Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, May 2, 2012

Hujafa hujaumbika-30`Kwanza kabisa nakuomba twende kwangu, kwani haya ninayotaka kukuuliza yanahitaji faragha, ..natumai hujawahi kufika kwangu, pili, hizo nguo ulizovaa zitakutia homa ya baridi, hiki ni kipindi cha baridi…twende kwangu ukabadili hizo nguo, uoge, halafu tutaingia kwenye mazungumzo, na baada ya mazungumzo tutakwenda huko gerezani…’aliniambia dada wakili..

‘Unasema nini, eti…nini hapana, kama ni hivyo naona tuagane…’nikasema na kumwangali machoni, akanitizamakwa muda akasema;

‘Nakuomba twende kwangu kwanza, nina mazungumzo na  wewe nii muhimu sana kwangu…’alinisisitizia mpaka nikakubali, na tulifika nyumbani kwake, sikutka kumdadisi zaidi kuwa anaishi pake yake au vipi,kwani swali nilihsmuulizia kuwa kaolewa au vipi, hakutaka kunijibu hilo swali, lakini nitamuuliza hilo swali  kwa wakati muafaka.

‘Unaishi kwenye nyumba nzuri, upo peke yako….?’ Nikauliza.

‘Hayo kwa sasa tuyaache, utakuja kuyajua baadaye kama ni lazima, kwanza nenda bafuni ukaoge, na ukija nitakuonyesha nguo za kubadili….’akanionyesha wapi bafu lilipoai,nami nikafanya hivyo, niliporudi alinionyesha nguo za kubadili, halafu akaniacha hapo nikibadili, na yeye akasema ananisubiri sehemu ya maongezi.

Nilimkuta akiwa anasoma kitabu, nikakohoa kumshitua, akaniangalia na kutabasamu, akasema;

‘Hizo nguo zimekupendeza sana, ..ukizivaa zinanikumbusha mbali…..uziniulize mbali wapi, maana ninaweza nikashindwa hata kukuuliza hayo niliyokusudia kukuuliza, na pili muda hutoshi kuyaongea ya kwangu, leo tunaongea kuhusu wewe…’akasema na kuniangalia  kama ananichunguza nilivyovaa, nikawa sijisikii vyema jinsi anavyonichunguza kwa macho, naye akagundua hilo akasema.

'Usijali ni kumbukumbu za nyuma zinanirejea, lakini ..ndio dunia ilivyo, haya kaa hapa tuongee....'akasema na kunionyesha kwenye sofa.

‘Sawa mimi ni mgeni wako….’nikasema.

‘Tukimaliza kuongea hapa tunakwenda huko magereza, ni muhimu sana….’akasema na kunifanya nitakae kuinuka na kuondoka, nikasema

‘Unasema nini, eti nini…mbona hujanielewa. .hapana,  huko bwana sitakwenda kabisa, huko nimeapa,labda iwe kwa shinikizo la nguvu ya dola, lakini sio kwahiari yangu mwenyewe, huko siendi, naomba tafadahli unielewe hivyo,nasisitiza tena ….’nikasema.

'Utakwenda tu, lakini tuyaace hayo kwanza...'akasema na kutabasamu,nami nikiwa sina raha, maana naona huko kwenda Gerezani ni muhimu sana kwake, na inavyoonyesha hajali hisia zangu, lakini nikatulia kuonyesha heshima kwa wema wake.

 Alitengeneza kinywaji , na tukawa tunakunywa na muda mwingi tulikuwa kimiya kwa muda, nafikiri alikuwa akinipa muda nimalize kwanza hicho kinywaji kabala hajaanza kunihoji, ....na baadaye mahojiano yakaanza;


‘Hebu niambie kuhusu mke wako wa kwanza, ni ni hasa kilikusukuma mpaka ukamuacha,maana alikuwa na sifa zote za kuwa mke mwema,…..?’ akaniuliza na kuniangalia mchoni.

Nilitulia kwa muda nikitafakari hilo swali na nini nimjibu, kwasababu hakuna ambacho nitamwambia mtu akanielewa, hata mimi najijutia moyoni, nashindwa kujua kitu hasa muhimu kilichonishinikiza hadi nikamuacha yule mwanamke, na hapo nipo na mtu ambaye anataka jibu,ili liweze kumsaidia katika utafiti wake na pia liweze kuwasaidia wanawake wengine kama alivyodai,…nikafunua mdomo na kusema;

‘Ina maana huyo aliyekamtwa huko gerezani ni huyo mke wangu wa kwanza,haiwezekani,..kwa kosa gani…?’ nikauliza nikiwa na wasiwasi.

‘Nimeshakuambia kuwa sasa ni muda wa wewe kujibu maswali nitakayokuuliza,sio muda wa wewe kuniuliza maswali,na pia mimi mwenyewe sijafika huko, kwahiyo sina uhakika ni nani ….nataka jibu tafadhali, ..’akasema na kuniangalia machoni…na safari hii nikawa anona yale macho ya mahakamani, macho ambayoo yanamsoma mtu undani wake,na kuwa ukidanganay anajua umedanganya….

