Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, April 10, 2012

Hujafa hujaumbika-19



Niligeuza kichwa huku na kule sikuona mwanaume hata mmoja katika mkutano huu nilioalikwa nikashangaa na ilifikia hatua kutaka kutoka nje, lakini nikatulia kimiya,...nikikumbuka ujumbe nilioupata toka kwa mwanadada mmoja, mwana dada huyu ndiye yule niliyekutana naye kule hotelini akiwa mmoja wa wahudumu.

‘Nina ujumbe wako,...nataka kukupa...’aliniambia.

‘Hata mimi nilikuja hapa nikiwa na maongezi na wewe...kuna kitu nataka kukuuliza....’nikamwambia.

‘Hapana, nakushauri kwanza angalia huo ujumbe na fuatilia....ni muhimu sana , ukitoka huko utakuja uniambie nini unachotaka kuniambia,...kama nilivyokuambia unatakiwa uwe na tahadhari na..na mke...wako, kwani upo ndani ya mtego mkubwa....’akaniambia huku akiangalia huku na kule.

‘Mbona hunifafanulii, kila tukikutana wewe unanipa mambo juu, juu, na ...mengi nimeshaanza kukutana nayo, inaonekana unajau mengi kuhusu mke wangu sijui na nani....’nikamwambia akacheka na kusema;

‘Sijui mengi kuhusu mkeo,...tafadhali ondoka..nipo kazini...’akasema na kuondoka, mimi nilichukua chakula nilichotumwa na bosi wangu nikarudi kazini, ...siku hizi bosi wangu kabadilika kabisa, alikuwa hakai ofisini kama kawaida yake, au kuniita ita ndani, ....na wala hakutaka kuongea na mimi, akija ananituma chakula halafu anaondoka zake, nikashangaa kuna nini kikubwa kinaendeela, na siku hiyo nikaamua kumuuliza;

‘Vipi bosi mbona umebadilika sio kama ile mara ya kwanza...?’ nikauliza.

‘Nyie mitu mibaya sana...sitaki hata kuongea na wewe, na ingelikuwa naweza ningelishafukuza kazi weye, lakini.....ipo siku ..ondoka nenda fanya kazi ako...’akaniambia na mimi sikubisha nikaondoka kufanya kazi yangu, huku nikiwaza,....kuna nini kimetokea au ndio ile simu imeshafiksha yale yaliyofanyika siku ile....

Pamoja na hili , nimekuwa nikitumishwa katika maswalamwengine, ambayo sikuyapenda, nimejikuta kama changudoa wakiume,..wakutumwa, nikutane na mwanamke huyu na yule na yanayotakiwa kufanywa nai yale yale niliyomfanyia bosi wangu, na hili likafikia hatua nikaona sio vyema, ni bora tuongee vyema na mkewangu, kwangu sasa imetosha, sasa basi...lakini kuna huu ujumbe natakiwa kuufuatilia....

*******
‘Hiki ni kikao maalumu, ni kikao cha ushauri, kikao cha kukumbushana na kuelimishana...hiki ni kikao maalumu cha akina mama,...cha kupeana majukumu, mpo tayari...’akasema mwendesha kikao...na wakati watu wanajibii kuwa wapo tayari,  akanigeukia kuniangalia mimi;

‘Ingawaje kuna mwanababa mmoja hapa tumemwalika hapa kwasababu maalumu...tunakuomba mwanababa usijisikie vibaya tukitumia hiyo lugha ya kikao maalumu cha akina mama,  wewe hapa umealikwa kwa kazi maalumu, ili ujue umuhimu wa akina mama na majukumu yao. Na baadaye tutakuwa na  mazungumzo maalumu na wewe...

Hapo kidogo nikaingiwa na hamu ya kukaa kumbe nimealikwa kama mgeni maalum, sijui hayo mazungumzo maalumu ni mazungumzo kwasababu gani. Nilikumbuka ule ujumbe ulikuwa na masharti kuwa nisiende na simu au saa, na tulipofika hapo mlangoni tulikaguliwa na vyombo maalumu.

‘Kama mnavyojua sisi akina mama ndio walezi, tunaolea watoto na waume wetu, hilo ni jukumu letu na kama yupo mwanamama hajui hilo,bas hajakamilika kuitwa mwanamama. Hebu jiulize kwanini hakuna kitchen party ya wanaume...hilo ni jambo dogo tu, wengine watadai ni kwasababu ya kukusanya vyombo vya jikoni...ukiwaza hivyo utakuwa na ufinyu wa kutafakari, na wengine wakifika pale wanaleta mzahamzaah tu, hasa wale ambao hata ndoa hawaijui, mnatia aibu na vitendo vichafu, kwasababu waankuwepo hapo hawajui nini wanatakiwa wakifanye...’akasema huyo kiongozi au mwenyekiti.

