni nini, lakini nikufahamishe wazi, kuwa hapa, hatuangalii  swala la kujenga na kusimamia ujenzi. Katika nyumba kuna wajenzi, kuna wasimamizi,…na yoyote anaweza akafanya hivyo na bado asiwe mumiliki halali wa hiyo nyumba, sijui unanielewa maana nakuona haupo makini na sheria…’akasema mjumbe akionyesha kujiamini, na baadaye akaendelea kuongea kwa kujikoga;

‘Unasikia sana, …tunapoangalia mumiliki wa nyumba, tunasimamia kwenye sheria, maana hapo kuna maandishi…kuna stakabadhi za umiliki, kisheria, ….hayo mzee ni mambo ya wasomi, sio enzi zenu za kuaminiana kwa mdomo tu..siku hizi ni mambo ya karatasi, ….natumai umenielewa,…na kama umenielewa au hukunielewa,…naomba sasa unisikilize na mimi, ili tunamalize kazi….’akasema akionyeshea kwa vitendo kama vile kashika katarasi au hiyo hati miliki mkononi.

‘Mjumbe mimi ni mkazi wako, na nina haki ya kukuuliza ili tuwe sambamba, na bado hatujamalizana, nakuona wewe unachukulia haya mambo kwa haraka, ….na haraka haraka haina baraka, ….’nikasema na akanikatiza kwa kusema;

‘Sasa naona tusipotezeane muda kwa maswali yako ….hayo yatahitajika baadaye kama ni lazima, muda ukifika…mimi hapa nimekuja kwa kazi moja, ambayo kisheria, umekiuka,….na tumeliangalai hilo na wenzangu, tukaona ni bora tufanye hivyo, na naomba wewe kama mzee mwenzagu unielewe….ili tusije tukafikishana kubaya….na tumeishi vyema kwa muda mrefu, bila kuleteana utata, na hili lisitufikishe huko,….hapa naona mzee mwenzangu umeteleza…’akasema huyo mjumbe pale aliposikia watu wakiongea na kulalamika huko nje.

Sauti za watu zilisikika zikisema, ‘mjumbe mbona unatupotezea muda, atoke nje huyo mtu…’

‘Mjumbe, ni kweli unayoongea kuwa kuna sheria, za maandishi…sijui karatasi, hati miliki na mambo kama 
hayo…., lakini ukumbuke kuwa sheria hizo zinatokana na ushahidi wa vitendo, na watu siku hizi ni wajanja, hasa hawa wanaojifanya ni wasomi… maana ukiwa msomo wa kweli, huwezi ukafanya hayo wanayofanya wao….’nikasema huku nikiwa sibandui macho yangu kwake, japokuwa yeye alikuwa akiniangalia na kugeuka huku na kule.

‘Vijana wetu hawo wanaojiita wasomi, wanaweza kutumia karatasi na kalamu vibaya, bila kujua madhara yake baadaye,…imefikiwa wakati sasa mwenye haki anadhulumu kwa kutumia karatasi na kalamu, kwa vile huyo mtu hajui sheria,au hata kama anajua kidogo, lakini ulaghai unaweza ukapita chini kwa chini , watu wakatafutwa, na hadaa ikatumika, na haki ya mtu ikapotea hivi hivi, tumeyaona hayo mara ngapi yakitendeka…tena kwenye kaya zako mwenyewe…’nikamwambia mjumbe.

‘Kama nilivyokuambia hayo kama yatakuwepo, tutayaangalia kisheria, …na udhaifu huo upo, lakini mwisho wa siku tunakuja kusuluhisha, yanakwisha, au sio…hata kama yalitokea kwangu, lakini mimi kama mjumbe, nilijitahidi tukayaongea kwa heri, yakaisha, na ndivyo ninavyohitajia iwe hivyo,…lakini kwa sasa….naona nikumbie wazi moja kwa moja, kuwa sisi watendaji wakijiji, tumeonelea, ili kuleta sluhu ya hilo …. unahitajika utoke humu kwenye hii nyumba, ili iwe mikononi mwa wahusika…’akasema.

‘Hawo wahusika ni akina nani?’ nikamuuliza huku nikiwa najaribu kuangalia nje japokuwa sikuweza kuona huko nje, lakini kwa hisia nikawa nawachora hawo waliomtuma, na hawo wahusika aliokuwa akiwamaanisha huyo mjumbe, huenda wapo huko nje wanasubiria.

