Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, May 28, 2013

WEMA HAUOZI-13


Kipindi cha msiba wa baba yako, nilikuwa nina wakati mgumu sana, na siku zote nilizokuwa hapo kwenye msiba kwa shemeji , yaani kaka wa mume wangu sikuwa najitambua. Nilikuwa hapo kimwili, lakini akili, ilikuwa siyo yangu, nilikuwa kama nimepooza mwili mzima, akili ilikuwa kama imeganda, siwezi kufikiri zaidi, na kwa hali kama hii mwili ulikuwa hauna mawasiliano na ubongo, hata kutembea ikawa shida, …ilibidi kuwa na mtu wa kunishikilia kila nilipotaka kwenda haja…nikawa mtu wa kulala, na skutamani kula kabisa.

‘Huyu sasa ni mgonjwa, ….tusipoangalia tutaita msiba mwingine sasa hivi….’akasema huyo wifi aliyekuwa akinisaidia . Huyu wifi yangu, alikuwa ndugu yao wa kike, na kidogo tulikuwa tukielewana, na mara kwa mara wakati kaka yake yupo hai, alikuwa na tabia ya kunitembelea, japokuwa baadaye nilianza kumuogopa, kwani alikuwa kama mpelelezi wao, anachukua mambo yetu na kuyapeleka kwenye familia yao.

 Kwa sababu ya mazoea, hayo nilikuwa karibu naye kuliko ndugu zake wengine, na hata kwenye huu msiba, yeye alikuwa karibu na mimi, na hata alijitolea kuja hapo nilipotengwa na kushinda na mimi, hakuruhusiwa kukaa sana, na hata hivyo kwa hali ya kawaida ilikuwa inachosha, palikuwa sio mahali pa kukaa muda mrefu.

Wifi yangu huyu ndiye aliyekuwa akiniletea chakula, maji, na hata kunisaidia kwenda haja na shughuli nyingine, na hakuata msaada, lakini siku zilivyozidi kwenda na yeye akajikuta anachoka, akaanza kulalamika kwa ndugu zake wengine, hasa kaka yao mkubwa ambaye alionekana kama kiongozi wa familia yao yote.

‘Huyo sio mgonjwa bwana , …..wakati mwingine ni kujidekeza, hata hivyo, hiyo tunaweza kusema ni hali ya akwaida ukipatwa na mshituko kama huo, na inahitajia uwezo wako binafsi kujituma, na ili hilo liondoke, alihitajia kulia, akilia kwa haja, hali hiyo itatengamaa…..muacheni kama alivyo….muda utafika atabadilika, akizidi sana, sisi tutajua nini cha kufanya….’akasema huyo shemeji mkubwa.

Huyo shemeji mkubwa, sikumpenda hata kumwangalia, maana mimi na yeye damu zetu hazikuendana kabisa, na kila niliposikia sauti yake, nilihisi mwili ukichemka kwa hasira, na wakati mwingine, nilimuhisi vibaya, kuwa huenda yeye alitaka mume wangu aje kwake, ili asipate huduma muhimu afe haraka. Sikumpenda kabisa….na hatuelewani hadi leo.

‘Sasa tufanyeje….maana hata mimi nimechoka, sitaweza kukaa naye siku zote, na hivi kaka arubaini imebakia siku ngapi?’ akauliza huyo wifi. Huyo wifi yangu alikuwa kipenzi chao, na alionekana kuwajulia na kuishi kutokana na mtu mwenyewe, na ndio maana nikawa makini naye sana, japokuwa nilizoeana naye.

‘Leo ni siku ya ishirini, zimebakia siku kumi, vumilia tu mdogo wangu,…baada ya hapo, utakuwa huru, na mjane ataamua mwenyewe kuwa anataka kwenda wapi, ama kwao, au atabakia pale kwenye nyumba ya marehemu, hadi hapo atakapopata mume mwingine, , kama atakubalia kukaa hapo na kukubalina na msharti ya familia hatuwezi kumfukuza …..’sauti ya shemeji mkubwa ikasema. Moyoni nikawa najiuliza hayo masharti ni yapi, maana kama niyakurithiwa mimi siwezi kukubali…

‘Lakini mimi nijuavyo, wifi ndiye aliyesimamia ujenzi wa hiyo nyumba mpaka inakamilika, kipindi kaka marehemu yupo jela…yeye alipotoka nyumba ilikuwa imeshakamilika na yeye kwa vile ni fundi, akawa anafanya marekebisho ya hapa na pale, lakini aliyeijenga ni wifi.’sautii ya wifi ikasema na kunifanya nitege sikio vizuri.

‘Wewe, acha kidomo domo chako, hayo hayakuhusu, na nikusikie tena ukiongea hayo maneno, …..hata kama alisimamia ujenzi, pesa zilitoka kwa nani na huo ulikuwa ni wajibu wake, maana mwenzake alijitolea hadi kupelekwa jela, sasa yeye angekaa tu….yoyote yule angelifanya hilo alilolifanya, vinginevyo angelikuwa ni mnyonyajii tu…wewe kwa akili yakol pesa hizo za ujenzi zilitoka wapi?’ akauliza shemeji.

