Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, July 11, 2012

Hujafa hujaumbika-66 Hitimisho 24



Hakimu hakuingilia kati yale mabishano yaliyokuwa yakiendelea kati ya wakili mwanadada na nesi, alichofanya ni kuyafuatilia kwa makini, na kuangalia munkari wa huyu nesi una maana gani, alianza kuingiwa na wasiwasi na majibu anayotoa huyu nesi, akawa akijiuliza kwanini anakuwa kama mtu anajihami, au kuficha jambo, au kuna mtu anamlinda, ili ukweli usijulikane!

‘Inatosha… 'Hakimu akakatisha yale mabishano, akatulia kuhakikisha kuwa wote wamenyamaza halafu akasema;

'Nesi jibu swali uliloulizwa maana sioni kwanini unabisha wakati unajiamini kuwa wewe hujaua. Kwanini ushindwe kutoa jibu moja, ndio au hapana,....Pia wewe umedai kuwa ulipitia uaskari au sio?'akauliza Hakimu

'Ndio Muheshimiwa, niliwahi kuwa askari, ....'akasema kwa sauti ya kinyonge,kuonyesha kuwa anaonewa.

'Kwahiyo unajua siri nyingi za kumshinda adui yako, moja ya siri ya kumshinda adui yako ni kumpandisha hasira, na kama ujuavyo hasira zikimpanda mtu mara nyingi mtu huyo anajikuta ukifanya mambo bila mpangilio, na hapo mwenzake ambaye alishajiandaa kwa hilo anakuja kumshinda kirahisi…asu sio?’akaulizwa.

'Ni kweli Muheshimiwa, ila wakili ..muheshimiwa wakili ananisakama sana...'akajitetea.

'Kwani huna swali hujalielewa...?' akaulizwa.

‘Muheshimiwa hakimu,sio kwamba sina jibu la kumjibu muheshimiwa wakili, jibu ninalo nalipo wazi, Ila nilikuwa najiuliza kwanini mimi anishinikize hivyo, maana sote tulikuwepo hapa tangu mwanzo na maelezo ya kila mmojawapo yalikuwa kama yangu,...wote wamebaini wazi kuwa kila mmoja alikuwa na lengo la kutaka kumuua huyo Kimwana kutokana natabia yake, lakini mwisho wa siku haikutokea hivyo….’akatulia na kumwangalia hakimu.

‘Kama ni kuitwa muuaji, basi mke wa wakili na rafiki yake wangelikuwa wauwaji namba moja, maana wao walifikia hadi kuishika ile bunduki na kuwa tayari kufyatua risasi kama walivyodai, lakini kwa namna moja au nyingine, wakijifanya kuwa hawakufyatua hiyo risasi, eti wakakimbia, na baadaye mtu mwingine akaja kufanya hayo mauaji…'akacheka kwa kebehi, halafu akasema;

Hivi kweli inaingia akilini…hapo, kwangu mimi ningewashinikiza kwa maswali hawo watu hadi waseme ukweli…lakini cha ajabu nashinikizwa mimi...huoni kama naonewa.’akamwangalia hakimu halafu akamgeukia wakili mwanadada.

‘Halafu wewe unakuja kunipakazia kuwa, eti, `kwahiyo ukaamua kumuua, …iwe rahisi hivyo,…nikubali tu kwa kitu ambacho sikukifanya, mimi nilitoka saa ngapi huko hospitalini aliponiacha wakili mkuu, na kwenda kuyafanya hayo mauaji….eeh hebu niambie muhushimiwa ---sana, wakili mwanadada?’ Akauliza.

‘Hujajibu swali langu, ..sijakuambia unipe maelezo,nijibu kama nilivyokuuliza kwanza, na kama ninahitaji maelezo nitakuuliza hivyo, wewe unaelewa hivyo, usijifanye kuwa hujui, labda kama kuna kitu unajihami au unataka kuficha,....nitakuja kukuuliza hayo, maana nisingeliweza kukimbilia huko, kabla sijakuuliza jinsi gani ulivyoweza kutoka hapo hospitalini, na kwenda kumuua huyo Kimwana hayo ni ya baadaye, sisi hapa tunataka tuende hatua kwa hatua…’akasema wakili mwanadada.

‘Kwanza nitakujibu kwa kifupi kuwa mimi sijamuua Kimwana,kama unavyodai, na kama una dai kuwa mimi nimemua Kimwana, naomba ushahidi, na kama huna ushahidi mimi nitakushitaki kwa kunipakazia uuaji ambao sijawahi kuufanya….’akasema kwa hasira.

