Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, March 4, 2013

Uchungu wa mwana Aujuaye ni mzazi-67




Tajiri, aliondoka kituo cha polisi ambapo walikuwa wameshikiliwa, baada ya taratibu za dhamana kukubaliwa, kwa ubinadamu alitaka kumdhamini Malikia wa Marerani, lakini masharti yake yalikuwa magumu zaidi, kwahiyo akaona ni bora arudi nyumbani.

‘Huyu mtu ni hatari, hatuwezi kumkubalia dhamana, hadi hapo kesi yake itakapofikishwa mahakamani, yeye na mwenzake ni viongozi wa kundi haramu, ….hawaaminiki, ’mkuu wa polisi wa eneo hilo akamwambia.

‘Lakini dhamana ni haki ya raia….yeye ni mtuhumiwa tu,..’akajitetea Tajiri.

‘Wewe humjui huyu mtu vyema,…tafadhali achana naye,….tumewachunguza kwa miaka mingi, na tuna ushahidi wa kutosheleza, …lakini hali ilivyo, ….tuna wasiwasi mkubwa kuwa ana watu wake wanamlinda, na akipewa mwanya, ….hata huo ushahidi unaweza ukaharibiwa…’akaambiwa na huyo musika wa hiyo kesi.

‘Kwahiyo unanishauri nini….?’ Akauliza Tajiri.

‘Ushauri wangu mkubwa na wewe kuangalia kesi yako, kwani hata wewe unahusika kwa namna moja hadi nyingine, japokuwa tuliamua kukutumia kama chambo,…tafuteni wakili, kwani wakili wenu huyo ni mmoja wa watuhumiwa, na ni kiongozi wa kundi, japokuwa hakutaka kujionyesha wazi wazi….huyo tutapambana naye’akasema huyo mkuu, akionekana kuwa na wasiwasi.

‘Basi ngoja nitaangalia nini cha kufanya…..maana najua yote sasa yapo mikononi mwangu, kuondoka kwa mjomba ni pigo kubwa kwangu….’akasema ilionekana dhahiri kuwa mkuu wa kituo hicho hataweza kutoa dhamana kwa Malikia na mwenzake, wakili wa mzee wake, ndipo akaona ni vyema kurudi nyumbani kwanza ili ajue taratibu za huko zinaendeleaje.

‘Kila –laheri….’akasema huyo mkuu, huku akiangalia makabrasha yake, na alipohakikisha kuwa kaondoka, akachukua simu yake na kuongea na watu wake.

Tajiri akiwa njiani alikuwa na mawazo mengi, kwanza alikuwa akimuwazia mjomba wake, akilini mwake, alijua keshampoteza, mjomba wake hayupo duniani, na kwahiyo yeye ndio kaachiwa majukumu yote ya kuendeleza miradi na kuhakikisha haki za familia zinalindwa.

‘Mbona itakuwa kazi kubwa sana, ……’akajisema akilini, na akakumbuka kuwa ni muhimu akawasiliana na watoto wa huyo mzee, ili kama ikiwezekana warudi nyumbani, na kuhudhuria mazishi ya baba yao,..

Lakini mbona nilisikia Maua akisema `hajafa…..alikuwa na maana gani, haiwezekani, kwa jinsi ilivyokuwa, mjomba hayupo tena duniani…ngoja niwapigie simu watoto wake….’akasema huku akichukua simu yake na kutafuta jina la mmoja wa watoto wa mzee, akajaribu kupiga zile namba, lakini hali ya mitandao ikagoma, alijaribu majina yote hakuweza kufanikiwa kumpata hata mmoja,…

‘Nitawapigia nikifika nyumbani….’akasema na baadaye akafika nyumbani.

Aliingia ndani, na moja kwa moja akaingia kile chumba maalumu cha mjomba wake, na ile hali ya kumbukumbu, ya kuwa mjomba wake, alikuwa akiishi humo ikamfanya asite kufungua mlango, akarudi nyuma na kusimama. Akawa anamuawaza mjomba wake,….lakini kuna hali ilikuwa haimpi uchungu sana…akaguna,….

Akauosogela mlango, na kushika kitasa cha mlango, ili kuufungua mlango,wakati huo alishajipa moyo, na kusema kimoyomoyo, kuwa sasa yeye ndio anatakiwa kuwa kiongozi, kwahiyo anatakiwa kuwa jasiri, akawa kama kafumba macho, akazungusha kitasa na huku akivuta tambo za kishujaa...na kitasa kikazunguka na kujivuta kuuingia ndani kama vile anausukuma mlango…..

