Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, November 19, 2012

Uchungu wa mwana Aujuaye ni Mzazi-25




Kwa marejeo: Kais alipohisi kuwa huyo mwanaume, aliyemuona na yule mwanamke, ni askari wa mzee Hasim, alikimbia….., je alikimbilia wapi, na huko alipokwenda aliishia wapi, ukumbuke kuwa binti huyo alikuwa mja mzito, je ujauzito wake uliishia wapi….tuendelee sehemu hiyo ya Kaisi……..

Kais, alipozindukana alijikuta yupo kwenye kitanda, na wakati hupo tumbo lilikuwa likimuuma sana, na harufu aliyoisikia hakuwahi kusikia kabla, akageuza kichwa huku na kule, lakini hakuona mtu kwa upeo wa mcho yake. Akainua kichwa na , kwa mbali akaona watu wamevaa nguo nyeupe, moyoni akajua ni malaika, akakumbuka hadithi alizowahi kusimuliwa za malaika kuwa ni wao ni weupe, na kwasababu hawana dhambi, kila kitu chao ni cheupe.

‘Ina maana nimeshakufa nipo mbinguni,…nipo peponi na malaika’akawaza na kabla hajaweza kuinua kichwa vyema, mara akahisi kuna watu wameshikilia miguuni yake, na sauti zikawa zinaongea, mmoja akasema,;

‘Huyu tusipomfanyia upasuaji, tunaweza tusiwaokoe wote’

Kais akawaza hawa malaika wanataka kumfanya nini, kumfanyia upasuaji, haiwezekani, kwao hakuna kitu kama hicho, wanaamini kuzaa ni kwa njia ya kawaida tu, kuna dawa unakunywa, na haichukui muda kujifungua, na kabla hajajua nini kinachoendelea, akahisi tumbo likaanza kumuua, liliuma sana, maumivui ambayo hakuweza kuyavumilia akaanza kupiga ukulele.

Mmoja wa wale, watu ambao yeye aliwaona kama malaika, wakaja na kumshika vyema, na mmoja akawa kashika sindano,..Kais aliogopa sana, lakini hakuweza hata kujitetea, kwani mwili ulikuwa hauna nguvu hata ya kuinua mkono, kutokana nay ale maumivu, akapigwa sindano, ambayo ilimfanya atulie, na kuzama kwenye giza, …alipozindukana akasikia kitoto kikilia..

‘Mtoto wako mnzuri ana afya njema,..’ akaambiwa, na alipogeuza kichwa pembeni, akaona kitoto kimelazwa kwenye kitanda kidogo pembeni yake. Kilikuwa cheupe, kizuri, akatabasamu, na akainua mkono na kukishika. Baadaye aliwageukia wale watu ambao kipindi cha nyuma aliwaona kama malaika, lakini sasa akili ilikuwa imetulia, na ile hali ya mwanzo aliiona kama ndoto, akasema;

‘Kumbe nyie sio malaika, nilipozindukana mara ya kwanza nilijua nyie ni malaika, na mnaongea lugha ambayo ni ngeni kidogo kwetu, lugha hiyo kule tulikuwa tuiita lugha ya watu waliopotea,….tunaifahamu, na tunaisikia, lakini kuongea kwetu sio sawa na nyie, kama mnavyonisikia…’akasema.

‘Hapa ni hospitalini, kuna mtu aliokuokoa, kama asingelifanya hivyo, na kukuleta hapa haraka, huenda unengelikuwa kwenye hali mbaya….na jinsi ulivypotoza damu nyingi…..lakini tunashukuru, tumeweza kuwaokoa wote wewe na mtoto wako, …’akasema huyo mtu ambaye alikuja kumfahamu kuwa ni dakitari.

‘Ni nani aliyeniokoa?’ akauliza Kais, huku akiwa na hamu ya kumfahamu huyo mtu aliyemuokoa

‘Ni mwanaume mmoja, yeye anashughulika  na biashara za madini, na anasema kipindi wakiwa huko maporini kutafuta hayo madini, ndio akakuona ukidondoka kutoka huko milimani, na hali aliyokuona nayo, alijua umeshakufa, aliwaita wenzake, wakagundua kuwa bado upo, wakatafuta usafiri ukaletwa hapa hospitalini’akaambiwa.