‘Mimi sio msemaji hapa tuna wataalamu mbali mbali, kuna wataalamu kama madocta, kuna wataalamu wa haki za akina mama ,jinsia na watoto, kuna kungwi , na kuna wataalamu maalumu kwa hili tunalotaka kuliongelea hapa,na kabla ya kuongea kwanza kuna kuhojiana, hilo tumelianza kimiya kimiya...kujuana na kuelezana nini hasa kilichotuleta hapa nakama unakubaliana nalo, au vipi , na ukikubaliana unakula kiapo..ndio maana ya kuandikishana palemlangoni..’akasema.

‘Sasa na mkaribisha mama kungwi huyu tunataka atukumbushe kidogo majukumu ya kina mama ambayo yameshahaulika na matokeao yake ndiyo haya, kunatokea watu wengine, ambao mimi naweza kuwaita ni mawakala wa shetani, ..wengine wataona natumia lugha chafu, lakini sioni neno jingine la kuwaita hawa watu. ...’akasema huku akingalia huku na kule.

‘Kama mtu unajifunza jambo sio kwa nia njema utaitwa nani, ....wewe unajifunza mambo ya ndoa, lakini sio kwa ajili ya ndoa, ni kwa ajili ya kuharibu ndoa za watu, wewe tutakuita nani,kama mtu unadiriki kufanya uchafu ili uje uwachafue wenzako wewe tutakuita nani....lugha ya moja kwa moja wewe ni shetani tu...’wakina mama waliopo hapo wakashangalia,

‘Karibu sana mtaalamu wa mambo ya ndoa....tupashe kidogo kungwi wangu, maana mimi nimefundwa na huyu mama, ndio maana ndoa yangu inapeta, tuna raha , tuna Baraka, hatuna shida...’akamkaribisha mama mmoja ambaye lipoinuka ukumbi mzima ukalipuka kwa shangwe, hapo ndipo nikajua kuwa kumbe wapo wakina mama wengi kwa upnde wa juu, hapo nilipokuwa nimekaa nilikuwa siwaoni vyema.

‘Nashukuru sana mwenyekiti, na nikianza moja kwa moja naweza kusema, wakina mama tumechangia kwa kiasi kikubwa kuvunjika kwa ndoa zetu, hata kama nyingine hazijavunjika, ila zipo mashanini, watu hawan raha, kila siku kulalamika,mume wang hivi...kimpandakimeshuka....ndoazetu hazipo kama zilivyotakiwa ziwe , ...ndoa ilitakiwa iwe sehemu ya raha, kuliwazana, kupendana, kuheshimiana, ...lakini je hiyo ipo kweli, siri ya mtungi aijua kata...tumekwepa majukumu yetu....’akasema na kufungua makabrasha yake.

‘Sisi ndio walenzi wa watoto na waume zetu ndio kauli mbiu ya kikao hiki, anzia kuchukua maana halisi ya ulezi utaona kuwa muhusika mkuu ni mwanamke, mume ni kiongozi tu wa familia, katibu ni mwanamke,.... lakini huyo kiongozi hataiweza kazi yake kama hakulelewa vyema, ...hakutayarishwa vyema, ndio mama unaona katika picha za video yupo muhusika mkuu, lakini hataiweza ile kazi yake kama hakuyatarishwa, hakuongozwa vyema....sisi ndio watayarishaji, sio ndio walezi,sisi ndio familia ...’akatulia kidogo.

*******

Mimi nikiwa nimetulia kimiya huku huyo mwanamama akiongea, nilijaribu kuwaza mambo yanavyokwenda hadi hapo nilipofikia,ilishafikia mahali niamue kufanya unyama niishie zangu kijijini, au hata nikifungwa basi, maana sina uhuru tena, nimewekwa kwenye sehemu ambayo kazi yangu nikuamrishwa tu,leo nenda hapa utakutana na mama mmoja, fanya hivi na vile, baadaye unaweza kusikia hiyo mwanamama  kadondoka na kuzimia au ana haha huku na kule kutafuta pesa...

Jana tu nilijikuta na wakati mgumu, nilipokamatishwa na mama mmoja wa muheshimwa, nilipotoka hapo, yule mama alinipigia simu akaniambia kuwa akikutana na mama ama zake ama zangu, nilijaribu kujitetea lakini alikata simu,....kwa hali kama hiyo nikawa natembea kimashaka sijui itakuwaje baadaye licha ya kuthibitishiwa kuwa ninalindwa kila mahali ninapokwenda.

‘Kila unapokwenda hakikisha una simu yako , na hii saa ivae mahali popote kwa usalama wako,kama ukiwa kwenye hatari ni rahisi sana kujulikana na kuokolewa mara moja...’aliniambia mke wangu. Lakini leo sikuja na saa wala hiyo simu, nikifuata maagizo niliyoambiwa. Mwanzoni nipopata huo ujumbe nilizania isije ikawa ni mtego wa hawo watu wenye hasira na mimi.

