Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, May 14, 2012

Hujafa hujaumbika-35  Wakili mwanadada alitizama saa yake na baadaye akamtupia jicho mkuu wa kituo ambaye alikuwa kainama akisoma majarida mbali mbali ya kesi bila kumjali.  Ilikuwa kama vile hakuna mtu mbele yake, na kipindi cha muda kikapita bado wakiwa vile kimiya, mkuu akiwa na mafaili yake, na mwanadada akiwa kakaa pale, huku akionyesha uso wa kukereka.

Baadaye yule mwanadada akainuka kwenye kiti, akipiga miayo, halafu akajinyosha, na wakati anafanya hivyo yule mkuu wa polisi akainua uso na kumwangalia kwa jicho la kujiiba, akatisa kichwa, huku akiwaza yake kichwani, hakusema neno, ….

‘Hivi utaniweka hapa mpaka saa ngapi maana kila kitu nimeshakuambia, unataka nini zaidi?’ akauliza yule wakili.

‘Nataka uniambie kila kitu,….tatizo lako unatufanya sisi hatujui, sisi kila kitu tunajua,…wakati mwingine tunawezakukuuliza kitu kupata ukweli wako, sisi tunajua sheria, na tunaifuta baada ya kufanya uchunguzi na tunajua hata hicho ulichoficha kicwani mwako,…’akatulia na kumwangalia.

‘Unajua waakti mwingine nawaza sana, hebu nikuulize wewe binti mzuri kwanini unataka kujiingiza kwenye matatizo , hili nilishakuambi ni kazi ya polisi,lakini wewe unajifanya mjanja, sasa utakaa hapa mpaka tukamlishe huo uchunguzi wetu. Nisingelipenda wewe ukalale gerezani eti unashikiliwa kwa mauaji,….sipendi kabisa…’akatikisa kichwa huku akimkazia huyo mwanadada macho.

‘Mkuu, siwezi kufanya jamboo kama hakuna sababu, na ….ngoja kwanza, nikuulize ni muda gani wakili kama mimi nastahili kushikiliwa na polisi….?’ Akauliza.

‘Hata siku nzima, ilimradi zipo sababu za msingi za kukushikilia, na usizani kuwa hatuna sababu,  tunazo taarifa kuwa siku ile ya tukio ulikuwepo, na ukiunganisha na mashitaka yaliyokuja kuwa wewe huenda umehusika na kifo cha huyo mwanadada, tunasababu ya kukushikilia ili utoe ushirikiano, huku tukiendelea na uchunguzi….’akasema huyo mkuu

‘Kama hiyo ndiyo sababu muhimu ya kunishikilia,mbona mumeshanishikilia na sikukataa kuja hapa licha ya kuitwa bila utaratibu, hakuna maelezo kwanini naitwa huku kituoni, nimechukuliwa kienyeji tu,.... nimeitikia wito wenu, nimekuja hapa, mumeniuliza maswali nimewajibu, nimekaa muda muafaka, ….kitu gani zaidi mnahitaji kuhusu mimi…..?’ akauliza.

‘Tunaendelea kukushikilia kwasababu tuna imani kuwa hujatuambia kila kitu,….tumekuuliza maswali, lakini mengine umekataa kutujibu, kuonyesha kuwa  unatuficha ukweli,…sasa kwa vile unatuficha ukweli, ngoja tufanye uchunguzi kwa kupitia njia nyingine, huku tukiendelea kukuhoji, na tutaendelea kukuhoji mpaka turizike na majibu yako,…’akatulia na kuangalia saa.

‘Haya endelea kunihoji,….maana nusu saa imepita, upo kimiya,ndio kuhoji gani huko?’ akauliza huyo mwanadada.

‘Nasubiri majibu ya maswali niliyokuuliza  mwanzono ambayo hujanijibu...’Akasema mkuu.

‘Maswali yapi ambayo sijakupa majibu, angalia kumbukumbu zako vyema,kila swali nimeshakupa majibu yangu, sijui ulitaka majibu mengine yapi, labda unifahamishe vyema…’akasema wakili.

‘Kuna habari kuwa ulikuwepo wakati maujai hayo yanafanyika, na uchunguzi ukikamilika, tunaweza kukushika kwasababu ya kushukiwa katika mauaji,…isingelikuwa mimi nakufahamu vyema , ungelishashikwa kwa ajili hiyo, lakini mimi  nakufahamu vyema,huwezi ukafanya jambo kama hilo. Na usichukulie hilo kama kigezo kuwa, kwasababu nakufahamu kwa hivyo, ndio niache sheria isifanye kazi, yake, hapana, ….sheria ipo pale pale….’akatuli na kuangalia jarida moja wapo alilolifungua.

