Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, November 28, 2012

Uchungu wa mwana Aujuaye ni mzazi-29




  La mgambo limelia, kila mwenye sikio na asikie, na amfahamishe yule ambaye hajasikia, kuwa leo ni siku muhimu sana, siku ambayo ilikuwa ikisburiwa kwa hamu, siku ambayo haki inarejea, haki inarejea kwa mwana wa ukoo wetu, haki iliyokuwa imechukuliwa na kwenda kusipostahili inarejea kwake….’ilikuwa ni mbiu ya mgambo, iliyokuwa ikipigwa na mshereheshaji mashuhuri wa jamii ya Mzee Hasimu.

Kila mmoja alitega sikio kusikia ni nini anachotaka kukielezea, na kwa vile minong’ono ilishapita , minong’ono iliyojaa propaganda potofu, ambayo huwa inasikilizwa zaidi kuiko ukweli. Kutokana na propaganda hiyo, wengi walitaka kujua kuwa kuna ukweli gani kwenye hilo waliloliskia, na waliposikia hiyo mbiu ya mgambo, na kinachoelezewa, wakazidi kuingiwa na hamasa ya kuliona tukio zima.

Ama kwa hakika lilikuwa tukio kubwa ambalo kila mmoja alilisubiria, kwani kama ilivyobashiriwa, siku hiyo ndiyo iliyotakiwa mfalme, kupewa kiti chake, na malikia kumiki wana wa jamii zote bila ubaguzi, lakini ili aweze kulifanya hilo ni lazima apate mume bora, mume shupavu, jemedari, na kiongozi muadilifu.

Kipindi chote cha mwaka, walikuwa wakimsubiria kiongozi , ambaye ndiye atakayeweza kulifikisha taifa hilo kule walipoahidiwa baada ya miaka ya nyuma ya vita na kumwaga damu. Walikuwa wakimsubiria  malikia mtarajiwa, malikia mama wa wanajamii wote, kwani hata pale walipompata malikia malikia mwenyewe, bado, kiumri alikuwa hajafikia hatua ya kuingia kwenye sehemu takatatifu, , wakawa wanaisubiri hiyo siku ili waweze, kutawadhwa na kukabidhiwa majukumu ya kijami.

Muda uliokuwa ukisubiriwa ndio umefika, na majira yaliyokuwa yakisubiriwa ndio hayo yamefika, tatizo likabakia ni nani mfalme, maana huyo waliyetarajia kuwa ndiye mfalme, wamesikia kuwa kaliwa na mamba, jambo ambalo liliashiriwa kuwa huenda sio yeye aliyestahili kuwa mfalme.

Majira hayo yalikuwa ni ya mavuno, na majira hayo ya mavuno, kila mwanajamii hupeleka zawadi kwenye jumba, au sehemu wanayoitambua kama sehemu takatifu, zawadi hizo, wanaamini kuwa ni sadaka, kwa ajili ya baraka za familia zao, na zawadi hizo ndizo zinazotumika kwenye sherehe za kijamii, na mojawapo ya sherehe hizo ni ya kumsimika mfalme na malikia na mambo mengi ya imani zao.na pia kwa ajili ya kuweka akiba kwa siku zijazo.

‘Tumesikia kijana wa mzee mteule, kaliwa na mamba, hivi ni kweli hii, na kama ni kweli, ina maana kweli hakustahili kumuoa malikia mtarajiwa, sasa ni nani atakaye muoa?’ akauliza mama mmoja.

‘Unauliza jibu, eti ni nani wa kumuoa malikia, humuoni kijana wa mzee Hasimu,…hilo limeshapitishwa na baraza la wazee, nani atapinga hilo’akasema mama mwingine, huku akijiangalia alivyovalia, tayari kwa shughuli, kila mmoja alijioana kavaliwa zaidi ya mwingine, mavazi rasmi ya shughuli ya kimila.

‘Na kama ni hivyo, ni nini hatima ya ukoo wa mzee mteule, kwasababu kama uongozi wote utakwenda kwa hasimu wake, sizani kuwa ukoo huo utaruhusiwa tena kuwepo kwenye jumba takatifu….nawaonea sana huruma, ….maana wao wamejitahidi sana kuonyesha uongozi bora’akasema mama mwingine huku nay eye akijiangalia alivyovalia.

