Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, January 4, 2013

Uchungu wa mwana Aujuaye ni mzazi-43




Hebu turejee kidogo siku ile ya kikao cha usuluhisho;

Kijana mtarajiwa akageuka kumwangalia mzee wake, ….mzee wake alikuwa kamkazia jicho, akageuka upande wa msaidizi wake, na mshauri wake mkuu, huyo alikuwa kainama chini, na hakutaka kabisa kumwangalia, akamgeukia jemedari wake wa majeshi, ambaye yupo tayari kufa na yeye, na kwa mara ya kwanza alimuona huyo jemedari kaangalia chini….

Je hawa wote baadaye walienda wapi, mshauri mkuu na jemedari au mkuu wa vikosi vya hasimu, walipotoka hapo walikimbilia wapi,…..

Na ukumbuke mkuu wa vikosi hivi vya majeshi ni kaka wa yule kiongozi aliyekutana na malikia huko msituni, je ni kwanini huyu mdogo mtu, alipomsogelea malikia alidondoka na kuanza kutoa damu mdomoni…..tuendelee na kisa chetu tuone visa vya watu wa msituni, ……..

*******
Mkuu wa vikosi vya mzee hasimu, aligeuka na kuangalia ndani, alitaka kurudi ili amweleze bosi wake, kuhusu taarifa aliyoipata, kuwa mdogo wake hali yake ni mbaya sana na huenda keshafariki. Alijua kuwa kuondoka kwake hapo ni kinyume cha sheria, na sheria kwa muda huo, ambao ulikuwa kama vita, ilikuwa ni amri moja toka kwa jemedari, haijali tena familia ….akageuka kuangalia ndani, akakumbuka maji ya yamini,...

‘Siwezi kunyanywa hayo maji, kuyanywa ni kujitakia matatizo, na ili nisiingie kwenye huo mtego, ni bora kabisa nisiingie ndani…’akawa anaongea peke yake.

Alijua kabisa madhara ya kuyanywa hayo maji, hasa ukiwa umetenda hilo unaloapiziwa, madhara yake ni makubwa sana, na madhara yake hayaiishi kwako tu, madhara hayo yanakwenda mbali zaidi, hata kuathiri kizazi na kizazi.

‘Japokuwa familia yetu ina julikana kwa ubaya, lakini sitaweza kujiongezea tatizo,…sasa hivi nipo kwenye tatizo, maana nimeanza kukiuka mambo niliyoagizwa, kwasababu ya kubanwa na kazi za mzee hasimu…’akawa anaongea peke yake.

Akiwa kainama kwa uchungu akakumbuka maongezi yake na babu yake miaka ya nyuma,…..

‘Kijana sisi ukoo wetu kama unavyouona, ni ukoo tajiri na ukoo unaoogopewa sana, na tuna kiti maalumu kwenye serikali yetu, na kiongozi wetu anatuhitajia sana. Baba yako alikuwa mmoja wa kiongozi muhimu kwenye jeshi, na sasa wewe umechaguliwa kwenye nafasi hiyo, ina maana kila mwaka kama uongozi utakuwa huu huu, kiti chetu kipo pale pale…’Babu yake akasema.

‘Tunajua wewe ni jasiri katika kupigana , lakini ujasiri wako huo haukuja hivi hivi,….kuna watu wamejitolea, kuna mambo yamefanyika mengi ya hali ya juu hadi tukafikia hapo.Na ukoo wetu ni mkubwa sana, huenda tunaongoza kwa ukubwa katika koo za jamii zetu, japokuwa wengine hawajataa kujinasibisha na ukoo wetu, kwa vile wanaogopa kuambiwa wanatokana na ukoo wanaouita wa kichawi, hayo hayakutokea hivi hivi…’akasema babu yake huyo

‘Sasa ilikuwaje, na kwanini ukoo wetu uwe ni mkubwa, lakini sio viongozi kama alivyo mzee hasimu?’ akauliza huku akimwangali babu yake kwa makini.