‘Kwaweki mke yule alikuwa na sifa zote za mke bora, nakiri kuwa nilifanya kosa kumuacha, lakini sababu  kubwa ya msingi ya kumuacha ni kuwa, nilipomuoa…, nionavyo mimi ….inawezekaan nisieleweke kwahili, lakini lazima nijitete,au sio,….?’ Nikauliza na yeye akatikisa kichwa kuniitikia hakusema neon na nikaendelea kusema;

‘Kiukweli, alikuwa hajajua kabisa nini misingi mikubwa ya ndoa, …kuwajibika kikazi za nyumbani alikwua anjua sana, labda kimpangilio kuwa hiki kikae wapi na nisema ule eushamba wa kutojua mambo ya kisasa..hayo nilimfundisha akaelewa, tatizo lilikuwa sehemu muhimu kwangu, …yeye alikuwa akijua kuwa mwili wake hauna ruhusa kwangu, ….kwa ufupi hakujua matendo ya ndoa ya kurizishana na hakutaka kuelekezwa…au hata kujifunza kuhusu hilo’nikasema.

‘Una uhakika na hilo,maana mke anapoolewa mara nyingi anatarajia kupata maelekezo toka kwa mume wake, na yule alivyo ni mtiifu kwa mume wake, na sio nakuambia hilo kwa kukisia, nimelipata toka kwenye kinywa cha mumewe wa sasa….’akaniuliza na maelzo hayo,

‘Kwa muda niliokuwa nikiishi naye, hakuwa anajua hilo,nina uhakika kabisa na hilo, sema labda alipopelekwa shule na huyo mumewe wa sasa ndio akawa kajifunza au tuseme ubongo wake ulipanuka na pia huenda mwenyewe alijuta na kutafakari kosa alilolifanya, na pia huenda aliuliza na wakubwa wakamuasa, yote inawezekana…..’nikajitetea.

‘Kwanini hukumfundisha wewe, kwanini hamkukaa kama mke na mume mkafundishana,…..natumai angelijifunza hilo,kwani sio swala la kukaa darasani,….eti hilo linahitaji kukaa darasani?’ Akaniuliza.

‘Nilijaribu hilo,…nilichogundua ni kuwa, hakutaka kabisa kuamrishwa chchote kuhusu  mwili wake, alikuwa mgumu sana kutenda tendo ambalo kwake aliliona kuwa ni uchafu,…. na sikutaka kumlazimisha kwa kitu ambacho hakuwa akikitaka,ukizingatia historia yake ya mateso…’nikasema na huyu mwanadada akacheka.

‘Kwahiyo kitu kikubwa kilichokusukuma kumuoa huyo mke ni pamoja na huruma ya historia yake, sio mapenzi ya dhati…tunaweza kusema hivyo, au nimekosea….?’ Akaniuliza.

‘Siwezi nikahalalisha huo usemi, ….nilimpenda kwa dhati,na kama kweli angelijua nini ninachokitaka, akawa anakubaliana na mimi ,akanitosheleza …..sizani kama huyo mke wa pili anagliweza kunishawishi kitu….’nikasema

