Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, March 21, 2012

Hujafa hujaumbika-7




Pale nilipokuwa nimekaa kwenye kikao nilikuwa nikiwaza mengi,....’akaendelea rafiki yangu kunipa kisa chake, name nikatulia kumskiliza.

‘Mawazo yangu yalikuwa yanawaza hicho wazee wanachokijadili, nikawaza pia, je wazazi watanikubalia nimuoe bint Yatima, hata kama wazee wataamua iwe hivyo....na kama kweli wazazi watakazania msimamo wao huo nifanyeje,...Niliinama chinikama vile nasoma ile karatasi niliyokuwa nayo, lakini mawazo yangu hayakuwa yakiiiona ile karatasi.

‘Wakati mwingine nilijikuta nikiyasoma yale majina mawili ya mwanzo, nikifikiria nimchukue yupi kati ya hawo wawili kama wazazi watashikilia msimamo wao, lakini zile sura zao zilififia kabisa na mbele yangu nilikuwa nikimuona huyo binti, ...waliyezoea kumuita binti Yatima, ....na mara sura ikanijia na safari hii akawa kama inatoa machozi na kuwa kama inasema;

‘Naomba unisaidie,.... nakuomba uniokoe ....nitakufa kabla siku sio zangu...tafadhali, njoo nipo kwenye htarai, ukichelewa hutanikuta tena.....’nilipoona vile moyo ukaanza kwenda mbio, nakahisi kichwa kikiwanga, ...nikashika kichwa na hata kuziba masikio nisihisi ile sauti,lakini haikusaidia.

Niliangalia huku na kule, kama vile sipo mle ndani, ...nilipoona hali na hewa inaniwia nzito, nikainuka pale nilipokuwa nimekaa kwa haraka, nikajifanya kama vile nakwenda kujisaidia,....nilipofika nje nikajaribu kupata hewa, lakini hali yangu ilikuwa sio shwari, nikajiuliza kwanini najisikia hivyo.

‘Vipi mbona umetoka ghafla...’sauti ikanishitua karibu nidondoke kwa hiyo sauti, halafu nikajitahidi kujifanya kuwa hakuna tatizo.

‘Sio kitu mjomba....’nikasema na sauti liyotoka ilikuwa siyo ya kwangu kabisa.

‘Sio kitu wakati unaoenekana kuna kitu, na nakuona hali sio shwari unamuwaza binti Yatima nini, usijali utampata tu, wale wazee ni watu wa busara, watawashawishi wazazi wako watakubali tu...’akasema mjomba, ambaye nahisi naye aliamua kutoka nje, labda kunifuata mimi au alikuwa naye hajisikii vyema.

‘Mjomba wewe ni mtu wangu wa karibu, na kwa hili sitaki nikufiche jambo, ....Hali ninayosikia sasa hivi ina nipa ishara fulani, nahisi kama huyo binti Yatima hayupo salama...’nikasema

‘Kwanini unasema hivyo..?’ akauliza mjomba naye akianza kuingiwa na wasiwasi.

‘Mara nyingi ninapojisikia hivi, inakuwa ishara ya kutokea jambo fulani, na nimejisikia hivi nilipomuwaza huyu binti,....mjomba nahisi kuna jambo, tufanyeje mjomba...?’ nikasema na kugeuka kumwangalia mjomba usoni, ambaye kwa muda huo alionekana kunishangaa huku akionyesha uso wa mashaka.

‘Hakuna la kufanya kwa sasa, kwanza tupo kikaoni, na kikao kinakuhusu wewe, ukiondoka hapa unafikiri itakuwaje, na mimi ndio huyo najadiliwa, nikiondoka hapa wanaweza kusema nimekimbia, kwahiyo tumuachie mungu, atamlinda tu, kama alivyomlinda miaka yote....’akasema mjomba.

‘Mjomba nina uzoefu na hii hali, ....hali kama hii ikinitokea, kuna jambo, ....tutakuja kujijutia kwa hili, sikiliza mjomba, wewe tafuta njia ya kunilinda, ngoja mimi nikimbie huko nikaangalia ...’nikasema huku nikianza kuondoka.

‘Hapana sikiliza kwanza, tutamtuma mtu mwingine....’mjomba akasema, lakini mimi sikumskiliza...