Mawazo yakarudi kikaoni tena kumsikiliza huyo mwanamama, maana alikuwa akiongea vitu vizito...nikamsikiliza kidogo;

‘Imefikia hatua sasa tunadai usawa,....hebu tuulize usawa ni upi tunaodai, usawa wa kuwa sana na wanaume,..au usawa wakukwepa majukumu yetu kama wanawake, au usawa upi huo tunaodai, wengi hatujui hilo,  tunafuata mkumbo tu, ...tunadai tu usawa, tukae kwenye viti tukunje nne, wanaume nao waingie jikoni,au sio, tukae chini wanaume nao wafanye yale wanawake wanaofanya, inawezekana kweli,...haya waambieni wakabebe mimba....sio ndio usawa huo, wengi hatujui huo uswa unaotafutwa ni usawa wakitu gani...mnaujua huoi usawa?’ akauliza na baadhi ya wanwake wakasema;

‘Tunaujua na unawezekana....’halafu kikafuatia kicheko.

‘Hiyo ndio kauli ya wengi inawezekana, na matokeo yetu ndio hayo yanayotokea sasa, kuwa tunakwepa hata yale majukumu ya asili, ..majukumu ambayo mungu katuumba nayo, ambayo tukiyafanya sisi kama wanawake, yanaleta tija ba Baraka, lakini tukiwaachia wanaume, uwezekano wa kuwa kama ipasavyo ni nusu kwa nusu...matokea nyumba zinabakia kama mahema na mashetani wanakuja kujipenyeza na hata kujenga nyumba....’akasema na kutulia.

‘Ndugu zanguni, ndoa inajengwa na mke na mume, na asilimia kubwa ya ndani ya ndoa, inashikiliwa na mwanamke, ukitaka kujua hilo jaribu kuchunguza majukumu yote ya ndani utaona muhusika mkuu ni mwanamke,...ndio maana nasema mwanamke ndiye mlezi, ....sio ulezi kwa watoto tu, bali hata malezi kwa waume zetu...’akasema na wanawake wengine wakaguna.

‘Mimi nina miaka thelathini na mume wangu, watu wanasema labda nimempa mume wangu limbwata, kwa jinsi gani mume wangu anavyokuwa karibu na mimi...kweli ninakiri kuwa nimempa limbwata....’akasema na watu wakacheka.

‘Lakini sio limbwata la dawa zenu za kiganguzi, ...ni limbwata la mapenzi..najua nini maana ya ndoa, najua nini maana ya malezi ya familia, ....najua jinsi gani kama mwanamke natakiwe niwe...sivyo hivyo mnavyojua nyie......’watu wakacheka.

‘Msicheke,hili ni somo lenye uzoefu, na lengo langu ni kuwafunza wanawake wenzangu kutokana na uchunguzi wangu huo ambao nimeufanya kimatendo, na kutokana na hayo nimegundua mengi kuwa kama sisi wanawake tutafuata na kutimiza majukumu yetu ya asili, sio tu kuwa ndoa zetu zitadumu, bali pia baraka za kipato zitaongezeka mara dufu  

'Niwaambie ukweli, mnaniona mimi na mume wangu tuna hali nzuri, ....lakini wakati tunaoana, tulikuwa hohe hahe, tukianza maisha,...lakini kwasababu kila mmoja lijua nini maana ya ndoa, tukajituma, kila mmoja akitimiza majukumu yanayomstahili.....sasa wengi wanatuonea gele...limbwata limbwata..hakuna limbwata hapa ni mapenzi ya asili....’akaendelea kuelezea.

********

Mimi nikiwa namsikiliza huyo mwanamana, nusu ya mawazo yangu yalikuwa mbali, na hapo, nikamuwaza mke wangu wa kwanza maana taarifa nilizopata ni kuwa yeye sasa ni mwalimu, na wamerudi toka Kenya, huko alikuwa akisoma, na wameamua rasmi kurudi kijijini yeye na mume wake mume wake akiwa kafungua maduka ya jumla, na mke akiwa mwalimu, ...

Pamoja na kazi zao hizo, wamejichanganya kwenye jamii, ili kusaidia kuendeleza kijiji, na mke wangu huyo wa kwanza ni mwenyekiti wa akina mama,na moja ya majukumu yake ni kuwasaidia akina mama kujiajiri...

Nikiwa nawaza haya, taswira ya aliyekuwa mke wangu huyo wa kwanza ikiniangalia kwa huzuni,taswira hiyo ilikuwa siku ile ya mwisho wakati tunaagana,..kwakweli nilipofika hapo nilijikuta nikijilaumu, nilijiona mtu asiye na bahati, ...kwani sasa hivi najiuliza nini hasa nilichokuwa nikikitafuta kwa mke ....awe wa namna gani...na mara nikasikia yule mwanamama akionga kama vile anajibu swali hilo kama vile nimemuuliza yeye.

‘Wanaume wengi wanatafuta mke mwema, ...je sisi tumejiandaa vipi ili tuwe katika hilo kundi la wake wema, ...hebu tujiulize sifa hizo tunazo...sifa za mke mwema tunazo, kama hatuna kwanini hatuzitafuti, kwani zina gharama gani....na cha ajabu mtu huenda wakati anaolewa alikuwa nazo... kabla hajolewa, akishaolewa zinachujuka...na matokeoa yake nyumba zake zinapwaya, wanakuja hawa wajamaa wanatuchulia waume zetu, kwa uzembe wetu wenyewe....halafu unatumia ubabe...unatafuta miti shamba....hakuna haja ya miti shamba, rudieni uasili wetu...’watu wakashangailia.

