Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, January 2, 2013

Uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi-42


 

Malikia mtarajiwa akawa anaendelea na safari yake na sasa walikuwa wametoka kabisa kwenye eneo linalokaliwa na jeshi lao, na ili wafike huko wanapokwenda inabidi wakatishe eneo ambalo kikosi cha hasimu kimeweka kambi yao, hapo wale waongozaji wanaojua njia, wakasimama;

‘Mtukufu malikia, sehemu hii tunayohitajika kuvuka ndipo sehemu yenye kikosi cha hasimu, na mwenzangu kafanya utafiti, kgundua kuwa sehemu zote za njia za kutokea nchi za walipototea wamezizingira….’akasema.

Malikia akatulia kwa muda bila kusema kitu, na wazo likamjia kuwa atume ujumbe wa Hasimu amwambai kuwa anapita , lakini anahitaji kuwasalimia maana yeye ni mama wa wote, na sio vyema kubagua watoto wako hata kama wamekuasi.

Akawaambia washauri wake, washauri wake, waliogopa sana kukutana na watu, hasa askari wa hasimu, kwani pamoja na yote wanaweza hata kuwazalilisha, wakamwambia hilo, na malikia aliposikia kuwa askari hawo wana tabia hiyo, akamwambia muongozaji wa msafara.

‘Ina maana hayo yalishawahi kutokea na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa mbona kuna sheria kali zinasema askari atayemzalilisha mwanamke adhabu yake ni kutupiwa mamba?’ akauliza.

‘Hizo sheria zipo kwa watu wengine, lakini inapofikia kwa watu wa mzee hasimu, na askari wake, sheria hizo zinakuwa hazina meno, na ni nani atathubutu kwenda kushitaki,…maana ili ufike huko kwenye mhakama inabidi upitie kwa hawo hawo askari, akasema mshauri mmoja wa malikia akikimbuka kisa kilichotokea kwa mama yake.

‘Mimi hilo lilitokea kwa dada yangu, ambaye sasa ni marehemu, na kuuwawa kwake ni kwasababu ya hayp hayo madhila. Dada yangu alikuwa mrembo sana, na wengi tulijua kuwa huenda akaolewa na mmoja wa watu mashuhuri wa ukoo wa mzee hasimu.

Kumbe kuna wengi walimtaka na mmojawapo walikuwa mkuu wa kikosi cha maaskari, na huyo akawa kila mara anamshawishi dada yangu aolewe na huyo jamaa, lakini dada ayngu alikuwa hampendi, na wengu hawampendi huyo askari.

‘Kwanini watu hawampendi, mbona namuona ni mwanaume mwenye mvuto, jasiri…?’ akauliza, kwani malikia anmfahamu.

‘Tabia yake sio nzuri, hatulii na mwanamke , anapenda kila mwanamke, na akilewa, anaweza akapiga hadi kuua, …ana hasira sana, ..na wanaamini kuwa ukoo wao ni kichawi’akasema huyo mshauri.

‘Mbona niliskia kiongozi wa jeshi, au kiongozi yoyote anachagulia kwa uadilifu wake, na sababu kubwa inayoweza kumzuia kiongozi asipate hiyo nafasi ni kama ana ukoo wake ni kichawi, au kama ana tabia mbaya za kulewa sana…..’akauliza malikia akizidi kushangaa

‘Mtukufu malikia, jeshi la mzee hasimu, limejaa watu wa ajabu ajabu na wamewekwa hapo kwasababu maalumu, ili wamtii, kwa vile wanajijua kuwa wanamakosa, au kisheria hawatakubaliwa, basi mzee, akawachukuati  kwa masharti kuwa wamtii kwa kila jambo, na wasipofanya hivyo, sheria zao zitawaandama kwa tabia zao na makosa yao.

‘Kwa kuogopa hilo, na kupata nafasi ya kupewa uongozi au kuingia jeshini, ndio maana wengi wao wanamtii sana mzee huyo wakijua kuwa anawalinda kutokana na tabia zao. Na huyo jemedari anasifika kwa huo uchawi wake, kuwa anaweza kupambana na adui, na akamshinda kiajabu ajabu…anaweza akapambana na hata askari kumi peke yake, kwasababu ya mazingara yake…’akasema huyo mshauri.

‘Kwahiyo ilitokeaje kwa dada yako?’ akauliza.

