Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, November 30, 2012

Uchungu wa mwana Aujuaye ni Mzazi-31


Marejeo: Tukumbuke hiki kisa alikuwa akisimulia yule binti niliyekutana naye akiwa kajiinamia kashika shavu, ….akiwa kasimuliwa na mama yake. Huyu binti kwa hali aliyokuwa nayo, alifikia hadi kukusudia hata kujiua.

Binti aliona kabisa , kuwa maisha kwake hayana thamani tena. Na binadamu anapofikia hapo, ujue kweli kuna jambo…nani asiyependa kuishi, hata yule anayekusudia kujiua, muda roho ikitaka kutoka, huwa anajitahidi kuiondoa ile kamba shingoni, lakini anakuwa keshachelewa, siku yake imeshafika, inabidi aonje umauti…na jamani kutoka kwa roho sio kitu cha mchezo.

Katika kisa hiki utagundua kuwa kuna mwanamama hapo ambaye ana jina hilo hilo, …jina ambalo nilisikia akiitwa huyu binti na mama yake mdogo, wakati namuulizia kuhusu maisha yake, kwanini imetokea hivyo, sasa tuendelee na kisa chetu, ………….

*********

‘Mimi sikujua kabisa huyo baba mlevi ninayeishi naye sio baba yangu wa kunizaa, kumbe alikuwa ni baba wa kufikia, hayo niliyajua baadaye, wakati najiandaa na safari ya kuja kuishi huku Dar, mji ambao kila mmoja kule kijijini alitamani kuja kuishi.

Mama yangu aliniambia huyo baba ndiye aliyekuja kumuokoa pale alipoachwa pale porini…..ili wenzake wafike huko wanapohitajika kwa wakati muafaka, na baadaye watarejea kumchukua, au kumtafutia sehemu ya kumuhifadhi.

Wakati kaachwa pale, akiwa kachoka, kwani mwili ulikuwa hauna nguvu, baada ya safari ndefu, baada ya mapigano, na yeye kujitolea kumsaidia huyo jamaa aaliyeficha sura yake kwa kofia ya ngozi ….na haat kujeruhiwa tena…akawa anatamani kulala tu.

‘Wewe pumzika hapa, na utakula nyama hii…mimi nahitaji huko kwetu haraka, leo najua inawezekana ikawa siku ya mwisho, nimeota kuwa nahitaji haraka sana….na kama ulivyoona, hawa watu walikuja kuniua, lakini tumeweza kuokoka…..ngoja nifike huko nyumbani haraka, halafu nitarudi kuhakikisha kuwa upo mikono salama….’akasema.

‘Sawa wewe nenda tu, na nakutakia mafanikio mema, mungu yupo pamoja na wewe, ila ninachokuomba ni kuhusu mtoto wangu…..naomba siku ukija, uje na mtoto wangu, usije bila ya kuwa na mtoto wangu….’akasema huyo mwanamama.

‘Naahidi nitafanya hivyo…na wewe hakikisha unakuwa salama, usiondoke, hapa, …hapa ni salama zaidi’akasema na akambusu kichwani na kuondoka. Huyu mwanamama alikaa pale kwa muda, halafu akaona akatafute maji ya kuoga, maji yaliyokuwepo pale yalikuwa ni machache, …

Alitoka pale akaanza kutembea huku na kule akitafuta maji, akafika sehemu, na ghafla aaksikia kitu kama mchakato, mwili ukaanza kusisimuka, akahisi kuna balaa…akageuka nyuma,….mungu wangu, akaduwaa, akashikwa na ganzi, …simba, ambaye alikuwa kafunua domo lake akitoa sauti, alikuwa kajeruhiwa, sauti iliyotoka hapo, ilimziba masikio, ……hakusubiri, ….hajawahi kumuona huyu mnyama kwa karibu kiasi hicho, akageuka, ….kosa alilolifanya ni hilo.