‘Ina maana huyu mke wa pili aliweza kuingia akilini mwako baada ya kuleta kila ulichokuwa ukikikosa kwa mke wako huyu wa kwanza?’akaniuliza.
‘Tunaweza kusema hivyo….maana nilipokutana naye na kunifanyia yale moyo unapenda,….mmh, niseme ukweli, ilikuwa kama mtu kuja kulambishwa asali ambayo hujawahi kuilamba, unaisikia tu, na unaihitaji,….au kupata maji kipindi cha jua kali, ulikuw ana kiu sana, ukapata maji, niliona kuwa  hapo nimefika…nilichokitaka ndio hicho, akili ikiwa imezubaika,….’nikasema
‘Hebu niambia kuhusu huyu mke wapili, alikuwaje hadi ukaona yeye ana kitu tofauti na huyo wa kwanza , kitu ambacho huyo wa kwanza likuwa hana,na ulijuaje hilo na hata kudiriki kumuacha mke  ambaye kila kinywa nilichokutana huko kijijini kwenu, kilikuwa kikidai kuwa yeye ndiye mke mwema ambaye kila mwanaume alikuwa anatamani awe naye….nakweli nenda sas hivi kijijini uone maendeleo, mengikayahimiza huyo mwanamama, ….na hata mumewe anamsifia kwasifa zote…za kila idara..’akasema huyu mwanadada.
‘Kumbe ulibahatika kwenda huko Kijijini kwetu…..na kumbe ni kweli waanyosema watu….ni kweli yule aliksoa mwongozo wa mwanzo, na nafikiri alikuja kijifunza hayo baadaye,na ukichanganya na elimu….’nikasemamoyo ukijaa wivu.
‘Kwahiyo alikuwa mke mwema kwa wenzako,kwako haikuwa hivyo?’ akauliza.
‘Mimi kweli  nakiri hivyo kuwa huyo ni mke mwema,ana sifa zote, lakini hilo sikuwa naliona hivyo wakati nipo naye, kwasababu akili na hisia zangu zilikuwa zinahitaji kitu ambacho kwa muda huo yeye, labda kwa kutokujua, au kwa sababu aliona ndivyo inatakiwa iwe,hakuweza kunitimizia….’nikasema na akili yangu ikawa anamkumbuka huyo mke na huku moyoni nikijijutia. Na hapo nikajua kweli kitu utakioan ni kizuri pale kinapokuponyoka.
‘Hebu elezea kuhusu mke wako huyo wa pili,alikuwaje….’akasema huku akinisubiria.
‘Mke wa pili, naweza kusema alikuwa mtaalamu wa matendo ya ndoa, sio utani, nilipokutana naye nilijisahau kabisa, ikawa kama kapandikiza kitu mwilini mwangu na akili yangu ikawa inamfikiria yeye tu, alijua nini afanye kwa wakati gani,na hakuwa na kipingamizi pale unapomuhitaji,tofauti na mke wangu wa kwanza,….yeye muda wa mchana humpati, hata kama upo mapumziko nyumbani,,….ilikuwa vigumu,…na ….ilikuwa kukuru kakara nashindwa hata kuelezea…’nikasemahuku nikiona aibu.
‘Endelea mbona inasita…’
‘Sipendi kuwaelezea wake zangu mambo yao ya ndani, naona kama nafichua siri za ndani ambazo sikuhitajika kuzisema…’nikasema.
‘Najua hilo, lakini ukumbuke hapa tunachotafuta ni jinsi gani ya kuwasaidia wanawake ambao kwa namna moja au nyingine wanajikuta katika huo mtihani,na huenda katika kuliweka hili wazi tunaweza tukawa tumeokao ndoa za watu….na niamini mimi niafanya hili kwa nia njema kabisa…tafadhali usinifiche kitu….’akasema, name nilitulia kwa muda baadaye nikaona haina haja nitamuambia kila kitu anachokihitaji.
‘Mke wangu wa kwanza akiwa kitandani alikuwa kama gogo….hajui afanye nini,anakusubirii ufanye kila kitu,inakuwa kama hayupo hai, sio kitandani tu, hata ukija anapokupkea, na kukimbiza mzigo ndani, kama unataka kum…mmh, mbusu, au kumkumbatia…vitu kama hivyo..hataki,…hataki..…lakini mke wa pili yeye alikuwa kama mwalimu wangu,na ukiwa umechoka, atakufaya uchomvu wote uishe na ukijisikie mzimakabisa na unakuwa na hamu ya kuwa naye tena, kila mara ila….’hapo nikatulia.
‘Kabla haujifikia kwenye hizo kasoro zake, ngoja nikuulize kitu, …’akasema na kuwa kama anawaza jambo.
‘Unafikiri huyu mke wako wa pili aliyajuaje hayo,yaani jinsi gani ya kutenda lile mwanaume analitaka na huyo mke wako wa kwanza angelijuaje kuwa wewe unataka iwe hivi na sio hivyo, wakati hajawahi kukutana na mume, na wewe ndiye uliyekuwa mume wake wa kwanza…?’  akauliza.
‘Huyu mke wa pili nilipomuulizia kuwa alijifunzia wapi hayo, aliniambia ni kwa utundu wake, udadisi na hata kusomea mambo hayo kwenye vitabu au kuuliza kwa watu wengine, na aliniambia kuwa yeye alitaka akiolewa ajue nini atakifanya kwa mwanaume wake,ili sije akaachika, au kuonekana hajui kitu…ndivyo alivyodai,kabla hatujajua nyendo na tabai zao…’nikasema na kutulia kidogo.
‘Lakini pia alikuja kukirii kuwa mengi alijifunza toka kwa mama Docta, ..hata hivyo alisema kuwa licha ya kujiunga na hilo kundi na shule waliyopatiwa, bado yeye mwenyewe alikuwa ameshajua hayo,ila huko kundini ambako walimkuta mwalimu anayeujua mwili wa mwanaume vyema, walipta mafunzoo ambayo hakuwahi kuyajua kabla, alijua mengi sana kumuhusu mwanaume, na siri ya mwanaume,mego kuhsu ndoa na misingi ya ndoa, …ila….’nikatulia kidogo na yeye akaniuliza kabla sijamaliza hilo nililotakakusema;
‘Kwahiyo kujua nini atende kwa mwanaume, sio kwamba alizaliwa nako, alijifunza, na huenda alijifunza kwa wanaume wake wa mwanzo, au ….licha ya hayo waliyojifunza toka kwa mama Docta? ’akaniuliza nami nikamkatisha kwa kusema.
‘Kuna siku aliniambia kuwa shangazi yake aliyewahi kusihi naye alikuwa akimuelezea jinsi gani mume anatakiwa atendewe, na hata bibi yake aliwahi kumfundsha hayo, pia yeye alipitia unyago,alifundwa…na alipotoka huko unyagoni, ndipo utundu wake ulipoanzia, anadai kuwa unyago ulimjenga sana kimawazo, na akawa hawaogopi wnaueme, …hata hivyo alisema kuwa alipokuwa msichana, alikuwa mtundu wa kudadisi sana mambo hayo na hata kuanza mahusiano akiwa mdogo sana…’nikamwambia.
‘Ina maana kumbe hayo mafunzo ya ndoa na jinsi ya kuishi na mume, sio vyema kumfundisha msichana akiwa bado hajafikia muda wake, maana kama alivyokuambia hivyo kuwa na baadaye akaanza mahusiano akiwa bado mdogo,huoni hilo ndilo chanzo cha yote hayo, alitakiwa kufundwa wakati keshafikia umri wa kuolewa, na wakati anajua jema na baya , su sio…?’ akauliza huyo mwanadada.
‘Sio kuwa kutokana na mafundishi hayo toka kwa shangazi yake ndiyo yalimvuta kutenda hayo,inawezekana kweli, lakini wengi wanaowafundisha watoto wao ,pia wanawakanya ubaya wa matendo hayo wakiwa wadogo….sasa inategemea na hulka ya huyo mtoto, wengine dnio hao wanakimbilia katika majaribio , wengine walio na imani za kumuogopa mungu wansubiri….’nikasema hukuu nikikumbuka kuwa hata mimi nilianza utundu huo baada ya kusoma vitabu vya mapenzi.
‘Haya niambie kasoro za mke wako wa pili, nini kilichokusibu mpaka ukaona hakufai kuwa mke wako , maana ulidai kuwa alijua nini maana ya ndoa, kwa vitendo, au sio, sasa unadai humtaki tena, na nakupa tahdahari kuwa huyo bado ni mke wako kisheria maana hujampa talaka…, unalijua hilo?…’akasema huyu wakili mwanadada.
‘Hata baada ya haya yote aliyonitendea, sheri gani inamkubali kuwa abdo ni mke wangu, najua mweneywe keshajivua sifa ya mke wangu,….kwa vyovyote vile sitamkubali tena kuwa mke wangu,na hiyo sheria kama inamtaka imchukue yeyei,….’ Nikasema kwa hasira, naye hakunijibu kitu akwa anasubiri maelezo yangu.
‘Ndugu muheshimiwa wakili, ninaomba licha ya kuwa sina pesaya kukulipa,nakuomba unisaidie kisheria niachane na huyu mwanamke, kama unavyodai kuwa  kisheria bado ni mke wangu,licha ya hayo mabaya aliyonitendea, lakini najua kabisa kiimani ya dini sio mke wangu tena ingawaje sikumuoa kiimani ya dini, nilimuoa bomani…, kutokana na hayo aliyonifanyia…hata angekuwa nani angemuacha..hafai,kuwa mke mwema, kabisa…’nikasema.
‘Mimi sio wakili wa kuachanisha ndoa za watu,mimi sana sana ninapatansiha ndoa,na sitajaribu hata siku moja kuachanisha watu walio-oana, kwani lengo langu na madhumuni yangu ni kuhakikisha kuwa ndoa na maisha ya ndoa ni ya amani na upendo,…..kwahiyo hili nitakukatalia, ila kama unataka ndoa yako iwe nzuri, nitakusaidia… vinginevyo,  ni wewe mwenyewe kulijengee hoja hilo swala la talaka, lskini sio kupitia kwangu …..’akasema nakungalia saa yake.
Naomba unijibu hili kwa ukweli unaotoka moyoni,je kama huyo mke wako wa kwanza akataka umrudie tena upo tayari,…?’ akaniuliza

