Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, April 23, 2013

Uchungu wa mwana Aujuaye ni mzazi-84 hitimisho 4Wakati uchunguzi wa polisi ukikamilika kuhusiana na kadhia nzima ya genge la wauza madawa ya kulevya na wala mlungula(blackmailer), na kesi za maujaii zilizotokana na maswala hayo. Maua alipata mwanya wa kwenda kuonana na mama yake mdogo ambaye bado alikuwa kashikiliwa kuisaidia polisi, na alipofika hapo alimkuta akiwa mnyonge sana;

‘Mama vipi, unaumwa, au ni hali ya jela?’ akauliza.

‘Jela nani kafungwa jela, hawa wameniweka rumande, na nitatoka muda sio mrefu na nikitoka hapa nawafungulia mashitaka kwa kunipotezea muda wangu bure….’akasema kwa sauti kubwa.

‘Mama mdogo, kwanini unaongea hivyo, unataka kila mtu akusikie huoni unajiharibia ….’akalalamika Maua.

‘Kwanini niogope kuongea kwa sauti, ..nitaongea hivyo hivyo kwa vile ninajiamini kuwa sina hatia, ….’akasema kwa sauto ile ile.

Baadaye Maua alikwenda kuonana na mkuu wa upelelezi ili kujua hatima ya dhamana ya mama yake, na huko ndio akapata maelezo ambayo hakuyatarajia;

‘Maua nilikuwa mbioni kuja kuonana na wewe, baada ya kuongea na mama yako na kukubaliana kuwa yupo tayari kushirikiana na sisi,…..kwa ujumala kundi nzima la hawa wauza madawa na wala mlungula, lilokuwa na makao yake pale Mererai tumelisambaratisha, lakini kuna matawi yake, …..ambayo tunataak kuhakikisha na yenyewe yanakufa….’akatulia.

‘Katika uchunguzi wetu, tumegundua kuwa mama yako mdogo alikuwa akitumika hapa Dar, kuunganisha mambo yao ….alikuwa kama mtumishi wa kutafuta mabinti, ambao walitumika kukam ilisha kazi zao…’

‘Na tulikuja kugundua kuwa hata wewe ulikuwa mmoja wa mabinti walioingizwa kwenye kukamlisha kazi zao hizo, lakini tulikosa ushahisi wa moja kwa moja,….na tulikuwa mbioni kuoanana na wewe ili utusaidie kwa hilo…..’akamwangalia Maua.

‘Mimi nitawasaidia kwa vipi?’ akauliza Maua.

‘Ni rahisi tu, …kinachohitajika ni kuelezea walichokufanyia hawa watu, na ni nani, na kama kuna njia yoyote ya ushahidi,….kwani tuligundua kuwa walikuwa na utaratibi wa kuweka kumbukumbu za video, video ambazo walikuwa wakiwatumia wahanga wao, je wewe hawakuwahi kukutumia kanda za vide?’ akaulizwa.

‘Hata kama walinitumia nisingeliweza kuowaonyesha, kwasababu ni mambo machafu….sitaki hata kusimulia…’akasema Maua akionyesha hasira nz huzuni.

‘Pole sana…na nia yetu sio kuwadhalilisha na hizo kanda za video, kwani kuna utaratibu wa kimahakama ambao utalinda heshimz zenu, hatutazionyesha hadharani, ila zitatusaidia kama vielelezo, ili haki itenedeke….’akasema huyo mkuu.

‘Nisingeliweza kuziweka kanda hizo, na popote nitakapozipatanitazichoma moto….’akasema Maua.

‘Kwahiyo unasema kuwa waliwahi kukuumia hizi kanda, kwa yale waliyokufanyia?’ akauliza.

‘Mhh, ni kweli walifanya hivyo, lakini ….’akatulia.

‘Maua najua jinsi gani unavyojisikia, lakini ni vyema tukasaidiana na hili, ili haki yako ipatikane, na walihusika waadhibiwe…’akasema.

‘Wameshakufa, wataadhibiwa kaburini….’akasema Maua.

‘Hawo ni baadhi, tuna uhakika kuwa kulikuwa na kundi kubwa la watu, hata kama viongozi wao wameshakufa, lakini wale wote waliohusika ni lazima wafikishwe mahakamani ili iwe ni fundisho kwa wengine…’akaambiwa.

‘Sasa mimi nitawajuaje?’ akauliza Maua.

‘Kama tungelipata hizo kanda, tungelijua jinsi gani ya kufuatilia…na ndio maana bado tunamshikilia mama yako mdogo kwani tunahisi anao ushahidi kama huo..’akasema huyo mpelelezi.

‘Mimi kwakweli sijui, maana mama yangu mdogo ana mambo yake na hapendi kuingiliwa, mimi sina uhakika na hilo, ila ninachojua, ni kama mlivyosema, kuwa kuna watu kwasababu ya shida walijikuta wakiingizwa kwenye kufanikisha matakwa ya hawo wahalifu, na mama mdogo naye alijikuta kwenye huo mkumbo…’akasema Maua.

‘Kama mama yako mdogo angelikubali kushirikiana na sisi, kesi yake ingelikuwa ndogo,…tungemshirikisha kama watu waliojitolea kuisaidia polisi, na kimahakama angeliweza kusamehewa, kwani kwa mtindo  huo atakuwa kakiri kosa, kuwa alishirikishwa bila kujua, na pili kaisaidia serikali kuhakikisha hawo watu wanakamatwa..’akaambiwa.

