Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, March 22, 2013

Uchungu wa Mwana Aujuaye ni mzazi-75

‘Maua nilirejea Dar, nikiwa sina hamu kabisa ya kurudi Arusha, kwani ilibidi tuondoke haraka, baada ya mama mdogo kwenda kufanya utapeli kwa Mzee, mjomba wake, Tajiri, akidai kuwa tumeshikiliwa kwenye hoteli kwa kudaiwa deni kubwa, ….

Aliendelea kuhadithia kisa hiki.

*****
Mama mdogo alifika nyumbani kwa Mzee, na bahati nzuri, alimkuta mzee akiwa peke yake, mabinti zake wawili walikuwa wametoka kidogo, na hiyo ikawa nafasi nzuri ya mama mdogo kuongea na huyo mzee, akiwa na malengo yake kichwani.

‘Mzee nashukuru sana nimekukuta wewe mwenyewe, maana kuondoka kwa Tajiri, kumetuacha katika hali ngumu sana, yeye ndiye aliyekuwa akitusaidia, ikizingatia kuwa yeye ndiye aliyetuchukua Dar, kuja huku akiwa katupa matumaini mengi,....lakini sasa kuna tatizo limetokea, na hatuna oa kwenda zaidi ya kuja hapo kwako mzee...'akasema mama mdogo, akitumia lugha ya huzuni, na upole.

'Kwani kuna tatizo gani, mbona nilishawaambia mje mkae hapa,...lakini mlisema mna sehemu mumeshalipiwa, hamuwezii kuondoka huko, ...niambie ni shida gani, mimi nitawasaidia..'akasema yule mzee.

'Ni kweli tulisema hivyo, na ndivyo tulivyokuwa tunafahamu,...hatukujua kabisa kuwa tunadaiwa pale hoteli tunapokaa…hawa atu wa hoteli hiyo wametuchanganya kabisa, na sijui kwanini walisubiri hadi Tjairi afarikie ndio waje kutudai,.....mzee, nakuomba sana mzee, tupo chini ya miguu yako, …sijui utatusaidiaje,maana hapa tulipo hatuna mbele wala nyuma….’akasema mama mdogo, akifikia hadi kupiga magoti.

‘Lakini kama ni hotelini, mbona nilisikia kuwa mlishalipiwa mapema kwa zaidi hata ya miezi sita,….’akasema mzee.

‘Ndivyo tulivyokuwa tunafahamu hivyo, ….sasa sijui Tajiri, alituhadaa, au vipi, au huenda alikuwa na mipango nao, kuwa atawalipa, .....kwakweli mzee hatujui ni nini kilikuwepo kati ya mwenye hoteli na Tajiri, maana mwenye hoteli kabadilika kabisa, hatujali, na anaona hatapata pesa zake kwa vile Tajiri keshafariki,....naogoa hata kumuongelea marehemu…kwakweli alitujali sana’akasema mama mdogo

‘Basi mimi nitalilipa hilo deni kama lipo,....na sioni kwanini muendelee kukaa huko hotelini wakati nyumba hii ipo, ina vyumba vingi vinakaa bila mtu, njooni mkae hapa kwangu, kwani Maua yupo wapi...mbana hamkuja naye?’ akauliza Mzee.

‘Imebidi nimuache Maua pale kama dhamana,….hawatuamini, waliona kuwa tukiondoka wote , deni halitalipwa...basi tukakubaliana kuwa mmoja abakie hapo, kama dhamana, na mimi nije niongee na wewe, na kama kwako itashindikina , basi sijui tutakwenda wapi,.....kwahiyo Maua kashikiliwa, wamesema hawatamruhusu hadi hapo tutakapolipa hilo deni...na leo tusipowalipa, Maua atakwenda kulala jela...’akasema Mama mdogo huku akimwangalia Mzee kwa jicho la kujiba.

Mzee alitikisa kichwa kwa kusikitika, akainuka na  kujishika kwenye mifuko yake kama anatafuta pesa, na akasema;

‘Haiwezekani Maua alale jela,...kwani mnadai shilingi ngapi?’ akauliza huyo mzee, na mama akatabasamu kwa kujiiba, akapiga mahesbabu ya haraka haraka, akasema;

‘Milioni…eeh, ni milioni karibu na nusu, kwani pamoja na kodi, pia tulikuwa tukipata mulo, kwa bili, siunajua tena sisi bado vijana, wakati mwingine tunakunywa...na Tajiri alisema atalipa, tule , tunywe hakuna shida, yeye jina lake linajieleza,..kumbe hakuwahi kulipa hilo deni…huenda alipitiwa...na alikuwa anajua atalipa muda wowote....’akasema mama Mdogo.