‘Oooh,hiyo bahati nani ataikataa,hata leo ,akija akaniambia mimi nimeachana na mume wangu nirudie 
,nitashangilia sana, na nitamuoa siku hiyo hiyo….lakini hiyo naona ni ndoto…maana nasikia wanaishi na mume wake kwa raha ikizingatia kuwa mume wake anazo…’nikasema.

‘Utamrudia hata kama bado ana kasoro zile zile, ulizoziona,kuwa hajui mapenzi ya ndani,tuyaite tendo la ndoa….au sio?’ Akauliza.

‘Sikumaanisha tendo la ndoa tu, nina maanisha matendo ya ndoa. Mhh, kwasasa atakua anajua kwa vile keshaenda shule na keshajua nini anatakiwa afanye kwenye ndoa,hilo  nina uhakika, licha ya kuwa sijakutana naye….’nikasema.

‘Jibu swali langu….nasema hivi, kama atakuja kwako ili mrudiane, lakini bado ana kasoro zile zile ambazo zilikufanya umuache , bado utamkubali kumrudia…?’ akauliza na kunikazia macho yale ya kimahakamani.

‘Nitamarudia na nitahakikisha nampeleka shule, nitajitahidi kwa nguvu zangu zote ayajue hayo yanayostahili kuyajua kama mwanamke ndani ya ndoa…’nikasema

‘Na kama atakuawa mzito ,kama alivyokuwa mwanzoni, utamuacha,kama ulivyomuacha…..maana unasema sababu mojawapo ya kumucha ni kuwa, alikuwa mgumu kufundishika, na baada ya kupata kile ulichokuwa ukikosa kwake, kwamtu mwingine, ukaona haina haja ,ukamuacha… sasa kesharudi kwako tena,utafanyaje?’ akaniuliza.

Nilitulia kwa muda bila kulijibu hilo swali, nikiachanganua nisemeje,nikamwangalia huyu mwanadada ambaye alikuwanaye kaniangalai hapepesi macho,nikacheka nakusema;

‘Mnapooana ina maana hutahitaji tena kuangalia pembeni, kutamani mke, au wanawake wapita njia ,ina maana umeshajitosheleza,unapata kile unachokitaka, …kama mke hataki kuyafuata yale yanayotakiwa ili matamanio yaishe, unafikiri utafanyeje,hata kama ni mzuri wa namna gani, hata kama ana sifa nyingine zote, bado itakufanya wewe uishi kwa njaa….hapo bwana ….itakuwa vigumu kuishi naye,niseme ukweli, kwasababu najijua uzaifu wangu…’nikasema.

‘Kwahiyo kwako mke mwema …cha muhimu kwako kutoka kwa mke ni tendo la ndoa?’ akaniuliza.