‘Sasa mnataka mimi nifanyeje?’ akauliza Maua.

‘Mshawishi mama yako mdogo, ….sisi tuna mbinu nyingi za kushawishi, lakini hatupendi kufikia hatua hiyo kwa mama kama huyo, lakini ikibidi tutafanya hivyo, ….sasa kabla hatujafikia huko hebu jaribu kuongea naye mshawishi, …..’akaambiwa.

‘Mimi sizani kama ninaweza kumshawishi mama mdogo, ninamfahamu sana,…yeye ukitaka kumpata uwe na pesa,…pesa kwakwe ndio kishawishi kikubwa…’akasema Maua.

‘Oh,…sawa wewe kaongee naye kwanza, sisi tutajua jinsi gani ya kufanya, ahsante sana kwa ushiriukiano wako’akasema huyo mkuu.

******
‘Siku nilipofika kwa docta na kuongea naye, aliniambia yote yaliyotokea siku ile ulipobebeshwa hiyo mimba…’akasema mama mdogo baada ya kuachiwa kwa dhamana, na kukubali kushirikiana na polisi.

‘Ilikuwaje ?’ akauliza Maua kwa shauku.

‘Sijui kilichokuwa kimetendeka huko ndani, na wala sikuwa ninafahamu kuwa docta alikuwepo siku hiyo….’akasema mama mdogo

‘Sasa ulijuaje?’ akauliza Maua.

‘Nilipofika kwa docta nikiwa na mzigo, mzigo ambao thamani yake ni milioni ishirini na tano, …nilimwambia kuwa ili aupate huo mzigo wake, inabidi tugawane, hizo milioni, au tukubaliane jinsi gani ya kugawana…’akasema mama mdogo na kumfanya Maua atabasamu, na huku akimwangalia mama mdogo kwa macho ya kumshangaa.

‘Wewe tatizo lako hujaamuka, hujui hawa watu walikuwaje,…mimi nilikuja kugundua kuwa hizo ndio kazi zao, wanachokifanya ni kuwarubuni watu, na baadaye wanachukua picha zao mbaya kwa ajili ya kuwatishia kuwa wasipotoa pesa wanazipelekea hizo picha sehemu ambayo inaweza kumharibia huyo mtu maisha yake…na wanachagua sehemu ambayo kweli wakizipeleka kama ni bosi, ubosi unaondoka, na kama ni mwanandoa, ….ndoa inaharibika, maana wanaweza hata kuupeleka huo mkanda kwa wakwe zako….’akatulia.

‘Maua unisamehe sana kwa hilo,…japokuwa nitakulaumu kwa kutokutoa ushirikiano, maana sasa hivi tungelikuwa matajiri….’akasema huku akibenua uso kwa hisia za kukata tamaa.

‘Hata hivyo sikupenda kukuingiza kwenye uchafu huo, lakini nilikuwa na hali mbaya kipesa, na nikaona wewe ungelinisaidia kwa hilo, ndio maana nilikuingiza huko….lakini kwa mitego, kuhakikisha kuwa ninakuwepo kila hatua, ili wasije wakakufanya vibaya…wao waliniambia kuwa wanahitaji binti mdogo, ambaye hajaguswa, nikaona wewe ni dili…’akatulia.

‘Kwa muda ule nilichokuwa nimejali zaidi ni pesa….’akasema huku akionyesha vidole kuashiria pesa.

‘Sijui walijuaje kuwa nakulinda, na walitaka waniondoe kinamna… walichofanya ni kunilewesha sana , ili nisipate muda wa kuwa karibu nawe, kwani nilipanga kuwa kila hatua nitakuwa karibu nawe, ili wasije wakakudhuru,…mimi nakujali sana, wewe hujui tu, ilitokea bahati mbaya….’akasema akimwangalia tumboni.

‘Japokuwa kwa sasa utakula jeuri yako, maana hatuna pesa, na wewe una huo mzigo, ….hapa nyumbani kwangu, nakuambi aukweli, wewe sasa utageuka kuwa mfanyakazi wangu wa nyumbani….’akasema akikunja uso kwa hasira.

Maua hakusema neno akasubiria mama mdogo aendelee na maelezo yake, akisubiria kusikia kile alichokihitajia. Mama mdogo alipoona Maua hasemi kitu akaendelea na maelezo yake.

‘Siku ile wakaniwekea madawa kwenye kilevi nikapitiliza….nlipoamuka nilijikuta nipo chooni…hawana adabu hawa watu, walinificha chooni…..’akasema.

‘Nilijuta sana, na nilipoongea na Tajiri siku nyingine, akanijia juu kwa ukali, siunajua tabia yake…..ni mkali sana kwa wafanyakazi wake….japokuwa kwako wewe alikuwa akinywea….ole wake angelikuwepo hai, nina uhakika pesa ingemtoka…safari hii nilijipanga vyema…’akasema.

‘Basi siku ile nikaenda kwa docta…..’mama mdogo akawa anaelezea huku akikumbuka jinsi ilivyokuwa siku hiyo alipokwenda kwa docta.

********

‘Una shida gani mama yangu,…maana huku ni nyumbani sio hospitalini?’ akauliza docta.