‘Huyu mke mwema ana sifa gani...’nikajiuliza, anatakiwa awe mzuri sawa, anatakiwa awe na adabu sawa, anatakiwa awe mchapakazi sawa...na je kama vyote hivyo anavyo lakini hajui ....hajui.....nikawa nawaza hapo hajui nini ...nikiwa namlenga mke wangu wa kwanza...mapenzi...'akatulia kidogo.

Kwa hali niliyo nayo nikajikuta nikiwaza na hata kujiuliza, kwani mapenzi ni nini, ....hivi ni mapenzi gani hayo anayotakiwa mke au mume awe nayo, mapenzi ya kisasa, ya ukweli na uwazi....mara nikamsikia huyu mama akisema;

‘Hakuna mapenzi ya kisasa na ya kizamani,...mapenzi yalikuwepo toka enzi za Adamu,...ni yale yale...tatizo ni kuwa tunaolewa lakini hatujui tufanye nini kwa waume zetu, tunasubiri kama magogo, ....mume akisogeze huku akuinue huku, wewe umekaa tu kama gogo....umelala kama gogo...’hapo wanawake wakacheka na kushangilia..

‘Msicheke, hiyo ni aibu, ...na aninapozungumzia kulala kama gogo, sio kule kulala kwa kulala,ichukulieni hiyo kimapana, nazungumzia majukumu yote ya ndoa, ....’akasema na wanawake waliokuwepo hapo wakicheka wakatulia kusikiliza na hata mimi nikatulia kumsikiliza.

‘Mapenzi, ni tafsiri ndefu, inatoka mbali, hadi hitimisho lake ni kule kunapoitwa ..mmmh, la ndoa....ambapo wengi ndipo tunapogota, na kuzania kuwa huko ndipo penye maana ya mapenzi, ....mapenzi hayaanzii huko , yanaanzia mbali, toka nje,....hadi ndani, na baadaye ndio tunafika huko..hata huko kwenyewe, tumeshindwa....jamani mna nini nyie kizazi....?.’akasema kama anaguna huku akiniangalia mimi, naona kuwepo kwangu hapo kumezuia hata ile kauli aliyotaka kuongea, kuikatisha,  na mimi nikacheka.

‘Jamani hilo lilikuwa ni jukumu letu, tumelikwepa, hivi huko kwenye `kitchen party’ tunaambiwa nini...tunafika pale kwa nia ya kuupeana zawadi tu....najua hapo hapatoshi, muda ni mdogo sana hapo wakufundwa, na ukizingatia hapo mwanawali aanwazia zawadi gani atapewa, hawazii ni majukumu gani anayokwenda kuyabeba, maana hayajui.....atayajuaje wakati wameokotana barabarani,hata a hadi zedi ya ndoa haijui, anachojua ni kuwa kapata mume.

‘Ni muhimu sana mtu kabla hujaolewa ukajua nini maana ya ndoa, nini nahitajika kufanya, ...kwasababu wewe ndiye ulitakiwa kumuonyesha mume wako afanye nini, ...lakini tumekuwa magogo...tuliiii...umelele kama gogo, tuliii...haya wajanja wameibuka na mbinu mpya, wanatuibia, wanatuletea mgonjwa...wamgundua kuwa nyie mlioolewa, hamjui nini maana ya ndoa, na wakati wao wanahitji kuolewa,sasa ujanja ni kupata au ni kuwahi...wanawawahi mkiwa bado mumelala.....

‘Tunatakiwa tubadilike,...amukeni wanawake na hili halitafanikwia kama sisi wenyewe hatutajituma, tukaondokana na hiyo kasumba ya kutaka kujilinganisha na mwanaume, halafu tunasahau majukumu yetu ya asili....kwanza hata kama umeolewa, jaribu kutafuta muda wako, soma, siku hizi vipo vijarida, vitabu magazeti na hata mitandao, someni, jifunze jinsi gani ya kuijenga ndoa yenye furaha,..jamani mnataka tuongee lugha gani...’akasemahuyu mama kwa jaziba.

‘Jifunzeni,  jisni gani ya kulea watoto, jinsi gani ya kulea waume zetu....hilo halihitaji shule ya kukaa darasani, lakini tuonavyo sasa,..pengine kuna umuhimu huo, maana tumewazarau mashangazi, mabibi zetu ambao sasa tunawaita wachawi...ajabu kabisa,.....labda tuanzishe hizo shule....kama walivyokuwa wakifanya wazee wetu,....ziwe za kisasa kidogo, badala ya msituni, tuingie darasani,....’akasema na kuonesha picha ya wanawake wapo darasani.