Alipogeuka, akaanza kukimbia, kumbe ni kosa, aheri angelisimama, maana huyu mnyama alikuwa kajeruhiwa huko alipotoka,…na, alipona hivyo, akaanza kumkimbilia, kwa vile alikuwa kajeruhiwa hata ukimbiaji wake, ulikuwa ni wa kuchechemea,

Huyu mwanamke hakugeuka nyuma, kumbe hata hivyo huyo simba alishamkaribia, akawa anajiandaa kumrukia, lakini akatulizwa na mshale  mkubwa …..mshale ambao ulilenga shabaha yake vyema na kuzama shingoni mwa huyo mnyama, mshale huo ulitupwa na kijana shupavu, akitafuta ujasiri, wa mila zao, na yule simba akadondoka,

Yule mama alipogeuka kuangalia nyuma, akamkuta yule simba kalala chini,..na mara akasikia watu wakishangilia, na mara kundi la watu wa porini likatokea,..yule mama akaona kaokoka na simba sasa ataingia mikononi wa wale watu waliotaka kumuua, akakimbia zaidi, alikimbia , akakimbia na kujikuta ametoka nje kabisa ya ule msitu, akawa sehemu tambarare, na pale alipo alikuwa kihema sana.

Kichwa kikawa kinamuuma, akawa hawezi hata kuhema, akadondoka chini,…hakuweza kuinuka tena, akapoteza fahamu na alipozindukana akajikuta yupo kwenye kibanda cha majani, kalala kwenye mkeka, na pembeni yake yupo baba mmoja akiwa kakaa na watoto wake, wawili, ….na kitu kingine alicho kihisi ni harufu kali ya pombe...

*******
Maisha yangu yalikuwa hivyo, kuokoka, au kuokolewa kiajabu ajabu, ….akasema mama yangu.
‘Lakini mama hujanimaliza jinsi ilivyotokea huko porini, na huko Mererani, umekimbilia mwishoni, ilikuwaje siku ile wakati watu wanasubiria, …watu wanamsubiri mfalme kutokea?’ akauliza huyu binti, akimuuliza mama yake.

Maua, kabla hatujafikia huko, tukarudi siku ile malikia mtarajiwa alipojiwa na wageni, na wageni hawo walikuwa yule kijana wa mzee mhasimu akiwa kaandamana na mkunga, mkunga ambaye ndiye aliyemzalisha yule mama aliyetupwa ziwani ili aliwe na mamba. Mkunga huyu ndiye anayeaminika sana na ukoo wa mzee mhasimu.

Malikia aliposikia hivyo kuwa wageni waliofika hapo ni mkunga aliyemzalisha yule mama na kaja na yule mtoto mchanga, kumbukumbu zake zilirejea nyuma, akakumbuka kauli ya mama wa huyo mtoto, kuwa ajitahidi sana amlele mtoto wake. Kauli ile ilikuwa ikimuandama sana akilini mwake huyo malikia, lakini kwa utaratibu ulivyo, yule mtoto hakutakiwa kulelewa na mtu mwingine yoyote zaidi ya kulelewa na watu maalumu kwenye eneo wanalolitambua kama sehemu takatifu.

Watu hawo ni waumini wa imani za hapo, wanalea hawo watoto, waje kushika nafasi zao baadaye, wawe walimu, na wahudumu wa sehemu hiyo. Kwani sehemu hiyo, licha ya kuwa ni sehemu ya utawala , lakini pia kuna mahakama, kuna shule ya imani zao, na kuna sehemu maalumu ya kulea watoto wasio na wazazi wao.
Ndio maana kila msimu, ni lazima kila mwanamchi apelike sadaka huko....

Sadaka hizo za mavuno ziliweza kuwahudumia hawo watoto, walimu na wazee, viongozi na shughuli ambazo zilihitaji vyakula. Kulikuwa na utaratibu ambao, uliwawezesha watoto hawo, wasipate taabu, lakini mtoto bila mzazi wake, ni kumnyima haki ya msingi, hasa ikizingatia kuwa mzazi yupo, au kazulimiwa ….

Malikia alisimama haraka na kuelekea chumba cha wageni, na huko akamkuta kijana wa mzee hasimu, akiwa kasimama pembeni huku kambeba yule mtoto, akamchekesha chekesha. Malikia akamwangalia na huku akiwaza mbali, akiwazis siku ambayo nay eye atakuwa na mtoto kama huyo na baba yake awe amempakata kama vile, anamchezea, akatabasamu.

Tabasamu lile lilitafsiriwa vinginevyo na wale waliokutwa mle ndani, yaani yule mkunga na huyo kijana, wakijua mpango wao umefanikiwa, na iliyobakia ni kusubiria siku hiyo ya kuapishwa mfalme, na kijana huyo atakuwa mume halali wa huyo malikia.

‘Nashukuru kuwa umefika, pole sana na majukumu, na mihangaiko ya hapa na pale, najua jinsi gani unavyotaabika, na nashangaa kwanini wazee wa hapa hawataki kusema ukweli, ….’akasema huyo kijana wa mzee hasimu.