‘Shida yangu ni ndogo tu, ukikubali kushirikiana name, la sivyo,…shida hiyo inaweza kuwa kubwa , na huenda ikakuharibia kazi yako, na hata kukupeleka jela…’akasema mama mdogo.

Docta akakumbuka ile simu aliyopokea, japokuwa haikuwa na sauti ya kueleweka vyema, lakini ilikuwa ni 
sauti ya mwanamke. Akahisi huenda ni huyu mwanamama, na alipomchunguza vyema akakumbuka kuwa aliwahi kuonana naye kabla;

‘Mama ninahitajika kujiandaa, niwahi kazini,…sema kilichokuleta, …’akasema docta.

‘Hiyo kazi yako inaweza ikapotea kama usiponisikiliza mimi, hili nililokuja nalo ni jambo muhimu kuliko hta hiyo kazi yako, ndio maana nikawahi asubuhi na mapema kabla hujatoka…’akasema mama mdogo.

‘Jambo gani, elezea ili nielewe tusipotezeane muda..’akasema docta huku akishikilia taulo yake aliyokuwa kaifunga kiunoni, ilionekana ndogo kwa muda mfupi.

‘Ni hivi, mimi nina mzigo wako,…na nikisema mzigo, usijifanye hufahamu….na nilivyoupata hilo halikuhusu, ninachotaka ni kupata nusu ya hizo pesa, tunagawana,….la sivyo, mimi huo mzigo naupeleka polisi..’akasema.

‘Mzigo gani huo…..mimi sina mzigo wowote uliopotea,….kwahiyo fanya upendavyo, na naomba utoke hapa kwangu haraka…’akasema docta.

‘Kwani mzigo wako,…wa kanda za video, uliokuwa ukiutafuta, niliuchukua mimi, na …thamani yake ni milioni ishirini na tano…kama unauhitaji, sawa, nipe zangu kumi, basi nitakureejshea kama huuhitaji basi, ngoja nikawakabidhi polisi….’akasema na kuinuka kuondoka.

‘Subiri….’akasema docta.

‘Unafahamu ni nini kilichopo humo ndani?’ akauliza docta.

‘Hiyo haiinuhusu, nifahamu nisifahamu, cha muhimu kwangu ni pesa,…’akasema mama mdogo.

‘Wewe mwanamke unoata…Mimi nitazipata wapi pesa nyingi kama hizo….hebu jaribu kufikiria mwenyewe, hata kama nina hospitali, lakini pesa unazodai ni nyingi sana….’akasema docta.

‘Unajua wapi kwa kuzipata, kwa kukusaidia ni kuwa mimi nipo tayari kwenda huko ulipotarajia kuzipata, na lazimz zitapatikana, ….’akasema mama mdogo.

‘Wapi huko unapohisi zitapatikana?’ akauliza docta.

‘Wewe usinifanye mimi mtoto mdogo, usifikirie kuwa nimekuja hapa kwa kubahatisha, ninajua kila kitu, ninajua jisni gani mlivyokuwa mkifanya na akina Tajiri, na huyo Malaya wake…sasa kabla hawajakuwahi, maana ninajua wapo mbioni kuja kwako, tuwawahi mapema,…kesho kukicha tunaingia basi hadi Arusha, mzee yule ana pesa za kumwanga…’akasema na docta akajikuta akishikwa na butwaa.

‘Wewe umajuaje yote hayo, kwanza wewe ni nani….?’ Akauliza

‘Tatizo lenu nyie, mnajifanya wasomi,…lakini sisi tusioenda shule tuna akili zaidi yenu tatizo ni kuwa hatukubahatika kupata hizo nafasi, kama tungelibahatika, tungelikuwa zaidi yenu…..sasa sikiliza, tusipoteze muda, tafuta upenyo tuondoke…..’akasema.

‘Mama hilo halitawezekana…nikuambia ukweli, hapo nje kuna maaskari, jana walifika hapa kwangu wakachunguza, na kupekea kila mahali , walikuwa wakitafuta vtu kama hivyo…lakini walikuta hakuan kitu, kwani mimi nilishaharibu kila kitu, …’akasema docta.

‘Afadhali nimeuwahi huo mzigo, maana ungelikuwepo na wenyewe ungeliuharibu, tukakosa pesa, au huo mzigo ulikuwa umeuweka pembeni kwa ajili ya kupata hizo pesa?’ akauliza mama mdogo.

‘Nakuhakikishia kuwa kama ungelikuwepo ungelikuwa ni wa kwanza kuharibiwa, …hilo sasa hivi ni kaa la moto, ..ni bomu, wala mimi siuhitaji tena huo mzigo, kama wewe unajiamini,  endelea kukaa huo mzigo, na endelea kuwa na mawazo hayo yaliyopitwa na wakati,…, lakini mimi simo kabisa, nimeshatubu, na nahisi nipo mweupe, nasubiri kwenda mbinguni….ila kilichokuwa kikinisumbua ni huo mzigo maana, haujaharibiwa, na ni vyema, ukafika kwa mlengwa kwanza….naomba tafadhali uharibu au vinginevyo ufikishe kwa mwenyewe anayestahili kuwa nao, na nina uhakika akiuona atauharibu mwenyewe,….’akasema docta.

