Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, June 29, 2016

Mkweli hana deni-(Nimeikumbuka hii)  Tulikuwa tunakwenda Morogoro, ilikuwa asubuhi sana, kibaridi kilikuwa kikali na costa tuliyopanda ilikuwa na mwendo mkali ajabu….maana tulipoteza muda mwingi pale Ubungo kutokana na foeni za magari,…kwenye hilo basi pembeni yangu alikuwa kakaa jamaa mmoja, aliyevalia ile inayoitwa suti ya vipande vitatu, na mawani meusi machoni, nikajua nipo ni mtu wa watu,-kama sio muheshimiwa basi ni mkuu wa watu, kaamua leo, apande basi, na kuacha gari lake, huenda lipo kwa fundi,kwahiyo nahitajika kuwa makini. Siunajua tena unatakiwa uishi na mtu kutegemeana na alivyo.

Cha jabu Jamaa huyu alikuwa haongei,…moyoni nikajua huenda lugha inampa shida, hawa wenzetu waliosoma nje, wanapata shida sana kuongea Kiswahili, basi nikamkubali hivyo, na mimi nikakaa kimiya. Kila nilipopata nafasi nikawa namchungulia kwa kujiiba, na  mara nyingi alionekana kukunja uso pale watu wanapozungumza maswala ambayo hakupendezwa nayo….nikajua ahee, kumbe Kiswahili anakisia labda kuongea ndio kunampa shida…, na kama ni maswala anayopendezwa nayo, alikuwa akitikisa kichwa kuonyesha kukubali,na hata kutabasamu....nikajisema moyoni, ahaa, huyu jamaa anaonekana mwingi wa hekima na busara, hataki majungu....

Foleni ilikuwa kali, na hadi kutoka pale ubungo na kuingia Kimara ilichukua karibu saa nzima, kwahiyo tulipotoka hapo dereva akataka kufidia huo muda, akakanyaga mafuta kisawasawa. Tukifaka sehemu, nikamuona jamaa akihangaika, na kila mara alikuwa akijaribu kusimama, na akawa anamuangalia kondakita, mara anaangalia nje, na kusema; `ndio penyewe…’

Sikuelewa ana maana gani, na mara nyingine akawa anawaangalia abiria, na watu mle ndani walikuwa wakiongelea mambo yao na kucheka, hakuna aliyekuwa na habari na yeye sipokuwa mimi niliyekuwa nimekaa naye, kilikuwa kiti cha watu wawili, na kulikuwa na yale mapazia ya dirishani kwahiyo yaliweza kumfunika muheshimiwa,….huku mziki kwenye hilo gari ukisikika kwa sauti kubwa, mara huyu jamaa akaniuliza;

'Hivi leo hakuna sehemu ya kuchimba dawa….maana mara nyingi tunasimama eneo hili?' akaniuliza, na hapo nikajua kuwa kumbe ni mwenzetu hata kuchimba dawa anakufahamu, nikaingiwa na kujiamini,nikijue huyu ni mswahili mwenzetu hapo nikasema;

'Ulimsikia konda alivyosema, hakuna kulala, moja kwa moja hadi Moro, lkn kama umezidiwa mwambie konda...'nikamwambia, yeye akainama chini na kuchukua chupa ya maji aliyokuwa nayo tangu awali, akamalizia maji yaliyokuwemo.

'Oh, hapa nilipo, nikisimama tu nimeadhirika...na nina mwiko, nalinda miiko,....siunajua tena mambo ya miiko….'akasema, na hapo nikamuongezea sifa nyingine kuwa sio mwenzetu tu, bali ni mwafrika asilia, maana wengine wakisoma wanasema wao wamezaliwa Afrika kimakosa, lakini huyu alionekana kuwa mwafrika asilia...

'Una matatizo ya kibofu...?' nikamuuliza, nikiwa namtania, maana nilishjiamini kuwa kumbe hana shida, unaweza ukaongea naye hata kama ni utani

'Sio hivyo, na sijui .....oh, samahani sana, ....sijui kama utanielewa, lakini inabidi nifanye hivyo…'akasema na mara akachukua ile chupa ya maji aliyokuwa nayo, na kuhangaika kujifungua vifungo vya suruali, na huku akijificha…kwa kulivuta lile pazia, limfunike….na kwa vile kile kiti kilikuwa kirefu , watu wa nyuma hawakujua ni nini kinaendelea, na hata mimi nikajifanya simuangalii, na kujaribu kukaa vyema ili kumlinda asionekane na watu wa upande wa pili…, maana nilijua kuwa huenda jamaa alikuwa kazidiwa sana.