Watu walianza kujiandaa, kila mmoja akitafuta nguo yake maalumu, nguo ya kutokea, tayari kuwepo kwenye sherehe kubwa, na hakuna aliyekubali tukio hilo limpite, hata wazee vikongwe, wagonjwa, kila mmoja aliomba asaidiwe afike hapo kiwanjani, kwani wengi waliamini kuwepo kwao, kunaweza kuwasaidia katika maradhi yao,  na matatizo yao, na wazee wataweza kujaliwa nguvu za kuweza kuishi zaidi.

Katika imani zao , kiongozi, sio tu kuwa kiongozi, lakini kiongozi anatakiwa kuwa na karama, ya kuweza kuwaombea wagonjwa na wenye shida wapone. Kiongozi, anatakiwa mtu ambaye akiletewa tatizo anajua jinsi gani ya kulitatua, na kiongozi alitambulikana kama mzazi wa kila mtu, …kwahiyo kila mtu aliona ni muhimu kufika hapo kwa mzazi, na kwa mtoto kutokufika kwa mzazi ni kuvunja heshima na adabu.,

La mgambo lilipolia, kila mmoja akajua siku imefika, na asiye na mwana aeleke jiwe, na asiye na ngo ya maana akaazime kwa jirani, kila mmoja alikuwa na upendo uliopitiliza, na hakuna aliyeombwa kitu siku hiyo akakataa kama anacho. Na siku hiyo kila mwenye tatizo, hulibeba tatizo lake, na kulifiksha huko, kwa ajili ya maombezi, wakijua ndio mwisho wa matatizo. Siku maalumu iliyotabiriwa.

********

Malikia mtarajiwa alikuwa ndani kwake, akiwa kashika shavu, hakukubali moyoni kuwa kweli mumewe ndio basi tena, kila mara alikuwa akiinua kichwa kuangalia mlangoni, akitarajia kuwa ataingia mumewe, mumewe aliiyempenda kwa moyo wake wote, mume ambaye kwake yeye alijua kiwa karibu yake, hata kazi hiyo ya umalikia angeliiweza kuifanya kwa ufanisi zaidi.

Lakini kila alipoinua kichwa kumwangalia aliyeingia, alijikuta akiangaliana na wapembe waliotumwa na kutoka kwa wahasimu wao. Ingawaje kwa muda huo, hakutakiwa kuwaona kama mahasimu wake, kwani kama ni kweli mumewe keshakufa huenda wakawa sio wahasimu wake, tena, ni wapenzi wake.Hilo aliliomba listokee, lakini je dua yake ingekubaliwa, wakati mumewe hajatokea.

Alikumbuka babu yake alipokuja asubuhi, na wazee wenzake, ujio wao ulikuwa kama wa kumuaga, na ingawaje walisema bado hawajakata tamaa, lakini ilionyesha dhahiri kuwa kuja kwao ilikuwa ni sehemu ya kumpa baraka kuwa anaruhusiwa kuondoka hapo na kwenda huko kwenye jumba takatifu tayari kwa mume mwingine mpya ambaye anatarajiwa kutoka upande wa mhasimu wao.

‘Binti yetu, kama tulivyokuambia, siku ya leo ndio siku iliyotarajiwa, siku ambayo tuna uhakika kuwa mfalme alitabiriwa , ambaye anatakiwa amuoe malikia mtarajiwa atatawazwa, …hii ni kusema kuwa kila mmoja, hana mamlaka tena ya kulipinga hilo litakalotokea leo, ….tunatarajia, au tulitajia kijana wetu atafika, lakini hadi sasa kama unavyoona hakuna dalili yoyote….’akatulia huyo mzee, na malikia alikuwa kama kamwangiwa maji ya baridi kusikia kauli hiyo

Usiku kucha alikuwa akiombea kuwa wazee hawo wakifika watafika na kauli yenye matumaini, na alikuwa tayari kusikia kuwa watazua tukio hilo lisifanyie siku hiyo hadi kweli ijulikane kuwa mumewe hayupo tena dunia, na uchunguzi ufanyike ili kubainisha ni nini kilichomsibu mumewe, kwani huenda kuna hujuma ilifanyika, lakini kauli ikawa kinyume chake.