‘Wanasema ndio hizo pesa alizoiba kaka…..’akasema wifi.

‘Aliiba…! wewe ulikuwepo akiziiba, nyie hayo maneno ya kujiropokea yatawapeleka pabaya…unajuaje kuwa aliziiba, na kama aliziiba, kwanini wahusika baadaye wakaamua kumsamehe….walifanya hivyo baadaya kuona hawana ushahidi, walioiba walikuja kugundulika baadaye….huyu ndugu yetu walimpachika tu, na kwa vile alikuwa na tamaa, akajiingiza kichwa kichwa, lakini ….tuyaache hayo, ila nakukanya, tena usikie hili ninalokuambia, achana na tabia ya kuropka ovyo, itakuponza…’akasema huyo kama mkubwa.

‘Kaka naye bwana, yamekuwa hayo,..hapa sisi tunaongea tu, siwezi kuyaongea hayo kwa watu wengine, mimi niliongea tu, kama nilivyosikia, au hutaki tena niwe ninakuambia wanayosema watu…kama ni hivyo siongei tena hayo mambo….’akasema huyo wifi.

‘Ukiongea tena,…maneno kama haya, yakasikika kwa wabaya wetu,… ina maana hata hayo aliyokuachia ndugu yako hutayapata tena, sasa hivi lile duka ni lako,…utaliendeleza, tutakuongezea mtaji, na hutakuwa na shida tena, unakumbuka jinsi kaka yalko alivyokuwa akikupenda, ndio maana kakuachia duka, ….hebu fikiria upendwe vipi….tulizana, tusikilize sisi kaka zako, utaishi maisha ya rana na utapata mume ambaye hutapata shida….tutahakikisha kuwa mume atakaye kuoa anakufaa, ndio maana sijawakubalai wale wote waliotaka kukuoa, nawafahamu sana, wewe tulia, nisikilize mimi…’akasema kaka mtu.

‘Nashukuru sana kaka kwa kunijali, na kwakweli nina machungu sana, kwa kuondoka kaka yangu….ina maana sitaweza kumuona tena,…..na ule ulevi wake,….unajua kaka, kaka yetu yule, hata alewe vipi, akiniona mimi, atatulia,…na atanipa kila ninachokitaka, ndio maana hakusita kuniachia hilo duka kama urithi,…huko alipo najua atakuwa peponi kwa wema wake huo…’akasema wifi.

Kauli hiyo iliniweka njia panda, ina maana kweli mume wangu aliandikisha vitu vyangu, ….japokuwa vilikuwa vyetu, lakini nyumba duka, nilijenga kwa pesa yangu, ….alitakiwa kushirikiana na mimi kabala hajafikia hayo maamuzi, haiwezekani, hapo kuna kitu kimejificha, lakini nitajuaje hayo, na kwanini wanajiamini hivyo…..

Hayo yote nilikuwa nayasikia kama ndoto, japokuwa nilikuwa macho, na kuna wakati usingizi ulikuwa ukinijia na nikisikia sauti yao wakiongea, usingizi unakuwa wa mang’amung’amu, nawasikia kama vile wanaongelea kwenye sikio langu,…na baadaye nikipitiwa na usingizi wa kweli, na nilipokuwa kwenye usingizi wa kweli nikawa naota, kwanza ilianza kama watu wanaongea, na baadaye ikasikika sauti ya mtu ninayemjua, niliposikia sautu hiyo, nikashituka, na nilitaka kama kukimbia, lakini nipo usingizini, sauti hiyo ilinifanya nishituke, nahisi ni kwa vile ubongo ulishakubali hali halisi kuwa mume wangu keshafariki, kwahiyo ukisikia sauti yake, ni lazima ushituke, ilikuwa ikisema kwa sauti ya mwangwi:

‘Nilikuambia mke wangu….kwa hali kama ilivyokuwa, nisingeliweza kupona…nikakuambia mke wangu unahitajika tubadili hiyo hati haraka, kabla hali haijakuwa mbaya, sasa umechelewa,

‘Mke wangu nilijua kabisa kuwa nimetenda vibaya, kuandikisha mali yote kwa jina langu, najua ulikubali kwa vile ulikuwa uannipenda,  ..je huoni kuwa nitateseka kwa kosa hilo,…kwani sasa nimeshakufa na watu wakiona hizo hati zikiwa na jina langu, hawatakuamini tena, watakusumbua, hasa ndugu zangu, nawafahamu sana …nawafahamu sana ndugu zangu kwa ubinfsi wao,

'Mke wangu….nilikuambia kuwa ufanye hima-hima, kubadili hizo hati nikiwa badi hai, sasa umechelewa mke wangu, Napata taabu kwasababu hiyo mke wangu.….sauti ikasikia kichwani mwangu na muda huo kichwa kilikuwa kikiuma sana japo nipo usingizini.