‘Sawa hakuna shinda, najua polisi wanauhitaji sana huu mzigo,….na wao wataamua kuuharibu au la, ngoja niwapelekee..’akasema huyo mama.

‘Kwanini uwapelekee polisi,…ili kuondoa utata, na watu kuletewa matatizo, mimi naona ni vyema ukaharibiwa kabisa,….maana kuwepo kwake, hakutakusaidia wewe, ila utakuwezesha wewe kuonekana kuwa ualikuwa unahusika, na matokeo yake ni wewe kwenda jela, kwani ni vielelezo vinavyohitajika na polisi….mimi nimeshawaambia kuwa sina kitu chochote, na wamehakikisha, ….’akasema docta.

‘Sawa, kama wamehakikisha basi ngoja niwapelekee….na wao watajua unamuhusu nani, na nani kautengeneza na kwa ajili gani,….natumai wao watanishukuru sana…’akasema huku akiondoka.

‘Wewe mama hebu tulia kidogo, …tafadhali nakuomba kitu kimoja,…mimi sina pesa unazozihitajia, na sitaweza kwenda kwa huyo unayehisi kuwa anaweza kuzitoa hizo pesa,   mimi nakushari ni bora tukauharibu, au vinginevyo, naomba umpelekee Maua,….’aliposema Maua akanyamaza kwa muda kama aliyekumbuka jambo, halafu akasema;

‘Nakuomba tafadhali usiupeleke polisi..Tajiri mwenyewe, aliniagiza kuwa niuharibu…lakini sikuweza kupata nafasi ya kufanya hivyo…’akasema Docta

‘Tajiri eeh, unaona kumbe mambo yapo wazi,….sasa kwanini Tajiri alikuambia uuharibu?’ akauliza na Docta akawa akawa anamwangali yule mama kwa macho yaliyojaa wasiwasi kwani kumbukumbu za mazungumzo yake na Tajiri, yalikuwa yakimjia kichwani, na kuwa kama ndoto iliyopita, …kwani kumbe yalikuwa ni maongezi yake ya mwisho na mtu waliyeshibana sana….

*********

‘Tajiri, habari za siku nyingi, vipi maendeleo ya huko, …?’ akauliza kwenye simu, huku akiwa kaweka kumputa yake mbele, alijua kuwa kuna kazi anatakiwa kuifanya na huyo bosi wake kwenye kazi hizo za kudurufu kanda za video.

‘Sikiliza docta , hali iliyopo sasa hivi ni mbaya sana, polisi wamecharuka, na hawakamatiki kwa chochote kile, hawataki pesa…., hapa ninapoongea Malikia yupo jela…sasa sikiliza, kuna jambo kubwa nimeligundua, na najua wewe una nakala za zile video zetu….’akasema.

‘Nakala kama ipi, au ya tukio la wapi?’ Docta akauliza akifungua nakala za video zilizopita.

‘Lile tukio la kafara, lililofanyiaka Dar, …..najua bado una nakala yake,….ninachotaka ni kuwa, utengeneza nakala nyingine tofauti na ile ya mwanzo, nah ii ya sasa hivi, hakikisa mimi unaniondoa kabisa, …wabakie wahusika wengine, …sawa, na ukishamaliza, ifute kabisa hiyo kazi kwenye komputa yako,….’akasema na kutulia, halafu akaongezea kusema;

‘Kutokana na hali ilivyo,  futa kazi nyingine zote zinazotoakana na mambo yetu,…..,kwani unaweza ukaingiliwa na polisi wakati wowote…ukawa hatiani’akaambiwa.

‘Kuna nini kimetokea,….?’ Akauliza docta akiwa na wasiwasi

‘Polisi wameshagundua mengi, na ninachoogopa ni kuwa malikia anaweza kufanya lolote, hata kama akiwa jela, nataka akitoka, akukute huna ushahidi wowote, kwani alivyo anaweza akatugeuka,…kama anaona akifanya hivyo yeye ataokoka…natuma unanielewa?’ akauliza.

‘Ni kweli yule mama haaminiki, …nitafanya hivyo bosi, lakini …..’akataka kusema kitu.

‘Najua unataka kusema nini.…hilo nitafanyia kazi, najua hiyo kazi ulihitaji milioni tano, au sio…ni pesa nyingi sana, lakini kwetu sisi ni pesa kidogo, kwani hiyo kazi tukimpelekea mteja…., tungelikusanya zaidi ya shilingi milioni ishirni na tano…kama angelikuwa mtu tumemkusudia, ….na hayo yalikuwa mahesabu ya malikia, alipotaka kuzipata hizo pesa kwa mzee…., kwasasa kazi hiyo haina maana kwetu, kwani ni nani atatupa hizo pesa…siwezi kwenda kumdai mzee, ….’akasema.

‘Lakini mzee bado yupo, unaweza ukatumia watu ukazipata hizo pesa, sio kwamba nakushauri ufanye hivyo, hapana,nasema tu, kuwa kama  mtu unatamaa ya pesa ungeliweza kuzipata kwa mzee mwenyewe  ….’akasema docta.

‘Ndio mzee bado yupo, lakini ukumbuke mabinti zake wamesharudi, na wanataka kujishughulisha kwenye miradi ya baba yao,…kwa sasa hivi wanahitajia malipo yote ysilipwe mpaka wao wakahakiki, japokuwa kisheria Wakili bado ana haki ya kuidhinisha malipo maana hakuna barua yoyote iliyotumwa benki kumuondoa yeye…’akasema.