`Nauliza tena swali langu, je kwa mambo hayo ambayo unadai kuwa alikuwa nayo Kimwana, ya maasi,kuharibu ndoa za watu,kuchonganisha watu, kuibia watu kiujanja,….wewe uliona kuwa hakuna njia nyingine ya kumziba mdomo Kimwana,...sasa tuambie ni njia gani nyingine wewe uliyoona ni njema kwake,ambayo ingemfaa kumziba mdomo Kimwana?’akaulizwa.

‘Wewe kwa jinsi nilivyoelezea kuhusu huyu binti Kimwana,.... samahani, nina maana  marehemu Kimwana, jinsi alivyokuwa, tabia yake, kauli zake, ....na, na....wewe kama wewe ungeona ni njia gani ingemfaa huyu mtu ya kumziba Kimwana mdomo, maana njia nyingine zilishatumika,.....tulishazijaribu, sisi ni wataaalmu wa watu,tunawajua sana,.... tulimkanya, tukamshauri, tukatumia hata vitisho, natukafikia hata kumwambia kuwa tutamfukuza kwenye kundi,unajua nini alichosema….?’ Akamwangalia wakili mwanadada, wakili mwanadada akawa kamtizama tu bila kusema neno.

‘Sasa unaona hata wewe mwenyewe unashindwa la kusema, maana kwa Kimwana hakukuwa na njia nyingine zaidi, kila mtu alishamchukia, na zaidi ya hayo, tulipomtishia kuwa tutamfukuza kazi, yeye alisema kwa nyodo, bila kujali kuwa anaowaambia hivyo ni viongozi wake, akasema kuwa akiondoka hapo kwenye kundi atahakikisha kuwa analisambaratisha kundi letu…na atahakikisha kuwa kila mmoja anakwenda kunyea kopo…’akasema huku akiwaangalia watu walioshiriki hapo, halafu akatulia.

‘Wewe ni askari, au sio?’ akaulizwa na wakili mwanadada.

‘Mimi sio askari, mimi ni nesi, ila niliwahi kuwa askari…unasemaje ?’ akasema huku akimwangalia wakili mwanadada kwa uso ule uliojaa dharau.

‘Ulipokuwa askari, ukiambiwa nyuma geuka, unafanyaje?’ akaulizwa.

‘Ninageuka, ningelifanyaje..na hiyo ni amri ya kijeshi, amri ya kijeshi ni amri, haipingwi, hata kama sitaki ningeligeuka tu,…., mpendwa, mbona unanifanya mimi kama mtoto mdogo, kwanza mimi nakuzidi wewe kwa umri, inabidi uniheshimu…’akasema huku akitabasamu.

‘Mimi hapa nimekuuliza swali, …ni kama vile unavyoambiwa huko jeshini,  nyuma geuka, lakini badala ya kugeuka unaanza kuuliza je nigeukie upande gani,... hivi hapo tutafika kweli…ujua hapa ni mahakamani na mahakamani hakuna tofauti na amri za jeshini, ukiambia jambo unatakiwa ulifanye, ukiulizwa swali unatakiwa ujibu kama ulivyoulizwa’akasema wakili mwanadada.

'Wakati mwingine huwezi ukajibu swali kwa mkato , maana maswali hayo ni ya mtego, na mimi sio mtoto mdogo wa kutishiwa nyau, najua kabisa ni nini unachotaka kunitegea,.....hapa umedunda, nitajibu kwa makini kabisa....'akasema huku akitabasamu.

Wakili mwanadada, akamwangalia kwa makini huyu Nesi, na yeye akatabasamu,  hakujali tabia ya huyo mwanadada,….yeye anawajulia watu kama hawo,kwahiyo kwake ilikuwa ni jambo la kawaida, alijua wapi pa kumtuliza mtu kama huyo. Akamwangalia huku kamkazia macho, na yule nesi akamwangali huyo wakili mwanadada huku na yeye kamkazia macho, hafafu akasema  akatabasamu na taratibu akaiweka mikono kifuani, na kuisogeza mbele kama mtu anayetubu dhambi, akasema;

‘Haya hebu uliza tena hilo swali lako muheshimiwa mpendwa wakili mwanadada….’akatulia huku kainama chini kichwa kama mtoto mwenye adabu huku kaikunja mikono yake mbele kama  anatubu makosa yake,na kutulia kimiya.