Nikashika kichwa nikiwa ndani ya usungizi, na kutamani kupiga ukulele, na nilitamani niwaambie hawo watu wengine wanaoongea wanyamaze, kwani sauto zilikuwa zikiingiliana, na nilishindwa nimsikilize nani, kulikuwa na sauti za watu wengine, na hapo hapo kuna sauti hiyo inayokuja kama mwangwi , ambayo ni sauti ya mume wangu…ile sauti ya mwangwi ikawa inaendelea kuongea;

Mke wangu,….nilikuambia ukumbuke kubadili hati ya nyumba, mke wangu nilikusisitizia kuwa ufuatilia kubadilisha hati za mali zetu ikiwemo nyumba na duka, ilikuwa ni muhimu sana….sasa mke wangu umechelewa, mke wangu umechelewa…., nilikuambia ukumbuke kubadili hizo ili usipate taabu…sasa umechelewa, sasa umechelewa…,…mke wangu kwanini sasa unaona, kwanini sasa…..umechelewa, sas mke wangu umechelewa…..’ Haya maneno yakawa yanajirudia rudia kichwani kwangu, mpaka yakawa kama yanapandana pandana.

 Hata sikuelewa ni kitu gani, kichwa kikawa kinaniuma, na nikahisi mwili ukiwa sio wangu tena….na hapo nikapiga ukulele wa nguvu. Nikainuka na kusimama, sikujua nipo wapi, sikujijua tena mimi ni nani,kwani kilichotokea hapo, ilikuwa ni vurugu, na sikuelewa ni nini kiliendelea baadaye…

Nilizindukana siku ya pili yake asubuhi na mapema, nikajikuta nipo peke yangu, nimefungwa kamba miguuni na mikononi, nikajaribu kujifungua lakini sikuweza kabisa, walikuwa wamenifunga kama kuni, nimenyooka moja kwa moja, na kwa muda huo mdomo, koo vilikuwa vimekaua kabisa,  nilikuwa na kiu, na sikuona mtu wa kunisaidia, nikaanza kujitikisa tikisa ili kama kuna mtu karibu aje kunisadia, lakini walivyonifunga ilikuwa vigumu sana, nikawa najiviringisha hapo chini,

Nilikaa katika hali hiyo , nikiteseka kwa maumivi mwilini, kuchoka, kiu, maumivu ya zile kamba ambazo zilionyesha kabisa kukaza na hata sehemu zile zilizopita kamba zilionyesha kuvimba, na niliona ajabu kuhisi hata njaa, maaan muda nilikuwa sili chakula, wakiniletea chakula naonja tu nakusema sijisiki kula, na waoo hawakuwa na ushawishi wa kunifanya nile….nilikaa katika hali ile kwa muda mrefu hadi watu walipoanza kuamuka na bahati mtu mmoja akaja kuchungulia pale nilipolala, alichungulia kwa wasiwasi, akiogopa;

‘Sijui kama huyu mtu kazindukana, maana mimi naogopa hata kuingia, na muda mrefu hajala, anaweza akafa kwa njaa….’ilikuwa sauti ya kike

‘Usije ukaingia humo ndani, akikurupuka hapo ndani anaweza akakata kamba zote, na kubadilika kuwa mbogo, na akifanikiwa kuchomoka humo ndani akakimbia, hamtapata tena, atakimbia hadi kwenye mto, au ziwa, au bahari azame moja kwa moja, naona kakumbwa na shetani, kwani hiyo sauti ni ya kiume, na huyo ni jini mwanaume anayeitwa jinni makata….’ikasema suti ya kike, sikujua ni ya mwanamke gani.

‘Hiyo sauti ya kiume inafanana na sauti ya mdogo wangu, huyo marehemu…’ikasema sauti ya mwanaume.

‘Ndio ilivyo, mara nyingi hawa mashetani wakiwaingi wanadamu wanakuja na sura, sauti na umbo tofauti na kwa yule mtu mnayemfahamu , hasa wale marehemu. Na huyo ni kaigiza sauti ya mume wake, kuleta ujumbe fulani.

‘Sasa atakaa hivi mpaka lini…?’ ilikuwa ile sauti ya kike ikiuliza.

‘Subirini kidogo, hiyo dawa ifanye kazi, …na cha muhimu, ni kutokumkubusha lolote litakalomuathiri kiakili…kwa sasa, , na kama mlivyomsikia kuna mambo aliagiziwa na mumewe, akiwa hai, na huenda huyo mjane hakuwahi kuyatimiza, ….kama kuna mambo aliagizwa na mumewe, inabidi ayatimize, la sivyo hali hio itakuwa ikimtokea mara kwa mara….’sauti ya kike ikasema.

