Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, September 5, 2012

Mbio za sakafuni huishia ukingoni-sehemu ya pili-2


‘Ponda maisha rafiki yangu, huwezi jua ya kesho, mwenzako sasa hivi yuko huko kikaoni, wakimaliza kikao tu, usiku wanajimwaga kwenye mabaa, unajua nini kinachoendelea huko kama sio kunywa, kula nyoma choma na .....baada ya hapo utajaza mwenyewe..’hayo yalikuwa maneno ya shoga yangu, alipoanza kunijaza hisia ambazo sikuwa nazo kabla.

Kutokana na hayo maneno, vishawishi, na hata kwenda kujionea mwenyewe, nikawa nimebadilika kabisa,na kuwa na  tabia ambayo sikuwa nayo kabla,tabia ambayo mpaka sasa naijutia, na kujiuliza kwanini nilifikia hapo,…na ni nini nimekipata baada ya hapo, zaidi ni kuathirika kiakili , kimwilii na sijui kama afya yangu itatengemaa tena, kama sio kuelekea kaburini….nimeshakata tamaa ya kuishi.

Tabia hii ilianzia kubadilika kidogo kidogo, hasa pale nilipokutana na shoga yangu huyu. Yeye ndiye aliyeanza kunijaza maneno, na ndiye aliyenitoa kwenye tabia ya malezi ya wazazi wangu hadi kuwa mwanamke wa mafiga matatu, ….najuata sana, na hata kama nilivutwa na hali ya mume wangu, lakini sikustahili kujiingiza kwenye haya machafu…..hadi, hadi….’hapo alishindwa kuongea akawa analia.

Yaani tabia hiyo ilianza kama mchezo wa kuigiza,….naikumbuka sana siku ile nilipokutana na rafiki yangu huyu na hatimaye nikakutana na mke wa adui wa mume wangu, ilianza hivi....

***
 Huyu rafiki yangu alikuwa akija kwangu mara kwa mara, na tulikuwa tukiagiza bidhaa pamoja toka nchi za nje, na tulifikia hatua ya kuaminiana sana. Kutokana na msimamo wangu, alishindwa kabisa kuniingiza kwenye mambo mengine nisiyoyataka,hadi pale aliponiletea hii taarifa kuwa kaipata kutoka vyanzo venye uhakika. Nilimkatalia kata kata na kusema;

‘Mimi siwezi kuamini hayo maneno yako maana namjua vyema mume wangu, tunapendana na kuaminiana sana, na kazi yake hiyo aliyojiingiza nayo inahitaji awe msafi, hawezi kujiingiza kwenye hayo machafu’nikamwambia huyo shoga yangu.

‘Kama unabisha ipo siku nitakuleta ushahidi uone mwenyewe, mimi mwenyewe nilikuwa nikimwamini sana mume wangu, lakini siku moja nikaifuma barua toka kwa hawara wake wa nje, na hata nilipombana sana hakukubali ukweli,, nikasema ngoja, basi siku moja walipoondoka tu, na mimi nikafunga safari, nikawafuatilia nyuma…’akasema huyo shoga yangu.

‘Hayo mambo ndiyo siyataki kuyasikia, achana na hizo habari, kama huna kazi sema nikue kazi unisaidia kupanga haya marobota huku juu,....mimi najiuliza kwanini umfuatilie mume wako kwani hamuaminiani, huoni huko ni kujiumiza mwenyewe, na utajiweka katika hali mbaya ya kusononeka bure’nikamwambia huyo shiga yangu.

‘Ndio maana nakuambia kuwa na wewe usijifungie nyumbani, ukimaliza kazi hapa jichanganye na wenzako, katumie muda huu, maisha yeneywe mafupi, …kutana na wenzako hata ikibidi tafuta figa la pili na la tatu, pata rafiki wa siri wa kuaminika, ambaye siku moja moja unakuwa naye,anakutoa upweke, …’hayo maneno yake, yalinifanya nimfukuze, hapo ofisini kwangu,  na yeye  akabakia kunicheka, na kusema.