‘Hospitalini…mmh, kule kwetu, wanasema nyie watu mliopotea, mkiwapeleka watu hospitalini lazima kwanza muwachukue damu, kwa ajili ya kuuza, akasema na hasa alipoona ile mipira iliyoning’inizwa pembeni yake’akasema.

Watu pale ndani wakacheka na yule aliyesikia akiitwa Docta akasema;

‘Hizo ni imani zenu, nimewahi kusikia imani kama hizo, kuna mgonjwa mmoja aliwahi kuja kutibiwa, na alipoona tunamuwekea hiyo mipira kwa ajili ya kumuongeza damu, au maji, alitaka kukimbia, mpaka tulipomuelewesha, na alituambia habari kama hiyo, sio kweli, kuwa tumawanyinya damu, hapa tulikuwa tukikuongezea damu…’akaambiwa.

‘Damu hiyo imetoka wapi, ya wanyama, au damu ya nani?’ akauliza Kais.

‘Hiyo ni damu ya watu waliwahi kujitolea, …na lazima hiyo damu iwe sawasawa na ya kwako, huwa hatuchukui damu ya mtu yoyote tu, ni lazima ipimwe kuwa ni salama, na kuhakikisha kuwa ipo sawa na damu yako’akasema Docta.

‘Mnajuaje kuwa damu hiyo ipo sawa an damu yangu?’ akauliza Kais.

‘Kwanza tunachukua damu yako, tunaipima na vipimo maalumu vya kupimia damu, na kwenye vipimo hivyo ndipo tunagundua kuwa wewe damu yako ipo kwenye kundi gani, kwani kila mwanadamu ana kundi lake la damu, na baadaye tunatafuta damu sawa sawa na kundi lake’Docta akawa anamuelezea Kais, na Kais akashangaa sana, na kusema;

‘Kweli huo ni utaalamu, ningelipenda kuwa kuujua,..huko kwetu bibi yangu ni mtaalamu wa ukunga, na anajua dawa nyingi, hata za kuongeza damu, sikuwahi kumuuliza jinsi gani anavyowaongezea damu watu waliopungukiwa, lakini yeye anajua dawa nyingi sana’akasema.

‘Amesomea wapi bibi yako?’ akauliza nesi.

‘Amefundishwa na bibi yake…kwao ukoo wao ni wa matibabu..’akasema na baadaye akasikia wakiongea kuhusu malipo yake, na yule Dakitari akasema;

‘Usijali, tunashukuru, kuwa huyo mtu aliyekuleta hapa kalipa kila kitu, wewe ukipona utaruhusiwa na kurudi kwenu, kwani kwenu ni wapi?’ akaulizwa.

‘Kwetu..?’ akauliza kwa kushangaa, na baadaye akasema;

‘Mimi kwa hivi sasa sina kwetu, kwetu wameshanifukuza, kama nitabahatika kurudi kwetu, wataniua’akasema na watu pale ndani wakashikwa na butwa, na huyo dakitari akamuuliza;

‘Kwanini wakuue?’ akaulizwa.

‘Ni mila na desturi zetu, huenda nyie hamuwezi kuzielewa mila na desturi zetu, ni za kizamani, kutoka kwa mababu zetu, na huwa tunawajua nyie kuwa mliziogopa ndio maana mkakimbia na kwenda kuishi maisha ya laana’akaseman Kais, na watu wakacheka.

‘Hawa ndio wale watu wa msituni, kama yule mgonjwa aliyeletwa, akiwa kaumia, wakipigana vita, …hawa watu wanaishi mapangoni, na kama wakijenga nyumba, ni ndogo ndogo za udongo,…’akasema Docta.

‘Nyie ndio wale watu wa msituni,..nimeshawajua, eti nyie mnakula watu?’ akauliza nesi ambaye alisema anatoka karibu na hawo watu wa msituni.

‘Hapana, sisi hatuli  watu, hata sisi tunasikia kuwa kuna watu wanakula watu, lakini mimi siwajui, na sisi hatuli watu, japo kuwa tunaishi huko msituni’akasema Kais.

‘Na huyo mume wako aliyekupa huu ujauzito, hakuweza kukutetea?’akaulizwa.