‘Sio tendo la ndoa tu,ila tendo la ndoa linashika nafasi yake,na muhimu wanawake wakajua hilo, kuwa hilo ndilo linamfanya mwanaume atulie nyumbani,mkilibania na kutokuwajibika nalo,msija kulaumu mume akitoka nje ya ndoa,…hilo nasema kiukweli,…hasa mtu kama mimi niliye na damu inayochemka zaidi .’nikasema na huku nacheka .

‘Unajua sitaki kukupinga kwa hilo,ila natafuta njia ya kusaidiana , nia yangu ni kuboresha hayo uliyonayo na ili yawasaidie wengine, sasa wewe unasema hivyo ili wewe urizike katika matamanio yako, hasa ya kimwili zaidi…je wewe ,au wanaume wengine, wanajua nini wanawake wanataka ili na wao watulizane majumbani mwao, warizike, au mioyoni yao itulizane…?’akauliza.

‘Mimi ndio nimekwenda kuona, na nikumbie ukweli, mimi vitabu nilivyosoma,vilinipanua ubongo wangu, nikawa najua nini mwanamke anataka apate kutoka kwa mume, nini afanyiwe ili atulizane, najua kuwa wanawake wengine kwao mahitaji ya vitu ni muhimu sana kuliko….na kama hutampatia hivyo anavyotaka kwake mapenzi hakuna…lakini…’nikatulia.

‘Lakini nini…ongea natakakusikai kutoka kwako ukiwa unasimamia wanaume wenzako….’akaniambia.

‘Siri ya hayo anayotaka mwanamke,inapatikana katika kutimiza yale mwanaume anayoyataka, najua utasema ni mfumo dume,lakini tukumbuke kuwa wewe kama mke, umeolewa ..hujaoa,kwahiyo huyo aliyekuoa inabidi kwanza umtimizie yale anayoyahitaji, na hapo ndipo na wewe utakuwa na haki ya kudai yake unayoyahitaji…sijui unanielewa hapo…unapoajiriwa hudai kwanza mshahara, unfanya akzi kwanza, halafu baaaye unadai, ni mfano tu unaweza usitosheleze ninachotaka kusema….’nikasema.

‘Nakumbuka siku moja uliniambia mnapo-oana mnakuwa kitu kimoja,..au sio,kwamba mke ndio mume, na hisia zenu zinakuwa kitu kimoja, sasa iweje mke ndiye atakiwe kutenda, kujituma,na kutii kila kitu mwanaume anachotaka, kama mwili,basio utakuwa unatembea upande bega moja juu, maana upande mmoja utakuwa juu ya mwingine…huoni hiyo sio haki….?’akauliza

‘Nimeshakumbia siri ya mwanaume ipo hapo katika kumtimizia yale anayoyahitaji, ukiyawezea, umeshamshinda, atakuwa kama kondoo, kila unachokihitaji toka kwake utakipata, bila kutumia nguvu,nyie mumejaliwa hiyo siri,lakini hamtaki kuitumia, na badala yake mnataka kutumia mbinu za wanume,za kutumia nguvunyingi bila hekima, kujitutumua..kudai muwe sawa na wao, hapo kugombana kw amfahali….’nikasema.

‘Swali jingine, je kama mke wako wa pili atakuja na  kutaka mrudiane, akiwa kabadilika, hana tabia hizo chafu tena, tabia ambazo hazitakiwi kijamii na kwenye ndoa, na ikathibitishwa hivyo, utakuwa tayari kumrudia?’akaniuliza.

‘Hapana,..kwakweli huyo kwangu hana nafasi, pamoja na yakuwa anajua nini amrizishe mwanaume,lakini kwa alichonifanyia sitaweza kuishi naye tena, kwanza alinifanya nimuache mke wangu wa kwanza,…pili alinifanya nikosane na wazazi wangu na jamii yangu, na pia kunifanya nitengwe kabisa na jamii yangu, na hata kupoteza kazi…na….hatimaye nipo kama unavyoniaona, sina mbele wanyuma….’nikasema.

‘Ina maana yeye ndiye aliyekuwa akikuongoza…maana kwa mtizamo wako mume ndiye kichwa cha familia, ..sasa ilikuwaje yeye akawa ndye kichwa chako,huoni kuwa huo ulikuwa uzaifu wako , yeye kama mke alikuwa akitimiza wajibu wake ambao unauhitaji, na ili afanikiwe hilo ilibidi ahitajie yale ambayo hukuwa nayo….mambo muhumu…kwake?’

‘Hapo ndipo ninathibitisha usemi wangu kuwa kama mke anatimiza hayo mume anayoyataka,  mume atakuwa kama kondoo…mtiifu kila mke anachokitaka….ndio mke atapata kila kitu kutoka kwa huyo mumewe..sasa hapo napo inatakiwa mke awe na hekima kuwa sio vitu vyote vinapatikana….hasa tukiangalia hali halisi ya maisha na kipato…..usizidishe kudai…wengine hekima hiyo haipo, na matokeo yake, unajenga umbali...’nikaseman akusita kidogo.

‘Basi kumbe mume peke yake sio kichwa cha familia…kumbe na yeye anahitaji kuongozwa,kama ujuavyo kichwa kama hakina macho, ni kichwa lakini hakitaona vyema mbele na vile vile kama kichwa hakina masikioa,hakitasikia vyema, macho na masikio yake ni mkewe…unakubaliana na nadharia hiyo?’