‘Mkuu hujaniuliza swali hapo, hayo ni maelezo, naomba uendelee kuniuliza maswali, kama yamekwisha muniambia….’akasema mwanadada. Mkuu hakusema kitu akawa katulia akiandika kitu kwenye yale mafaili aliyo nayo pale mbele, na yume mwanadada akasema;

‘Sikiliza nikuambie kitu mkuu, ngoja niondoke, maana kunishikilia hapa tunapoteza muda na kuna mambo yanasimama, mambo ambayo yangelitusaidia kukiangamiza hiki kikundi, mimi nina njia yangu, na nyie mna njia yenu, habu niachieni nifanye nionavyo mimi, muone nini kitatokea….mtafurahi wenyewe…’akasema.

'Unafanya hiyo kazi kwa nani, hujatuambia mteja wako ni nani,...pili nimekupa huo muda umeshindwa kuutumia….’akasema huyo mkuu.

‘Muda gani ulionipa mkuu….?’ Akauliza.

‘Hapa nimekupa muda wa kutosha ili uniambie ukweli,…hujataka kufanya hivyo, hutaki kuniambia huo ukweli, hii ina-niweka katika mahali ambapo sitaweza kukuamini….na kama utaendela hivi, usishngae nikikubadilikia, maana mimi nafuta sheria na taratibu za kikazi yangu, kujuana isiwe ni kikwazo kwenye taratibu za kazi yangu…’akasema

‘Muda wa kukuambia ukweli ukifika nitakuambia mkuu, ujue mimi ni wakili, sitaweza kusema kitu mpaka niwe na ushahidi wa kutosha,….ndio maana naomba kibali chako,… kunishikilia hapa hakutasaidia kitu, wewe unanifahamu vyema, sio mtu wa kuongea ovyo bila ushahidi uliojitosheleza….na mkiendelea kunishikilia hapa ushahidi wote niliotarajia kuupata utapotea,…na hata huyo muuaji anaweza akapotea pia na matokeoa yake mtashikilia watu wasio na hatia….’akasema .

‘Haya tusaidiene , niambie ukweli siku ile ya tukio la mauaji ya huyu binti anayeitwa Kimwana, ulikuwa wapi, ukinijibu hilo swali tunaweza tukaenda sambamba….?’ akauliza.

‘Nimeshakuambia kuwa nitalijibu hilo swali  nikisha kusanya ushahidi wangu wa kutosha,… tunarudi kule kule kwenye maswali yenu, uliyoniuliza awali,, na amjibu nimeshawapa….na kama mna mashaka na mimi kuwa nimehusika katika hayo mauaji, basi nishikeni kwa uhalifu huo, …lakini fuatenu utaratibu wa kisheria...’akasema wakili.

‘Haya kama hutaki kunijibu hilo swali utaendelea kukaa hapa mpaka hapo vijana wangu watakapofanya uchunguzi wa kutosha….na ole wako ikigundulika kuwa ulikuwepo au unajua nini kilichotokea na wewe unaamua kutokushirikiana na polisi….na kuficha ushahidi’akasema huyo mkuu wa polisi na Mwanadada wakili akangalia saa yake, na alipoona muda wa yeye kushikiliwa pale umekwisha akachukua mkoba wake na kuinuka.

 Aliposimama, akasita pale alipoona anajiona kwenye kiyoo che meza, ya hiyo ofisi, akatabasamu na kusema;

'Nyie mnajitahidi sana mkuu, meza ya kiyoo....haya tuyaache haya ...hebu niambie, ushahidi gani ninaouficha...?'akasema na huku akiwa kashikilia ile meza huku akijiandaa kuondoka.

'Tatizo lenu mnawachukulia kuwa ofisi za maaskari hazitakiwi kuwa za kuvutia wateja,...nyie ni wateja wetu mnahitaji pia mjisikie vizuri mkiwa kwenye ofisi zetu, au sio....unaionaje hiyo meza.....?' akauliza na alipoona wakili hajibu kitu, kamkazia macho akisubiri jibu la swali alilouliza akasema;.

