Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, February 11, 2013

Uchungu wa Mwana Aujuaye ni mzazi-58
`Nimeamua kuwa mbali kabisa na jamii yangu, na sipendi kukutana na yoyote anayenifahamu, na sikuwa na jinsi ni kuja kuishi na mama huyu mdogo kwa vile ndiye chanzo cha haya yote, vinginevyo, nisingelikuja haoa kwake tena, …..’akaendelea kuhadithia huyu mwanadada, na wakati huu alionekana kama anajisikia vibaya.

‘Kwangu sina ndugu, na wala sina rafiki, ndugu zangu walinitenga, na kama walivyomfukuza mama yangu, nakumuona hafai kuishi na jamii zao, eti kwa vile katenda dhambi kubwa, basi mimi nimetenda dhambi kubwa zaidi ya mama, na kwahiyo sistahili kuwa karibu nao kabisa…’akaendelea kuongea kwa uchungu.

‘Na zaidi ya hayo, sina hata rafiki, maana wale niliowaona ni marafiki, wamekuwa ndio chanzo cha kunitumbukiza kwenye maangamizi zaidi…..je hawa ni ,marafiki au ni maadui, huenda basi sikustahili kuishi kwenye hii dunia…’hapo machozi yakaanza kumlenga lenga.

‘Huenda sistahili kuishi kwenye hii, dunia, na kila nilipoliwazia hili, najikuta nikiwa na wakati mgumu, nikijiuliza je, kama ni hivyo, nifanyeje, nijiue….mbona nilijaribu siku moja na taabu, uchungu na maudhi niliyoyapata siku ile, niliona ni heri, kama ni kufa nisubiri siku hiyo aliyonipangia muumba…’akatulia, na baadaye akangalia tumbo lake.

‘Lakini hata nikiamua kujiua, …je hiki kiumbe kilichopo hapa tumboni, kina kosa gani….?’ Akajiangalia tumboni na baadaye akainua uso,halafu akajikuna kichwa kwa muda mrefu hadi nywele zikatawanyika, kama mtu aliyechanganyikiwa, na nilipokumbuka kuwa alisema mara kwa mara anapandisha mshetani, nikaogopa, na kujiandaa kukimbia…

‘Hapana siwezi kujiua , kwanza lazima nione hawa walionifanyia hivi wanapata adhabu yao,….na wao wanakutwa na machungu kama haya yaliyonikuta mimi….wa kwanza keshaanza kuhangaika…na huyo ndiyo yule aliyejifanya ni tajiri, …na kutumia utajiri wake, kuniharibia maisha yangu, japokuwa kwa ujumla, amekiri kosa lake, lakini kwanini niteseke, wakati yeye yupo anafurahia utajiri wake…..’akatulia kwa muda…

Na yeye keshaanza kuipata adhabu ….hata kama ….akatulia kwa muda akiwaza yale yaliyotokea huko nyuma siku walipokwenda kumtembelea mama yao, akiwa na ndoto na kuanza maisha mapya, japokuwa hakuwa kajiandaa kwa hilo, lakini kutokana na shinikio lililokuwa juu ya uwezo wake, alikubali kuingia kwenye maisha hayo…ya kuwa mke wa mtu……japokuwa haikufanikiwa, ni kwanini haikufanikiwa, …..

************

‘Inabidi tupitie Arusha, maana huko nina biashara zangu, vinginevyo, itabidi nyie muende huko kwenu na mimi nitawakuta huko huko kwenu..’akasema Tajiri.

‘Haiwezekani, sisi tunakwenda pamoja wewe na sisi mguu kwa mguu hadi kwa mama, na tukitoka huko tutakwenda huko kwenye biashara zako, maana baada ya hapo, nitakuwa nimehalalishwa …..’akasema Maua, huku akisita sita kutamka hicho alichokusudia kukisema.