‘Hiyo ndhariia tu, haina mantiki, maana jiulize kabla mume hajaoa alikuwa akiona vipi, na alikuwa akisikia vipii..nataka kusema kuwa kuja kwa mke ni kuongeza nguvu na kukamilisha maisha ya mwanadamu, kwasababu kwa vyovyote iwavyo kuna mambo ambayo wakikutana mke na mume yatafanyika kwa ufanisi zaidi kuliko vile mtu akiwa peke yake,…’nikatulia kidogo halafu nikasema;

‘Mkikutana wawili mtapata watoto, kwa njia iliyokubalika,najua kuwa unaweza ukawapata watoto nje ya ndoa,lakini jiulize huyu mtoto akizaliwa na kuja kuambiwa ulizaliwa  nje ya ndoa atajisikiaje….akiambiwa hana baba,…ataamini kweli….hilo kwa ndoa linakwepeka…. Na mkizingatia hayo kizazi kinakuwa na nidhamu, na huo ndio utaratibu alioukubaliwa mungu.

‘Hapo sasa tupo pamoja,nakuja kwenye swali muhimu sana….rejea maisha yako ya utotoni, nilikuambia wewe ni mwanaume wa wanawake watatu, hukuniuliza mke wa ni yupi. …Mimi nilimaanisha kuwa ule uhusiano wako na mwenzako mkiwa watoto mpaka mkakubaliana kuwa nyie ni mke na mume,una sehemu yake…huyo ndiye mke wako wa tatu, mke wa utotoni.’akasema na kutabasamu.

‘Lakini ule ulikuwa ni utoto,…ila …kwakweli natamani ingelikuwa hivyo, kuwa yale yangelikuwa ni kweli tukaja kuoana,..na ndio maana natamani sana nikutane naye tena …..lakini ndio basi tena…sizani kuwa uwezekano huo upo tena….sizani..!’nikasema.

‘Kwanini ukate tamaa,una uhakika kuwa huyo mwanamke hayupo tena, au keshaolewa,…kuna sababu gani ya kukata tamaa,…?’ akaniuliza.

‘Kwanza muda mrefu umepita,na umri umekwenda, yule wa kipindi kile,hatakuwa sawa na huyo wa sasa ….najau kabisa miili inabadilika,na hata tabia zinaweza zikabadilika pia, ingawaje kwa yule alivyokuwa …..sijui, nahisi hatakuwa na tabia mbaya…licha ya wazazi wangu kuniambai kuwa tabia zao kama familia  haifai ndani ya familia yetu,lakini nahisi kuwa yeye alikuwa na sifa zote…..ninazozihitaji mimi kama mimi….’nikasema.

‘Una uhakika gani na hilo wakati hamkuwahi kuishi pamoja kama mke na mume, nyie mlikuwa watoto tu, na pale mlipofikia mahali amabapo mnaweza kutafsiri maisha mkawa mumesigishana,..na kukatisha mawasiliano yenu…?’ akaniuliza.

‘Nilikuja kuzirejea zile barua tulizokuw a tukiandikiana,nikagundua jambo,… licha ya kuwa tuliziandika tukiwa wadogo, lakini zilikuwa zimejaa hekima, jisni gani tulitarajia kuwa mke na mume,jinsi gani tutendeane, ili tuweze kujenga familia inayofaa, ili watoto wetu wakulie katika maadili mema,tulifiki hadi kuelezana jinsi gani ya kutendeana kama mke na mume….’nikasema.

‘Yaani kwa huo umri mlikuwa mumeshajua mambo ya ndoa  ni nini kifanyike ndani ya ndoa,msinidanganye na nani aliwafundisha, au ndio mliwahi kupitia mambo ya unyago….?’akauliza.

‘Ndio tulikuwa tunajua…lakini kinadharia zaidi….kama nilivyokuambia nilikuwa nikisoma vitabu nilivyovikuta kwa mjomba wangu, na vingi vilikuwa na hadithi za ki- mapenzi mapenzi, …kutokana navyo nikajifunza mengi na hata kujiingiza kwenye utundu. Hutaamini kwa umri ule nilikuwa nimeshajifunza mambo mengi ya kikubwa…’nikasema huku nikicheka.

‘Hapo,hapo…..,kwanini mjomba wako alikuruhusu kusoma vitabu kama hivyo,huoni kuwa alichangia kukuiingiza kwenye maswala ya kikubwa kabla ya umri wako, na matokeo yake ndiyo hayo ….ukawa unawaharibu watoto wa majirani,….huoni hilo, au unasemaje?’akasema huyo mwanadada na kuwa kama ananiuliza.

‘Kwa namna moja hivyo vitabu viliniharibu kifikira, maana badala ya kutuliza kili kwenye masomo nikawa nawazia hayo, nawaza mambo ya kikubwa wakti mimi bado muda muafaka....lakini ukubwani vimenisaidia nikajua nini nifanye kwa mke wangu, …..nikawa namjua mwenzangu….hata hivyo, siwezi kumlaumu mjomba, kuwa aliniachia nikawa navisoma hivyo vitabu,,,’nikasema huku nikiwa nimeshika kichwa.

‘Sasa na mwenzako alijulia wapi hayo mambo,….?’ Akaniuliza.