‘Kuna kitu alikuwa nacho marehemu, simu na saa, kama ujuavyo kuwa hivyo wamekuwa wakivitumia kama alama zaoza kujilinda na kujitambusliha wapi walipo,...na pia hivyo vifaa vinanaswa kwenye mitambao yao ,  na kama tungelivipata, vingelitusaidia kuona tukio nzima lilivyokuwa,.....tunao wataalamu wakuweza kuvitumia na kugundua nini kilitokea, ...hivyo vifaa  tunauhakika, alikuwa navyo marehemu, na ni ushidi muhimu kwetu,…’akasema huyo mkuu.

‘Kwahiyo mnanishikilia kuwa ninavyo hivyo vitu au sio, au mnanishilia kuwa nimehusika kwa hayo mauaji, ….niembeni wazi, ili nijue vipi nitajitetea…?’ akauliza huyo mwanadada.

‘Tumekuita hapa kwa kukuhoji, kutaka kujua ukweli, wewe kama wakili tuna imani kuwa utatuambia ukweli, ili na sisi tuweze kufanya kazi yetu vyema…’akasema mkuu.

‘Kama mnataka kunsihikilia kwa makosa hayo, ya kuwepo huko, ya kuchukua ushahidi, naomba mfuate taratibu,…., lakini muda wangu wa kukaa hapa umekwisha na naona huna maswali mengina ya kuniuliza, kwahiyo sina budi niondoke…’akasema huyo mwanadada na kuanza kuondoka.

‘Unakwenda wapi…?’ akauliza mkuu wa kituo huku akimwangalia kwa hasira.

‘Muda ambao mimi kama wakili wa kushikiliwa hapa umekwisha kama unataka kunichukulia hatua chukua, na mniambie ni kwanini mnanichukulia hizo hatua kwa kosa gani, ….lakini tafadhali, naombeni mfuate taratibu za kisheria, na tutakutana mahakamani….’akasema yule mwanadada huku akiwa hamuangalii huyo mkuu usoni, akiwa na wasi wasi na hiyo hatua anayoichukua…..

Yule mkuu wa polisi akamtizama kwa muda yule mwanadada,…alikuwa keshafiki hatua ya kumuachia, lakini kitendo cha yule mwanadada kuamua kujiondokea,  hakikumfurahisha, akiona kama vile kazarauliwa. Na hapo hasira zikampanda huku akiwaza achukue hatua gani ili huyo mwanadada amuheshimu, akasogeza mkono wake pale ilipo simu ya mezani, kutaka kuwapigia vijana wake, waje wamkamate huyo mwanadada na kumweka ndani.

Na kabla hajafanya hivyo,mara simu ya yule wakili ikalia kuashiria ujumbe mfupi wa maneno, akasimama , na kuusoma kwa haraka huo ujumbe, na baada ya kumaliza kuusoma ule ujumbe, akageuka na kumtizama mkuu ambaye alishainua simu ya mezani, kutaka kupiga namba, ila alisita pale aliposikia mlio wa huo ujumbe toka kwenye simu ya huyo mwanadada, wakataizamana machoni.

‘Haya niambie, maana nataka kuchukua hizo hatua za kisheria unazozidai, kwa mamlaka niliyopewa na jamuhuri,…sema kuna nini kimetokea maana wewe unajifanya polisi, ….badala ya kufanya kazi yako ya uwakili unaingilia kazi zisizo kuhusu,…niambie, huo ujumbe unasemaje, maana unavyoniangalia inaashiria jambo…?’ akauliza.

‘Umesema kuwa unanihitaji mimi nishirikiane na nyie, kuhusiana na mauaji ya Kimwana,, sasa soma huu ujumbe halafu uniambie unataka nini zaidi….’akasema na kumpa yule mkuu ule ujumbe wa maneno, ujumbe ulitoka kwenye namba isiyo na jina ulisema;

‘Yule muuaji yupo kituo cha Ubungo, anakimbilia Morogoro, ….fika haraka hapa kituoni, kanipa lifti, lakini kuna foleni, gari aina ya landcruiser T908 CSA…..

‘Huu ujumbe umetoka kwanani?’ akauliza yule mkuu huku akiuangalia ule ujumbe na kumtizama huyo wakili na kuutizama ule ujumbe tena.

‘Hilo sio swali la msingi kwa sasa, cha muhimu ni wewe kufanya akzi yako, au twende huko ukapambane na huyo muuaji mwenyewe,…..’akasema huyo wakili huku akiangalia saa yake, na alipoona huyo mkuu hasemi kitu, akasema;

‘Kama bado unataka kuendelea kunishikilia hapa , naona muda wangu wa kuwasubiri umepita, sina budi niondoke, na kama mna lolote juu yangu, fuateni taratibu za kisheria, kwaheri….’akasema yule wakili akianza kuondoka, na kabla hayatembea hatua mbili yule mkuu wa kituo akainuka na kusema.

