Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, November 24, 2012

Uchungu wa Mwana aujuaye ni mzazi-27

 Adam, alipotoka pale kwake, aliondoka kwa kujificha hadi sehemu ambayo walipanga kukutana na wenzake, alipofika hapo, akakuta taarifa hiyo kuwa anatafutwa sana na Malikia, akajua ni kwanini, akaona ili kuzuia shari ni bora amwendee huko huko nyumbani kwake, lakini akagundua kuwa hawezi kumkuta nyumbani kwake, kwasababu ya msako wa polisi.

Akamtafuta mtu wa karibu wa Malikia, na huyo jamaa akamwambia wapi anaweza kumpata Malikia, na hpo hapo akaelekea huko alipoelekezwa, na huku akielekea huko kwa tahadhari, maana hata yeye ni  mmoja wa watu wanaushukiwa kutafutwa na polisi, kwahiyo ilibidi awe makini, akawa anawaza;

‘Huyu nisipomuona anaweza kwenda kumsumbua Kais, na nisingelipenda itokee hivyo, ikizingatiwa ana mtoto mchanga,  …’akasema na wakati huo alikuwa keshafika eneo aliloelekezwa, na wakato wote huo, hakujua kuwa nyuma kuna watu wanamfuatilia. 

Alipofika mitaa ya vichochoroni, hapo akili yake ikatulia, na zile hisia zake za jabu ajabu zikaanza kumsumbua, na tangu afike hapo Mererani, amekuwa akizipuuzia hizo hisia, lakini hapo akahisi kuna jambo,…akatuliza akili, na kuanza kutafakari, afanye nini kuhusu hizo hisia, zinamuashiria kitu gani, akakumbuka kuwa polisi wapo kwenye msako, na hiyo hisia inamkanya kuwa awe na tahadahari.

Akaanza kuingia vichochoroni, kuhakikisha hakuna mtu anayemfuatilia kwa karibu, aliafanya hivyo hivyo, hadi, akafika mtaa  wa kichochoroni, na hapo akahisi yupo salama, ndipo akaanza kuitafuta ile hoteli aliyoelekezwa, ambayo ipo ndani kwa ndani, na ukifika hapo huwezi kujua kuna nyumba ya wageni.

Akagonga mlango wa ile nyumba ya wageni,  akaona kimiya, akagonga tena, na kusubiri, na wakati anasubiri, akahisi hisia ya taahdhari,…haraka akageuka nyuma, aliona kama mtu akijificha kwa mbali,lakini hakuwa na uhakika, lakini hisia zikamtuma kuwa yupo kwenye hatari,…

‘Lazima kuna mtu ananiufuatilia hii sio bure,…’ akaona ili athibitishe hilo, arudi huko alipotoka huenda akakutana naye, lakini swali likamjia kwa haraka je, kama ni askari, atafanaya nini, na yeye wiki nzima sasa amekuwa akiwakwepa.

Hakusubiri tena kuonana na Malikia,  akageuka na kuanza kurudi alipotoka, na hata alipofika pale alipohisi kuna mtu, hakuona mtu yoyote, akarudi hadi maeneo ya mjini, na alipofika huko mjini, akatafuta sehemu ya kupigia simu na kumpigia malikia, hakutaka kabisa kutumia simu yake.

‘Unasikia malikia, kuna watu wanakufuatilia, hapo ulipo ondoka haraka’akamwambia.

‘Sikiliza wewe…mimi sio wa kuja, hilo nalijua sana,.. na kwa taarifa yako nipo huku ulipomficha Malaya wako, na ole wake nikimkuta, atanitambua kuwa mimi ni nani, na huyo kifaranga wenu, atanitajia jina lake kabla hajafikia muda wake wa kuongea,…’akasema na kukata simu.

Adam, aliposikia hivyo, hakujali tena kuangalai nyuma, akaanza mwendo wa haraka kwenda huko alipompangia chumba Kais, alijua asipomuwahi huyo malikia anaweza akafanya lolote baya, na huyo mwanamke hataweza kuvumilia, na kwa vile ni watu wa huko msituni ambao wanajulikana kwa hasira lolote linaweza kutokea. Akakumbuka alivyohadithiwa na watu wanaowafahamu watu wa msituni

‘Wanawake wa msituni ni kama wanaume, wanaweza kupambana hata na simba, na wana hasira sana, kama mkikosana naye, inabidi ujifunge kweli kweli, kwani anaweza akakuumbua’alikumbuka jamaa yake akisema.