‘Ni njia gani uliyoona wewe inayomfaa kumziba Kimwana mdomo?’ akaulizwa.

‘Kwa jinsi alivyo kuwa …mimi na hata wenzangu walishauri kuwa ni bora kama ikiwezekana auliwe tu…yeye kwanza ni msaliti, ni kama msaliti katika mstari wa mbele kwenye vita,...najua hutaki maelezo mengi, jibu kuzibwa kwake mdomo kwa njia inayomfaa yeye ni kuuliwa tu..’akasema.

‘Kwahiyo wewe ukaamua kwenda kumuua?’ akaulzwa.

‘Kutoa wazo ni kitu kingine, na vitendo ni kitu kingine, hivi ni vitu viwili tofauti, wazo langu lilikuwa hivyo,kama walivyokuwa na mawazo kama haya wengine waliopita, tumewasikia kauli zao,  kuwa njia iliyokuwa ikimfaa Kimwana, ili domo lake lisilo la subira lizibwe, ....'akaonyesha kwa mkono, akipitisha kidole shingoni, kama ishara ya kuonyesha kuwa  nii kuuwawa.

 Lakini sio kwamba kwa vile nimekubalina na hilo wazo,....kuwa njia iliyomfaa Kimwana ni kuuliwa ndio nichukuliwe kirahisi hivyo kuwa mimi ndiye niliyemuua, hapana, hayo ni mawazo yangu kama yalivyokuwa ya wengine….’akatulia na kuinama tena kama vile anatubu dhambi zake,halafu  akaongezea kwa kusema;

‘Kama ingelikuwa hivyo, hata, wakili mkuu, Sokoti, na hawo akina dada wawili wote wangelikuwa wauwaji,….au na wao ni wauaji, tukubaliane hilo kwanza, kama na wao ni wauaji kwa kutaka kumuua Kimwana,..licha ya kuwa wamedai hawakufanya hivyo,…basi hata mimi mtaniita muuaji,…kitu ambacho sio kweli…..’Hakimu akaangilia kati na kuuliza lile swali.

‘Je ulipoona njia bora ya kumziba Kimwana ni kumuua, ukaamua kwenda kumuua,…natumai umelisikia hilo swali vyema unachotakiwa hapo ni kujibu, ndio au hapana…..’akasema muheshimiwa hakimu.

‘Aaaah,ndivyo mnavyotaka nijibu kimkato-,mkato, ....sawa muheshimiwa hakimu,...mimi nilikuwa natoa maelezo ili kuwasaidia kumbe nyie hamtaki maelezo mengi, lakini wenzangu walikuwa wakitoa maelezo mengi tu, na hawaingiliwi, mpaka tulikuwa tunaboreka,...ulizeni wenzangu kama nasema uwongo, sasa mimi inakuwa tofauti,  samahani muheshimiwa hakimu,sikujua hilo, kuwa ninachotakiwa mimi , nikujibu kimkatato, shwaa,....sasa nitaanza kujibu kimkato-mkato…waaah’akasema na kuinamisha kichwa chini, huku akijifanya mnyenyekevu.

Hakimu akamwangalia kwa makini, halafu akasema  kwa sauti ya ukali kidgo,
'Haya najua umeshaelewa, sasa ujibu maswali kama utakavyoulizwa, sitaki mchezo , hapa ni mahakamani, wewe unajue sheria vyema kabisa,....' Hakimu akamgeukiwa wakili mwanadada kumuashiria aendelee na maswali yake;

‘Haya jibu swali….,ni vyema ukajua kuwa kila swali lina jibu lake kama umeambiwa utoe maelezo unatoa maelezo kama umeulizwa ujibu kimkato, unajibu kimkato, ndivyo sheria za mahakamani zilivyo…najua,unazijua lakini naona kama unatafuta njia ya kukwepa swali..’akasema wakili mwanadada.

‘Hapana…’akasema nesi.

‘Hapana nini?’ akaulizwa na wakili mwanadada.

‘Hapana kutokana na swali lako la kwanza na la pili….’akasema na kutulia kimiya, huku kainama na kuweka mikono mbele kama anatubu, kiasi kwamba watu mle ndani wakajikuta wakicheka, maana alikuwa kama anafanya mzaha.

************

`Hebu tuambie siku ile ambayo inaelezwa kuwa ndipo Kimwana aliuliwa wewe ulikuwa wapi?’ akaulizwa swali.