‘Subiri….tunakwenda wote, maana hutaweza kupita kwenye foleni mimi nina uwezo wa kufanya hivyo…najua jinsi gani ya kufanya….’Akasema na kupiga simu kituo cha ubungo na kuamrisha kuwa gari aina hiyo ya Landcruser, T908 zSA…..lishikiliwe, lakini kwa mbinu ya kuchelewesha foleni, na kama huyo muendesha hilo gari atataka kutoroka wahakikishe wanamkamata.

*******

Jangiri, akiwa kashikilia simu sikioni, alisikiliza ile simu ikiita na kila mlio wa kuita ulivyokuwa ukisikika masikioni mwake ndivyo alivyozidi kupandwa na hasira, akatizama mbele yake na kuona msururu wa magari kuonyesha kuwa foleni ni ndefu ajabu, na nyuma yake halikadhalika,huku akiwa kashikilia hiyo simu sikioni,

Foleni kwa muda ule haikumtia wasiwasi sana, alijua muda wowote magari yataruhusiwa ataondoka, lakini kilichokuwa kikimuuma na kumtia wasiwasi ni jinsi gani ataweza kuishi huko ugenini, anahitaji pesa, na alishaahidiwa kuwa atazipata. Sasa hizo pesa hazijapatikana na kwa ujumla hana pesa kabisa, huwa yeye akipata pesa ni za matumzi kwa kwenda mbele, hana hata akiba….

Mara siku ikapokelewa na sauti ya mtu ikihema, kuonyesha kuwa hayupo katika hli njema ya kuipokea, ila kaipokea tu , kwa vile hakuna jinsi. Na huyo mpokeaji akasema kwa sauti nzito ya kike;

‘Niambie,…’

‘Bosi,Pesa zangu , vipi, ….unajua mimi hapa sina pesa, na hizo ndizo nategemea kunisaidia huko ninapokwenda,unakumbuka ulivyoniambia, …hapa penyewe sina uhakika wa petrol kuwa inaweza kunifikisha huko ninapokwenda…foleni imebana `uwese’ unateketea,’akasema na huyo mtu sehemu ya pili akawa katulia kimiya hamjibu kitu, na baadaye huyo mtu sehemu ya pili akasema.

‘Umemaliza….?’

‘Ulitaka niongee nini zaidi Bosi,….mimi naona nimemaliza….nakusikiliza wewe bosi,’alitaka kupayuka, lakini akagundua kuwa anaongea na nani ,akatulia kusikiliza.

‘Hivi wewe umenisahau, ushajiona mtu wa maana sana, ...kwanza umeharibu, pili unadai pesa kama zako, wakati huna ulichokifanya,….nini makubaliano yetu, fanya kazi upate pesa, ukiharibu hupati kitu,…umeharibu,…nakuuliza hujaahribu?’ akaulizwa.

‘Lakini Bosi….’akaanza kujitetea.

‘Jibu swahli, umeharibu au hujaharibu,  mimi nimeamua kukupa tu hizo pesa…. tu,kwa vile wewe ni mtu wangu wa siku nyingi, vinginevyo nisingekupa hata senti moja, kwanza hustahili hata kupata hiyo nafasi  yakuongea na mimi, ilitakiwa sasa hivi umeshabadilika jina na kuitwa marehemu….umenisikitisha sana,…hujui tu, ….unajua thamani ya huyo mtu uliyemuondoa duniani bila hatia…’akasema huyo mtu na kutulia.

‘Bosi nilishakuambia ni bahati mbaya…na tupo kweny simu, hayo tuyaache,….unajua bosi hata mimi imeniumiza sana wewe hujui tu, ..nashindwa hata kulala, kuona kuwa mkono wangu umemuondoa mtu niliyekuwa nikimpenda sana….sijui nifanyeje,lakini sina jinsi maji yameshamwagika, lakini naahidi kuwa nitalipiza kisasai chake tu….’akasema.

‘Utalipiza kisasa chake kwa nani , wakati wewe ndiye uliyemuua, ni nani aliyekuambia umuue..basi jiue mwenyewe ndio tuseme umelipiza kisasi chake….na inabidi iwe hivyo, sioni umuhimu wako tena kwangu…’akasema.