‘Na ole wake umguse mtoto wake, wana hasira hawo, ni sawa na kuku umguse kifaranga chake, atakutoa macho…..’akakumbuka, na hapo akajua huko kutakuwa na vita vikali, maana na Malikia naye hana dogo…akazidiwa anaweza kutumia silaha yoyote, na kumtoa roho mwanadamu mwenzake, kwake kazi rahisi, tu….

Alifika sehemu ya nyumba hiyo, akagonga mlango , kulikua kimiya, akagonga tena, na mara mlango ukafungulia, akajikuta yupo uso kwa uso na malikia, wakaangaliana kwa macho ya kuulizana bila kusema neno, na Adam, akageuka nyuma, akahisi hali ile ile ya kuwa kuna mtu anamfuatilia, akahisi mwili ukimsisimuka kwa woga,..lakini  kwa muda ule hakujali, alichojali ni kuhakikisha usalama wa Kais na kichanga chake.

‘Yupo wapi Kais, ….maana naona nyumba ipo kimiya?’ akauliza.

‘Ndio jina la huyo Malaya wako, eeh, Kais, jina gani hilo lisilo na mvuto …..’akasema Malikia akiwa kakunja uso kwa hasira.

‘Nimekuuliza swali,  yupo wapi Kais, maana huyo ni mgeni hapa mjini, na hahusiki lolote na maisha yetu, na ukumbuke ana mtoto mchanga..’akaanza kuongea Adam.

‘Hayo maelezo yote ya nini,….mimi hayanihusu, kinachonihusu ni pesa yangu unayotumia kuhongea ,Malaya wako, na kulelea watoto wasio wako, toka lini ukawa msamaria mwema, mtu ambaye hata senti moja yako hutaki ipotee hivihivi…’akasema Malkia akitokeza kichwa nje kuangalia huku na kule.

‘Kwanza niambie huyo jamaa aliyesimama pale mbele ni jamaa yako?’ akauliza Malikia.

‘Jamaa gani, mimi sikuja hapa  na mtu yoyote, nipo peke yangu’akasema Adam, huku akiangalia huko nje bila ya kuona mtu yoyote, lakini kwenye hisia zake alihisi kuwa kweli kunawezekana kuna mtu bado anamfuatilia, lakini kila akigeuka huwa hamuoni.

‘Tatizo lako haupo makini kabisa, na hujajifunza kila ninachokufundisha, sasa naona una doa jeupe kisogoni mwako, uwe makini,….’akasema Malikia akiwa bado anaangalia nje kwa makini.

‘Nilihisi kuna mtu, nikampoteza….sizani kama atakuwa kaja hadi huku, nimechukua tahadhari zote, lakini nahisi….., ‘akasema Adam, akiwa na wasiwasi, akikumbuka jinsi alivyoteseka siku moja aliposhikwa na kuweka mahabusu, na akaambiwa kuwa hapo ni mahabusu tu, huko jela ndio balaa…akaanza kuhisi wasiwasi.

‘Tatizo lako huyajui haya maisha ya kutafuta pesa, unachojua wewe ni kutumia tu, hujui pesa hizo unazotumia zina jinsi yake ya kuzitafuta, na maadui wapo kila kona, na nimepata taarifa Komandoo yupo hapa mjini….’akasema Malikia.

‘Kwani huyo Komandoo ni nani, maana kila mtu anamuongelea yeye tu, ana tofauto gani na askari wengine?’ akauliza Adam.

‘Ipo siku utakutana naye, utajionea mwenyewe, huyo hajali pesa, akiamua kazi ni kazi tu, na huwezi ukajificha, popote ulipo atakupata tu, sijui ni mwanga yule jamaa….sasa kwako wewe nahisi jela inakunukia, na mimi sikubali kukamatiwa hapa…nilikufuata kwa kazi maalumu…’akasema huku akichungulia tena nje.

‘Kazi gani kipindi kama hiki….’alalamika Adam, na Malikia akamwanalai usoni, kwa macho ya kumsimanga, akahisi moyo wa huruma ukimwingia, kitu ambacho anajiuliza kwanini anapokutana na huyo mwanaume inakuwa tofauti na wanaume wengine…akamsogelea na kumshika shavuni kwa mkono wake lakini, akasema;

‘Huu sio muda muafaka wa kukupa hiyo kazi,….mimi naishia, tafuta muda tuonane tena haraka, ukiwa na pesa yangu, la sivyo, utaozea jela….hilo nakuhakikishia, …na kama sio jela, utarudishwa kwenu na jeneza’akasema Malikia huku akichukua mfuko na haraka akatoka nje.