 ‘Hilo halitawezekana, ….mimi nina mpangilio wangu wa maisha na ninajua kwanini nafanya hivyo..maisha yangu yamegubikwa na maadui,….kuna watu hawapendi niwe hivi…kuna watu hawataki niwe tajiri…., wananionea kijicho, nahitajika kuwa makini na watu kama hawo…..’akasema na kuangalia saa yake.

‘Kwanini uwe na maadui….kiasi hicho, inaonyesha kuwa wewe sio mtu mwema, na huo utajiri wako hukuupata kwa halali?’ Akauliza Maua, na yule Tajiri akacheka kwa dharau.

‘Kwa halali..?’ akarudia hayo maneno huku akizidi kucheka, halafu akatulia na kumwangalia Maua kwa macho ya kupepesa, kama vile anamchunguza ndani ya akili yake, halafu akasema;

‘Usione watu ni mtajiri…ukafikiria kuwa utajiri wao umekuja kirahisi,…kuna mambo yamefanyika,….na nikuambie ukweli ukitaka upate utajiri wa kihalali, hutafanikiwa kamwe….na hata hivyo sijui una maana gani kusema `kihalali’ maana dunia hii ilivyo, mambo mengo sio ya halali, hasa yanapofikia kutafuta mali,…ili upate jambo, hasa mali na utajiri kuna dhambi nyingi zinatendeka…’akatulia na kuangalia juu.

‘Sio lazima utende dhambi, ndio upate ,mali au utajiri, hizo ni hulka zenu, nyie watu mnaopenda kutenda dhambi…kwani hakuna njia za halali za kupata mali, zipo, ila kwa vile nyie ni mawakala wa shetani, basi mnaona njia rahisi ni hiyo hiyo ya kishetani…’ akasema huku mama yake mdogo akimfinya lakini hakujali .

‘Na baya zaidi, mnatafuta mali hizo kwa kuwadhulumu wanyonge, ndio maana hamuishi kwa amani..nje na ndani…’akasema Maua huku akisogea mbali na mama yake mdogo, kwani aliona anamsonga, na alijua anafanya hivyo , kwa vile anatamka maneno ambayo kwake yeye aliona yatamharaibia kupata kile alichokitaka.

‘Una maana gani nje na ndani?’ akauliza huyo Tajiri huku akimwangalia Maua kwa macho ya kushangaa, alikuwa akiushangaa ujasiri wa huyu binti.

‘Ndio nje na ndani, nje, mnaogopa kuwawa….ndani mioyo yenu haina amani, kila mara mna wasiwasi…na ni heri niwe masikini kuliko kuwa na utajiri wa namna hiyo..’akasema Maua.

‘Hongera sana binti, napenda sana watu majasiri kama wewe,…unaonekana utanifaa sana, sio tu kama mke, bali pia katika shughulizangu,….’akawa anamwangalia huku akitikisa kichwa.

‘Shughuli zako zipi….?’ Akauliza Maua huku akiwazia jinsi gani atakavyoishi na huyu mtu aliyemzidi umri kwa mbali sana.

‘Nina shughuli nyingi sana,…..wewe unasema upo tayari kuwa masikini, kuliko kupata utajiri kwa njia isiyo halili, unajua nikuambia ukweli,….wengi wanasema hivyo, kwa vile tu wameshindwa kupata, lakini kama wangligundua njia yoyote ya kufanya ili waupate huo utajiri, wangelifanya…. Kiuhakika hizo ni zile hadithi za Sungura za sizitaki mbichi hizo,…ukishindwa kupata unasingizia mengine….tuachieni wenyewe tunaojua kuutafuta utajiri…na nyie mtaishia hivyo hivyo, mkitamani kuwa kama sisi, huku hamjishughulishi….’akasema huku akingalia saa yake.

‘Kwahiyo umesemaje?’ akauliza mama mdogo alipoona huyo jamaa kiangalia saa yake, kwani alijua kuwa huyo jamaa akitoa amri waondoke, hawatakuwa na muda wa kusmhawishi tena, wataondolewa hapo kama wezi.