‘Ni familia ya merehemu, …wao ndio wahusika  wa muda, ambao watahakikisha kuwa mali za marehemu zipo kwenye usalama kabla swala la mirathi halijatangazwa, na wao hawana nia mbaya, wanachohitajia ni kuwa mali zote zinazotambulikana kisheria kuwa zilikuwa na za marehemu ziwe mikononi mwao ili baadaye kila mwenye haki yake apate..’akasema mjumbe akiniangalia machoni, mimi hapo nikawa kimiya kumsikiliza na hapo akapata mwanya wa kuongea zaidi, akasema;

‘ Kwa mfano marehemu alikuwa, na mtoto mdogo, ….na pia alikuwa na mke, na walikuwa na mali zao, kwasasa, baada ya msiba, tunasema ule `ubia’ tunaweza kutumia neno hilo, ingawaje linaweza lisiwe na maana ya moja kwa moja,…`ubia’ nikiwa na maana makubaliano ya ndoa, mahusiano ya ndoa yliyokutanisha watu wawili, wakapata mtoto, au watoto,…hayo sasa yamevunjika…’akatulia.

‘Kama huo ubia haupo tena, ni lazima kuwe na masuluhisho….ili kuelewa ni vipi hatima ya baadaye, tukiangalia mke, mtoto na mali zao….na hivyo vyote kimila, kisheria vinatakiwa visimamiwe, na watu waka karibu, ambao ni familia…na familia hapo tuna maana, baba na mama, au ndugu wanaohusiana na hiyo familia…’ akatulia kidogo.

‘Tukiangalia kwa hapa, wanaohusika sasa ni ndugu, kaka wa marehemu, wao ndio wapo karibu na familia hii, maana wazazi wao hawapo….umenielewa mzee mwenzangu?’ akauliza.

‘Nakuelewa sana,…na hilo silipingi kwa msingi huo…kama kweli lina lengo jema,..’nikasema na hapo akatikisha kichwa akitabasamu , akijiaminisha kuwa huenda nimelainika kwa maneno yake, halafu akasema.

‘Kwa maelezo hayo, na kwa vile umenielewa,…ni kuwa basi, mtoto, mke wa marehemu na mali yote, vite hivyo vinahitajika kuwa mikononi mwa hiyo familia, na hilo nafahamu sana kuwa wewe unalijua vyema, hayo unayatambua vyema mzee mwenzangu, tusitake tukosane kwa vitu vilivyo wazi…’akasema.

‘Mjumbe,…neno kukosana kwa sasa halipo,..ila mimi nakushangaa wewe unalitamka sana, kuonyesha kuwa huenda umekuja kwa lengo hilo. Mimi sihitaji shari, wala kukosana na mtu, maana baada ya arubaini ikiisha, mimi nitakwenda kwangu, na kumuachia mwenye mali hizi …mali zake…sasa wewe mjumbe naona unavutika kirahisi kufanya yale utakayokuja kujijutia baadaye…’nikaongea kuhitimisha.

‘Mjumbe…..kwanini watu wanakuteka kiakili, ukasahau majukumu yako, ukasahau ile busara yako…, ndio maana kwanza nilikuuliza ni nani aliyejenga hii nyumba, ukasema ni mama wa hii nyumba, na aliijenga kuanzia mwanzo hadi mwisho ukishuhuda wewe mwenyewe kwa macho yako, mumewe kipindi hicho hakuwepo,…kwahiyo kivitendo na kihaki, hizi sio mali za urithi, ….labda hapo tuliongee kivingine lakini sio mali zinazohitajika kuweka kwenye meza ya urithi…sijui mjumbe hapo tupo pamoja…?’ nikamuuliza.

‘Tusirejeshe mazungumzo nyuma, hayo yatakuja baadaye, kama kuna utata wowote, mimi sioni kama kuna tatizo hapo…kwani baadaye ndipo tutajua hiki ni cha urithi, au sio cha urithi, wewe unafanya haya mambo yawe magumu, yaonekane kuwa kuna tatizo,….hapa hakuna tatizo kila mtu anajua kuwa hivyo inavyotakiwa iwe ndivyo ilivyo, sheria zipo wazi, na sisi ni viongozi, tutahakikisha hilo linatendwa kisheria,…kama mali hii ni ya mjane, haipo kwenye kundi la urithi, hilo tutakuja kulisimamia, na hapo huenda ikahitajika kwenda mahakamani kama kutakuwepo na kutokukubaliana.. kwanini mzee mwenzangu hutaki kunielewa’akasema.

