Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, February 7, 2013

Uchungu wa mwana Aujuaye ni Mzazi-57
  Hali yangu ilikuwa yenye utata, maana ilifikia hatua naweza kufika sehemu na kujisikia vibaya, na hapo hapo nikapandisha, na kuwa mtu tofauti kabisa, na kitakachotokea hapo siwezi kukijua, nakuja kuhadithiwa baadaye, kuwa nimefanya maajabu,…sikumbuki, na hata sielewi jinsi nilivyoweza kufanya hayo ninayokuja kuhaditihiwa baadaye kuwa eti ni mimi nimeyafanya’ 

Akaendelea kuhadithia kisa hiki, msimuliaji wetu mkuu, Maua binti Maua.

**********

‘Haya uliyo nayo ni mashetani, inabidi tukahangaike, …na nashukuru sana pamoja na hayo uliyomtendea yule tajiri, bado amekubali kukusaidia, hali yake kwa sasa inaendelea vyema,…’akasema mama mdogo.

‘Lakini yote haya namtupia lawama yeye, huenda yasingelitokea kama isingelikuwa ni yeye,…..mbona mwanzoni nilikuwa sina matatizo kama haya’akasema Maua.

‘Huenda ulikuwa nayo, ila yalikuwa hayajachokozwa…au ndio umekumbana nayo, au kuna mtu kakutupia, ….binadamu hawana wema, kijicho na husuda kwa binadamu ni kawaida..., ‘akasema mama mdogo.

‘Wanionee kijicho kwanini, kwani mimi nina nini cha kuonewa kijicho, wanataka umasikini wangu, au wanataka nini…mimi siamini hayo, nahisi yote yamesababishwa na huyo Tajiri wenu..’akalalamika Maua.

‘Tatizo lako huangalii mbele, unachoangalia na nyuma, hayo aliyokutendea yamepita, ….na alifanya hivyo kwasababu,…’akatulia

‘Kwasababu gani?’ akauliza Maua.

‘Hayo ni siri kubwa, sisitahili kuyasema, ila yanafungamana na utajiri wake’akasema mama mdogo huku akiangalia huku na kule , kama kuogopa,watu wasije wakamsikia.

‘Huoni, ina maana utajiri wake, ni wa kishirikiana, na kwahiyo hatasita kunifanyia lolote baya, ilimradi afanikiwe zaidi’akasema Maua.

‘Afanye nini baya…kama ni yeye, basi usingelimdhuru yeye…’akasema mama mdogo huku akikimbuka kashkashi la siku ile………….

******

 Mama mdogo, wakati anamsubiri Maua ,akijua Maua yupo ndani na bosi, na huenda mambo yakawa mazuri, siku hiyo wanaweza kuondoka na mshiko wa nguvu, akaona walinzi wa Tajiri, wakikimbilia ndani, na yeye kwa umbea akajitosa, …

‘Na wewe unataka kwenda wapi?’ akauliza na mmoja wa walinzi

‘Mwanangu yupo huko ndani, lazima nijue kuna nini kimetokea….’akasema huku akisukumana na yule mlinzi.

‘Mwacheni aingie, huenda akatusaidia, maana sisi huku ndani tumechemsha, …na bosi kasema tusimua’akasema mmoja wa walinzi.

Mama mdogo aliposikia hivyo, `tusimuue…, ‘akahisi kuna tatizo kubwa limetokea, akaruhusiwa na kuingia ndani, na pembeni akaona Tajiri akiwa kalala kwenye sofa, na kitambaa kikiwa kimelowana damu, alikuwa akilalamika maumivu..

‘Docta keshafika…’akasikia mmoja akisema.

‘Kwanini tusimkimbize hospitali..’mwingine akasema

‘Bosi kasema hataki kupelekwa hospitalini, anahitaji kutibiwa hapohapo….’akasema huyo mlinzi.
Mama mdogo, akageuka huku na kule akimtafuta mwanae, na pembeni kabisa, akamuona Maua kalala chini, na alionekana kabisa hana fahamu….akamsogelea, na mmoja wa walinzi, akasema;

‘We mama we unataka kufa, wenzako wote waliomsogelea sasa hivi ni majeruhi, mwanao kageuka kuwa simba, ananguruma kama simba….’akasema mmoja wa hawo walinzi. Na mama mdogo aliposikia hivyo,akasimama na akakumbuka kile kichupa, ambacho, walishapewa na mmoja wa mtaalmu ambaye siku moja walikwenda kwake kupata tiba.

