Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, December 5, 2012

Uchungu wa Mwana Aujuaye ni Mzazi-33




Marejeo: Turejee pale Maua alipokuwa akiikimbia Simba iliyojeruhiwa, na baadaye akapoteza fahamu, na alipozindukana akajikuta yupo kwenye kijumba, na harusi kali ya pombe ikitawala, kuashiria kuwa hapo, kama sio kilabu ya pombe, basi kuna mnywaji aliyebobea….Haya tuendelee na kisa chetu, tuyaone maisha ya mama huyu kwa huyo mukozi wake.

‘Naona sasa umezindukana, una…bahati sa..ana wewe mwanamke, ungakufa, sijui kwanini mwanamke mrembo kama wewe unaishi porini,…wewe ulitakiwa uishi na sisi huku duniani. Sisi ndio, matajiri wa hiki kijiji, ….mimi watu wananiita mlevi, lakini…sijanywa pombe zao,….ooh, ngoja nicheua kidogoooh, Bhoooh’ akawa anaongea kilevi na altulia pale alipokuwa akicheua na harufu iliyotoka hapo.

Mama alisema harufu ilitoka hapo, …hajawahi kuiskia katika amsiha yake yote, ni harufu ya uozo,…na hapo hapo, akashikwa na kichefu chefu, na kuanza kutapika, na yule mwanaume alipoona hivyo, akaanza kucheka, alicheka sana, hadi akadondoka, na baadaye akaondoka zake huku akisema;

‘Unatapika…hujanywa, unatapika, je ukinywa itakuwaje,…usisumbuke, matapishi nimeyazoea, naishi nayo, nashinda nayo,…ni kawaida tu, ..ngoja nikadai pesa yangu, …’akaondoka hapo akiwa anapepesuka.

 Baadaye walikuja watoto wawili, wakamletea chakula, na alipowadadisi mama yao yupo wapi, mwanzoni walisita kumwambia. Nafikiri walikuwa wakimugopa baba yao, au kuna jambo limejificha hapo, na hawo watoto hawakupenda kuliongelea, ila baadaye mmoja wao ambaye ni mdogo ukilinganisha na mwingine akasema;

‘Mama alimtoroka baba kwasababu …..’alipoanza kuongea mwenzake akamfinya na kumwambia atapigwa na baba.  Maua akawaangalia kwa muda, na walionekana kujawa na huzuni kutokana na swali hilo, na akasema;

‘Mimi nilitaka tu kujua mama yenu yupo wapi, kama mnaogopa kupigwa basi, ila nawashukuruni sana chakula huki kizuri ni nani kawapikia hiki chakula?’ akawauliza. Kwanza waliangaliana na huku wakitabasamu, na hata kucheka na yule mkubwa akasema;

‘Tumepika wenyewe, ….nani angetupikia, …sisi wenyewe tunajua kupika, mama alitufundisha, ‘akasema huyo mkubwa.

‘Chakula kizuri kweli, inaonekana mama yenu alikuwa akiwapenda sana’akasema Maua. Na swali hilo lilionyesha kuwagusa sana, kwani sura zao zilionyesha huzuni, na Maua alizania huenda wangeliangua kilio, lakini inaonekana walishazoa haya maisha na yule mdogo akasema;

‘Mama alitufundisha kupika kwasababu alikuwa hashindi nyumbani,…’akasema yule mdogo ambaye alikuwa tayari kuelezea kuhusu mama yake, na mwenzake akachukua vyombo na kuondoka navyo, na hapo Maua akaona amuulizie vyema huyo mtoto kuhusu mama yao.

Huyo mtoto alikaribia miaka kumi au kumi na moja, ..na kaka yake huenda ni kati ya kumi tatu, au kumi na nne, walionekana wakakamavu mwilini kuonyesha kuwa wanafanya kazi nzito, au kazi za suluba, na nguo zao zilichakaa sana, na chafu.

‘Mama alikuwa akifanya biashara ya pombe na walikuwa wakishirikiana na baba, …lakini kila mara wakirudi nyumbani, wanaishia kugombana, kila mmoja anamshuku mwenzake kuwa kachukua pesa za biashara yao, na wakianza hivyo, hawalali mpaka wapigane..’akasema huyo mtoto.

‘Na nyie wakati huo mko wapi?’ akamuuliza.