‘Kuna lolote mnalolijua zaidi ambalo mkewe alitakiwa kulifanya na mumewe lakini hakuweza kulitekeleza, au hayo yalikuwa siri ya watu wawili,….naweza kulitafuta, lakini sioni haja kwasasa, kama mnalifahamu ni bora mkalifuatilia…nyie mnaweza mkalitekeleza kwa niaba yake’akasema huyo mwanamke mgeni

‘Hakuna , tujuavyo sisi hakuna, maana mimi nilikuwa na marehemu hadi anakata roho, hakuwahi kuniambia jambo zaidi ya kuwa tuitunze familia yake…., kwahiyo hayo aliyoropka, nahisi ni hisia zake kutaka mambo yawe hivyo anavyotaka yeye…na sisi kama wanafamilia hatuwezi kukubaliana nayo maana tulikuwa na marehemu hadi anakata roho, zaidi ni yale ya kawaida ambayo tutakwenda kuyatekeleza,na mengi ya hayo tulikwisha kubaliana na marehemu akiwa mzima, haiwezekani aje kuyasema baadaye….' akatulia na kuwa kama anawaza jambo fulani.

'Labda kama aliyasema kwa shinikizo, maana huyo mwanamke na watu anaoishi nao, sio wa kawaida, inawezekana walimfanay watakavyo ili afuate masharti yao, na hilo tuliliona, ando maana tukawahi kumchukua mdogo wetu mapema….’sauti ya kiume ikasema…nahisi alikuwa shemeji mkubwa.

‘Sasa nyie mnataka mimi nifanye nini, …maana huo ndio ukweli,…..na ukweli mwingine huenda anaujua mke wake vizuri kuliko hata nyie, …je tumsubiri, ili tuje tumuulize, au tumreejshe huyo makata aongee mwenyewe, ili atumabie ni kitu gani anahitajia,…..’akauliza sauti ya kike.

‘Hapana, hatuwezi kuvumilia hiyo hali tena, fanya vinginevyo unavyoona wewe , ilimradi huyo shetani aondoke…’sauti ya kike ikasema.

‘Lakini kama mnataka iwe tofauti, kunahitajika mambo mengi, makafara ya kuchinja, mlete, ngombe, kondoo na mbuzi wa rangi tofauti…..na ili kumtoa huyo shetani kichwani mwake, inabidi haya yakafanyikie baharini, na ….hili ni hatari, maana anaweza akatuzidi nguvu, akakimbilia baharini, na kupotea moja kwa moja….lakini tukifanya kama tulivyoagizwa, hiyo ni kazi ndogo sana, maana hiy ndio fani yangu…’akasema hiyo sauti ya kike.

‘Sisi tunaomba ufanye kila iwezekanavyo, hali hii iondoke,…na kama ikishindikana basi , ni bora tumpeleke kwao, japokuwa nasikia kwao hawaelewani….Huyu mwanamke ni mkorofi kweli, hebu fikiria tangu afike hapa toka huko alipokuwa kakimbilia, nasikia hana habari kabisa na familia yake, …mama yake anahangaika lakini yeye hamjali, baba yake ndio kabisa, nasikia hawaongei,…sasa hicho kiburi hatuwezi kukivumilia kwenye familia yetu, sisi tutakiondoa au vinginevyo aondoke….’sauti ya kiume ikasema.

Nilishangaa sana kusikia hivyo, kuwa mimi sielewani na familia yangu,  kwani mimi na familia yangu, yaani baba na mama yangu tulishamaliza mfarakano wetu, na nilikuwa mara kwa mara nakwenda kuwatembelea japokuwa baba alikuwa bado ana hasira na mimi, lakini sio kiasi cha kununiana, na mara moja moja alikuwa akinitembelea, na tulikuwa tukiongea vizuri tu.

Kitu ambacho nilikuwa na uhakika nacho ni kuwa Baba alikuwa hampendi mume wangu, kwani anadai kuwa ni jambazi, na jambazi hawezi kuishi na mtoto wake. Na kila anapofika akimkuta yupo, hakai, anasalimia juu kwa juu na kuondoka, ….Mara nikasikia huyu mwanamke akisema;

‘Sawa mimi nawasikiliza nyie, lakini je baba yake huyu binti, huyo baba mnayesema aiansihi naye, mumeongea naye , maana hapa kuna kazi tunahitajika tukaifanye ndani ya hiyo nyumba ya marehemu, ….na kuzunguka miradi yote ya marehemu ili  kuondoa yaliyofungwa humo, na kuyazindika ili yasiingiliwe na mtu mwingine tena?’ Akauliza.

