Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, January 22, 2013

Uchungu wa mwana Aujuaye ni mzazi-51




‘’Nilifika Dar, nikiwa na ndoto nyng kichwani, na kwa jinsi mama mdogo alivyokuwa akinipamba kuwa mimi nina umbo zuri, sura nzuri ya mwanamitindo, nilijikuta nikiwazia mbali, hata kutaka kuwa muigizaji, kama wale waigizaji kwenye runinga;’’ akaendelea kuhadithia kisa chake huyu binti.

‘Wewe kwa urembo wako huo, unaweza ukawa sio mwanamitindo tu, bali pia unaweza kuwa muigizaji filamu….’akasema mama yake mdogo.

‘Kweli mama ina maana naweza kuwa muigizaji filamu bila hata ya kuwa msomi?’ Maua akamuuliza mama yake mdogo.

‘Unaweza, kwani usiweze, kuigiza hakuhitaji shule kubwa sana, ni kipaji na kujulia nini unachokifanya, hata hivyo, hawo watu wakikuchukua, watakusomesha wenyewe,….,..wewe unafaa sana. Cha muhimi ni wewe kutulia na ufanye vile ninavyokuelekeza, ukifuta yale ninayokuelekeza, utajikuta unafika mbali, hata Ulaya utafika…mjini hapa, bongo hapa.’akasema huyo mama akicheka kicheko cha kebehi.

‘Nitafurahi sana mama, nataka nipate kazi, niweze kumsadia mama yangu aondokane na huo utumwa alio nao, maana pale kwa yule baba, alikuwa akiishi tu, ili nikue, hakuwa an sehemu nyingine ya kuishi, angelishaondoka,….’akasema Maua huku akikumbuka jinsi walivyoachana na mama yake, ….

‘Mwanangu, nimeonelea uondoke tu hapa nyumbani,…maana ukikaa hapa ni lazima huyo mwanaume mlevi, baba yako wa kufikia, atakuozesha kwa huyo jamaa yake, kwa tamaa ya pesa, na kuendekeza ulevi….’akasema mama yake.

‘Sawa mama, mimi nipo tayari kuondoka na mama mdogo,….nimeshajiandaa, na nikifika huko nitatafuta kazi , nije nikuchukue……’akasema huku akiwa na furaha, lakini kwa upande mwingine, moyoni alikuwa akihuzunika kumuaha mama yake.

‘Mwanangu usiwe na tamaa sana ya kupa mengi, tamaa ni mbaya, rizika na hicho kidogo utakachopata, na usiwaze mambo mengi ambayo hujui kama yapo, hizo ni ndoto za Alinaha….’akasema huku akiwa kainama chini.

‘Mwanangu maisha haya, yana mitihani mingi, na wakati mwingine unaweza ukakufuru ukasema kwanini mimi, ….ukifika huko cha muhimu ni kumsikiliza mama yako mdogo, sijui ana malengo gani kwako, lakini kwa hali ilivyo, sina la kufanya,…najua mzazi ni mzazi, na kama ana uchungu na mwana, atafanya kama anavyomfanyia mwanae, …..’akatulia na machozi yalimlenga lenga.

‘Mama kwanini sasa unaanza kulia,…mimi nilijua kuwa utafurahia kwasababu mtoto wako naenda mjini, na nitapata kazi, nitakuja kukusaidia….’akasema Maua akilaza kichwa chake kwenye mapaja ya mama yake, na mama yake akawa anapitisha mikono kichwani kwake, na hakuweza kuvumilia machozi yakawa yamemdondokea mwanae.

‘Mwanangu, nihisivyo, …nakuona kama nakutumbukiza baharini, na sijui utakutana na wanyama gani,….sijui kama utaweza kuogelea na kufika huko kusikojulikana, na sijui oooh…….naogopa sana mwanangu,..lakini ukibakia hapa ni yale yale, uwezo wa kukulinda hapa nauona ni mdogo, ninaweza nikashindwa, kama unavyoniona mwili wangu umezoofu kwa kuumwa, na sijui lini nitapona, au ndio tiketi ya kuondokea…..’akatulia.

‘Mama sasa unanitai huzuni, ……kwa hali hii naona bora nsiondoke, sitaweza kukuacha hapa mwenyewe, bora nisiende…..’akasema Maua huku na yeye machozi yakimlenga lenga.

‘Hapana mwanangu lazima uondoke hapa…’akajikausha na kujipa moyo.

‘Sawa mama, mimi naomba usiwe na wasiwasi..nitajilinda, nitapambana kwa ajili yako,…najua mama mdogo atanisaidia …’akasema Maua akiwazia mbali.

