Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, October 22, 2012

Uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi-12
Adamu alimwangalia yule binti akiongea, na kuingiwa na hamasa naye, hasa pale alipokuwa akiongea kwa haraka haraka, kama redio iliyofunguliwa kwa mwendo kasi, Adam akawa anamwangalia huku akimsikiliza kwa makini, na kwa vile kulishapambazuka,aliweza kumuona vyema usoni. Kwa muda alikuwa keshaondoa ile khanga aliyokuwa kajifunika.Na nywele zake zilikuwa ndefu.zikiwa kama zimepakwa rangi,...

Adam akamwangalia usoni, anavyotabasamu anavyobenua mdomo kwa dharau, kwakweli kila kitu chake kilimvutia sana Adam.

'Huyuu binti mnzuri sana,mbona sijawahi kumuona kabla?' akajiuliza kimoyomoyo,na hapo hapo akamkumbuka binti rafiki yake wa shuleni, na kumlinganisha na huyu binti, akashindwa kutofautisha nani zadi, baadaye akamuliza yule binti;

‘Hebu niambie wewe ulifikaje Mererani, maana naona wewe unaonekana ni mwenyeji huko, na unaonekana kufahamu mengi ya huko kama vile na wewe ni mmoja wa wachimbaji wa madini,  uliwahi kuingia machimboni nini?’ akauliza Adam.

Yule binti akacheka kidogo, uso ukameremeta, halafu ghafla ukawa unafifia, uso ukawa unabadilika kutoka kwenye tabasamu na kwenda kwenye huzuni. Adam aliangalia yote yale, alimuona huyu binti kama wale waigizaji aliowahi kuwaona kwenye sinema.

Yule binti alitulia kidogo kama anatafakari kitu, halafu akamuangalia Adam kwa makini,na yale macho yake, gololi za ndani zikawa zinazunguka, kama vile anamchora Adam. Macho yake yalikuwa makubwa  yanayovutia, na yalionekana kuwa na usiri mkubwa, au jambo ambalo limejificha ndani ya nafsi za huyu dada, na huenda alitaka kuliongea lakini bado alikuwa na wasiwasi, Adam alihisi hivyo, na pia Adam, aliingiwa na mawazo mengine kuwa huyu binti sio kuwa ana mvuto, bali inaonekana kuwa ana kitu cha zaidi.

Adam, huwa ana kipaji cha kumsoma mtu, lakini yeye mwenyewe hajijui kuwa yupo hivyo, hili alikuwa nalo tangu akiwa shuleni, alijikuta yupo hivyo tu, kuwa anaweza akamwangalia mtu akamjua kuwa huyu ana kusudio gani, au ana nia gani, huenda ikawa mbaya au nzuri, na kweli akimwangaia mlengwa ,huyo mlengwa anasema kweli alikusidio hivyo. Hata siku moja alipomuuliza baba yake kwanini ana hulka hiyo, baba yake akamwambia;

‘Binadamu tulivyo, kila mmoja kazaliwa na kipaji chake, na hili utaweza kulifahamu  kwa mtoto wako akiwa bado mdogo, sisi wazazi wako tulikugundua hivyo, kuwa una kipaji fulani, tangia ukiwa mtoto, na tulijua kuwa huenda kipaji hicho kikakusaidia kuwa msomi mzuri, lakini tulishangaa, ulivyobadilika ghafla.

Kweli mwanzoni darasani Adam alikuwa akifanya vizuri sana, lakini alipoingia darasa la tano akaanza kupoteza muelekeo, akawa akifika darasani anaonekana kuwa na mawazo sana, na kidogo kidogo akaanza kushuka kielimu, na ikifika mahali hata darasani haingii, kabisa, au anaweza akaonekana mara moja moja.

Walimu walijaribu kumhoji, na hata kuwaita wazazi wake, lakini haikusaidia kitu, ikabakia kusubiria amalize hilo darasa la saba akabidhiwe kwa wazazi wake. Hii hali ilianza pale alipokuwa akirudi nyumbani na kukuta wazazi wake wakigombana, au wakati mwingine anakuta ndugu kwa ndugu wanagombana, baba yake na baba wengine, au wakati mwingine anakuta baba na mama yake hawaelewani kwasababu hali ya uchumi ni ngumu, basi Adam akajiona hana raha.

