Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, May 25, 2013

WEMA HAUOZI-12


‘Niambe ukweli, kuna nini kimetokea ….? Nikauliza. Babu yako akanisogelea na kunishika , na machoni hakuweza kuvumilia, machozi yakaanza kumtoka.Nikajua ni msiba, je ni wa mume wangu au kuna ndugu yangu mwingine. Lakini mume wangu hali yake ilishaanza kuwa nzuri, niliongea naye usiku akionyesha kupona…haiwezkeni, sio yeye….’nikawa najipa matumaini.

Mara yule mwanaume aliyeingia na babu, bila kuvuta, au kusubiri, akasema;

‘Mume wako hayupo duniani….’akasema huyo mtu, ambaye ni kaka mkubwa wa mume wangu. Nilimwangalia kama vile sijasikia vyema, nikatoa jicho, kumwangalia kama vile simuoni vyema, nikapanua masikio, nisikie vyema, lakini hakurudia, alikuwa akiniangalia, bila kupepesa macho.

Nikajau hicho nilichosikia ni kweli, mume wangu hayupo duniani, hapo akili ikaanza kuliingiza hilo tukio, na mwili ukaanza kulegezwa, hapo sikuweza tena kuvumilia, nilimfuata yule shemeji, nikaanza kumparura kwa makucha, huku nikisema

‘Nyie ndio mumemua mume wangu….mumemchukua hapa akiwa keshaanza kupona na kwenda kummalizia,huko kwenu kwanini mlimchukua, wakati alisema kama ni kufa anataka afie kwenye nyumba yake ….’ Lakini jinsi muda ulivyokwenda, nilijikuta nguvu zinaisha hata kuinua mkono ikawa shida, na hapo hapo nilishuka chini kwanza taratib, halafu mwili ukadondoka kwa kishindo sakafuni.

Wakati nadondoka,, yule shemeji aliona hiyo dalili ya mimi kuishiwa na nguvu na kuwa asiponishika nitadondoka, lakini...., hakutaka hata kunishika, na kwa mbali nilimuona babu yako akivua hatua kuja kunidaka, lakini alikuwa kachelewa,….nikadondoka sakafuni na kupoteza fahamu…..’ Mama akamalizia sehemu hiyo.

Na hapo nikakumbuka babu alivyoendelezea sehemu hii kwani yaliyotokea baadaye mama hakuwa na taarifa nayo.hata alipozindukana, hakuweza kuongea hadi siku kumi zilipopita, alikuwa kama bubu…

********

Mjukuu wangu, kufiwa kusikie kwa wenzako, lakini ikitokea kwako ndipo utajua uchungu wake, …ukisikia kwa wenzako utakwenda na kusema;`yote ni mapenzi ya mungu..’ utaondoka, lakini sasa ni wewe umefiwa, ...halafu aliyefariki ni yule ulikuwa naye karibu,....manakula naye, mnashinda naye, mnalala naye....patamu hapo....na machungu yanazidishwa zaidi kutoka kwa watu wanakuja kwako,...'babu akatulia kidogo.

'Unajua kila mtu ana silika zake,  na kila mmoja anakuja kwa hisia zake, na wengine hawana elimu ya kumliwaza mtu, na wengine hawajui kutoa pole isiyorejesha hisia nyuma kwa mfiwa ambayo itaweza kumuongezea machungu...' babu akaendelea kuongea.

Basi ilikuwa kazi kubwa sana, na nilimuonea huruma sana mama yako, maana mila zetu zinatambulikana, mke akifiwa anakuwa kama mtu asiye na thamani tena, anaanza kuteswa, ....mimi nakuita kuteswa, kwani yanayofanyika sio mambo ya kungwana, jinsi anavyotengwa, sehemu anayolala, na jinsi gani anatendewa, anakuwa kama yeye ni mkosi fulani, uliosababisha hicho kifo, na hayo anayotendewa ni kama adhabu fulani, nilijua kuwa akizindukana, alihitajika kuwa na mtu wa karibu anayemjali,…lakini haikuwezekana, maana alishachukuliwa na huko atakuwa ugenini, nyumbani kwa shemeji yake.

Katika familia hiyo, shemeji huyo ambaye ndiye kaka mkubwa, walikuwa hawaivani kabisa na mama yako na mdogo wake, na siku zote, alikuwa akisema kuwa mdogo wake, anaumwa kwasababu ya huyo mkewe. Na anateseka kwa vile hataki kuwa karibu na familia yao, kajietenga, hasikii..., alifikia hadi kusema mama yako ndiye kamuambukiza baba yako huo ugonjwa, au vitu kama hivyo.

