Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, April 17, 2012

Hujafa Hujaumbika-22



‘Kesi hii imekaa vibaya kweli, kwasababu mumegusa sehemu isiyogusika,tamaa itawaponza, utajiri wa namna hiyo utawafikisha pabaya,nikuulize wewe unayejiita mtoto wa Msomali, kwanini hukufanya kama tulivyoahidiana, unafikiri hawa watu watakusaidia nini katika maisha yako,…’akaniuliza na kutilia kidogo halafu akasema;

‘Mara nyingi hawa matajiri wanakuthamini pale tu unapowafanyia kile kitakachowaingizia faidia na si vinginevyo….hawana urafiki wa kudumu, leo anakuchekea kesho huijui, atakutupa barabarani kama hakujui, ….’akaniambia Yule mwanadada mtaalamu wa mitandao, kumbe sio tu kuwa ni mtaalamu wa mitandao, lakini pia ni wakili wa kujitegemea.

‘Unjue mpendwa, hutaweza kunielewa, kwa lolote nitakalokuambia….kwa hali niliyo nayo…,labda ukutane na hii hali niliyonayo ndio unaweza kusema kitu…maana kitanda usichokilalia huwezi kujua kunguni wake…’nikaanza kujitetea.

‘Sizani kuwa kuna sababu ya muhimu ambayo mtu na akili zake anaweza kujiingiza akijua kuwa kuna hatari mbele ajipeleka kama mbwa anavyojipeleka kwa chatu. Hebu nikuulize unaweza kulamba asali baada ya kuambiwa imechanganywa na sumu..?’ akaniuliza huyo mwanadada, nikamwangali akwa makini, na yeye alikuwa kanikazia macho bila kupepesa,na nikajikuta napepesa mimi macho, nikaangali chini na kusema;

‘Huwezi,…hata kama ni tamu namna gani,huwezi….’nikasema huku nikijiuliza akilini ujasiri wa huyu mwanadada, kama anaweza akakuangali a machoni moja kwa moja bila kupepesa macho, aanonyesha kuwa ni mtu jasiri na anajiamini kupita kiasi au ni kwasababu ni wakili, moyoni nikasema, hataniweza nitahakikisha napambana naye.

‘Ndio maana nakuambia hakuna sababu kubwa itakayokufanya kujiingiza katika hatari ukiwa kweli una akili sawasawa,… hakuna sababu,labda uniambie kuna kitu kipo nyuma yake,na kitu hicho nadhani ndio hicho hicho kinachowaponza hata hawa waheshimiwa waliojiukuta wanafanya hata yale ambayo kama yasengeliwakuta wasingelikubali kuwa wangilifanya hayo, na chanzo chake ni kushindwa kuihimili tama ya kimwili….’akasema huyo mwanadada.

‘Mhh, nashindwa nikuambie nini, ndio maana nasema  kitanda usichokilalia huwezi kujua kunguni wake….lakini naamini haya yote yana mwisho wake,na kwa vile nimeshafulia nguo, sina budi kuyaoga haya maji…nitajitahidi kupambana kiume, ….mwenyewe hata bila ya msaada wa mtu, kuhakikisha nayamaliza haya matatizo yangu….’nikasema kwa kujipa moyo.

‘Ndio kosa kubwa ulilo nalo, ubinfsi, na mfumo dume…..sikulaumu sana, ila ninachokuambi ani kuwa peke yako hutaweza , huko ni kujidanganya, huko ni kujipa moyo kusiko na msingi, ujue wenzako wapo wengi wamekamilika kila idara, wamejiandaa kwa muda mrefu, ….na sio kiubabe, kutumia miguvu, hapana wenzako wanatumia akili, sio kiujunja-ujanja tu wa kuongea mdomoni, bali kwa utaalamu, kisheria na kisaikolojia…unasikia sana….’akasema huyo mwanadada.

‘Ili iweje….?’ Nikajikuta nauliza swali la kijinga.

‘Ili iweje…unanichekesha kweli, ….wewe mwenyewe umeamini kuwa wao watakutafutia kazi, au sio, ina maana wana uwezo wa kuwashawishi waajiri wakuchukue, waajiri ambao mwanzoni ulipoenda mwenyewe walikukataa…wao wanaweza kumfanya muheshimiwa akasalimu amri, na kutoa kiasi kikubwa cha pesa ambacho hakikuwa katika bajeti yake…halafu unauliza ili iweje, unaniuliza swali kama hilo…nikujibuje….?’Yule mwanadada akaniangalia kwa mshangao.