‘Bosi tupo kwenye simu bosi,…..na eti nini, ina maana mimi sasa huoni umuhimu wangu tena, siamini masikio yangu….’akasema huku hasira zikimpanda, na akawa anawaza jinsi gani ya kufanya kutokana na kauli ile,….hasira za siku nyingi kuhus huyo bosi zikamrejea, alishaapa kuwa akimpatia nafasi atamfanyoa kitu mbaya aishilie pasipojulikana, lakini ndiye aliyemfanya aishi hapa mjini,….akanywea.

‘Hebu niambie, hivi sasa una umuhimu gani, wakati unatafutwa kila kona, na wewe ukishikwa unaweza ukapanua hilo domo lako, nakuhakikishia kuwa kama utapanua hilo domo lako, hutakatiza masaa, …nitahakikisha mwenyewe unalia kama mtoto mdogo kabla hujaenda kuwa chakula cha mchwa….unasikia ?’ akasema.

‘Bosi…bosi, ina maana huniamini..mimi sio mtu wa kuongea ovyo,…watanifanya nini mpaka niongee….bosi , tafadhali naomba sana, kuhusu hizo pesa , mimi nitalipiza kisasi kwa huyo aliyesababisha hayo, maana kama isingelikuwa huyo wakili, natumai mambo yangelikuwa safi…sasa huyo wakili ndio kaharibu, nitakula naye sahani moja, wewe utaona tu,…..ngoja nikatulie huko mafichoni kwa muda….’akasema.

‘Hayo unajua wewe, …ila kama ulivyosema, sitaki nkuone hapa mjini,na nikikuona hapa jijini sitaongea mara mbili, mimi mwenyewe nitahakikisha risasi imepenya kwenye ubongo wako kama ulivyofanya kwa huyo binti yangu,…..natamani kama ungelikuw akaribu nikafanya hivyo, ….pesa nimeshatuma kwenye mtandao, nenda kibandani kachukue….’sauti ikasema.

‘Nimekwenda kibandani hakuna kitu, hapa kwenye salio la simu inaonyesha kabisa hakuna pesa iliyoingia, …nimeangalia sasa hivi kabla sijakupigia simu hii ni mara ya tatu naangalia, hakuna pesa iliyoingia….’akasema kwa sauti.

‘Unajua unaongea nani, na kamwe usiniongelee kwa sauti ya ukali,…. kwasababu hunidai, unasikia mimi natoa pesa kukusaidia tu…na pesa hiyo nimeshaingiza kwenye namba ya simu yako, labda ni tatizo la mitandao, usinisumbue, …’akatulia na kabla Jangiri hajasema  kitu, akasikia sauti ya ukali ikisema;

‘Unasikia na ukinipigia simu tena na kuniongelea kwa hasira kama vile mimi ni mkeo,…ukirudia tena,  nitahakikisha simu yako haitoi sauti,na masikio yako nayaziba…unasikia, usione upo mbali ya upeo wa macho yangu,ukazania ziwezi kukufanya kitu, ….angalaia salio hata mara kumi,ni juu yako ….unasikia …akili yako ndogo isiyo na maana….’simu ikakatika.

‘Na wewe akili yako kubwa lakini chafu, haina maana pia….’akasema lakini alipohakikisha kuwa simu haipo hewani, na akawa mawazoni akijuliza kwanini huyo mwanamke anamchezea, hajui kwake kumaliza uhaii wa mtu ni mara moja,…alipofikia hapo akaanza kujuta, alijuta kwa vile mkono wake umemuua mtu aliyempenda, akaivuta sura ya huyo binti na kumuwaza na kukubuka siku ile ya tukio livyokuwa.

*******

‘Huyo mwanadada wakili yupo, anaonekana katika mitambo yetu, ingawaje imekatika, hatuna uhakika na usalama wa mtu wetu, hakikisha unammaliza huyo wakili,….hakikisha hakuna ushahidi….’simu ikamwambia.

Harakaharaka akaichukua bastola yake na kuivalisha kiwambo ya kuzuia sauti, akasogea hadi kwenye dirisha, dirisha hilolipo ndani ya chumba kinachoangalina nachumba kingine,…lakini pazia ikawa kizuizi, asingeliweza kulisogeza hilo pazia, kwasababu lipo upande wa pili ….

Akatafuta upendo na bahati akamuona bosi wake yupo kwa ndani na kweli akamuona huyo aliyeambiwa ni wakili, akiwa kasimama, ulikuwa usawa wake, na hapo ilikuwa nafasi nzuri kabisa, alijua kabisa hapo anaweza kuitumbikiza risasi kwenye kichwa cha huyo wakili, bila ya kumzurubosi wake.

