Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, January 9, 2013

Uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi-45
Mama alinilea kwa shida sana, ikizingatia kuwa mwanamue aliyekuwa akiishi naye ni mlevi, na hakuwa akimjali sana kama mke wake, na mimi mwenyewe aliniona kama mzigo aliobebeshwa na hata kufikia kuniita mtoto wa haramu….’aliendelea kuhadithia kisa hiki huyu binti.

Kama utakumbuka sehemu ya kwanza, nilipokutana na huyu binti nilimuuliza wazazi wake wapo wapi, na jibu alilonipa ndilo lililfanya tuchimbue undani wa maisha yake kuanzia kwa wazazi wake. Tumefanya hivyo, ili kuonyesha kuwa taabu, shida, maumbile na tabia inaweza ikatokana na historia za kimaisha.

Hebu turejee sehemu hii, kwanza ili tuwe pamoja;

‘Habari yako binti?’ nikamsaili na akawa kama kashituka aliposikia sauti yangu na kitu cha kwanza alichofanya nikujiweka vyema.

‘Sija-shikamoo..’akainuka pale na kusimama huku akisalimia kwa kigugumizi akaishika ile ndoo na kuangalia huku na kule.

‘Samahani nilikuwa napita tu, bahati nikakukuta ukiwa katika hiyo hali, kwanini upo hivi na asubuhi hii, na jinsi ulivyovaa, huoni kuwa unaweza kuumwa na magonjwa ya ubaridi?’ nikamuuliza.

‘Kama nikuumwa nimeshaumwa sana, na taabu niliyo nayo anayejua ni mungu, iliyobakia ni siku ifike roho yangu itolewe tu, ili nikapumzike huko ahera, ingawaje sijui kuwa kuna kumpumzika huko mbeleni lakini naona ni heri tu nijifie…na ipo siku tu, nitaamua moja, maana nimechoka,kwanini mimi…’akasema huku machozi yakimtoka.

‘Kwanini uwaze hivyo,hujui kujiua ni dhambi, ni sawa na kuua mtu’nikasema nikiwa nahisi kuwa anaweza kweli akafanya hivyo.

 ‘Mungu ndiye anyejua ni kwanini nawaza hivyo, kwani hakuna ambaye nitamsimulia matatizo niliyo nayo akanielewa, hakuna atakayejua jinsi gani ninavyoteseka, na ninaendeela kuteseka, hakuna anayejali, …. Ina maana mimi nilizaliwa katika dunia hii ili nije kuteseka, hapana,….labda sistahili kuishi’akasema huku akifuta machozi.

‘Kwani wazazi wako wapo wapi?’ nikamuuliza.

Sasa tumalizie sehemu hiyo ya Wazazi wako wapi, na baadaye tukijaliwa tutaendelea na sehemu inayoonyesha mateso ya huyu binti ambayo yanampelekea hadi kutaka kujiua…..

******

‘Wewe mwana...haha-ramu, mbona hujafagia huku nje?’ baba akasema kwa ukali, huku akionyesha kuwa kalewa, na hata chakula hajala. Maua alimwangalia baba yake huyu wakufikia, inabidi amuite baba, kwani ndiye anayemulea,…kwanza alimwangalia kwa huruma, na baadaye alipoliwaza hilo neno `mwanaharamu’ hasira zikampanda.

Siku zote alizokuwa akiishi na baba huyo, amekuwa makini sana, kama alivyoagiza na mama yake kuwa akimuona huyo baba kalewa, ajaribu kuwa mbali na yeye, na wala asijibishanne naye, lakini siku hiyo hasira zilimpanda akaamua kumtolea maneno.

‘Baba kwanini unaniiita jina hilo?’ Maua akamuuliza huyo baba kwa hasira

‘Jina gani nimekuita, …na kwanini nakuamrisha jambo badala ya kulifanya unanishikia kiuona na kusema..kwanini…nenenene…’akasema huku akipepesuka.

‘Baba hivi unafikiri mimi nimependa kuwa hivyo, kuzaliwa hivyo, …sikupenda kabisa, hata mama hakupenda itokee hivyo, yote ni majaliwa ya mungu, kuzaliwa kwangu kwa  njia hiyo sio sababu ya kuniona sina maana, sina haki kama watoto wengine. Kwani mimi sikupenda na wala sikuingia mkataba na mama yangu, aje anizae hivyo…nasikitika sana ukiniita hilo jina….’akasema Maua.

‘Bado unatoa hotuba yako…eeh, au kwa vile umeshaanza kuota maziwa eeh, unajiona umekuuuuwa ee….huna lolote wewe…kwanza, nimewabeba saana, na nimechoka, mama yako kila siku kuumwa, anaauuumwa weeee, hadi anatia kero, au anakwepa ili asiwe mke wangu…’akasema huku akijikakamua asianguke.