‘Tuombe iwe hivyo…na najua huku nyuma mtaniachia balaa, lakini nitapambana nalo,…na najua ukiwa haupo, itakuwa rahisi kwangu kupambana na hawo watu, lakini ukiwepo hapa, itaniwia vigumu sana, nyie nendeni, ya huku nyuma niachieni mwenyewe…….’akasema na kipindi hicho mama mdogo alishafika, tayari kwa safari ya Dar.

************

Mama Maua alizishika zile pesa mkononi, akaziangalia kwa muda, halafu akazishika kwa mikono miwili, na kumwangalia yule jamaa, yule rafiki wa muoaji, macho yalikuwa yamejaa ukungu wa mahozi, akatikisa kichwa na kusema;

‘Nashukuruni sana,….kama nia yenu ilikuwa njema, mungu awabariki sana, lakini kama lengo lenu ni kuninunua kama mtumwa, ….mungu awasamehe, kwani kwa hali mlio nayo hamtajua kamwe, shida, taabu, na mauzi, tunayopambana nayo sie watu wa hali ya chini….’akawa ananyisha mikono kuelekea kw kwa huyo jamaa,

‘Wengi twajiona tumefika pale tunapokuwa hatuna shida…sawa mubarikiwe sana….lakini sio kila mtu ni mtumwa wa pesa, …sio kwamba sipendi pesa, lakini sio kila pesa ni safi, nyingine ni sumu,…..’akatulia na kumsogelea yule jamaa, akanyosha mkono ukiwa na zile pesa …

‘Chukua pesa zako,…..tafadhali, sina haja nazo,……’akasema na yule mwanaume wake mlevi, akafunua macho ya mshangao, na kwa haraka akamsogelea na kutaka kuzichukua hizo pesa, lakini yule mshenga akamuwahi na kumshika ….akamvuta pembeni na akawa kama anamnong’oneza akasema;,

‘Hiyo haikuhusu mkuu,…’akasema huyo mshenga.

Yule jamaa, akabakia ameduwaa, akiwa haamini macho yake, kwani hajawahi kukutana na mtu ambaye anapewa pesa, halafu anazikataa, katika maisha yake, amekuwa haamini kuwa kuna mtu kama huyo,….akaziangalia zile pesa zikiwa mikononi mwa yule mama, na akasita kunyosha mkono wake, akageuka na kumwangalia yule jamaa anayetaka kuoa;

‘Naona hapa ngoma nzito….unasemaje mkuu’akasema.

‘Tatizo ni kuwa huyo mwanaume wake amekula pesa zangu nyingi…na katika maisha yangu sijawahi kuzalilishwa kiasi hiki…sijui nifanye nini ili kuondoa hili doa,…naona tuondoke,…’akasema huku akigeuka kuondoka, na yule mwanaume mlevi akamkimbilia na kusiamama mbele yake,…akapiga mgoti

‘Sikiliza mkuu, mimi nitahakikisha mambo yanakuwenda vyema, nitamuweka sawa, nahisi ana tatizo linamsumbua,..usiwe na shaka mkuu, nakuomba tafadhali….’akasema huku akinyosha mikono juu, ya kumuomba, na yule jamaa akasogea pembeni na kuendelea kutembea pale aliposimamisha gari lake.

‘Jamani hapa naona mambo yameharibika, na ……’akawageukia wale wanafamilia wawili, na kusema kama ananong’ona;

‘Poteeni haraka, sijui mtapotelea wapi, maana jamaa ana masikio na macho kila kona ….nawasikitikia sana, ….sina cha kuwasaidia, subiribi matokea yake’akasema na kuondoka huku mwenzake akimfuatia nyuma,
Yule mwanaume, akionekana kuwa pombe zimemuishia kichwani, akajizoa zoa pale chini alipokuwa kapiga magoti, na kutembea kuelekea ndani, lakini kabla hajafungua mlango, akamuona yule jamaa akirudi kwa haraka, na alipowafikia akatoa kufuli kwenye mfuko, akasema;

'Toeni kila kilicho chenu humo ndani….kwani nataka kufunga nyumba ya watu, hamtambulikani tena kama wapangaji wa hii nyumba….’akasema huku akiliweka kufuli kwenye mlango, na kuwaangalia wale wanafamilia wakiwa wameduwaa…

‘Natumani mumenielewa, na ujumbe wako mzee wa kinywaji, amesema, adhabu yako, kwa vile huna mbele wala nyumba, ukajitundike mwenyewe, …akukute umeshajimaliza….natumai unamfahamu, …..amekusamahe mara mbili, hawezi kufanya hivyo mara ya tatu, kwani umeshamzalilisha, kitu ambacho hajawahi kufanyiwa ….’akangeukia yule mwanamama, na kumwangalia kwa macho ya huruma.
Yule jamaa mlevi akandondoka chini na kujilaza kwenue ukuta na kusema;

'Sasa nimekwisha.... basi tena sina changu....' Yule jamaa akamwangalia na kutabasamu, na hakumjali akamgeukia mama Maua na kusema;

‘Mama Maua, …kwanza nikupe pole kwa haya yote, najua yote ni kwasababu ya mume wako, ambaye kakukana kuwa wewe sio mke wake, ndio maana jamaa yetu kwa moyo safi aliataka akuoe, na hakuwa anatania…lakini umekataa, sio mbaya, mapenzi hayalazimishwi, ….ila kama utabadili nia, bado nafasi ipo wazi, hadi jioni…..’akatulia pale mama Maua alipoinua mkono wa kukataa.

