Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, February 8, 2013

Utangulizi wa kisa kipya -WEMA HAUOZI
   ‘Dereve wodo wado, chukua juu kwa juu….’ Hii ni sauti ya kondakta wa mabasi yatokayo Msasani hadi gongolamboto, ni kawaida yao ya kutokusimama kituoni, kwani abiria wao ni wengi, na hawana haja ya kupiga debe, ….

Kwa hali kama hiyo ya `juu kwa juu…’ wanaoweza kudandika hayo mabasi wengi ni vijana, wazee na akina mama hupata shida sana,…na inawalazimu wapande hayo mabasi wakati yakipita kwenda Gongolamboto,, walipe nauli ya kwenda huko na kurudi nalo, wanaitwa `kegeuza nalo.

Hayo ndo maisha ya asubuhi na jioni ya wakzi wa eneo hili,..ili uwahi kibaruani, au kuwahi kwenda kuhangaika kutafuta riziki yako na huenda ili uipate inabidi kuelekea maeneo hayo, inakubidi uamuke saa kumi alifajiri , na unarudi saa tatu usiku,…..kiasi kwamba kwako unapoishi, unajiona mgeni kila siku.

‘Juu kwa juu, ndio maisha yetu siku hizi, kila jambo, lazima liwe hivyo, hata biashara, au makubaliano ya biashara maofisini, bila `cha juu’ hutajafanikiwa,….ukiona mabosi au watu wa kitengo cha mauzo, wakifukuzia jambo, unaweza ukazania kuwa hawa watu wanawajibika kweli, kwa manufaa ya kampuni yao, lakini ukiuliza zaidi utagundua kuwa ndani ya hicho wanachokifukuzia kuna `cha juu chao’

Hata siku hizi ukienda hospitali, ili mgonjwa wako atibiwe hataka, lazima uwe na cha juu, muwezeshe yule unayeona atafanikisha hilo jambo lako, ili faili lifike kwa dakitari haraka, na kama mgonjwa wako kalazwa, docta aweze kumtembea mara kwa mara…ukitaka iwe hivyo, mkono wako usiwe mnzito,…..hayo ndio maisha yanatotuzunguka.

Hata ukienda kimtaifa, angalia kwanini mataifa makubwa yanavamia sehemu, na hata kupiga vita, angalia kwanini wakubwa wa mataifa hayo wanatembelea nchi fulani mara kwa mara , sio bure, `kuna cha juu huko…’

Wakati nayawaza haya, nikamkumbuka babu na bibi yangu ambao sitawasau kamwe, na mola awalaze mhala pema peponi huko walipo, babu na bibi walipenda sana kutuasa hasa pale wanapotuona tunahamanika na jambo fulani, au akituona tunagombea kitu kidogo, au tukikwepa kuwajibika, kwa kutegeana, kila mmoja akimtupia mwenzake lawama kuwa yeye ndiye anayestahili kufanya.

Nakumbuka siku moja, babu alituona tukibishana na kutegeana...na ndio akaanza kutuasa huku bibi akiwa pembeni.

‘Wajukuu zangu, kama mngelijuwa thamani ya kujitolea msingetegeana, na kama mngelijua athari ya kupupia, na kutaka ziada, msingelipenda hata siku moja kula au kupata jambo bila kufikiria uhalali wake. Sogeeni hapa niwape mambo yajayo….’akasema babu.

‘Babu naye bwana, badala ya kutupigia hadithi, unataka kutuambia mambo yajayo….’akalalamika kaka yetu. Na sisi wengine tunaomjua babu, kuwa akiwaita kwa jambo, kuna jambo ndani yake, anaweza aakzunguka, lakini mwisho wa siku atatoa kisa kizuri…ambacho baadaye nimegundua kuwa ni hazina kubwa ya maisha yetu.

‘Sikilizeni wajukuu zangu, maisha ya kuhamanika, na kutamani, hata kile kisichokuwa chako, ni hatari, ni sawa na kujaza gunia, vitu vingi kwa wakati mmoja bila kujali kuwa vingine vitaharibika au kuharibu vingine,….’akatulia kidogo kutafakari jambo.

‘Ngoja niwape siri ya kufanikiwa katika maisha, …ukiijulia hiyo, hutahaangaika kamwe, na moyo wako utakuwa wa kurizka na kuwa tajiri, hata kama huna mali nyingi….’akasema babu.