‘Ipo siku utaamini maneno yangu, ..’akasema lakini sikutaka kabisa kumsikiliza, na nilijitahidi sana kumkwepa kuongea naye nikijua huyo ni ibilisi wa kibinsadamu, ukimfuata anaweza ukapotea,

Lakini siku moja nikakutana na yule  mke wa aliyekuwa rafiki wa mume wangu,....huwa anakuja hapo dukanikwangu akihitaji nguo mpya. Siku ya kwanza alipokuja hapo kwangu nilimuheshimu sana,kwani yeye nilimuona kama mkombozi wangu, maana isingelikua yeye, ningelikuwa nimeshaolewa na huyu jamaa anayejifanay ni tajiri.

Ingawaje baadaye, baada ya mume wangu kujiingiza kwenye siasa, tulianza kujenga uadui na huyo mwanamke, hasa kipindi kile cha kampeni na uchaguzi,..tulifikia hadi kuwa maadui, kwasababu ya mambo hayo ya kisiasa, kwahiyo kukutana kwetu ilikuwa sio kwa urafiki , ni kwa vile alihitaji nguo mpya, na mimi ndiye niliyekuwa nikileta nguo anazozipenda.

Siku hiyo nilikuwa kwenye duka langu la nguo, na humo ndani kuna vitu vingine vya urembo, nikiwa nimechoka na nilijiandaa kufunga duka, nikajipumzikie,kwani nilikuwa nimekata tamaa ya kupata wateja kwa siku hiyo ya jumapili.

Nikiwa nafunga funga amhesabu, mara mlangoni akaingia huyu mama, alikuja na wafanyakazi wake, wakasema wanahitaji nguo za harusi ya ndugu yao, na mapambo yake, nikaanza kuwahudumia. Na moyoni nilijua nitaingiza pesa ya maana , kwani mara nyingi akija huyu mwanadada, huwa ananunua vitu vingi.

Kwa namna nyingine alikuwa mteja wangu mzuri, licha ya upinzani wa kisiasa , na kwangu mimi, mteja ni mfalme, nikampokea kwa kunyenyeka, na yeye bila hiana akajikaribisha, baada ya kuchagua alichokitaka, akaniomba tuongee ndani ya ofisi yangu.

Nikashikwa na mshangao, maana sio kawaida yetu , yeye akija, na kununua alichokihitaji, analipa pesa nakuondoka zake,na alishanaimbia, kama hizo nguo zingelikuwa zinapatikana sehemu nyingine asingeliweza kuja hapo kwangu. Sasa leo kaja na mpya, anataka tuongee, na maongezi yenyewe anahitaji yafanyikiea kwenye ofisii, sehemu yenye faragha, nikaogopa.

`Kwani una maongezi gani na mimi hadi tuongelee hko ofisini...?' nikamuuliza.

'Usiwe na wasiwasi, ....ni maongezi ya akwaida tu ya akina mama, sina baya na wewe, mambo ya kisiasa yasitufanye tukose ubinadamu, sitachukau muda wako mwingi maana hata mimi nina kazi nyingi sana,....'akasema na kutangulia kuingia kwenye ofisi yangu ambapo huwa sikaribishi watu ovyo.

Tulipoingia na yeye kukaa kwenye kiti, akaanza mwenyewe kuongea;

‘Unajua kwa vyovyote iwavyo, kuna kitu kimoja kinatuunganisha’akaanza kuongea pale alipohakikisha kuwa nimefunga mlango na hakuna wa kutusikia hayo tunayoyangea, na moyoni nilijua kuna jambo kubwa anataka kuniambia.

‘Kitu gani hicho cha kutuunganisha maana kisiasa sisi ni maadui, labda kibiashara….nikuulize mapema, unahitaji nini kutoka kwangu, maana hali ilivyo, wewe huna urafiki na mimi, ni kwa vile tu unahitaji bidhaa kwangu...ulishasema ni kwa vile nguo kama hizo zangu hujaweza kuzipata mahali pengine ungelikuwa hufiki hapa kwangu tena...una taka kuongea jambo gani....?’nikamuuliza huku nikiwa naogopa, asije akatokea mume wangu na kuniona nikiwa na huyu mtu,  maana mume wangu alishanikanya kuwa nisiwe na ukaribu na hawa watu.