Walifikia hadi …..kusema kuna mkono wa mtu....., lakini maneno yake yalielekea hivyo, kuwa mama yako kuna dawa kamuwekea mumewe, …au tuseme kamloga, lakini alikuwa akikwepa kauli hiyo,ya kusema kalogwa na alisema;

Hawa wanawake hamuwajui, huenda alitafuta dawa, akiwa na lengo, a kumweka sawa mumewe, na bila kujua madhara yake, akamuumiza mumewe, hamuoni, kwanini haponi, mbona wengine wanaumwa ugonjwa huo mbona wanapona….’akawa anasema.

‘Mimi nikiweza kumtoa mdogo wangu kwenye makucha ya huyo mwanamke, nitahakikisha mdogo wangu hamrejei tena huyo mwanamke…hafai kabisa kwenye ukoo wetu…’akawa anasema kwa watu.

 Kwakweli kama ningelielewa hilo, kama ningelikuwa na mtu wa kunisaidia, ningelimchukua mama yako na kuhakikisha kila anayekuja kumpa pole nampa somo kwanza ni kwa jinsi gani atakavyongea, lakini haikuwa rahisi hivyo.

‘Kwanza kitu cha ajabu ni pale huyo kaka wa marehemu alipokuja kutoa taarifa, hakutumia busara, alikuwa kama anaongea na mtu baki, hakujua kuwa anaongea na mke wa marehemu, mke ambaye ni ubavu wa  mwenzake, ina maana ubavu ulioondoka ni ubavu wa huyo mjane, sasa haupo tena, kwahiyo mwenzake hana nguvu za kujishikilia, anahitajia msaada, na msaada utatoka wapi, kama wanandugu ndio hawo, wanaotaka kumtelekeza.

‘Hili nililiona kwa vile lilinitokea na mimi, alipofariki mke wangu, nilikuwa kama nimekatwa upande mmoja wa mwili, nikawa sina nguvu kabisa, ….sasa fikiria mimi mwanaume, na tunajitapa kuwa wanaume kidogo tuna ustahimilivu,….hebu geukia upande wa mama yako uhisi hali aliyokuwa nayo.

Wakati nimesimama karibu na mama yako nilijua kuwa lolote linaweza kutokea , kwahiyo nilikuwa nipo tayari kumsaidia, lakini alivyochomoka na kumwendea shemeji yake, na kuanza kumpiga makofi, akisema kuwa wao ndio waliomuua, nilijikuta nimeshikwa na bumbuwazi.

Na alipoishiwa nguvu na kudndoka, nilikuwa ndio nimezindukana kiakili, na hata niliposogea pale walipokuwa wamesimama, nilikuwa nimechelewa, kwani mama yako aliodondoka chini, bila ya msaada wowote, shemeji yake alikuwa akimwangalia tu….Nilitamani nimzabe kibao, lakini nikajua kuwa haya yeye yupo kwenye machungu, maana yeye ni ndugu wa damu, ana machungu yake kumpoteza ndugu yake.

‘Hivi wewe unashindwa hata kumshika, huoni alivyodondoka angeliweza kuumia namna hiyo….’nikasema.

‘Ningelifanya nini hapo, …nai aisiye na amchungu ya kufiwa, au kwa vile anajua kesho na keshokutwa atapata mume mwingine, sasa mimi nitampata wapi ndugu mwingine ……mimi nina machungu zaidi yake, lakini siwezi kufanya anavyofanya yeye….achana naye bwana…’akasema huku akiangalia huku na huku, akiikagua nyumba kwa macho.

‘Sasa taratibu zitakuwaje, maana hapa ni nyumbani kwa marehemu, na ingelikuwa bora maiti ikaletwa hapa nyumbani kwake?’ nikamuuliza.

‘Hayo ni mambo yetu, tumeshayajadili, nilikuwa tu niwape taarifa kuwa kuanzia sasa kila kitu cha marehemu kitakuwa kwenye mikono ya familia anayotoka, na mimi kama kaka mkubwa natakiwa kufuatilia na kuhakikisha mambo yote yanakwenda kutokana na taratibu za mila na desturi zetu…’akasema

‘Hilo halina shaka, na nijuavyo, taratibu za mila nyingi za hapa kwetu, hasa za misiba hazitofautiani sana, na mke ana nafasi yake, kwa mumewe, sio kwa vile mumewe kaondoka, ndio aachwe pembeni, na sehemu ya marehemu ni muhimu sana, na mwili wa marehemu unahitajika kuhifadhiwa hapo hadi dakika ya mwisho…’nikamwambia.