Akatoa kile kichupa, na kumsogelea Maua, akachukua kisogo na kuyatupia mwilini kwa Maua. Na mara Maua akainuka, kama anataka kusimama, halafu akarudi chini na kulala, akatulia kimiya….

‘Kumbe unayo dawa…’akasema mmoja wa walinzi.

‘Sikujua kuwa kumetokea matatizo, ningelijua ningelimuwahi’akasema mama mdogo.

‘Kwani binti yako ana matatizo gani?’ akauliza mmoja wa watu wa karibu wa huyo mlinzi.

‘Sijui, tunahisi kakumbwa na mashetani’akasema mama mdogo.

‘Basi muhangaikieni…..hali aliyo nayo sio ya kuicha hivyo….hilo ni tatizo kubwa, na nawashauri ili atibiwe vyema, rudini huko alipotokea, kijijini kwenu, ….mara nyingi mambo hayo chimbuko lake ni huko kijijini, na mara chache inakuwa ni kukubwa na hayo mashetani ….lakini ukichunguza sana chanzo chake ni huko alipotokea….kama mna imani kweli, nendeni kwenye dini zenu akaombewe,…..’akasema huyo mtu wa karibu wa Tajiri.

‘Tumeshaanza matibabu, …’akasema huku akitulia pale alipomuona Maua akiinuka na kukaa vyema, na alionekana kama kushangaa, akawa anaangalia mikono yake, ikiwa na damu.

‘Kwani kumetokea nini?’ akauliza

‘Ulitaka kumuua bosi wetu…’akasema mmoja wa walinzi.

‘Kwanini nimuue bosi wenu,….?’ Akauliza Maua huku akimwangalia yule tajiri kwa wasiwasi, na kujaribu kukumbuka ni nini kilitokea, lakini akili ilikuwa haikumbuki…ilikuwa kama mtu aliyekuwa kwenye usingizi mnzito…hata akili zilipotulia alichokumbuka ni ila hali ya kujisikia vibaya, na kichwa kuuma, na kusikia sauti zikimuamrisha kufanya jambo, na baada ya hapo hakukumbuka jingine…..

‘Mimi sikumbuki kitu…’akasema Maua huku akishjika kichwa, na kushangaa jinsi nywele zake zilivyovurugika, tofauti na zilivyokuwa mwanzoni.

‘Huyo binti keshazindukana, ….hakikisheni kuwa yupo sawa, ….?’ Akauliza mmoja wa walinzi

‘Ndio keshainuka, naona yupo shwari kwa sasa….’akasema mlinzi mwingine

‘Basi bosi anahitaji aletwe mbele yake…’akasema yule mlinzi wa mwanzoni

Walinzi kama kawaida yao ni kutii amri, na kwa haraka wakamsogelea Maua, japo kwa tahadhari, wakikumbuka kile kilichotokea kwa wenzao, wakamshika Maua mikono huku na huku, wakimuongoza kwenda kwa tajiri yao.

‘Msinishike hivyo, kwani mimi siwezi kutembea mwenyewe..’akalalamika Maua pale alipoona wanakuwa kama wanambeba kama anavyobebwa mgonjwa, na walipoona Maua akilalamika, wakamuachia, atembee mwenyewe hadi pale alipolala Tajiri yao,.

Tajiri, aliinua kichwa, na kumwangalia Maua kwa muda, halafu akajiinua na kukaa vyema, akakohoa, na kusema;

‘Natumai sasa nafsi yako imesharizika,….lengo lako lilikuwa ni kuniua au sio ndio maana ukabeba kisu…’akageuza kichwa kumwangalia mama mdogo, wakati huo mama mdogo alikuwa mbali , hakuweza kusikia vyema wanachoongea, ila alionekena kushika mdomo, kuonyesha kushangaa jambo, huenda wale walinzi walikuwa wakimsimulia yaliyotokea.

‘Maua,….kubeba kwako kisu inaonyesha ulidhamiria,….aaaah, lakini tutaona,…, bahati nzuri, hukuweza kutimiza lengo lako,…sijafa, sasa una nafasi ya kufanya hivyo tena, lakini safari hii sitaweza kukupa muda huo,…..itakuwa zamu yako…huwezi kunitoa damu yangu hivi hivi nikuachie…’ akasema kwa ukali.

