Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, March 15, 2012

Hujafa Hujaumbika-4
‘Wewe ni nani unakuja kumsumbua binti yangu....?’ lilikuwa swali la kwanza kutoka kwa huyo mama na huku kashika kiuno kuonyesha kuwa anataka shari. Alikuwa kanisogelea huku anahema kama mtu aliyekuwa akikimbia, ikiwa na hasira.

Nilimuagalia yule mama nikashangaa, kwani alikuwa tofauti na akina mama wa huku, licha ya unene wake,lakini alivyojiweka, ni tofauti kabisa, nywele zake alivyoziweka kama mzungu,....na alivyovaa aliashiria kuwa yeye labda aliwahi kuishi mjini, au ndio anataka kuiga mambo ya mjini au ndio tusema ni nani vile....nikabaki nimeduwaa kwanza.

‘Shikamoo mama, ...’ kwanza nikasalimia lakini sikujibiwa nilikuwa naangaliwa tu, kuonyesha kuwa alikuwa akisubiri jibu la swali lake, nami nikaona isiwe shida nikaanza kumuelezea kuwa mimi ni nani na lengo langu;

‘Mama mimi sikuja kumsumbua binti yako, nilipita kuja kukusalimia,maana siku nyingi nilikuwa sipo hapa, nikaona niwapitia majirani mmoja mmoja...’nikasema.

Kwanza macho yalianza kumeta meta, halafu uso uliokuwa umejaa makunyazi ya hasira, ukaanza kujifungua , na sura ya kawaida ya kike ikarejea,na moyoni nikasema, kumbe naye ana sura nzuri. Aliniangali juu chini,halafu akatizama nilivyolowana kwenye suruali yangu,akataka kusema kitu, lakini kabla hajakisema akageuka kumwangalia binti yake aliyekuwa akihangaika huku na kule kwa pilika pilika za nyumbani, na alionyesha dhahiri kuogopa maana mama alimuona akiongea na mimi,hana cha kudanganya.

‘Wewe ni mtoto wa nani sikumbuki kukuona hapa kijijini...?’ akauliza bado akinitizama kwa mshangao,na ilionyesha dhahiri kuwa hasira zilianza kumpungua. Akajaribu kubasamu,huku akiendelea kunikagua kwa macho, ...

‘Mimi ni mtoto wa Mzee Msomali,...nilikuw nasoma nje ya nchi...sasa ndio nimerejea karibuni na.....’nikasema na kabla sijamaliza, mama akanisogelea huku akifunua macho kwa bashasha karibu anikumbatie , lakini aliponikaribia akasimama na kugeuka kumtizama binti yake ambaye naye alikuwa kuduwaa kidogo kutuangalia, na alipoona mama yake kageuka kumwagalia , akawa kama kaona kitu gani, kwani alishituka karibu kudondoka na akakimbilia ndani.

‘Ndio wewe kumbe, umebadilika kweli, uliondoka hapa ukiwa mtooto....sasa umekuwa na kuwa zinga la `handsome’,umeacha ule utundu wako, ehe....’ akanisogelea na kuanza kunichunguza usoni kifuani akashuka chini...akasogeza mkono wake kwenye sehemu zangu za siri...nikashituka na kuruka nyuma, nay eye akacheka halafu akageuka kumwangalia binti yake ambaye kwa muda ule alikuwa anatoka mlangoni.

`Usiogope....unasikia.....halafu ehe, hebu niambie maana nimesikia kuwa ulikuwa Ulaya ukisoma, ooh, my God, umebadilika , umekuwa kama mzungu, lakini naona sijui ulianguka kwenye maji, ...na hivi visima vyetu bwana,pole sana, karibu ndani, nataka tuongee, nataka unipe habari zote za Ulaya, maana nikizijua watanitambua kwenye vikao vyetu...’akasema huku akinishika mkono na kuvutia ndani.