‘Baba kwanini unaniita mwanaharamu, …mimi hayo ya mama sijakuuliza, nakuuliza kwanini unaniita hilo jina, kila siku, mwanaharamu, nani mwanaharamu….mbona akina kaka huwaiti hivyo, ….’Maua akasema kwa sauti ya huzuni.

‘Ahaaah, kumbe,…ina maana muda wote unazunguka tu, hutaki kusema kwanini.. , kumbe umekasirika kuitwa mwana…haraaamu, kwani ni uwongo, kama sio uwongo, niambie baba yako yupo wapi….?’ Akauliza huku akiwa kashika kiuna.

‘Baba yangu ndio wewe maana mimi nimekulia kwako, tangu nikue sina baba mwingine zaidi yako,nimjikuta nikiishi hapa na wewe, na nikuulize kaka zangu mama yao yupo wapi, kuna tofauti gani kati yao na mimi, wao mama yao hayupo, na mimi baba yangu hayupo,….’akasema Maua.

‘Acha hiyooo’akasema huku akiushusha mkono kama vila askari anavyotoa heshima kwa mkono. Akawa anatembea kuelekea mlangoni, na kipindi hicho mama yake Maua alikuwa kasimama mlangoni, tayari kumtetea mwanae akijua kuwa huyo baba anaweza kukimbilia kumpiga mwanae, maana mara nyingine akirudi, akiuliza jambo akabishiwa, yeye hukimbilia kupiga.

Alipokaribia mlangoni, akashituka, kumbe alikuwa hajui kuwa mama Maua yupo pale mlangoni, akasimama na kuinua kichwa kama vile haoni, au macho hayataki kuona mwanga wa jua, akasema;

‘Na wewe mwanamke, umepika nini?’ akawa anatikisa kichwa juu chini, huku akiwa kama anatafuna meno.

‘Nipike nini, kwani ulipoondoka uliacha nini, hukuniachia hata senti moja, ningepata wapi pesa ya kununulia chakula’akasema mama yake Maua.

‘Unaona…..unaona hii ndio shukurani yenu,mumekaa tu hapa kama vile mpo nyumba ya wageni, hamuhangaiki, mnasubiri mimi na wanangu tuwahangaikie, nyie mumekaa hapa nyumbani kama wanawali, au mnasubiri kuolewa, oleweni basi nipate hayo mahari…’akasema huku akicheza cheza kuashiria harusi.

‘Juzi nilikuambia niondoke nikatafute vibarua ukasema nikiondoka hapa nyumbani atakaa nani,…leo tena umebadilika, unatusakama kuwa tunakaa tu, kazi gani tutafanya bila mtaji, bila kutoka ….?’ Akauliza.

‘Wewe unajua kazi wewe…,mwanamke uliyelelewa msituni, labda, ukawinde,..kwanza nataka uvae yale mavazi yako ya msituni, maana mkiyavaa yale mnapendeza, matiti nje..hahaha…..hebu kayavae unikumbushe enzi zile….’akasema huku akiwa kashika kidevu.

Na wakati anaongea hayo, mama Maua machozi yakawa yanamtoka, akikumbuka matukio ya nyuma, akikumbuka hayo maisha anayoishi, hajui afanye nini tena. Alimwangalia binti yake, ambaye sasa keshakuwa mkubwa, lakini bado anastahili kuwa na wazazi wake, asingelipenda kuachana naye. Mara mbili alijiwa na watu wa masituni wakitaka wamchukue, na kama yeye hataki bai wamchukue huyo mtoto, lakini hakukubali.

‘Sipendi mtoto wangu akaishi msituni….’akasema kimoyo moyo. Na wakati amesimama pale akimwangalia binti yake huyo, mara akili yake ikarudi nyuma na kukumbuka siku ile alipotembelewa na ujumbe mnzito, ujumbe wa malikia , na wivu ukawa ume,mwingia …lakini ilibidi ashukuru na kuushukuru ule ujumbe.

‘Kwanini namuwaza sana huyo mwanaume?’ akajiuliza na hata ule ujumbe wa kwanza ulipofika, bado ile hali ya kumuwaza huyo mwanaume ndio ulizidi, kwani hakujua lolote kuhusu huyo mwanaume kuwa alikuwa ni nani, zaidi ya kumjua kama mwanaume aliyekuwa kajifunika uso. Akakumbuka ule ujio wa malikia kwenye kibanda cha miti na majani, ambapo walikimbilia na kujificha.

