Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, April 29, 2013

WEMA HAUOZI-UTANGUZI



   ‘Dereve wado wado,…. juu kwa juu….hapa kuna mtiti, lakini mbayu wayu ni wengi, ….’ Hii ni sauti ya kondakta wa mabasi yatokayo Msasani hadi gongolamboto, ni kawaida yao ya kutokusimama kituoni, kwani abiria wao ni wengi, na hawana haja ya kupiga debe, …na kwa vile kuna wanafunzi, na hawawataki wanafunzi waingie kwenye mabasi yao, …..wanachofanya wao ni kuendesha basi huku abiria mmoja akidandia….ni hatari

Kwa hali kama hiyo ya `juu kwa juu…’ wanaoweza kudandika hayo mabasi wengi ni vijana, wazee na akina mama hupata shida sana,…na inawalazimu wapande hayo mabasi wakati yakipita kwenda Gongolamboto na kuwalazimu walipe nauli ya kwenda huko na kurudi nalo, nauli mara mbili, wakisema buku haina chenji, …huu mtindo wa kulipa nauli mara mbili wanauita `kegeuza nalo’…hiyo pesa haiendi kwa mwenye basi.

Hayo ndo maisha ya asubuhi na jioni ya wakazi wa eneo hili,..ili uwahi kibaruani, au kuwahi kwenda kuhangaika kutafuta riziki yako na huenda ili uipate inabidi kuelekea maeneo hayo ya mbali na, inakubidi uamuke asubuhi sana, muda wa alifajiri asubuhi , na unarudi saa tatu usiku,au zaidi…..kiasi kwamba kwako unapoishi, unajiona upo mgeni kila siku.

Haya ndio maisha yetu, hata hapo utakapoilipia haki yako bado kuna adha nyingine,…hii ni adha ya foleni, hutaamini, mtu anaweza akafika Morogoro kutoka Dar, lakini yule wa kutoka gongolamboto hadi Msasani hajafika….wenye mamlaka hili hawalioni, wanachoona ni gharama zao zirejeshwe, lakini zirejeshwe na nani,….mbona anyesababisha haya habebeswhi mzigo, anayebebeshwa huo mzigo ni abiria, mlaji, mwananchi wa kawaida….

**********
‘Juu kwa juu, ndio maisha yetu siku hizi, kila jambo, lazima liwe hivyo….juu kwa juu, hata biashara, au makubaliano ya biashara maofisini, bila `cha juu’ hutajafanikiwa, ‘juu kwa juu’….ukiona mabosi au watu wa kitengo cha mauzo, wakifukuzia jambo, unaweza ukazania kuwa hawa watu wanawajibika kweli kweli…. , kwa manufaa ya kampuni yao, lakini ukiuliza zaidi utagundua kuwa ndani ya hicho wanachokifukuzia kuna `cha juu chao’ ….

Hata siku hizi ukienda hospitali, ili mgonjwa wako atibiwe haraka, lazima uwe na cha juu kwa mfukuziaji, muwezeshe yule unayeona atafanikisha hilo jambo lako, ili faili lifike kwa dakitari haraka, na kama mgonjwa wako kalazwa, docta aweze kumtembelea mara kwa mara…ukitaka iwe hivyo, mkono wako usiwe mnzito,…..toa cha juu, hayo ndio maisha yanatotuzunguka, kama huna basi cha moto utakiona.

Hata ukienda kimtaifa, angalia kwanini mataifa makubwa yanavamia sehemu, yakijifanya yanatetea hicho kinachoitwa `haki za binadamu’ na hata kukimbilia kupiga vita nchi fulani, wakisingizia hili au lile, chunguza rasilimali za hiyo nchi, kama sio mafuta ni madini, yanayofukuziwa….ni nini hicho kama sio cha juu kwa ajili ya manufaa ya hawo wanaoitwa `bwana wakubwa’ Pia angalia hawo wakuu wan chi, wakiwa wanatembelea mataifa fulani,  mara kwa mara , sio bure, `kuna cha juu chao  huko…’

Kama unabisha angalia mataifa yenye uwezo wao, yanayomiliki hizo silaha za maangamizi, hawagusi, ni mazungumzo kwa kwenda mbele,…wanaogopa au kwa vile hakuna maslahi….tunarudi kule kule, ni kwa vile huenda hakuna `cha juu….’

********
Wakati nayawaza haya, nikamkumbuka babu yangu akituasa hasa pale anapotuona tunahamanika na jambo fulani, au akituona tunagombea kitu kidogo, au kubishania jambo fulani…ubishi kidogo unatupelekea hadi kutukanana, au hata kushikana mashati,…lakini ni nini yote haya, huenda kwa utoto wetu tulikuwa tukifanya hivyo tukiwa ni `watoto..’