‘Ndio maana tumekuita hapa, kwani umeshakabidhiwa uongozi, wa kuongoza majeshi ya eneo letu, na huo utakuwa ndio mwanzo wa sisi kuongoza eneo hili, kama utafuata masharti….masharti ambayo babu na babu zako walifuata…..na kama tusipofanya juhudi hizo kwa sasa, ..sizani kama itawezekana tena…’akaambiwa

‘Mimi nipo tayari kuyafuata hayo masharti kama yatafanya ukoo wetu uongoze nchi hii…’akasema akiwa anawaza kumpata msichana ambaye anatarajiwa kuchukuliwa na kijana wa mzee hasimu. Msichana huyo alimpenda sana, lakini juhudi zake ziligonga ukuta pale alipoambiwa kuwa ni mpenzi wa kijana wa mzee hasimu.

‘Kijana, kuna mambo mengi ambayo babu na babu zako wamekuwa wakiyafanya, ndio maana hata wakismama kwenye jukwaa kila mtu anatetemeka, na hata tukipita mitaani, kila mtu ananywea, na wengine wanaogopa hata kutuongelea ubaya…..hiyo ni kutokana na juhudi za wazee wa ukoo wako…

Kijana huyo aliposikia hivyo, akashituka, akakumbuka siku akiwa mdogo aligombana na mwenzake na vijana wengine waliokuwa karibu na yule mgomvi wake, wakaanza kusema kuwa huyo kijana kajitakia matatizo, kesho haitafika, atakuwa maiti…wakamsogelea yeye na kumuomba msamha kuwa yeye asiende kusema nyumbani….

‘Lakini yeye ndiye mgomvi, na kaniumiza, sikubali kabisa….’akawa anajitutumua kupigana, lakini hakuweza kupambana na huyo mgomvi wake kwa vile yeye bado alikuwa mdogo na mwenzake alikuwa kamzidi kiumri na hata nguvu.

Wenzake wakamsihi sana, na yule mgomvi wake naye ikabidi amuombe msamha, na hapo akahisi kuna jambo limejificha ndani ya ukoo wao. Na aliporudi nyumbani na kumuuliza baba yake kwanini wanaogopewa, hivyo, na kwanini wanaitwa wao ni wauwaji, baba yake akamuuliza kwa hasira ni nani kaongea hivyo…..aliogopa kumwambia baba yake, chanzo cha yote hayo, akamwambia kuwa amesikia tu mitaani. Baba yake akamwangali kwa macho ya hasira halafu akasema;

‘Ukoo wetu unaogopewa, na kuitwa ukoo wa wachawi,…lakini nani anajali hilo, ilimradi tunakipata kile tunachokitaka, kwani wao wanafanya nini hadi wanakuwa matajiri, waulize hawo matajiri nini wanachokifanya hadi wakafikia hapo….wanafanya mambo mengi mabaya kuliko hayo ya kichawi, ….wengine wameua watu kwa kupitia utajiri wao, wamesababisha watu kufa,….ili mradi wafanikiwe kuujenga utajiri wao, huo sio uchawi….

‘Baba kwa vipi, mtu afanye mabaya yanayoshinda uchawi…?’ akauliza kijana wake

‘Nikuambie kitu, hebu angalia matajiri wenye miradi, ambao wameajiri watu, wanawatumikisha watu na kuwalipa mishahara midogo, mishahara ambayo haiwasaidia, watu hawo wanapoteza nguvu zao, wanakufa kidogo kidogo, …ikifikia hatua fulani wanafukuzwa kazi wakiwa hawana nguvu tena ya kumudu maisha yao…wanakwenda kujifia..huo si zaidi ya uchawi…

‘Pia, wengine wanapatwa na mishutuko ya moyo wanakufa kwasababu ya hofu, hofu ya kukosa ajira hofu ya kudhulumiwa…hilo haliangaliwi, achilia mbali wale wanapatwa na majanga wakiwa makazini, huo hauitwi ni uchawi….achilia mbali kufanya kazi katika mazingira magumu yanayoathiri afya….huo sio uchawi….?’ Akawa kama anamuuliza kijana wake.