Akajikuta akipigana kikumbo na mama mmoja aliyekuwa akitoka, na yule mama akasema `oh, samahani..’ na wakati huo mkoba wa yule mama aliokuwa nao mkononi ukadondoka. Kwa haraka akainama kumookotea huyo mama mkoba wake, na kumbe yule mama naye alikuwa kainama kuuokota, wakajikuta wameshikilia ule mkoba, na ndipo akapata nafasi ya kuinua uso, …

‘Huyu mama anatokea wapi, au ndio wenyeji wameshaanza kuja kwenye msiba, lakini kwanini waingie huku ndani…?’ akawa anajiuliza wakati anainua kichwa kutaka kumwangalia vyema huyo mama,

Wakaangalia….na huyo mama akageuza uso haraka na kuanza kuondoka, …Tajiri moyo wake ulishituka kidogo,..hakujua kwanini….akajaribu kukumbuka,..akasimama pale mlangoni na huku akimwangalia huyo mama akiondoka kwa haraka, na yule mama akageuka ….wakaangaliana….

*********

Mama Maua, akili yake haikuwa safi, ….alijaribu kuyawaza yote yaliyotokea wakati akiwa ndani ya boda boda, akielekea huko alipokuwa mume wake, hakupenda kuchelewa zaidi, kwani biashara ndio kazi yao, ndio kazi yao na mume wake, na walihitajika kuchukua mzigo ambao wataondoka nao kesho yake, hadi huko kwao Singida…

Kila alipomuwazia binti yake, alijiona kama anazidi kumtelekeza binti yake, lakini kwa hali ilivyo, asingeliweza kufanya lolote, kwani binti yake alishakataa kuondoka naye, …akakumbuka jinsi alivyojaribu kumashawishi, bila mafanikio…na hapo akafumba macho, huku akilini akikumbuka jinsi alivyokuwa akiongea na binti yake;

‘Maua hebu nieleze kiukweli, ina maana ulifikia hatua hiyo, bila aibu ukalala na huyo mzee..….hadi ukapewa uja uzito na huyo mzee, huoni aibu mwanangu, kulala na mzee kama huyo, sawa na babu yako….unachotaka kwake ni nini..ndio huo utajiri….’akawa analalamika mama

‘Mama nakuomba utulizane na haya mambo….naomba usiyaingilie yatakuja kukuumiza kichwa chako bure,….’akasema Maua huku akikwepa kumuangalia mama yake usoni.

‘Mimi ni mama yako,….mimi ndiye niliyakulea, na mabaya yakitokea nahiajika kuwajibia,..mwanangu, sikumbuki kukulea katika tabia ya namna hiyo…unakumbuka nilivyokulea, na nilikuasa wakati unaondoka kuwa , usipende kisicho jasho lako, usiwe na tamaa, epukana na vishwawishi hasa vya wanaume, kama ana mali yake, ni mali yake, chuma na tafuta chako kilicho halali…mwanangu,nimekosea wapi mwanangu….,hadi ufanya huo uchafu,…’akalalamika mama yake.

‘Mama haya yaliyotokea sio kwasababu ya ulezi wako, mama umenilea vyema kabisa…wala usijilaumu kabisa,…hata hivyo mimi sio mtoto mdogo tena….najua nini ninachokifanya…’akasema Maua akijiskia vibaya, hakupenda kabisa mambo yaliyotokea juu yake yamuhusishe mama yake, japokuwa safari yako walipotoka Dar, ilikuwa kwenda kwake.

Kwenda kwa mama yake, ilikuwa kwa lengo jema, kuwa amepata mume, na huyo mwanaume ajitambulishe kwa wazazi wake, kama utaratibu ulivyo, na hakujua kuwa kutakuwa na vikwazo vingine,..

‘Mwanangu hata kama unajiona umekuwa mkubwa…bado hujawa mkubwa, usijidanganye,….kama ungelikuwa na akili za utu uzima, usingelifanya hayo uliyoyafanya…..hayo yatakufanya uishi maisha yasiyo na amani…jamii itakutizama kwa jicho baya, kila mtu atakuwa na lake la kukuongelea…’akasema mama yake.

‘Mama haya yaliyotokea mimi sikupenda,  kiujumla yote yaliyotokea, hayakutokea kwa matakwa yangu….kama kuna mtu wa kumlaumu, …basi umlaumu ndugu yako,…yeye ndiye aliyeniingiza kwenye masahibu yote hata…na mama naomba usijiweke katika msononeko,..haya nitayamaliza mwenyewe….usiwe na shaka….vyovyote iwavyo, ni lazima haki ipatikane, ……’akasema Maua.