‘Ukweli gani huo unaoutaka wewe, ambao hawajausema, hebu fikiria kama wewe ungelikuwa katika nafasi yao ungelisema nini…je ungalikubali uvumi, bila ushahidi,…ina maana wewe kama ungelikuwa mzazi ungelikubali tu, kuwa mwanao kafa bila ya kuthibitisha,….hii ni kuonyesha jinsi gani, usivyokuwa na hisia kwa watu wengine…’akasema malikia.

‘Sio kweli kuwa sina hisia na watu wengine, ningelikuwa hivyo, nisingelikuja hapa tena, kuwa nawe karibu, kuja kukuambia ukweli, ili usiszidi kuteseka, ..hawo wazee wa upande huu , ndio wasio kuwa na hisia za watu wengine, kwanini waendelee kukutesa, wakati wanaujua ukweli’akasema huyoo kijana.

‘Bado hujaniambia huo ukweli, ni upi, na una ushahidi gani?’ akauliza malikia huku akimwangali yule mtoto, ambaye alikuwa anafanana sawa kabisa na mama yake.

‘Ukweli ni kuwa mume wako hayupo tena duniani, na wanachotaka kufanya hawo wazee ni kupoteza muda, kwa ajili ya maslahi yao binafsi. Kwa hli hiyo, wewe huoni kuwa wanachojali hapo ni maslahi yao kuliko kujali hisia zako, hisia za jamii, ….je hawo wanakupenda kweli, je hawo wanafaa kuwa watawala bora?’ akauliza huyo kijana.

‘Wewe una ushaidi gani kuwa mume wangu hayupo tena duniani?’ akauliza malikia.

‘Kwanza hawo walioandamana na yeye walisemaje,….walisema kuwa mume wako kwa kujitia ujasiri, alizamia kwenye ziwa, akitaka kuokoa huo mzigo uliozama, hebu fikiria , mtu hajali maisha yake, hajali kuwa nyuma kaacha mke, kaacha majukumu, anazamia mzigo…mzigo unathamani gani mbele ya maisha yake, mbele ya nyie aliowaacha huku nyuma…’akasema huyo kijana.

‘Je kuzamia huko ndio ushahidi wa kuwa alikufa, kuna wangapi waliwahi kuzamia kwenye mazingira hayo, na bado wakawa hai….?’ Akauliza malikia.

‘Hivi wewe ulishawahi kukutana na mamba, akiwa na njaa, ukumbuke kipindi kile, ni kipindi ambacho mamba ni wengi na wana njaa sana, hakuna mifugo, na wengi wanategemea wanyama wanakuja kunywa maji mtoni, na wanyama kipindi kama hicho ni adimu kweli….sasa mtu azamie akutane na hawo mamba atoke mzima, haiwekani…’akasema huyo kijana.

‘Kuna ushahidi mwingine zaidi ya huo…?’a kauliza malikia.

‘Huo ni ushahidi mzito sana,….na kama angelikuwa hai, ….angelionekana baadaye, wenzake walisubiria kipindi kirefu, na hawakumuona akiibukia sehemu nyingine, na baadaye waliona moja ya vitu vyake alivyokuwa kavaa mwilini vikielea ….hapo unataka kusema nini tena, na kama kweli yupo hai, kwanini asionekane muda wote huo, ina maana hana mapenzi na wewe?’ akauliza huyo kijana wa mzee hasimu.

‘Tatizo lenu, mnakimbilia hitimisho,….na hilo io jambo jema, mikimbilia hitimsihao kwa vile mnaona litawasaidia nyie, …tafuteni ushahidi wa kutosha, unahalalisha hilo hitimisho lenu,..ni waulize kwanin kabla ya yote haya, kwanini msiombe uchunguzi wa pamoja, ili kuthibitisha hilo, kwanin mnakimbilia kutaka madaraka….kutaka kunitoa mimi hapa?’ akauliza malikia.

‘Jamii yetu ina utaratibu, utaratibu huo uliasisiwa, na ndio uliotufanya hadi tukafika hapa, ukumbuke jamii hizi zilipofika hapa kwa mara ya kwanza, zilikuwa haziaminiani, zikawa na uhasama, kukawa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, na wenzetu wakaja wakasuluhisha, na kukaweka sheria za kulinda, …sheria hizo zimesaidia kuiweka jamii hii katika mariziano…’akatulia huyo kijana, halafu akamwangalia yule mtoto.