‘Mimi sielewei unaasema nini…kwani ni mimi nimekufanya hivyo?’ akauliza Maua huku akionyesha mshangao.

Tajiri akamwangalia Maua kwa muda, halafu akageuka kuangalia kule alipo mama yake mdogo, akaonyesha ishara huyo mama aletwe mbele yake, na yule mama alipofika hapo mbele yake akaulizwa;

‘Binti yako ana matatizo gani?’ akauliza kwa sauti ya ukali

‘Nahisi kakumbwa na mashetani’akasema huyo mama

‘Kwanini hujamshughulikia, huoni kuwa hii ni hatari, angeliweza kunitoa roho, …sikuamini binti mrembo kama huyu anaweza kugeuka kuwa simba, na kunishinda mimi…mimi mwenyewe nina yangu yana nguvu, lakini ya huyu binti yalizidi….ilikuwa ni balaa…ananguruma kama simba….anakuwa kama jamaa mmoja, sijui ni wapi,….nilihadithiwa kuwa ana tabia kama hiyo’akasema huku akitabasamu.

‘Bosi na wewe una mashetani?’ akaulia mmoja wa watu wake.

‘Ya kwangu sio mashetani bwana, huwezi kuyaita hivyo,…ni mambo ya kimila….hata hivyo, mimi siwezi kudhibitiwa, kama wanavyodhibitiwa watu wa mashetani, mimi nayadhabiti ya kwangu, ….nayapa amri,…na napata kile ninachokitaka, sio kama haya, …..’akatulia na kumwangalia huyo binti.

‘Mimi sina mashetani….siamini mambo hayo…’akasema Maua, na Tajiri akamwangalia kwa muda, halafu akageuka kumwangalia mama mdogo

‘Sasa kama anahitaji msaada wangu ninaweza kumsaidia, nina mtu mmoja ninayemfahamu, anaweza kuyaondoa hayo madude, kabisa…..’akageuza kichwa na kumwangalia huyo binti.


‘Mimi sihitaji msaada wako, ninachohitaji ni kuilea hii mimba’akasema Maua.

‘Hilo tumeshamaliza binti,…’akamwangalia yule binti na huku akiwa kama anataka kuinuka, akaendeela kuongea kwa kusema;

‘Mbona nilishakuandikia ushahidi, unataka nini tena….au unataka hayo aliyoagiza huyo shetani wako, maana kaamrisha kuwa twende huko kijijini kwa mama yako,…huko nitapata maagizo mengine, eti kuondoa ….sijui alitumia neno gani, hata sikumbuki vyema,…eti….nisipofanya hivyo, akinijia tena, atahakikisha kuwa anaichukua roho yangu…hahaha…mimi sio mtu wa kutishika, kirahisi, lakini….’akasita pale alipomuona Maua kama anatetemeka.

‘Aaah, mwangalieni, aisije akapandisha tena….’akasema huyo Tajiri.

‘Atapandisha tena, kama usipotii hayo maagizo yake’akasema mama mdogo huku akitoa kile kichupa na kumnynyuzia huyo binti mafuta.

‘Huwezi kunilazimisha kwa njia hiyo, ila mimi sina shida, tutapanga hayo, ….na nilikuwa na mazungumzo nyeti na nyie wawili,….’akatulia na kuwaangalia wale akina mama wawili kwa zamu, na baadaye akawageukiwa walinzi wake na kusema ‘Naomba mniache na hawa watu wawili, msiwe na shaka hawezi kupandisha tena…’aaksema Tajiri.

Baada ya wao kubakia wawili, akainuka na kukaa vyema, aliangalia sehemu ile aliyoumizwa, akawa anapitisha kidole juu kuiweka vyema ile bandeji, na baadaye akamwangalia Maua, na mama yake mdogo, akasema;

‘Nimejifunza jambo moja…..pamoja na mambo mengine yote, mimi nimetokea kumpenda binti yako,…’ akainuka na kusimama.

‘Vinginevyo, asingelitoka hapa hai,….ningeliweza kufanya lolote, na bila kufanywa lolote, ….mtu kaja kwangu na kisu….ushahidi ungelionekena…..na wewe huenda unajua, atachukuaje kisu aweke kwenye mkoba wake wewe usijue?’ akamuuliza mama mdogo, ambaye alibakiwa kushangaa, alikuwa hajui kabisa kuwa binti yake alikuja hapo na kisu.