‘Tupo hapa hapa nyumbani,..tunaangalia tu, maana ukitaka kuingilia ugomvi wao, unakugeukia wewe, na unaweza ukachapwa mpaka uvimbe, …na mara nyingi tukiwaona hivyo, tunajifungia hapa chumbani kwetu, tukiomba mungu wasiumizane’akasema huyo mtoto.

‘Ina maana wanapigana hadi kuumizana?’ akauliza na yule mtoto akacheka kicheko kidogo, na kusema

‘Kuumizana…Watu wanapigana na chochote kilichopo mbele yao, kama kuna vyombo, wanarushiana,….kuna siku mama alipigwa hadi akapoteza fahamu na kuvunjika mkono’akasema

‘Kwahiyo ndio akaondoka, na kuwaacha peke yenu?’ akamuliza. Yule mtoto akatulia kwa muda kama anawaza jambo, halafu akasema;

‘Hapana hakuondoka siku hiyo hiyo…, kwani kesho yake, baba alimsadia wakaenda hospitalini, na alikaa hadi akapona, na kipindi chote hicho, mama alichokuwa akiumwa, baba hakuwa akilewa sana, alikuwa analewa kidogo, kwa vile biashara yenyewe ilihitaji kuonja onja….lakini alionyesha kumuhurumia sana mama, ….’akasema

‘Sasa kwanini mama aliondoka, inaonyesha walikuwa wakipenda sana’akauliza Maua.

‘Baba mwanzoni walikuwa wakipendana sana, tukiwa wadogo, walikuwa na maisha mazuri,…baadaye baba akaachishwa kazi huko alipokuwa akifanya, akaanzisha biashara, ….lakini bishara haikudumu, ndio wakajiingiza kwenye biashara ya pombe, hapo amani ikawa haipo tena.

‘Hebu niambie, mliwezeje kuishi katika hiyo hali, hakuna chakula, …wazazi wanapigana?’ akauliza Maua akiwazia mbali, kuwa na yeye ana mtoto, na huenda mtoto wake huko alipo atakuwa anateseka, hapo aakjikuta machozi yakimlenga lenga…

‘Mwanzoni tulipata shida sana, tnalia njaa mama hana cha kupika, inabidi wakati mwingine aende kufanya kibarua kwa watu, wanamsimanga, na wanamuibia,…hadi walipoamua kuanzisha hiyo biashara ya pombe..lakini ikawa ni tatizo jingine,…maana ule upendo wa wali ukaondoka, …mwanzoni walipokuwa wakipigana tulikuwa tnalia sana,…hadi tukazoea…tutafanyaje tena….’akasema akionyesha uso wa huzuni.

‘Wakati mwingine ni marafiki,…lakini tatizo ni wakilewa..’akasema na kutuliwa..

‘Kwahiyo mama akaondoka?’ akauliza Maua akiwa keshazama kwenye huzuni na mawazo

‘Siku mama alipoondoka, ni pale baba alipomshuku mama kuwa kaiba pesa, na ana mwanaume mwingine, na mama akawa anakataa, lakini baba aliendelea kumshuku hivyo, na kauli hiyo kila mara baba alikuwa akiiongea, na mama hakupenda kusikia hivyo, kuwa ana mwanaume mwingine, Na siku hiyo ambayo mama  hakuweza kuvumilia tena hadi akaamua kuondoka , na pale alipofika mwanaume mmoja akidai pesa zake…’akatulia.

‘Pesa gani hizi, ina maana huyo mwanaume alimkopesha mama yako?’ akaulizwa.

‘Hapana sio kuwa alimkopesha mama hizo pesa zinazodaiwa, huyo mwanaume alisema alinunua pombe, lakini hakupewa chenji yake, na mama akasema hakumbuki kupokea pesa yake, labda kama baba ndiye alichukua. Wakawa wanabishana na huyo mtu, ambaye alionekana kulewa, hadi kufika kuanza kupigana.
Wakati huo huo baba akatokea na kuwaona mama akiwa kashika na yule mwanaume, wakiwa wanapiga, baba yeye alichukulia vingine , aliona kama wapo kwenye….’ Yule mtoto pale akatulia na kuinama chini.

‘Sawa nimekuelewa endelea ikawaje?’ akauliza Maua.