‘Tunaona aibu kupelewa msituni,...au kwa bibi, au kwa shangazi, ....maana zamani kabla ya kuwa ndani ya ndoa, ulihitajika kwenda unyango, kulikuwa na majina mengi yaliyotumika, lakini lengo lilikuwa ni kumfunda mke ili ajue majukumu yake ya ndoa, sasa hiyo haipo, tunakwenda na wakati, huku wakati umetuacha mbali ajabu, maana wenzetu wajanja, wale ambao ndoa imewashidna ndio hawo wanapiga parapanda la haki sawa...haya haki sawa, sijui kwa vipi...

‘Tunadai haki, ..sawa si sawa, ....?’ akauliza pale alipona watu wanaguna, ...na hapo watu wakasema `sawa, haki sawa kwa wote...’

‘Ni haki yenu kudai hiyo haki,...lakini tunapodai haki , tudai haki za msingi,sio haki za asili yetu, tusidai kile tusichokijua...maana sasa tunataka wafanyaakzi wa ndani, bustanini, na hata kitandani....’akasema an watu wakacheka.

‘Ndivyo ilivyo, tumekuwa wavivu hata kitandani...tunatia aibu....maana kila siku watu wanapiga mayowe, mume katembea na mfanyaazi wa ndani, ..kwasababu ya uvivu wetu, ....uzembe wetu, tukubali susikubali huo ni uzemeb wetu...’akasemana kuangalia huku na kule.

‘Uzembe wetu ndio uliotufanya  kuwaachia wafanyakazi wa ndani hadi yale majukumu ya msingi ambayo yanafikia hadi hawo wafanyakazi wa ndani wanatembea na waume zetu, yeye ale wapi, kila mtu anakula ofisini kwake...ukiona mfanyakazi wako  wa ndani katembea na mume wako,jiulze mara mbili kosa lipo wapi....ujilaumu wewe mwenyewe kwasababu umeshindwa majukumu yako....ukiona mume wako anatemeba nje, jiulize wewe mwenyewe kosa lipo wapi....maana umeshindwa majukumu yako....!

 ‘Namaliza kwa kusema...sawa tudai haki zetu tupambane na mfumo dume, ...kama nilivyoona hiyo fulana aliyovaa mwenzetu hapa, kuwa haki sawa kwa wanaume na wanawake,...lakini tuwe makini na hicho tunachokidai, kwanza tuwe tumetimiza wajibu wetu, ...je mnatimiza wajibu wenu....?’ akauliza na wanawake wakasema;

 `Ndioooooooo’

‘Sasa kwanini waume zenu wanatembea na wafanyaakzi wa ndani, kwanini waume zenu wanatembea na mahawara, uliwahi kukaa chini ukatafakari, ukafanyia uchunguzi wa kisayansi, au unachukulia jaziba, na kulipiza kisasi, na wewe unakwenda kutembea na mtunza bustani,...ndivyo tulivyo, hasira hasara, badala ya kujenga tunabomoa, tunajiau wenyewe....?’ akauliza swali ambalo hakutaka jibu, kwani aliendelea kuongea kwa haraka ili kwenda na muda....

‘Nimewauliza hilo swali, je ni kwanini, inakuwa hivyo....?’ akauliza tena.

‘Ni tamaaaa zaaaoooh wanaume....’wakasema kwa sauti.

‘Je mna uhakika na hilo mnalolisema, kuwa ni tamaa zao ...mumefanya utafiti wa kisayansi mkaona kuwa kweli sababu ni tama zao....?’ akauliza na watu wakawa kimiya.

‘Sikilizeni, ndugu zanguni, mimi nimefanya utafiti wa kisayansi, nimegundua kuwa asilimia kubwa tatizo lipo kwetu sisi wanawake, ndio wenye mataizo, najua wengi hawatakubaliana na mimi, lakini ndio ukweli ulivyo...ndio maana tumeamua wale ambao tumeligundua hili tuanze mchakato wa kufundishana hatua kwa hatua, na ikibidi tufungue shule,...’akasema huku watu wakiwa wametulia.

‘Ingelikuwa amri yangu, na hili linawezekana ni kuwa kabla mwanamke  hujaolewa ni lazima upitie hizo shule,apitie mafundisho, afundwe kiukweli...’ aliposema hivyo wanawake wengine wakaguna.

‘Hilo ndilo tatizo, kuwa hatutaki kujifunza, utakuwaje dakitari bila kwenda shule ya udakitari, utakuwaje mwananda bila kuisomea hiyo ndoa, mbona mnaizalilisha hii sehemu muhimu ya maisha yetu, ...kama hutaki , kama unajifanya unajua haya kaolewe, lakini ukiumwa an manyigu usipige ukulele....’watu wakacheka.

‘Tatizo ni kuwa tunataka na sisi tuwe kama wanaume,  sio mbaya..., lakini tujue kuwa hata siku moja wewe hutakuwa mwanaume, kama wewe umezaliwa kuwa mwanamke, ...usikwepe majukumu, usikimbie umbile lako, maana hata hao wanaojibadili ipo siku watajuta,...maana sisi ni wanadamu tu, ...leo tupo kesho tutarudi kwa huyo aliyetuumba, na ukiuliza nani alikuumba hivyo sijuii utakuwa na jibuu gani la kumjibu muumbaji....’akasema huyo mama.

