Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, March 14, 2012

Hujafa Hujaumbika-3



Hapa anaishi binti mmoja, huyu binti ana kila sifa ya mke mwema, na kama ingelikuwa mimi enzi zangu ningemuoa, tatizo kubwa lipokwa wazazi wake,...hata hivyo sitaki kusema sana, na ukumbuke hawajui kuwa umekuja kwa lengo gani,sisi tumekuja kusalimia tu,na tutatafuta nafasi ya kumuona, kama yupo tutajua la kufanya, ....‘Akasema Mjomba.

‘Sawa , lakini wote niliowaona nyuma, bado nawatafakari, sijarizika nao moja kwamoja, sijui labda, kwa vile hawajajiremba, maana wote nimewaona wakiwa wametoka shamba au wakiwa wanafanya kazi za suluba,...ngoja tumuone huyu, huenda akanibadili mawazo...’nilimwambia mjomba huku nimeshakata tamaa ya kumpata nimtkaye.

‘Hilo usijali ,haihitaji haraka,hatua ya kwanza ni kuwaona, hatua ya pili kama umerizika na yupi, utapata muda wa kuongea naye, maana hata yeye anatakiwa akukubali, huenda akawa na mtizamo wake na yeye, au ana mtu wake,au haikubali familia yetu kutokana na mitzamo yao ya kifamilia, hayo yapo,kwahiyo jambo lamuhimu ni kuwa muangalifu kwa sasa , hatutaki wajue nini kusudio letu...tumekuja kusamia tu...’akasema mjomba.

Tulifika tukapiga hodi na mara mlango ukafunguliwa na mtoto, akatsalimia na sisi tukamuuliza mama aua baba wapo, akasema hawapo, tukamuuliza na dada, akasema kaenda shamba...tukaona tumekwama,na tukaona tuje siku nyingine. Na wakati tunatoka,tukamuona msichana akiwa kabeba kuni, na juu ya kuni kaweka majani ya ngombe, na mkononi kashika ndoo ya maji...hebu fikiria vitu vyote hivyo na ni vizito kweli, mimi mwenyewe ingenipa shida kuvibeba.

‘Duh, hili jembe kweli, masikini binti wa watu, ...mbona mateso namna hiyo...’nikasema

‘Huku ndo kijijini, ...na hebu angalia ukipata mke kama huyo utasemaje, anajua kazi,na kazoea shida,na ukisikia historia yake utamuonea huruma..’akasema mjomba.

‘Ina maana ndio binti mweneywe ambaye nahitajika kumuona...?’ nikauliza

‘Haswa,kazi kwako,na bahati nzuri wazazi wake hawapo wewe jivunge kama unamsaidia halafu piga maneno mawili matatu utaniambai , nakusubiri pale mbele...’akasema mjomba.
Nilimwangalia yule binti, alivyo, kwa haraka utafikiri ni mgonjwa,maana kakonda,mchafu,nguo alizovaa...duh,.....kwa kweli inatia huruma, na huruma ya kibanadamu ikanishika, na wakati namkaribia, kwanza yule binti akawa kama ananikwepa akijua nataka kupita, kwa kufanya vile akajikwaa,na hata alipojaribu kujizuia , hakuweza mzigo uliokuwepo kichwani ukamzidi...

Akawa anahangaika, maana mguu ulikuwa umenaswa na majani na kwa muda huo alichojali ni kuyaokoa yale maji yasimwagike, lakini haikuwa rahisi maana sijui ni kwasababu ya kuchoka au vipi, kwani alijikuta akielekea kudondoka chini, na mimi kwa vile nilishamkaribia, kwa haraka nikamuwahi , kwanza nikasaidia kuishika ile ndoo ya maji kwa mkono mmoja, na huku nikitaka kumwahi asidondoke kwa mkono mwingine,lakini haikuwa rahisi hivyo, kwani mshika mawili moja humponyoka.

Mtoto wa mjini sikuweza kuhimili vyote viwili, yale maji kwenye ndoo yakanimwagikia mimi , nakujikuta nikilowana, na yule binti akawa kama kaangukia mikononi mwangu, ilikuwa picha ya aina yake, maana mtoto kajaa mikononi na kusogea hadi kifuani, halafu akawa ananiangalia usoni, na macho yamechoka, akionyesha aibu, na huku akijitahidi kujiinua....mmmh, kwakweli nilitamani nishushe mdomo wangu ni mbusu.....

‘Tamaa hiyo rafiki yangu, ilikuwaje...na kwa muda huomjomba alikuwa wapi...?’ nikamuuliza
Mjomba alikuwa mbali akiiangalia ile picha huku akitikisa kichwa kwa kufurahia lile tendo, kwani baadaye aliniambi ile ni ishara nzuri ...

