Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, December 7, 2012

Uchungu wa Mwana aujuaye ni mzazi-35
Siku zikapita, Maua hakuona wageni wala kumuona mtoto wake, na akawa anamsumbua sna yule baba mlevi aende huko msituni, akajue nini kinachoendelea;

‘Hivi wewe una akili kweli wewe, yaani mimi nikawe kitowoe cha hawo watu wa msituni, hujasikia kuwa hawo watu wanakula nyama za binadamu’akasema huyo mwanaume mlevi.

‘Sio wao ….wao hawali kabisa nyama za binadamu, hata wao, wanasikia hivyo, hivyo, na wanaogopa kukutana na hawo watu wanaozaniwa kuwa wanakula nyama za watu….’akasema Maua.

‘Hata wao wanasikia hivyo….ndivyo unavyojidanganya, eti kwa vile uliwahi kuishi na wao,…, hakuna atakayekubali kuwa anakula nyama za biandamu, hata wanga….wale wachawi wa usiku, hawakubali kuwa wao ni wanga,  na  watu hawo wanakula nyama za binadamu, lakini muuliza kama atakubali kuwa anakula nyama za watu, hakubali ng’oo ….mimi, nisikilize kwa makini, mimi siendi huko’akasema huyo baba mlevi.

‘Basi fanya mbinu, uwaulize watu wa huko, umesema wanakuja hapo unapofanyia biashara zako, jaribu kuwauliza kwanini hawajafika , maana ni muda sasa’akasema kwa uchungu’

‘Hawo wanaokuja kwangu hawajui kabisa mambo ya huko kwa watawala wao, wao ni watu wasiofahamika kabisa na watawala, na wameweza kujichanganya na sisi, kiasi kwamba,wakati mwingine huwezi kuwajua, …utawajua tu kwa mavazi yao, lakini wakati mwingine wanavalia kama sisi….hawajui lolote’akasema.

‘Sasa ulipataje habari kuwa wanataka kuja na mtoto?’ akaulizwa.

‘Wao ni watawala, na watawala wana kila mbinu za kupata taarifa, ….walimtuma jamaa yao mmoja, kuna kunipa hiyo taarifa, ….na huyo jamaa sijawahi kumuona kabla’akasema.

‘Mimi sitaweza kuvumilia,….nitafanya kila njia ili nimpate mtoto wangu, na ikibidi nitaenda huko kumtafuta mwenyewe’akasema Maua.

‘Kama umechoka kuishi haya nenda, lakini usiniletee balaa, maana huyo mtu aliyetumwa, alisema nihakikishe nakulinda, hadi atakapokuja kukuona mwenyewe….huyo wanayemuita mfalme wao mpya, nasikia wana mfalme mpya…hawa watu bwana, wanajipa madaraka, ….hawajui ni makosa’akasema.

‘Ni makosa gani?’ akauliza Maua.

‘Wewe unajua maana ya mfalme, mfalme, maana yake ni mkuu wa nchi, ni mtu mkubwa sana kama raisi, sasa tutakuwa na maraisi wangapi kwenye hii nchi,….wao wanajiona kama wana nchi yao, …sijui wataelimika lini hawa watu,…..hawataki kusoma, hawaki kujichanganya, wapo maporini, na wanaishi kwenye mashimo kama wanyama….’akasema huyo baba.

‘Wao wanafuta mila na desturi zao, kama wafanyavyo wamasai,..mimi siono kosa, hizo ni mila zao, na serikali haiwezi kuingilia mila zao’akasema Maua.

‘Hiyo haipo, sheria za nchi ni za kila raia, …mfano kama ulivyosema walitaka kukua,..ungewaitia polisi, wangelifungwa, lakini kwa vile hayo yanafanyika kificho, na nyie mliofanyiwa hivyo hamtaki kutoa taarifa, basi yanaishia kinyemela…..’akasema huyo mwanaume mlevi.

‘Kwahiyo kesho naomba unifanyie uchunguzi huo,….tafadhali, vinginevyo nitaondoka hapa’akasema Maua.

‘Kwani ukiondoka utanipunguzia nini…mwenyewe nakuona kama umekuaj kuniongezea mzigo, maana sasa inabidi nikupigie mahesabu yako, inabidi nirudi kuja kukuangali kama upo au haupo…mnanipa kazi isiyo na malipo, sikia, ipo siku utalipa….’akasema na kuondoka.