‘Lilikuwa sio swali kwako,ila nilikuwa najiuliza mwenyewe…’nikajitetea

‘Kwahiyo sasa umepata jibu...?’akaniuliza.

‘Unajua…mpendwa hujanisaidia katika hili linalonikabili,unachofanya hapa ni kuniogopesha tu,…nini lengo lako la kuja hapa, kunilaumu kuwa sijatekeleza hilo tulilokubaliana au umekuja kunisaidi kama wakili…?’ nikauliza.

‘Yote hayo yapo ndani ya uwezo wako, kwasababu tunaogopa hata kukuamini tena, maana wewe tuliona ni seehmu muhimu ya kuwanasa hawa watu,lakini bado hukutaka kushirikiana na sisi,inaonyesha una tamaa, tamaa ya kazi, ….sawa kazi ungelipata, lakini je ingekuwa ndi mwisho wa yote hayo…’akasema huyo mwanadada.

‘Kwanini….isiwe ndio mwisho, ulishawahi kukaa bila kazi ukaona jinsi gani unavyozaraulika, unavyodhalilika…?’ nikamuuliza.

‘Tatzi lako hujajiamini…ndugu yangu, ina maana unafurahia hiyo hali ….hujijui kuwa wewe ni mtumwa…..wewe unatumiwa kwa ajili ya kuwatajirisha wenzako,na kujiweka hatarini…unawajua hawa watu vyema, wanakujali kama utakuwa ni faida kwao, wakigundua kuwa wewe ni mzigo kwao,….watakumaliza bila huruma…?’ akaniuliza.

‘Kwa hivi sasa siogopi, hata kama wanataka kuniua waniue tu…mimi nina fadia gani tena, nimeshawekwa uchi mbele ya wakwe..mbele ya watu ninaowaheshimu, sina maana tena….iliyobakia ni kutembea uchi tu mitaani…kama punguani ’nikasema huku nikionyesha uso wa huzuni.

‘Mwanzoni nilikuwambi wewe ni mwanaume au sio….hukujiuliza kwanini nimesema hivyo…sio kwamba nyie wanaume mna ujasiri sana wa kupambana na hatari…sio kwamba ndio maana wanakutumia kama dume la mbegu, …hapana, ila niachotaka kukuambia hapa ni kuwa wakati mwingine sisi wanawake tunakuwa na ujasiri zaidi yenu …..Je wewe unalikataa hilo,au hujajua kuwa mfumo dume, unawakweza hata pale msipostahili kukwezwa….? Akaniangalia machoni.

‘Inategemea,…huo ujasiri ni wa kitu gani, lakini mume ni mume tu…na mke ni mke tu…kutoakana n hilo unalopambana nalo….’nikasema huku nikiwaza hiyo  kauli ya huyo mwanadada.

‘Mimi hapa ni mwanamke, na nipo tayari kukabiliana a hilo kundi….licha ya kuwa najua hatari iliyopombele yetu, ni kama kujiingiza ndani ya mdomo wa mamba, ili ukaukate ulimi wake….wewe unaweza kufanya hivyo,…?’ akaniuliza na kuniangalia machoni.

‘Kwanini nisieweze kama inawezekana….’nikasema kwa kujiamini,maana hapo unatetea udume wako, hata kama haiwezekani inabidi ukubali tu, kufa na tai shingoni.

‘Nakuona umeshasita,…kama unaweza kwanini tulikuagiza mengine, umefanya mengine….huoni ulivyoukana udume wako,…sisi tunataka kuleta mageuzi, kwasababu athari kubwa ni kwetu sisi wakina mama na watoto, nyie mnatumiwa kama chambo tu, hamjali familia, hamjali athari kwasababu nyie ni madume…..’akasema huyo mwanadada.

‘Lakini huyo …anyeendeleza haya ni mwanamke….’nikajitetea.

‘Tuyaache hayo,….maana naona hujanielewa,bado kichwa chako kimetawaliwa na mfumo dume, tafakari haya kwa makini na angalia athari zake, kwako na kwa vizazi vijavyo,…..Nakuomba ujue kuwa mbele yako kuna kesi, na kesi hii kama itafuta sheria bila kupindishwa, utakuwa hatarini, …lakini najua kundi hilo litakusaidia na huenda ukaonekana huna hatia, kama kawaida yao, ila safari hii hatutakubali,hata kama utajiua…’akasema na kuangalia saa yake.