Mjomba alitaka kunizuia lakini akaghairi na kusimama kwa muda, akiniangalia nikichukua baiskeli ya baba niliyomnunulia na kuanza kuondoka kwa mwendo wa kasi. Sikujali kuwa kuna watu wameniona nikiondoka, ...kwani kwa muda huo hisia zangu zote zilikuwa kuwahi huko ninapokwenda.

Nikiwa njiani mawazo yangu yalikuwa yakimuwaza huyu binti, je nitamkuata yupo salama,...kwaani kwa hali kama ile nilihisi kabisa kuna hatari, kuna jambo linatokea huko....sijui ni jambo gani, au ni hatari gani, lakini hisia ziliniashiria hivyo, je nitamkuta yupo salama ni majliwa ya mungu na nikamuomba mungu nimkute hivyo.

Ghafla nikajikuta nikiingia porini, baada ya kumkwepa mzee mmoja ambaye alikuwa akitembea katikati ya njia, kwekweli kutokana na mawazo sikumuona na yeye alionekana kuwa na mawazo mengi pia, kwasababu baiskeli ilikuwa karibu kumgonga, lakini hakuweza kushituka hadi nilipomkwepa na kupiga kengele.

‘Wewe vipo mzee, huoni, ...oooh, ..’ nikasema.

‘Samahani sana nilikuwa mbali, mawazo mengi.....’akasema Yule mzee, huku akiendelea na safari yake, na wala hakutaka kuniangalia, na mimi sikuhangaika kumtizama tena nikaannza kunyoga baiskeli yangu, nilipofika mbele kidogo, akili ikatulia na kuwaza, nikakumbuka, ....

‘Hivi yule si baba yake Binti Yatima, oooh, bahati nzuri hakunigundua....inaonekana ana mawazo mengi sana, au ndio kuna jambo limetokea huko nyumbani kwake ndio maana kachanganyikiwa....’nikasema na kutaka kusimamisha baiskeli nirudi nimuulize, lakini nikaona nitapoteza muda, nikaendelea na safari yangu.

*******

Nilifika nyumbani kwao Binti Yatima, ....kwanza nilisikia sauti ya kitu kama yowe la kuomba msaada na kwa sasa sauti ile ilikuwa ikififia, na hapo mwili mzima ukaanza kuniishia nguvu, nikasimamisha ile baiskeli na haraka nikaufikia mlango, nikausukuma, nikaona umefungwa kwa ndani.

Hapo nikashikwa na butwaa kidogo, na kusema moyoni nikawaza huenda wazazi hawa waliamua kumpiga huyu binti mpaka wakamuumiza na sasa wameamua kumfungia ndani , ndio maana wote wameamua kumfungia ndani.

Pale nje nikaona panga, sijui kwanini nililichukua, lakini niliona ni silaha kamakuna lolote inaweza kunisaida ndani, nakausogelea ula mlango na kuuangali kwa makini, nikajiuliza, nipige hodi kwanza au nifanyeje, nikasema hapana nikipiga hodi nitapoteze muda.

Nikahesabu moja mbili tatu, nikaupiga ule mlango kikumbo, na nilichosikia ni sauti ya msumari uliofungwa kwa ndani ukidondoka na mlango ukafunguka. Niliangaza macho na nikasikia sauti ya kama watu wanapigana chumba ambacho ni cha watoto, na huko ndipo anapolala binti Yatima na watoto.

Mara moja bila kusibiri nikajitosa ndani,....mungu wangu, moyo ulisimama kwa muda nikashikwa na butwaa, na kabla sijasema kitu nikainua panga...

**********

‘Wazazi wa kijana wetu, sisi wazee tumelifikiria hili kwa makini sana, na tumeifikiria na hoja yenu kwa makini sana, na tukajiweka sehemu yenu kama wazazi, ...lakini tnahisi kuna jambo jingine ambalo mnalijua , ambalo linawashinikiza ...tunaomba ushirikianao wenu, ili na sisi tujue kama lipo jambo, huenda na sisi tukabadili muelekeo wetu....’akasema Yule mzee wa busara, na alipofika hapo akatulia kidogo.