‘Nasema kwa moyo wangu wote,…kuwa pamoja na haya, mimi nimemsamehe, sina kinyongo na yeye, ….lakini kama anataka haya yaishe kwa usalama, atahitajika na yeye kutimiza wajibu wake....hata hivyo siwezi kumlazimisha, ila kiukweli, moyo wangu utauma sana, kama atachukuliwa na mtu mwingine…’akatulia na kumwangalia huyo binti.

‘Kwahiyo unataka kumuoa?’ akauliza mama mdogo.

‘Huko unakwenda mbali saana…umekimbilia hatua ya juu, hayo yatakuja baadaye, kama mambo yatakwenda vyema, tutafanya hivyo…ni kweli nahitaji mke, kwani maisha haya ya kuishi leo huyu, kesho huyu nimechoka nayo,….sasa nahitaji kutulia na mke mmoja ninayempenda, ….na nakiri huyu binti ananifaa’akatulia kidogo.

Yule mama akatabasamu huku akimwangalia binti yake, akamshika begani, na kusema kwa sauti ya kunong’ona..’Unaona, bahati hiyo….’

‘Hayo hayana haraka, cha muhimu…na kwanini unataka mambo hayo kwa haraka…?’ Yule Tajiri akamgeukia mama mdogo safari hii akionyesha uso wa tabasamu.

‘Sasa mara nimekwenda kwa haraka,..wakati wewe mwenyewe  umeshazimia kwa binti yangu, na kwa ujumla unahitaji mke, ungenipenda mimi, mzee mwenzako….’akasema kwa utani, na yule Tajiri akaceka hadi jino la mwisho.

‘Mimi sioni kama kuna kizuizi, maana umeshampa uja uzito, haina haja ya kuruka huku na kule, wewe toa mahari….ndoa haina umuhimu sana maana umeshaifunga kwa nguvu’akasema mama mdogo.

‘Tatizo lako wewe mama una tamaa, tamaa ya pesa, pesa ni ibilisi mkubwa, ….’akatoa pesa mfukoni na kuzishika hewani, na wakati huo yule mama akawa anaziangalia kwa hamasa, na yule tajiri alivyoona jinsi yule mama anavyoziangalia zile pesa kwa tamaa akamtupia usoni.

Yule mama bila aibu akaziokota na kuzifutika kifuani,…..Maua akamwangalia mama yake kwa uso wa hasira, alitamani kumwambia azirudishe kwa mwenyewe lakini akaona ajinyamazie, tu, na wakati huo huo yule jamaa alikuwa akiongea utafikiri hilo tendo alilofanya halikuwa na maana kwake, akaendelea kusema;

‘Wewe mama kwa tamaa yako ya pesa …..utafika kubaya,….na nahisi kabisa kuwa wewe, ndiye umemchuuza huyu binti wa watu, sikupenda kabisa haya yamtokee huyu binti, wakati mwingine najuta sana,…..huyu sio mtu wa kutendewa hivi, huyu binti sio watu wa aina yako,….lakini imeshatokea hakuna jinsi, na mimi naahidi kuwa nitamsaidia kwa nguvu zangu zote, lakini kama yupo tayari kwa 
hilo….’akasemaTajiri huku akimwangalia huyo binti.

‘Mimi kama ulivyosema, ….kuwa umeambiwa twende huko kijijini, kwa mama yangu, hilo wazo naliunga mkono,…twende huko huko kwa mama ili akuone wewe ….uliyeniharibia usichana wangu, ….’akawa anatoa machozi.

‘Unalia nini sasa….’mama yake akasema kwa ukali huku akimminya begani, na akawa kama anamnong’oneza….`sasa usiniangushe hapa ndipo pa kucheza karata vyema…’.

‘Naona tumemalizana, nyie kajiandaeni, nikiwa tayari, nitawaambia, safari ni lini, …na mumesema kwenu ni wapi vile?’ akauliza.

‘Singida,..mpakani….’akasema mama Mdogo.

‘Aaah,, basi haina shida, maana huko ndiko njia yangu nikiwa na mambo yangu,….hata hivyo nilikuwa na safari ya huko, ….ni siku nyingi sijafika, …’akawa katulia akiwaza jambo,….akamwangalia Maua, kwa makini, baadaye akajikuta akiuliza;

‘Kwani wewe mama yako huko kijijini anaitwa nani?’ akauliza

‘Maua….’akasema Maua.

