Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, January 16, 2013

Uchungu wa mwana Aujuaye ni mzazi-49
Baba na mama, wakahamia sehemu nyingine, karibu na mji, na kuanza maisha mpya, maisha ambayo  yalikuwa magumu kuliko hata huko walipotoka, ukizingatia kuwa baba hakuwa na kazi, na kazi yake aliyokuwa akitegemea kule alipokuwa mwanzoni ilikuwa ya kuuza pombe, pombe yenyewe ya gongo. Sasa hapo walipohamia isingeliwezekana kufanya biashaa hiyo.

‘Sasa tutaishije hapa, maana hali ni ngumu, nimehangaika kutafuta vibarua kila kona , hakuna hata kazi ya kufagia kwa mtu’akasema baba huku akiwa kajiinamia kama mkiwa. Mama alimwagalia mumewe wa kufikia, maana walishakuwa kama mume na mke, japokuwa hawakuwahi kufunga ndoa.

‘Sasa tutaishije na kodi ya nyumba inahitajiwa,….je watoto wako hawawezi kukusaidia kulipia kodi ya nyumba, maana tangu tuhame kule, siwaoni kabisa wakifika hapa, wamekwenda wapi?’ akauliza mama.

‘Achana nao wale wahuni, …..siku hizi wanajiona wamekuwa, ..tabia zao hazina tofauti na alivyokuwa mama yao….’akasema na kuinuka. Siku hiyo alikuwa hajalewa, na baba akiwa hajalewa ni mtu mwema kabisa, tatizo ni pombe, na wakati mwingine niliombea asipate pesa, maana akipata pesa, yeye ni kukimbulia kununua pombe.

Baadaye akarudi bila kutarajia, alikuwa kama kasahau kitu, mara akasogelea pale mama anapoweka biashara zake za vitumbua, na kusema;

‘Biashara yako ya vitumbua leo haikutoka?’ akauliza huku akipekua pale mama anapoweka pesa zake za biashara

‘We…acha hizo pesa, ..ndio pesa ya kununulia unga wa ngano, ..nataka nijaribu kupika maandazi kesho,…acha…..’akasema mama na kukimbilia kumzuia baba asichukue pesa, na baba akawahi kuchukua pesa kidogo na kukimbia nazo, na hapo tulijua akirudi baadaye kutakuwa hakukaliki atakuwa sio yeye, maana pesa kidogo kwake, ni nyingi, atakunywa ….kwa hadaa hadi atalewa.

‘Mwanangu haya maisha yananishinda, hali yangu kama unavyoiona, kila siku kuumwa, na naumwa kwasababu ya kukosa chakula bora, na hizo biashara za kupika maandazi na huo moshi wake, unaniathiri sana kifuani, sipati pesa ya kununulia maziwa , maana biashara kama hii inahitaji maziwa, …lakini nitafanyaje,…nashukuriu nimekulea na sasa umefikia hatua hiyo, umeshafunja ungo, kilichobakia ni ujitulize upate mume akuoe, ….

‘Mama umeanza , …..mume ,mume hawo waume ni wa kuokota kama njugu,….hata hivyo mama, mimi bado mdogo, sijafikia makamo ya kuolewa…..mniache kabisa, kama mumepanga kuniozesha ili mupate pesa,…hilo msahau’akasema Maua.

‘Baba yako kasema kuna mwanaume anataka kukuoa…’akasema mama.

‘Nilijua tu….kama mnataka niwakimbie, mnitafutie mume, …kwanza ni mwanaume gani huyo,….?’ Akauliza Maua.

‘Mimi sijakubaliana na hilo wazo la baba yako,…..na nisingelikubali kamwe, maana huyo hakufai mwanangu, ni mwanaume wa kuoa na kuacha….lakini kaahidi kuwa akikuoa wewe hata kuacha kamwe’akasema mama.

‘Kwanini, anaoa na kuacha, hamuona kuna tatizo hapo….mama….’

Mara mlango ukagongwa, na mama na binti yake wakaangaliana, wakijua huenda ni baba mtu kesharudi, na mama akatoa ishara binti aende chumbani akajifungie,….

‘Hodi hapa wenyewe hawapo’sauti iliyosikika ni ya kike, iliyomfanya Maua asimama, kwani alishaanza kukimbilia chumbani kwake, na mama mtu akasogea pale kwenye mlango na kufungua kwa kusita. 

Wamekuwa wakiishi hivi kwa wasiwasi, kutokana na madeni wanayoandamwa nayo, na  wakati mwingine inabidi wajifungie ndani kuogopa watu ambao wamevumilia kwa muda bila kulipwa madeni yao, na wengine subira imewaishia wanataka kuchukua hatua nyingine ya kupiga.

‘Oooh, ndio wewe ndugu yangu, upo dunia hii,….’huyo mgeni akasema huku akimwangalia mama huyo bila kuamini. Mama alikuwa kasimama mlangoni, na alionyesha kuwa hataki huyo mgeni aingie ndani, na Maua akawa na hamu ya kumuona huyo mtu ni nani.