‘Tatizo la mpwa wangu, alipenda sana kujifaharisha,...na matokeo ayake watu wanamtumia vibaya, simlaumu sana, kwani hata hivyo, alikuwa mtu muhimu sana....lakini mbona pesa nyingi kiasi hicho,…..?’ akauliza Mzee akiingiwa na wasiwasi.

‘Kama huna basi…..namsikitikia sana Maua kwani kashikiliwa na huenda sasa hivi atakuwa mbioni kupelekwa polisi…mimi inabidi niende sehemu nyingine nikaombe ombe, maana msichana wa watu bado mdogo, na anajikuta kwenye matatizo ambayo hata hakuhusika nayo…oh, mzee, tumeumbuka wenzako..’akasema Mama mdogo.

‘Sijasema kuwa sitawasaidia....na sitapenda kabisa Maua, akashikiliwe na polisi, yule ni msichana mdogo, na akifika huko polisi, wanaweza wakamuumiza...hapana, au niwapigie simu hawo wenye hoteli, niwaambie mimi hilo deni nitalipa mimi....'akasema akaenda kuchukua simu.

'Mzee, haina haja, kama huna pesa kwa sasa , usisumbuke, maana walishanionya, wakasema sasa hivi wanachohitajia  ni fedha taslimu, sio ahadi tena....'akasema mama Mdogo akiinuka kuondoka.

'Oh,Ngoja, kidogo.......', Mzee wa watu akaingia ndani kwenye ofisi ndogo, na hapo Mama Maua akatabsamu na kuinua kidole juu kuonyesha ushindi.

Baadaye Mzee akatoka na pesa mkononi, akasema;

'Unajua huwa sipendi kukaa na pesa nyingi ndani, na hapa nimepata hizi milioni moja,....kawalipe na waambie kuwa hiyo laki tano, nitalipa mimi mwenyewe, nitaagiza pesa hiyo iletwe hapa, na nitakuja kuwalipa,.....'akasema huku  akimpa mama mdogo hizo pesa.

Mama mdogo alipoziona zile pesa, akawa anaigiza kama mtoto mdogo vile, mnyenyekevu, kama mtumwa wa fulani, akainama kidogo, na kuzipokea akiwa kama anataka kupiga mgoti, na akatoa shukurani nyingi.

'Hamna shida, msijali kabisa.....'akasema mzee na kuzidi kumshauri kuwa wakishalipa hiyo pesa waondoke huko hotelini waje wakae hapo kwake, kwani hata hivyo alikuwa na maongezi na wao wote.

‘Peleka hizi milioni moja, hiyo nusu waambie nitakuja kuwalipa mwenyewe, na wakibisha wape simu yangu wanipigie…’akasema huyo mzee. Na yule mama akiziweka zile pesa kwenye pochi yake, na kuitumbukiza pochi ile kwenye mkoba wake, na kusema;

‘Tutakuja tu mzee, hapa ni nyumbani, ….’akasema na kuondoka kwa haraka.  Baadaye yule mzee alipoona kimiya akaamua kwenda kwenye hiyo hoteli kuulizia mwenyewe na kumalizia hiyo elifu hamsini iliyobakia.

Mzee wa watu akiwa anaamini kuwa kweli watu hawo walikuwa wakidaiwa, na akiwa na wasiwasi wasije wakampeleka Maua jela, akainama akimuwaza Maua, akataka kupiga simu, lakini akaona kwa muda ule haikuwa na umuhimu sana, kwani pesa hiyo inatosha kuwaonyesha hawo wenye hoteli, kuwa wana dhamira ya kweli ya kulipa hilo deni.

Aliagiza kijana wake ambaye ndiye anayemtuma shughuli ndogo ndogo, kuwa aende ofisini kwake, akachukue pesa , kwani ana shida nazo, na zilipoletwa, akaondoka, kuelekea huko kwenye hoteli, ambayo anafahamu ndipo Maua na mama yake mdogo, wamepanga, aliondoka akiwa na shauku kubwa ya kukutana na Maua.