‘Kitu ambacho sikipendi jamani ni kuulizwa maswali yenye majibu, watu mnajua majibu mnaniuliza majibu, maswali yamewaishia nini, kwani hamukumsikiliza wakili mkuu alipokuwa akitoa maelezo yake, yeye huyu wakili mkuu wenu, aliniacha pale hospitali, wodini ambapo alikuwa kalazwa….’akatulia halafu akawa kama kashituka na kusema;

‘Siku hiyo,....mmh, nilikuwa hospitalini….’akasema na kuinama chini.

‘Ulikuwa hospitalini ukifanya nini?’ akaulizwa swali.

‘Kwani hospitalini watu wanafanya nini jamani, hivi, …’akajishitukia , na kusema;

‘Labda sikulielewa swali vyema, una maana gani kuhusu hilo swali,`eti kazi gani ninazozifanya hapo hospitalini’ au …kama nesi..au,…naomba ufafanuzi hapo, samahani sijaelewa hilo swali vyema’ akasema na kutulia na kabla hajajibiwa akaongezea neno `muheshimiwa wakili mwanadada’ huku kainama.

Wakili mwanadada akawa katulia akimwangalia, na nesi alipoona hapati jibu, akainua kichwa na kumwangalia hakimu, na halafu akageuka kumwangalia wakili mwanadada, na kukuta bado kamkazia macho, alipoona hivyo akasema;

‘Tatizio lako, unanikazia macho sana, ukifikiria kuwa mimi nitaogopa, hiki ni chuma cha pua, mimi ni mwanajeshi mstaafu kabla ya muda wake,..na pia ni nesi anayejua kupambana na wagonjwa. Kule hospitalini wanakuja watu wa  ajabu, wanatoa macho ya kutisha …kuna wengine wakubwa, jitu kubwa, lina mwili wa kutisha, lakini linaogopa sindano, mwisho wa siku unalishika na linapigwa sindano, sembuse wewe….’akasema na kucheka kwa dharau, na watu mle ndani wakacheka pia, hata haimu akatabasamu,lakini wakili mwanadada alikuwa vilevile, kamkazia macho.
.
Wakili mwanadada akamgeukia muheshimiwa hakimu na kusema; `Muheshimiwa hakimu, hiyo ndiyo hali halisi ya ndugu yetu huyu, na ndio  maana nikatanguliza angalizo mapema,maana namjua sana huyu Nesi, …nilishasema mapema kuwa kuna watu wengine watajaribu kuficha ukweli,…’aaksema wakili mwanadada na kugeuka kumwangalia huyo nesi, na hakimu akawaangalia wote na kutabasamu.

Wakili mwanadada akawageukia watu  na kusema;

‘Jamani tulilifanya hili hapa kwa nia njema ili tuweze kusaidiana kuhusu hii kesi, tunajua kuwa kuna watu wana tabia zinazokera, katika jamii,  kama alivyodai mwenzetu  huyu nesi kuwa Kimwana alikuwa na tabia ambazo zilimkera,…kwamtizamo wangu, Kimwana na huyu Nesi, hawatofautiani sana, walikuwa kama mafahali wawili waliokutana. Lakini hata hivyo niliona kuwa njia rahisi ya kusaidiana katika tatizo hili ni kukutana na kuliongelea kama hivi, ili kila mmoja aseme ukweli wake, na tuone jinsi gani ya kulitatua, kwa njia ya heri,lakini yote yakitegemea ukwelii wenu!...’akatulia.

‘Kama alivyosema nesi, kuna watu wengine wakorofi, huwezi kuwashauri kwa lolote lile, hata muongee kwa vipi, na kwamtizamo wake yeye, watu kama hawo  ni wanastahili kuzibwa midomo,…hebu angalieni nyie wenyewe yeye alivyo na majibu yake yalivyo, kama ungelikuwa unachukulia hayo mawazo yake, na kauli zake yeye, …na y eye tungelimfanya nini…?’akawa kama anauliza swali na watu bila kusubiri wakasema;

‘Tumzibe mdomo….’

‘Eti nini,subutu yake...,ajaribu mtu aone, Kimwana mwenyewe alishasalimu amri….hata hivyo huwezi ukanilinganisha mimi na Kimwana, hivi nyie ina maana hamkuwahi kuishi  na Kimwana,….mmh, shauri lenu, mshukuru sana kuwa katangulia mbele ya haki, na mungu amsamehe makosa yake…’akasema nakuinama chini.