‘Akasogeza na kulenga shabaha, na wakati keshabonyeza kitufe cha kufayatulia risasi, bosi wake akasogea ni kuwa sambamba na wakili, na wakati huohuo wakili alishainama, ….ooh, kilichotokea hakuamini…
.
‘Lakini nakumbuka kama vile risasi niliyoipiga hakulenga, …maana yule mwanadada aliinama...na bosi hakuwa katika lengolangu, alikuwa kasimama tenge,....ilikuwaje pale.....hapo sina uhakika,....na mimi mjinga kweli, kwanini sikuutafuta huo uhakika, ….maana alivyokuwa kasimama yule wakili na akainama,risasi isingeliweza kumlenga yule bosi wangu, .isingeliwezekana….pazia lile lilificha ukweli,…sijui, lakini nani mwingine angeliweza kufanya vile, …maana tulikuwa peke yetu, nina uhakika huo…ooh, nimemuua Kimwana  tulizo la roho yangu , hapo sina cha kujitetea….’akasema kwa sauti ndogo.

Alipofikia hapo akahisi machozi yakimlengalenga, ingawaje hana hisia za kulia, `Ina maana mimi kweli nimemua mtu ambaye moyo wangu ulishampenda,na nakumbuka siku moja nilishamuambia kuwa ninampenda kuliko kitu ingine, na nilikuwa tayari kumpa chochote ili anikizie matakwa, yangu, akanitolea nje, lakini nilijua ipo siku atanikubalia tu, sasa keshaondoka imebakia hadithi….,

Kumbukumbu zile zilipoyeyua kichwani, akaangalia salio  kwenye simu yake, kwenye mtandao, akakuta pesa hakuna, akairusha simu kwa hasira kwenye kiti, mpaka ikafunguka na vifaa vyake vikasambaratika kila kitu kivyake, na wakati anataka kuviokota vifaa hivyo vya simu alipogundua kuwa kafanya ujinga, mara akaona mtu kasimama pembeni ya gari akimwangalia, na yeye akjikuta nashikwa na hamasa ya kumuangalia.

‘Huyu mtu nilimuona wapi….’akajiuliza na kusahau kuokota vile vifaa vya simu, na cha kushangaza akaona huyo mtu akisogea karibu na gari lake, akasema kimoyoni, asije akawa askari kanzu katumwa kumkamata, kama ni askari kanzu hatakubali kukamatwa kirahisi hivyo, lakini alipomuangalia yule mtu kwa makini akagundua kuwa hana sura ya uaskari kanzu.

‘Rafiki, unaelekea Morogoro….’mara akasikia huyo mtu akiuliza, na akashusha kiyoo na kumwangalia kwa makini,nankumuuliza huku akiwa kakunja uso kwa hasira.

‘Kwani wewe ni nani mpaka unaniulzia swali kama hilo..?’ akasema kwa hasira, na baadaye akaona ajilainishe maana asije akaleta vurumai na polisi wakaingilia kati.

‘Mimi ni msamaria mwema tu, nimekwama na nahitaji kufika Morogoro haraka, hapa jijini hakukaliki tena….’akasikia huyo mtu akiongea, na maneno hayo yakampa faraja, na alipomuon ana begi la safari, akaona atapata mtu wa kusadiana naye akikwama njiani, na mawazoni akasema kumbe na wewe una mawazo kama ya kwangu.

‘Ingia, najua utachangia mafuta, hakuna cha bure hapa….’akasema na huyo jama akafungua mlango na kukaa pembeni kama abiria.

‘Sura yako sio ngeni kwangu, nilikuona wapi vile?’ akamuuliza.

‘Kwakweli sikumbuki,tatizo mimi huwa sikumbuki sura za watu, …kwanza nizikumbuke za nini..zitanisaidia nini mimi,labda kama ni suta za pesa, njua nitapata pesa,….’akasema huyo jamaa.

‘Ina maana sura yangu sio ya pesa…?’akauliza Jangiri.

‘Siwezi kujua, …..cha muhimu ni kuzitoa sio kuonekana, …na hizi foleni bwana , mbona leo hizi foleni zimezidi, watu tunataka tuongelee ndani ya mji wa Moro…’akasema huyo jamaa.