‘Ni vyema kwanza tukaliangalia hili swala kinamna ya kipekee sana, na hata kabla ya kulifikiria hili jambo kwa undani hebu tujaribu kummkumbuka mama mzazi wa huyu binti, amabye sasa ni marehemu, mola ailaze roho yake pema peponi, ...nafikiri wote mnamkumbuka na alivyokuwa akiishi na sisi, na zaidi ya hayo kama sikosei, alikuwa rafiki mkubwa wa mkeo hapa, au nimekosea...?’ akauliza mzee.

‘Nakumbuka sana, alikuwa rafiki yangu kipenzi na kifo chake kiliniuma sana, sitaweza kusahau, na mara kwa mara namuota...sijui kwanini... na nikikumbuka maongezi yake na mimi siku kabla ya kifo chake ninaishia kusononeka sana, ....siku hiyo tulikutana kisimani na tuliongea mengi na mwishoni aliniambi kuwa `hatarajii kuonana na mimi tena,....’

‘Kwanini alikuambia hivyo...?’ akauliza mzee akiwa na hamasa, ilionekana ni mara yake ya kwanza kusikia hayo maneno toka kwa huyo mama.

‘Sikumuuliza kwasababu kwasababu nakumbuka kauli hiyo aliitoa wakati tunaagana, tumeshabeba ndoo zetu na kila mmoja alikuwa akielekea njia yake,....’akasita kidogo kuongea, alafu kwa haraka akasema;

‘Hata hivyo kwa wanaomjua kauli kama hizo alizizoea kuzisema kwasababu ya hali aliyokuwa nayoo yeye na mume wake, na tetesi zilizokuwa zimezagaa kuhusu mume wake...na aliniambia kuwa alishatishiwa amani na huyo hawara aliyekuwa akimuibia mumewe....’ akaongea kwa huzuni, na akatulia na mzee alitaka kuuliza swali, lakini mama akaongezea maneno haya kwa haraka;

‘Ila kwa kweli, siku ile alionekana hana raha kabisa, kuliko siku zote na kauli yake nyingine ilisema..mmh, nashindwa hata kuisema maana mnanikumbusha mbali na kuniuliza naomba tusimuongelee sana....ni hayo tu mzee wangu’akanyamaza.

‘Iseme hiyo kauli yake,.... labda kwa kuisema inaweza ikasaidia , ikatusaidia na sisi hata kama sio kwa hili, lakini hata kwa baadaye....na pia inaweza kukusaidia na wewe kuondoka na jambo linalokukera....’akasema Yule mzee, na baba wa kijana ambaye alikuwa karibu ya mama akamkanyaga mguu kama ishara ya kumkanya jambo.

‘Tatizo ni kuwa nyie mnatafuta njia ya kumlazimisha mtoto wetu amuoe huyo binti, na sisi nafsi zetu zimeshamkataa, hamuonai kuwa mnatutendea sio halali....’akasema mama kwa haraka.

‘Kwahivi sasa unaweza kusema hivyo, lakini kiukweli tunalotaka kufanya hapa ni halali na ni kwa manufaa ya huyo binti na tuna imani kuwa ni heri kwa kijana wetu...hilo tumeliangalai sana kama wazee wenu mnaotuamini ...na wapo watu wamemchunguza sana huyo binti kiundani na wana uhakika kuwa hatutaokota garasa....na kijana wenu kampenda....’akasema huyo mzee.

‘Ina maana mumeshaamua hivyo kuwa kijana wetu amuoe huyo binti...?’ akauliza baba kwa hamaki.

‘Ndipo huko tulipokuwa tukielekea kusema hivyo, ila kauli yenu imesita kwasababu kwanza tunaithamini sana kauli yenu, ...lakini pia tulihitajii sababu ya msingi ya kauli yenu, ili itusaidie na sisi...’akasema huyo mzee.

‘Kauli yetu ya nini, wakati inavyoonekana mumeshaamua hivyo...’akasema baba kwa hasira.

‘Sijasema hivyo, nimesema kuwa kauli yetu itatoka pale tutakapopata hoja ya msingi kutoka kwenu, kwanini, ndio maanai tumewaita ili tulijadili kwa makini, na tukipata maoni yenu na sisi tutaoa ushauri wetu wa kwanini tumefikia huko, .....’akatulia na kumwangali baba wa kijana kwa makini.