Kijana wake akawa katulia akiwaza, lakini hakuona ubaya uliopo hapo, hadi uonekane kama uchawi, kwani anajua ubaya na mambo ya hatari wanayofanya wachawi

‘Sasa kijana wetu sisi nasi tuna njia yetu ya kupata utajiri, lakini kila utajiri, hauji hivi hivi tu,…kuna mambo yanatakiwa kufuatiliwa….hayo yalikuwepo, na ili yaendelee kuwepo, na ili ukoo wetu uendelee kuwepo, na ikibidi ….na ni lazima iwe hivyo, kwasabbu sisi ndio wengi, katika jamii, hii, unajua kwanini sisi ni wengi…?’ akauliza.

‘Kijana akatulia akiwaza,…hakuweza kupata jibu, akatulia bila kusema neno

‘Ni kwasababu moja ya msharti yetu, …ni kupata wasichana wabichi…..’akasema huku akitabasamu, halafu mara ghafala akakunja uso na kusema;

‘Lakini kuna sharti gumu, …ambalo ndipo hapo wenzetu wanatuita sisi eti ni wachawi,….lakini utafanyaje, maana ukimwambia mtu akupe damu yake wa ajili ya kukamilisha tambiko au mambo yako,hatakubali, na wewe ili ufanikiwe unahitaji kupata damu, sasa utafanyeje,… inabidi utumie nguvu, na hapo unajikuta umeua…..’halafu akakunja uso kuonyesha kuwa anayozungumza sio ya utani.

‘Akupe damu, damu ya nini,….?’ Akauliza kijana huyo, kipindi hicho alikuwa bado mdogo, hajapata huo ukuu wa majeshi, alimwangalia baba yake kwa mshangao, huku akianza kuogopa, na yale aliyokuwa akiyasikia kwa watu akaanza kuyaamini, kuwa kumbe ukoo wao kweli una mambo ya kichawi, ….kumbe kweli wao ni wachawi.

*****

Siku alipopata huo ukuu, akaitwa na wazee, na kipindi hicho baba yake alikuwa hayupo, aliitwa na babu yake, akakutanishwa na wazee wa huo ukoo.Mbele yao kulikuwa na mzee ambaye anaaminika kama mtaalamu, alikuwa kashika kisu na vibuyu, ambavyo vilikuwa na damu.....

Yule mzee mtaalamu alikuwa kakaa kimiya, anaweweseka mdomoni kama anaongea na watu wasioonekana. Na wakati anaendelea na mambo yake, kijana huyu akamsogelea babu yake na kumuuliza kusudio la kuitwa pale. Na hapo ndio akaanza kupewa mikoba ya uongozi, …

Babu yake alianzia mbali,na babu yake akaweza kumfafanulia ni kwanini wanahitajika kupata damu ya watu, hasa pale alipouliza kwanini kila mara analazimishwa kumwanga damu za watu wasio na hatia.

‘Kijana wetu, kweli, tunahitaji damu,…, ili mambo yetu yakamilike, damu hiyo ndio chakula cha mizimu,na bila hiyo hatutaweza kufanikiwa…’akaambiwa, kwani yeye pamoja na kuutaka huo uongozi, pamoja na kuutaka utajiri, lakini matendo hayo na mengine ambayo yalikuwa yakifanywa na ukoo, wake hakuyapenda kabisa.