‘Utajikuta unaishi maisha ya raha, …..kama tajiri, hata kama huna kile alicho nacho tajiri, maana unaweza ukamuona mtu ni tajiri, lakini hana raha,…..usishangae’akasema na kutuangalia akijua hapo hatkuelewa kitu

‘Haiwezekani, ina maana gani sasa kuitwa tajiri, uwe na mipesa, magari, nyumba na kila kitu cha kifahari, na bado usiwe na raha?’ akauliza ndugu yetu mmoja ambaye ni mdadisi sana.

‘Kwasababau utajiri wake, aliupata kwa kupupia, aliupata kwa kulimbikiza vya halali na visivyo vya halali, mali yake ina jasho la watu, ambalo lipo mikononi mwake, na jasho hilo linamuandama, na matokeo yake, ndio hayo,….moyo wake hautulii, na kwa jinsi alivyojijenga maisha yake, haweze hata kukumbuka hilo, kuwa utajiri wake, una ziada za watu, na angelikumbuka hilo, akazitoa hizo ziada za watu, hangehangaika kamwe…angeliishi kwa raha mstarehe…..lakini wapi, maisha ni juu kwa juu, kama huwezi kudandia unaachwa na basi….’akatulia.

Tulicheka, na hadi hapo hatukuwa tunajua ni nini msingi wa maneno yake hayo,…nimekuja kuyagundua hivi sasa….babu huyo akaendelea kusema;

‘Niwaambia siri moja ya maisha ….siri ya jinsi ya kufanikiwa katika maisha yenu ya baadaye,….?’ akatuuliza na sisi tukasema

‘Tuambie babu..’

‘Mfano umepita njiani ukaona mwiba, upo kati kati ya barabara, utafanyaje?’ akatuuliza babu.

‘Nitauruka huo mwiba , na kupita na safari zangu….’kaka akasema

‘Nitausogeza pembeni ili usinichome, nipite, ili niwahi nisije nikachelewa kama nimetumwa…’akasema mwingine.

‘Unaona hapo kila mmoja anachojali ni yeye, ….apite, hajali mwenziwe anayekuja nyuma, hajali kuwa kuna wenye matatizo ya macho hawataona huo mwiba, wapo watoto….

‘Ndivyo maisha yalivyo, kila mtu anataka apate, afaidike zaidi, awahi afike huko anapotka kwenda….hakuna anayejali kuwa huenda yeye anahitaji kufanya jambo, ili na mwenzake apate…..kuna watu wengine wanastahili kupata riziki zao kwa kupitia watu wengine…lakini kwa uchoyo wetu, hatutaki kuzitoa hizo  riziki , hatutaki kujitolea,... hebu niambieni wagonjwa, mayatima, na wasiojiweza riziki zao zinapatika wapi kama sio kwa kupitia kwa watu wengine….sio hao tu, hata wale wanaojiweza, wengine wanapata kwa kupitia wengine…..

‘Tunatakiwa tujitolee, tusitegeane, ili tuwezekeze kwenye riziki zetu, na tukifanya hivyo, tutapata , tutafaidiki,na muda wote , mioyo yetu itakuwa na amani……’akaendelea babu.

*******

Nilipokumbuka hiyo kauli ya babu ya `kujitolea kwa ajili ya watu wengine’ nikamkumbuka jamaa mmoja wakati tukiwa shuleni.Jamaa huyo alikuwa akipenda kujitolea sana, hadi tukamuita jina la Valmeti, kwa sasa tunapenda kuwaita wa namna hiyo `jembe’

Jamaa yangu huyo, alikuwa akipenda kujitolea na kuwa mbele kwa jambo  la kujitolea, tofauti na wengine, kama ujuavyo `utoto’ hulka ya kutegeana kwenye kazi haichezi mbali. Lakini mwenzetu huyu, hata siku moja hakupenda kabisa kutegea, akiona mnasita kufanya jambo fulani, yeye husema’`ngoja nifanye mimi, niachieni nifanye mimi….’

‘Valimenti hilo…’basi tunamshangilia, na y eye bila hiyana, avua shati lake na kubakia kifua wazi, na atalifanya jambo hilo huku wenzake tupo nyuma tukimwangalia na kukonyezana, na hata kuelekeza, `fanya hivi, sogeza kule,….na wengine hata kumuona ni `mjinga au anaipendekeza vile’ lakini kumbe mwenzetu alikuwa na siri yake, siri iliyojaa hekima ndani yake, na hekima hiyo aliipata toka kwa usia wa babu yake.