Haya aliyaongea siku baba yake alipotumia mbinu nyingi za kumbana mwanae, baada ya kugundua kuwa kutumia nguvu, kwa kumchapa viboko haikusaidia lolote, akaamua kutumia hekima, na kuwa karibu naye, na siku mmoja kijana wake akamwambia baba yake kwanini hali ilifikia kiasi hicho, akasema;

‘Baba mimi nimebadilika kutokana na hali halisi iliyopo hapa nyumbani, mimi sioni raha nikiwaona wazazi wangu mnataabika, kula kwa shida, matatizo mengi yakugombea ardhi, wakati mwingine mimi nagombana na ndugu zangu, nyie mnaingilia, unakuwa ugomvi mkubwa. Mimi naona ajabu sana wewe na ndugu yako juzi mumegomabana kwasababu ya ardhi, sehemu ndogo tu, sasa nikaona labda ni kwasababu ya umasikini wetu’akasema Adam.

‘Sio hivyo mwanangu, hayo yote ni kwasababu wote tulikaa tukitegemea mali ya baba, urithi wa baba, baba yetu alikuwa tajiri sana enzi zake, na kutokana na utajiri wake, sisi watoto tukalemaa, kila mmoja akiwa anauchungulia huo utajiri, kuwa na mimi nimo, hatukutaka kusoma, na mama zetu wakawa wanatukumatia kila mmoja na watoto wake,…hilo ndilo kosa tulilofanya.

‘Baba yangu alipofariki tu, tukaanza kugombea mali yake, kila mmoja akidai haki yake na kuona anahitaji zaidi ya mwingine, haki ambayo hatukuitolea jasho, na wala hatujui jinsi gani baba na wazazi wetu kwa ujumla walivyohangaika na wake zao hadi kufikia hapo na kuitwa matajiri wa enzi hizo…

‘Maana baba yangu alikuwa na wake wengi enzi zake. Alikuwa ni mmoja wa viongozi wa kabila letu, kwahiyo,pamoja na mali nyingi, pia alitakiwa kuwa na wake wengi….alikuwa na mifugo mingi, mashamba , ambayo wake zake walikuwa wakiyahudumia kwa bidii kubwa. Enzi zao wake walichaguliwa kutokana na bidii zao katika kazi..

‘Hayo ni maisha ya baba yangu na enzi zake, lakini sio maisha yetu, sio maisha yenu, maisha yetu, na sasa yenu yamegeuka, enzi zeni bila shule utakuwa mtumwa wa wenzako,…usituige sisi kwasababu tulilemaa, kwa vile hatukutaka kujiendeleza, hatukutaka kutafuta kwa jasho letu,ili tuweze kukiendeleza kile alichokiacha baba yetu, ili kiwe kikubwa zaidi.

‘Mwanangu, hakuna kitu kinachorudisha maendeleo kama kugombana, kama kuwekeana chuki, kwani ndani yake kuna adui shetani, ambaye kawekeza kwenye ubinafsi, kila matu anaona kila kitu ni chake,na anahitaji zaidi sio kwa kuhangaika,bali kwa kumdoea mwenzake,na kumuonea kijicho. Maana sisi tulibakia kukigombea kile kidogo alichokiacha baba, kilionekana kidogoo kwasababu ya wingi wetu, na hatukutosheka na mgawo, tukawa tunaingiwa na husuda.

‘Mimi na ndugu zangu tukawekeana kijicho, kila mmoja sasa anataka kuchukua haki ya mwingine, tukajenga uadui, ndugu kwa ndugu wa damu moja. Kwasababu baba alikuwa na wake wengi, kwahiyo hata watoto walikuwa wengi pia, na itikadi tofauti, na hilo lilichangia sana kukuza mgogoro. Mgogoro ukikita kwenye itikadi ya mtu, unafanya mambo yanadumaa, hata akili ya kutafakari, kutumia hekima, au kutumia ile elimu yenyewe ya itikadi ile inasimama,kinachobakia mbele ni ubinafsi …ni hii ni hatari kubwa

‘Vita vya wenyewe kwa wenyewe vikazuka, …mwanangu usione hivi kumepoa, hapa kulikuwa hakukaliki, kila mara kulikuwa na vita vya kupigana mapanga mimi na ndugu zangu, kwa kosa dogo tu, ilimradi kila mmoja anatafuta chanzo, ili aweze kumuondoa mwenzake, tumesahahu kuwa enzi za baba tulikuwa tunakaa meza moja tunakula pamoja.

‘Enzi za baba ilikuwa kama sherehe, baba anatukutanisha pamoja, tunakula pamoja, tunahadithiana hadithi , tunacheza, yaani kulikuwa na raha ya aina yake, lakini mdudu mtu amekuja pale tu wazazi wetu hawo, walipoondka duniani, kila mmoja na mama yake, kila mmoja na mambo yake,tukawa tunaanza kunyosheana vidole na hata kuitana wachawi…tulisuluhishwa sana, na baadaye sijui upepo gani umepita, wengi wameamua kutawanyika, kutafuta maisha sehemu nyingine maana ile mali tuliyokuwa tukigombea imekwisha.