Mara akafanya alichofanya na kuendelea kujihudumia na, chupa ya nusu lita karibu ijae….na ashukuru kuwa sauti ya mziki kwenye hilo gari ilikuwa kubwa, kwahiyo hakuna aliyesikia ile…borooooo!

'Oh, afadhali...ningeadhirika,...samahani sana, haja ilinibana kweli, na haya...mambo ya miiko, la sivyo ningelimsimamisha konda,....aah, mambo haya bwana....nikifika kijijini nitayamaliza....maana huyo mtaalamu kaniambia nikitimiza kila jambo, udiwani ni wakwangu mwakani tena..hata nikitaka ubunge, nitaupata…ni kazi kweli…' alitamka hayo maneno na kunifanya nishituke.

'Kumbe ni muheshimiwa, ...'nikajisema moyoni.

'Unajua huwezi kuamini haya mambo, hata mimi nilikuwa hivyo, ...lakini sasa hatua kwa hatua nimeshatimiza karibu kila kitu…'akasema. Sikuweza kumsemesha maana ile hali niliyoiona usingeliweza kuongea, na hicho anachoongea na jinsi alivyo, haiviendani kabisa....nikawa najifanya kulala.
 
Mawazo yangu yalikuwa ni jinsi gani atavyoweza kutupa ile chupa iliyojaa  haja yake…na kama angelitupa nje, ningelimshambulia, kwa maneno, maana watoto wataokota hizo chupa na wengine wakiona kitu kama maji wanaishia kuchezea,…nikashukuru kuwa hakutupa, akawa kaweka mapajani kwake…
 
Tulipofika sehemu, nikamuona akiniangalia kwa kujificha,....mimi nikajifanya nimelala, mara akafungua ile chupa, aliyohifadhi  haja yake, ....na hutaamini, jamaa akaiweka mdomoni,....akamimina....ile haja yake yote tumboni,...huku akiwa kafumba macho kuonyesha kuwa hakupendezewa na hicho anachokifanya...mimi sikuweza kuvumilia, nikafungua macho ya mshangao nikamuuliza...

Mbona hivyo...huoni huo ni uchafu...'nikasema na mara akanifinya kuashiria kuwa ninyamaze, akasema;

'Oh, sasa nimeokoka, mambo safi kabisa.....nimepona, sina shida tena.....'akasema.

'Vipi mbona unaongea peke yako...?' nikamuuliza kujifanya sikuliona hilo alilolifanya.

'Hakuna shida.....nimemaliza shida yangu, na kila kitu kimeenda kama ilivyotakiwa nifanye,...sina wasiwasi tena, maana ningeliweka wapi huo mzigo, ni mwiko...sitakiwi kufika nao ukweni,... sitakiwi kutupa....sasa nimeuhifadhi mahali pake, na...nikifika kwa mtaalamu naumwaga ..'akasema akionyesha furaha Fulani usoni

'Unajua maana yake ....hiyo inaashiria kumwaga sera, .kazi imekwisha, hata nikitaka ubunge mwakani, ninataupata..bila shida..haya mambo ukiyajulia, hayakupi shida.......'akasema huku akiitupa ile chupa nje,....na kwa haraka akachukua leso yake, akajifuta mdomoni.....

 Sikuamini,...na wewe sijui kama utaamini, lakini ndivyo ilivyokuwa....

WAZO LA LEO:Uongozi sio hisia za kishirikina, uongozi ni wewe na wale unaowaongoza, ukawatendea kile walichokutuma, huwezi ukacheza na nguvu za giza huku umewasahahu waajiri wako, waliokupigia kura,...ukazania utafanikiwa, tusijidanganye kwa hilo, kwani ahadi ni deni,.....timiza ahadi yako, kama ulisema kweli, na kama umeshindwa kwa yale uliyoahidi, rudi kwa waliokutuma waambie ukweli, kwani mkweli siku zote hufanikiwa

Ni mimi: emu-three

No comments :