‘Sasa unataka nifanyeje kwenye huo mkanda?’ akauliza.

‘Ukishautengeneza kama nilivyokulekeza , na kuniondoa mimi kabisa, wakabakia wahusika wengine, hapo mimi sitajulikana kabisa kuwa nilikuwepo,na hata kama nilikuwepo, lakini sikuhusika  kwenye tendo lenyewe,…atabakia huyo muhusika mwingine, ambaye yupo tayari kubeba dhamana zote,…kwa huyo binti….’akasema.

‘Mimi nilikuwa nahisi ni kwa ajili ya kupata pesa kwa mzee, kumbe ni kwa ajili ya huyo binti, …..kwa vipi tena imekuwa hivyo eeh?....Maana tangu mwanzoni uliniambia kuwa huyo ndiye anayekufaa, au sio , anayekufaa…kuwa mke wako, kuna nini kimetokea ambacho mimi sikijui?’ akauliza docta.

‘Hayo yaache kama yalivyo, maana ….hapa nilipo natamani dunia ipasuke nizame ndani yake, lakini yote ni maisha, na ….kwa vile , kuna huwo uwezekano,. ….naomba ufanye hivyo, kwani tukio zima limeharibu mpangilio wangu wa kimaisha…yaani hata sijui kama nitaweza kusahau hilo ,….na huenda yote yametokea kama adhabu kwangu….maana hii njia ya kutafuta utajiri, naona unanitumbukiza kwenye kina cha moto….najihisi kuwa wakala wa ibilisi…’akasema.

‘Una maana gani kusema hivyo,mbona unaonekana kama vile kuna jambo kubwa umeligundua, na nakushauri, uwe makini na hayo mawazo, unaweza ukajikuta ukipatwa na mshituko wa moyo, usiwazie kihivyo, kama limetokea jambo, tafuta ufumbuzi, na ulitatue, usiliweke kichwani ….kwani kuna nini mzee wa mapesa, ….?’ Huyo docta akauliza na kabla Tajiri hajajibu, huyo docta akasema;

‘Mimi kwakweli, nilishawaambia kuwa hayo mnayoyafanya ipo siku mtakuja kujijutia, japokuwa mumeniingiza kinamna, lakini moyo wangu haupo radhi na haya yote,…..kwanza imeniumiza sana,pale mnapochukua mabinti wa watu wadogo wasio na hatia kwenye mambo yenu….lakini hamjachelewa, acheni, tubuni, …na tafuteni njia nyingine ya kuishi…..’akasema docta.

‘Unajua docta unaongea hivyo, kwa kuwa hukuingia ndani kabisa ya haya mambo,….natamani nifanye hivyo, lakini..oh,…..nimekuwa kama nimenaswa kwenye ulimbo wa haya yote. Kwa ujumla yote hayo niliyafanya, na moja ya masharti ya zindiko….tungelifanyeje, ….’akasema Tajirikujitetea.

‘Hapana,hayo ni mambo yakishetani, kwani zindiko ni lazima, kwani wanaofanikiwa wanafanya hayo, hebu angalia hawo wazungu wanafanya hizo biashara, ina maana na wao wana mazindiko ya kizungu, hakuna kitu kama hicho, mimi kama mtu wako wa karibu nakushauri uachane kabisa na mambo hayo….’ Akasema docta.

‘Nimekuelewa docta…..’akasema Tajiri, lakini kauli yake ilikuwa ikiashiria unyonge fulani, na dota akaona hapo ndipo sehemu ya kumpa vipande vyake huyo jamaa , akasema;

‘Angalia kama hilo mnaloliita eti ni zindiko, hilo la Dar, ambalo unataka tulichakuchue….huyo binti emeniuma sana, kwani hafanani kabisa na kutendewa hayo mliyoyatenda….sijui kama mtasamehewa kwa hilo,….sio halali kabisa,……’akasema.

‘Lakini docta,….mimi sikujua wewe ulifika hapo na mzee, na mliyoyafanya sikuwa nayajua,kama nisingeliuona huo mkanda wa video,nisingelijua kuwa mlifika na sikuwa ooh, tuyaache hayo maana yananiuma sana, sikujua kuwa najiumiza mwenyewe…ooh, docta naona hayo tuyaache….’akasema Tajiri.

‘Sawa tutayaacha ila nataak nikuweke sawa, maana sikuwa nimepata muda wa kukuelezea vyema ilivyokuwa siku hiyo, huenda ukaniona na mimi nilikuwa mmoja wa hayo mambo yenu, …’akasema docta.

‘Kwahiyo unataka kusemaje…?’ akauliza Tajiri.

‘Kama nilivyokuwa nimekuambia…japokuwa sikuwa nimekufafanulia vyema …ni kuwa, hayo maelekezo niliyapata kutoka kwa Malikia, na kama sikosei lengo na nia yake,ilikuwa kukuzuia wewe usije ukawa na uhusiano wa karibu na huyo binti, kwani kama sikosei, alishaambiwa na watu wake,kuwa wewe upo mbioni kumfanya huyo binti kuwa mchumba wako….’akasema docta.