‘Hatujakata tamaa, kwanii saa ya mwisho ni saa ya jioni, …wenzetu wao wameshajihakikishia kuwa kijana wetu hayupo tena, ndio maana wamejiandaa kwa kila kitu…na ndio maana wametuma wapambe wao kuja kukuweka sawa…sisi hatuwezi kuwazuia, na wewe usikatae kwa lolote lile…ila bado tunasubiri hadi saa ya mwisho…’akasema mzee

‘Dalili kuwa kijana wetu bado yupo hai, zinajionyesha….na mimi nina uhakika atajitokeza …lakini je imani hiyo ipo kwa wote,…kwahivi sasa hakuna mwenye imani hiyo tena, kila mmoja keshaamini kuwa kijana wetu hayupo hai tena. Mawazo ya kila mmoja ni kuangali ni nini atakipata siku kama ya leo, ….hakuna anayejali uhalali, hakuna nayejali, kuulizia ni kweli kijana yetu aliliwa na mamba, au kuna hujuma ilifanyika.

Siku ya leo, kila mmoja ni kama watu wenye njaa walioona chakula mezani, unafikiri nini kitafuata, kama sio kila mmoja kufikiria jinsi gani atashibisha tumbo lake, hata kama wengine watakosa, ….hakuna mwenye kumjali mwenzake, zaidi ya tumboo lake….

Hata hivyo, tukubali ukweli kuwa siku ya leo nii siku tukufu, ni siku ya matarajio, sisi kama wenzetu, siku ya leo ni siku ya matajio, ya kumsimika kijana mpya ambaye ndiye atakayekuwa mfalme…..sisi kama wazee, tumekuwa tukijiuliza kama hivi ndivyo ilivyo, je ni kweli huyo kijana wao anastahili kuwa mfalme,mfalme yule tuliyemtarajia…’akawa kama anauliza huyo mzee.

‘Kwahiyo binti yangu, hapo ndipo tunaingiwa na wasiwasi, lakini hata hivyo hatuwezi kufanya lolote, siku kama ya leo haitakiwi kumwaga damu, siku kama ya leo, inaongozwa na baraka, zilizoasisiwa na wazee wetu waliotangulia, na lolote litakalofanyika leo, ni matarajio, na limebarikiwa, ya kesho yatajileta yenyewe,….

Kama itatokea kama ilivyo, keshao itasema, nakuhakikishia kuwa kama sio kweli, kama hafai, na wametumia ujanja, ulaghai na nguvu, lazima kutatokea kipingamizi…kwa upande wetu hatuwezi kufanya lolote hadi siku hii ipite…’akasema huyo mzee.

‘Tunakuomba uvute subira, na ukubali kwa lolote lile, hadi hatua ya mwisho…sisi kama wazee tunaojua haya mambo, hatuna wasiwasi, …ndio kama binadamu tuna wasiwasi kuwa huenda kijana wetu kazuiliwa sehemu, na ndio maana kashindwa kutokea…lakini tutafanyeje kwa hali kama hii….’akasema huyo mzee.

‘Jeshi tunalo na limejiandaa kwa lolote lile, linasubiri amri..lakini sio siku kama ya leo…hatuwezi kutumia nguvu,…usije ukaona kuwa tumekutelekeza, hapana, …siku kama ya leo ni siku muhimu sana hapa kwetu, na inayoaminika kuwa ni siku tukufu, sote tunatakiwa tutulize shughuli zetu, tuombe, tushukuru, …’akasema huyo mzee huku akinua mikono juu, na wenzake wakafuatilia hivyo hivyo.

‘Na wewe malikia mtarajiwa, huna kipingamizi, wote wamekukubali, kwahiyo  baraka zako zinahitajika kwa wanao wote, uwakubali wote kuwa wewe ni mama yao, bila kujali kuwa anatokea huku au kule, bila kujali kuwa ni ukoo gani, ni hali gani,…hiyo ndiyo hulka ya mama , malikia mtarajiwa…tuliza kichwa chako na elekeza maombi yako kwa mwenye nguvu wa kila jambo, najua tutafanikiwa…’akasema huyo mzee na kuinamisha kichwa

Hapo malikia hakutakiwa kusema lolote au kuongea lolote, anachotakiwa na kuinua kiganja chake cha mkono na kuwashika wazee wale kichwani mmoja mmjoa,, na baadaye wote wakaondoka, akabakia peke yake, na hapo hakuweza kuyazuia machozi tena, akashindwa kuvumilia machozi yakamtoka , akajitahidi kuziia kwikwi,…akijua kuwa yeye ni mama wa wote, na anhitajika kukubali yote kuwa ni mapnzi ya mwenye nguvu zaidi ya wote…..