‘Kwanini nijiue…sasa kwahiyo..?’nikauliza.
‘Kwahiyo ni akili kichwani mwako,..je upo na sisi…ufe kiume,  au bado upo nakundi lako ukaendelee kuishi kama mtumwa…hilo nakuachia wewe mwenyewe ulitafakari….’akasema Yule mwanadada na kutaka kundoka, na baadaye akasema;

‘Sisi kwa hivi sasa tuna ushahidi wote tunaouhitaji, na itafika muda tutakuhitaji wewe kama shahidi…na hapo hutakuwa na ujanja tena, na tunachogopa ni kuwa ikifikia hatua hiyo, huenda ukasimama mahakamami mara moja na baada ya hapo tunaweza tusikuone tena…..’akasema huyo mwanadada.

‘Kwa vipi..?’  nikauliza

‘Kwa vipi, …kama tungelijua ni kwa vipi, ingesaidia sana, lakini wengi tuliwashauri hivyo, na pale walipokubali kuwa watashirikiana na sisi, sijui ni kwanini, hawakuweza kusimama mahakamani mara ya pili yake…..….’akasema huyo mwanadada.

‘Walifanya nini….?’nikauliza

‘Walijiua….’akasema huku akionyesha uso wa kutafakari na kunifanya na mimi niwe mwenye mawazo mengi kichwani, nikijiuliza kwanini watu wafikie hatua hiyo,na mara huyi mwanadada akaangalia saa yake, na kabla sijauliza swali akainuka na kuondoka na alipofika mlango akasema;

‘Wewe ni mwanaume au sio…? ‘ akauliza na kuniangalia machoni. Na mimi nikamwangalia kwa makini halafu nikatingisha kichwa kukubali.

‘Basi pambana kiume,….’akatabasamu na kuondoka.


‘Mume wangu usijali,  wakili wetu keshafanya vitu vyake, unachotakiwa wewe ni kutokujibu maswali yoyote utakayoulizwa na askari au mtu  mwingine yoyote pasipo na wakili wetu…unanielewa ninalokuambia..?’akaniambia mke wangu.

‘Nimekuelewa,…lakini nina maswali nataka kukuuliza…’nikasema

‘Maswali mengine hayana msingi hapa, kama ni kuhusu hiyo kesi yako utamuuliza wakili wetu, lakini kama ni maswala ya nyumbani,au sijui ya nini,…ya kazi, huu sio muda wake….utafanyaje kazi na wakati umeshikiliwa huku,…..cha muhimu wekeza fikira zako katika kukabiliana na hawa watu,maana inavyoonekana safari hii wanajaribu kupenya kweney ukuta wetu,..nawasikitikia kwani hawajui ndani kuna nini..’akasema mke wangu.

‘Wakina nani hawo….?’nikauliza.

‘Kuna makundi mawili, moja ni hawo wanaojiita serikali, hawa htunajua jinsi gani ya kufanya, lakini kuna kundi jingine limeibuka, eti watetezi wa haki za akina mama na watoto…wao wanajifanya wanajua sana, ngoja tuwaone, …wanadai eti huyo mke wa muheshimiwa, kauwawa, wakati mazingira yote yanaonyesha kafa kwa mshituka wa moyo, ….’ Akatulia na kuniangalia kwa makini.

‘Ndivyo ilivyokuwa lakini…..’nikasema, na bila kujali akaendelea kuongea

‘Na wamefikia kusema eti, kutokana na hicho kifo cha mke wa muheshimiwa ndio maana hata muheshimiwa mwenyewe kapatwa na kiharusi, …na sasa hivi hawezi hata kuongea…’akasema mke wangu.

‘Kwani huo si ndio ukweli wa hilo, ….na kwanini haya yote….?’nikauliza

‘Ndio maana nakuambia utulize kichwa chako,na mambo yote muachie wakili, ukianza kuropoka, utaozea jela, …..na usipende kuuliza uliza ….kwanini, kwanini….ukijua kwanini ndio utafanya nini…’akasema mke wangu.