‘Ninasemaje kuhusu nini…’akasema kwa ukali, hadi Maua akamwangalia huyo Tajiri kwa kushituka, maana muda huo mfupi alikuwa akiongea kwa kawaida, lakini aliposikia sauti ya mama yake mdogo akiuliza, ghafla kabadilika.

‘Si kuhusu hiyo safari….’akasema mama mdogo kwa sauti ndogo ya kunyenyekea,..Maua akawa akijiuliza iweje mama yake ambaye ni mkali kwake, lakini kwa huyo mzee anakuwa mnyonge kiasi hicho.

‘Mimi nawasikiliza nyie, …ila msimamo wangu ni kuwa sipangiwi wapi pa kwenda na kwa muda gani, mimi nina ratiba zangu,…. muda ukifika wa kuondoka ndipo napanga hapo hapo wapi….na lipi, nyie mjiandae na safari,…nauli natoa mimi, msiwe na  wasiwasi na hilo’akasema huku akiinuka akaonyesha ishara kwa walinzi wake.

Maua na mama mdogo wakainuka kuondoka.

********

‘Huyo mwanamke unasema anaitwa nani?’ akauliza Malkia wa Mererani, huku akiwa kashika kiuno.

‘Anaitwa Maua?’ akasema jamaa yake huyo kwenye simu.

‘Maua..maua ya namna gani, njano,….waridi….au, hata akiwa maua, hawezi kufikia uzuri wangu, mimi ni zaidi ya Maua, mimi kila mahali nikienda waandishi wapo nyuma, kuchukua picha zangu ili wapate kuuza mgazeti yao….unasema ni mwenyeji wa wapi?’ akauliza huku wivu ukimsumbua akilini.

‘Singida mpakani, ….’akasema huyo jamaa kwenye simu. Aliposikia kuwa huyo Maua anatokea kijiji mkoa anaotoka yeye, akatikisa kichwa….

‘Kama ni huko….hana jeuri na mimi, wasichana warembo wote wa huko nawafahamu….hilo jina kwangu sio geni…lakini, lakini...’akasema huku akijaribu kufikiria.

‘Sasa bosi, nitashindwa kufanya mambo yako, kwa vile sipo karibu tena na Tajiri…keshanifukuza nisiwe karibu nay eye….’akalalamika huyo jamaa.

‘Ina maana huyo Maua ndiye kasababisha ufukuzwe kazi ..au sio,….?’ Akauliza na hata kabla hajajibiwa akasema;

‘Lakini usijali, nitahakikisha kuwa unarudi kuwa karibu na yeye, maana wewe ndiye mtu wangu wa kunipatia taarifa, ….mwenzako hajawa mzoefu, …sasa sikiliza,….nataka nijue anatokea kijijini gani, na wazazi wake ni akina nani…na hapo Dar anaishi na nani..unasikia?’ akasema.

‘Nitafanya hivyo bosi…’ na simu ikakatika.

‘Maua….Maua…nitaona kama yeye ni Maua, mimi nitakuwa jua kali la kufanya Maua yanyauke……’akasema huku akipiga simu, na akashangaa simu ya huyo anayempigia haipatikani.

‘Ina maana kwasababu ya huyo Maua wako, umeamua kuzima hata simu…ngoja atanitambua, sizani kaka wiki itakwisha, akiwa na wewe, ….’ Na kabla hajamaliza kusema simu yake ikaita, akasikiliza kwa makini na baadaye akasema.

‘Basi nimekuelewa,…..nitakwenda leo leo hadi huko kijijini na kumtafuta huyo Maua ndio nani….’ Akaongea huku akitembea kuelekea kituo cha mabasi…

*********

‘Hapa ndio Arusha, na nimewatafutia chumba cha namna hii, ili muwe karibu, ni chumba kimija lakini kina vyumba viwili….maana nataka pia nikifika hapa niwe karibu na wewe…mrembo wangu..’akasema huku akimwangalia Maua

‘Nani mrembo wako, usifikiri, nimekubali kuwa mkeo…mimi ninachohitajia ni malezi ya mtoto wangu,…..’akasema Maua.