‘Hata mimi zinanichosha,….lakini hakuna jinsi, hapa huwezi kupenya popote, kwa hali ilivyo, inabidi kusubiri tu, tukipata upenyo, gari litapaa , maana spidi ya kuondoka nayo, inabidi ufunge mkanda,…au unaogopa kufa, mimi nikiwa kweney gari siogopi kufa,….naendesha kama sina roho….shauri lako,kama umwoga bora ushuke kabisa….’akasema Jangiri.

‘Wewe usijali, ….ilimradi tufike tu, ……mbona naona vifaa vya simu,….hii betrii ya simu, aah, hiki kifuniko,…na ile pale simu yenyewe,,,, ni simu yako nini…?’ akauliza huyo abiria alipoona anakanyaga baadhi ya vifaa vya simu.

‘Aaah, ….ndio ndio, wewe unafika kwenye nyumba unauliza vyombo vilivyopo ndani ni vya nani,….unajua kuna mtu ninamdai, kanipandisha hasira, na …’

‘Hasira unaimalizia kwenye simu, huoni kuwa utakuwa umepata hasara mara mbili…’akasema huyo abiria.
Jangiri akainama kuokoteza vifaa vyake vya simu, na hapo jamaa akapata muda wa kuandika ujumbe wa maneno kwa haraka na kuituma kabla Jangiri hajainuka. Alipoinuka akaifunga simu yake vyema, na baadaye akajaribu kupiga, lakini huko alikopiga ikawa simu haipatikani, akajaribu kuangalia salia, akakuta hakuna pesa iliyoingia, akasonya na kushkilai usukani wa gari kwa hasira,….

‘Sasa itakuwaje,maana sina pesa, na ninapokwenda natakiwa gharama,hoteli na ……na kwamtaji huo itabidi nifanye jambo ambalo sikutaka kulifanya,…sasa utaishije na halikama hii,..ndio maisha yetu…’akasema akiwa kasaahu kuwa kuna abiria pembeni yake.

‘Jambo gani la kuingiza pesa maana hata mimi ni mtafutaji….nipo tayari nikupe mkono, …..hata kama ni kubeba mizigo, au kuwa otingo wako nipo tayari….’akasema huyo abiria na kumshitua dereva wake,ambaye alishasahau kuwa ana abiria, kutokana na hasira alizokuwa nazo, akamgeukia na kusema.

‘Hebu niambie tulikutana wapi,maana nina uhakika kuwa nimekuona mahali, sura yako naikumbuka, lakini sijaweza kukumbuka ni wapi…..na kwa vile leo akili yangu haijatulia vyema, nashindwa kufikiria nilikuona wapi,….kwani unafanyia  wapi shughuli zako..?’ akauliza.

‘Nimeshakuambia kuwa mimi huwa sikumbuki sana sura za watu, mimi ni mbangaizaji tu hapa na pale, leo tunafuuzwa na city hapa. Tunakimbilia kule, leo nimepata kibaru hapa, ilimradi siku zinakwenda, kwa ufupi mimi ni mtu wa kufanya vibarua hapa na pale, ….nimejikuta maisha hayaendi vyema, nikaona sasa ni bora nirudi kijijini nikatambike kidogo,….na wewe una kazi gani?’ abiria akauliza.

‘Misheni town….mimi ni mtu wa dili za hapa na pale,….’akasema dereva, akijaribu kuangalia salio tena kwenye simu yake….na kabla hajaweza kufikia sehemu ya kuonyesha salio, mara simu yake ikaita, na akabonyeza sehemu ya kupokea bila kuangalia nani mpigaji, na aliposikia sauti ya mpigaji akataka kuanza kualalamika, lakini sauti aliyosikia iliashiria vinginevyo, akatulia kusikiliza kwa muda,na sura ikabadilika, ….simu ikanyamza na hapo hapo akatizama huku na kule, na baadaye akasema;

‘Sikubali,….hapa lazima nitafute njia ya kuondoka,’ akasema kimoyomoyo,… akaangalia nyuma, hakuna nafasi , mbele hakuna nafasi , akaangalia pembeni kuna mtaro,gari haliwezi kupita…kwingine halikadhalika mtaro, akaguna, akashika mlango kutaka kuufungua, lakini kwanza akageuka kumwangalia abiria wake, na kusema;

‘Unasikia…, wewe kaa humo kwenye gari,nakwenda hapo dukani kununua vocha, …’akasem Jangiri huku akiangaza macho huku na kule.