‘Najua jinsi mnavyojisikia, najua jinsi gani mlivyo na hamasa mtoto wenu ampate binti asiye na dosari N hilo ni kwa kila mzazi, na ujue hapa sote tunasimama kama mzazi wa kijana wetu, hatutaki litokee baya,...lakini bado sisi tunajiuliza ni nini dosari za huyo binti mnayemkataa, ni kwasababau anaishi na huyo mama, au ni kwasababu ni yatima, au ni kwasababu gani...?’ akauliza huyo mzee.

‘Hilo la kwasababu ni yatima sio sahihi, hata sisi inatuumiza sana hiyo hali, lakini kikwazo kikubwa ni mama yake huyo,kwasababu kauli yake mwenyewe tulishaisikia kuwa kwa yoyote atakayemuoa, ajue atakula naye sahani moja, alishwahi kusema, kama ana uwezo kidogo, atahakikisha kuwa mali yote anaipata yeye...na mengine mengi ambayo sio muhimu, ila tunahisi mtoto wetu atakuwa haan amani na huyo mkwe wake....’akasema mama.

‘Na ujue akishaoa huko umeshaunganisha familia mbili, sasa tutaishije na huyo mama na tabia zake, na ukumbuke watoto au wajukuu zetu watakaopatikana hapo wana haki ya kwenda kwa huyo mama, hauoni kuwa wanaweza wakafunzwa visivyo....mumeliangalia hilo kwa marefu na mapana...’akasema baba.

‘Yote hayo tumeyaongela na tumeyaona, lakini sisi ni wazee wenu tumeishi muda mrafu na tumeona mengi, na hayo tumeshawahi kuyaona, na kiukweli huyo mwanamke tunamjua sana kuliko nyie manavyofikiria, na familia anayotoka huyo mwanamke inajulikana toka enzi za zamia, kuwa siyo nzuri, lakini tunahitajika kukiondoa kizazi chema mikononi mwa huyu mama ili asije akakiangamiza....’akasema Yule mzee.

‘Kwa kupitia mgongo wetu, au sio...?’akauliza mama huku akigeuka kama kuondoka.

‘Lazima tukubali hilo kuwa nyie mumejaliwa kuwa sehemu ya kukiokoa hicho kizazi, hebu niambie mama yake alikuambai kauli gani,maana hata mimi jana niliota kuwa kunakauli ulipewa na mama wa huyo mtoto lakini hujaitimiza....niliwaza sana, ingawaje ndoto haikusema jambo, imesema umepewa barua uifikishe kwa wahusika, lakini hujaifikisha, je ni barua gani hiyo....?’ akauliza huyo mzee.

‘Barua....?’ akauliza Yule mama na kugeuka kumwamgalia mumewe.

‘Hata kama sio barua lakini kuna jambo ambalo linafananana hilo, inaonekana uliambiwa ulifikishe mahala lakini hukuwahi kufanya hivyo, je alikuwambia nini....kumbuka jambo kama hilo ukilificha madhara yake yanaweza kuwa makubwa, utalichukulia kama kauli zake tu kama alivyozoea kusema, lakini kumbe ulikuwa ujumbe muhimu sana....’akasema mzee.

‘Aliniambia kuwa kama akifa anaomba mtoto wake asilelewe na huyo mama, kwani lishajua kuwa mumewe anaweza akamuoa huyo mwanamke,na akasema nimchukue huyo binti niishi naye....’akasema huyo mama na kuanza kulia.

‘Unaona sasa....mungu alivyo na hekima yake, ulitakiwa umchukua kama mtoto umlee, ukapuuzia, sasa inatakiwa umchukue kama mkwe mwana wako....utaikataa ha hiyo, je utakuwa na radhi, au utajisikiaje kama huyo binti atakuja kuzurika, au kufanyiwa uabaya kabla hujatimiza hayo uliyoambiwa na aliyekuwa rafiki yako, je huo ndio urafiki gani wa kutokukumbakana wakati wa shida....?’ akauliza mzee
Yule mama alimwangalia mumewe, huku machozi yakizidi kumtoka, na mumewe akatizama chini kwa huruma , halafu akasema;

‘Mimi ndiye niliyemkataza tangu awali,....kama mume nilijaribu kuangalia maisha ya family ana hali halisi, .....ndio mke wangu, alikuwa rafiki kipenzi wa marehemu, na alipofariki, mke wangu aliniambia hayo maneno ....’akatulia kwanza huku bado kaangalia chini.