‘Hivi mimi mnanionaje kuwa sijasoma, kuwa sijui kuongea kuwa…yaani mnanvyonifanya mimi ni kama zezeta tu, kila kitu nafanyiwa au kuelekezwa tu fanya hivi, usifanye hivi….mnanifanya kama mtoto au mtu asiye na akili,kwanini nisijue nini kinachoendelea, kwanini mnanifanyia hivyo….’ Nikakunja uso kwa hasira huku nimemkazia machoo mke wangu.

‘Hasira hasara…..’akasema huku akitabasamu.

‘Hasira hasara,…..tutaona, …sasa nikuambie ukweli, mambo yamefika kikomo… sasa nimeshindwa kuvumilia, hamuwezi mkanifanya mimi chombo chenu cha….’nikasema kwahasira na kablasijamaliza, mke wangu akaniwekea kidole chake mdomoni.

‘Kama umeshindwa kuvumilia, njia ni rahisi, nitakuleeta tindikali,…..unakunywa mwenyewe….’akasema mke wangu huku akiniangalia machoni.

‘Sikiliza wewe mwanamke, mimi sio hawo waheshimiwa, unajua kwanini wanafikia hapo, kwasababu wameweekza huko, wanaogopa kuumbuka,…mimi naogopa nini…nitakosa nini….usinitishe,na kama ni kunywa hiyo tindikilai utakunywa wewe….’nikasema huku moyoni nikiwa na wasiwasi.

‘Unajifanya jasiri sana,mume wangu unajua nakupenda sana, naogopa hicho unachojiringia nacho…mimi sitaweza kukutetea ikifika muda huo,…na hata hivyo kama nilivyosikia, huenda …’akatulia na kuangalia nje.

‘Huenda nini…sema usinitishe kabisa…’nikasema.

‘Wameshachoka na wewe, na wanasema ukiendelea kuwepo unaweza ukawa kikwazo…’akasema mke wangu akwia na wasiwasi.

‘Kwahiyo….?’ Nikauliza.

‘Nisikilize kwa makini,….sikiliza nikupe ushauri wa bure….wewe usisumbue kichwa chako bure kwa hivi sasa, wapo watu wanalipwa pesa nyingi kwa mambo hayo, wanajua nini wanachokifanya, wewe hutaweza kufanya lolote, ila kama umechoka na maisha, sikukatazi, ingawaje nakupenda sana, na ni wewe peke yake ambaye niliona tunaweza kuishi na kuwa na familia yetu,….’akasema huku akiangalai pembeni.

‘Familia yetu…nimechoka na lugha yako hiyo ya hadaa….sikuamini tena, nikuambie kitu,….wewe umetumwa kunimaliza na kufikia malengo yenu, sizani kama hayo unayoongea yanatoka moyoni,  ..na kama hayo ni mapenzi ni yenu sio mapenzi halisi…’nikasema huku nikimwangalia Kimwana.

‘Jamani….ndio uansema hivyo….hivi jiulize nani angelikubebe katika hiyo hali kama sio mapenzi…kuna wanauem wangapi, lakini nimekuja kukuchagua wewe…kwalipi bora…kaam sio kwamba nakupenda, tatizo lenu wanume mkiambiwa mnapendwa mnaringa…’akasemamke kwangu nakuniangalia machoni.

‘Hebu tuacheni na hizo hadaa,  mimi nitafanya hicho msichokitaka, na tutaona nini mwisho wake, tindikali sinywi, na wala sumu gani,labda mninywishe wka nguvu….’nikasema huku nikiwa na wasiwasi.

‘Wewe….jifanye unajau sana….usifikiri hata mimi napenda kuishi haya maisha ….kama kungelikua na njia ya kuyakwepa ningelishayakwepa zamani, lakini sina ujanja, niliingia kilaini sana nikijua hapa nitaukata, lakini…haya nikasema ngoja niachane nao, mungu wangu…najuta kwanini siku ili niliongea hivyo, ….’nakasimama na machozi yakawa yanaonekana machoni.

‘Ilikuwaje….?’ Nikamuuliza kwa wasiwasi.
‘Siwezi kukuambai kwa sasa, ila ninaloweza kukuambia ni kuwa hakuna njia,…. njia ni moja tu ambayo ni rahisi,…ambayo wengi waliamua kuitumia, hatunao tena duniani, marafiki zangu wapendwa,….’akasema huku akiniangalia usoni huku machozi yakiwa yametanda kwenye mboni za macho.