‘Lile tendo mungu kalijalia makusudi ili uweze kuyaona yale macho ya huyo binti, sio rahisi kuyaona kwani ana aibu balaa, halafu angalia ule mdomo mmmmh, na hata sura yake,licha ya kuwa kachakaa kwa kazi za suluba,lakini unamuonaje....?’ hayo yalikuwa maneno ya mjomba , ambayo aliniambia baadaye, lakini akili yangu ilikuwa imetekwa na hali halisi ya yule binti, nay ale niliyowahi kuongea naye.

*******

‘Oooh, `be careful..’ angalia usije ukaumia na hizo kuni...oooh pole sana na maji yamemwagika ..oooh, mungu wangu...’nilijikuta nikamaka na kuhangaika,na hata pale nilipomwagikiwa an maji sikuweza kujihis hivyo,macho na akili yangu ilikuwa imetekwa nay ale macho yaliyokuwa yakianiangala kwa aibu huku nikiwa nimemshikilia yule binti na macho yake yakiniangalia na huku ndoo imeshaniponyoka,maji yote yameishia chini.

Yalikuwa macho makubwa, na nyusi nyingi, ambayo hata hayahitaji kupakwa wanja, mdomo wake mdogo, lakini umeumbwa kinamna kwamba hauhitaji kutabasamu au kucheka, vyovyote iwavyo anapendeza, yaani, we acha tu. Licha ya kuwa uso ulisawajika kwa uchomvu,kazi na huenda njaa,lakini sura yake ya asili haikupotea.

Nilijikuta nikiwa nimemshkilia kwa muda,na yeye akawa anahangaika kujitoa pale mkononi,lakini kwasababu bado yale majani yalikuwa yamemnasa, akawa kila akijitoakwangu anaishia kurudiamkononi mwangu,sijui kwasababu ya kuchoka au alikuwa akijisikia vibaya, ....na mimi kwamuda ule mkono ulishachoka kumshikilia tena,bila kukusudia nikamwachia akadondoka chini kama furushi,na kwa vile nilikuwa sijasimama vyema, na mimi nikajikuta namfuata chini nikadondoka na bahati mbaya nikamdondoka na kujikuta nikimlalia....


Yule binti alinisukuma haraka na kusimama huku akihangaika kujiweka vyema,na nilimuona kama anapepesuka, na kutaka kudondoka tena, nikainuka haraka na kabla sijamshika, akawa keshaifikia ndoo yake na kuiangalia kwa macho ya masikitiko, kulikuwa hakuna hata chembe ya maji,akaanza kulalamika nakusema.

‘Jamani hivi nitarudi tena kisimani,maji ndani hakuna na muda huu mama atarudi, sijapika ...balaa gani hili leo...’akasema huku akiniangalia jinsi nilivyolowana.

‘Usijali, hiyo ni bahati mbaya,wote tumeona nini kimetokea, hukudhamiria iwe hivyo....kamaikibidi tutamwambia mama yako ilivyokuwa..., kwani kisimani ni mbali..?’ nikamuuliza.

‘Hapa kila kitu ni mbali, shambani ni mbali,sehemu ya kutafutia kuni ni mbali,kisimani ni mbali na hata maisha yenyewe yapo mbali...sijui niseme nini,....ngoja nikimbie kisimani nikachote hayo maji,maana mama anakuja sasa hivi...’akasema huku akichukua ndoo na bado alionyesha kupepesuka.

‘Lakini nakuona haupo sawa,...wewe nipe hiyo ndoo nitakusaidia kubeba, kama sio mbali huko kisimani...’nikamwambia.

‘Hahaha,...kama sio mbali....hata hivyo, wewe ni mwnaume utachotaje maji,mbona utaangaliwa kwa jicho la ajabu hapa kijijiini,maana kila kitu anafanya mwanamke, kubeba maji,kuni, kupika,mwanaume anabeba jembe na panga, labda na fito zakujengea,lakini sio kuni...lsio kwamba nalaalmika,haya ndio maisha yetu...’akasema huku akianzakuondoka,nami nikamwangalia mjomba,na mjomba akanipa ishara nimfuate, yeye akawa anaondoka kurudi nyumbani.

‘Hebu niambia kwanini kazi zote unazifanya wewe, kwani hakuna ndugu wengine au mama yako wakukusaidia ...?’ nikamuuliza, na yeye akaniangalia kwa haraka na halafu akageuza macho haraka kuangalia mbele kwa aibu.

‘Sio kitu, mbona ni maisha ya kawaida tu, ilaleo najiskia kizunguzungu,sijui ni kwasababu gani, ...hata hivyo hakuna kazi ngumu kwetu, mimi naziweza zote maana nimeanza kuzifanya nikiwa bado mdogo hata kabla sijaanza darasa la kwanza...’akasema.