‘Ninachotaka kusema hapa ni kuwa,….yeye huyu nesi, aliona  ana njia yake njema yakumziba mdomo Kimwana, na tunataka kuijua sote, je njia hiyo ni ipi, ….ndicho tulichokuwa tukikitaka kukijua….’akatulia na kumgeukia huyo nesi ambaye alikuwa akimwangalia kwa macho yake yale yale ya dharau.

`Tuanataka kujua hilo,…tafadhali tusipotezeane muda hapa…jibu swali langu.’akasema huku akimkazaia macho huyo nesi, na huyo nesi akatabasamu na kutingisha kichwa kwa dharau.

Hakimu akamwangalia yule nesi na akasema ;

‘Narudia tena kwa mara nyingine, jibu swali utakavyoulizwa, kama utahitajika kutoa maelezo utaambiwa, sawa?’

‘Ndio muheshimiwa,samahani kwa kutoa maelezo…sikujua kuwa maelezo kwangu mimi hayatakiwi….’akasema.

‘Haya jibu swali..’

‘Naomba aulize tena hilo swali….’akasema

‘Ulikuwa hopitalini ukifanya nini?’ akaulizwa.

‘Nilikuwa nikifanya kazi zangu nilizoajiriwa nazo kama nesi’akasema kwa sauti ya nzito.

‘Wewe kama nesi, uliajiriwa kumruhusu mgonjwa atoke hapo hospitalini kabla hajaruhusiwa na dakitari?’ akaulizwa swali kwa kuigizwa suti yae aliyotoa , huyo nesi kashituka kidogo na akabetua mdomo na kusema;.

‘Hiyo ilikuwa dharura, na hata hivyo huyo jamaa nilimzuia lakini alikuwa mbishi…akaondoka mwenyewe bila rizaa yangu…mlimsikia mwenyewe akitoa maelezo yake hapa…sijajitungia mwenyewe’akasema.

‘Kwahiyo ikitokea dharura kama hiyo unamuachia mgonjwa anaondoka tu, ..?’ akaulizwa.

‘Hapana na hata hivyo, huwa haitokei kitu kama hicho mara kwa mara ,labda kama mgonjwa huyo kachanganyikiwa….’akasema kwa utulivu.

‘Kwahiyo unafanyaje kwa mgonjwa kama huyo?’ akaulizwa

‘Ina maana unauliza kwa mgonjwa aliyechanganyikiwa,…au?’ akauliza na kabla hajaambiwa chochote, akasema;

‘Kwa mgonjwa ambaye ….mfano aliyechanganyikiwa, au yule ambaye katumia nguvu kuondoka tu,…huwa ninatoa taarifa kwa mahala husika, au ninaweza nikaomba kibali cha kumdunga sindano ya kumvunja nguvu kama ni mgonjwa mwenye kesi inayojulikana…’akaongea kwa utulivu kama sio yule aliyekuwa akifanya mazaha awali.

‘Haya kwa huyu mgonjwa wako, wakili mkuu, ulichukua hatua gani, au kesi yake nayo ilikuwa inajulikana?’ akaulizwa.

‘Hali hiyo ipo wazi hapa haina haja ya mimi kufafanua,…hii ni kesi inayojulikana hapa na sisi sote tupo kwenye mkumbo, ..., siwezi kuficha ukweli huo, …. huyo aliondoka na …..kwa vile kuna kitu ambacho alitaka kukifanya chenye maslahi kwangu, kwahiyo niliamua kumlinda…’akasema.

‘Ni maslahi gani kwako, na utuambie kwanini uliamua kumlinda…ukijua kabisa kuwa huko ni kuvunja sheria…?’ akaulizwa.

‘Maslahi kwangu,.....'akasema na kutulia, halafu akaongezea kwa kusema `Kwasababu nilijua kaondoka kwa hasira, na hasira hizo zingenisaidia mimi, kwani kama kweli atafanya kama alivyosema,...kuwa anakwenda kumkomoa Kimwana, angelikuwa kanipunguzia mzigo wa kumziba Kimwana mdomo, ndiyo , hayo ni maslahi kwangu….hamuoni hilo.

`Na niliamua kumlinda kwasababu ni mtu wangu, mpemzi wangu…mmh, wa siri, samahani kwa hilo…,licha ya kuwa ni mume wa mtu…lakini nilishaelezea awali kwanini ikawa hivyo’akasema na kumwangalia mke wa wakili mkuu kwa jicho la kujificha.