‘Sasa unakwenda wapi,  hujaniambia kuhusu Kaisi na mtoto wake, umewapeleka  wapi?’ akauliza.

‘Kama bado muda huu unamuwaza huyo Kais, badala ya kuwaza jinsi ya kujitoa kwenye mtego wa maaskari, hivi huoni kuwa umeshazungukwa na maaskari, hao watu wanakufuatilia ndio hawo vijana wake, wanachotafuta ni muda muafaka wa kukunasa, kuwa makini, mtoto wa mama, ….unadeka sana,….haya nakutakia kila la  heri, na kwa jibu la swali lako, utalipatia huko huko jela , zubaa hapo hapo uone….’akasema Malikia na akitokomea mitaani.

Malikia, akatoa khanga kwenye mkoba wake, akachukua wigi, akalivaa, halafu taratibu akatoka nje, na haikuchukua muda, kukawa kimiya, akabakia Adam, akihangaika huku na kule, hakujua wapi Kais, kaeleeka na mtoto mchanga, au huenda Malikia kamtimua…..na mara hisia za hatari zikatanda akilini mwake.

Adam, akatoa kichwa nje, na kuangali huko na kule, lakin hakuona mtu, ila alihisi kuna mtu…..hisia zikamtuma hivyo….kuna mtu yupo nje, anamsubiri. Akarudisha kichwa ndani na kwa haraka akaanzakukagua mle ndani, ndipo akakuta kuwa nguo na vitu vyote vya Kais havipo, na hata nguo za mtoto hazipo, akajua huyo mwanamke atakuwa keshaondoka, na kama keshaondoka atakuwa kaelekea wapi na mtoto, …akatoka nje, na kuwauliza majirani.

‘Yule mama mwenye mtoto asiyejua Kiswahili vyema, ameondoka na mtoto wake, amesema anahisi sehemu hiyo haina usalama kuishi na mtoto wake,…alituambia ukija,  kama unamuhitaji unaweza kumpata sehemu ile ulipomchukulia’akaambiwa.

‘Aliondoka peke yake?’ akauliza.

‘Ndio alikuwa peke yake….’akaambiwa.

Adam, aliposikia hivyo, akajua huyo mwanamke huenda karudi kule eneo la mlimani na lengo lake ni kurudi huko kijijini kwao. Akaona ni vyema kumfuata huko huko, lakini safari hii akaona awe mwangalifu, kwani hizo hisia kichwani mwake, zinamtahadharisha kuwa kuna hatari, kwahi kwanza cha muhimu ni lazima amjue huyo anayemfuatilia nyuma ni nani, na je kuna usalama kwake, asije akawa ni polisi.
Kabla hajaondoka, akaanza kutafuta ….

Akafunua godoro, na kuangalia pale alipokuwa kauweka mzigo wake, …hakuna kitu, akaanza kuingiwa na wasiwasi, akaliondoa godoro lote, hakuona kitu, akachukua kistuli, akapanda juu yake, na kwa juu akafunua kifuniko cha mbao, ambacho alikibadua mwanzoni na kwa juu akaweka sehemu ya mzigo wake, na hapo ahkuona kitu, ….

‘Huyu atakuwa na Malikia, maana yeye ndiye alinifundisha mbinu hizo za kuficha mizigo ….hakuna angeligundua kuwa nimeficha mzigo mwingine sehemy kama hiyo, na sizani kuwa ni Kais, huyu hawezi kujua nimi umuhimu wa huo mzigo, au ni huyo jamaa aliyekuwa akinifuatilia, ….hapana huyo atakuwa ni  Malkia.

‘Yaani kaamua kuchukua mzigo wote na pesa yangu yote, ..nitaishije mimi, …hata mimi sikubali’ ‘ mara akasikia sauti za watu wakiongea kwa nje, akachungulia dirishani, ….akaona ni jamaa wawili wageni usoni mwake, mmoja alikuwa akionyeshea kidole mlangoni kwake, 

‘Hawa ni polisi….’akasema kwa wasiwasi, akageuka na kuangali dirishani la nyuma,, akalifungua na kuchana nyavu zake ambazo zilikuwa kama nguo, na bila kupoteza muda, akaruka, na kuanza kukimbia,….

********

Malikia alifika sokoni, na alijhisi kuwa kuna mtu yupo nyuma yake anamfuatilia kwa muda mrefu, akajua ni hawo vijana waliokuja karibuni, ambao hajazoeana nao, akawa anatafuta njia ya kumvuta ili amuone sura yake lakini kila aliposimama , jamaa huyo hujificha…

‘Huyu anaonekana ni mgeni wa kazi hii, ngoja nimuonyeshe kuwa mimi ni mtoto wa mjini’akasema na kujichanganya na watu pale sokoni, akaingia kwenye mgahawa halafu akaingia chooni, alipotoka alikuwa sio yule Malkia wa mwanzo, na akaelekea kule alipotoka, hakufika mbali,akakutana na yule jamaa ambaye kwa muda huo alikuwa akihangaika kumtafuta mtu wake.