'Oooh mzee vipi leo mbona umefika mwenyewe una kikao jioni tukuandalie ukumbi?' akauliza MENEJA ambaye alipewa taarifa haraka kuwa kuna gari la Mzee limefika hapo, na meneja akatoka kwenye ofisi yake haraka kwenda kukutana na huyo mzee, hakutaka mzee huyo aongee na wahadumu, maana mzee huyo ni mtu mashuhuri sana.
'Nimekuja kuwaona watu wangu, ambao wamepanga hapa....'akasema mzee akiangali huku na huku, kama vile akitarajia kumuona Maua au polisi wakiwa wamemshikilia Maua.

'Watu gani hao mzee, mbaona hatuna watu wako, siku nyingi hujatutembelea mzee, ....'akasema Menaja.
'Wapo watu wangu hapa, akina mama wawili, Maua na mama yake mdogo....'akasema mzee.
'Maua, ....?' yule meneja akawa kama anafikiria, kwani hakumbuki vyema hilo jina.....akageuka kumwangalia mhudumu wake, na mhudumu wake, akasema;

'Hawo watu mbona wameondoka muda kidogo,....waliondoka siku nyingi, na kuhamia hoteli nyingine, baada ya kufukuzwa kwa shinikizo la Malikia.

'Mbona sielewi, Malikia, ….mbona huyo mtu alishafungwa, japokuwa....eeh?’ Akauliza mzee kwa mshangao na akawa bado anangalia huku na kule, alitarajia atawaona Maua na mama yake mdogo

‘Ndio kipindi hicho Malikia alikuwa hajashikwa na polisi…kama tungelijua kuwa huyo mwanamke ni mbaya kiasi hicho tusingemsikiliza, lakini aliwatumia polisi, na ikabidi tuwafukuze hawo watu…Maua na mama yake wakaondoka...’akaambiwa na mhudumu wa hiyo hoteli.

‘Kwahiyo mlikuwa mnadai shilingi ngapi?’ akauliza mzee akimwangalia Meneja.

‘Hakuna deni lolote kwa hawo watu, kwanza ilibidi tuwaombe radhi, kwa hayo yaliyotokea,, hawatudai chochote mzee,  Tajiri alilipa deni lote,….’akasema huyo meneja, akimwangalia mhudumu wake ambaye alitikisa kichwa kukubali kuwa watu hawo hawadaiwi.

‘Mbona nimeambiwa kuwa mnadai milioni moja na nusu, na mumemshikilia mmoja wao, anayeitwa Maua, na mlikuwa mpo mbioni kuwapeleka polisi…’akasema mzee.

‘Sio kweli, huyo aliyekuambia hivyo kakudanganya…hawana deni lolote kwetu,….wenyewe waliondoka hapa na baadaye alikuja Tajiri, tukamalizana naye kwani alikuwa na pesa yake alilipa zaidi, ikabidi tumrejeshee...., hawana deni lolote kwetu mzee….’akasema huyo meneja.

‘Na unajua wapi walipoelekea?’ akauliza huyo mzee akiwa katahayari, hakutajia kuwa itakuwa hivyo, na hakupenda kuulizana zaidi, kwani aliona kuongea hapo, kunaweza kukazua minong'ono miongoni mwa watu, kitu ambacho hakukipenda.

‘Sijui kwakweli, kwani waliondoka kwa haraka…..kama nilivyokuambia, na hatukuwa na haja ya kuwafuatilia…’akasema huyo meneja.

'Basi hakuna shida, nilitaka kujua hilo tu, kama kuna deni nilipe, kama hakuna basi kwa leo nimewatembelea tu, huenda nikaja hapa kwa shughuli nyingine....'akasema huyo mzee, na yule mweneja, akamsindikiza huyo mzee hadi kwenye gari lake.

'Haya mzee, unakaribishwa sana...tunashukuru kwa kututembelea, akasema huyo meneja, wakati gari likiondoka.

Mzee akarejea nyumbani kwake, akiwa amatahayari, hakuamini hayo aliyosikia, hakutaka fahamu yake, ihangaike, na kufikiria mambo mengine mabaya dhidi ya hao akina mama wawili, akajikuta kiongea peke yake kwa sauti.