‘Usijali, haya tutayaweka sawa,….mimi ni Tajiri bwana,pesa inaongea, mwenyewe utanyweza na kukubali kuwa na mimi ..maishani….mimi usnione hivi, najua kupenda, na ninayempenda anakuwa kama mbwa kwa chatu….hahaha’akasema huku akimwangalia mama mdogo.

‘Kweli Tajiri..maana huishi kubadili wanawake,..lakini ni kwa vile una pesa, unafikiri wanakupenda wka vile …wewe ni mpendevu’akasema mama mdogo.

‘Wewe hujui undani wa maisha yangu…..’akasema huku akiangalai simu yake, ambayo aliondoa sauti, na akaona ujumbe ukiingia, akausoma na haraka akainuka.

‘Sasa tutaonana baadaye, maana naona mzee ananihitaji haraka..’akasema.

‘Mzee gani.?’ Akaulizwa

‘Aaah, ni huyu Mjomba wangu….’akachukua mkoba wake na kuanza kuondoka.

‘Mjomba wake…huyo ndiye wa kuonana naye, ili tuhakikishe kuwa anatekeelza yote yanaoyostahili….’akasema mama mdogo.

‘Sasa utamjuaje, na kumpataje?’ akauliza Maua.

‘Wewe subiri, sisi ni watoto wa mjini, kuna ndugu yangu mmoja anaishi hapa, ……Arusha nitawasiliana naye, atanmfuatilia, na tutamjua ni nani…..’akasema huku akipiga namba ya simu.

‘Kuna tajiri mmoja……aaah, hapana, sio mzee sana….ana mjomba wake….nahisi ndio huyo….anasafiri –safiri sana kwenda Dar, ndio huyo…..nataka kumjua ni nani na wapi nitaweza kumpata’akasema.
Akakata simu na kwenda kukaa karibu na Maua, na kipindi hicho Maua alikuwa kasimama akiangalia nje, kwani kulikuwa na gari limesimama,….kwa nje,…

‘Kuna msichana mrembo, yupo nje, na ana walinzi, utafikiria huyo Tajiri wako, anavyonata, ajabu….kapanga rangi kwenye macho, na kila anavyofanya utafikiri wale warembo wa maonyesho, na waandishi wanampiga picha….’akawa anaongea na mama yake, na mama yake mdogo akasogea pale dirishani kumwangalia huyo mrembo ni nani..na kabla hawajatulia simu ya mezani ikaita.

‘Hapa ni mapokezi, kuna mgeni wenu, anataka kuonana na nyie…’

‘Sisi hatuna wageni…..’akasema mama mdogo kwa mkato, na kabla hajaiondoa ile simu masikioni huyo mtu wa mapokezi akasema;

‘Tunajua hilo, lakini huyo ..ni mtu wa karibu wa Tajiri,…hana matatizo, ….’

‘Anaitwa nani?’ akauliza mama mdogo huku akiwa na wasiwasi.

‘Anaitwa Malikia wa Mererani….’
 

 NB: Wakati ukuta, ....wikiendi ilikuwaje? JE TUMALIZE?

WAZO LA LEO: Usikubali kuingia kwenye mahusiano, bila kujua huyo unayetaka `kuhusiana' yupoje na ni nani, kwani athari zake huja baada ya matendo, ....jichunge na utahamini mwili wako, kwani mwili wako una thamani kubwa sana.....

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Yasinta Ngonyani said...

"nukuu" "‘Na zaidi ya hayo, sina hata rafiki, maana wale niliowaona ni marafiki, wamekuwa ndio chanzo cha kunitumbukiza kwenye maangamizi zaidi…..je hawa ni ,marafiki au ni maadui, huenda basi sikustahili kuishi kwenye hii dunia…’hapo machozi yakaanza kumlenga lenga. mwisho wa nukuu hapa nimeguswa sana ....kazi yako ni nzuri sana Hongera...