‘Vipi kaka yangu unamtafuta nani?’ akamuuliza, na yule jamaa akashituka na kusimama kumwangalia huyo mwanadada, kwanza alionyesha uso wa mwanaume pale anapomuona binti mrembo, na baaadaye akajifanya kujionyesha yupo kazini, akasema.

‘Hapana simtafuti mtu…..’akasema na kugeuka kutaka kuondoka.

‘Kama unamtafuta Malikia najua wapi pa kumpata’akasema huyo binti
Yule jamaa akashituka na kugeuka kumwangalai huyo mwanadada, na huyo mwanadada akageuka uso haraka kuelekea kule sokoni, kama vile anamuonyeshea yule askari huko alipo huyo Malikia.

‘Nani kakuambia kuwa namtafuta Malikia, na wewe ni nani, mbona unafanana naye sana, Malikia ni ndugu yako?’ Safari hii akashindwa kuficha ile sauti yao ya kiaskari .

‘Wengi wanasema hivyo hivyo, kuwa nafanana na Malikia, ….lakini hatuna udugu wowote na yeye, Nimekuona ukimfuatilia toka kule, hukuweza kujificha, kwa jinsi ulivyokuwa ukimfuata kwa nyuma na kumtizama tizama, …haya niambie una nia ya kumpata huyo malikia au umeghairi uliponiona mimi….?’ akamuuliza.

‘Wewe niambie yupo wapi, ….mengine sina haja nayo?’ akasema.

‘Mengine yapi…afande, unafikiri mimi ni Malaya au,…mimi nimeamua kukusaidia tu, sina haja ya mengine, twende huku nikakuonyeshe alipo huyo Malikia maana kila mwanaume akiingia huu mji anampapatikia huyu binti,…. mungelimjua vyema huyo mwanamke, mngekuwa waangalifu sana….’akaambiwa, na yule jamaa kwanza alisita kumfuata huyo binti, lakini baadaye akaamua kumfuata nyuma huyo dada, huku akidadisi;

‘Kwanza kwanini unaniita afande, kwani…’akasita kidogo , na baadaye akauliza swali jingine, kwani huyo Malikia yupoje, inaonekana ni mtu wako wa karibu japokuwa sio ndugu yako, huyo Malikia yupoje, hebu niambie….?’ Akalegeza sauti na kuuliza.

‘Utamjua mwenyewe ukikutana naye, haina haja ya kuumiza kichwa chako, pesa yako itaongea, kama huna pesa, sizani kama mtaelewana….’akaambiwa na wakati huo walishafika kwenye mgahawa mmoja, mlango wake ulikuwa na pazia kubwa jeupe, na walisikika wateja wakiongea kwa ndani, na yule jamaa akaangalia huku na kule kwa nje, ..baadaye akanyosha mkono kulifungua lile pazia

Hapo hapo wakati ananyosha mkono,  akahisi hatari, alipotaka kugeuka kuangali kwa nyuma yake, kitu kizito kikigonga kichwani kwake, hakuweza hata kujitetea, akaona vinyota, na giza likatanda usoni, alichosikia kwa mara ya mwisho ni sauti nyingi zikibishana, nyingine zinasema hivi, nyingine hivi;

‘Huyu ni kibaka, achomwe moto,….. nendeni mkachome moto huko mbali sio hapa hotelini kwangu…hapana msimchome moto sio kibaka…’fahamu zikampotea.

 NB: Hayo ndio maisha ya Kais na Adam, je hawa wataishia wapi, naona sehemu ijayo turudi porini tujue ni nini kiliendelea pale tulipoishia.

WAZO LA LEO:  Jitahidi sana usitawaliwe na tamaa, hasa tamaa mbaya, ni vyema ukarizika na kile ulichojaliwa nacho, kama unataka zaidi fanya yale yaliyo mema, epuka vishawishi vibaya, usitamani vya watu,  kwani tamaa mwisho wake ni mauti.


Ni mimi: emu-three

2 comments :

Anonymous said...

Sasa ni mwendo wa kusua sua...sio mbaya hata hivyo ubarikiwe sana

Anonymous said...

Hiyo display yako ya nyuma nimeipenda sana