‘Nilikuwa namuazima vitabu vya mjomba, …..hata hivyo aliwahi kuniambia kuwa shangazi yake alikuwa akimuelekeza mambo mengi, na hata alipokuwa akirudi likizo shangazi yake alikuwa akimfunda, na kumuelekeza nini kama mwanamke anatakiwa afanye. Baadaye tukawa hatuwasiliani nayr tena baada ya kunifumania kule kijijini.

‘Hapo ndio nataka kujua, ….mlisema mliwekeana ahadi kuwa mkiwa wakubwa mtaoana,….kwanini sasa ukaingia kwenye mahusiano na wasichana wengine na ilihali umesema kutokana na hivyo vitabu ulikuwa umejifunza mambo mengi ya ndoa, huoni kuwa hukijifunza bali vilikuharibu tu, vilikukomozakihisia kuliko kiakili, kwani kwa utoto uliokuwa nao, bado ulikuwa hujajua na hujajengeke kiutu uzima,…kujua, kipi kifanyike na kwa wakati gani?’ akauliza huyo mwanadada.

‘Ni kweli, kwa umri ule, sikuweza kuchanganua, nilikuwa nasahawshika kutenda zaidi bila kujali madhara yake, na bila kujali hisia za mwenzangu kuwa nitamuumiza akiona nipo na wasichana wengine, kuna wakati nilikuwa nawaza hivyo, lakini kwasababau ya utoto, nikawa sijali, hasa damu inaponichemka….’nikasema na kutabasamu.

‘Je kama nay eye angelifanya hivyo ungechukua hatua gani au ungeliskiaje?’

‘Kwakweli sijui, ….kwa utoto wangu, nilikuwa najifikiria mwenyewe, na kama ingetokea nikamuona na mvulana mwingine,kungechimbika,….hutaamini kuwa nilikuwa nikimchunguza, kila ninapomuona anatoka kwenda sokoni au popote, kuhakikisha kuwa hana mvulana anayeongozana naye…nilikuwa na wivu lakini sikutaka kuuonyesha’nikasema.

‘Nikuulize swali moja muhimu sana, je bado una mapenzi na huyo msichana?’ akaniuliza.

‘Kiukweli bado yupo kwenye moyo wangu….niseme ukweli bado nampenda, …..lakini sijui nikimkuta leo atakuwa kama yule yule, au kabadilika, hata akibadilika, nitakuwa bado nampenda maana pendo letu lilitoka moyoni, ….’nikasema.

‘Kwa mafano leo akija akakuambia kuwa anataka murudiane….ili ahadi yenu itimie utakuwa tayari, hata kama kuna mabadiliko, hata kama ana mambo ambayo hayataendana na matakwa yako?’ akauliza.

‘Hiyo bahati naisubiri sana,maana naona kama ndiye peke yake naweza kuishi naye, ana kila kitu ninachokihitaji,….hata hivyo….mmh,…..sijui kwakweli, maana nikikutana naye kitakachotawala ni hisia zetu za utoto, sitajali hayo mabadiliko….’nikasema bila kuwaza zaidi.

‘Wewe umemuacha mke wako wa pili kwasababu unadai ana matendo ambayo hayaendani na jamii,….hayakubaliani na familia, na huenda huyo msichana , na sijui kwa sasa atakuwa mwanamama, au bado ni mwanadada, ukutane naye, kumbe naye ana tabia kama hizo zinazoenda kinyume na maadili….utamkubali tu kwasababu ya hisia za utotoni, sema ukweli, utamkubali hivyo hivyo alivyo,kwasababu mliahidiana….?’ Akauliza na kuniangalia.

‘Ndio maana natamani nikutane naye, huenda nikikutana naye mengi yatajieleza,lakini kwa yule sizani kwamba anaweza kujiingiza kwenye mambo mabaya, kwanza ni msomi, pili anajua nini anachokifanya….na …siwezi kusema zaidi mpaka nimuone…’nikasema.

‘Wanasema ukipenda unakuwa kipofu, au sio,…, lakini ngoja Nikuulize tena, je mkionana naye akasema yeye yupo tayari mrudiane, na yupo tayari kuacha mambo hayo yanayokwenda kinyume na jamii, yupo tayari kutii mambo yenu ya kimila sijui, au kama alikuwa na mmbo machafu, huenda akawa, natoa mfano tu, je utamkubalia?’ akauliza.

‘Kwakweli …mmmh, mbona nitafurahi, nitamkubalia tu, maana hapa nilipo natamani saa zirudishwe nyuma, nimuoan tena…natamani nikutane naye…hata hivyo sina uhakika kama atakuwa yule yule….maana watu hubadilika, hasa miili yetu , na hata tabia, huenda yule niliyemjua kipindi kile atakuwa siye tena…’nikasema kwa mashaka.

‘Kwani wewe ulimpendea kwa maumbile yake, maana ukiwa msichana kuna mvuto mungu kaujalia,mvuto huo huja baadaye kufifia kutokana na mabadiliko ya kimwili…sasa je kama huo mvuto aliokuwa nao haupo tena, utasemaje..?’ akaniuliza akionyesha mashaka fulani usoni.

‘Nakubali hilo, ….lakini yule nimjuavyo,…hata akiwa na umri gani, uzuri wake ni wa asili….hata hivyo mimi nilimpenda toka moyoni,pendo hilo sidhani kama linahusu maumbile….sina uhakika na hilo,mpaka nimuone….’nikasema.