‘Narudia tena kama kweli tunataka ndoa zetu zidumu tusikwepe  majukumu ambayo ni ya asili, aliyotujalia mwenyezi mungu, kiuzoefu wangu na utafiti wangu hayo majukumu ukimuachia mwanaume  ulezi wa familia hautatekelezwa kama inavyopasavyo, amini usiamini,...’akasema huku akifunga funga makabrsha yake kuonyesha kuwa anamalizia.

‘Majukumu ya asili  ni swala nyeti la wanawake, sisi ndio tuaoijua hiyo kazi, kulea watoto na kuwalea wanaume,tusikwepe haya majukumu jamani kwa masilahi ya familia zetu, kwa masilahi ya vizazi vijavyo na kwa baraka za riziki zetu...’akamalizia huyo mama na kuashangaliwa sana, halafu akaingia mwanamama mwingine,...huyu alivaa kabisa fulana imeandikwa `haki sawa kwa mwanaume na mwanamke, ...’ moyoni nikasema hapo kuna kazi, ....

Mimi akili ikawa inahama nusu nipo hapo nusu nipo nje nikiwazia matatizo yangu,...ni kijiuliza hivi hayo aliyoongea huyo mwanamama yameeleweka, ....hivi kweli sisi wanaume hatuji malezi, ....na mara akili yangu ikahama na kumwazia mke wangu,  nikijua kabisa huko sasa natufutwa, nitakuwa natafutwa na bosi, sijui nikikutana naye nitamwambia nini,....Bosi wangu.

*******

‘Umesema hujamuona tangu asubuhi na hakuwahi kukuagana kuwa anakwenda wapi, ....mbona siamini hayo maneno....’akasema na kumkodoleamacho Kimwana.

Kimwana alitulia kimiya akiwa nawasiwasi,kwani tangu asubuhi alipoachana na mume wake, hawajawasiliana naye na hata alipojaribi kumpigia simu ikawa haipatikani, na aalipoona hivyo alikwenda nyumbani, na huko hakumkuta..

‘Huyu mtu kaenda wapi, ..mbona ananiingiza kwenye matatizo...’akajikuta akiongea peke yake,alijua nini kitafuta kama mume wake huyu atakuwa kafanya kinyume na inavyotakiwa.

‘Akawasha chombo chake maalumu cha kumtafuta, na kilipowaka akakuta mwanga wake ni mkali zaidi kuonyesha kuwa kitu anachokitafuta kipo hapo hapo karibu, ...akafuatilia hadi akafika  kwenye kabati la nguo, na humo akaikuta simu ya mume wake ikiwa kwenye mfuko wa suruali, na saa...akavitoa na kuviangalia, simu ilikuwa imezimwa.

‘Huyu mtu kafanya nini...?’ akajiuliza. Vifaa vile aliambiwa asiachane navyo, kila anapokwenda, kwani ukiwa na hivyo vifaa unaonekana moja kwa moja katika mitambo yao, na wao walimwamia kuwa kuwa akiwa an hivyo vifaa atakuwa analindwa aili asije akazurika na maadui wanaomtafuta.

‘Hapa kuna jambo, huenda huyu mume wangu akgundua jambo, ndio maana kaamua kuviacha hivi vifaa,hata simu..hapana kuna jambo, sasa nitamtafutia wapi....?’ akajiuliza na wakati anahngaika mara simu ya mama ikaita.

‘Natakauje hapa na mumeo haraka...’sauti ya mama ikasema.

‘Mume wangu...ooh, shajarudi bado..’akajikuta akijiuma uma.

‘Ndio maana huku haonekani, alikuwa akzima simu yake, ..mtafute haraka uje naye, nakupa nusu saa uwe uemshafika hapa, na yeye...’sauti ya amri ikasema.

‘Haya, ngoja nimtafute...’akasema lakini hakujua amtafutie wapi.
Alijaribu kumtafuta kila mahali anapohisi kuwa anaweza kumpata, lakini hakufanikiwa, na baadaye akjipeka mwenyewe kwa mama.

‘Una maana gani kusema hivyo,...haonekani....sikusikii vyema, kwasabubu huyu tulikuambia ni mtu wako, halafu ni mumeo,...ndivyo nilivyowafundisha hivyo, ndio jinsi ya kuishi na mume hivyo, mume atoke bila kukuaga, ina maana mnaishi vipi,  na huyo mume wako au ...umekiuka yale niliyokufundisha kwasababu wewe ni bosi wake...wewe ni mke wake...kama unafanya jinsi mke anatakiwa kuishi na mumewe, hilo lisingelitokea kamwe...nieleze kuna tatizo gani..?’ Mama Docta akawa anongea kwa jaziba.