‘Tunataka sheria hizo ziweze kuwepo na kuwezesha vizazi hadi vizazi kuishi kwa amani, na moja ya sheria hizo ni kuhakikisha utawala unakuwepo..na kama kumetokea tatizo, kama la msiba, mmoja wa mtawala, au mtarajiwa, kafariki, kuna kipengele cha jinsi gani, ya kufanya…

‘Unajua kunapotokea tatizo kama hili, watu wanataharuki, …na kama hakuna utaratibu wa haraka wa kuweka mambo sawa, kunaweza kukatokea fujo, kwahiyo wenzetu waliliona hilo, kuwa kama mtawala au mtarajiwa kafariki ni nini kafanyike kwa haraka, na isizidi siku saba…kuwe na mtu anakaimu ile nafasi, ili mambo yaendelee kama kawaida.

‘Na malikia hatakiwi awe anasononeka kwa muda mrefu, ujua huku malikia ni mama wa jamii, kila mmoja anamtegemea yeye, sasa tukimuachia akawa anasononeka kwa ajili ya mtu mmoja, je hawa wengine watahudumiwa na nani, ukizingatia kuwa huduma hizo zinahitajika kila muda…ndio maana sisi tunaojua sheria, tukalichukulia hilo kwa uzito wake’akasema huyo kijana.

Yule kijana akamchukua yule mtoto na kumuinua juu, na akawa kama anamchekesha, akasema;

‘Mtoto huyu ni mzuri sana,…., na wapo wengine kule makaoni kwao, hawajapata huduma , …hawajapata baraka zako, ukiuliza unaambiwa malikia yupo kwenye mjonzi, …sasa huduma za watu kama hawa zinapatikana wapi, ndio maana wenzetu waliliona hili, wakaona kuwa pindi ikitokea jambo kama hili haraka, utaratibu unafuatiliwa na mambo yanakwenda kama kawaida’akasema huku akimtizama huyo mtoto.

Malikia hapo akatulia, na kumwangalia yule mtoto kwa mbali, na ilimsikitisha sana, aliposikia kuwa kuna watoto wengine, wanasubiri huduma zake, na yeye amekuwa kikwazo,….akamsogelea yule mtoto, pale aliposimama huyo kijana, na alimpokaribia akatulia, amgeukia yule mkunga, na kusema;

‘Nakuomba umchukua huyo mtoto’akasema na yule mkunga akasita na kumwangalia yule kijana, ambaye alikuwa bado anamchezea yule mtoto kwa kumshika vidole vyake vidogo, akasema

‘Sasa hivi ndio unaliona hilo…au kwa vile huyu mtoto ni mtoto wa aliyekuwa rafiki yenu,….?’ Akauliza huku akiwa bado kamshikilia yule mtoto.

‘Ndio maana tumekuja naye, ili huruma ikujae, , kwani huenda tungelikuja na mtoto mwingine usinglijali hilo’’akasema huyo kijana, na malikia, akaenda na kumchukua yule mtoto mkononi mwa yule kijana na kwenda kukaa naye karibu na yule mkunga.

‘Zaidi ya kupaat baraka, ana matatizo gani mengine, ….na kuna watoto wangapi wanahitaji huduma zangu?’ akauliza

‘Matatizo yake makubwa, ni kulia….analia sana, lakini cha ajabu tulipomfikisha hapa ametulia kabisa, utafikiri sio yeye, hii ni kuonyesha kuwa alikuwa kihitaji huduma zako, na pili, anakuhitaji wewe kama mama, na huenda anakuhitaji wewe zaidi, uwe naye karibu’akasema yule kijana, badala ya kuonge ayule mkunga, yule mkunga akatikisa kichwa kukubaliana na hayo maelezo.

‘Kutokana na hayo, mimi nikawaona wazee, kuomba kibali chao, kuwa huyu mtoto, anahitaji watu wa karibu, na mmoja wa watu ambao wanakubalika ni mimi, nikaomba kuwa mimi niwe baba yake, …..wakakubali, lakini bado akawa analia, …mimi nimeshakuwa baba yake, na anahitajika mama yake, na huyu mtoto anakulilia wewe….baba yupo , mama yupo wapi’ akawa kama anauliza.