‘Docta acha hayo maelezo yako….sipendi kuyasikia….kwasababu mwanzoni sikuwa naelewa hivyo…’akasema Tajiri.

‘Ndio hivyo Tajiri, mimi nataka kukufafanulia tu…kuwa watu wake ndio huenda waliokuwekea kilevi,ili uzidiwe na ushindwe kufanya lolote kwa huyo binti…ingawaje wewe ulisema unahisi Malikia kuna mchezo kakufanyia ili usiwe na nguvu, ukikutana na watu asiowataka….lakini siku ile ilikuwa ni lazima zindiko lifanyike au sio, na watu waliokubalika kwenye hilo mnaloliita zindiko wewe na mzee…..bila nyie nguvu ya huo ushirikina wenu usingelifanya kazi au sio?’akasema docta.

‘Oh,.. unajua docta sasa naanza kuelewa….huyu mwanamke,…ndiye kaniingiza kwenye haya yote, bila yeye sizani kama ningeliinga kwenye dhambi hii kubwa….sasa nitahakikisha ama zake ama zangu…’akasema Tajiri kwa hasira.

‘Hilo wewe na malikia nii sawa na pwagu na pwaguzi, ….ila ninalotaka kuliweka sawa na hiloo tukio la siku ile, ili uelewe kuwa mimi sikupendelea hayo, kwani aliponielezea Malikia kuwa Wewe na mzee, ndio pekee mliostahili kulifanikisha hilo na wewe hutaweza kufanya lolote, akanishauri nimchukue mzee…’akasema.

‘Lakini mzee alishaniachia kila kitu…’akasema Tajiri na kukatiza maelezo yake.

‘Ndio kwa maelezo ya malikia kutoka kwa shangazi yako, aliambiwa …unakumbuka shangazi yako, yaani mke wa mzee, ndiye anayejua zaidi mambo hayo kwa vile yeye ndiye aliyemuingiza mumewe kwenye shughuli hizo..’akasema docta.

‘Hayo nayafahamu sana…’akasema Tajiri.

‘Sasa malikia aliongea an huyu mama, ndio huyo mama akamuelekeza njia mbadala kuwa wanaoweza kufanikisha hilo ni wewe na mzee, hilo halifutiki mpaka mkutane tena na huyo mtaalamu ambaye kwa sasa hajulikani alipo,..sawa si sawa?’ akauliza docta.

‘Hilo ni sawa….’akasema Tajiri.

‘Na ukumbuke siku ile, nilikuwa na mzee huku Dar, kwasababu alitaka nimfanyie upasuaji kwa ajili ya kumrejeshea hali yake ya kumuwezesha mbegu kubebesha mimba tena…’akasema docta.

‘Oh,….mbona hukuniambia hilo docta…oh, sasa kumbe mambo yatajiweka sawa,…Kwahiyo ina maana kumbe uliwahi kumrejesha  mzee uzazi wake…mambo sasa yamejiweka sawa…’akasema Tjiri akionyesha hali ya furaha.

‘Unakumbuka wazo la kumfanyia huyo mzee huo upasuaji , lilitoka kwa mkewe, kuwa ili mumewe asije akawa na watoto wan je, basi afanyiwe huo upasuaji, lakini ionekanae kuwa ni kwa ajili ya fya yake, na hata mwenyewe, …mzee asijuie hilo, ….na kweli mzee alijua kuwa anafanyiwa huoo upasuaji kwa ajili ya afya yake,….’akasema docta.

‘Kwahiyo na wewe kumbe umehusika..huwezi kukwepa hilo?’ akasema Tajiri.

‘Oh, siwezi kuhusika…kwa kipindi kile niliona ni jambo la busara, kama kila kipindi huyo mzee alitakiwa kutafutiwa mwadada…kwa ajili ya hilo zindiko, huoni uwezekano wa kuwa na watoto wan je ungelikuwa mkubwa…..?’ akawa kama anauliza.

‘Ok, sasa niambie ina maana ulimrejesha mzee, kwenye hali yake,na ikafanikiwa?’ akauliza Tajiri.

‘Kwanini isifanikiwe, ni upasuaji mdogo tu….,na siku ile nilipopata simu ya malikia kuwa wewe hutaweza kufanya lolote siku hiyo, na  hilo zindiko ni muhimu kwenu, nikaona mzee,akapate mazoezi… na malikia kwa vile alikuwa akijua nipo na mzee huku, na japokuwa hakujua kuwa mzee yupo huku kwa upasuaji huo…yeye akanisahuri nimshinikize mzee mpaka akubaliane na hilo tendo….’akasema docta.

‘Lakini mbona….hizo dawa za malikia,…..hazikufanya kazi….kama ilivyokuwa siku nyingine,maana nilipoamuka, sikuwa na hali kama ile iliyonifanya ninywe pombe …..kwa hasira,niliposhindwa kufanya kile nilichokuwa nimekitamani kukifanya siku nyingi….nilikimbilia kulewa na nilipoamuka..oh, sitaki hata kukumbuka…?’ Akasema Tajiri na kutulia kimiya.

‘Hayo mimi sijui,….kama nisingeliuona huo mkanda, nisingelijau kilichotokea baadaye,….maana mimi niliondoka na mzee…hata hivyoo kuhusu hizo dawa kama unahisi alikuwekea malikia ungelimuuliza yeye….huenda nguvu za dawa yake aliyokuwekea ilikuwa imeisha muda wake, ndio maana alinisisitizia nihakikishe wewe huamuki hadi asubuhi….’akasema docta.