‘Hapana mimi sijakiuka kabisa miiko ya ndoa kama ulivyotufundisha,....ila naoana kuna jambo linaloendelea ambalo huenda silifahamu, kwasababu kaacha simu na ile saa, hii ni kuonyesha kuwa huenda keshagundua kuwa hivyo vifaa vinamuonyesha kila anapokwenda....’akajitetea mke wangu.

‘Hapo hujaniambia kitu, maana mimi nawajua wanaume ipasavyo,kama ungelifuatilia kama nilivyowafundisha huyo mwanaume asingelishawishika na kitu chochote, huenda umejifanya wewe ni kidume, na hili litakutokea puani...sitaki utani kwenye hii kazi,....’akagonga meza kwajaziba.

‘Unajua nyie mnafanya itani,  nimewekeza hela yangu nyingi sana, na hivi sasa ni muda wa kuirudisha, ...mimi nimetumia hela nyingi sana kuwafanya muonekane hapa mjini ...mnatamba mnaitwa wasichana warembo,..hamjui yote hiyo ni gharama, na nani wa kurudiha hiyo gharama kama sio waume zenu, leo hii unakwenda kinyume....sasa nakupa masaa mawili nataka huyu mtu apatikane...na akipatana nataka umlete hapa..kuna kazi muhimu sana...’akasema mama.

*********

‘Hebu niambie ulikuwa wapi mume wangu..?’ nikaulizwa kwa sauti ya kinamna, sauti ya kumnasa ndege tunduni, nikamtupia jicho mara moja na kuangalia pembeni, maana nilitarajia ile sauti ya ubosi, maana mke wangu ni bosi ...alishaniambai hilo, na kweli sehemu kubwa ya mambo yetu alikuwa yeye ndiye mweney amri, Mume kama huna pesa una usemi gani.

‘Nilitoka kidogo ....kupoteza mawazo, ....kuna jamaa yangu mmoja aliniita , huyo jamaa ni rafiki yangu mkubwa, nilishaongea naye kuhusu maswala ya kunitafutia kazi, na leo alivyoniita nilijua kapata kazi mahali, tumeongea wee, nikajisahau kabisa ..’nikasema uwongo.

‘Mume wangu unajua ukisema ukweli ninafahamu na ukisema uwongo ninafahamu pia, ndio tatizo la kusomea haya masomo ya hulka za binadamu, nilishakuambia katika shughuli zetu hizi, ilibidi niyasoem hayo masomo, ....’akasemahuku akiniangali machono moja kwa moja.

‘Hata hivyo usijali, mimi ninakuamini mume wangu, ...kwasababu nakupenda sana...fanya ufanyalo lakini usije ukadanganyika kunisaliti....maana ninavyokupenda sitafurahi nikikusa moja kwa moja...unajua hilo...’akasema mke wangu na  yale madoido yake akanifanya niwe katika dunia nyingine, lakini hata hivyo akilini mwangu nikajua kuna jambo linakuja. Sio bure ,ingelikuwa siku zile za mwanzo ningesema ni mahaba yake, lakini tangu alivyonitamkia kuwa yeye ni bosi wangu , nimekuwa nikijihami kwa kila jambo,ingawaje  imekuwa kama mbwa mbele ya chatu.

‘Sikiliza mume wangu, najua kabisa unavyojisikia, lakini yote ni mitahani ya misha, najua kabisa wewe ulitakiwa uwe kwenye ofisini yako , au umeajiriwa mahali, katika wadhifa wa meneja, au sio.....’akasema kama ananiuliza huku akifanya mambo yake. Nikuambie ukweli huyu dada alijua nini akifanye kwa wakati gani, na ni mjanja wa kughilibu akili, ....kwanii mimi hapo sikuwa najielewa,zaidi ya kumuona yeye ni kila kitu. Huku namuitikia kila kitu anachosema;

‘Kweli kabisa mke wangu, ....hivi kweli unanijali kiasi hicho, ....kama umeligundua hilo, nakushukuru sana, maana imefikia hatua naadhirika sana, unajua kuadhirika, hali iliyopo sasa naadhirika, katika maisha yangu sikutegemea kuwa ningelifanya haya niliyoyafanya...hata hvyo mke wangu mengi ni wewe unanikamatisha,...unajua mimi sipendi mambo hayo....sasa naogopa hata kukutana na wanzangu, na wakiniuliza upo wapi siku hizi inabidi niwadanganye...’nikasema.

‘Pole sana mume wangu, wakati mwingine nakufanya hivyo ili ufunuke macho na masikioa,..uijue dunie ilivyo, ....Sasa mume wangu wakati umefika, ...kuna sehemu nimeshakutafutia, utakuwa meneja....unasemaje.?’ akaniuliza na mimi nikashituka kwa hamasa.

‘Eti nini kazi, halafu niwe meneja....unasema kweli au unanitania...?’ nikauliza.