***********

‘Wewe mwanamke kuna wageni huku nje?’ alisikia sauti ya kilevi ya mume wake. Na aliposikia hivyo akatokeza kichwa chake kwenye upenyo wa majani yaliyozungushiwa nyumba  na kuangalia kwa nje, kwa vile nyumba yenyewe ni ya miti na kuta zake zimezungushiwa majani, ukishika yale majani sauti inasikika, kwahiyo wale watu waliopo nje waliona lile tendo.

‘Ndipo mnapoishi hapa, kwanini mumekimbia nyumba yenu?’ akauliza malikia pale walipokuwa wamekaa pamoja akina mama hawa wawili.

‘Ilibidi tukimbie, maana tuliogopa kuwa watu wa msituni watakuja kulipiza kisasi, kwa vile mume wangu anahisi alivyompiga yule mama aliyedhamiria kunidhuru ili kumchukua mtoto, atakuwa ameua…’akasema mama Maua.

‘Sina uhakika na hilo,…kwani hakuna anayejua wapi huyo mama alipokwenda, na kama kafa au kakimbia, kwani hata hawo akina mama wengine unaowaona hapo nje, wanamkimbia mzee hasimu. Siunamkumbuka yule mzee kwa sheria zake, za ukatili’akasema malikia.

‘Kwahiyo wanakimbilia wapi hawo akina mama?’ akauliza mama Maua.

‘Wamekimbilia kwangu,..wanahitaji niwalinde mimi kama mama yao?’ akasema.

‘Wewe kama mama yao?’ akauliza Mama Maua kwa mshangao.

‘Ndio taratibu za huko malikia ni mama wa jamii, na mama wa jamii, ni kama mama mzazi wa kila raia, na wote wanamuheshimu sana malikia,..hata huyo mzee hasimu na ukatili wake , anaponiona mimi ananywea na kuniheshimu..’akasema malikia.

‘Basi una bahati kubwa sana, sasa kwanini mimi walitaka kuniua?’ akauliza.

‘Hizo ni sheria za mzee hasimu, na ni imani kuwa mtu akizaa bila mume, ..na hasa mgeni, anakuja kuleta mikosi….na hili tumelijadili na mume wangu, tutahakikisha kuwa linaondoka, na tutahakikisha taratibu potofu tunaziondoa’akasema malikia.

‘Ina maana mume wako alikuja kushinda, na kuwa mtawala?’ akauliza

‘Ndio, japokuwa alishinda kwa shida, na hata hivyo, bad hajatambulika na kusimikwa kama mtawala, kwani siku naondoka kulikuwa na kikao cha usuluhishi, nimesikia kuwa mzee hasimu, kapatwa na majanga, ….’akasema.

‘Majanga gani,…?’ akauliza Maua na kabla hajajibiwa hilo swali, mtoto akawa analia, na wote wakageuka kungalia huko sauti inapotokea

‘Huyo mtoto gani anayelia?’ akauliza malikia.

‘Ni mtoto wangu…..’akasema Mama maua.

‘Mtoto wako, ulimpataje mtoto wako, maana ujio wetu ulikuwa mahususi kukupa habari za kupotea kwa mtoto huyo.

‘Yaani yote ni miujiza, sijui nilipata wapi ujasiri huo, ….siwezi hata kusimulia, …na siku ile niliamua kufa au kupona, na hata hivyo namshukuru sana huyu mwanaume, kama singelikuwa yeye, yule mwanamke angeniua na kumchukua mtoto….’akasema.

‘Sisi tulikuwa tukifuatilia hilo kwa karibu, wasingeliweza kumfanya lolote, …watoto kama hawo wanalelewa kwenye sehemu yetu takatifu, wanaheshimika, ….tunajua walitaka kumchukua kwasababu za kisiasa…’akasema.

‘Kwanini mtoto kama huyu ahukuliwe kwa sababu za kisiasa?’ akauliza

‘Kwanza walihitaji kupata nasafi za kiutawala, pili kijana wa mzee hasimu alitaka kumchukua huyu mtoto awe ni mtoto wake, ili pia awe karibu na mimi, kwani lengo lao kubwa ni kunitaka mimi niwe mke wake’akasema malikia.

Mama huyu aliinuka na kwenda kumchukua mtoto ndani, alipoona kuwa hakuna tatizo lolote, na alipomleta wale akina mama walioongozana na malikia wakamchukua na kuanza kumnywesha maziwa waliyokuja nayo

‘Nashukuru sana kwa zawadi hii ya maziwa, ….umeniokoa sana’akasema mama huyu huku machozi yakimlengalenga. Akiwaza jinsi gani anavymlea mtoto huyo kwa shida, maziwa kama hayo kuyapata ni shida, …

‘Kwani mnaishije na huyo mwaname, maana namuona ni mlevi sana?’ akaulizwa.