‘Ulitakiwa ufanyeje….?’ Akauliza Tajiri kwa hasira, na kabla docta hajajibu akaendelea kuuliza

‘Kwanini sasa hukufanya hivyo…kwani ingelisaidia mengi….aheri ungelifanay hivyo, kwanini hukufanya hivyo?’ akawa aanuliza Tajiri kuonyesha kusikitika.

‘Sikuwa na muda huo, mzee, alikuwa katahayari baada ya hilo tukio, akaniomba turejee kwake,ilionyesha kukerwa sana na tukio hilo kwani aliniambai kuwa yeye alishajitoa kwenye mambo hayo, ila alifanya ….oh, eti kwa vile nilimshauri mimi, hakujua kuwa mimi nilimshauri hivyoo kutokana na Malikia….na kesho yake tukarudi Arusha haraka, kwahiyo wengi hawakujua kuwa mzee, alikuwepo hapo, kama isingelikuwa huo mkanda wa video kuonyesha hilo tukio…..’akasema.

‘Docta, sasa hapo mpango wangu utafanyika vyema, …..fanya kama nilivyokuambia,….vinginevyo nahitajika kufanya jambo ambalo huenda sitaliweza…’akasema Tajiri.

‘Kwanini sasa unakata kufanya hivyo, una wasiwasi kuwa huyo binti atakushitaki kwakutumia huo ushahidi?’ akauliza docta.

‘Hapana,….kuna mengine zaidi ya hayo….naombe usiyachimbue zaidi…kwani vinginevyo natakiwa niende hapo alipozaliwa huyo binti, yakaanyike mambo ya kutakasa, huko nikakutane na watu wa msituni, watanisaidia….nani atajipeka kwenye mdomo wa simba…..oh, tuyaache kama yalivyo.’akasemaTajiri

‘Kwanini sasa yafanyike hayo yote, ….kwani siku zote mnafanya hivyo, kwanini hilo tukio liwe tofauti, na ama kwa mzee wako yaliyotokea sio kwa nia mbaya,ilikuwa ni kwaajili yakufanikisha hilo mnaloliita zindiko….na najua baadaya hapo,hakupendelea tena….’akasema docta

‘Ungelijua yaliyotokea huku…, usingelisema hivyo…nilikuwa karibu nikosane na mzee…lakini kumbe ni  kwa maslahi yangu, sikujua kabisa…..kuwa hali hiyo itakuja kunisaidia baadaye….oh, we acha tu…na hapa tumeshachelewa, ….nilitakiwa kwenda hukoo kijijini niende kwenye hilo posi alipozaliwa huyo binti, vinginevyo…mabalaa yatatokea, ikiwemo vifo….’akasema Tajiri.

‘Oh, achana na imani hizo….wewe sasa angalia muelekeo mwingine,…hata hivyo nikuulize, kuna nini kinaendela kati yako na mzee, ina maana mnamgombea huyo kimwana au sio?’ akasema docta  kwa mzaha na kucheka.

‘We acha tu, ….sitaki hata kukumbuka…natamani,dunia ipasuke nizame….. lakini nahisi yote yalitokea ili iwe heri kwangu, kati yangu na mzee na….fanya hivyo, hakikisha unaondoa kila kitu kuhusu mimi, na mimi huku nitajua la kufanya,….sipendi kabisa nionekane nilikuwepo kwenye hilo tukio, ….na huo utakuwa msimamo wangu hadi kifo, ….vyovyote iwavyo, nataka iwe hivyo… ni heri isijulikane hivyo, ….na safari ya kwenda huko msituni, ….sijui kama itawezekana kwa sasa….lakini ni muhimu..’ Akasema.

‘Sawa bosi….hiyo safari yako ya msituni, naona unaisema sana, kuna zindiko jingine tena au kuna nini zaidi….sawa naona hilo hutaki kuniambia, ila nakuuliza kuhusu hii kazi yako ,nikashamaliza nifanye nini? ’akauliza docta.

‘Hiyo nakala utampa Maua….pale nitakapokuarifu ufanye hivyo, au kama kutakuja kutokea lolote maana haya mambo sasa yananitisha, nakuomba umpe hiyo kazi Maua, ili ajikoshe moyo wake, huo utamsaidia kama ushahidi wake….sina zaidi, tutaongea ukikamlisha hiyo kazi…’akasema na kukata simu.

Docta alitafuta hiyo kazi kwenye komputa yake, na kuitengeneza kwanza kama ilivyokuwa, na kutoa nakala moja,….

‘Hii nakala nitaiweka kama akiba…huenda milioni ishirini na tano nikazihitaji….’akasema na kuiweka ile nakala kwenye sehemu yake maalumu, halafu akaanza kuitengeneza hiyo kazi kama alivyotaka Tajiri, na alipokuwa karibu kuimalizia hiyo kazi, komputa yake ghafla ikasimama,…na akahindwa kuimalizia hiyo kazi kwa kuiweka kwenye CD’s.