‘Ina maana baba, kumbe babu yangu alikuwa tajiri, na pia mgogoro w augomvi wenu umatulia baada ya watu kutawanyika kwenda sehemu nyingine kutafuta maisha?’ akauliza Adam.

‘Sio tajiri tu, baba yagu alikuwa mmoja wa viongozi wa kabila letu, sisi ukoo wetu ni mashuhuri sana, lakini ulikuja kuharibika kipindi chetu. Baba yetu alituacha tukiwa bado vijana, na mawazo yakuona  mbali yalikuwa hayapo, kwasababu tulilelewa kitajiri, kila tunachotaka tunapata, hatutaka kujituma zaidi.

‘Ndio maana mwanangu nataka usome ili uweze kuirudisha heshima ya ukoo wetu, tunajua ukisoma ukawa na elimu, kizazi chako kitaiga, na ukoo huu utasonga mbele, kuliko kuwa na tamaa ya mali ambayo kuipata kwake ni kwa kubahatisha na hata ukiipata hutaweza kujua jinsi gani ya kuiendeleza, na ili ujue hayo ni kwa kupata elimu safi.

‘Baba mimi akili yangu ni kuondokana na huu umasikini, na sioni sababu ya kusoma, wangapi wamesoma lakini hali zao hazina tofauti na mimi, na baba ukumbuke kuwa elimu yenyewe inahitaji pesa, siku hizi elimi bila pesa hakuna, sasa hizo pesa mnatarajia tutazipata wapi, nasikia enzi za nyuma wenzangu mlikuwa mkisoma bure, siku hizi hiyo haipo tena!’

‘Tutatafuta mwanangu,…tutachangishana, wanafamilia tupo, kidogo kidogo utasoma’akasema baba.

`Sasa ina maana tuanze kuchangishana,wanandugu, wanandugu wenyewe kula yao ni shida, wanandugu wenyewe hamuelewani, na hebu nikuulize, mkishachangishana nikaamua kusoma, na bahati nifanaikiwa na kupata kazi, ni nan nitamsaidia maana kila mmoja atakuwa na matarajio kutoka kwangu kutokana na mchango wake alioufanya kwangu?’ Adam akamuuliza baba yake.

‘Ukisha pata elimu, ukapata kazi, utakuwa na mwanya wa kuwasaidia wenzako kwa njia nyingi tu, kwa mfano unaweza ukawa kiongozi, kama vile  mbunge wa eneo letu, utakuwa na nafasi ya kuwasaidia wenzako  kwa mapana zaidi, sio tu familia yenu tu, bali wilaya nzima, huoni ni faida kubwa sana,..’akasema baba yake Adam, lakini Adam hakumuelewa.

‘Niwe mbunge,niwe meneja,lini…baba tuwe wakweli, angalia majirani zetu, watoto wao wamesoma,nini walichofanya…wengine wamekuwa walevi, wengine, ndio hawo, kila siku wapo wa mabarabarani, wamegeuka wanasiasa wasio na jukwa, kila mahali kwao…baba mimi nipeni mwanya, mtaona wenyewe’akasema huku akionyesha ngumi mbele.

Baba alimwangalia mtoto wake kwa muda, akiwa haamini kuwa huyu ndiye yule mtoto wake aliyemuelewa, au ni mwingine, akatikisa kichwa,  na kwa muda huo Adam,alikuwa akiendelea kutikisa ngumi hewani

Adamu alikuwa mbali akiwazia mali, akiwazia kuchuma kwa haraka ili aondokane na huo umasikini ulikithiri ndani ya familia yao, na aliona sehemu muhimu ya kupatia hiyo mali ni huko machimboni. Na hili lilijijenga pale alipomuona mjomba wake akiwa katajirika, ana miradi na ana maisha mzuri, akaaona huko ndiko kwa kupatia maisha bora,

******

Adam alishituka toka kwenye mawazo ya familia yake, pale yule mwanadada alipomshika bega, alihisi ulani wa mkono wa yule mwanadada, na mwili ukamsisimuka, na akilini akawa anajiuliza, vipi mkono laini kama huo ukaweza kufanya kazi, ina maana huyu mwanadada huko machimbo atakuwa anafanya nini…

Yule mwanadada hakusema kitu kwa muda ule, alitulia kimiya huku mkono ukiwa bado umeshikilia bega la Adam,  na Adam akatulia akisubiri, kuwa huyo mwanadada atasema lolote, lakin hakuna neno, alilosema huyo mwanadada, alikuwa kimiya, alishangaa sana kuona ukimiya huo wa ghafla wa yule mwanadada, kinyume na jinsi alivyomzoea kwa muda huo mfupi waliokuwa naye, akahisi huenda hilo swali alilomuuliza mwanzoni limemkera.