‘Yule sio baba yake, yule mzee hana familia, yeye kwa upweke wake, maana mke wake aliuwawa kwa vile ni mchawi….yeye akona sehemu ya kujisitiri ni kwa mdogo wangu, sasa mdogo wangu hayupo, na sisi hatuwezi kumsitiri, maana hatuelewani naye, …kwa mtaji huo hana jinsi yeye atakwenda kuishi kwenye nyumba yake, ….japokuwa haijamalizika….’ikasema sauti ya kiume

‘Sasa kwanini hataki kuondoka…?’ sauti ya kike ikauliza

‘Sisi tunamshangaa, kwani aliyasema hayo mbele yangu, ….na kasema hawezi kutoka hapo kwenye hiyo nyumba ya marehemu, hadi hapo kitakapoeleweka, akisisitizia kuwa nyumba hiyo na mali zote ni za mjane,….huyu mtu ana akili kweli, toka lini mali ikawa ay mke, mbona hazungumzii watoto. Mke ataolewa, na mume mwingine kwenye ukoo mwingine tofauti, ina maana hiyo mali tapelekwa huko, na hawo watoto wa marehemu watabakia na nini….ndio maana tunahitajai kuilinda kwa ajili ya mtoto wa mrehemu, kwani kuna leo na kesho…mimi yule nimemwambia kuwa kwangu kwangu kafika…simuogopi hata siku moja, mzee mwenyewe kajichokea, …..anatafuta mada kesi’sauti ikasema, alikuwa ni shemeji mkubwa.

‘Huyo anahitaji kuwekwa sawa, ni kazi ndogo kwangu, nitamlegeza viungo vyake, na mwishowe atalainika, mtaweza kufanya lolote mnalolitaka, maana inavyoonekana ana ulinzi mkali,…lakini mimi nitausambaratisha,….hilo niachieni mimi, nitaona jinsi nitakavyofanya, kwahiyo yeye ndio yupo kwenye hiyo nyumba peke yake si ndio,?’ akauliza.

‘Yupo na hataki kutoka, na hataki mtu kuingia kule…nahisi yale waliyomfanyia mdogo wangu wamemfanyia na huyo mzee, ndio maana huyo mzee anakuwa upande wa huyo mjane sana, mpaka anasahau kabisa mambo ya kimila, mwenyewe alishawekwa sawa na mkewe, na isingelikwua watu kumuua, kijiji hiki kingeharibika kwa mambo yake…..hutaamini, yale yaliyotakiwa kufanyika baaada ya msiba, anayapinga, eti yamepitwa na wakati….huyu mzee balaa kweli, anataka kutuletea nuksi kwenya familia yetu…..watu kama hawa tukiwakumbatia watakiharibu kijiji chetu..’akasema.

‘Sasa vyovyote iwavyo, kuna mambo yanahitajika kufanyika ndani ya hiyo nyumba,….kuondoa hiyo mikosi, kuondoa hayo mazinduko yaliyowekwa,na kama kuna lolote lilifanyika, liondolewe,  ……na hayo ni lazima yafanyike, ndani ya hiyo nyumba, … sasa niambieni tutafanyaje kama bado huyo jamaa yupo humo ndani, na je yupo tayari kuturuhusu tufanye mambo yetu, hata kama akiwemo humo ndani?….na kama unavyosema kuwa anazuia watu wasiingie, huyo mtu huenda keshajua ni kitu gani kinakuja mbele yake…maana inavyoonekana ana mambo yake…mimi hapa namuona na watu wengine, hayupo peke yake kama mnavyodai…?’ akawa kama anauliza.

‘Sisi chakufanya, ….kwanza tumeshamuona mjumbe, na sijui kama mjumbe ataweza kumshawishi, maana hata mjumbe mwenyewe anamuogopa huyo jamaa, mimi sijui wanamuogopea nini yule mzee, unasikia mtalaamu, huyo mzee hana lolote, …kama alikuwa na miguvu, ni hizo enzi zake, kwa hivi sasa keshajichokea,….njaa na shida vime mmaliza kabisa,…. hawezi kabisa kupambana na vijana….lakini tunamuheshimu tu, …sasa la kufanya tutamuitia polisi,…ili tusionekane wakorofi, kuwa tumejichukulia sheria mkononi..’akasema na kuangalia nje.

‘Fanyeni hivyo haraka….’ikasema hiyo sauti ya kike, huku akipiga chafya mfulululizo.

‘Tutafanya hivyo mtaalamu kwa vile tuna sababu muhimu, kuwa anang’ang’ania mali ambayo sio yake,…..mimi mwenyewe nilishaongea na polisi, na tumewaonyesha nyaraka zote muhimu, na wao wametushauri kuwa, kiutaratibu kwanza ni muhimu tumwambie mjumbe, na kama mjumbe akishindwa kumtoa, sisi tutafika na kumshika kwa kosa la kuingilia vitu vya watu, na hilo kosa ni sawa na kuvamia mali za watu…polisi watafika tu, kwani yupo jamaa nafahamiana naye, nimeongea naye na yeye kasema hivyo hivyo kuwa huyo jamaa ni mkorofi tu, lakini cha muhimu  kwanza nikuongea na mjumbe. …’akasema.

‘Na mumeshafanya hivyo…yaani mumeshaongea na mjumbe?’ akauliza huyo mwanamama.

‘Mjumbe naye tumeshamuelezea na kumweka sawa,…hana shida, ila hakutaka tutumie nguvu, yeye mwenyewe kasema atakwenda kuongea naye na huyo mzee, na nimefika kwake kujua wameonega nini, lakini hayupo, mkewe kasema mjumbe aliondoka asubuhi hajarudi…’akasema.