‘Naomba ujibu hili swali kitaalamu, ….Je wakili mkuu alikuwa mgonjwa kweli, maana mpaka anaweza kuinuka kitandani na kuondoka, na hali tuliyokuwa tukiijua sisi ni kuwa hata kutembea ilikuwa shida, mbona haituingii akilini, hebu tuambie ukweli, je wakili mkuu alikuwa mgonjwa kiasi hicho tulichokuwa tukijua awali, au ilikuwa ni mbinu zenu wawili….?’akaulizwa.

‘Kwanini msimuulize yeye mwenyewe, alikuwepo hapa akitoa maelezo yake, nyie mngeliweza kumuuliza hilo swali, nawashangaa mnakuja kuniuliza mimi, hilo swali siwezi kulijibu mimi ,atalijibu yeye mwenyewe…maana yupo hapa’akasema kwa sauti ya kawaida lakini kama ya ukali.

‘Tunakuuliza wewe kama mtaalamu, nesi uliyekuwa ukimhudumia na kauli yako itatusaidia sisi kutoa maamuzi yaliyosahihi kama mtaalamu, maana wewe unatambulika kisheria kwa swali kama hilo, ni muhimu sana …’akasema hakimu.

‘Ndio alikuwa mgonjwa kweli, na hata alipoinuka pale kitandani alikuwa akijikakamua kuinuka nilimuona kabisa akipepesuka, ila nilimpa dawa ya kumuongeza nguvu….’akasema.

‘Je hizo dawa ulizompa zilikuwa zimeandikwa na dakitari?’ akaulizwa.

‘Mhh, hapana,…kiukweli hazikuwa zimeandikwa na dakitari, nilikuwa nazo mwenyewe…..’akasemahuku akionyesha wasiwasi, uleujasiri wa mwanzo ukawa kama unayeyuka.

‘Ulikuwa nazo mwenyewe au ulizichukua bohari ya  madawa?’ akaulizwa.

‘Nilikuwa nazo mwenyewe, nilikuwa nimezinunua kabla….’akasema kwa sauti kama ya ukali.

‘Kwahiyo ni kitu ambacho kilijulikana kabla kuwa hizo dawa zitatumika,?’ akaulizwa.

‘Ndio,…unaweza kusema hivyo....’akasema na kukatiza alilotaka kusema baadaye.

‘Hebu turejee nyuma kidogo, kuna kipindi mgonjwa mmoja alilazwa hapa, na mtu akataka kuja kumuua, na wewe ulikuwa kwenye zamu siku hiyo, je huyo mtu alikuwa nani, maana tunaamini kuwa hilo lilifanyika kutokana na kundi lenu, na wewe ni kiongozi wa upelelezi, na pia ulikuwa zamu siku hiyo kamanesi wa zamu wa kumhudumia huyo mgonjwa, je tuambie ukweli huyo mtu alikuwa ni nani ….?’ Akaulizwa.

‘Mimi hilo tukio silikumbuki vyema, na sizani kuwa lilikuwa ni jambo lililoandaliwa na kundi letu, sikumbuki vyema, samhani kwa hilo, siwezi kuljibu hilo swali…’akasema.

‘Huwezi kujibu, au hukumbuki?’akaulizwa na hakimu.
‘Kwakweli sikumbuki,….’akasema
‘Na je ukikumbushwa ilivyotokea na kuonyeshwa vielelezo kuwa wewe ulikuwa nesi siku hiyo, ….’utaweza kulijibu hilo swali?’ akaulizwa.
‘Nitalijibu, kwanini nisilijibu,lakini kwa ujumla kwa sasa sikumbuki kitu kuhusu hilo tukio,na sijui kama linahusiana na Kimwana…maana hapa vyovvyote tunahitaji kutoa maelezo yatakayosaidia kifo cha Kimwana
‘Je unajuaje kuwa hilo tukio halihusiani na Kimwana?’a akulizwa.
‘Kwasababu ni la muda, mpaka mimi mwenyewe silikumbuki, ina maana ni kitu ambacho kilitokea kitambo, labda hata Kimwana hajauliwa..hata hivyo sikumbuki vyema, kama mnataka nilijibu vyema hilo swali nikimbusheni ilikuwaje, na hivyo vielelezo mnavyodai kuwa vipo, nionyesheni, nikikimbuka nitawajibu…..’akasema.