‘Mume wangu…?’ akauliza kwa mshangao, na baadaye akasema;

‘Hakuweza, kwanza ujauzito huu nilikuja kuugundua nikiwa naishi porini, ..sehemu ambayo nilitupwa, ili nikaliwe na majoka, kama adhabu, na sijui kama kweli anajua kuwa nina mimba yake, angelijua,wangelinichukua, hadi nijifungue, na wanahakikisha kuwa naliwa na mamba, na mtoto wanamchukua …’akasema na watu pale wakazidi kushangaa, hawakuamni kuwa kuna watu wana imani kama hizi, wakawa na shauku sana ya kujua hizo mila za huko.

‘Kwanini hasa waliamua kukutupa ili ukaliwe na mijoka,?’ akaulizwa, na kabla hajajibu, mlango ukafunguliwa, na wakaingia jamaa wawili, na mmoja alikuwa kabeba mfuko kuonyesha kuwa kaleta chakula cha mgonjwa.

Docta, akawakaribisha, na yeye akaondoka, alibakia nesi, ambaye alikuwa karibu na mtoto. Yule nesi alipowaona hawo wanaume, akawachangamkia, inaonyesha alijuana nao sana, na kila mara huypo nesi, alikuwa akiwaangalia kwa uso ambao Kais, alihisi ni wa kimapenzi, na yule mmojawapo ambaye likuwa kashika mfuko akasema;

‘Jamani mgonjwa wangu anaendeleaje,…na mtoto?’ akauliza huyo mwanaume huku akiwa anamwangalia Kais.

‘Mgonjwa wako hajambo ana shauku sana ya kukuona, anataka akupe ahsante kwa kujitolea kumsaidia’akasema yule nesi. Na yule mwanaume akasogelea kitanda, na macho yake yakaangaliana na yule mgonjwa. Kais akatabasamu, na kusema;

‘Ahsante sana , ndio wewe uliyetuletuokoa, nashukuru sana…’akasema Kais

‘Usijali, vipi unaendeleaje?’ akauliza huyo mwanaume mmoja, wakati huo yule mwanaume mwingine alikuwa akiongea na yule nesi.

‘Sijambo, kama ingelikuwa kwetu, ningelitoka nje, kufanya shughuli mbalimbali, huwa ukishajifungua unatakiwa ufanye kazi ili upone haraka’akasema Kais.

‘Huwezi kufanya kazi kwa sasa hivi, unahitajika kupumzika,ili upone vyema, ..’akasema huyo mwanaume.
Na baaadaye yule mwanaume mwingine akaja na wote wawili wakasogelea kitanda na kumwangalia yule mtoto, ambaye kwa muda ule alikuwa kalala. Na wakati huo Kais, macho yake yakatulia kumwangalia huyo mwanaume ambaye ndiye aliyemuokoa, na hakupoteza muda akasema;

‘Nashukuru sana kwa kuniokoa na mtoto wangu, sijui hata cha kukulipa, ….’akasema Kais

‘Usijali, hilo ni jukumu la kila binadamu, ukiona mwenzako katingwa na shida, au yupo kwenye hali kama uliyokuwa nayo wewe, inakuwajibu kumsaidia, maana sisi sio wanyama, sisi ni binadamu, leo kwangiu kesho kwao..au sio?’ akasema yule mwanaume, na Kais akawa anamwangalia huyo mwanaume huku akili yake ikiwa inatamani kuendelea kumwangalia. Na yule mwanaume alikuwa akiongea na mwenzake.

Baadaye yule mwanaume akawa anaaga kuondoka, akisema atajihahid kufika hapo baadaye, na hapo Kais akashindwa kuvumilia, akauliza

‘Kwani wewe ni nani, mbona unaongea kama unafahamu sana kabila letu?’

‘Kwa jina mimi naitwa Adam, nafanya biashara ya madini na kule kijijini ninapotoka, nilikuwa mara nyingi nikikutana na watu wa kabila lako, na vijana wengine walikuwa wakifika kwetu, …nawafahamu sana watu wa kabila lako’akasema Adam.