‘Najua wengi mlishajua kuwa nimekufa, na huenda mumeshanitengenezea kaburi’akasema mama Maua.

‘Masikini mbona upo hivyo, unaumwa…..umekwisha unaonekana mzee kuliko umri wako, vipi kulikoni?’ akauliza huyo mgeni akiwa bado huko nje.

‘Naumwa natesekeka, …hayo hayawahusu, mimi kwetu ni maiti….’akasema mama

‘Usiseme hivyo ndugu yangu wee….wewe na mimi tumekuwa pamoja, urafiki wetu ni zaidi ya udugu, umesahau hilo’akasema huyo mgeni.

‘Hilo siwezi kulisahau ndio maana nikaongea na wewe, sikutaka kukutana na ndugu yangu yoyote, mimi kwa sasa sina ndugu, mimi hapa nilipo nina kila aina ya shida hapa dunia, na sijui nikimbilie wapi, maana huenda bora ningeliongozana na watu wa msituni nikaenda kuishi huko’akasema mama Maua.

‘Watu wa msituni, unawajua au unawasikia, Usiseme hilo kabisa, yaani unataka ukaishi na watu wanaokula watu’akasema huyo mgeni.

‘Hizo ni hadithi, za kufikirika,…hawo watu wa msituni ni wastaarabu kabisa, hawali watu, na wao wanasikia hivyo hivyo kama unavyodai wewe, kuwa kuna watu wanaokula watu…’akasema mama Maua.

‘We jidanganye tu, hawo, wanakuchukua na kukulea vyema unone, baadaye wanakufanya kitoweo, ..haya niambie maana siamini macho yangu, mbona hunikaribishi ndani, au mumeo hataki wageni,na …mumeo yupo wapi, maana ni lazima una mume unayeishi naye hapa…niliwahi kupita nikamuona mwanaume mmoja akiwa bwiii?’ akauliza.

‘Kwahiyo unamuhitaji yeye, au unanihitaji mimi ndugu yako?’ akauliza.

‘Wote mumeo ni shemeji yangu, ni lazima nimjue,..’akasema huku akiingia ndani na macho yake yakamuona huyo binti, na akashikwa na butwaa akimwangalia yule binti.

‘Ohhh, huyu mrembo ni binti yako…yaani huyu, kama angelikuwa mjini, mbona ungelikuwa huna shida’akasema huyo mgeni

‘Kwanini unasema hivyo?’ akauliza mama Maua kwa mshngao.

‘Binti kama huyu anahitajiwa sana huko mjini,kwa wanamitindo,..ni mrembo wa kutosha….ooh, umbile lake, …mashalaah, unaitwa nani binti?’ akauliza huyo mgeni. Maua akasita kidogo halafu akasema kwa upole;

‘Mimi naitwa Maua..’akasema

‘Utaitwaje jina la mama yako,..usinitanie , mimi ni mama yako …’akamsogelea na kumshika begani, huku akisema;

‘Mama yako huyo na mimi ni ndugu tumechangia babu…yaani babu yetu ndiye aliyemzaa baba yake, na pia ndiye aliyemzaa baba yangu,…’akasema huku akimwangalia huyo binti kwa makini, toka juu chini na akawa anarudia kumwangalai hivyo hivyo mara nyingi.

‘Mimi sijui kama mama yangu ana ndugu, nilijua kazaliwa peke yake, maana matatizo aliyo nayo, ni makubwa, kama kuna ndugu yake kwanini mama hajawahi kwenda kuwaona….’akasema huku akimkwepa huyo mgeni kuangaliana naye usoni.

‘Ni matatizo tu ya kidunia, yaliyotokea huko nyuma, hakuna aliyependa yatokee hivyo,…na chanzo ni wewe,….’akatulia kidogo.

‘Kwanini chanzo iwe ni mimi, na huenda nilikuwa sijazaliwa?’ akauliza Maua.

‘Mimba yako ndiyo iliyozua balaa lote hilo…..baba mtu akapandisha na kuwa simba…ilikuwa balaa wewe, sijui leo mkionana atasema nini, lakini hayo yameisha nasikia hata mwenyewe anajuata, na anasema yeye hajui ni nini kilikuwa kikimtokea,….anamkumbuka sana binti yake, na anatubu sana kwa hayo yaliyotokea’akasema huyo mgeni.

Mama Maua alikuwa katulia kimiya akiwa kaangalia chini, alitamani kumwambia huyo mgeni aondoke, asimkumbushe yaliyopita, yeye, alishaandika kuwa hana ndugu, na hataki kuonana na ndugu yoyote yule, hata wazazi wake, ndio kabisaa….