‘Hayo ni ya kwako, sisi kama familia, tunaheshimu sana utawala, ….katika familia yoyote, kama mkubwa ana heshima yake, na kila jambo linahitajika kufanyikia kwake,…hilo la kuwa mwili uwekwe kwenye nyumba yake, kwetu halipo, mambo yote yanafanyikiwa kwa kaka mkubwa, au sehemu ya familia alipotoka marehemu….’akasema huku akiendelea kuikagua ile nyumba.

‘Kama mama na baba wangelikuwepo, tungelienda kwao, kwani hata uwe mkubwa vipi, bado wao ni wazazi wetu, lakini hawapo, mimi kama kaka mkubwa ndiye nasimama badala yao…kwahiyo mambo yote  yatafanyikia kwangu, na taratibi zote zitafanyikiwa kwangu,…na huyu mjane, tunaondoka naye, ili akafuate taratibu zote zinazomstahiki. Na kila kitu cha marehemu,…..kinatakiwa kikabidhiwe kwangu, ili tujua hatima yake….taratibu zote zitafuatwa…’akasema huku akiendelea kuikagua hiyo nyumba kwa macho.

‘Sawa ….kwa vile tupo kwenye msiba, sihitajiki kulumbana sana, ila mnatakiwa muwe waangaliafu kwa hilo, msije mkaingiza maswala ya tamaa, kwenye mali za watu, hamjui wenyewe walichuma vipi, kwahiyo vyovyote itakavyo kuwa, mimi nasimama kama mzazi wao, na kwa vile nimaishi nao, na walinitambua kama mzazi wao, ….nayafahamu sana mambo yao…’nikasema.

‘Sikatai, …hilo silipingi mzee wangu, kila kitu kitafikiriwa, na wewe utashirikishwa kila hatua, kwa kutoa mawazo, tunakutambua sana, na tunashukuru sana kwa mchango wako mkubwa kwenye hii familia, lakini mambo ya familia yetu yanakuwa mbele, hatuwezi tukavuruga taratibu za familia kwa ajili ya kuwaridhisha watu wengine….tunakuomba ulijue hilo, na tunakuomba uheshimu taratibu zetu, maana hatujawahi kuja kuwaingilia kwenye taratibu zenu….au tuna uhasama na wewe…sizani, ni mambo ya kawaida, ambayo kuanzia sasa mimi kama kaka mtu nitahakikisha hayo yamekwisha…’akasema na kumwangalia mama yako ambaye bado alikuwa kalala sakafuni.

‘Huyu watakuja kumchukua wenzao, na ingelifaa wafike haraka wambebe, ili akizindukana ajikute kwenye sehemu yake…siunajua taratibi zilivyo,kuwa mke akifiwa anajengewa sehemu yake maalumu, …atakaa hapo hadi siku arubaini zitakapoisha, hataki kulala kwenye starehe, anatakiwa aonyeshe uchungu, analala kwenye mkeka, na katika hali ya taabu, tutasema hivyo, lakini ndivyo ilivyo, kwasaabbu mwenzake anakwenda wapi, …si kwenye udongo, sasa yeye anatakiwa aiihisi ile hali,….hayo yanajulikana au sio mzee?’ akawa kama ananiuliza.

‘Hayo mambo mengine ni ya kutesana tu, hayana msingi wowote, hayajaandikiwa hata kwenye vitabu vya dini,,…hilo tumekuwa tukilipiga vita sana, haiwezekani, mtu atengwe, ajengewe kibanda cha ovyo, alale kwenye udongo, …yaani mtu kafiwa, ana machungu na bado mnataka kumtesa, …..huko sikumuongezea uchungu…jaribuni kuwa waungwana….’nikasema kwa hasira.

‘Mzee, mbona unavunja mila na desturi, sisi hayo tumeyakuta, na wewe uliyakuta,…kwanini sisi tuwe wa kwanza kuyavunja,…kama unayavunja wewe, sio mimi…mimi nimelelewa kimila na nitazifuata mila zetu moja baadaya jingine, na hili ni amri, niisingelipenda uliingilie hili na mengine tutakayoyafanya, ..mjane bado yupo kwenye himaya yetu,hadi hapo itakapomalizika arubaini, na kutoka hapo ndio tutaangalia taratibu nyingine, natumai mzee hutatuingilia kwa hilo…’akasema huku akianza kutembea mle ndani.

‘Nakuona unaikagua hii nyumba ….kama vile ndio mara ya kwanza kuingia humu, vipi kulikoni, au ndio mtu akifa, basi kila mtu anamezea mate mali za watu…wacheni hiyo jamani, ..wakati wanahangaika mlikuwa hampo, sasa mmoja keshaondoka mnaanza kupiga mahesabu kichwani,….hii nyumba….’kabla hajasema wakina mama wakafika.