‘Kijana wetu nikuulize wewe umesema unataka utajiri, unataka uwe mtu mkubwa, upate utawala, upate raha zote za dunia, hebu niambie hayo, au hivyo vitu utavipataje..kirahisi rahisi hivyo?’ akaulizwa na kabla hajajibu, huyo mzee akasema

‘Hebu niambie, ina maana wenzako hawo wa koo nyingine hawataki hayo unayoyataka wewe, angalia wenzako wanavyohangaika, kila siku wapo mashambani, kila siku wapo na mifugo yao, ….wanahangaika,usiku na mchana, lakini ukiwaangalia wapo pale pale, hawana mbele wala nyuma, …’akaambiwa.

‘Wazee wangu, kwani hakuna njia nyingine, ina maana haiyo mizimu hainwyi damu ya wanyama, mbona tuna mifugo mingi, tuchukue damu ya mifugo tuwape,…’ akasema

‘Damu ya mnyama,..hahaha…hiyo haitakiwi,…inahitajika damu ya binadamu, …kila mwezi unatakiwa kupata damu, damu ambayo utaitumia kama kafara,bila hilo hutaweza kufanikisha hilo kafara, na usipofanya hivyo, balaa lake ni kubwa, ….’yule mzee akakunja uso kuonyesha uchungu.

‘Balaa linaanzia kwenye kizazi chenu…. mmoja baada ya mwingine ataanza kuangamia, na ilivyo, inaanzia kwenye yule unayempenda sana, halafu…mwingine , mwingine na mwishowe inakujia wewe, na wewe kifo chako, utatamani ufe , lakini hufi, unaoza kidogo kidogo….’akaambiwa.

‘Kama umeharibu, ukachelewa kutoa hilo kafara, utahitajika kutoa mtoto wako,…au mzazi wako….au …ili kuzima hilo balaa lisiendelee’aliposikia hivyo akatamani kuziba masikio.

‘Kwanini mnanipa kazi nzito kiasi hicho,…mimi sasa hivi ni kiongozi, sihitajiki kufanya hayo tena, nitatumia ujuzi, na nguvu zangu kuendelea kuwa kiongozi bora, sio lazima kutumia hayo mambo…’akasema.

‘Hahaha, umeshachelewa, ….kijana, ukishaingia humu hutoki, na kama unataka kutoka , tunahitaji roho yako, tunahitaji damu yako, ili kazi hii apewe mdogo wako, au mtu mwingine ……na kwasada kinachohitajika ni damu ya binadamu, kama unawexa kuipata bila kuua, ni sawa..lakini ni damu inayojaa kiganja cha mkono, …’akaambiwa.

‘Hebu tuambie baba yako yupo wapi…alianza kulega lega kutimiza masharti, unaona alivyokufa kifo cha aibu na mateso…..’akaambiwa, na hapo akamkumbuka baba yake alivyokufa kwa shida, alioza mwili mzima, lakini roho ilikuwa haitoki……

‘Ina maana adhabu yote hiyo ilikuwa kwasababu alikiuka masharti, kwanini msimsaidie akapona, …’akasema kwa hasira.

‘Ukishaharibu na kufikia hatua ile..huwa hatuwezi tena kukusaidia, maana ni lazima fundisho litolewe kwa wengine…’akasema huyo mzee akiwa kakunja uso …..

‘Lakin yapo masharti mengine ambayo nahisi utayapenda sana, ….’akaambiwa

‘Masharti gani tena mengine, ….mimi kiukweli mambo yenu ya uchawi siyapendi, ila nafanya kwa vile ni lazima iwe hivyo…’akasema.

‘Ni hivi, …pia kila mwaka unahitajika kumpata binti mwali, …msichana ambaye hajaguswa, …ushiriki naye tendo..’akaambiwa na hapo akachekelea kwani hiyo ndiyo starehe yake. Lakini kuua, …yeye anajua kuua ni kwenye vita, sio katika hali ya kawaida, kumshika mtu na kumtoa roho yake, eti kisa ni kutaka damu yake, hilo hakulifurahia kabisa.