‘Ina maana hawa watu ni matepeli,…haiwezekani,… mbona hawafanani na watu wenye tabia hiyo,..ni lazima niwatafute…na kama ni kweli nitawaweka ndani, ….au huyo mwanamke ndio tabia yake, na …anaonekana kuwa hivyo….ila Maua hawezi kuwa hivyo…..na mama yake Maua, alisema anafanya biashara,…oh, ngoja, nitawatafuta’akasema na baaadaye aliwaita vijana wake na kuwaagiza wakawatafute Maua na mama yake mdogo, wajue wapi walipo…

********.
‘Jamani tuondokeni haraka, tunatafutwa na polisi…na tiketi hizi hapa nimeshakata, kesho asubuhi na mapema tunaondoka…’akasema mama Mdogo.

‘Tunatafutwa na polisi kwa kosa gani?’ akauliza Maua kwa mshangao.

‘Mzee kaenda polisi, kutushitaki, kuwa tumedanganya, tumemsingizia mimba ambayo sio ya kwake, na ushahidi anao, kaenda kutushitaki kuwa sisi ni matapeli, kwahiyo tunatafutwa na polsi, cha muhimu tuondoke hapa haraka, tukatafute sehemu ya kujificha hadi hapo kesho asubuhi.

Maua, akawa na wasiwasi na maneno ya mama yake mdogo, na kwa vile alikuwa na miadi ya kukutana na mama yake kwa ajili ya kufuatilia maswala ya baba yake, kama yupo hai, au la…., akashauri waende huko alipo mama yake,,

'Haya twende huko huko haraka, kutafaa sana hadi kesho asubuhi....'akasema mama mdogo.

Na kweli wakaondoka kwenye hiyo hoteli nyingine ambayo walihamia baada ya kutoka ile hoteli ya mwanzo, japokuwa hoteli hiyo ipo karibu na kituo cha mabasi, lakini waliona kuwa hapo ni rahisi kukamatwa na polisi....wakaondoka kuelekea kwa mama yake Maua.

Kabla ya kuondoka ikabidi wafike kwa meneja wa hiyo hoteli,ili kuangalia maeshabu yao, walifahamu kabisa kuwa hawadai, lakini mama mdogo, aklini mwake, akajua kuna rejesho litakuwepo, kwani Tajiri alikuwa kalipia kwa matazamia ya kukaa hapo kwa muda mrefu.

'Wewe nenda kanisubiri kwa nje, lakini uwe makini, polisi wasije wakakumata, ngoja mimi nikaage kwa huyo meneja wao, ....siunajau tena sisi tulikuwa watu muhimu sana humu kwenye hii hoteli kwasababu ya Tajiri, itakuwa sio vyema tukiondoka bila kumuaga....'akasema mama mdogo.

Maaua akatoka nje na kutafuta sehemu ya kukaa, akimsubiri mama yake mdogo, ambaye alikwenda moja kwa moja hadi ofisi ya menaja wa hiyo hoteli na kuanza kuongea naye.

'Nimesikia kuwa mnataka kuondoka, mbona haraka hivyo?' akauliza huyo meneja.

'Tunawahi bongo kuna mambo ya kibishara, siunajue tena....'akasema mama mdogo.

'Kwahiyo sasa ....?' akauliza meneja, akikuna kichwa.

'Angalia mahesabu yako, hatutaki kuondoka hapa kukiwa na deni nyuma..', akasema mama mdogo;

‘Nyie hamdaiwi kabisa, Tajiri alikuwa kalipa, na kumbukumbu zinaonyesha kuwa bado kuna pesa yenu hapa, kwani ailipia kwa muda wa….’akawa anaongea huku akiangalia kumbukumbu zake.

‘Tunaomba hiyo pesa iliyobakia….’akasema mama mdogo.

‘Ndio kuna pesa imebakia, tunahitajika kutoa kiasi kwa vile nyie mumekatisha mkataba, kwahiyo kuna pesa yetu imebakia hapa….shilingi…..’akasema huku akichukua mashine ya hesabu kutafuta hesabu iliyo sahihi.