‘Vocha si hizo hapo pembeni muite huyo jamaa akuletee, foleni inaweza ikatembea na wewe haupo, na mimi hapa sina leseni…nani ataendesha hili gari lako’akasema abiria,na mara sauti ya ving’ora vya magari ikasikika kwa mbali, ikiashiria kuwa huenda  kuna msafara unapita …

‘Kumbe kulikuwa na msafara , ndio maana wanatugandisha hapa…hawa watu bwana ina maana muda wote huo tunasubiri wakubwa wapite,hawajui kuwa kuna watu wana safari zao za muhimukuliko hawo wakubwa zao…’akasema huyo abiria.

‘Ngoja tuone kama kweli ni msafara, au kuna jingine….hapa nimechanganganyikiwa , kila dakika inanuka hatari,….na huyu, keshanichanganaykabisa….sijui…’akasema Jangiri na kuangalia huko mlio wa king’ora unapotokea.

‘Ni msafara huo, huoni kule….’akasema yule abiria, na Jangiri akawa anaangalia huko sauti inapotoka kwa makini,lakini moyo wake ulikuwa ukienda mbio, hakuwa na amani kabisa, alishahidi kuwa hakuna usalama, a lengo lake lilikuwa kutoka pale kwenye gari na kukaa kwa mbali hadi atakapoona kuwa magari yameruhusiwa ndipo aingie kwenye gari lake, hakutaka kabisa kukamatwa kirahisi rahisi, akakumbuka bastola yake alioificha ndani ya gari, lakini haikuwa an haja kwa muda.
  
 Ni wakati sasa keshafungua mlango anajiandaa kutoka, kumbe kwa nyuma kuna watu waliokuwa wakimchunguza kwa makini,na walipoona kuwa anatakakushukakwenye gari, mmoja wapo akamsogelea na, na kusimama karibu yake, lakini Jangiri alijua ni kati ya watu wanaopita barabarani, akamwambia abiria wake.

‘Hapa siwezi kukaa, wewe bakia humo kwenye gari……na….’kabla hajamaliza kusema akashitukia mtu akija pale mlangoni ,ambapo alishaufungua tayari kushuka, na mtu huyo akatoa bastola na kumuonyeshea na kusema.

‘Mimi ni mwana usalama upo chini ya ulinzi…’ sauti kali ikatoka na watu wengine wawili wakatokea kwa nyuma ya gari wakiwa nao wameshikilia bastola tayari tayari. Jangiri kwa hasira akageuka kumwangalia abiria wake ambaye alikuwa kaduwaa akishangaa, na alitaka kusema neno, lakini alipomuona abiria wake akiwa akuduwaa, akanyamaza na kuwasikiliza wake maaskari watasema nini, mara yule abiria kwa woga akasema;

‘Mimi simo,… niliomba lifti tu…..’yule abiria akajaribu kufungua mlango akitoka kutoka, lakini akajikuta akionyeshewa bastola na kuambiwa atulia kimiya.

‘Wewe unataka kwenda wapi, wote mpo chini ya ulinzi….’amri ikatolewa.
NB: Haya jamaa haitaki jela, lakini alivy na bahati mbaya, kila jambo analijiingiza anajikuta jela ikimnyemelea ni nini kitatokea, tuwepo ….je hakuna maoni, je hii kazi mnaionaje…. ?

WAZO LA LEO: Unapohangaika katika maisha yako,kamwe usisahau ulipotoka, tusiwasahau wazazi wetu, na pia tusiwasahau wale tuliohangaika nao, hadi kufikia hatua tuliyo nayo sasa, mshukuru mungu huku ukikumbuka kuwa inawezekana kabisa ukaporomoka…yote ni mjaliwa ya mtoa riziki,…, kama wahenga walivyosema kuwa mpanda ngazi hushuka, na huwezi jua,  kwani hujafa hujaumbika.Ni mimi: emu-three

4 comments :

Rachel siwa Isaac said...

Ahsante kwa Wazo za Leo ndugu wa mimi,pia nafurahi kuona kazi inasonga mbele,daima Pamoja ndugu yangu

emu-three said...

Rachel, Wewe kweli ndugu wa mimi kwa shida na raha, mungu akubariki sana,Tupo pamoja

samira said...

kazi nzuri m3 da yaani jamaa ana bahati mbaya kila anapopita lazma itokee ishuu
jela inanukia nasubiri nione itakuwaje
big up me upo juuuuuu

Rachel siwa Isaac said...

Amina ndugu wa mimi, Atubariki sote Ndugu yangu Pamoja daima!