‘Mjumbe, sijasema sitaki kukuelewa, nakuelewa sana, ndio maana nikajaribu kukumbusha mambo ambayo ni muhimu sana,….nahisi , na hili ndilo linanifanya mnione kuwa ni mtata. Nakuona kabisa kuwa wewe unafuta matakwa ya watu ambao nia yao sio njema, kwani nawajua vyema hawo watu na malengo yao, na nini wanakusudia kukifanya…na sio kihisia bali wao wenyewe wamenihakikishia hivyo, kuwa wanataka kumiliki mali zote za marehemu na mjane hana chake, hivi wewe mjumbe hayo yangetendeka kwa binti yako ungelikubali?’ niiamuuliza huku nikimwangalia na yeye akawa kama anakwepa kuniangalia machoni moja kwa moja.

‘Mzee mwazangu, tusitake kupotezeana muda, mimi kama mjumbe nitahakikisha kuwa haki ya kila mtu inatendeka, na ikishindikana tutalipeleka hili swala mahakamani, na mimi kama mjumbe nitatoa ushahidi wangu, kama nilivyoona, kama mjumbe, ….kwahiyo sioni tatizo lipo wapi, sheria zitamlinda kila mtu bila kubagua …wewe toka kwenye hii nyumba ya watu, na kabidhi kila kitu kwa wanafamilia ili kuepusha shari, maana wenyewe wanakuona kama mvamizi wa mali za marehemu….’akasema mjumbe.

‘Mjumbe, kwanini unatekwa kimawazo na hawa watu…?’ nikamuuliza nikimwangalia kwa makini, na kabla hajajibu nikasema;

‘Mjumbe, kabla ya haya tulishawahi kuongea jinsi gani watu wanavyokuja kuchukua mali za marehemu, na kuwatelekeza wajane na watoto wao, na wewe ukaahidi kuwa hilo halitaweza kutokea kwenye kaya zako, ….unakumbuka mjumbe?’ nikamuuliza na mjumbe akaangalia saa na kusikiliza kelele za watu wakipiga ukelele kumuamrisha nitolewe nje.

‘Mjumbe nakukumbusha pia kuwa mke wangu ameuwawa ndani ya kaya zako na kundi linalojifanya kuwa linapambana na wachawi,…na hukuchukua hatua yoyote, na hilo lilikuwa moja ya ahadi zako kuwa utapambana na watu wanaowazalilisha wazee kwa imani zao haba za kishirikina, unakumbuka hilo wakati unapita nyumba hadi nyumba kuomba ujumbe wa nyumba kumi, wenzako wote tulikataa hilo jukumu japokuwa tuna uwezi zaidi yako…?’ nikamwambia na hapo nikawa kama nimemkasirisha.

‘Mjumbe siku tukio lilipotokea la kuvamiwa nyumba yangu, niliitwa nikaambiwa kuwa unanihitaji, kwa vile mimi ni mmoja wa wazee wa kijiji, na nilijituma kama kawaida yangu kuja kwako, kumbe ni uwongo, kumbe ilikuwa mbinu ya kunitoa mimi kwenye nyumba ili watu hawo, wahalifu wafanye lile walilokusudia, na huenda wewe ulishirikishwa maana kwanini siku hiyo ulitafuta kisngizio cha kutokuwepo nyumbani, …huenda ulijitungia safari za ajabu ajabu ili hilo tendo litokee, …ninakuonywa mjumbe, kuwa hayo yote sisi raia tunao-onewa tunayaona….’nikasema.

‘Hayo ni dhana yako potofu ….ni mawazo yako haba, na hayana ushahidi wowote, na hayahusiani na hili, mimi kama mjumbe nafuata sheria, wewe hukustahili kuzuia hii nyumba, kwa vile huna haki yoyote, wenye haki hiyo ni wanafamilia na kama mjane angelikuwepo hapo, labda angelikuwa na mamlaka hayo, lakini sio wewe…mjane, mtoto wote wapo kwa familia husika kwanini hawi hukuwazuia,…sasa hivi unakuja kuzuia mali….huoni hapo unakuwa mtata!’akasema mjumbe

‘Mjumbe mimi nilikuwa naishi hapa na wanafamilia wa hii nyumba, na walinikubali kama mzazi wao, na hata walifika kwako wakanitambulisha kwako hivyo, na hata baada ya hujuma ya kumuua mke wangu na kuchoma nyumba yangu ilipotokea mke wa marehemu alikuja kwako…oh, alikuelezea ulipofika hapa kuwa mimi nitaishi naye kama baba yake…..je umeyasahau hayo?’ nikamuuliza.

‘Ndio aliniambia na pia alifika kwangu, hilo silikatai, lakini hilo linahusiana vipi na hii nyumba na mali za marehemu?’ akauliza.