Huyo mama ni bonge na mkono wake ulikuwa na nguvu, maana alivyonishika na jinsi alivyokuwa akinivuta nilikuwa kama mtoto ....nilikuwa kama nakokotwa na sikuwa na jinsi ila kumfuata nyuma.

Tulipofika mlangoni huku akiwa kanishikilia, akaingia kwa haraka, na mimi nilikuwa naangali nje watu wasije wakaniona jinsi huyo mama alivyonishika kama mtoto wake, ....nikiwa sina jinsi ila kumfuatili ahuku mara nyingi natizama nyuma, na wakati tunaingia mlangoni, kumbe yule binti wake alikuwa anatoka na ungo ukiwa na mahindi ndani yake,...

Yule binti alikuwa abdo anaogopa, na kwa vile hakujua kuwa tunaingia pamoja na mama yake,akawa kampisha mama yake, huku kashikilia ule ungo wa mahindi na mama yake alipopita bile kumgusa,akakurupuka mbio kutoka nje, kwa muda ule hakuwa ameniona mimi kuwa name nilikuwa nafuatia nyumakuingia ndani,nafikiri mawazo yake yalikuwa kwa mama yake tu , na ghaflaakaniona, akawakama kaduwaa, na tukajikuta tukigongana tena, na yale mahindi yakamwagika kidogo, kilichofuta hapo sikuamini, ..

Mama alikuwa kaingia ndani na aligeuka ili kunikaribisha, akaona yale mahindi yamemwagika chini,sio mengi sana,....Yule mama alikurupuka toka na ndani akaja mbio na kumshika yule binti masikioni akamvuta juu, juu, na kwa vile ni mama kibonge, aliweza kumuinua yule binti juu kama kitoto, hebu fikiria wewe mtu akuinue juu juu kwa kutumia masikio yako utajisiaje, na sijui alikuwa kajisahau kuwa mimi nipo kwani alipogeuka na kuniangalia akashituka na kujifanya hakufanya kitu..

‘Wewe binti umeniuzi kweli,kwanini unamwaga haya mahindi, unajua thamani yake wewe....aaah’ akageuka na tulipokutanisha uso akaona haya na kujifanya kutabasamu.

‘Samahani mgeni, maana mtoto huyo ni mtukutu ajabu, hasikii, nimejaribu kumweka sawa ili baadaye aweze kuishi na mume atakayebahatika kumuoa, lakini haelekei,sijui ataolewa na nani, na ukizingatia kaishia darasa la saba...mbumbumbu wa kutupwa, sijui ..kama mama yake...aah, nimechoka, unajua kuchoka, basi mama kwa mtoto huyu nimechoka..’akasema na kugeuka kumwangalia yule binti kwa hasira.

Kitu cha ajabu nilichoona ni kuwa huyu binti licha ya kufanyiwa hivyo, hakukimbia, alikuwa kasimama ,kainama chini, kama vile anasubiri kusulubiwa zaidi, nilimuonea huruma, nikataka kumwambia akimbie, maana huyo mama anaweza akamuumiza, ....lakini alikuwa aktulia kainamachini... nikamtizama huku machozi yakilenga lenga.

‘Lakini mama hayo mahindi nimemwaga mimi, maana hakujua kuwa tunaingia tukagongana naye kwa bahati mbaya, kwahiyo kama wakulaumiwa ni mimi sio yeye...’nikasema huku nikionyesha sauti ya hasira kidogo.

‘Usimtetee kabisa huyu binti, usiwe kama hawa watu wa hapa, wamezoea kunisema mimi kuhusu huyu mtoto, eti namtesa, eti na mnyanyasa, kama ningelikuwa smpendi, ningelimchukua huko alipokuwa, na kuamua aje tukae naye,mama yake alikufa akabakia hana mtu wa kumlea,hata bibi yake alipomchukua hakuwa na hata chakula cha kumlisha mimi nikajitolea kuishi naye, napigika kwa ajili yake, naongea mpaka koo linakauka....lakini nani atakushukuru kama sio lawama...’akasema huku akimwangalia yule binti ambaye alikuwa bado kasimama pale pale kainama....