Maua akamwangalia na kutabasamu, alishaanza kumzoea huyu mwanaume, alishajua muda gani uanweza kuongea naye na muda gani unatakiwa uwe mbali na yeye, na alishawazoea hao watoto wake kama watoto wake mwenyewe, na walikuwa wakimuheshimu kama mama yao.

Siku zilivyozidi kwenda, Maua akashindwa kuvumilia, akaona ni bora aingie huko huko msituni, akakutane na hawo watu.Aliona ni bora akafie huko huko  msituni,  kuliko kumkosa mtoto wake, na siku hiyo akaamuka asubuhi, akiwa na lengo la kutoroka hapo nyumbani, kwani alijua akisema anaondoka huyo mwanaume hatamruhusu, walishamuona ndiye mama wa nyumbani wa kupikia na kuwafanyia shughuli nyingine.

Alitoka alifajiri, wakiwa wote wamelala, na taratibu akafungua mlango na kuondoka. Alijifunika khanga, kwasababu ya baridi, na kwa ajili ya kujifichia ili watu wasimuone sura yake, akatembea hadi akafika msituni, hakujua aelekee wapi, lakini alichotaka na kufanya lolote….

Alijua humo msituni kuna maaskari wa msituni, huwa wanatembea huku na kule katika kazi zao, za uwindaji, au kazi walizotumwa kuzifanya, na wengine walikuwa wakiwinda simba kwa ajili ya mila zao, kwani kijana mwanaume lazima aonyeshe ushujaa wake kwa kumuua simba. Maua alijua kabisa akikutana na mmoja wa maaskario wa msituni, au mtu mmojawapo wa huko msitunu anaweza kupelekwa kwa hawo waliomchukua mtoto wake.

Wakati anatembea aliombea akutane na yule mtu aliyemuokoa, alijua huenda akawa mmoja wa maaskari wa huko, ….alitamani sana aonane na huyo, ili kwanza amshukuru, na pili aione sura yake, na kwa vile yeye mwenyewe alimuahidi kuwa atamsaidia kumpata mtoto wake, itakuwa ni rahisi kwake kumfikisha kwa huyo mfalme wao.

Alipofika eneo linalotenganisha msituni na mashamba ya watu waishio sehemu za kawaida, akaona kikundi cha watu, wakitoka hapo msituni na kurudi tena huko msituni, na walikuwa ni watu wa msituni, kwa jinsi walivyovalia, …akajificha, …huku akiogopa, maana alishaambiwa kuwa watu hawo wa msituni wapo makundi mawili, kuna kundi jingine bay asana, ambalo linaaminika kuwa linakula nyama za watu.

‘Hawo hata sisi tunawasikia tu, hata sisi tunawaogopa, lakini chanzo chake ni kuwa hawo watu walitupwa kwenye bonde la kifo, na huko wakawa wanakulana wenyewe kwa wenyewe kwa vile hakuna chakula ,mpaka wakazoea hiyo tabia, na wengine walikuja kuzaliana, na kuendeleza hiyo hulka…’akakumbuka sauti ya yule mwanaume alipokuwa akimsimulia hatari za huko.

‘Wale ni maaskari wa kawaida, …na inaonekana wapo na mzee, ….’akasema huku akijaribu kuangalia kwa makini.

Kundi lile lilikuwa kama limepiga kambi, kwani walionekana wakipika, na  kulikuwa na akina mama wachache, wengi wao walikuwa ni maaskari. Alitamani afike karibu, lakini aliogopa, akatulia pale pale kwa muda, na baadaye akaona wale maaskari wakiondoka, kuingia ndani, na pale wakabakia akina mama na askari wawili.

Akasogea karibu, …hadi akafika sehemu ambayo wakina mama walikuwa wakipika, na hapo akatulia, ..kwa jinsi walivyokuwa wakiongea ingelikuwa ni vigumu kujua wanaongea nini, kwani walikuwa wakongea lugha yao, na wakati mwingine walichanganya na lugha anayoifahamu Maua, …akasikia wakitaka kuhusu mtoto.