‘Ni wewe..lakini mimi siogopi hilo, kufa ni kufa tu…hata kama upo humo au haupo, ipo siku utakufa tu..sasa kwanini ufe kwa aibu, kwanini usife ukiwa unatetea haki…..’nikasema kwa ujasiri.

‘Bravo…haya jitahidi ufe kwa ujasiri…unaijua tindikali wewe…ukimwagiwa machoni itakuwaje, ..au ukitiliwa kwenye kinywaji ukainywa itakuwaje huko tumboni…ni mifano tu midogo…wenyewe hawatumii nguvu sana,..wewe mwenyewe utachukua hiyo gilasi yenye tindikali au chochote utakunywa,...'akasema huku akionyeshea kwa mikono.

Nikamwangalia anavyoonyeshea kwa mikono yake, na  kukunja uso, na sikusema kitu kwa muda na yeye akaendelea kusema;

'Au utajimwagia hiyo tindikali mwenyewe usoni …..bila hata mtu kukufanyia hivyo…hiyo ni mifano ya kujimaliza mwenyewe, lakini sio lazima wafanye hivyo moja kwa moja, na sio lazima tndikali kama tindikali….’ Akasema huku akionyesha uso wa kutahayari.

‘Hivi wewe unanionaje mimi, yaani, una akili zako timamu, uchukue tindikali..ujimwagie..sikuelewi…? ’ nikauliza

‘Mimi mweneywe nilikuwa najiuliza hivyo,…lakini zipo njia nyingine,…huoni hawo wanaushikwa na kiharusi,….walipenda iwe hivyo…mwili wa binadamu upo upo tu, lakini kuna mambo ya kiingizwa kichwani,yakayumbisha akili yako, huchukui muda, …..nimeona wengi  na mengi, ndio maana nasema ukiingia kwenye hili kundi ni rahisi tu, lakini kutoka, njia ni moja tu,…..’akasema mke wangu nikamkatiza kwa kusema.

‘Kujiua…mumejidanganya …sio mimi…’nikajipa moyo.

‘Zipo njia nyingi, lakini muda utasema…kwani watu wanye rongo nguvu, maaskari, wakubwa, waheshimiwa…unafikiri wao hawana ubavu, wana kila njia ya kufanya , lakini waliasalimu amri….wenzako wanakujau kuliko unavyojijua wewe…ndio fani yao…wamjiandaa….naona wakili huyo anakuja , usije ukaropoka haya tuliyokuwa tukiongea….uwe mwangalifu na kauli yako…’akaniambi mke wangu, na wakili akaja na mke wagu akaondoka.

‘Kesi imekaa vibaya kidogo, natakiwa kupamba na mawakili wawili...sio hoja maana sio mra ya kwanza. Ila mengi yanategemea ushirikiano wako na mimi,  ….kinachotakiwa ni kuwa mkweli,muwazi na mwepesi wa kuelekezwa….na cha mhimu kwa sasa, usiongee na mtu yoyote kuhusu hii kesi kama mimi sipo….tatizoo ni kuwa huna jinsi ila ukubaliane na hilo nitakalokuambia….’akasema wakili

‘Lipi muheshimiwa, maana umesema niwe mkweli,na bado unanipa masharti…’nikasema na huyo wakili aakniangalia sana machoni akasema.

‘Unataka kufia jela, au kubakia uraiani….?’akaniuliza.

‘Hiyo ni kazi yako…’nikasema

‘Ndio maana nasema unatakiwa ukubaliane na huo ukweli, ….ushirikiane na mimi kwa kusema ukweli…na hilo litaweza kukusaidia vinginevyo…mtajuana wenyewe, mimi kazi yangu nikuangalia ukweli na atakavyo mteja wangu….’akasema huku akifungua `briefcase’ yake.

‘Haya ngoja tuanze kuongea jinsi ilivyo kuwa,….’akasema wakili huku akifungua makabrasha yake, na mimi hapo nikajua kweli sasa nimekamatika, ….

WAZO LA LEO: Ni vyema tukubali kuwa kama binadamu hatuwezi kujua kila kila kitu, wewe kama unajua hili mwenzako anajua lile cha muhimu ni kushirikiana.
 Na pia tukubali kuwa kama binadamu kila mmoja ana udhaifu wake,  hatuwezi sote tukawa wakamilifu, kwani unapomnyoshea mwenzako kidole, ukumbuke vidole vitatu vinakunyoshea wewe...

Ni mimi: emu-three

No comments :