‘Mimi sina uadui na wewe, na wala sina urafiki na wewe, mimi ni mteja wako tu, na kama ningelikuwa na dhana potofu, ningelikata kabisa mguu kuja kwako, lakini kuna mambo mengine tunahitajika tuwe pamoja kama wanawake, tukae tuongee na tuwe na mashirikiani,maana mimi ni mwanamke kama ulivyo wewe , kuna leo na kesho…’akaniambia na alinishangaza kwa kauli yake hiyo, nikatulia kumskiliza.

‘Kuna jambo muhimu nataka nikuambie, hili usilichukulia pupa, kwani ukichukulia puapa hutaweza kufanikiwa, unatakiwa uchunguze kwanza mwenyewe ili ulthibitishe. Ni kuhusu hawa waume zetu…’aliposema hivyo, nikajua ni yale yale.

‘Mimi nimesikia mengi, lakini mimi sijali, kama wana yao, mimi  siwezi kuvunja miiko yangu ya ndoa’nikamwambia na yeye akasema kwa upole.

‘Ni kweli, najua hilo, na najua sana tabia yako, na ulitakiwa unishukuru sana siku ile, nilipoamua kujitolea na kushika ile nafasi yako. Kama isingelikuwa mimi , wewe sasa hivi ungelikuwa upo kwenye haya maisha yangu, au umeshakufa kwa kihoro,….inahitaji moyo na ujasiri kama wakwangu, na sio kwamab siumii, naumia sana…’akasema huku akizuia machozi.

‘Nikuambie ukweli, wakati mwingine najuta kwanini niling’ang’ania kuolewa na yeye, maana mimi ndiye niliyelazimisha, na hata nikimlalamikia mtu, nitaonekana mjinga, ndio maana nakomaa kiume, nitahakikisha tunakula sahani moja hadii kieleweke, ingawaje najua huenda mwishoo wa siku nikaumuiamimi, ..hizi zote ni mbio za sakafuni,…’akasema na kutulia.

‘Haya ni yenu na mume wako, mimi wala sikukulazimisha ufanye hayo uliyoyafanya, na wala sikujua mipango yenu, ‘nikamwambia.

‘Ni sawa…na nakubaliana na wewe, na msimamo huo ni mzuri sana, lakini ni bora ukajua nini kinachoendelea mapema, kuliko kuja kushitukiziwa…ni bora ukamjua adui yako mapemakabla hajakuingilia ndani….’akasema na kuniangalia kwa makini.

‘Kwanini mnapenda kuingilia ndoa za wenzenu,….’nikalalamika.

‘Nani kakuingilia kwenye ndoa yako  wewe!…’ akasema kwa jaziba, na baadaye akatulia, na kusema kwa sauti ndogo ya unyenyekevu,

‘Sikiliza mpendwa, mimi sina mpago wowote wa kuingilia ndoa yako, …niingilie ili iweje, yangu yenyewe inanishinda, ….mimi nimekuja kukusaidia tu, kwa vile mimi yameshanikuta, …! Na kukuambia haya sio lazima ukaamini, kwasababu hata mimi nilikuwa kama wewe mwanzoni, sikuwa naamini hayo,…’akasema na kutabasamu kidogo.

Nilikuwa kama wewe, hivyohivyo, sikutaka kufuatilia kabisa mambo ya mume wangu,  hadi pale nilipohakikisha kwa macho yangu mwenyewe…nikajua labda ni kwa vile nililazimsiha hii ndoa, ndio maana ananifanyia hivi, sikujua kuwa kumbe avumaye baharini ni papa kumbe wengine wapo…’akasema na kutabasamu, tabasamu la mbali.

Sikuamini macho yangu, na mpaka sasabado najiuliza, hivi ni kweli au kuna kitu kimetumika…hapana, kweli tembea uone…’akasema na kuangalia juu.

‘Macho hayana pazia…sikutaka kabisa, kukuambia hilo,lakini limeniuma, na naona nikusanye nguvu kwa wenzangu kama tutaweza tuchukua hatua, maana kumbe sipo peke yangu,….’akacheka kwa ile sauti ya juu kidogo.

‘Kumbe sio mimii tu, niliyetendewa huu unyama,….maana kiukweli mwanzoni nilumia sana, niliteseka sana,  nilijua ni kwangu tu, lakini nimekuja kugundua kuwa hata kwako mambo ni hayo hayo, ila ni kwa vile hujui tu, …’akasema, na mimi nikashituka na kutaka kujua anataka kusema nini.