***********
‘Unasema siku hiyo alipouliwa Kimwana wewe ulikuwa hospitalini ukifanya kazi zako za unesi, lakini hapo hapo ulikuwa ukimlinda mgonjwa aliyetoroka, ili isjulikane kuwa hayupo, hebu tuambie uliwezaje kuyayafanya hayo?’ akaulizwa.

‘Mimi nilichofanya nikutulia mle ndani kama vile namhudumia huyo mgonjwa, na kama ikibidi kutoka naufunga ule mlango, na kwahiyo mtu akija hapo anajua kuwa kuna nesi ndani anamhudumia huyo mgonjwa…ilikuwa ni rahisi tu…”akasema.

‘Ina maana hukutoka humo ndani muda wote huo, na kama ulitoka ulitokaje na mara ngapi?’ akaulizwa.

‘Nilitoka mara chache, maana nilikuwa nikihitajika kwenye kazi nyingine, lakini kama nilivyosema. Kila nikitoka nilikuwa nikifunga mlango,…’akasema.

‘Ulifunga kwa ufunguo?’ akaulizwa.

‘Ndi…o….’akajibu lakini kama vile anasita kulijibu hilo swali.

‘Mbona unasita kulijibu hilo swali,huna uhakika najibu lako?’ akaulizwa.

‘Najaribu kukumbuka vyema,…lakini nakumbuka kuwa nilikuwa nimefunga huo mlango kwa ufunguo…’akasema.

‘Ina maana huyo mgonjwa ulikuwa ukimhudumia wewe peke yako, mpaka ufunge huo mlango kwa ufunguo, kama mwenzako angelikuja kwa huduma nyingine ilikuwaje…na kama angezidiwa ni ?’akaulizwa.

‘Huyo mgonjwa alikuwa katika mikono yangu,nilikabidhiwa mimi na dakaitari kuwa yupo kwenye mikono yangu na lolote litakalohitajika juu yake, mimi ndiye niliyestahili kwenda kumuona dakitari…na kwasaabbu nilijua hayupo, swala la kama angelizidiwa lilikuwa halipo…ningelijua jinsi gani ya kujitetea kama wangeligundua kuwa mgonjwa hayupo’akasema.

‘Ina maana hakuna mtu mwingine aliyekuwa akishirikiana na wewe katika kumhudumia huyo mgonjwa,..na amabye labda alikuja kutaka kuingia humo kwenye chumba?’ akaulizwa.

‘Walikuwepo wengine, lakini mimi ndiye niliyekuwa nikimhudumia kwa wakati huo, na kama alikuwepo mtu mwingine ambaye alikuwa na shida na huyu mgonjwa, angelikuja kwangu kuniuliza mimi kwanza….’akasema.

‘Kama alikuja kwako kukulizia , ingalikuwaje na wakati umesema mlango uliufunga, tena kwa ufunguo…wakati umetoka…?’akaulizwa.

‘Kwasaabbu hakuna aliyekuja kuulizia, hilo swali halina maana yoyote, ..kwasababu kama anglikuwepo mtu alikuja akakuta mlango umefungwa angelinitafuta hata kwa simu ya mkononi,….’akasema.

‘Akutafute kwa simu ya mkononi, kwani kuna muda ulitoka, na kwenda mbali n ahapo hospitalini?’ akaulizwa.

‘Simu ya mkononi, siolazima utoke mbali na hapo, ila inarahisisha kumtafuta mtu kwa haraka, natumai hili lipo wazi muheshimiwa…’akasema huku akimwangalia hakimu, safari hii alijibu kwa unyonge.

‘Kwahiyo hukuwahi kutoka mbali na hapo hospitali kwa muda wote…wakati mgonjwa huyu  hayupo?’akaulizwa.

‘Niende wapi wakati nilikuwa namlinda mgonjwa wangu…sikuwahi kutoka mbali na hapo hospitalini..’akasema.

‘Una uhakika na hilo jibu lako…?’ akauliza wakili mwanadada huku akimkazia macho.