Malikia mtarajiwa akainua uso na kumwangalia yule kijana, safari hii, akawa anaiona sura ya mume wake, hakujau ni kwanini…akatukisa kichwa kuondoa ile taswira, na kugeuka haraka kumwangalia yule mtoto, akauliza;

‘Kwahiyo hata jina bado hajapatiwa?’ akauliza malikia.

Kijana yule akacheka na kusema; ‘unaona ulivyo…unasahau hata majukumu yako, huyo angelipatiwa wapi jina wakati wewe upo na mambo yako….hamjali jamii, mnajali ubinafsi,….huyo na watoto wengine bado hawajapata huduma yako, ahwajapata majina..kwa sababu yenu,..je hili mtalisahihisha vipi, hasa kwa wazee wenu, hawaoni kuwa wamekiuka sheria na katiba yetu, na mtu akikiuka sheria na katiba yetu ni ni adhabu yake?’ akauliza huyo kijana.

‘Sheria na katiba haijavunjwa…tulikuwa katika kutafuta ukweli, na kwa hili , nasikitika sana, kama nimekuwa kikwazo, na leo nitajitahidi kuhakikisha kuwa natimiza wajibu wangu…’akasema malikia huku akimshika yule mtoto kichwa.

‘Je na hilo na kuwa mimi ni baba yake, na kwasasa anamuhitaji mama yake, unalionaje,….maana kwa vyovyote iwavyo, kesho ndio siku ya mwisho siku ambayo, unahitaji kufika sehemu yako ya utawala, na huwezi kufika hapo hadi uwe na mume…na …na kwa mapenzi yako kwa huyu mtoto, unatakiwa unikubalie mimi kuwa mume wako’akasema kijana.

Malikia akaacha ile kazi aliyokuwa akitaka kuifanya na kusimama, akamwangalia yule kijana, na mara ile sura ya mume wake ikawa anamzonga machoni mwake, akatikisa kichwa na kujiuliza kwanini hali kama hiyo inamzinga machoni mwake, akageuka na kuangalia kule alipokuwa yule mtoto, akasema;

‘Nakuomba tafadhali….utoke, ili niweze kutimiza wajibu wangu…’akasema kwa sauti ya huzuni.

‘Vyovyote iwavyo….wewe kesho ni mke wangu, na inatakuwa kwa furaha ya mtoto huyu, je unamtafutia jina gani, maana ..mtoto huyo ni mrembo, ….namfananisha na ua …kama ura waridi,….au tumuiite ua waridi?’ akauliza yule kijana.

‘Ataitwa Maua….’akasema akikumbuka jina la mama wa huyo mtoto.

NB: Niliona niiandike sehemu hii kabla ya kuendelea mbele ili tuwekane sawa,

WAZO LA LEO: Tuweni makini kwa dhamana za watu, kuna baadhi ya watu walikabidhiwa dhamana za watu wengine, wakaahidi, na kwa bahati mbaya, huenda hawo watu ni marehemu kwa sasa, na kwa tamaa zao, wamezitumia au hawakufuata jinsi walivyokubaliana na hawo marehemu. Hilo kosa kubwa,…..dhamana ni deni, na kama usipotimiza ahadi yako kwa huyo uliyemuahidi, deni hilo halifutiki hata kama mwenzako keshafariki, hadi utimize ahadi yako mliokubaliana naye,.. kufa kwake, sio tija, timiza wajibu wako, au fikisha ahadi hiyo kwa walengwa..tukumbuke kuwa ahadi ni deni.
Ni mimi: emu-three

5 comments :

Anonymous said...

Hongera mkuu

Rachel siwa Isaac said...

Mmmhh ndugu wa mimi kazi nzuriiiii!!!!

Asante pia kwa Wazo la Leo;Pamoja DAIMA!!!!

Anonymous said...

Everything is very open with a precise explanation of the challenges.
It was definitely informative. Your site is very helpful.
Thank you for sharing!
Also visit my site :: Liver Active

Anonymous said...

Woω that wаѕ unusual. I juѕt wrоtе
an гeallу long commеnt but afteг Ӏ clickeԁ submit mу comment ԁidn't appear. Grrrr... well I'm not writing all that oveг agaіn.
Rеgаrdlеѕs, ϳust ωаntеd to say supеrb blοg!
Also visit my blog ; Capsiplex Reviews

Anonymous said...

Pretty component of content. I simply stumbled upon your weblog and
in accession capital to claim that I get actually loved account your blog posts.
Anyway I will be subscribing in your augment and even I success you get entry to persistently rapidly.Also visit my weblog - wycieczka szkolna do krakowa