Sisi wakati huo kwa utoto wetu, tulikuwa tukibishana bila kuelewa athari za mambo hayo, na wakati mwingine ni kwa ajili tu ya kukwepa kuwajibika, au kutafuta sababu ya kutegeana, kila mmoja akimtupia mwenzake lawama kuwa yeye ndiye anayestahili kufanya. Na hili sio la utotoni tu, angalia maisha yetu ya kila siku yalivyo, watu wataanzisha mjadala usio na tija, ambao utakwenda hadi kurushiana maneno mabaya…tujiulize ili iweje,….je baada ya ubishi huo kuna faida au hasara, au ni njia ya kupoteza muda tu.

Kwa wengine hayo kwao ni faida, ….lakini huenda wengine wanafanya hivyo, ili mwisho wa siku litokee ambalo huenda lilipangwa liwe hivyo,..swali kubwa hapa ni je hayo yote yanafanyika kwa maslahi ya nani….jibu unalo mwenyewe….turudi kwa babu

‘Wajukuu zangu, kama mngelijuwa thamani ya kujitolea katu msingalitegeana, msingelipoteza muda kwa kubishana jambo lisilo na manufaa, au kutukanana, ….hizi lugha zisizo na busara, hazitawasaidia, sana sana,  ni kuwapa manufaa majirani na wapiti njia…

‘Wajukuu zangu,  kama mngelijua athari ya kupupia, kugombea kile kidogo mlichojaliwa nacho, badala ya kugawana sawa, au kwa haki, …..au kutaka ziada au hicho kinachoitwa cha juu,…nawaambia ukweli mngelijua madhara yake, hata siku moja  msingelipenda kurudia hayo mnayoyafanya ambayo mwisho wake sio mwema, …hayo ya kula au kupata jambo bila kufikiria uhalali wake…ni hatari, sio kwa afya zenu tu, bali pia kwa amani na utulivu wenu….’akasema na sisi tukawa tumesimama tukiangaliana.

‘Wajukuu zangu hebu sogeeni hapa niwape mambo yajayo….’akasema babu.

************
Ikabidi ile fuko, kuzozana na kutupiana vijembe, ikaisha na sote tukamfuata babu, na wale wasiokubali kushindwa wakaanza kulalamika na kusema;

‘Babu naye bwana, badala ya kutupigia hadithi, unataka kutuambia mambo yajayo…mambo yajayo yanatuhusu nini, wakati sisi ni taifa la leo….’akalalamika kaka yetu.

‘Wewe unajua nini, ujinga tu umekujaa kichwani…..ubishi tu, twende kwanza tukamsikilize babu….’akasema ndugu yetu mwingine.

‘Unaona huyu ananitukana, ananiambia mimi ni mjinga,….’akalalamika kaka.

‘Kama anakuambia wewe ni mjinga, basi mwambie yeye mwerevu wa wajinga….’akasema babu na kutufanya tuangaliane tena huku tukimsogelea. Hasa sisi tunaomjua babu, kuwa akiwaitia jambo….kuna jambo….tena sio la hivi hivi, japokuwa kwa muda ule tuliona sio la muhimu sana, lakini sasa tunaona umuhimu wake…na kila akizungumza jambo mwisho wa siku atatoa kisa kizuri…ambacho baadaye nimegundua kuwa ni hazina kubwa ya maisha yetu.

‘Sikilizeni wajukuu zangu, maisha ya kuhamanika, na kutamani, hata kile kisichokuwa chako, ni hatari, ni sawa na kujaza gunia, vitu vingi kwa wakati mmoja bila kujali kuwa vingine vitaharibika au kuharibu vingine,…je unaweza ukachanganya magarage , unga, mahindi kwenye gunia moja….’akatulia kidogo kutafakari jambo.

‘Ngoja niwape siri ya kufanikiwa katika maisha, …’akasema na kutulia.

‘Kuna mambo muhimu katika maisha na ukiiyajulia hayo, hutahaangaika kamwe, na moyo wako utakuwa umejaa lulu ya utajiri, wa `kinaa’ moyo wa kurizka kutokana na kile ulichojaliwa nacho,…wewe utajiona tajiri, kuliko yule mwenye magari na majumba, na ukichunguza ndani yake hana raha kabisa….’akasema babu.