‘Haya ...hii hapa ndio hesabu yenu kamili,....mnadai pesa hiyo niliyoandika hapo, nendeni kule kwa mhasibu mtalipwa kiasi hicho kilichobakia kwa siku zilizokuwa zimelipiwa kwa ziada, karibuni sana…’akasema huyo meneja wa hiyo hoteli.

‘Mambo si hayo..angalau tutakuwa na kianzio…lakini hii pesa haitoshi..sijui niende kwa nani,…’mma mdogo akawa anaongea baada ya kupewa hiyo pesa na Maua, ambaye alikuwa ana mawazo yake, hakuwa akifuatilia mambo ya pesa, akawa yupo nje akimsubiri mama yake mdogo.

‘Ulikuwa unafuatilia nini mbona umechelewa hivyo?’ akauliza Maua.

‘Hujui hapa ni hotelini, huwezi ukaondoka hivi hivi, ni lazima uhakikishe, kuwa huna deni,..unaweza ukafungwa kwa kitu kidogo,…..walikuwa wanadai pesa kidogo, nimewalipa,….twende zetu’akasema.

‘Wandai, mbona nakumbuka Tajiri, alisema kuwa alishatulipia pesa za zaidi ya miezi sita….’akasema Maua.

‘Nimeshamalizana nao,……hakuna shida, wewe twende zetu….’akasema na Maua akamwangalia mama yake mdogo huyo kwa mashaka, akahisi kuna kitu mama yake huyo mdogo anamficha, lakini hakutaka kumuuliza, …wakaondoka

Walipofika kwa mama yake Maua wakakaribishwa kwa furaha, kwani mama huyo alikuwa kawashauri wafenye hivyo muda mrefu, lakini walikuwa hawataki kufanya hivyo.

‘Imekuwaje,..maana niliwashauri toka siku ile, kua mje tukae hapa, maana sisi hapa hatulipi chochote, hii ni nyumba ya kaka yake mume wangu,….’akasema mama Maua.

‘Aaah, tutaongea baadaye, …..’akasema Maua na wakaambiwa kuwa, mume wa mama yake huyo hayupo alishaondoka kupeleka mizigo huko kijijini, kwahiyo kuna nafasi ya kutosha kukaa wote watatu bila shida.

‘Sasa ile safari ya kwenda kuliona kaburi la baba yako, itakuwa imeshindikana…’akasema mama Maua.

‘Wewe niamini kauli yangu,baba yako hayupo duniani….hata hivyo, mimi sipendi wewe uondoke na huyu mama yako mdogo, …bakia hapa tutakwenda wote kijijini..tunaweza kuishi kwa biashara zetu, mbona hakuna shida….’akasema mama yake.

‘Mama nilishakuambia kuwa siwezi kulinyamzia hili, mpaka, nihakikishe kuwa nimempata aliyenipa huu uja uzito, na kwa vile wametuambia kuwa huyo dakitari yupo Dar, nikifika huko cha kwanza ni kwenda kuonana na huyo dakitari…. nikimalizana naye, nitakujulisha, na mengine yatafuata baadaye…’akasema Maua

‘Sawa mwanangu, lakini sitakuwa na raha ukiendelea kuishi na huyo mama yako mdogo,..simwamini kabisa, anaweza akakufunga kwa ajili ya tamaa yake ya pesa, …na hatajali hata kama ikibid kukutoa wewe mhanga,..unaona alivyofanya, huo uja uzito, umetokana na yeye, akitaka pesa,…..’akasema mama yake.

‘Mama usijali, mimi nitakwenda naye hivyo hivyo, hadi hapo nitakapoweza kujimudu mwenyewe…sitakaa naye milele…’akasema Maua.

‘Mwanangu…kuwa makini na huyo mama,….’akasema mama yake, akimwangalia binti yake kwa mashaka.

‘Na sijui kaenda wapi, maana yeye mwenyewe kasema kuwa tusitoke nje, kwani tunatafutwa na polisi…hata hivyo siwezi kumwamini, …ngoja nimpigie simu huyo mzee nimsikie mwenyewe anasema nini…’akasema Maua.

‘Mzee yupi, …mjomba wake Tajiri,…nilishakuambai achana na huyo mzee, sitakubali kabisa wewe kuolewa na huyo mzee, achana naye, …kama ulivyosikia mkewe wake anataka kumrejea, ukiwemo hapo utakuwa ni pingamizi….’akasema mama Maua.