‘Sawa fanyeni hivyo, muondoeni hapo kwenye hiyo nyumba kwa njia yoyote isiyoleta vurugu, maana serikali inaweza ikatuweka pabaya kuwa tumevunja sheria, na haya mambo yetu hayathaminiki kwenye serikali, japokuwa watu wake, viongozi wakubwa wanakuja kwangu kuomba niwafanyie mamb hay ohayo wnayosema hawayaamini….na ni vyema tufuate sheria, ili tuweze kufanya mambo yetu kwa haraka na kwa amani….’ikasema hiyo sauti ya mwanake ambayo ilikuwa ngeni kwangu.

Nilivyosikia hivyo, nikaona kumbe jambo jema nikujifanya kuwa sielewi kitu, hadi hapo arubaini itakapokwisha, na hapo nitajua jinsi gani ya kufanya,…kwani sikujua wana kitu gani cha kuwafanya wajiamini kupita kiasi, na je nyaraka hizo wamezipata wapi,….hapo nikakumbuak siku ile nlipofika na kukuta vitu vimevurugwa vurugwa, huenda walikuwa wakitafuta hati za nyumba na duka…sikukumbuka kuviangalai vitu hivyo….mungu wangu ina maana walivichukua,….mbona itakuwa kazi..

Na nilipofikiria hivyo, mara nikasikia sauti ya mume wangu kwenye ubing ikisema;

Mke wangu,….nilikuambia ukumbuke kubadili hati ya nyumba, mke wangu nilikusisitizia kuwa ufuatilia kubadilisha hati za mali zetu ikiwemo nyumba na duka, ilikuwa ni muhimu sana….sasa umechelewa….’

Sikubali, na sijachelewa, nitapigania kile kilicho change hadi hatua ya mwisho…’nikajikuta nikisema kwa suti ndigo, na akili yangu ikamkumbuka huyo baba yangu wa kufikia, kuwa wanaweza kumfanya lolote baya mzee wa watu, na nisingelikubali hilo litokee, kama nikuumizana tuumizane wenyewe, huyo mzee wa watu keshaumia tayari, wanataka nini tena kwake…

Mara nikasikia watu wakija upande wangu, nikafumba macho haraka na kujifanaya bado nimelala..

‘Huyu keshazindukana lakini bado hajawa tayari, , …nitampa hizi dawa, ili akizindukana vyema asiwe na nguvu tena, na wengine muanze hiyo mikakati ya kuhakikisha huyo jamaa anaondoka kwenye hiyo nyumba,…’akasema, na sauti yake ikakatishwa na sauti nyingene zilizotoka huko nje, ilikuwa ni sauti ya kilio kuashiria kuwa kuna mtu mgeni kafika, na anajitambulisha kuwa kaja kutoa pole. Huwa akija mgeni, huja na kilio, na baadaye anatulia , na kuanza kusalimia, kwahiyo huyo aliyefika inaonekana hakuwepo toka awali msiba ulipotokea ,ni mgeni….

‘Oh …tumekusubiri sana, …maana uliondoka mapema sana, hatutakulaumu maana kazi za watu zina umuhimu wake, lakini najua umeweza kulifuatilia lile swala letu , kwani hilo ni sehemu ya mambo ya msiba, na lina umuhimu wake, hebu nipe taarifa, umefikia wapi?’ akaulizwa.

‘Hayo na mambo mdogo bro, tumeshayamaliza, kwa vile kaka aliweka saini yake..kabla hajafariki, na alifanya hivyo akiwa na fahamu zake timamu, haikuwa na shida,…,maana kubadili umiliki wa nyumba au eneo achilia mbali usumbufu, lakini ni gharama kubwa sana, …asilimia kumi ya thamani ya nyumba unatakiwa kuwalipa watu wasiohusika kabisa….inachukuliwa, na hapo hujafanya lolote, hujauza hiyo nyumba au….kwahiyo kuna vipengele vyake vingi, lakini kwa vile sisi wenyewe tunajuana…..tulisaidiana. 

Kilachosaidia ni kuwa kila kitu kilikuwa kimejieleza kisheria, basi hakuna shaka,…tumeshalimaliza hilo iliyobakia ni utekelezaji tu’sauti ikasema.

‘Mambo si hayo, najua kwako kila kitu kitakwenda shwari, maana hatutaki kuonekana hatufuati sheria,…na sasa umefika, …au sio,..na kabla hujaondoka tena hakikisha kila kitu kimekuwa sawa kisheria….

‘Kama utaondoka karibuni,…uhakikishe umekutana na viongozi wa serikali na kuthibitisha haya yote kwao, ili wasije wakatuona sisi ni wababaishaji, na kuanzia sasa tunakukabidhi hilo swaia,la, ni lako….familia hiyo ni yako, mtoto huyo ni wako, kama mama yake hatapenda kukaa na wewe, basi yeye tutamruhusu aondoke, lakini mtoto haondoki, maana hiyo ni damu yetu, na huo ndio mshiko wetu kisheria na kimila ….’ikasema shemeji mkubwa.