‘Kama nilivyokuambia, wanaume wote wapo sawa, ni kama shilingi ilivyo, ukiigeuza huku au huku kote ni sawa, kilichobadilika ni picha, lakini shilingi ni ile ile,….hawa wenzetu hawariziki, hata kama wana malikia nyumbani ambaye ana kila sifa ya  uzuri, wao wakipata mwanya wa kukutana na mwingine ambaye huenda hana hata hizo sifa alizo nazo mke wake, lakini kwa vile kamlegezea tu,…basi keshalainika…’akasema huku akikunja uso kuonyesha anakerwa na jambo fulani.

‘Kwani unataka kuniambia nini, mimi nimeshakuambia kuwa sijali mambo yao, kama kuna mambo yao wanayafanya, waacha wayafanye wanavyotaka , ni zambi zao wenyewe, ilimradi mimi sijui kwangu ni sawa tu….hayanihusu…’nikamwambia lakini moyoni nikiwa na dukuduku,maana huyu ni mtu wa pili ananiambia mambo kama hayo, huenda kuna ukweli.

‘Juzi nilikuwa huko Dodoma, huko wanapokutania, nilikwenda kwa ajili ya mambo yangu ya kibiashara, huwa nakwenda mara kwa mara, lakini mume wangu hajui, maana mimi na mume wangu ni jina tu, mke na mume,…na haya yote labda niseme nilijitakiwa mwenyewe. Basi bwana wakiwa huko kwenye mambo ya kisiasa, wakishamaliza yale waliyokusudia, kuna kitu kinaitwa utawala binafsi.….’akasema.

‘Mimi na wenzagu huwa tuna biashara zetu, na kunapokuwa na vikao kama hivyo, tunapata wateja wengi, kuna biashara tuanpeleka huko kwa ajili ya mahoteli, kwahiyo mambo mengi yanayotokea kwenye mahoteli tunayajua,….’akasema na kutulia kidogo.

‘Ndio maananikakuambai kuwa wanaume wote ni sawa na shilingi, unaweza ukasema mume wangu ni mtakatifu, hawezi kufanya mabaya, …unajidanganya, kama anakunywa, ujua ulevi ulivyo,ni kishawishi chamambo mengine, akilewa,anakuwa hajitambui, anaweza akafanay machafu hata na mkwewe,….’akasema na kutulia.

‘Mimi sijakuelewa mpaka sasa…’nikamwambia.

‘Leo sitataka unielewe, lakini ipo siku utanielewa, …na ukiwa tayari mimi nitakusaidia , tunaweza tukaongozana mimi na wewe mguu kwa mguu, hadi huko, wakiwa kwenye vikao vyao ukajionea mwenyewe na hapo utajua kuwa kumbe, niliyokuwanikiambiwa ni kweli, kumbe….mimi nilikuwa nafugwa tu ndani, wenzangu wanaifaidi dunia,….sasa hebu angalai hii picha kwa makini, ….’akasema huku akibonyeza ile simu yake na akanipa niangalia. Nilisita , lakini baadaye nikasema kwani nikiangalai nitazurika na nini…

Mwanzoni sikuelewa vyema, maana niliangalia kwa papara, lakini nilipotulia vyema, nakufautilia kile nilichokiona, ndipo nikagundua ni nini…ilikuwa ni picha ya video, inaonyesha kabisa matendo, kwahiyo sio ile picha ya kupiga mtu kasimama, unaweza kusema ni picha ya kugushi,, ….

Niliwaona watu wamekaa wawili wakinywa, huku wanaongea, sauti zao zilikuwa zikisikika kwa shida maana kulikuwa na sauti za mziki wa taratibu, na sauti zingine za watu wakiongea, kwahiyo sauti zilikuwa zikiingiliana, na unashindwa kujua vyema wao walikuwa wakiongea nini….