‘Mama…sina mipango hiyo, ila ni kuhakikisha tu kuwa mama mdogo hayalikoroga huko..namfahamu sana mama yangu huyo mdogo..’akasema Maua

********

‘Baba unaona….’akasema binti wa mzee, na mwingine akadakia na kusema.

‘Tulikuambia hawa watu wanaweza kuwa ni matapeli, …walikuja na lengo lao, na kwa vile hawakufanikiwa , sasa wameona watumie mbinu nyingine…’akasema huyo binti mwingine.

‘Mimi sina uhakika na wale akina mama wengine, hasa yule binti na mama yake mzazi,…kwasababu aliyefika hapa ni yule wanayemuita mama mdogo, …’akasema Mzee.

‘Ndio akasema wenzake wameshikiliwa, ….?’ Akawa kama anauliza yule binti.

‘Maua ndiye kashikiliwa, hakusema kuhusu mama yake Maua…hii inanipa mashaak kuwa huenda ni mbinu za huyo mama peke yake.

Na kwa muda huo, mama wa hawo mabinti akaingia, kwani walikuwa na kikao kingine cha familia, na alipofika alionekana kuwa na wasiwasi, akatulia kwanza , na akawa wa kwanza kuongea, akisema;

‘Mzee, wale akina mama washikaji zako wamehamia wapi, maana nimefika pale hotelini hawapo?’ akauliza.

‘Ulikuwa na shida gani na hawo watu?’ akauliza Mzee.

‘Nilikuwa na mazungumzo nao, …nilikutana na yule wanayemuita mama mdogo, akanielekeza hpo hotelini kwao, nimefika hpo hotelini, sijamkuta, na nimeambiwa waliondoka siku nyingi, hawa watu sio matapeli kweli?’ akauliza.

‘Na wewe wamekuingiza mjini nini?’ akauliza yule binti, na mama yake akamwangalia kwa mashala na kusema;

‘Mimi hawawezi kuniingiza mjini…nitawafuatilia hadi huko walipotokea, na ikishindikiana, nitawatumia kitu ambacho hawataweza kunisahau,….kwahiyo mzee hujui wapi wanaishi kwa sasa?’ akauliza huyo mama.

‘Mimi mwenyewe nawatafuta….’akasema na mara simu ikaita….na mmoja wa wale mabinti akaipokea na kujitambulisha;

‘Nani Maua, mpo wapi?’ akauliza, na mzee akasogelea akitaka kuchukua simu aongee naye, lakini yule binti akamzuia kwa mkono.

‘Tuliwaita kwenye kikao hamkuonekana, ila tulisikia kuwa mlifika mkaondoka, kwanini mlifanya hivyo?’ akauliza huyo binti.

‘Ndio kilikuwa kikao cha familia, mkihusishwa na nyie, …’akasema

‘Kwahiyo kwa sasa mpo wapi, maana huko hotelini hamuonekani?’ akauliza.

‘Mnajiandaa kuondoka,…..mbona huko hotelini tumesikia kuwa mlikuwa mkidaiwa?’ akauliza.

‘Ndio alifika mama yako mdogo, akasema umeshikiliwa, na hautaruhusiwa kuondoka mpaka mlipe hilo deni, na mzee akatoa pesa milioni na nusu, akampa mama yako mdogo…..’akasema.

‘Unasema sio kweli, kwahiyo ni kwamba mama yako mdogo alidanganya ili mpate pesa,…huo ni utapeli’akasema huyo binti.

‘Wewe hujui, huyo mama yako mdogo mnaye hapo, ..?’ akauliza

‘Kaenda wapi , maana anatafutwa na polisi, vinginevyo aje arudishe hizo pes, na tuongee vyema,…’akasema

‘Hayupo, ina maana hamkai naye hapo,…?’ akauliza

‘Sasa kwa amani yenu, tunaomba mje, na huyo mama yako mdogo, tuyamalize kifamilia, vinginevyo, ….’akasema.

‘Mumeshakata tiketi ya kuondoka,…kesho asubuhi,….ooh, sasa sisi tutawatumia polisi wawakamte huko huko, mkalale jela,…’akasema huyo binti.