‘Basi baba akaja kwa hasira na kuwavamia akaanza kupigana na huyo mwanaume akidai kuwa ndiye anayemuibia mkewe…..na mama alipoingilia kati ikaanza kupigwa yeye, ikawa baba anapiga na watu wawili, baba akazidiwa, na aliumizwa kweli kweli..’akasema huyo mtoto.

‘Na ndio mama akaondoka?’ akaulizwa.

‘Walipigana sana siku hiyo na kesho yake, pombe zilipowaishia, bado baba akasisitiza kuwa mama na huyo mwanaume ni marafiki, ndio maana wamemhangia na kumuumiza, …mama hakukubali, ….akasema kama hamuamini basi anaondoka,..…’akasema huyo mtoto.

‘Baba alipoambiwa hivyo alisema nini?’ Maua akauliza

‘Baba aliingia ndani na kukusanya nguo za mama akazitupia nje, na kusema kuwa hataki kumuona tena mama hpo ndani, kwani keshawafuma na mbaya wake, na mbaya zaidi wamemchangia na kumuumiza,…’akasema huyo mtoto.

‘Ina maana kumbe baba ndiye alimfukuza mama, na mama alipoondoka hakurudi tena, au hakuna mtu aliyekuja kuwasuluhisha?’ akauliza Maua.

‘Mama hakurudi tena, ..na hakuna mtu aliyekuja, ..nani angekuja huku, wakati mama na baba wametengwa na jamii, kwasababu ya biashara yao, na kulewa, watu wanawapiga vita, na kila mara maaskari huja hapa kuwatafuta, na mara nyingi wanakwenda kujificha huko porini’akasema huyo mtoto.

‘Sasa nyie mnasoma shule?’ akamuuliza.

‘Shule tuliacha…mimi niliachia darasa la tano, na kaka naye aliachia la saba, hakuwahi kufanya mitihani, …tunafanya vibarua, ….kupata pesa ya kula’akasema huyo mtoto.

‘Ina maana hata pesa za matumizi baba yenu hawapatii?’ akauliza.

‘Kuna siku anatupatia, siku nyingine, ….kama ndio kakimbilia porini, akitafutwa na maaskari, inabidi tujua wenyewe tutaishi vipi, sisi sio watoto wadogo tena, tunajua kuishi, leo nikipiata kidogo, naleta tunapika chakula…’akasema huyo mtoto.

‘Kwahiyo mama yenu hakuwahi kurudi hapa tena?’akamuuliza

‘Toka siku hiyo alipoondioka hajawahi kurudi tena, na hatujui kabisa kaenda wapi, na baba ameapa kuwa akimuona atamchinja’akasema huyo mtoto

‘Kwanini afikie hatua ya kusema hivyo?’ akaumuuliza.

‘Anasema mama alipoondoka aliondoka na pesa yake yote ya mtaji, …’akasema huyo mtoto na mwenzake akawa keshafika. Na usiku ikaingia, na kwa mbali wakasikia sauti ya mtu akiimba, …na watoto wakamwangalia huyo mgeni wao pale kitandani, na mmoja akaguna  na kusema;

‘Baba huyo anakuja,….sijui kama kutakuwa na amani hapa ndani….’akajifunika gubi gubi, na muda huo huo mlango ukagongwa kwa fujo…ulifunguka kama vile unavunjwa, na huyo jamaa akadondokea ndani, huku akilalamika.

‘Mimi nagonga hamtaki kufungua…huyu mwanamke hajarudi eeh, akija hapa ama zake ama zangu….na nasema siku nimuona kichwa chake ni halali yangu…nyie watoto,..mmh, ooh, nimekumbuka, huyo mwanamke bado yupo humu,….?’ Akatulia kidogo kama vile anasikiliza jibu.

‘Mnajifanya mumelala, su sio….mumeshakuwa madume, nyumba hii dume ni mimi peke yangu…nyie bado watoto…kama mumekuwa madume, tafuteni nyumba yenu…mnasikia, kesho mkatafute sehemu yenu,…sitaki presha hapa’akasema halafu akatulia, ikawa kama amelala, na muda wote huo, alikuwa kalala pale sakafuni alipoangukia.