 ‘Haiwezekani babu, ina maana gani sasa kuitwa tajiri, uwe na mipesa, magari, nyumba na kila kitu cha kifahari, na bado usiwe na raha?’ akauliza ndugu yetu mmoja ambaye ni mdadisi sana.

‘Kwasababu utajiri wake, aliupata kwa kupupia, aliupata kwa kulimbikiza vya halali na visivyo vya halali, mali yake ina jasho la watu, ambalo lipo mikononi mwake, na jasho hilo kwa vile ni la watu linamuandama , na matokeo yake, ndio hayo,….moyo wake hautulii,….kwa kelele za waru wakidai haki yao japoukuwa hawapo hapo,….

‘Hawa watu wana shida kweli, kwa jinsi walivyojijengea maisha yake, hawawezi hata kukumbuka hilo, kuwa utajiri wake, una ziada za watu, na wangelikumbuka hilo, wakazitoa hizo ziada za watu, wasingepaat shida, kamwe…wangeliishi kwa raha mstarehe…..lakini wapi, maisha yao yamejaa pupa na kuhamanika na hicho cha ziada (juu kwa juu), …ndio maisha hayo, kama ya kukimbilia dala dala kama huwezi kudandia unaachwa na basi….’akasema babu na kutulia.

Tulicheka, kwa kipindi kile tulikuwa hatujui alikuwa na maana gani na ni nini msingi wa maneno yake hayo,…nimekuja kuyagundua hivi sasa katika maisha halisi….babu huyo akaendelea kusema;

‘Niwaambia siri moja ya maisha ….siri ya jinsi ya kufanikiwa katika maisha yenu ya baadaye,….?’ akatuuliza na sisi tukasema

‘Tuambie babu..ili tuwe matajiri, kama akina…..’ tukaangaliana tukitaka kuwataja matajiri tunaowafahamu. Babu akatabasamu na kutuangalia kila mmoja kwa zamu yake, na baadaye akasema

‘Mfano umepita njiani ukaona mwiba, upo kati kati ya barabara, utafanyaje?’ akatuuliza babu.

‘Nitauruka huo mwiba , na kuendelea na safari zangu….’akasema kaka yangu kwa kujiamini

‘Mimi babu, nitausogeza pembeni ili usinichome, nipite, ili niwahi nisije nikachelewa kama nimetumwa, kwasabbu ukichelewa utachapwa…’akasema mwingine na mwingine akatoa hoja yake na mwingine na mwingine, na babau alipotuona tumeishiwa na hoja akasema;

‘Unaona hapo kila mmoja anachojali ni yeye, ubinafsi wake …ili apite…., hajali mwenziwe anayekuja nyuma, hajali kuwa kuna wenye matatizo ya macho hawataona huo mwiba, hajali kuwa wapo watoto, hata watoto wake, au jamaa zake wanaweza kupita hapo na wakaukanyaga bila kuuona huo mwiba….

‘Ndivyo maisha yetu yalivyo, kila mtu anataka apate, afaidike zaidi,….hata maofisini, bosi anataak zaidi nna zaidi, anajilimbikizia marupurupu, akiona hayo ni haki yake, …..wewe au yule anachojali ni kufanya jambo kwa manufaa yake, kama mfano huo wa mwiba, kila mmoja anajojali na kuangalia jinsi gani afanye ili awahi afike huko anapotka kwenda….

‘Ndio dunia yetu ya sasa hakuna anayejali kuwa huenda yeye anahitaji kufanya jambo, ili na mwenzake apate, hebu fikiria kila mmoja angekuwa na mwamko huo, kuwa afanye jambo ili na mwenzake apate dunia ingekuwaje, lakini hata hivyo tukumbuke kuwa…..kuna watu wengine wanastahili kupata riziki zao kwa kupitia watu wengine…

‘Hilo hatuwezi kulijua kamwe, kwasabbau ya ubinfasi wetu na uchoyo wetu, hatutaki kuzitoa hizo  riziki , hatutaki kujitolea,... hebu niambieni wagonjwa, mayatima, na wasiojiweza riziki zao zinapatika wapi kama sio kwa kupitia kwa watu wengine….sio hao tu, hata wale wanaojiweza, wengine wanastahili kupata kwa kupitia wengine, huo ni mpango wa muumba, sisi hatuwezi kuujua…..