‘Toka lini nikakutania mume wangu, mimi nakupenda sana mume wangu ndio maana naishi na wewe kwa dhida na raha nikujua sasa itakuja,na najua sasa raha ndiyo hiyo ushindwe mwenyewe, .....unajua mume wangu, kufanikiwa kwako ndio mafanikio yangu pia,kwahiyo usiku na mchana nakuhangaiia wewe ili na wewe ufanikiwe...’akasema na kuniangalia mchoni.

‘Nchi hii ukiijulia huwezi kufa njaa, nchi hii ukiIjulia unaweza ukafanya lolote lile...na hilo limafanikiwa , ila kama ujuavyo nchi hii ili ufanikiwe jambo, lazime upenyeze rupia....na ni pesa nyingi kidogo, maana unakwenda kuwa meneja, ambapo utalipwa mshahara mkubwa, gari na gharama zake, utapewa nyumba...kama sio nyumba,utalipwa pesa sawa na kulipia nyumba....sasa ili kulifanikisha hilo, kuna jambo dogo linahitajika kufanyika...’akasema na hapo nikajua ni yale yale.

‘Jambo gani tena hilo wakati umeshasema kazi imepatikana, au ndio danganay toto...’nikasema kwa hasira.

‘Sikiliza nimeshakuambia ili upate kitu, ni lazima ufanye kitu, na hali ilivyo wanasema penye uzia ufanye nini,..penyeze rupia! Sio rahisi rahisi tu kama unavyozania, utatemeba mpaka umalize ofisi zote usipate kitu, lakini ukiijulia hii dunia, hupati shida...’akasema na kutabasamu.

‘Lakini mimi nikaona ili uondokane na huu utumwa,..utumwa wa kuwa tegemezi, ni  lazima ufanya jambo kwa jasho lako mwenyewe...sitaki utafutiwe kazi na hapo hapo zile gharama za kuipata hiyo kazi pia ulipiwe....wewe uuna onaje, maana nimemwambia huyo mtu kuwa utalipa mwenyewe....’akanimabia.

‘Ningependa iwe hivyo, lakini kwa pesa gani, pesa ninayopata niya kuniwezesha kula tu...sasa huoni hapo unanitega, nitapaat wapi pesa za kulipia hiyo gharama na je ni kiasi gani,,,,?’ nikauliza.

‘Ina maana huniamini...mimi nimebuni njia ya kupata hizo pesa, unafanya kazi na alzima ulipwe kiasi kizuri, na kazi hiyo ni nyepesi tu, ...kuna kazi ndogo ambayo ukiifanikisha tunapata mshiko  mzuri, na mshiko huo utakuwezesha kumlipa huyo wakala ...kama ujuavyo, kila kitu lazima kiwe na wakala siku hizi, ...’akainuka pale alipokuwa amekaa huku na kusimama akasema’

‘Unajau wakala wanalipwa sawa  na mshahara wako wa hiyo kazi....ndio gharama zao....lakini pia kuna watu wengine wameingiahapo, na wao wanahitajika kulipwa, watu waliosuka huo mpango ili uingizwe kwenye hiyo ofisi kwani wewe kutokana na historia yako hakuna kampuni ingelikukubali ....’akasema.

Niliwaza mengi, ni kweli ofisi nyingi nilizokwenda kuombakazi kila inapofikia hatu ya kujielezea wananiambia nikasubiri nikirudi mara ya pili wanakuja na hoja kuwa baaada ya kuchunguz ahistoria ya kazi wameona hawanihitaji...nikiuliza historia yangu ina ubaya gani, wanasema hawana haja ya kuniambi, ila kama watanihitaji wataniita..na hapo imeshatoka...

Nilihangaika kila ofisi kuomba kazi mpaka nikakata tamaa na kusema huenda ofisi zote wameshawasilina kuhusu mimi, au kuna mtu ambaye kila anapoulizwa kutoa habari zangu huko nilipoanzia kufanya kazi ananipakazia ubaya..basi nikaona nikubali ukweli, na kujituma kwenye kazi za kuwa kibarua,...sasa leo naletewa habari kama hii, kuwa imepatikana kazi ambayo inaendana kabisa na kiwango cha elimu yangu,....nitafanya lolote ili niipate, nikasema moyoni...

WAZO LA LEO: Tukumbuke kuwa kila mtu ni marehemu mtarajiwa, na kila kifo hakikosi sababu, kwani sote ni mavumbi, tumetoka kwa udongo tutarudi kwa udongo. na kazi ya mungu haina makosa. Blog yenu hii inaungana na wengine kutoa mkono wa pole kwa familia, ya jirani yetu mwanablog mwenzetu, na muigizaji mashuhuri Marehemu Steven Kanumba, Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. AMIN


Ni mimi: emu-three

2 comments :

Yasinta Ngonyani said...

Darasa hili ni tamu mno kila nikiingia hapa natoka na maarifa kibao..Ahsante sana na kumbuka tupo Daima pamoja.

elisa said...

Yani huwa natamani hata weekend uwe unaupdate ,kutaka tu kujua nini kinaendelea. Kweli maisha ni safari,pia njiani kuna milima na mabonde.