‘We acha tu….nashindwa nifanyeje..isingelikuwa huyu mtoto, ningelitokomea mbali kabisa, lakini nahitaji nimlee huyu mtoto akue kidogo,…tatizo linakuwa jinsi ya kupata maziwa , kwa vile sikuweza kumnyonyesha maziwa yangu baada ya kuwa mbali naye kwa muda mrefu…’akasema kwa uchungu.

‘Usijali, …kama itawezekana tunaweza kutafuta mtu wa kukuletea maziwa mara kwa mara,….nitamuambia mume wangu’akasema malikia.

‘Sizani kama huyo mlevi atakubali….’akasema mama Maua

‘Kwanini asikubali kwani ameshakuwa mume wako?’ akauliza.

‘Hapana, sio mume wangu, ila anavyonifanyia …..nashindwa hata kuelezea, japokuwa wakati mwingine akiwa hajalewa ni mtu mwema sana,namshukuru kuwa anajitolea na kuniona kama mtu wa familia yake, kwani hali ilivyo,ningelikwenda wapi,….naogopa hata kwenda kuwatafuta ndugu zangu,….’akasema kwa uchungu.

Walitulia kidogo, kila mtu akitafakari jambo, na hapo, maua akamwangalia malikia, jinsi alivyovaa, na hali aliyokuwa nayo kama malikia, na ghfla akamuuliza.

‘Ina maana mume wako sasa hivi ndiye kiongozi,kama alivyokuwa mzee hasimu?’ akauliza.

‘Ndio, …’akasema malikia akionyesha kuwa muda umefika anataka kuondoka.

‘Na huyo mwanaume aliyekuja kuniokoa ndio nani, ….naomba nionane naye nimpe shukurani zangu’akasema akimkumbuka huyo mwanaume ambaye hakuwahi kumuona sura yake, na kila mara alikuwa akimuota kwenye ndoto zake.

‘Ina maana hamjui na hakuwahi kujitambulisha kwako?’ akauliza malikia.

‘Muda wote alikuwa kajifunika uso wake…..na ni mtu mwema sana….mwanamke yoyote anahitaji mwanaume kama huyo, ambaye anajali maisha ya wenzake, ana huruma…na sijui nikumuona tena nitamshukuru vipi..’akasema na malikia akatulia kwa muda, akamwangalia Maua, halafu akamwangalia yule mtoto.

‘Mtoto wake jina lake ni Maua, tuliamua kumpa hilo jina kwasababu yako, wakina mama wengi, wanakukumbuka sana, kwa ujumla hawakufurahishwa na tendo uliloanyiwa,….kwasasa siwezi kukuambia lolote, lakini hali ya kisiasa ikiwa shwari tutakuja kukuchukua ….’akasema na mara yule mwanaume mlevi akaifika.

‘Mje mumuhukue nani, ….yaani nyie mnamteleekza mtu, mlitaka kumuua, halafu…..eti mnataka kuja kumchukua, hatoki mtu hapa….’akasema huku akiyumba yumba, japokuwa pombe zilishaanza kumtoka.
Malikia alimwangalia yule mwanaume, halafu aakgeuka kumwangalia yule mtoto,..moyoni akawaza mengi, aliona heri wangelikaa na huyo mtoto, kuliko kumuachia aishi hapo, lakini hakuwa na uwezo huo tena,…..

‘Haya sisi tunaondoka, tunshukuru sana kuwa mtoto amepatikana, na …safari ijayo tutakuja mimi na mume wangu,…’akasema malikia.

‘Na naomba mkija mje na huyo mwanaume aliyeniokoa….tafadhali mtafuteni popote alipo, …’akasema Maua.

‘Hilo usijali,..tutakuja naye….’akasema malikia huku akitabasamu,….na akafunua mdomo ili kumuelezea ukweli, ….

NB: Ni nini kitaendelea baadaye.

WAZO LA LEO: Wakina mama wengi husihi katika maisha ya dhiki , mateso, na hali mbaya ya kiuchumi, na wengi wameolewa, lakini hawajui kabisa raha ya ndoa. Je ndoa ni mateso, je kuolewa ni kifungo ha utumwa? Hapana, hilo sio kweli, tatizo kubwa ni uelewi mdogo wa nini maana ya ndoa, na wanandoa kutokuwa na uhuru, elimu na uthubutu wa kukaa pamoja na kujadiliana kuhusu ndoa yao. Wazazi na jamii wanachangia kwa hilo. Tusaidieneni, kulitatua hili, kwani ndoa ndio chimbuko la familia zetu, zikiwa safi, jamii itakuwa safi, yenye amani na furaha.
 

Ni mimi: emu-three

No comments :