‘Kwanza mumempa chakula huyo mgeni….aah, mgeni…ndio huyo namuita mgeni, kwa leo,…nauliza mumempa chakula, …lakini mgeni siku ya kwanza, ya pili, ya tatu, chukua jembe ukaafanye nini…..nimesema hivyooooooooh’ akatulia na kuanza kukoroma pale pale alipodondokea na baadaye akashituka na kusema

‘Kesho wanakuja wageni…wageni wa mgeni, wanasema wanamleta mtoto…nani atalea mtoto mchanga hapa, hilo nimelikataa…sikubali, unasikia wewe mwanamke, …ooh, nisemehe, mgeni, aah, ngoja nilale, maana mnajifanya wote mume lala, ila nata unielewe….’akatulia.

‘Wakilte huyo mtoto, eti mtoto mdogo,…sijui ana umri gani,…nani atamlea….sitaki presha..utapanga mwenyewe kunyoa au kusuka, ukae hapa, usiwe na mtoto, kama una mtoto, tafuta sehemu nyingine, kwanza nasikia ulitakiwa ufe….sasa nimekuokoa, …mimi ndiye muokozi wako, unisikilize mimi..haya usiki mwema…’akaanza kukoroma, kama radi.........

NB, Hayo ndio maisha ya mama Maua, tukutane sehemu ijayo

WAZO LA LEO: Ukijiona umekuwa, ujue kuwa kuna wazazi waliokulea, na malezi mengine ni ya taabu sana, …taabu hiyo aijuye ni huyo mzazi, kwani uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi,. Kwahiyo ni  vyema, tukawakumbuka wazazi watu, au walezi wetu ….kwasababu vyovyote iwavyo, bila wao, usingelikuwa hapo ulipo.

Lakini wazo letu la leo linasema; Kuna watoto hawajui kabisa ,mzazi wake ni nani, huyo hakupenda kabisa kutokuwa na wazazi, …alihitaji pendo la wazazi kama wewe, lakini kwa sababu mbalimbali hamjui mzazi wake. Wewe na mimi ndiye mzazi wake, ukila , ukasaza, ukatupa jalalani, ujue unafanya kosa kubwa sana, ulitakiwa umkumbuke huyu mtoto…

Jamani tuwakumbuke mayatima na watoto walio kwenye mazingira magumu.

Kwa hali ya sasa hivi watoto wanaopita mabarabarani wakiomba wanaongezeka, hao ni wa mabarabarani tu, kuna watoto wapo mitaani tunapoishi, kuna watoto wapo mjumbani, ambao hawajui leo au kesho watakula nini …hebu tujiulize ungejisikiaje kama mtoto huyo ni wa kwako, ndio ni wa kwako, lakini fikiri katoka tumboni kwako, na ndio huyo yupo katika hali hiyo, yupo barabarania akiomba, au yupo nyumbani lakini hana chakula, analilia chakula, lakini chakula hakuna, wewe umejaliwa, unakula unasaza, unatupa,..mnaandaa masherehe ya mamilioni..…

Mimi na wewe ni mzazi wa huyo mtoto, …ukila ukisaza na kutupa, au ukashinda kwenye baa na kunywa hadi kupitiliza, ukafanya sherehe ya kufuru,….unafanya makosa kwani umemsahau mmoja wa mtoto wako….

********************************************************************

Kumbe tarehe 5-December ndio siku ya kuzaliwa kwa emu-three, ooh, jamani siku zinakwenda kama mchezo, nashukuru kwa kunikumbusha hili;



Ni mimi: emu-three

3 comments :

Yasinta Ngonyani said...

Hii leo imeumiza imekata kabisa utumbo..maana ni kweli kuna watu wana maisha mazuri na watoto wao wanaangaika wanakula na kusaza ...hakika sisi binadamu sijui tumeumbwaje?:-(

Anonymous said...

Unanimaliza kabisa pale unapoweka wazo la leo, twakushukuru sana na kazi ya mikono yako ikuwezeshe ili uzidi kutupa zaidi. C.R

Anonymous said...

Inaumiza sana kwakweli, watoto wanahangaika hawana msaada, tunasahau kuwa ni malaika tu wasio na hatia, na hata ikitokea wamekuwa wezi au majambazi ni sisi watu wazima ndio tumesababisha hivyo kw akutojali familia zetu na watoto wasio na wazazi tunawatumikisha bila kujali nao wanastahili kuwa shule n.k tunawanyanyasa kijinsia na kimaumbile. Tusimame pamoja kuwatetea watoto jamani