‘Hilo halina shida, ….mimi nitaweza kuishi nao bila shaka, kwanza nina likizo ndefu kidogo, naweka mambo yangu sawa, kama mnavyoona nimekuja na….na mwenzangu, yeye ni mwanasheria pia…tulikuwa naye huko chuoni japokuwa nilimtangulia, na tukaona kuwa tunaweza tukaishi pamoja, mategemeo yetu ni kuishi kama mke na mume.’akatulia kidogo, akimgeukia mwenzake ambaye alikuwa katulia akiangalia chini.

‘Kwahiyo unasema huyu ni shemeji yangu…oh, hiyo kama umeitamka kama una mashaka vile, kama hutamuweza mimi ananifaa sana huyu..!’ akasema kaka mtu, ikawa kama utani, wakacheka, nay eye akaendelea kuongea kwa kusema;

‘Safi kabisa, maana famiia yenu itakuwa ya wanasheria, na tunawahitajai sana kwenye familia yetu kongwe, maana tukiwa na watu kama nyie, tuna uhakika hakitaharibika kitu, karibu sana shemeji…..japokuwa kama kaka mkubwa, hilo neno shemeji halijabarikiwa, nahitajia mjitambulishe rasmi,kwa wakati muafaka, sio siku kama ya leo, bado tupo kwenye maombolezo ….na kwa vile sasa hivi mumekuja kwa ajili ya kumalizia msiba, siwezi kumlaumu sana bwana mdogo , karibuni sana….!’ Akasema huyo kaka mkubwa

‘Ndio bro, sisi tumeshakaribia,…ndio yeye, ni mtarajiwa wangu, nataka tufunge ndoa haraka iwezekanavyo , ila huu msiba ndio umekwamisha hayo tuliyokuwa tumekubaliana,…nimakuja anye, ili na yeye afike kutoa rambi rambi zake, kama mlivyoona kuwa keshaitoa kwa taratibu zetu, kwanza kulia, pili sasa anhitajika kumuona mjane, na ndugu wengine….sijamleta rasmi, naomba hilo mlifahamu, msije mkanipiga faini ya kutokufuata utaratibu’akasema.

‘Sawa hayo ni ya baadaye, tutayamaliza muda ukifika, sasa hivi ndio tupo kwenye kumalizia maombolezo, na mimi kwa hivi sasa jukumu kubwa lililopo mbele yangu lilikuwa hilo, la kuhakikisha kuwa kila kitu cha marehemu tumekiweka katika, maana haya mambo yakitokea, wajanja wanakuwa wengi,..’akakohoa kidogo, halafu akasema;

‘Dunia sasa imebadilika, wanawake wa sasa sio wale wa zamani, enzi hizo ikitokea msiba kama huu, wanawake wenyewe wanajua taratibu zao, hatupati shida, lakini siku hizi mume akifa, famiia ya kikeni, kwa marehemu, wanakuja kuvamia….sasa hili inabidi sisi tunaojali mila na taraibu tulifungie kibwebwe…’ akatulia na kukohoa tena, halafu akaendelea kusema

‘Eeeh,…bwana mdogo, na shemeji, cha muhimu na hayo majukumu yao bwana mdogo, aliyokuachia ndugu yako, hakikisha unayatimiza ipasavyo, na usione haya, maana ndugu yako alikuamini sana,…mimi kama kaka mkubwa nitakuwa kama mshauri tu…nasimamia pale nitakapoona unakwama,…au sio japokuwa sijasoma, lakini huniwezi kwa mambo ya kimila na uongozi, hapa ni jembe, wazazi wenyewe walinivulai kofia….’kaka mkubwa  akasema.

‘Kwani huyo shemeji yupo wapi?’ akauliza huyo mgeni, na hapo nikajua muda wowote wanaweza kuingia, na nafsi yangu ilitamani sana kumuona huyo mdogo wa hawa ndugu zangu, maana kila mara ,mume wangu alikuwa akimtaja sana, kuwa ni msomi,mstaarabu, mpole na sifa nyingi ….sikuwahi kuonana naye kabla ana kwa ana….

‘Shameji yako yupo kwenye sehemu yake ya maombolezo, unahitaji kumuona sasa hivi?’ akaulizwa.

‘Ndio ni muhimu sana, maana kama nimekabidhiwa hiyo familia, ni lazima nijue afya yake,….. na mtoto yupo wapi?’ akauliza.

‘Yupo na wenzake wanacheza, mtoto hana shida kabisa…kwa umri wake, hawezi kujua ni kitu gani kimetokea, na hatutaki ajisikia hivyo….basi karibu huko alipowekwa shemeji yako’wakasema na mara wakaingia pale nilipolazwa.