‘Umesema unaitwa Adam,…basi na mtoto wangu nitamuita Adam,?’ akasema Kais na kutabasamu. Adam, naye akatabasamu na kusema;

‘Ndio naitwa Adam, kama unalipenda hilo jina , hakuna shida, na baba yake anaitwa nani? akauliza na kabla hajajibiwa Kais akageukia upande ule aliolazwa mtoto , kwani kitoto kilikuwa kikilia,…na nesi akawa anamwangalia kama yupo sawa, na yule mwanaume akasema;

******

‘Unafanana sana na msichana mmoja nilikuwa namfahamu,…yeye alikwenda kusoma, na baaadaye kukatokea matatizo na familia yao, sijui kama atakuwa hai, maana baba yake ni mkali kupindukia, alitaka kumuua mtoto wake kwa sababu …….,’akasema halafu akasita kuendelea.

‘Kwanini alitaka kmuua, au baba yako ni mtu wa huko kwetu, maana watu wa huko kwetu hawatakiwi kuacha asili, wakiacha asili yao, wanakuwa kama wehu…’akasema Kais.

‘Huenda  baba yake ni watu wa msituni, sina uhakika kwa hilo, ila hata mimi nimeponea chuchupu, ilibidi nikimbe huko nyumbani, japo kuwa nilikuwa na mipango ya kuja huku kutafuta maisha’akasema Adam, baada ya kuja kumtembelea siku nyingine na siku hiyo ilitakiwa Kais atoke hapo hosptalini.

Mara docta akaingia, na kuwaelezea, kuwa mgonjwa na mtoto wake wanaruhusiwa kuondoka, na hawa deni, hapo Kais akamgeukia Adam, na kumuuliza yeye atakwenda wapi, na Adam akasema keshatafuta chumba ambapo wataishi yeye na mtoto.

‘Mimi ni mtu wa migodini, huko nisingelipenda wewe kwenda kuishi na mtoto, wewe utaishi huku mjini, hadi hapo nitakapojua jisni gani ya kufanya. Bado ninhangaika na misha. Sijaweza kufanikiwa, na siku nikifanikiwa nitajenga nyumba utaweza kuishi wewe ni mtoto…’akasema Adam.

‘Mimi nimezoea popote naishi, nimeishi porini peke yangu, kwahiyo kama hakuna jinsi, nitatafuta wapi pa kuishi, ilimradi tu, nisije nikaishi sehemu ya watu’akasema Kais, akiwa anajiandaa kuondoka.

‘Hapana, huwezi kuishi porini, mimi nimejitolea kwa jaili yako, nakuona kama yule msichana wangu niliyemuacha, ni kwa vile mambo yangu hajawa sawa, nineglikuchukua tukaishi pomoja huko migodini,…’akasema akita kumwambia ukweli, kuwa kuna msichana mmoja anayeishi naye matata, na hata hapo keshapigiwa simu mara nyingi kwanini anachelewa kurudi.

‘Huyu msichana bwana ananifanya kama mtoto wake, hataki niwe huru, yeye ananiendesha kama gari bovu, keshanianay nikosane na mjomba wangu’akawa analalamika kwa rafiki yake.

‘Nani malikia, yule nilishakuambia uachane naye, wewe umeona umefika kwake, ukiendelea naye, ujue unaweza ukakosana na hata wazazi wako, yule anachojali ni pesa, na ukiwa huna pesa huwezi kuwa rafiki yake,..achana naye’akaambiwa.

‘Sio rahisi hivyo…’akasema, akikimbuka kuwa huyu msichana alimsababishia wakamuibia mjomba wake, na anadai siku akikiuka masharti yake, atamwambia mjomba wake kuwa yeye ndiye aliyemuibia, na pia kwa vile anajuana na maaskari, atawaambia biashara wanayofanya ya haramu ya madawa ya kulevya.

Adamu alijikuta akifanya biashara hiyo baada ya kuishiwa, kwani biashara ya mdini aliyotegemea hakufaulu, kazi za migodini, zilikuwa ngumu, na madini yamekuwa adimu, na kile kidogo alichowahi kupata kikawa kikishia kwa Malikia ambaye alikuwa hatosheki.

Siku moja Malkia akamjia na kazi  hiyo mpya, na kumwambia biashara hiyo ina faida, kubwa, na ili aweze kuishi inabidi aifanye, la sivyo, atarudi kijijini akiwa mikono mitupu. Adam, alikataa kata kata, lakini haikuwa rahisi kwa binti huyo, akashawishika mpaka akakubali.

Alianza kama mzaha, na baadaye akajikuta keshazoea, na ikawa kazi ya kukwepana na maaskari, na hata siku aliyomkuta Kaisi milimani, walikwenda huko kujificha baada ya kutafutwa na maaskari.