 Na mara kweli akasikia sauti ya mtoto, ilikuwa ikitokea sio mbali na pale alipojificha Maua, ..na mara mama mmoja akatokea na kuelekea pale sauti ilipotokea, …alikaa kwa muda na baadaye akarudi akiwa kambeba mtoto, akawa anambembeleza., na hapo akasikia mmoja akisema.

‘Huyu mtoto anafanana sana na mama yake’ akasema yule mama. Maua akamkumbuka kuwa ni yule mkunga aliyemzalisha. Yule mama akawa anamchekesha yule mtoto, akimuinua juu, na hapo Maua akatamani awe ndio yeye anamfanyia hivyo mwanae, na akasikia mama mmoja akisema;

‘Mimi sikuwahi kuiona sura ya mama yake, inaonekana alikuwa mrembo, …..na kwanini akapewa jina hilo. …mngempa jina zuri la huku kwetu, la kuashiria kuwa mama yake alifanyiwa ukatili, wa kutupwa aliwe na mamba bila kosa lolote…’akasema mmojawapo, na hapo Maua akatamani awafikie wale akina mama awalilie wampe mtoto wake, lakini akaona ni bora avute subira.

‘Kwanini unasema alifanyiwa ukatali, wakati mnajua sheria za jamii yetu, mtu kama yule hakustahili kuishi kwenye jamii yetu, angeiharibu, ndio maana hakutakiwa kabisa, ..na hata damu yake ni nuksi kwa jamii yetu, nyie hamjui mambo ya wazee wetu' akasema huyo mama mkunga.

'Kosa gani alilolifanya, maana hakuwahi kuishi na sisi alionekana porini, na kuchukuliwa na huyo mfalme mpya, na alipogundulikana wazee wakamuhukumu' akasema mama mmoja.

Yule mama akawa anamuinua juu yule mtoto huku akimwangali usoni, na aliona hayo mazungumzo wanayozungumza muda hayafai, akauliza:

'Jina gani lingemfaa huyu mtoto, maana hilo jina alipewa na malikia mtarajiwa, na kulibariki….?’ Akauliza yule mama aliyembeba yule mtoto.

‘Angeitwa Bahati…’akasema mmojawapo

‘Kwanini aitwe Bahati?’ akauliza mwingine

‘Hamuoni kuwa mtoto huyu ana bahati nyingi, isingelikuwa ana bahati, asingelikuwa hai ,….isingelikuwa bahati, angeliteseka sana huyu mtoto, wangeishi porini peke yao na mama yake, na huenda angeingia mikononi mwa wale watu wanaokula nyama za watu...., lakini unaona sasa ilivyo, kwa ajili ya bahati yake,.sisi tunahangaika kwa ajili yake, ….kule wanamtaka, sisi tunamtaka, na huyo kijana wa mzee, sijui kwanini anamtaka mtoto sio wa kwake, kwanini asioe mwanamke akamzalia mtoto wake’akasema mama mmoja.

‘Hayo ni mambo ya ushindani wa kutambiana katika mambo ya utawala, huyo kijana wetu anautaka utawala kama alivyo mzee wetu, lakini ndio hivyo kaukosa, sasa anataka kumtumia huyo mtoto kudai  nafasi katika nyumba ile takatifu. Anajua kabisa akimtumia huyu mtoto, na kudai jambo, ili wakubali kubadilishana na huyo mtoto atapewa’akasema mama  mmoja.

‘Ina maana ndio kikao cha jana kilivyokuwa kikijadili, maana walivyoondoka hapa inaonekana wamekubaliana jambo…?’ akauliza mwanamke mwingine.

‘Waliojadili kule ni siri ya wanaume, lakini mimi niliyasikia wakati napeleka chakula, na mzee alisema, huyo mtoto ndiye mukozi wao, watamtumia kudai mambo mengi, kwahiyo alindwe kwa ghuvu zote, na asitolewe mapaka wakubali kuwaachia sehemu ya madaraka’akasema huyo mama.

‘Kweli huyu mtoto anastahli kuitwa Bahati, basi majina yote ni yake…’akasema huyo mama na pale akawa anamnywesha yule mtoto maziwa kwa kutumia kibuyu kidogo, na alipomaliza akainuka naye na akasema.