‘Sasa huyu binti una mipango gani nay eye?’ akauliza huyo mgeni, na hapo mama Maua akainua uso , uso ukaingiwa na nuru, maana akilini alikuwa akitafuta njia ya kumuondoa huyo binti hapo, kwani baba mtu, anataka aolewe, na huyo jamaa anayetaka kumuoa, sio mwanaume mwema, na shikiniko hilo limekuja kwa vile muwewe huyo anadaiwa pesa nyingi na huyo jamaa.

‘Mke wangu huyu jamaa anayetaka kumuona binti yetu, ndiye aliyetukopesha pesa ya kodii yah ii nyumba, ujue kuwa hii nyumba ni yake, na aliamua kufanay hivyo, kwa vile ananitumia kwenye biashara zake, ..hata ile pombe, ..yeye ndiye mdhamini,…mtaji wote ulikuwa ukitoka kwake, sasa tukakimbilia huku nikijua nimemkwepa, ….kumbe tunaingia kwenye  yake…’akacheka kicheko cha dharau.

‘Usiniambie lolote kuhusu huyu binti yangu…madeni yako ndiyo yafanye aolewe na wanaume nisiwajua, kama ni tajiri wako, mnajuana wenyewe……hilo sikubalini nalo kabisa’akasema mama Maua.

‘Utakubali tu…hatuna jinsi, mwenye pesa mpishe, …’akasema na kuondoka.

*****

‘Binti yangu, kama nilivyokuambia, baba yako kashinikiza kuwa uolewe na huyo mtu wake, na hutaamini, eti keshaanza kupokea sehemu ya mahari…’akasema mama Maua.

‘Mama mbona siwaelewi, yaani mpokee mahari wakati hata mume mwenyewe simjui,….’akasema Maua huku akitoa jicho kumwangalia mama yake.

‘Unamjua sana, huyo baba anyekuja na zawadi kila siku , ….’akasema mama mtu.

‘Ina maana zawadi hizo alikuwa akitoa kama chambo, mama, mtaolewa wenyewe,….mimi sikubali kwa hilo, yaani mimi nikaolewe na huyo mzee, sikubali kabisa…simpendi, namchukia, na nilikuwa napokea zawadi zake nikijua ni mgeni wa hapa, na sikujua lolote kuhusiana na hilo, maana nakuomba sana, kama hamnitaki nikae hapa, nitajua wapo pa kwenda na kwa vile umeshasema kuna ndugu zangu,…nitawatafuta’akasema.

‘We…acha kabisa kuhusu hayo, hakuna ndugu yako hapa, sina ndugu kabisa, watu waliotaka kuniaua, leo hii uende kwao, hilo sitaki kulisikia, kama ni kwenda kwao uende nikishakuwa sipo duniani..’akasema mama huku machozi yakimlengalenga.

Walitulia kwa muda, huku mama mtu akiwaza jinsi gani ya kumuondoa mtoto wake hapo nyumbani, na akaliona wazo la huyo ndugu yake aliyejitokeza , ambaye utotoni walikuwa marafiki sana, na ndio maana  alipokuja hapo na kuonana naye hakuwa na ubaya naye, japokuwa alishaapa kuwa hataki kuona ndugu yake yoyote.

‘Yule mgani aliyekuja jana, kasema huko mjini kuna kazi,….anataka akuhukue mkaishi naye huko, na atakutafutia kazi, na hata kukusomesha …hapa darasa la saba umemaliza kwa bahati, siku uankwenda shule, siku nyingine huendi, lakini huko mjini ataweza kukutafutia sehemu ukasoma vizuri zaidi…’akasema mama mtu.

‘Mama hilo ndio wazo…mimi ndoto yangu yote ni kwenda kuishi mjini….hilo mama ndio wazo, na akija tu huyo mgeni mimi nipo tayari tutaondoka naye, na wala usimwambie baba,….’akasema Maua.

‘Sitamwambia lakini balaa lake sijui kama nitaliweza, tuombe mungu, ….’akasema mama huku akiwa kashika shavu

NB: Hiyo ni sehemu ndogo kwa leo. Na tunatarajia kuingia kwenye hitimisho

WAZO LA LEO: Ugumu wa maisha na shida zake, anayezijua ni mtu mwenyewe na maisha yake.

Ni mimi: emu-three

5 comments :

Yasinta Ngonyani said...

Duh! nimechelewa kweli hapa ..maana sasa inabidi niongeze spidi kali kweli kuwa pamoja nawe...Nimependa wazo la leo na kazi yako nakuamini..Pamoja daima

emu-three said...

Duuh, umesharudi majuu bila kuaga, kweli ww ni mngoni asilia.

emu-three said...

Mpaka sasa hivi najiona kama naongea peke yangu,....Je niendelee au nikatize?

EDNA said...

Jirani heri ya mwaka mpya.

Anonymous said...

Usuallу I don't read article on blogs, however I would like to say that this write-up very pressured me to take a look at and do it! Your writing taste has been surprised me. Thank you, quite great post.
Feel free to surf my web blog ... hvor meget kan jeg låne