‘Ni kwasababu mimi kama mzazi wao, nina haki ya kuhakikisha kuwa mali zao zinakuwa kwenye usalama hadi hapo arubaini itakapokwisha na hadi hapo mumiliki halali wa mali hizi ikiwemo hii nyumba an duka watakapofika, na yeye ndiye atajua ni nini cha kufanya…natimiza haki yangu kama mzazi, …na hili uliangalie kwa macho mawili, kuwa hata wewe una watoto, linaweza likatokea kwako, je utakaa kimiya, ukiona kuna watu wanataka kumdhulumu binti yako?’ nikamuuliza, na mara mlango ukafunguliwa kwa fujo, akaingia askari mgambo wa kijiji na vijana wengine wakafuatia baadaye.

‘Mjumbe tumeingiwa na wasiwasi, ..tunaona huyu jamaa asije akakufanya vibaya, …je tufanye kazi yetu, maana huyu jamaa ukienda naye kisiasa hutamuweza, …tupe nafasi tumtoe nje, hata kama ana nguvu za giza, sisi tutazimaliza…..’akasema mmoja wa vijana mwenye mwili uliotuna na mikono ilikuwa imejaa misuli.

Nilimwangalia mjumbe kwa makini, nikusbiri kauli yake…ingawaje nilijua hatakuwa na jipya, hapo nilikuwa kwenye vita ya kujihami, na panga langu lilikuwa vyema mkononi, sikuwa nimewaangalia hawo watu, nikatulia.

‘Kwa mara ya mwisho nakuomba utoke humu ndani…’mjumbe akasema, nikahema na kutabasamu nikasema;

‘Kama nilivyokuambai mjumbe, mimi nalinda mali za watoto wangu, ….kama mlinzi halali, na kama mzazi wao sitaweza kutoka hapa hadi hapo mama wa nyumba hii, ambaye ndiye ndiye mjenzi, ndiye  mumiliki halali, aliyejenga kwa pesa zake….’nikasema na kabla sijamaliza, hawo jamaa wakacheka kwa dharau, hata mjumbe naye akaungana nao.

‘Mzee mwenzangu unajua mwanzo nilikuwa nakusikiliza tu, ili kujua mawzo yako yamelenga wapi, hivi kweli unaamini kuwa huyo mwanamke alijenga nyumba hii kwa pesa zake, …alikuwa akifanya kazi gani hadi akapata hizo pesa, huwezi kujiuliza maswali kama hayo…Mzee mwanzangu hujajiuliza maswali mengi kuhusiana na hili, na kutambua kuwa kuwa hizo pesa zilikuwa za marehemu….!’akatulia huku akishika kichwa kwa kidole chake.

‘Huyo marehemu alizipata wapi hizo pesa, hebu na wewe niambie, kwasababu marehemu tulikuwa tukiishi naye hapa siku zote, na aliondoka, huko alipokwenda na hakukaa kwa muda mfupi na kureejshwa hapa , kukabiliana na mashitaka ya wizi,…..na akafungwa, na mnakumbuka akiwa kifungoni, kulipita muda, na ndipo huyu binti, mwenye nyumba hii, akafika, toka huko mjini…na kuanza ujenzi wa hii nyumba, sasa nimbieni huyu marehemu alipoletwa hapa alikuja na hizo pesa, au aliwahi kuwaambia kuwa alimuachia mkewe pesa na ndizo hizo alizokuja kujengea hii nyumba, au mnafikiria hivyo tu…?’ nikamuuliza.

‘Hayo maswala yalishamalizwa mahakamani, na walioibiwa pesa zao, walishasamehe, lakini pesa hazikuwahi kurejeshwa, ina maana hizo pesa zilikuwa wapi?’ akaniuliza, na wenzake waksema;

‘Alibakia nazo mkewe…’wakasema.

Mimi nikachekwa kwa dharau na kusema,;

’ Ama kweli jambo msilo lijua ni kama usiku wa giza, hivi mnakumbuka kuwa huyu binti aliwahi kusakamwa kwa hilo kuwa haya maendeleo aliyoyaleta kwa kujenga nyumba na miradi yake ni kutokana na hizo pesa za wizi, na wale waliokuwa wameibiwa, wakafuatilia lakini baadaye walikuja kugundua kuwa sio hizo pesa zao….kwanini hawakumshitaki huyo binti, kwa kupatikana na pesa za wizi, kwanini hamjiulizi hilo…’nikawaambia.

‘Hahaha…sasa unataka kusema nini, huo ulikuwa ni ujanja wa mwanamke, aliwahadaa tu, lakini kiukweli hizo pesa zilikuwa za mumewe….’akasema mmoja wapo.