‘Mimi nina imani kuwa milima haikutani, lakini wanadamu hukutana, ipo siku mtakutana na hapo huenda ndoto yako ikatimia, nami nitafurahi nikiwa ni mmoja atakayeshuhudia jinsi gani itatokea,hasa pale mkikutana tena, na huenda mengi yatatokea,ukumbuke hapo kuna swala la muda, mabadiliko na mengine mungu ndiye anayejua….’akasema na kutabasamu.

‘Ni kweli….sijui itakuwaje nikikitana nye tena, sijui….nashindwa hata kuelezea….’nikasema nakutulia.

‘Sasa naona muda umekwenda na huu ndio muda muafaka wa kuelekea huko gerezani,…’akasema.

‘Aaaah, umeanza tena,…tulishakubaliana kuwa huko siendi,…siendi siendi…nimesema hivyo!’nikasema hivyo huku nikisisitizia kwa mikono.

‘Ina maana hutaki kwenda kukutana na mkeo,…? ‘ Akaniuliza na kunianglia kwa muda halafu akasema;

‘Kwa maana kwa taarifa nilizozipata ni kuwa anayekuita ni miongoni mwa mmoja wa waliokuwa wake zako, sijui ni yupi. Na aksema kabisa, nataka nionane na mume wangu, nina mengi ya kumwambiakbla sijahukumumiwa….nakuomba tafadhali kwa hisani yako usikatae kwito, nenda kamuone ili ujue nini kilichoko nafsini mwake,….’akasema.

Nikatulia kwa muda nikiwaza,na kujaribu kujiuliza, ni yupi huyo, na moyo wangu ukajua ni huyo huyo mwanamke nisiyetaka kumuona tena,….lakini kwanini ananitafuta, huenda ana jamboo muhimu, au anataka kuniomba msamaha,….nakasita, halafu nakajiuliza, hivi nikienda na kumsikiliza kitaharibika nini, nakisama.

‘Najua atakuwa ni huyo Kimwana, kwakeli sitaki kukutana naye tena, huenda kuniita hivyo anataka kuniingiza kwenye majanga mengine….!’ Nikasema.

‘Hata mimi kwa uhakika sijui kuwa ni huyo au ni yupi mwingine, ukumbuke wewe umewahi kuwa na wanawake watatu, unakumbuka hilo…?’ akauliza na kabla sijajibu akasema;, `Inawezekana akawa yeye, auaasiwe yeye,….cha muhimu ni kufika…..’akaniangalia kwa muda,halafu akaendelea kusema;

‘Je akiwa ni yule mke wako wakijijini utasemaje,…huwezi jua, dunia hii ina mambo na hujafa hujaumbika,….jaribu kujiuliza wewe ulitaraji ungeliingia jela,….hukujua katika maisha yako kabisa kuuwa utaingia huko,…lolote linawezekana kwa maisha haya ya mwanadamu,…sasa fikiri pengina ni huyo wa huko kijijini,kakuita hukuenda,na lolote likatokea,…?’ akaniangalia kwa makini,lakini mimi nilikuwa bado natingisha kichwa kikuataa.

‘Nakuuliza kamani huyo wa huko kijijini, hukuenda, na likatokea baya,….lazimanafsi yako itasononeka sana baadaye, na huenda kwa kufika kako ukamuokoa, akawa ana la moyoni, hata kama ni huyo Kimwana,…likatokeala kutokea, katika maisha yako yote utakuwa ukijiuliza hivi alikuwa akiniitia nini, huoni kuwa utaumia sana…., ndio maana nakushauru twende ukamuona ili tujue ni nani, na anataka kukuambia nini, twende muda unakwisha….’akaniambia na kutangulia nje kwenye gari lake.
Nikajibaragua,na kabla sijaamua kitu, nasikia gari nje likiwashwa na kupigwa honi….

NB. Lengo la sehemu hii ni kudodosa kujua ni nini hasa anahitaji mwanaume kwa mwanaume kwa mwanamke katika maswala ya ndoa, ni sehemu ndogo tu iliyochukuliwa katika mahojiano hayo, huenda yapo maswali mengi ya kujiuliza ,hasa kwako wewe mtarajiwa au yule aliyepo kwenye ndoa, je ni nini hasa mwanaume anataka  kwa mke, na mke anataka kwa mume.
Labda inachosha sehemu hii, lakini ni sehemu muhimu sana katika kisa hiki, na utagundua baadaye....tuzidi kuwepo.

WAZO LA LEO: Siri iliyopo kichwani mwa mtu ni vigumu kuijua, na mkiwa wanandoa ili kujua nini mwenzako anakihitaji, na ni nini kifanyike ili kila mmoja arizike, ni vyema muwe  wawazi kuelezana na kujadiliana.Msifichane, kwanini umfiche mwenzako, wakati nyie ni kitu kimoja,sema naye usione soo, ili mjenge ndoa ya upendo na amani.


Ni mimi: emu-three

2 comments :

Anonymous said...

humu leo kuna mafunzo mazuri sana ya ndoa..big up m3

Raj-uk

emu-three said...

Ni kweli Raj, tunajaribu kugusia mambo ambayo wengi wayazarau na mwisho wa siku inakula kwake. Tupo pamoja