‘Kwani huko Singida unakujua?’akauliza mama mdogo, na yule Tajiri hakujibu kitu, alikuwa anamwangalia Maua, pale alipoulizwa jina la mama yake, akataja `Maua’, alihisi kuwa huenda huyo binti akili yake haijakaa sawa.

‘Wewe binti nakuuliza swali la msingi, huwezi ukaitwa Maua na mama yako akaitwa Maua..’akasema yule Tajiri na Maua akabakia kimiya huku akiangalia chini.

‘Haina shida…’akasema huyo Tajiri….huku akiwa kama anawaza jambo, akamgeukia mama mdogo na kusema;

‘Kwani kiutaratibu, huko kwenu inatakiwaje, kwanza natakiwa kwenda mwenyewe kujitambulisha au natuma mtu, maana mimi nataka nianze kufuatilia taratibu zote, sitaki utani, nataka kuyabadili maisha yangu…’na kabla hajamaliza simu yake ikaita. Akaipokea bila kuangalia nani aliyempigia.

‘Oh, ….nisamehe…mpenzi….’akasema pale aliposikia huyo anayepiga simu ni nani, akageuka kumwangalia Maua, na baadaye akainuka na kuelekea chumbani kwake,..
Binti akawa anaangalia kule alipoelekea huyo Tajiri na huku akisema;

‘Unaona…..nilikuambia huyu mtu ana mke wake, na mimi anataka kunifanya mke wa pili…’akalalamika Maua.

‘Hana mke huyu….’akasema jamaa ya huyo Tajiri

‘Sasa huyu anayeongea naye ni nani?’ akauliza.

‘Ni dada mmoja mtata,,,,,malikia wa Mererani….sijui mtaivana kama akisikia wewe unatakiwa uolewe na huyu bosi, maana, mwanamke huyo ana wivu, lakini hataki kuolewa,…..’akakatisha pale Tajiri aliporudi.

‘Natumai tumemalizana,…Maua upo tayari kuolewa na mimi?’ akauliza

‘Kama utamuacha huyo hawara wako,….’akasema Maua.

‘Hawara gani?’ akauliza Tajiri akishangaa.

‘Huyo anayeitwa Malikia wa Mererani’akasema na yule tajiri, akabakia akishangaa, akawageukia watu wake akiwa kakunja uso,…..akasema kwa hasira;

‘Ni nani katoa siri zangu za ndani….’akatoa sauti ya hasira, na yule eliyeoongea akapiga magoti akiomba msamaha,….

‘Mkuu, sikuwa na nia mbaya ….niliongea hivyo ili kuongeza wivu, ….wivu unasaidia kwenye mapenzi…..’akasema .

‘Toha humu ndani haraka,…na hutakuwa kwenye kikosi changu tena, na adhabu nyingine zitafuata baadaye, ….sitaki msaliti kwenye kundi langu…’alaipomaliza kuongea tu, wale walinzi wakambeba yule jamaa juujuu, huku yule jamaa akilia na kuoba msamaha…

‘Kama maisha yenyewe ndio haya,….mimi siolewi na wewe’akasema Maua na kutoka nje…

NB: JE tumalize ….?

WAZO LA LEO: Ni kweli tunahitaji pesa kwa ajili ya maisha yetu, lakini kupenda pesa huko kusivuke mipaka, na kujikuta tunasahau ubinadamu, pesa ni mtaji, lakini pia pesa ni kishawishi kibaya, zinaweza kutupeleka kubaya..Tuwe makini na hilo.

Ni mimi: emu-three

3 comments :

Anonymous said...

Oh my God! Maua katembea na babaake mzazi! nimeshahisi huyo tajiri ni Adam ambaye ndio alimpa mimba Maua kijijini akakimbia!

Anonymous said...

Hi there evегу onе, hегe every
peгson іs sharіng ѕuсh κnow-how, therеfore
іt's nice to read this weblog, and I used to go to see this webpage daily.
My page :: loans for bad credit

emu-three said...

Tusubiri hatima yake, na kisa hiki kipo wazi tuone ni nini kitatokea. Swali kubwa la kujiuliza, kama wewe ni mzazi yamekufika hayo ungelifanya nini?