‘Haya mchukueni huyo mwenzenu, na kama inawezekana mbebeni akiwa hivyo hivyo, msihangaike kumzidua, atazindukana kwenye kibanda chake…’akasema huyo kama mtu, huku akipuuza yale niliyomwambia, maana sasa likuwa kiingia chumba baada ya chumba akikagua .

‘Lazima nitimize wajibu wangu kama kaka mkubwa, lazima nijue mali za marehemu ili wasije watu wakazifanyia ubadhirifu, na mzee, nitafurahi sana ukitoa mchango wako, wa kunisaidia kuzitambua mali zote, ambazo huenda hata mimi sizijui….’akasema huku akiwa kashika karatasi.

‘Nafikiri huu sio wakati wake…hapo nakuona, unakimbilia mali badala ya msiba, hiki ni kipindi cha msiba, ni kipindi cha mashituko, inahitajika watu tuomboleze, sio muda wa kupigiana mahesabu ya mali ya marehemu, …hata hivyo wenyewe walishajipanga, mke wa marehemu anajua kila kitu, na anajua ni nini afanye…nyumba hii ni ya kwake…’nikasema.

‘Ndio ni ya kwake…ni ya ndugu yangu hilo halina shaka,….mke yupo tu, kesho anaweza kwenda kuolewa shemu nyingine, lakini nyumba inabakia kuwa mali ya familia, na kwa vile wana mtoto mmoja, huyo atakuwa chini ya himaya yetu, …kama familia tutamlea, kama familia tutamiliki mali yote ya marehemu, na muda ukifika …mtoto akikua, tunamkabidhi mali yake…kwa hivi sasa mtoto wake ni mdogo sana, hajui lolote, hapo unasema nini…..mama yake hana mamlaka tena…ni kama ndugu zetu wa kike,….wapo, na siku yoyote wataolewa, na kwenda kwa waume zao….’akasema

Sikutaka kubisha naye sana, maana ulikuwa sio wakati wake, lakini niliahidi moyoni,kuwa mimi kama mzazi nitapigania mali za hawa wanangu hadi tone la mwisho…

‘Kwahiyo mzee, tunaomba ushirikiano wa kututajia mali zote za marehemu, ili nikawakilishe kwa wanafamilia, ili tujue taratibu nyingine zitakuwaje, ….na kuanzia sasa hivi, hii nyumba tutaifunga, na haitatumika hadi arubaini ikiisha, na wewe kwa vile umebahatika kuishi hapa, una sahemu yako, ya kutoa mawazo…ila kwa vile nyumba yako ipo karibu kuisha, ni bora uende ukakae hapo kwako, ili tuwe na nafasi ya kufanya mambo yetu kifamilia,,…’akasema akiniangalia kwa jicho la kujiiba, akihisi kuwa nitasema kitu.

‘Hayo tutakuja kuyaaongelea, kama nilivyosema nyumba hii inajulikana ni nani kaijenga,…..lakini naona hayo sio wakati wake muafaka, na sina cha kushirikiana na nyie, maana kila kitu kilishawekwa sawa, kati ya marehemu na mkewe, na mtu wa kumuuliza ni mkewe, na hilo huwezi kulifanya muda kama huu, tusbiri muda ukifika tutaliweka sawa…mimi ndio ushauri wangu…’nikasema.

‘Huwezi ukaacha mali zikae bila usalama, ni lazima kila kitu kiwekwe katika usalama, na kuwe na utaratibu, huku mambo mengine yakiendelea, hivi watu wakija na kuiba, au kudai hiki ni changu, mimi kama kaka mkubwa nitasemaje…ni lazima nianze kuchukua hatamu, pale mdogo wangu alipoishia, na hili halitakiwi kusubiri…vipi mzee, mbona unakuwa kama umezaliwa leo….’akasema na kauli hiyo ilinichefua, kwani alikuwa akitamka kwa kejeli huku akizungusha macho huku na kule kutizama kila kona ya nyumba.

‘Kijana, usione kuwa umekuwa….mimi nimekuona ukizaliwa, …leo hii unaota mapemba, halafu unaota mapembe kwenye jasho la watu,…hivi nyie watu mtabadilika lini, hangaikeni kutafuta vya jasho lenu, msisubiri wenzenu wahangaike, halafu wakifa mnakimbilia kumiliki, …mtalaanika….nawaambia ukweli, mali yote iliyopo hapa ni mali ya mke wa marehemu na mwanae, na mimi baba yako nitailinda kwa nguvu zangu zote….’nikasema na jamaa huyo akaniangalia kwa jicha la kushangaa.