‘Ina maana alifika akasema Mzee kawashitaki kwasababu ya kuwa umemsingizia kuwa una uja uzito wake, kwahiyo ndio akashauri kuwa muondoke haraka, sio kwa vile katapeli,..?’ akauliza.

‘Kwahiyo hilo swala la kodi ya hoteli, hulijui?’ akauliza.

‘Na mama yako yupo wapi?’ akauliza

‘Yeye ana bisahara zake….na yeye hajui lolote?’ akauliza.

‘Oh , kwahiyo huyo mama yenu mdogo ni tapeli, ….?’ Akauliza.

‘Sasa sikiliza,…mimi nitakuja huko ulipo, atayarishe hizo pesa alizotapeli, …..vinginevyo, tutawatumia polisi…’na mama yake akamnong’oneza binti yake akisema;

‘Mwambie na pesa alizochukua kwangu zinahitajika….’akasema.

‘Na pia nasikia kachukua pesa kwa mama yangu, mwambie hizo pesa zote azirejeshe haraka, vinginevyo wote mtalala ndani….’akasema.

‘Hayupo kaenda wapi, …atarudi,…akirudi mpe hiyo taarifa…’akasema na wakakata simu.

‘Mnaona , niliwaambia kuwa hawa watu ni matapeli wa mjini, huenda hata huko Dar, wametimuliwa, …’akasema mama wa hawo mabinti.

‘Inavyoonekana tapeli na huyo mama yao mdogo,..lakini kama wanamfahamu kuwa ana tabia hiyo, nab ado wapo naye, watajikuta wote wakiingia matatani…ngojeni mimi niende huko nikakutane nao,…’akasema huyo binti na mwenzake akasema wanaondoka wote.

‘Hata mimi nakwenda huko huko nikakutane nao…’akasema mama yao.

‘Hapana wewe kaaa hapa na baba, na tunakuomba muongee kwa amani, na kama tukirudi hapa tukakuta hali ya baba imebadilika,….hatutakusamehe mama…’akasema binti.

‘Hivi nyie mnaniona mimi ni mtoto mdogo, baba yenu nimeishi naye miaka mingapi, mkazaliwa nyie, hadi mumefikia hapo, leo hii nishindwe kumhudumia….kama hamuamini, basi mmoja abakia hapa na mimi tuongozane huko ….’akatoa ushauri.

‘Ni kweli, wewe nenda na mama yako, mdogo wako abakie hapa…’akasema mzee.
Wakakubaliana hivyo, na wakaondoka kuelekea huko walipoelekezwa na Maua.

*********       

Mama mdogo alikuwa kasimama mlangoni, pembeni kabisa, na alikuwa kajifunika khanga, kiasi kwamba usingeliweza kujua ni yeye, na alipoona gari linatoka, akasogea mbali kidogo, akajaribu kuchungulia lela gari , kama ataona ni nani wapo mle ndani , hakufanikiwa.

Baadaye alikwenda hadi pale mlangoni, na akakutana na mlinzi akamuuliza;

‘Namuulizia mzee yupo ?’ akasema mama mdogo akitabsamu, huku akijirembua kwa yule askari, na yule askari, akamwangalia kwa mashaka.

‘Kwani wewe nani?’ akauliza huyo mlinzi huku akiwa kasimama mlangoni.

‘Mimi ni mmoja wa wafanyakazi wa Mzee kwenye kampuni yake ya kule mjini Arusha, niliongea naye kwenye simu, kuwa nitakuja hapa kuonana na yeye….’akasema.

‘Mzee yupo, lakini mpaka nimuulize, na …hebu subiri, ….’akashika simu na kuanza kupiga, na akiwa kashikilia simu, akamuuliza mama mdogo;

‘Jina lako ni nani….?’ akauliza.

‘Wewe mwambie, mmoja wa wafanyakazi wake wa Arusha, kwani anawajua wote majina, wewe mwambie hivy hivyo tu ataelewa….’akasema na yule mlinzi, akaondoa simu sikioni na kumwangalia yule mwanamke..’akasema huyo mama.