‘Ngoja nikamlaze, …nahitaji kupumzika, ….akilia umpatia haya maziwa….nitayaweka hapa’akasema huyo mama akainuka na kuondoka naye. Hapo Maua akainuka na kumfuatilia kwa macho, akamuona akiingia kwenye kibanda cha majani, na kwa nje yake kulikuwa na maaskari.  

Maua pale aliposimama, akaona nguo zimaanikuwa zilikuwa nguo za hawo watu wa msituni, na hapo hapo wazo likamjia, akavua zile nguo zake na kuzivaa hizo nguo, akijua kuwa atakuwa amefanana na hawo akina mama.

Alipomaliza hivyo, akawaangalia wale maaskari ambao walikuwa wamesimama kwenye mti, wakiwa wanaangalia huku na kule, kuhakikisha usalama, Akasubiri, na mara askari mmoja akaondoka kwenda kule walipokuwepoa akina mama, …alikuwa anakwenda kuchukua maji, …yule mwingine akabakia na alionekana kuchoka, akawa kama anasinzia sinzia,..

Maua hakupoteza muda, akatoka pale alipokuwepo, na kutembea kuelekea kwenye kile kijumba, alijifanya kama mmoja wa akina mama , akafika pale palipokuwa pamewekwa kibuyu kidogo chenye maziwa, akakichukua na kuelekea kwenye kile kibanda, alipofika pale mlangoni, yule aaksri akamuona.

‘Unataka kumpa tena maziwa,….’akauliza na yule mama akatikisa kichwa kukubali, hakutaka kutoa sauti, na yule askari, akaona ni nafsi ya yeye kulala, …na hapo Maua akaingia na kuchukua yule mtoto taratibu akatoka naye.

Kule walipokuwa akina mama kumefichika kidogo, nafikiri walifanya hivyo, ili kutenganisha sehemu ya kina mama na akina baba, kwahiyo alipofikia ile sehemu ya katikati inayotenganisha, akapenye kwenye hayo majani na hapo akatulia na kuangalia huku na kule.

 Yule askari mwingine akawa anakuja, ….alipofika kwa mwenzake, akataka kuingia ndani kumwangalia mtoto, lakini akasita na kugeuka kuongea na mwenzake, akampa kibuyu huku akiuliza.

'Nilisikia kama mtoto analia...sasa naona kimiya,, nafikiri kilikuwa na maji, au vinywaji vyao, wakawa wanakunywa huku wanaongea. Maua akaona asisubiri zaidi, akaanza kutembea kwa kunyata huku akiwa kambeba mtoto wake, alifanya hivyo kwa muda mrafu hadi alipohakikisha kuwa yupo mbali na hiyo kambi, na hapo akainuka na kuanza kukimbia.

Alikimbia na huyo mtoto hadi akafika kwenye mashamba ya watu wa kawaida wasioishi msituni, na hapo, akabadili nguo zake na kuvaa nguo zile alizokuwa nazo mwanzoni, akamvua yule mtoto zile nguo za msituni, na kumfunga khanga yake aliyokuwa nayo toka mwanzo, na hapo akajiona yupo salama.

‘Wewe ni nani…?’ akasikia sauti ya kutisha nyuma yake, na alipogeuka akamuona yule mama wa msituni ambaye ndiye aliyekuwa akimnywesha maziwa huyo mtoto, mama mkunga, mama ambaye ndiye aliyemzalisha na kwa utii wake alihakikisha kuwa anamzalisha na kumkabidhi kwa maaskari wakamtupe kwenye mto wa mamba, mama mtiifu wa mzee Hasimu.Hapo Maua akaanza kutetemena kwani alijua kuwa sasa mtoto atachukuliwa.

NB: Naishia hapa na naomba dua zenu kwa wingi, kwani mitihani ya maisha ni mingi sana.

WAZO LA LEO: Uchungu wa mwana , na machungu ya uzazi anayeweza kuyasimulia ni mama peke yake. Tuwapende wazazi wetu, tuwapende na kuwajalia mama zetu, ....ni ajabu ya leo, matusi mengi yanayotoka midomoni wa vijana ni ya kuwalenga akina mama, ....hebu fikiria wewe unayetoa hilo tusi, kama asingelikuwa huyo mama kuvumilia hayo machungu ya uzazi ungeliweza kuwepo hapo,....Acha tabia hiyo,
Ni mimi: emu-three

No comments :