‘Kipindi hicho kilikuwa kigumu, kila mtu alikuwa najua, njaa ilikithiri, maisha magumu, na kila mmoja alikuwa akihangaika na familia yake, lakini hilo silo hasa lililonifanya nismchukue huyo binti, tulishapanga tufanye hivyo, lakini haikuwa rahisi kama tunavyoongea hapa...’akatulia na safari hii akawa anamwangalia mkewe.

‘Huyo ni mtoto wa mtu, na huwezi kwenda na kusema mama yake alisema hivyo, na sisi hatukusema hivyo kuwa mama yake alisema hivyo, tulienda kisiasa na kumuomba baba wa mtoto. Mnamjua vyema yule mvuvi, .... alisema tumemdharau, kuwa hawezi kuishi na watoto, kuwa labda yeye ni mmasikini, na manen mengine mengi, na mwisho akasema yeye anaweza kumlea bint yake bila ya msaada wa mtu yoyote, ....’ akawageukia wazee.

‘Na hata alipooa, nikajaribu kumuelezea kuhusu matatizo ya mama wa akmbo nay a kuwa huyo ni mke ambaye hajazaa, huenda hataweza kuishi na huyo binti, tunamuomba tuishi naye, , mazungumzo yetu yaliishia pabaya, ikifia hatua ya kunitishia kuwa naingilia maisha yake....na kwasababu ya watu kusema kuwa huyo mke mpya ndiye aliyemuua mke wake wa kwanza, na mimi naoenekana naunga mkonoo kwahiyo urafiki wetu uuishe...tukawa hatuongei kabisa....’akacheka kicheko cha kebehi.

‘Hebu fikirieni, juhudi zote hizo, bado tunataka kumuingilia maisha yake...Aaah, mimi nikaona kwanini nihangaike, basi nikamshauri mke wangu tuachane na hilo, kwasababu tumejitahidi imeshindikana. Sasa ilipofikia hili, niliwaza sana, nikamshauri mke wangu asitoe hii kauli kwasababu italeta uzito na hata kumfanya kijana wetu asiwe na maamuzi yake mwenyewe, na pia hatuna maelewano mazuri na huyo jamaa,na yamezidi kuwa mabaya alipomuona huyo mke....’akasema baba.

‘ Hayo yote yalitokea, na binadamu ndivyo tulivyo, hata hivyo hatutakiwi kuchoka kusaidia pale inapobidi, tusijali hayo, kwasababu huenda sio yeye, huenda ni ibilisi anamchezea tu,....tumsaidie kwa hilo, na nia yetu hasa ni kumsaidia huyo binti, mimi naona sasa inawezekana, ...nahisi jamaa atakuwa kajifunza ukweli....’akasema Yule mzee huku akiwaangaliai wenzake, halafu akamgeukia baba wa kijana na kumuuliza;

‘Je unasemaje kwasasa, maana hayo so madogo, tusizani kuwa mtu akifa ndio keshaondoka moja kwa moja, anaweza akawa anatutembelea kinamana ambayo anaijua mungu mwenyewe, nab ado anaona binti yake yupo matesoni...ndio urafiki huo jamani....?’ akauliza na kumwangalia mama wa kijana.

‘Uliambiwa na kweli kumbe mlijitahidi kadri ya uwezo wenu, ikashindikana, sasa hilo tutajitahidi lifanikiwe,...na kauli ya rafiki mpendwa kwa mwenzake ni vyema sasa itekelezwe.. na lile ulilokuwa ukiliogopa kuwa huenda kutakuwa na ushawishi kwa kijana wako, ambao utafikia kumfanya kijana wetu akubaliane na huyo binti kwa ushawishi sio kwa upendo, ....nafikiri sasa umefutika, kampenda mwenyewe kwa ridhaa yake....’akasema mzee huku akimwangalia mama na kugeukakwa baba .