Wale watu walikuwa wakinywa, na kula nyama, na ilionekana kuwa wanaongea jambo muhimu sana, na haikupita muda, mara wakaja wanawake wawili wakajiunga nao. Ilivyoonekana pale, ni kuwa wanajuana maana wala wanawake hawakuonyesha kusita, kila mmoja alikwenda kukaa kwa mtu wake, na moja kwa moja wakashikana mkono nyumba ya mgongo wa kila mmojawapo, kama wafanyavyp wapenzi, wakabusiana kwa mahaba

‘Kwa muda ule niliwajua tu, kama wanaume, wakistarehe na wawanwake wao, nilikuwa sijaweza kugundua ni akina nani, kwani hisia zangu hazikuwa zinafikiria lolo te baya,  …

Picha hiyo ilichukuliwa kwa mbali, lakini kila hatua ilikuwa ikikuzwa, hadi sura za wale watu zikawa zikionekana wazi,…hapo mwili ukaanza kunisisimuka, jaziba, hasira, zikatawala ubongi wangu, ..jasho likaanza kunitoka.

‘Haiwezekani, huu ni ujanja wa mitandao, ….’nikasema, huku nimetoa macho ya kushangaa, yule mwanamke hakusema kitu, alikuwa kama hayupo, alikuwa akiangalia pembeni, kama anawaza mambo yake,hakutakahata kunisemesha au kuniambia lolote, katulia kimiya. Nikaendelea kuangalia ile video kwenye hiyo simu, akili kwa muda huo haikuwa yangu tena…..

Mara wale watu, kila mtu na wake, wakainuka na kuanza kucheza mziki, na wakawa wanashikana shikana,…huku wakabadilishana, mara huyu anacheza na huyu, na baadaye mwingine anacheza na mwingine, ilikuwa ni aibu tupu, na uchafu mtupu, kwa watu kama hawa, ambao sikutegemea kabisa wangelifanya mambo kama hayo, nilitamani niibamize ile simu, lakini akili iliniambia nisubiri nione zaidi.

Baadaye nikawaona wakiondoka kila mtu na mwenzake, wakaingia kwenye vyumba tofauti, kila mtu na wake,…na pale ile video ikasimama,….. Pale nilipo mwili ulianza kuniishia nguvu,kwasababu kwa hali waliyoondoka nayo pale, ilionyesha wazi kuwa hawo ni wapenzi wa siku nyingi, na huko kwenye vyumba kuna mabaya yanakwenda kufanyika, kwani walionekana kama vile mke na mume…

‘Hayo mengine ya chumbani siwezi kukuonyesha kwa sasa, yapo ymehifadhiwa kwa manufaa ya ubindamu, maana tuliamua kuchukua kila kitu, ila najua  wewe mwenyewe utajua ni nini kilifanyika zaidi ya hapo,…’akasema yule mwanamke na kuinuka,huku akiangalia saa yake, kuonyesha kuwa kachelewa anahitaji kuondoka haraka.

‘Haya niambie unanidai shilingi ngapi…?’ akaniuliza huyu mwanamke huku akiweka simu yake kwenye mkoba wake,kama vile hakuwahi kuongea na mimi.Mimi sikuwa na nguvu kabisa ya kumjibu, nilichofanay ni kumpa bili ya vitu alivyonunua, na yeye bila kusema zaidi,  akanilipa pesa yangu na taratibu, akaondoka zake.

NB: Haya niambieni akina mama, kumbe ndivyo mnavyowaona waume zenu hivyo, sijui ukweli upoje, lakini ndiyo ilivyotokea kwenye hiki kisa,....tuzidi kuwepo.

WAZO LA LEO: Utofauti wa kiitkiadi, ziiwe za kisiasa, au za kijamii, zisitufanye tuwe maadui, tukasahau ubinadamu wetu, tukumbuke kuwa sote ni watoto wa baba na mama mmoja, Adam na Hawa(Eva).

Ni mimi: emu-three

6 comments :

Anonymous said...

Tatizo ukiamini sana majungu , unaweza ukaingia mkenge.

Yasinta Ngonyani said...

Si wote wapo hivyo ..wazo la leo ni bonge la wazo..

Anonymous said...

Jibu ni kuwa je na wanaume wote mpo hivyo. Ujumbe umefika, kwa wenye kuelewa, twakupenda sana M3

Pam said...

napata mafunzo hapa angalia waume wenzio watakulaumu kutoa siri za 'vikao'

Anonymous said...

Wewe unatusaliti, mambo mengine hayazungumzwi, ....aaah, umeharibu m3

Ammy K said...

wazo la leo zuri sana,wanasiasa kama watalipata hili itakuwa poa sana.