‘Hebu niondokee hapa,nataka kuongea na msomi...angalia ulivyonyata....huoni hata aibu mbele ya mgeni...nisikuone hapa mapaka nikuite...’akasema na hapo yule binti akatoka mbio kukimbilia nje.
Kwakeli sikuweza kuvumilia niliona nimtolee uvivu huyu mama nikamwambia;

‘Mama huyu mtoto kama ulivyosema ni yatima,hana mama,licha ya kuwa ana baba , lakini katika hali kama hiyo utakuwa ukimuongezea unyonge na ukiwa, huyu anatakiwa alelewe vyema,ili asijisikie mnyonge,unavyomtendea hivyo atajiskia vibaya na moyoni atakuwa akisononeka kuwa kwa vile mama hayupo duniani...nashauri hivi...’kabla sijasema akanisogelea na kusimamambele yangu akasema;

‘We achana naye hebu niambie, maana wazungu nasikia wanajua mapenzi.....’ akanisogelea lakini kwa muda huo nilikuwa nikimwangalia yule binti kwa kupitia mlangoni, nilimuona akiwa kasimama kashika msikio yake akilia, nahisi alikuwa akisikia maumivu bado.
Na yeye akataka kuangalia natizama nini nje, na alipomuona yule binti nje, akausukuma mlango kwa nguvu, ukajifunga na kujibamiza kwa sauti,hata nyumba ikatikiska,akasema;

‘Unamwangalia huyo chokoraa,...hahitaji kabisa kuonewa huruma huyo,namjua mimi mwenyewe, ukimuonea huruma na kumdekeza ataharibika,....hamjui kabisa kuwalea watoto wa namna hiyo,mimi ni mwalimu wamachokoraa...’akasema na kunisogelea na kuwa karibu na mimi hata kuhema kwake kulikuwa usoni kwangu, akawa kasimama sambamba na mimi, akaniangalia usoni, halafu akafanya jambo la ajabu, akawa kama ananishika shika kinamna ambayo sikujua ana malengo gani.

Nikasogea nyuma huku nikiwa nimeshikwa na mshangao,sikuamini kuwa mama kamahuyu anaweza kunifanyia vituko vya namna hii, nikakumbuka Ulaya, kuwa kulikuwa na akina mama wazee wenye tabia kama hizi, lakini kwa huku kwetu ni nadra sana kwa mama kama huyu kufanya hivyo. Na aliponiona nikihangaika kwakutahayari akacheka na kusema;

‘Wewe umetokaUlaya bwana usijifanye hujui mambo haya,huko nasikia mama mkwe , mama mzazi, watoto wanaweza wakashikana na kubusiana bila kujali...,mbona wewe unaniogopa, au aulikuwa Ulaya ipi,nataka kujua jinsi wanavyo..mmh,... hebu sogea huku bwana....’akanisogelea na bila kujijua akawa kanishikilia kama kunikumbatia.

Rafiki yangu, mimi damu inachemka kweli,lakini kwa muda kama huyo na mama kama huyo damu iliganda, nilitamani nimzabe kibao, lakini nikamstahi,nikajaribu kujinasua katika kifua chake,.....lakini ilikuwa kama mtoto anamsukama mama yake akiwa kifuani kabebwa.

Ujue mama huyo ni pandikizi, kwahiyo alivyonishika mimi , sikuwa na uwezo wa kufurukuta, usije ukafikiri kwa sababu ya tabia niliyokuambia kuwa damu yangu inachemka, ukazania nilijileegza makusudi ili anifanyie analotaka, hapana....na bahati nzuri aliingia mtoto wake mdogo na kutibua hicho alichokuwa akitaka kukifanya. Nami kwa haraka nikatoka mle ndani na kukimbilia nje,na hapo nikakutana na yule binti akiwa anafuta futa machozi, nikamwangalia na kusema;

‘Usijali hayo yana mwisho na nitahakikisha kuwa huteseki tena....jipe moyo na ujiamini...’nikamwambia na kusubiri yule mama atoke nimuage,... alichelewa kidogo ndani na baadaye akatoka huku kafunga khanga moja...na ulemwili, ile khanga ilikuwa ikimuacha sehemu nyingine wazi...nikashangaa,...maana huku kijijini,wanawake wanajisitiri sana, ...nikageuka kumwangalia yule binti, lakini yeye hakuwa akituangalia alikuwa kihangaika huku na kule kwa kazi za nyumbani.