‘Mimi nitakuacha hapa nimeshalipia hiki chumba kwa mwaka mzima, cha muhimu na jinsi gani ya kupata hela ya kula, na humu ndani nimenunua vifaa vya karibu mwezi mzima, ni wewe tu uangaliajinsi ya kuvitumia, ….nitakuwa nikifika mara kwa mara kuangalia kuwa una shida gani’akasema Adam.

‘Wewe usijali kuhusu maisha yako, nashukuru umenisaidia vya kutosha…’mara simu ya Adam, ikaita na Adam, akaipokea, na kusikia sauti ya Malikia ikimkoromea.

‘Unasikia wewe usipofika leo na pesa yangu, nitahakikisha unakwenda kuozea jela, pesa yangu hujanipa na ule mzigo ulishamaliza, pesa yangu ipo wapi?’ akaulizwa.

‘Sikiliza wewe mwanamke, ile pesa imeibiwa..hapa nilipo sina hata senti moja, kama unataka nikafe jela, sawa….’akasema Adam.


‘Eti nini imeibiwa wakati nimesikia umeonekana na Malaya mmoja mwenye kichanga, utaniambia ulimpia wapi hiyo mimba, ni nikimuona atanitambua kuwa , kwanini naitwa malikia wa Mererani. Adam, aliposikia hivyo, akageuka, kumwangalia Kais, na mtoto wake, na alipogundua kuwa hakustahili kuipokea hiyo simu hapo, akatoka nje. Na aliporudi alimkuta Kais akifungasha mizigo yake akitaka kuondoka.

‘Unakwenda wapi?’ Adam, akamuuliza huku akiichukua ile mizigo kuiweka ndani.

‘Mimi sitaki matatizo, nimesikia ukiongea na mke wako, na inaonyesha kuwa anakudai pesa yake, umesema huna senti hata moja, mbona umesema umenipia kodi ya nyumba, pesa umepatia wapi, mbona unamdanganya mkeo naogopa akija kunikuta hapa anaweza akaniua na mtoto wangu’akasema Kais.

‘Mimi sina mke, huyo ni tajiri wangu tu, tunafanya naye biashara, kuna pesa alinikopesha ndio anazidai, na wala hajui kuwa wewe upo nami, hakujui kabisa kuwa wewe unaishi hapa…’akamwambia.

‘Kwahiyo haya yote unayafanya kwa kijificha, sio pesa yako?’ akauliza Kais.

‘Kwa hali uliyokuwa nayo, ilibidi nifanye hivyo, lakini sio tatizo, haya ndiyo maisha yetu, uisogope. Hata hivyo huwezi kuondoka hapa kwasababu nimeshapalipia, ukiondoka hapa, atakaa nani kwenye hii nyumba, na kodi ya nyumba nimeshalipia, usiwe na wasiwasi…’akaanza kumshawishi ili asiondoke, akimwangalia na yule mtoto.

`Mimi sitaki matatizo , maana huko nilipotoka nimeyakimbia matatizo, na ikizingatiwa kuwa nina hiki kiumbe cha watu, hakina hatia, ni bora mimi niumia lakini huyu mtoto aisguswe, ….na yoyote atakayeninyanyasa kwa ajili ya hiki kiumbe, sitamsamehe…ujua mimi ni mwanamke wa porini’akasema Kais, na Adam, akageuza kichwa pembeni, akiombea mungu, Malikia asije akafika hapo.

NB. Je Malikia hataweza kufika hapo, na akifika hapo itakuwaje?

WAZO LA LEO: Ni vyema kutowahusisha watoto wetu kwenye migongano yetu, ama iwe ya kifamilia, au kijamii, kwani watoto ni sawa na malaika, hawana dhambi. Hususani kwa wanandoa, inapotokea mgongano wa hapa na pale, hakikisheni watoto wenu wanakuwa mbali, na sio vyema kuwahusisha, kama bado ni wadogo.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Yasinta Ngonyani said...

Hapa naona Malkia akija itakuwa matata kweli nasubiri kwa hamu kusoma nini kilitokea. Nimelipenda wazo la leo maana ni kweli huwa tunawasahau kabisa watoto. Tupo pamoja!!