‘Oh, mbona ilikuwa karibu nimalize….’akasema na mara simu yake ikaita kuwa anahitajika kazini kwake;

‘Hii kazi nitakuja kuifanya baadaye….’ Akasema na haikuwezekana kuifanya hiyo kazi tena, kwani kesho yake alisikia kuwa Tajiri keshaiaga dunia.
******
 Docta akahisi kuwa kasikia mlango ukifunguliwa, na akafunga taulo lake vyema kiuoni, na kugeuka kuangalia mlangoni.

‘Nahisi hawo ni polisi, kama umekuja na huo mzigo, tafuta sehemu ukaufiche, ….tafadhali, sitaki waje wauone upo hapa kwangu…’akasema na mama mdogo akageuka kuangalia mlangoni, na mara mlango ukafunguliwa kwa kasi, akaingoa mtu aliyekuwa kajifunika uso mzima na kubakiza macho, akiwa na bastola mkononi..

Mama mdogo, akanyosha mikono juu kwa haraka kujisalimisha,a , huku akitetemeka, na kabla hajasema kitu , yule mtu akaielekeza ile bastola kwanza kwa mama mdogo, na mama mdogo, akashika kichwa kama analinda kichwa chake kisipasuliwe na risasi, na alikaa hivyo kwa muda,….., hata pale aliposikia sauti ya mtu akilia kwa  maumivu, bado aliendelea kukaa  vile  vile, akiogopa kuondoa mikono au kumwangalia huyo mtu ….
Kukawa kimiya, na mama mdogo , akainua kichwa kwa pole pole akiangalia mlangoni,….hakukuwa na mtu tena,…hakuamini, kuwa amepona, akajikagua..na alipoona yupo salama, akageuka kumwangalia docta, ….Docta alikuwa kalala kwenye sakafu huku kashikilia kifuani,…damu zikiwa zinamvuja,…

‘Oh, ….hawa watu hawana maana ina maana wamemuua docta…..ina maana mamilioni ndio sitayapata tena..hapana mimi sikubali …’akasema akimwangalia docta aliyekuwa akigugumia kwa maumivu.

`Sasa hili ni balaa….’ Akasema mama mdogo, na kugeuka kutaka kuondoka, na sauti ya docta akiomba msaada ilisikia, na mwisho akasikia sauti iliyoashiria kukata -tamaa ikasema;

‘Ta-fadh-li, ha-ri-bu  ka-bi-sa huo mka-nda,..p-le-ase…au m-pe Ma-ua ooooh’ ilikuwa sauti ya mwisho wa docta, na mara akatulia kimiya….

 Mama mdogo ambaye alikuwa kashikwa na butwaa, akishindwa kuondoka,na hakujua afanye nini kwa wakati ule,…..alipoona docta katulia kimiya, akamtupia jicho kwa haraka, na bila kumsogelea, akageuka kuondoka,….

 Alitembea hatua tatu…halafu akili ikawa inamtuma kufanya jambo jingine, na hapo kwa haraka akaangaza mle ndani kama kuna kitu anachoweza kuondoka nacho,…. lakini kabla hajalisogelea kabati, ambalo alihisi anaweza kupata kitu, akasikia sauti ya mlango wa getini ikiashiria kufunguliwa , akajua kuna mtu kaingia…

‘Oh,…mbona sasa huu ni mkosi,…ina maana nitaondoka hapa hata bila senti…’akasema huku akikimbilia mlangoni, na kweli akasikia mtu akifungua mlango wa hiyo nyumba, akajificha, hadi huyo mtu alipoingia ndani….alikuwa mwanadada, akiwa kavalia  nguo za kutokea, na alionekana mrembo, na mmamdogo akahisi huyo atakuwa mfanyakazi wa hapo,….

Huyo mwanadada alipoingia ndani kwanza kabisa alielekea chumba chake cha kubadilishia nguo, hakuingia moja kwa moja kusalimia kwa bosi wake, na hii ilimsaidia mama mdogo, kutoka pale alipojificha bila kuonekana na huyo mwanadada

Mama mdogo alipoona huyo mwanadada haonekani tena, yupo huko ndani kwenye chumba ambacho alihisi nisehemu anapobadilishia nguo,yeye  kwa haraka akatoka pale alipojificha na kuelekea nje, hakusubiri, ….akakimbilia kwenye geti la nje, na alipofungua geti tu,  yowe likasikika toka ndani ya hiyo nyumba, ….yeye hakutaka kugeuka…alichojua yeye ni kuhakikisha anaondoka kabisa eneo hilo…..

NB: Nimekuwa sipo hewani karibu wiki sasa, sababu ya mambo yaliyojuu ya uwezo wangu, likiwemo la ukosefu wa mtandao, na umeme…tuwiane radhi maana sikuwa na jinsi nyingine, hizi ni sehemu mbili kwa pamoja, nimefanya hivyo nikichelea kupata tatizo jingine kama hilo….natumai sehemu ijayo huenda ikawa ndio mwisho wa kisa hiki, …..

WAZO LA LEO: Yaliyopita ni sawa na ndoto,…kunapopambazuka au ukiamuka ndoto hiyo imekwisha. Hatahivyo matendo yetu yaliyopita yawe ni dira, kama nuru ya jua …. yanayotuonyeshea muelekeo wa kimaisha, kama matendo hayo yalikuwa ni mabaya, jisahihishe kwa kutenda mema, na kama yalikuwa ni mema, yawekeze kwenye msimamo wako wa  kimaisha. 

No comments :