Mama aliposikia hivyo, kwanza aliinama, akilini akawa anajijutia, akijua kabisa yeye ndiye aliyemtoa mtoto wake kwa ndugu yake , na ilihali anajua tabia mbaya za huyo ndugu yake, …japokuwa waliishi pamoja walipokuwa wadogo na walielewana, lakini ndugu yake huyo alikuwa na tabia ya ubinafasi hasa kwenye pesa.

‘Namfahamu sana ndugu yangu huyu, naijua tabia yake ya utotoni, lakini sikujua kuwa ataendelea nayo….ndio maana hakuweza kuishi na mwanaume wake wa kwanza…aliachika, na kila aliyejaribu kuishi naye, hakuweza kumvumilia…..sikujua kuwa namtelekeza mwanangu…..’akawa anaongea huku machozi yakimlenga lenga, akageuka akitaka kutoka nje, akasema;

‘Kwanza yupo wapi huyo mama yako mdogo, nasikia mliongozana naye kuja hapa…., nataka nionane naye….oh, simu, nahisi ni mume wangu ananiita..’akakatisha maneno yake , pale simu yake ilipolia. Na kweli alikuwa mume wake, akasikiliza huku bado akiangalia huku na kule kama anatafuta kitu,…alimsikia mume wake akimsisitizia kuwa anahitajika haraka,  kwenye maswala yao ya bisahara.

‘Ninakuja mume wangu….’akasema na kukata simu, akamwangalia Maua.

‘Mwanangu, mimi nimefikia uamuzi kuwa tunaondoka pamoja, sitakuwa na amani nikikuacha tena hapa au nikikuacha uendelee kuishi na mama yako mdogo, ….tuondoke zetu, hatutashindwa kuishi pamoja, na hata kama una uja uzito, tutajitahidi tutaitunza hiyo mimba utajifungua, na mtoto tutamlea wenyewe, ….nimekulea wewe …sitashindwa kumlea mjukuu wangu, au …?’ akasema mama, hakutaka kusikia mengine zaidi, alikuwa yupo radhi waondoke naye kuliko kumuacha hapo akaolewa na huyo mzee.

‘Mama wewe ondoka,….mimi sitoki humu hadi kieleweke,….wao ndio walioniharibia maisha yangu, na kwa hilo, itabidi nihakikishe haki zangu zote zinapatikana, sitajali umri….wala …sijui kitu gani…’akasema Maua.

Mama Maua akatulia, akamwangalia mwanae, na baadaye akasema;

‘Haya mwanangu, ….kama umeamua hivyo, ….siwezi kukulazimisha, ila naomba, tuwasiliane ili nijue imafikia wapi…’akasema mama na kumgeukiwa yule mzee, safari hii, alimwangalia kwa jicho baya, hakutaka hata kusema naye,lakini yule mzee, akasema kwa sauti ya taratibu;

‘Nakuomba usiwe na wasiwasi na binti yako,…yupo mikono salama,… mimi nitahakikisha haki zote za huyu binti yako zinapatikana, mimi sikujua hilo la ujazito, nahitajia kuongea naye zaidi, …hata hivyo, kama ana uja uzito, nipo tayari kumuhudumia, na hata mtoto nitamlea kama mwanagu…’akasema huyo mzee.

‘Utamlea kama mwanao…au ni mwanao..hiyo `kama’ ina maana gani…hata kama u mzee, lakini kama umeshamuharibia maisha yake, kwa kumbebesha huo ujauzito, ujue huyo ni mwanao….sasa hiyo `kama’ inatoka wapi?’ akauliza mama Maua.

‘Inahitaji niongee naye, ….’kabla hajamaliza simu ya huyo mama ikaita tena, na yule mama akaipokea na kusema `nakuja….’ akakata simu na kuanza kuondoka,…

‘Mama usiwe na wasiwasi, haya nitapambana nayo, ….naomba usiyaingilie…’akasema Maua.

‘Mwanangu, ..uwe makini , hasa kwa huyo ndugu yangu-mama yako mdogo, anaweza akakutumbukiza shimoni,namfahamu sana yeye anathamini sana pesa, na yupo tayari kufanya lolote kwa ajili ya pesa, hatajali kuwa wewe ni mtoto…mimi nakuomba, ukiona vipi rudi nyumbani,…sisi biashara inachanganya, tutasaidiana…’akasema mama yake.

‘Huko sikanyagi kabisa, hadi hapo, nitakapohakikisha mambo yangu yamekwenda shwari,….hadi hapo nitakapohakikisha nimejifungua, …..na haki yangu imepatikana, na hili ndilo lililonileta huku, itakuwa nimefanya nini kufunga safari yote hadi huku halafu niondoke bila kujua majaliwa na masahibu haya…hata kama wana kesi,….lakini najua huyu mzee, ni mzazi wake….’akasema Maua.