‘Mzee, toka lini ukawa mzazi wa hawa watu, wewe tunajua kabisa huna mtoto, hukuwahi kuzaa, na kama ulizaa, bahati haikuwa yako, hayo ni mapenzi ya mungu…lakini kwanini udandie yale yasioyokuhusu, leo hii unaingilia watoto wa wenzako, na kujifanya wewe ni mzazi wao, mzee, jiheshimu, na sisi tutakuheshimu…sitaki kabisa kuvunjiana heshima na wewe, na kama huwezi kutusaidia kwa hilo, basi ondoka…acha mambo ya watu wenye familia na wanaojua taratibu za kifamilia…haya hayakuhudu, wewe ni wa kutoa mawazo tu, na ukitoa mawazo sio lazima yote yatakubaliwa….’akasema, na hapo nikashindwa kuvumilia.

‘Kijana naona hatutaelewana, na hili sio muda wake, wewe ondoka humu ndani…, ila nasema, kuanzia sasa kila kilichopo humu ni mali ya mke wa marehemu,…wakati hawa watu wanahngaika haaukuwepo, mimi nilikuwa nao, naijua familia toka jiwe linawekwa, toka ….huyu binti alipotelekezwa, nimemlea mwenyewe, hadi alipokutana na huyo mwenzake, kwahiyo huwezi kunidanganya lolote,….mimi waliniheshimu kama mzazi wao, na waliniomba niwalinda kama baba anavyowalinda watoto wake, na hilo nitahakikisha nalifanya, hadi hapo nitakapoingia kaburini.

‘Mzee ….mzeee….’akawa anaita mzee, mzee bila kusema neno, na mimi nikaendelea kuongea;

‘Niliahidi mbele yako, na sasa naahidi mbele yako, kuwa nitawalinda, na nitalinda mali yako usiku na mchana, hadi hapo muafaka utakapopatikana, na kama kuna mtu anataka shari , basi mimi nipo tayari kupambana na yeye….kama ni kwa shari ama ni kwa heri, basi hilo tutalijua wakati ukifika, kwasasa sio muda wake….’nikasema na kulichezesha panga langu hewani

‘Mhh, naona sasa mzee unatingisha kiberiti….ngoja nikalichukue jeshi langu, maana siku nyingi nimekuwa nikilitaka hilo hili litokee, nipambane na wewe,….wewe mzee, umekuwa ukiwaharibu sawa hawa watu, ndugu yangu alikuwa mbali kabisa na familia yao, kwasababu yako…mkewe akaota mapembe, haheshimu mila na desturi za familia yetu, hili ni kwasababu yako, tumejitahidi lakini tulikuja kugundua kuwa wewe ndio kikwazo…’ akaninyoshea kidole.

‘Sasa muda wa kuliweka hili sawa umefika, utapambana na mimi, mzee, utapambana na mimi…’ akawa napiga piga kifua, na mimi nikawa namuangalia tu, akasogea akionyesha kutaka kuondoka, na akaendelea kuongea kwa majigambo;

‘Lakini kwanza ngoja nikalifikishe hili kwenye familia, ili wasije wakaoa nimechukua sheria mikononi mwangu…mimi mzee sikuogopi wewe kabisa, nasikia kuwa una nguvu za ziada,…mimi siogopi, uchawi, siogopi ubabe wako,….kama una hizo nguvu za ziada, hebu nikuulize mkeo wako yupo wapi…’akasema huku keshafika mlangoni, akionyesha kujihami ….alimpomtaja mke wangu sikuweza kuvumilia, nikamfuata na panga likiwa juu…

NB: Haya yapo kwenye jamii zetu, tukio hili ni kielelezo kidogo tu ndani ya jamii, tusaidieni ili tuweze kufikisha ujumbe huu


WAZO LA LEO: Wanapohangaiaka wawili, yaani mke na mume, mnawaona, wakifanikiwa mnawaona, lakini anapokufa mmoja kati ya wanndoa hawa hasa mume, akamuacha mke, tunayasahau haya yote, na kwenda kuwadhulumu wanafamilia hao.Tumuogope mungu, haki yao tuwape, kamwe tusiwadhulumu mayatima, wajane maana haya ndiyo yanayochangia kuleta laana kwenye hii dunia.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Either employed by hackers, or by a suspicious spouse
or parent, a Keylogger for Mac at hand, you will be checking
with them.

Also visit my web site: keyloggers