Huyu binti alikuwa akianza kuongea anakuwa kama redio iliyofungulia kwa sauti ya kasi, huwa anaongea kwa haraka haraka bila kutulia, utafikiri anaogopa muda utaisha kabla hajamaliza kile alichokusudia kukisema. Akageuza uso na kwamwangalia moja kwa moja Adam machoni mwake, na akatabasamu, na kusema;

‘Adam hivi mimi unanionaje?’ Adam, akashangaa kwa lile swali.

‘Nakuonaje kwa vipi…?’ akamwangalia kwa muda halafu alipomuona yupo kimiya na huku kamkazia macho Adam akasema;

‘Mimi nakuona ni binti mrembo, na sioni kwanini usiolewe na kutulia na mume wako kuliko kwenda huko Machimbo, ambapo nahisi kwa binti kama wewe hakukufai’akasema Adam.

Yule binti akawa akawa anajiangalia kama vile anajikagua, halafu akatulia huku kainamisha kichwa chini, alitulia vile kwa muda, hadi Adam akahisi kuna kitu kizito ambacho huenda kakisema na kumkwaza huyo binti.

Adam,  akajaribu kurejea mazungumzo yake kichwani, jinsi walivyokuwa wakiongea, ili kuona kama kuna kitu kakisema ambacho anaweza kukihisi kuwa ndicho kimesababisha hayo yote, na ndipo akakumbuka hali hiyo ilijitokeza pale alipomuuliza huyo binti kama aliwahi kuingia machimboni, na alikumbuka alipomuuliza hivyo, ndipo hapo huyo binti alipotulia ghafla na kuwa kama anawaza jambo

Adam, akaona aliulize tena lile swali ili kuona kama ndilo linalomfanya huyo binti awe hana raha, kwanza akamuangalia yule binti kwa makini, na wakati huo huyo binti alikuwa kainama chini, na mkono mmoja kautumia kama kushika kichwani karibu na macho, kama vila anataka kulala, lakini yale macho yalionekena hayajafumbwa, ina maana alikuwa akiwaza jambo.

Baadaye yule binti akahisi anaangaliwa, akainua uso kumwangalia Adam, halafu akatabasamu, na huku bado anamwangalia Adam usoni, na wakawa wanaangaliana kwa muda bila kusema kitu.

Adam, hapo alihisi kitu kwenye mwili, wake, alihisi kitu kwenye fikara zake, na kutamani kumwangalia huyo binti, na ile hali ikamfanya yule binti ashikwe na aibu, na kuinama chini, halafu akainua uso tena na kumwangalia Adam, na kusema;

‘Hivi mimi naonekana Malaya?’ akauliza swali ambalo Adam hakulitegemea kabisa, na Adam, akaangalia pembeni kuwaangalia abiria wengine waliopo humo ndani kama wamsikiea hiyo kauli, lakini wengi wao walikwua wametulia, kila mmoja akiwa na mawazo yake, Adam, akageuka kumwangalia yule binti, aakmkuta kama anaangalia hewani,au juu,akionyesha kuwa mwingi wa mawazo, na Adam akasema;

‘Kwanini unaniuliza swali kama hilo, mimi sikujui  vyema, na siwezi nikamwambia msichana mrembo kama wewe neno kama hilo, kiujumla huonekani hivyo, ..kwanini umeniuliza hivyo?’ akauliza Adam.

Yule binti akatulia na mara macho yakajawa na ukungu, na ghfala machozi yakaanza kumtoka yule binti, na baadaye kwa haraka akayafuta na kuangalai pembeni, hakusema kitu kwa muda, alikuwa kimiya kiasi kwamba Adam alijiona mpweke, na ndipo akaona ni bora amuulize tena huyo binti, na kaba hajauliza yule binti akasema;

‘Mimi naweza kuwalaumu wazazi wangu kwa haya yote, ingawaje sio vizuri, kwani wao kwa muda huo walikuwa wakiona kuwa wanachonifanyia ni  sawa, na wanafanya hivyo kwa vile wananipenda,lakini kumbe walikuwa wakinitumbukiza shimoni, shomo la tala, shimo la moto….’ akasema huyu binti huku machozi yakiwa yametanda usoni, na ndipo akaanza kusimulia maisha yake.


Ni mimi: emu-three

2 comments :

Anonymous said...

Tulikumiso mkuu, usituache muda mrefu, maana moyo unashindwa kusubiri, kazi nzuri m3

Anonymous said...

yaani mpaka kufikia hapa nishasahau stori ilipoanzia manake nadani yake kuna stori za watu kama watano hivi,hata sielewi tena. labda ungekuwa angalau unamalizia stori ya mmoja mmoja au unaipeleka hadi pale itakapokutana na ya mwenzake ndio unasonga mbele, inshort umenichangaya sana natamani hata nisiendelee, ila stori inaonekana nzuri sana.