‘Ya kuwa kijana wako kamkubali, kapendezewa na huyo binti bila ya kishawishi chochote, ..binti wa watu ana sifa zote, mzuri, ana adabu...ni kwa vile maisha anayoishi nayo ni magumu tu....’akatulia kwanza akiwaza jambo, halafu akawageukia wanadnoa hawa wawili na kuuliza;

‘Au labda mimi navumisha, ....kama sio kweli, sema mwenyewe, ...labda kuna mtu katia shinikizo, la ushawishi kwa kijana wenu....kama yupo tuambieni,ili tubadili mawazo, sisi hatutaki kumlazimisha kijana wetu kama kweli hana mapenzi na huyo binti....lakini kama kamkubali na mambo kama hayo yalitolewa kwenu, mnahitaji kutimiza hayo....’akasema huyo mzee huku akiwaangalia wanandoa hawa kwa makini.

‘Sawa, lakini tunaomba jambo moja...kuwa kabla hatujafikia huko kwenye kuchumbia, wazee wakaongee na hiyo familia wahakikishe kuwa huyo mama, anafuta kauli zake chafu alizowahi kutamka na ya kuwa hataweza kuingilia maisha ya kijana wetu, ...vinginevyo kunaweza kukazuka mabalaa, na mtafaruku baadaye, tukaanza kunyosheana vidole....’akasema baba na mama akakubali kwa kichwa huku akimwangalia mumewe kwa macho ya kushukuru, kwani mapaka hapo alijiona kama kamsaliti mumewe.

‘Hilo tutalishughulikia, na ...tukitoka hapa tutatuma ujumbe wa wazee kukutana na familia ya huyo binti, kikeni kwao na kiumeni kwao, ....tunafanya hivi kwasabbu kubwa mbili, kwanza kikeni kwao ili kupata uungwaji mkono na pia kwa vile huko tunakukubali sana, ni familia tunayoiheshimu na wao najua watatupa uzito mkubwa...’akasema huku akionyesha kurizika na kazi yao kubwa walioifanya.

‘Na kwasababu ni jambo la haraka tutatuma ujumbe mwingine ambao kazi yake ni kufuata utaratibu wa kawaida kwenda kwa wazazi wa huyo binti,kujitambulisha....tunajua kuna pingamizi linaweza kutokea kwa huyo mama, lakini kwenye wazee hakuharibiki neno, tunajua jinsi gani ya kukabiliana na pingamizi kama hzio, hilo tuachieni.

Mara wakasikia yowe kwa mbali....yowe lililoashiria hatari, na watu wote wakasimama na wengine kuanza kufuatilia huko yowe lilipotokea, .....

‘Kuna nini tena huko....’ wazee wakauliza huku wakiinuka kwenye viti vyao....

NB Ni nini kimetokea jamani, hata mimi najiuliza, tusubiri sehemu ijayo

WAZO LA LEO: Moyo ukipenda umependa, hata chongo utaita kengeza. Hata madoa ya uchafu utayaita maua.

Ni mimi: emu-three

3 comments :

Rachel Siwa said...

Hahahahahaaa ndugu wa mimi leo umeniacha hoi na wazo; hata madoa ya uchafu utayaita maua, nimeipenda hii,Nafurahi kukuona unaendelea vyema Ndugu yangu,Pamoja sana.

Yasinta Ngonyani said...

Kisa hiki ni kisa ambacho kinaamsha fikra za watu sana... Kimenikumbusha mbali kimewahi kutokea na nimewahi kushuhudia ...mtu unasoma mpaka unajistukia chozi linatoka la furaha au la uchungu .....labda niendelee kwanza kusoma sehemu ijayo na nitaweza kusema ...

emuthree said...

Kweli ndugu wa mimi ukipenda unakuwa kipofu,....unaambiwa hapo kuna shimo angalia wewe unapinga unasema sio shimo, ni kabonde kadogo tu, mara tii...unbakia kulalama...ndio kidunia wa mimi.
Dada Yasinta, hata mimi ninayekiandika kuna wakati hisia za hata kutoa machozi zinanipata,na wakati mwingine, naona nipunguze kidogo,ili watu wasije wakajisahau na kulia maofisini..ndivyo ilivyo kihalisia.
Tupo pamoja nashukuruni sana kwa kunipa moyo tupo pamoja daima