‘Mjumbe nilishakuambia ukianza kuongea na huyu mtu kisiasa hutamuweza, sisi tunamfahamu sana, dawa yake ni kumtoa kwa nguvu…’akasema yule jamaa aliyejazia kifua, na alionekana akitoa jasho la hamasa, akiwa na rungu lake mkononi.

‘Naona tumefunga mjadala, nakuamrisha utoke humu ndani, na unikabidhi ufungua wa nyumba na wa duka…’mjumbe akasema.

‘Mjumbe msimamo wangu umeshausikia sijabadili msimamo wangu, sina zaidi la kusema…’nikasema

‘Narudia tena,….ili kuepusha shari tunakuomba, tunakuamrisha utoke humu ndani na utukakabidhi ufungua za nyumba na duka…’akasema mjumbe , mimi nikaa kimiya, akawageukiwa wenzake na kuwaangalia kila mmoja kwa wakati wake.

‘Kwa mamlaka niliyopewa na serikali ya mtaa, kuwa mtu anapokuwa mkaidi kama huyu, tunaweza kumshawishi kwa njia nyingine iliyo salama ili tuepushe shari, naombeni mmtoe huyu mtu, kwenye hii nyumba na mchukue funguo ili tuzikadhi kwa wenyewe,…’akasema mjumbe na kutoka nje.

Hapo kazi ikaanza, sikukubali, na wao walikuja kutambua kuwa mimi sio lele mama kama wanavyoniona kuwa ni mzee, kwani kwa dakika kumi tu, wote walikuwa hoi…hakuna aliyeweza kunisogeza pale niliposimama.

‘Mjumbe huyu mtu ni mkaidi, inabidi tutumie nguvu…’akasema mmoja wapo

‘Kama mumeshindwa, ngoja niwaongezee nguvu mpya…’akasema mjumbe na wakaingia vijana wengine na jumla yao wakawa watu saba, na hawa walioingia sasa hivi waliingia kwa shari, kwani walianza kunipiga na marungu yao kwenye mabega na magotini, hapo wakanipandisha hasira.

Kila dakika ikipita mtu wao mmoja anadondoka chini, hajitambui….niliwabana sana, lakini unajua tena uzee, na wao walikuwa wengi, na sehemu ya tuliyokuwemo ilikuwa ni ndogo, usingeliweza kusogea huku na kule ili kumkwepa adui,…na walipobakia wawili, wakiwa hoi wakipambana na mimi, wengine wao walikuwa wamelala chini, wengine wakiwa wamepoteza fahamu,….

‘Na ukumbuke hapo, nilikuwa simkati mtu kwa panga, nilichokuwa nikifanya nikuwaginga na sehemu ile isiyo na makali…na wale waliozidiwa walikuwa hawana hamu na mimi, ila hawa wawili walikuwa bado wakaidi….nikawa napambana nao, na wakati huo nilishapandisha zile hasira za kizamani, kwa bahati mbaya mmojawapo aliyekuwa kadondoka chini, na nikijua kuwa kapoteza fahamu, alisimama, bila mimi kumuona…

Nilichosikia ni kitu kama chuma kikigonga kichwani kwangu, na begani nikasikia kisu kikizama upande wa  kulia karibu nakwapa, hapo nikajua wameniweza, maana maumivu yalikuwa makali…. Nikaanza kuona vinyota,  na kudondoka chini, huku wakinishambulia kila mtu kwa silaha yake, na sikuweza kujua nini kilitokea baadaye maana giza lilitanda usoni, nikapoteza fahamu….

NB: Haya niambieni nyie, mkikaa kimiya sawa, hakuna shida..

WAZO LA LEO: Unapotaka kujua haki za watu, na kutetea haki za watu au pande mbili tofauti, ni vyema ukasimama kati kati, na kusahau lolote la sehemu hizo mbili zinazohasimiana, na hapo unahitajika kuwasikiliza wote kwa usawa bila kuingilia kati, na ujaribu sana kutokusimamia upande wowote, hata kama wewe upande mmoja unakugusa zaidi.  


Kama una jukumu hilo la kusimamia haki, na ukatekwa na imani za kutetea upande mmoja, ujue wewe ni mkosaji mkubwa sana, na kama kutatokea uvunjifu wa amani, ujue wewe ndio chanzo, na utawajibika, sio hapa duniani tu,na kesho kwa mwenyezimungu utaulizwa hilo.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Yasinta Ngonyani said...

Duh! nimesisimka na nimependa jinsi alivyokuwa akiwapiga kwa panga ...natumai atakuwa hajaumia hapo alivyopigwa na chuma ...nasubiri kwa hamu. Vile vile nimependa wazo la leo ningefurahi kama wengi wangesoma hapa. Ahsante pamoja daima.