‘Dada yangu na familia nzima haikukubaliana na maombi hayo, ndipo huyo askari akaamua kufanya uchawi wake, na dada yangu aliondoka siku moja akamfuata mwenyewe huyo askari hadi kwenye nyumba yake….’akasema huyo mshauri kwa huzuni.

‘Alipofika hapo, akasema yupo tayari kuolewa na huyo askari, hapo alikuwa sio yeye, alikuwa katekwa na hizo dawa zake, …basi akaolewa na huyo askari, …watu wakabakia mdomo wazi, na hata familia haikuamini hilo ikajua kuna madawa yametumika, na ikabidi familia ianza kufanya njia za kumuondoa binti yako kwenye makucha ya huyo askari.

‘Huyo askari kama anavyojulikana hatosheki na mwanamke mmoja, japokuwa limuoa dada yangu, lakini bado alikuwa akiwatafuta wanawake wengine, na wakati mwingine kwa nguvu, na dada aliyaona hayo kwa macho yake, na hata alipochoka, na zile dawa zilipoisha, akaamua kumkimbia..

‘Alipofika nyumbani, akawa kama kachangayikia,…anaongea maneno ya ajabu ajabu,…na wakati mwingine anasema huyo mume wake, alikuwa akimkamatisha askari wengine na kumzalilisha mbeel yake…’
‘Eti nini, si umesema alishaolewa na huyo askari?’ akauliza malikia kwa hamaki.

‘Ndio, eti alikuwa akianya hivyo, kama kutoa adhabu,kwani huenda alifanya kosa, au hakutii amri ya jambo Fulani, basi adhabu yake ilikuwa kama hivyo….’akasema huyo mshauri.

‘Hayo ni madogo, jeshi la huyo mzee lina vituko vingi, wengine wanasema kuna wakati wanachukua watoto wachanga na kuwaua, kwa ajili ya kufanikisha madawa yao’akasema huyo mshauri…

‘Hayo sasa umezidisha, hilo siwezi kuliamini…maana pale kwenye kundi lao kuna wanasheria, kuna wazee mashuhuri wanaoaminika,…ina maana wao hawajui hilo?’ akauliza malikia.

‘Wanajua lakini wanaogopa, kama nilivyokuambia wengi wao wamewekwa hapo kwa masharti, na kwa vile wanajijua , basi inabidi wamtii tu,..vinginevyo, wanaweza kujikuta wakitupiwa mamba, ni kwa mshari kuwa nitii, au nitoboe siri zako, ambazo mwisho wake ni kuishia ziwani kwa mamba, au hata ukipona huwezei kupata tena hicho cheo…

‘Na wengine wanaogopa siri za uchawi, kwani mzee huyo ana wataalamu wake, ambao humsaidia katika kufanikisha mambo yake..’akasema huyo mshauri, huku akiangalia huku na kule.

‘Sasa kwanini unaongea kwa mashaka mashaka?’ akauliza.

‘Kuna imani kuwa ukiongolea kuhusu machafu ya huyo mzee hutamaliza siku, …sasa mimi naanza kuogopa’akasema huyo mwanadada ambaye ni mmoja wa washauri wa malikia. Malikia anampenda sana huyo mwanadada , kwani pamoja na kuwa na akili sana , ni jasiri , anaweza kupambana kama mwanaume, na pia humtumia katika kuchunguza mambo ambayo anahitaji kuyajua.

‘Kwanini uogope, mbona sisi hatuogopi…..na huwa tunayazungumza machafu yake,…ujue mambo kama hayo ukiogopa ndio yanakupata, lakini ukiwa jasiri, ukasema mimi siyaogopi, na hayawezi kunipata, na kweli hutaweza kuzudhurika  na uchawi…ukiwa na mimi usiogope kabisa mambo ya uchawi…’akasema malikia.

‘Nashukuru sana, na kweli tangu niwe na wewe nimejikuta nikiwa na moyo wa ujasiri, na hata yale yaliyokuwa yakinitokea, ..hayanitokei tena…’akasema huyo mwanadada.

‘Kama yapi yaliyokuwa yakikutokea?’ akauliza malikai akizidi kuingiwa na hamasa ya kumjua huyo mwanadada, ambaye kwa kweli alikuwa mmoja wa warembo.