‘Mbona mumemfunga hivi?’ akauliza huyu mgeni. Alikuwa mvulana mtanashaji, na hakuonekana mdogo au mkubwa sana, tofauti na jinsi walivyokuwa wakimsimulia, na alivalia kiofisini, kwani hawa watu wa sheria wanapenda sana kuvai tai, ….akaniagalia kwa muda mrefu, na mimi nilikuwa nimefungua macho kidogo, na baadaye nikayafunga, sikuyafungua kabisa, lakini nilihisi bado ananitizama.

‘Alipandisha mashetani, akawa anaongea sauti ya mume wake, ilikuwa kivumbi hapa, ndio tukamuita mtaalamu akayaweka sawa, …lakini kasema kwa hivi sasa tunaweza kumfungua’sauti ikasema na mara nikasikia mtu akinifungua hizi kamba, nikatulia hadi wakamaliza kunifungua, na nilishi mikono milaini ikiniinua na kunikalisha. Sijui kwanini maana hiyo mikono ilipokutana na mwili wangu nilihisi mwili mzima ukinisisimuka, nikafungua macho.

‘Oh, pole sana shemeji,…naomba ujitahidi kuyahimili haya , ni mipango ya mweneyzimungu, …..na wote ni watarajiwa, ujaribu kuyasahau japo hayasahauliki, ….usijiweke katika hali ambayo utakuja kuumia, ukumbuke kuwa yupo mtoto anakuhitajia sana, ….na sote tuna machungu kama wewe….na…’akawa anaongea huku akiwa bado kaweka mikono yake shingoni, kunisaidia nikae vyema.

Sikusema kitu, nilimwangalia mara moja, nikakwepesha amcho yangu na kuwa nimeangalia chini, lakini kila mara nijaribu kugeuza macho yangu na kuangalia naye…alikuwa mdogo kwangu, kwahiyo nilimuona kama mdogo wangu, ila kuna hali ailiniingia ambayo sikuweza kuitambua kwa wakati ule.

Nikajitahidi ni kukaa vyema, na baadaye akaingia wifi yangu ambaye nilimzoe, nilipomuona nikamuonyesha ishara kuwa nina kiu, na wifi yangu akaelewa, maana kuishi naye hapo, nimekuwa nikiongea naye kama mtu mwenye udhaifu wa kuongea, …wifi akaligundua hilo akatoka kwenda kuniletea maji, niliyanywa kama ng’ombe mwenye kiu ya muda mrefu…

Niliyanywa yale maji yote na, nikaomba niongezwe mengine, na baadaye nikapatiwa chakula kidogo, nilikula kwa kujilazimisha, ili nisije nikazimia kwa njaa, kwani nilikuwa sijisikii kula kabisa na baadaye usingizi ukanijia, lakini kabla ya kupitiwa na usingizi ulionijia kwa kasi, nilisikia shemeji mkubwa akisema;

‘Tumefanikiwa kumtoa huyo jamaa kwenye nyumba, lakini baada ya kupambana na kikosi chetu kwa muda mrefu, ameumia vibaya sana,…anaweza hata asiishi, lakini polisi wamemshikilia kama mleta vurugu…’

‘Oh, kwanini mumemuumiza,  ina maana imefikia hatua hiyo yakuumizana, ….lakini nyie mliniambia kuwa huyo sio baba yao, sasa kwanini aingilie mambo yasiyomuhusu, ….’ Akamgeukia huyo mchumba wake akionyesha kutahayari, kama vile hayo yanayoongelewa hapo yanamzalilisha kama mwanasheria, na alipomuona mchumba wake akiwa na uso wa huzuni, akiwa habandui macho yake kuniangalia mimi, akasema;

‘Mimi nahisi huyo atakuwa na sababu kubwa, ambayo mimi siijui,… lakini kama hana sababu ni ubishi tu, na kama anahitajia kupambana na mimi tutapambana naye….’akasema huku anatikisa kichwa na alipogeuka kumwangalia mchumba wake, alishangaa kumuona akitoa machozi na baadaye yule mchumba wake akasema;

‘I cant believe this…’ akiwa na maana haamini hayo anayoyaona na kuyasikia.
Na mimi mwili ukawa hauna nguvu tena, usingizi, au kupotewa na fahamu kukanijia na kuzama kwenye giza…

*******

NB: Ni kazi kweli kweli kufanya mambo haya kwenye mazingiraj magumu ninayokabiliana nayo, lakini nitajitahidi hadi nifikishe ujumbe wa kisa hiki kama tukio lilivyotokea.


WAZO LA LEO: Ukiona haki inapindishwa, ukiona haki inavunjwa itetee, ama kwa mikono yako,au kwa kukemea, au kama umeshindwa, basi ikatae moyoni.  Usisubiri hadi hayo wanayotendewa wenzako yafike kwako ndio uanze kupiga ukulele, maana leo kwa mwenzako kesho ni kwako. Ulewe kuwa wavunja haki hawachagui mlango wa kuingia. 
Ni mimi: emu-three

No comments :