Moyoni malikia alikumbuka ndoto yake, ndoto ambayo iliashiria harusi, …harusi ambayo aliiona ni tofauti na harusi za hapo, akiwa ndani ya hiyo ndoto, alijiona kavalia nguo za huko alipotokea, na wazazi wake wakiwa pamoja naye, na muda huo walikuwa wakimsubiria mume mtarajiwa kutokea, lakini alikuwa kachelewa, kiasi cha kuwakatisha tama watu…haikupita muda mara kwa mbali wakasikia vigelegele, kuashiria kuwa mume keshafika.

Akiwa kwenye hiyo ndoto, alijiona yupo kasimama akimsubiri huyo mume mtarajiwa afike ili wafungishwe ndoa, na muda ulikuwa ukienda, ….na ndoa hiyo ilikuwa na muda maalumu, ukipita haiwezi kufungwa tena, na kila akiangalia mishale ya saa, ilikuwa ikionyesha kuwa kumebakia dakika chache, …akawa anageza kichwa kungalia huko mumewe anapotokea, mara kwa mara kwa matarajio, lakini hakutokea na muda ulikuwa ukienda kwa kasi….

Na ikawa imebakai dakika moja..mume hajatokea….akawageukia wazazi wake, na wao, walikuwa wakiangalia kule mlangoni ambapo mume anatakiwa atokee..haonekani, nje ni vigelegele na shangwe, na hapo akataka amwambie mmoja wa watu wake aende nje akamlete huyo mume kwani muda unapita, na alipogeuka kuangalia saa akakuta imebakia dakika moja inakimbilia kwenye sekunde, na mara mlango ukafunguliwa…

Kipindi hicho yeye alikuwa akiongea na mpambe wake, kwani alitaka kumuelezea kuwa aende akawaharakishe huko nje, na mpambe wake alikuwa kamziba, kwahiyo hakuweza kuone kule mlangoni, kitu ambacho hakutaka kiwepo, kwani yeye alitaka kuona jinsi mume wake atakavyotokea pale kwa mara ya kwanza…..akawa anataka kunyosha mkono, kumuondoa mpambe wake, kwani alichotaka kumwambia hakina maana tena.

Kila mmoja pale ndani kwanza alipumua kwa shauku, na huku wakishukuru, na nyuso zilizoanza kukata tama zikabadilika na kujaa furaha, kila mmoja akijiandaa kuona huyo mume ametokelezeaje.
Mara mtu wa kwanza akatokea, ambaye ndiye alitakiwa kuwa mumewe mtarajiwa, …mara nyuso za watu zikabadilika , kutoka kwenye nyuso za tabasamu, na kuelekea kwenye nyuso za woga,..macho yakawatoka pima kwa woga,…

Vipi tena, …mara watu wakainuka kwenye viti vyao,.. hakuna aliyesubiri…kwa sekunde chache tu, kila mmoja  alitafuta sehemu ya kutokea, ……ikawa ni purukushani….bibi harusi akajikuta yupo peke, yake, akawa sasa anageuza kichwa, kwani muda huo alikuwa akiwaangalai watu wakikimbia, akashikwa na mshangao, sasa akawa anageuza kichwa taratibu kuanglia kule mlangoni, kuona nini kimetokea hadi watu wote wakimbie…mara akafumbua macho, …..kumekucha.

NB: Nimeona niitoe sehemu hii kama ilivyo, ...sina jinsi, 

WAZO LA LEO: Sasa hivi ni hapendwi mtu, hasa kunapokuwepo na masilahi, na hata wengine husihia kusema `mjini hapa' ...lakini tukumbuke kuwa haki ya mtu haipotei bure, kula utakula, lakini ipo siku utaulizwa. Tafuta riziki yako kwa chumo halali ili upate baraka.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Yasinta Ngonyani said...

Tupo pamoja..kazi nzuri sana....