‘Mimi sio mtoto mdogo, wa kubembelezwa na pipi, ….uamuzi wangu upo pale pale….sitaki kabisa, utu wangu haununuliwi kwa pesa, na ni heri kufa, na kama ulivyosema kuwa huyo jamaa ni hatari, ….sawa yeye ana kila kitu, pesa..na yupo juu ya sheria, aje aniue, ili moyo wake ufurahi, lakini mimi kamwe, siwezi kumpigia magoti,….fikisha huo ujumbe, mwambie nipo tayari kufa kwa umasikini wangu, ….’akasema na kuingia ndani.

‘Haya mama ujumbe umefika, ila nilichotaka kukuambia ni kuwa, yeye kasema hili lilitokea hapa ni aibu kwake, kwa vile hakujua kuwa wewe hukukubaliana na hilo, kinyume na alivyoongea mume wake,….kwake yeye ni kuzalilishwa, maana angelikwenda kumtafuta mwanamke mwingine, na wapo wengi wapo tayari kuolewa na yeye, ila alivumilia akijua binti yako keshakubali…..sasa…amesema, hataki kuiona sura yako,…..ni vyema ukaondoka kabisa hapa kijijini…..’akatulia aliposikia huyo mama akiongea huko ndani.

‘Haina haja ya kurudia rudia maneno, ujumbe wako umeshafika,…mimi leo hii naondoka,..nawaachia nyumba yenu na mtu wenu,….na ama kwa kuondoka hapa kijijini, yeye hawezi kunipangia niende wapi, yeye sio serikali,….nitakwenda kuishi popote nitakapo, ……’akasema na baadaye akatoka akiwa na mfuko wake uliojaa nguo zake na baadhi ya vyombo, akamgeukia yule mwanaume wake mlevi na kusema;

‘Nashukuru sana kwa wema wako, sina cha kukulipa zaidi ya kusema, ahsante, ….wema wako atakulipa mungu, na hayo ya kuniuza mimi kwa huyo tajiri wako, imenisikitisha sana, sikujua unanihukia kiasi hicho, na kwa hilo, sizani kama nitaweza kuishi na wewe nyumba moja,….nakutakia kila la heri….’akasema .

‘Sasa ndio umeamua kuniacha….huoni kuwa mimi natakiwa kwenda kujitundika…..yaani hunionei huruma,….maisha yangu yanakwenda kuisha kwa kujinyonga mwenyewe…..nakuomba usiniache, nisaidie ukaniombee msamaha,…..humjui huyo mtu alivyo, huwezi kabisa kumkimbia…’akasema akienda kusimama mbele ya mama Maua.

‘Sijamkimbia yeye, mimi nipo tayari kwa lolote analotaka kunifanya, kama anataka kunai aje tu, kwani nimebakia nini tena…..ila katu sitaweza kwenda kumpigia magoti….wewe nenda kampigia magoti, ….mwanume mzima unampigia mwenzako magoti kwasaababu ya pesa, au kwasababu ya kuwa yeye ni tajiri….aibu kubwa,…..’akasema akimkwepa huyu mwanaume na kupitia sehemu nyingine.

‘Haya wewe niache tu,….mimi kesho utasikia taarifa zangu, naomba ukiwaona watoto wangu wape salamu zangu, waambie nawapenda sana, na wanisamehe kwa tabia yangu ya kutokuwajali….na wewe pia anomba unisamehe, kwa haya niliyokufanyia, najua hutanielewa, lakini nilifanya hivyo kwa vile nakujali…..niliona nisikae na wewe, maana sina mbele wala nyuma….ukaishi na huyo tajiri, ….’akawa anafuta machozi.

‘Nisamehe sana……sio kweli kuwa nakuchukia, nakupenda sana, ndio maana nilitaka ukaishi kwenye hali nzuri, wewe hukustahili kuteseka na kuishi na mlevi kama mimi…kwaherini….akachukua pombe yake aliyokuwa nayo akaimalizia, akadondoka chini na kuwa kama amelala’ Yule jamaa akamsogelea na kumtimba kwa mguu, akasema;

‘Umeelewa lakini….usijifanye umelewa, ujumbe huo unaujua maana yake, usipofanya hivyo, atakuja mwenyewe, mtaonana, uso kwa uso…’akasema huyo jamaa.