‘Haya kila-laheri mwanangu,….maana naoana unanichanganya, na wala sijui ni nini kinachoendelea kati yako na mama yako mdogo, na inavyoonekana hutaki kunihusisha kwenye mambo yako, …..na mama yako mdogo, haya…mimi naondoka, ….’akasema mama Maua na kufungua mlango.

Maua alipomuona mama yake anaondoka, akashika shavu, mkono ulikuwa kidevuni, akawa kazama kwenye mawazo , …na hata hivyo moyoni aliona ni bora iwe hivyo, kwani kwa hali ilivyo, mama yake atakuwa kaondoka na fikira nyingine tofauti, na jinsi mambo yalivyo….yeye aliona ni bora iwe hivyo,…hadi hapo muda muafaka utakapofika….akagueza macho kumwangalia yule mzee, na yule mzee, alikuwa kaangalia nje,…kwa kupitia dirishani, alionekana kuwa na mawazo yake.

Ilikuwa kipindi hicho mama Maua anaongea akimuaga mwanae huku anatembea upande upande, huku akiwa anajaribu kugeuza kichwa kumwangalia binti yake, huku anaangalia huko anakokwenda , na alipokaribia kitasa cha mlango akatulia, akijua akitoka hapo, keshamuacha mwanae, na hajui ni nini majaliwa yake, …akahisi kitasa kikizunguka, akageuka…..na mlango ukafunguka, hakutaka kuangalia tena kwa binti yake, akatoka kwa haraka na hapo akajikuta akipigana kikumbo na jamaa mmoja aliyekuwa naye anataka kuingia.

‘Oh samahani..’akasema mama Maua, huku akiokota mkoba wake uliokuwa umedondoka chini, baada ya kupigana kikumbo na huyo jamaa. Na kwa muda huo akili yake ilikuwa ikiwaza mengi, na aliona ni vyema kumuwahi mume wake huenda wakapeana mawazo , huenda wakashauriania, wakaja naye ili kumshawishi binti yao waondoke naye.

‘Huyu anaweza akawa mmoja wa watoto wa huyu mzee….’akasema huku akiinama kuokota mkoba wake, na kumbe huyo jamaa na yeye alikuwa kainama kuuokota huo mkoba, na hapo akajaribu kuinua uso kumwangalia, wote wakajikuta wameshikilia ule mkoba, na wakajikuta wanaangaliana.

Mama Maua akili yake haikuwa hapo, alimwangalia mara moja, na kuuchukua mkoba wake, na kuanza kuaondoka kuondoka, ….alipofika mbele akageuka kumwangalia yule jamaa tena, na kumbe yule jamaa na yeye alikuwa kasimama pale mlangoni, akimwangalia, wakajikuta wanaangaliana…

********

NB: Kidogo kidogo tutafika, japo kwa kuchechemea.

WAZO LA LEO: Kunapotokea tatizo, wengi hukimbilia kunyosheana vidole,…hata kama mmojawapo anajua kuwa ndio yeye katenda hilo kosa, sio vyema,…na sio sahihi, cha muhimu ni kutafuta njia ya kulitatua hilo tatizo kwa pamoja,….na huenda ikaleta heri na mshikamano kutokana na hilo tatizo.

Ni mimi: emu-three

6 comments :

Yasinta Ngonyani said...

Hapa pana noga kweli ...tupo pamoja ndugu wangu..Kazi nzuri kwelikweli...Wazo la leo bonge la ujembe nimependa mno.

Anonymous said...

Hello There. I discovered your blog the usage of msn. This is an extremely well written article.
I will be sure to bookmark it and return to learn more of your useful information.
Thank you for the post. I will definitely comeback.

Here is my website :: mouse click the up coming website page

Anonymous said...

My brother ѕuggesteԁ I might like this wеb ѕіte.

He waѕ entirеly right. Тhis post аctually mаdе mу ԁay.
You cаnn't imagine just how much time I had spent for this info! Thanks!

My webpage: http://www.glowingcasino.com
Also see my web site - http://www.glowingcasino.com

Anonymous said...

Pleasе let mе knoω if уou're looking for a writer for your blog. You have some really great posts and I feel I would be a good asset. If you ever want to take some of the load off, I'd absolutely
loѵe to ωrіte some cοntent foг уour
blog іn eхchange fοr а link back to mine.
Please blast me an е-mail if interesteԁ.
Regards!

Visit my homeρage casinoer

Shalom said...

Hongera sana unaenda vinzuri napenda sana.

emuthree said...

Nashukurini nyote kama tupo pamoja,...na nitafurahia kama tutakuwa pamoja, hadi mwisho wa kisa hiki,....kuna mengi nimefunika, lakini kisa kinafikia ukingoni,...TUPO PAMOJA