‘Usinitania wewe mwanamke…siwezi kumwambia ni lazima atataka kujua jina lako,…kama kweli una nia ya kumuona nipe jina lako …’akasema huku akimwangalia mama mdogo kwa makini, na mama mdogo, akafanya kama alivyofanya mwanzoni, akajirembesha, na kutabasamu, huku akisema;

‘Hivi wewe unanionaje mimi….?’ Akauliza.

‘Sikiliza…mimi nipo kazini hapa, sina muda wa kupoteza…’akasema na akawa anafunga mlango.

‘Au kama ana kikao nitakuja baadaye..’akasema mama mdogo.

‘Hana kikao, maana sasa hivi wametoka mkewe na binti yao, humo ndani kabakia yeye na binti mdogo…kama ukinipa jina lako nitampigia na kama yupo tayari, atasema,….sasa hivi hapokei wageni bila taarifa….’akasema yule mlinzi akiwa bado anamtizama huyo mwanamke.

‘Oh, vyema, …basi mwambie ni mimi …mama mdogo’ukisema hivyo tu, ataelewa na yule mlinzi aliposikia neno hilo `mama mdogo ‘akasema;

'Mama mdogo,….au ndio wewe….nasikia umemtapeli mzee’akasema huyo mlinzi.

‘Wewe ni mgeni hapa nini,..ni nani kakuambia kuwa nimemtapeli mzee,..mbona watu wanasikia manenoo ya mitaani na kuyavumisha bila ushahisi,….ndio maana nimekuja kuongea na mzee kukanusha huo uvumi…..’akasema mama mdogo.

‘Kama wewe ndioo huyo mama mdogo, kuanzia sasa upo chini ya ulinzi, ….sogea huku ndani’akasema huyo mlinzi.

‘Wewe ni askari kweli, unaifahamu kazi yako vyema wewe ….unamweka mtu chini ya ulinzi bila hatia, hebu niambie nimefanya kosa gani, …nimekuambia mama mdogo,…ina maana ndugu wa mzee humo ndani wakija kwa jina hilo la mama mdogo wote ni  sawa na huyo mnayemtafuta…’akauliza mama mdogo.

‘Mimi sijui hayo, ila nimesikia kuwa kuna mama mmoja anatambulikana sana kwa jina la mama mdogo, kamtapeli mzee….’akasema huyo mlinzi.

‘Sikiliza wewe askari usiyeenda shule, kwanza  nitakuchukulia hatua kwa kunisingizia kuwa mimi ni tapeli,….na hivi wewe unanifahamu vyema, huko Dar, polisi wote waaniheshimu, …..mzee mwenyewe akiniona hapa, utamuona akitamani kunipigia magoti, kwa jinsi anavyoniheshimu..’akasema mama mdogo na yule mlinzi akanywea na kusema;

‘Sasa kwa usalama wako subiri hapo, nimpigie mzee simu….nitamwambia hivyo hivyo kuwa wewe ni mama yake mdogo, na ole wako unidanganye…..’akasema na kuanza kupiga simu tena kwa mzee, na huko ndani akaambiwa amruhusu huyo mama aingie,…

‘Haya sasa unaona…wewe askari wewe,…ole wako, sizani kama kazi hii unaiweza…’akasema mama mdogo akiingia ndani, na kuelekea kwenye lile jengo, akafika kwenye mlango mkubwa, akakuta upo wazi, na akaingia ndani. Akiwa ndani alisogelea kile chumba maalumu cha mzee,na  alipofika karibu na ule mlango ambao ulikuwa nusu wazi, akasikia ndani, sauti ya binti ikiongea na simu;

‘Nawaomba hawo polisi wafike haraka , maana huyo mama yupo hapa….’mama mdogo akasimama na akawa kama kaganda, …halafu, akaanza kurudi kinyume nyume, hadi mlango wa kutokea, akageuka kwa haraka na kuanza kuondoka, na mara, …akajikuta akiangaliana na askari ….askari wa kike….


NB: Muda..hautoshi,ooh, inatosha kwa leo. Tupo pamoja

WAZO LA  LEO:Usiwe na tabia ya kudanganya,..hata kama una shida namna gani, ni vyema ukawa mkweli, kwani kwa kufanya hivyo, utaweza kujijenga sifa njema kwa watu. Na sifa njema, tabia njema, za umainifu,ukarimu, upendo kwa watu, ni mtaji katika maisha yako.

Ni mimi: emu-three

No comments :