‘Ina maana kila mwaka nitakuwa naoa mwali….?’ Akauliza huku akionyesha uso wa furaha.

‘Kama unaweza kumpata mwali bila ya kumuoa hiyo ni juu yako, ila damu ya mwanamwali huyo inahitajika iguse mwili wako, ili kafara hilo liweze kufanikiwa, usipofanya hivyo, familia yako na kizazi chako kitapatwa na balaa,…..ndugu zako watakuwa wanakatika mmoja baadaya mwingine,….katika vifo vya ajabu ajabu, …mfano kama alivyoangamia baba yako, na tumeweza kuzuia balaa hilo lisiendelee kwenu ndio maana nyie mpo huru.’akaambiwa.

‘Usipofanya hivyo,hiyo mizimu itakuja kudai damu yao,…..maana yenyewe imeshakupa utajiri… lakini wewe hujaifanyia kitu,…hakuna jambo la bure…usipofanya hayo, hiyo mizimu itaivamiwa familia yako na kuanza kunywa damu zao, ….’akaambiwa.

‘Na ili ujue kuwa ni wao wamekuja kudai ujira wao, moja ya ishara ya kujua hayo ni kuwa huyo mhanga atadondoka, na kutoa damu mdomoni na puani, na baadaye atakauka, kwani damu yake itakuwa imeshanyonywa..na hawo mizimu na wakianza kazi yao, ni vigumu sana kuwatuliza…itahitajika damu ya kizazi chako,….’akaambiwa.

*******

‘Itahitajika damu ya kizazi chako…’
Alipokumbuka hivyo, akajikuta mwili ukitetemeka kwa uwoga, kwani mwaka ulishapita, na baadhi ya masharti alishaanza kuyapuuzia, akijua kuwa yale yalikuwa maneno tu, yameshapitwa na wakati, na alihis huenda mizimu hiyo imeshapotea, lakini ili kuwa na uhakika akamuuliza yule mtu aliyemletea taarifa;

‘Mnasema huyo ndugu yangu alidondoka ghafla, ilitokeaje mpaka akadondoka ghafla?’ akauliza.

‘Alikuwa akiongea na malikia, na wakati anamsogelea karibu ndio ghafla, akatoa macho kama mtu aliyeona kitu cha kutisha, akadondoka chini na kuwa kama mtu anayeumwa kifafa, na baadaye akaanza kutoa damu mdomoni na puani, …na haikupita muda, ile damu iliyokuwa ikimtoka,ikakauka muda sio mfupi, na yeye baadaye akawa kama mtu aliyenyauka na kuwa kama kizee kikongwe …..’akaambiwa.

‘Hilo sasa balaa…’akasema huku akiangalia huku na kule na kichwani akasikia sauti ikisema;

‘Usipitimiza masharti hayo, kizazi chenu kitaangamia mmoja baada ya mwingine…..’sauti ile ikawa inajirudia kichwani hadi akashika kichwa na kuanza kukimbia kuelekea huko msituni.

NB Je atafanyaje, …tuwezpo kwenye sehemu ijayo. Wapendwa na wapenzi wa blog hii, naona wengi wameanza kulalamika kuwa siendelezi kisa chetu kama kawaida. Mimi mwenyewe natamani iwe hivyo, ila nipo kwenye wakati mgumu, …lkn yote maisha, tuombeane heri,

WAZO LA LEO: Imani ni kitu cha ajabu sana, na kile mmoja ana imani yake, na na njia zake za kuamini. Hata hivyo, imani za kishirikina za kutaka utajiri, imani zinazoambatana na kuua, kujeruhi..sio imani, na huo utajiri unaoutaka kwa imani hizo, hutakufa nao, ipo siku utarejea kwa muumba, sijui utakwenda kusema nini…Tumuabudu mungu aliyetuumba, na tumtegemee yeye kwa kila jambo.


Ni mimi: emu-three

No comments :