‘Kwanini unanisisitizia kuwa na uhakika  na hio jibu langu, kwanza hapa hatupo mahaamani, kila mmoja anatoa maelezo yake akiwa huru, na kwa vile nimegundua kuwa unanishurutisha naona sasa akiliimechoka….’akasema na kukaa kimiya

‘Je una uhakika nahilo jibu lako kuwa hukuwahi kutoka nje ya hiyo hospitalini kwa muda wote huyo mgonjwa alipokuwa hayupo?’ akaulizwa na hakimu

Hapo akanyamaza kimiya

‘Vipi nesi, mbona unaanza kunywea wewe ulikuwa ukijibu maswali kwa mbwembwe, mbona unaulizwa swali dogo kama hilo unashindwa kulijibu kama kawaida yako….?’akauliza na hakimu.

‘Maswali mengine yanachosha,….hapa mimi sasa nimeshachoka, na naona kama mnanisakama vile inavyoonekana mnanifanya mimi  kama vile nina kosa, naomba muda nitulize kichwa changu kwanza…’akasema

‘Una taka muda gani, ili utulize kichwa chako kwanza?’ akaulizwa.

‘Dakika tano tu zinatosha….’akasema huku akishika kichwa.

‘Haya tunakupa dakika tano zakutuliza kichwa chako,…’akasema hikimu baada ya kumwangalia yule nesi kwa macho ya huruma, halafu akawageukiwa watu wengine na kusema;

‘Wkati tunampa muda huyu nesi,nawaomba wakili mwanadada na mkuu, waje hapa tutete kidogo. ..’akasema hakimu. Na nesi aliposikia hivyo, akaonekana kushituka kidogo, akageuka kumwangalia wakili mwanadada, ambaye alikuwa akimwangalia kwa makini, halafu akageuza kichwa haraka kumwangalia hakimu,.ambaye naye alionekana kuandika kitu kwenye kitabu chake, ….nesi akasema kwa sauti.

‘Muheshimiwa hakimu, naomba tuahirishe haya mazumgumzo kwa leo kwanza sijisiki vizuri, na pili sitaweza kujibu maswali mengine yoyote kuanzia sasa, mpaka nionane na wakili wangu,….’akasema.

‘Kwani una wasiwasi gani,hatupo kwenye mashitaka hapa, haya ni mazungumzo ya awali tu, kama utahitaji wakili ni baada ya haya mazungumzo, mlshakubaliana hilo kuwa hapa tunazungumza tu, ili tujue nini kilitokea, na mengine yatafuata baadaye,sioni kuna tatzio hapa mpaka uhitaji wakili, eti nimabie kuna tatizo gani…?.’akasema hakimu na kumuuliza huyo nesi.

‘Kwakweli muheshimiwa hakimu,….mimi sitajibu lolote mpaka nionane na wakili wangu, maana hapa naona sitendewe haki…kama wenzangu,’akasema na hakimu akatabasamu na kuwaita wakili mwanadada na mkuu wasogee pale alipo, akainama kuongea nao,…., na wakati huohuo yule nesi akainuka pale kwenye kiti akitaka kuondoka.

‘Unakwenda wapi wewe…!’akauliza askari mlinzi.

‘Hujasikia nilivyomwambia muheshimiwa hakimu, sitaongea lolote mpaka nionane na wakili wangu,….’akasema akiwa anataka kuondoka huku yule askari akijaribu kusimama mbele yake kumzuia, ,na mkuu ambaye alikuwa akiongea na hakimu akageuka na kwa sauti akasema;

‘We askari mkamate huyo mtu….’

‘Kwa kosa gani…’akauliza Nesi kwa dharau huku akiendela kuondoka kuelekea mlango wa kutokea kwa ujasiri, ….

NB,Je nini kitaendelea hapo, kuna kipande nimeshindwa kukimalizia kwenye sehemu hii kwasababu ya muda


WAZO LA LEO: Siku hizi mdomo ni kila kitu, mtu anaweza akafanya kosa,lakini kwa vile ana mdomo wakuongea atautumia huo mdomo na kujitetea kwa nguvu zote, hata kama kweli yeye kalifanya hilo kosa. Kosa kwake ni pale atakaposhindwa kuongea.

Tuchungueni kauli zetu,  tuwe wakweli, hasa katika ndoa nzetu, tusiwe waongo, kwani hata kama utamdanganya mwenzio, bado kuna yule mjuzi anayejua ya siri na yadhahiri,…ujue mkiwa wawili yeye yupo nanyi, lakini hamumuoni, hata kama upo pekeyako, bado yeye yupo nawe, hata ujifiche shimoni, yeye yupo nawe,…. je yeye utamdanganyaje! Tukumbuke kuwa njia ya muongo wakati wote ni fupi

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Nimependa sana ujumbe wa leo. Ubarikiwe