‘Amakweli umenishangaza,...hebu twende ndani mara moja...’akasema, na mimi nikamkatalia na kudai kuwa mjomba wangu yupo hapo njiania ananisubiri.

‘Sawa leo umeshinda wewe, lakini lazima tukutane, lini utakuja....?’ akaniuliza kama vile ananilazimisha.

‘Kesho niweza kuja nina zawadi yako ntaka kukupa, lakini kwa msharti kuwa ....’nikasema aliposikia zawadi akaruka kwa furaha na kusema;

‘Sema lolote unalotaka kutoka kwangu nitakupa, mimi ni mzungu bwana, tofauti ni kuwa nimeolewa na mtu asiyejua mapenzi ya kizungu,mimi nitahakikisha..’kabla hajamaliza akamtizama yule binti yake ambaye alikuwa kasimama kidogo akiduwaa, kwani ile khanga ya yule mama,ilikuwa imefunuka karibu kuwa uchi, na alivyomuona yule mama akimwangalia alishituka karibu kudondoka.

‘Sharti langu ni kuwa nataka huyu binti abadilike,....muone alivyo, anatia huruma sana,kwa umri kama wake ni msicha mkubwa, lakini kwa hali aliyo nayo, kukonda, anaonekana kama mtoto wa shule...unajua wazungu wanapenda sana wenzao, kama akija mzungu akamuona huyu binti alivyo atakushangaa sana, ukijiita wewe ni mzungu, mlishe vizuri, mvalishe vyema...na muonee huruma, chukulia kama angelikuwa binti yako, halafu afanyiwe hivyo ungelifurahi...kwahiyo zawadi yakokesho lakini nimkute binti kapendeza,sawa.....?’ nikasema na kumwangalia.

Aligeuka akamwangalia yule binti, nafikiri alimwangalia kwa jicho baya kwani yule binti alikimbilia ndani, na alipohakikisha kuwa kaondoka , akanisogelea, akaniangalia kwa jicho la ukali akasema;

‘Sikiliza sio kwa vile wewe umesoma sana sio kwasababu upo vipi ndio uniingilie maisha yangu,mimi najua nini ninachokifanya, huwezi kunifundisha kulea , wewe ni mtoto mdogo sana, sasa sikiliza ...’akanisogelea na kuanza mchezo wake, bila kujali kuwa tupo nje,...

Nilijaribu kujinasua lakini alikuwa kanishika kwa nguvu,na mara nikasikia sauti ya mtu ikikohoa kwa nyuma yangu, nilipogeuka, nilihisi mwili mzima ukinywea na kabla sijasema kitu yule mama akasema;

‘Huyu kijana hajaacha tabia yake ya uhuni,unataka hata kunibaka mimi,huoni kuwa mimi ni sawa na mama yako....huna adabu nyama mkubwa wewe....akanisukuma, na mimi nikadondoka kama gunia ,halafu akamkimbilia mumewe....

Je nini kilifuata, tuzidi kuwepo;

WAZO LA LEO: Ukiiona shari ubora wake ni kuiepuke mapema,...usijitie matatani kama haina ulazima,kama walivyosema wahenga ni bora nusu ya shari kuliko shari kamili.


Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Sehemu hii imenichekesha kweli, imenikumbusha mbali, yupo mama mmoja namjua huko kijijini kwetu ana tabia hiyo...Mkuu nakupa heko, wewe mkali!