‘Tunatakiwa tujitolee, tusitegeane, ili tuweze kuwekeza kwenye riziki zetu, na tukifanya hivyo, tutapata , tutafaidiki, sote na mioyo yetu itakuwa na amani……’akaendelea babu….na maelezo yake

*******

Nilipokumbuka hiyo kauli ya babu ya `kujitolea kwa ajili ya watu wengine’ nikamkumbuka jamaa mmoja wakati tukiwa shuleni.Jamaa huyo alikuwa akipenda kujitolea sana, hadi tukamuita jina la `Valmeti,(majina ya matrekta )na kwa sasa tunapenda kuwaita watu wa namna hiyo kwa majina `majembe’…..hilo ni jembe

Jamaa yangu huyo, alikuwa akipenda kujitolea na kuwa mbele kwa kila jambo  la kujitolea, tofauti na wengine, kama ujuavyo `utoto’  na hulka ya utoto, wengi hupenda kutegeana kwenye kazi zozote. Lakini mwenzetu huyu, hata siku moja hakupenda kabisa kutegea, akiona mnasita kufanya jambo fulani, yeye husema’`ngoja nifanye mimi, niachieni nifanye mimi….’

‘Valimenti hilo…’basi tunamshangilia, na  yeye bila hiyana, atavua shati lake la shule na kubakia kifua wazi, na atalifanya jambo hilo huku wenzake tupo nyuma tukimwangalia na kukonyezana, na hata kuelekeza, 

`fanya hivi, sogeza kule,….na wengine hata kumuona ni `mjinga au anajipendekeza vile’ lakini kumbe mwenzetu alikuwa na siri yake, siri iliyojaa hekima ndani yake, na hekima hiyo aliipata toka kwa usia wa babu yake.

Tatizo hivi sasa, hatuwajali wazee, babu zetu na bibi zetu, ….watu wanawageuza babu na bibi, kuwa sio wanadamu wanostahili kuishi, na wengi wakiwaona wazee hawa, na mabadiliko ya miili yao ya macho, au mkunyazi kwenye nyuso zao hukimbilia kuwaita `wachawi..’ vigagula…ni kama vile watu wa dar walivyo sasa hivi, wakiona paka wanampiga mawe na kuwafukuza, ukiwauliza kwanini, utasikiwa wakisema

‘Wanga hawo….’

‘Jamani toka lini paka akawa mwanga,…ni utaalamu gani huo wa kisayansi, uliowawezesha hawo wachawi wakaweza kumgeuka mtu , au wao kugeuka kuwa paka, kama ni hivyo, mbona tungekuwa matajiri, maana mnaweza kujigeuza vyovyote mtakavyo, na kwa mtindo huo mnaweza kuingie popote, na kama tuna uwezo huo kwanini tusiwe matajiri…..au uchawi hauna mema, hautaki mtu kuwa tajiri

Sasa imefika hatua wazee wetu, hazina ya hekima, baraka ya dunia, tunawaita wazee hawa `vigagula, wachawi, tunawafananisha na hawo paka, ….wanga, wala nyama za watu….tunajisahau kuwa , ni swala la muda tu, kesho na kesho kutwa, na wewe utakuwa kama huyohuyo babu au bibi….na wewe ni mwanga , kigagula au mchawi mtarajiwa, au sio.

*********

‘Mjukuu wangu, unaona maisha tuliyoishi, huna baba, baba yako alikukana, akasema wewe sio mtoto wake, kampa mama yako uja uzito, na baadaye akadai kuwa sio yeye peke yake aliyekuwa na urafiki na mama yako,… huenda mimba hiyo sio yake, na hata ulipozaliwa hakutaka kabisa kukulea…lakini baadaye akaja kuishi na mama yako…..’Babu akawa anamsumilia mjukuu wake na huyu mjukuu wake ndiye aliyekuwa akinisimulia hiki kisa….

Tuanze kisa hiki ambacho tutakiita tenda wema uende zako au wema hauozi..

NB: Nilipatwa na misiba ya wapendwa wangu, shemeji yangu, na mtoto wa mdogo wangu, misiba hii ilifuatana, kwahiyo nimekuwa nipo sipo ndani ya diary yangu, Yote mapenzi ya mungu. Na mungu akipenda tutakuja na kisa hiki cha WEMA HAUZI,…

WAZO LA LEO: Uchungu wa matatizo hauelezeki, yule aliyepatwa na  hayo matatizo ndiye anayeweza kujua ni kiasi gani uchungu huo ulivyo.  Tujaliane hasa mwenza anapokuwa kwenye matatizo, ya ugonjwa, au misiba, kwani hayo yanamkuta kila mtu.


Ni mimi: emu-three

1 comment :

Yasinta Ngonyani said...

Duh..kaaaazi kwelikweli nasubiri kwa hamu hiki kisa..Tupo pamoja ndugu wangu,,