‘Nimekuelewa mkuu….nitafanya hivyo, haya bwana, ….ngona niende nikafanye hivyo, simnataka nikajitundike, haya nakwenda kufanya hivyo,…..’akasema huku akiinuka na kuanza kutembea kilevi kuelekea huko kwenye miti mingi, ambapo mara nyingi wamekutwa watu wakiwa wamejinyonga.

Mama Maua akajikuta akisita kuondoka, akageuka na kumwangalia yule jamaa aliyekuja kufunga mlango, alyaona hayo kama maigizo ya kumteka akili, lakini hali ilivyoonekana kwa huyo mwanaume wake mlevi, ilimtia mashaka kidogo, akamwangalai huyo jamaa, ambaye kwa muda huo alikuwa kasimama mlangoni akisubiri, na macho yake yalipokutana na hayo ya mama Maua, akatabasamu na kusema;

‘Amajitakia mwenyewe, mtoto akililia wembe, mwache, …huyoooo, anakwenda kujitundika mwenyewe, hatuna la kufanya,…wewe kama nilivyokuambia….fanya yako, sahau kuhusu huyo mtu, ….msahau kama mliwahi kukutana,…. na….’akakatiza maneno na kujishika mfukoni, akasema;

‘Unajua mambo yamekuwa mengi, nimeshahu kukupa nauli yako,….hukua hii pesa, ni haki yako, na fanya hivyo, ondoka kabisa hapa kijijini….’akatoa pesa na kumsogelea yule mama.

‘Mimi siwezi kupokea pesa za huyo mtu, pesa zake ni chafu,….na kama niliwahi kuzitumia kabla,  hapo awali nilikuwa sijui yupoje, sasa kwa vile nimeshamjua, katu sitapokea pesa zake…..’akatikisa kichwa kwa ishara ya kukataa, na kuangalia pembeni.

‘Mimi tena,sitapokea pesa yake kwa njia hiyo,….labda iwe anakuja kununua kitu kwangu, kama nina duka, lakini sio kwa taratibu za kuuza utu wangu, nashukuru sana kwa huo wema wenu wa mitego, sina haja ya hiyo nauli mrejeshee mwenyewe…’akasema mama Maua akimwangaia yule mwanaume wake mlevi akitokomea kwa mbali kuelekea eneo lenye miti mingi.

‘Ina maana kweli anakwenda kujiua?’ akauliza mama Maua.

‘Wewe unafikiri anatania, ni bora akajinyonge, kuliko kusubiri adhabu ya huyo tajiri,…..kifo chake ni kichungu, ana mateso makali, muonenei hivyo hivyo tu ….yeye mwenyewe anamjua, ndio maana kaona bora akajitundike,…hana la kufanya, hiyo ni adhabu ya msaliti….anajua yote aliyoyafanya , yeye ni mwanachama, na ukiwa kwenye kundi ni lazima ufuate taratibu zetu…..’akasema huyo mtu.

‘Mwanachama wa chama gani?’ akauliza mama Maua akionyesha mshangao.

‘Hiyo ni siri ya wanachama,…..hustahili kujua,…..kwaheri mama Maua, kumbuka umepewa muda hadi jioni, kama utabadili nia, unakaribishwa, na huenda ukawa mwanachama mpya, …nakuhakikishia hutaweza kupata taabu tena…..mume wako, angelitulia na kuacha pombe, angelikuwa mtu mwingine, lakini …..mmh, kalogewa na pombe huyo…’akasema huyo jamaa akimazia kufunga ule mlango.

Mama Maua akawa kasimama huku kaduwaa, akiwa hajui afanye nini….aende kumuokoa mwanaume wake, au aelekee wapi, …hakuwa na sehemu ya kwenda, yeye alijiona kama yatima, hana baba wala mama, na mtu aliyekuwa akimtegemea ndio huyo anakwenda kujiua…..

Akaanza kutembea kuelekea huko alipokwenda huyo mwanaume wake….akawa anakimbia kumwahi, na alipofika mbali kidogo, alikutana na watu wakiwa wanakimbia kutokea huko, akawauliza kwanini wanakimbia

‘Kuna mtu akajiua……’mmoja akasema

‘Haiwezekani…’akasema mama Maua akitupa ule mfuko aliobebea nguo zake na vyombo na kukimbia kuelekea huko walipotokea hawo watu.

NB: Naona kila nijitahidi nmalizie hiki kisa, nahisi sitakitendea vyema. Kidogo kidogo, tutafika mwisho

WAZO LA LEO: Mkiishi pamoja, mkatendeana ubinadamu, japo kwa wema mdogo, hamtasahauliana, hasa pale mmojawapo anapofikwa na matatizo, hasa ya ugonjwa au msiba, kwani wema katu hauozi.

Ni mimi: emu-three

No comments :