‘Mara kwa mara nilikuwa nahisi nafuatwa na uchawi wa huyo askari aliyemchawia dada yangu, kama nilivyokuambia hutamani kila mwanamke, na dada yangu alipofariki, akata na mimi nishike nafasi yake, nilimkatalia kata kata, nikamwambia albda achukue maiti yangu…

‘Haya dada yako alifariki je,…na kweli mna uhakika kuwa aliuwawa na huyo kiongozi wao wa askari, maana mimi mwenyewe nitahakikisha watu kama hawo wanapambana  na mkono wa sheria, lakini ili iwezekane hilo, nahitajika kupata ushahidi, na ina maana nyie mliowahi kuzalilishwa, inabidi mjitokeze, mseme ukweli wa hayo mliyotendewa..

‘Malikia hapana, usifanye hivyo, kwani mwanamke aliyezalilishwa hataweza kujitokeza tena na kusema uchafu aliofanyiwa, hatapata mume, na kila mtu atamnyoshea kidole , akisema huyo alibakwa, huyo, alifanyiwa uchafu, siwezi kumuoa…tunaomba malikia hayo yaliyopita yaache kama yalivyo….’akalalamika huyo mshauri.

‘Inaonyesha kuwa hata wewe uliwahi kufanyiwa hivyo….sema ukweli kwangu, na msiwe na wasiwasi kwa hilo, kwangu nyie ni watoto wangu, nitahakikisha mnaolewa na waume bora, na kwa ajili ya kuwa wakweli, na waaminifu….unanisikia, ukweli, uaminifu, …’akatulia akiwa anawaangalia wengine ambao walikuwa wakisogea wakitaka kuja kusikia nini malikia anaongea.

‘Nyie mliopo karibu na mimi , na wanawake wengine wote, watakajenga tabia ya uaminifu, wakawa wakweli, …wakawa wanatenda mume, ninawahakikishia kuwa maisha yenu yatakuwa mema, kwani nyie mumedhihirisha kuwa ni wanawake bora, ambao hawakupenda hayo machafu yawafike,lakini ukificha madhambi, uliyotendewa, unamficina mkosaji, ina maana mumeshirikiana naye kuyatenda hayo madhambi, najua kabisa hakuna alipenda yatokee hayo, kumbuka mifcha uchi hazai…

‘Mtukufu malikia, mimi yalinikuta lakini sio kwa huyo mkuu aliyemfanyia hivyo dada yangu, ….ilikuwa ni mdogo wake huyo mkuu,  ambaye pia ni mkuu wa kikosi kidogo, …wote tabia zao ni moja,…..na kila mara nahisi vibaya ninapomuwaza, natamani nipate  silaha niitumie kulipiza kisasi, na malikia siku nikumuona tena, naomba unipe nafasi hiyo, nilipize kisasi….’yule binti akaanza kulia.

‘Nilishakuambia ili uwe jasiri, ili uweze kuyashinda madhila yaliyokupata, unahitajika kutokuwa mnyonge, hayo yalishatokea, ni kama maji yaliyomwagika, huwezi tena kuyazoa,…kisasi hakitasaidia kwani hutakuwa umeliweka hilo kwani mizani ya sheria, na huyo mtu akajulikana kuwa kweli ni mkosaji…’akatulia kidogo.

‘Wewe kweli ulitendewa hivyo, lakini kosa lako ni kuwa ulinyamaza, hukulifuatilia kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake….ni kweli kulikuwa hakuna nafasi ya kulisema hilo kwa vile utawala haukuwapa nafasi hiyo, lakini usingeishia hapo, ungeenda hata kumwambia babu wa mume wangu, wao wangejua jinsi gani ya kuwatetea, …..’ akilini alijua hilo kwa jinsi ilivyo lisingeliwezekana.

‘Hata hivyo, bado ipo namna,…..’akatikisa kichwa kama kukubalina na hilo wazo lake, akasema kwa sauti ya chini, kama kuwaambia jambo la siri;

‘Mimi na mume tunajua madhila hayo na mengine mengi,..nawahakikishia kuwa sasa tutahakikisha kuwa sheria inafuatwa, lakini yote hayo hayatawezekana bila ushirikiano wenu,….kuna mengi yanaweza yakaendelea kufanyika huko majumbani, hatutaweza kuyajua, kama nyie msipotoa sauti, pigeni kelele tusikia,..kwenye vikao ongeeni bila kificho,….mkifanya hivyo, watendaji wote kama viongozi, wataogopa kufanya makosa, watawajibika…’akatulia hapo, na kuwaangalia kwa macho ya huruma.