Tatizo hivi sasa, hatuwajali wazee, babu zetu na bibi zetu, ….watu wanawageuza babu na bibi, kuwa sio wanadamu wanostahili kuishi tena eti wamekula chmvi nyingi, na wengi wakiwaona wazee hawa, na mabadiliko yaliyopo kwenye miili yao, macho kubadilika rangi , hukimbilia kuwaita `wachawi..’ au vigagula…ni kama vile watu wa Dar walivyo sasa hivi, wakiona paka wanampiga, ukiuliza kwanini, wanasema;

‘Wanga hawa….’

‘Jamani paka toka lini akawa mwanga,…ni utaalamu gani huo wa kisayansi, uliowawezesha hawo wachawi wakaweza kugeuka kuwa paka, kama ni hivyo, mbona tusiwezeke kwenye huo utalaamu, ili tuweke rekodi duniani, na huenda tungelitajirika kwa ugunduzi huo, maana mnaweza kujigeuza mtakavyo, kwanini tusiwe matajiri…..

Sasa imefika hatua wazee wetu, hazina ya hekima, baraka ya dunia, tunawaita `vigagula, wachawi, tunajisahau kuwa , ni swala la muda tu, kesho na kesho kutwa, na wewe utakuwa kama huyohuyo babu au bibi….hakuna ujanja hapo.

*********
‘Mjukuu wangu, unaona maisha uliyoishi, huna baba, baba yako alikukana, akasema wewe sio mtoto wake, kampa mama yako uja uzito, na baadaye akadai kuwa sio yeye peke yake, huenda mimba hiyo sio yake,.....haya mama yako akalea mimba hiyo peke yake, ukazaliwa, sura haikopeshi, na bado akakuna….’akawa anamsimulia babu yake na yeye alikuwa akinisimulia mimi hayo aliyosimuliwa na babu yake….

Hiki ni kisa kingine kifupi kinachokuja, ambacho kitafichua siri ya mafanikio, ambayo haitumii nguvu, haihitaji mihamaniko, haihitaji maisha ya `juu kwa juu’ ….ni kisa chenye siri  kubwa sana na ni moja ya usia wa babu na bibi zetu, tunawanyanyapaa….

Kitaitwa `WEMA HAUOZI.....'
 
Tumuombe mungu atujalia niweze kukusanya matukio yote ya kisa hiki, ili kisiwe kirefu sana.

WAZO LA LEO: Kila chumo unalolipata ukumbuke kuwa ndani yake kuna sehemu isiyo halali yako, kuna sehemu ya wazazi wako, kuna sehemu ya maskini na wasio jiweza, ukiweza kuliwazia hilo na kutoa sadaka, au fungu la kumi, na kuwakumbuka wazazi wako, kwa hicho ulichokipata hata kama ni kidogo, utafanikiwa sana katika maisha na riziki yako itakuwa na baraka

IJUMAA NJEMA.

NB: Tunatarajia kuhitimisha kisa chetu cha `Uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi…’ na huenda tumeruka sehemu, au kuna sehemu hazikueleweka vyema , tunaomba maoni yenu, ili hitimisho liwe la kukidhi haja ya kisa chenyewe…
Wazazi mpooo! Mbona kimiya, au mambo ya Facebook yanawachanganya…hakuna shida tupo pamoja. Na hata kama sio mzazi kwa sasa, lakini tunatarajia kuwa wazazi, kisa hicho kilikuwa ni sehemu ya kukumbushana, kutokana na yalimtokea Maua, na kuwatokea wahusika wengine ndani ya kisa hicho, ,mengi tumejifunza, ninachoomba ni kuwa tushirikiane, kulea jamii , na hasa vizazi vyetu,….visa hivi viwe ni akiba kwao wakisoma wajengeke,….leo ni porojo tu, ni visa tu,lakini hatujui ni nini hekima yake..nashukuruni sana, na tnasema;
Shukurani kwa wapenzi wote wa blog hii, TUPO PAMOJA DAIMA, hata ukinichunia mimi nitakuwa nawe bega kwa bega.

Ni mimi: emu-three

2 comments :

Yasinta Ngonyani said...

Nimefurahi sana kuwa utaandika kisa hiki maana nilikuwa nawza siku moja nitafanya hivi..nasubiri kwa hamu kwelikweli:-) "Wema hauozi"

emu-three said...

Ndugu wangu,dada Yasinta, nahisi mara nyingi mawazo yetu yapo pamoja, unaonaje ukawa pamoja nami kwenye kukamilisha kisa hiki, nitumie mawazo yako, ili nichnganye na tukio la kisa hiki, huenda kisa hiki kikawa bora zaidi?