‘Kwahiyo nawaomba tushirikiane….kosa lilishatokea, kwasasa usikubali kosa hilo lijirudie tena. …’akatulia huku akimwangalia huyo mwanadada, kama mama anavyomwangalia bintI yake

‘Sawa hivi nyie ni majasiri, mna nguvu sawa na hawo wanaume, na hata kuwashinda baadhi yao,mnaweza kupambana na yoyote yule …msijiweke wanyonge, …mnanisikia….’akasema akiwageukia wengine ambao walishasogea karibu, na wote wakasema;

‘Tumekusikia malikia,…’wakasema kwa sauti ya ukakamavu.
Malikia akawaangalia mmoja mmoja, na moyoni akawa anatamani kusikia madhila waliyofanyia HAWO wengine, na ikibidi atafanya hilo zoezi, kusikia nini alifanyiwa nani kwa kila mmoja wao, akasema kimoyo moyo, ‘nitahakikisha waliyofanyiwa hayarudii tena, akamgeukia yule mwadada aliyekuwa akiongea naye, akasema;

‘Hebu niambie dada yako aliuwawa vipi?’ akauliza

‘Dada yangu, alikutwa kajiua….na kujiua kwake ni kwasababu ya kuzalilishwa huko, kwani taarifa zilishavuja kuwa alikuwa akizalilishwa na maaskari wa mzee baada ya kujipeleka kwa huyo mwanaume ili aolewe kwa kutaka utajiri…kwa kule kunyanyapaliwa na watu, hakuweza kuvumilia, na kweli tukamkuta kajinyonga na kamba…’akasema huyo mwanadada huku akizuia machozi.

‘Kama tuhuma hizo zilizisikika kwanini mzee Hasimu, kama kiongozi ambaye alionekana mbele ya watu kama kiongozi jasiri, kwanini hakuchukua hatua yoyote kwa hawo maaskari, na kwanini aliendelea kumlea huyo mkuu wake, ambaye ana nafasi kubwa kwenye jeshi lake…?’

‘Hizo tuhuma zilipofika kwake, kesi ilifanyika, lakini hakukuwa na ushahidi, na wazazi wangu walioshitaki wakaonekana kuwa wao ndio wenye hatia eti kwa kumpakazia mkuu wa kikosi cha mzee, uchafu kama huo, na karibu wazazi wangu hawo watupwe kwenye bonde la mauti, lakini akapona kwa kuombewa masamaha na huyo kiongozi wa askari, akasema yeye kawasamehe na ndio ikawa salama yao…
Malikia alimwangalia yule binti kwa muda huku mwili ukimtetema kwa hasira za ndani kwa ndani, baadaye akasema;

‘Siku nitakapokutana na huyo kiongozi, nitahakikisha anatubu hayo makosa yake…..na kama nitapata ushirikiano wenu, adhabu kali itawaandama watu kama hawo…’akasema malikia akiwa na huzuni, akageuka kwa yule muongozaji wa msafara na kusema bila kuogopa;

‘Chagua njia unayohisi inaweza kutuvusha kwa usalama zaidi, na kama tukikutana na hawo maaskari nitajua nni cha kufanya, ….’akasema na msafara ukaendelea mbele na kabla hawajakatisha na kupita hilo eneo wakasimamishwa.

Mara kundi la maaskari wa ahsimu likatokea, lilipomuona kuwa ni malikia wote wakainamisha vichwa chini, na kama ilivyo ada, malikia ikabidi ashuke na kuwashika wote kichwani kwao, na baadaye akawauliza;

‘Nyie najua ni askari wa mzee hasimu, je mimi mnaniamini mimi kama malikia wenu?’ akawauliza.

‘Tunakuamini malikia mtukufu, na tunaomba baraka zako..’wakasema.

‘Basi mimi nina safari za kuwatembelea watoto wangu na nimefurahia kuwakuta nyie mpo salama na poleni sana kwa kazi hii ngumu ya kumtumikia mzee hasimu, lakini nawaombeni kwa vile nina haraka, nahitajika kuondoka, ili nimalize ziara yangu ya kuwatembelea wote waliopo huku msituni…’akasema malikia.

‘Mtukufu malikia, sisi tunakuamini na tunakuheshimu, lakini tumapewa taarifa kuwa tusikuruhusu kuondoka, hadi mkuu wa kikosi hiki afike …’akasema kiongozi wa hicho kikosi.

‘Hapana, sitaweza kumsubiri…mwambieni kuwa nina majukumu mengi, kusubiri kwangu hapa tunawanyima wengine haki yao ya kukutana na mimi….’na kabla hajamaliza mara kikaja kikundi kingine, cha maaskari na walipokaribia pale alipokuwa malikia na watu wake, wakainama kwa heshima;

Na mara kiongozi wa kile kikosi akajitokeza akiwa kavalia mavazi ya kiaskari, na kichwani kafunikwa na kaofia ya chuma, alipomkaribia malikia akainamisha kichwa chake na malikia akamshika kichwa, na wote alioongozana naye wakafanya hivyo, na alipomaliza hilo zoezi, yule kiongozi akavua kofia lile lilokuwa limefunika sehemu kubwa ka kichwa chake, ili apate baraka , kwani ilistahili ashike kichwa kikiwa wazi
Kipindi akalivua hilo kofia alikuwa kageukia upande mwingine ambapo malikia hakuweza kumuona sura yake, na baadaye akageuka kumwangalia malikia;

Yule mwadada mshauri wa malikia alipomuona huyo jamaa,akamsogelea malikia na kuonyesha wasiwasi , ni kama vile mtoto kuona kitu cha kutisha, na akawa anamsogelea mama yake, kupata ulinzi, na malikia akamuuliza kwa sauti ya ndogo, ya chini kwa chini kuwa anaogopa nini;

‘Ndiyo yeye malikia, ni mdogo wa yule mkuu wao wa askari, ndiye aliyenizalilisha mimi…naomba idhini yako nilipilize kisasi cha hayo aliyonifanyia….’akasema huku akionyesha uso wa hasira, na kweli alichomoa silaha yake akawa tayari kufanya lolote.

Malikia akainua uso wake, na wakawa wanaangaliana na huyo askari, ambaye kwa muda huo, hakuwa ametamtambua yule binti, alikwa muda mwingi akimwangalia yule malikia, na macho yake yalionyesha hisia zake, hakuweza kuzificha, akabenua mdomo, na kusema ..

‘Mimi ni mmoja wa wakuu wa vikosi vya mzee hasimu….salamu kwako malikia, tunaomba baraka zako katika uwajibikaji wako…je tuambie mnakwenda wapi, na kipindi kama hiki ambacho mume wako yupo mbele ya kesi kubwa ya kukiuka sheria, ya kujitangazia kuwa yeye ni mfalme mtarajiwa, wakati sio kweli..?’ akauliza huyo kiongozi.

Malkia alihisi kama kutaka kutapika,…akamwangalia yule askari,….na alishindwa hata kusema neno, moja, kwa wakati huo, akatikisa kichwa chake, na moyoni akawa anataka kusema neno baya lakini akajizuia , na hapo hapo akainua mkono wake hewani, akasema;

‘Tubu dhambi zako, kabla mabaya hayajakufika…’

Yule askari akabenua mdogo wa dharau, akamsogelea malikia, akainua mkono wake, kutaka kumshika malikia,…na kabla mkono wake haujamfikia, akatoa jicho …na kuanza kutetemeka,…..mara akadondoka chini, na askari zake kuona hivyo, wakamsogelea, ….domo zikawa zimatoka mdomoni, akaanza kukoroma,….haichukua muda, akatulia …uhai ukatoweka.

NB: Je kulitokea nini kwa huyo askari, je hawo maaskari wengine watachukua hatua gani, tuzidi kuwepo, na kama ninakwenda ndivyo sivyo, tuambiane.

WAZO LA LEO: Imani ya kweli ya kumwamini mungu ni pale utakapowapenda najirani zako, na ukawa tayari kutoa kile unachokipenda wewe kwa wenzako, kwa kuona kuwa ni vyema , kwanza akipate mwenzako kabla yako…je upendo wa namna hiyo upo katika dunia hii. Kama ungelikuwepo, dunia ingekuwa kisiwa cha upendo na amani.


Ni mimi: emu-three

1 comment :

Unique said...

Ahsante kwa kuandika. Ulitutosa kwa muda ila nashukuru umerudi. Unakwenda vizuri keep it up