‘Ina maana mama yako mzazi alianza kukufanyiza kazi hata ukiwa mdogo...?’ nikamuuliza kwa kushangaa , na mara akanitupia jicho la haraka na niliona kama anataka kuniambia nimuache namisha yake, lakini kwa adabu akanijibu kwa kusema;

‘Mama....sitaki hata kuliongelea hilo, kwani kama mama angelikuwepo duniani, sizani kama ningelifanyishwa yote haya,mama alipoaga dunia, na mimi ingawaje nipo hai,lakini utu wangu, utoto wangu na maisha yangu nayo yaliaga dunia, hapo ulikuwa mwanzo wa mimi kuwa kibarua,kuwa mtu nisiye na thamani...namkumbuka sana mama yangu,hata sitaki kumuongelea, nisje nikaanza kulia,maana nimekuwa nikilia hadi machozi sasa yamekwisha,iliyobakia nikulilia moyoni tu....’akasema kwa uchungu.

‘Pole sana ...hiyo ndio mitihani ya dunia,na huyo mama unayeishi naye hakuhurumii...?’ nikamuuliza.

‘Anasema ni vyema nikomae nijue maisha, ndio maana anataka kila kazi niifanye mimi..sasa hivi yupo kwenye vikao vyao vya akina mama , akirudi hapa kama sijapika kutachimbika....na alisema nifue nguo zake, sijafua,maana maji kisimani ni madogo, ....huko shambani nako nahitajika kuoanda mbegu zote, kwani mvuo ipo karibu,...nimejitahidi lakini njaa nayo hainiachi...sikuwahi kunywa chai, kwani masharti ni kuwa mpaka nimalize kazi ndio ninywe chai....’akasema huku anataka kama kulia.

‘Sikiliza hakuna sehemu wanauza maji,kuna lile bomba la maji ya kuuza, nimeliona pale wewe chukua pesa hii ukanunua hayo maji haraka,...halafu ujifanye umeteka kisimani...kwani atajua...' nikamwambia huku nikimpa pesa, lakini hakukubali katu..

Nilipoona kakataa katu , nikamuonea huruma, nikijua anaweza akadondoka, njiani kwa hali aliyokuwa nayo, ukimuona licha ya kuwa kava nguo, lakini dhahiri tumbo lilikuwa karibu lishikane na mgongo, nilichofanya kwa haraka ni kumnyang’anya ile ndoo nikakimbia nayo hadi kwenye bomba la kulipia, na hapo nikajitosa kumsadia kubeba maji. Yeye akabakia kaduwaa tu

Nilipomletea ndoo ya kwanza akasema `Ahsante,....’ nikarudia tena mara ya pili, na nilijikuta nikilowana jasho mwili mzima, lakini moyoni nikisema bora ya inzi kufia kidondani,na baadaye nilipoleta hiyo ndoo ya pili, akaniangalia kwa mastaajabu akasema;

‘Wewe ni mwanaume gani unayebeba maji huonii kwamba hapa kijijini watakucheka,....’akaniambia na huku akiniangalia kwa iabu halafu akawa anaangalia huku na kule kama hakuna watu walioniona nikifanya lile zoezi, na bahati nzuri kwa muda ule kulikuwa hakuna watu kwahiyo mambo yalikwenda shwari.

‘Nikiwa hoi kwa kuchoka,maana kazi hizo sikuzizoea,nimeshakuwa tepetepe kwa maisha ya Ulaya, nikakaa kwenye gogo na kusema;

‘Hebu niambie maisha yako,....?’ nikamuuliza.

‘Maisha yangu, kwanza wewe ni nani na kwanini unanifanyai hivyo...?’ akauliza huku akionyesha uso wa wasiwasi.

‘Usijali mimi ni jirani yenu, nimerudi karibuni toka masomoni, nikaona niwapitie majirani kuwasalimia, hapa tulifika tukamkuta mdogo wako, tulipomuuliza aksema baba na mama hawapo, ndio baaaye tukakuona wewe,....’nikasema.

‘Wewe ndiye mtoto wa Msomali, nilisikia unasoma Ulaya....?’ akaniuliza.

‘Haswa kumbe unanijua....’ nikamwambia.

‘Wanakujua wengi, kijijini hapa kilamtu wanamjua, ...’akasema huku akihangaika na kazi za ndani, maana hapo alitakiwa kuosha sufuroa abandike mboga, moto ukawa unamsumbua hauwaki, na bahati nzuri, nilikuwa an kibiriti mfukoni nikampa, na moto ukakubali.

‘Ahsante sana unaonekana mtu mkarimu sana, lakini...mbona uanzidi kukaa hapa, naogopa saan mama asije akakukuta ukiwa unaongea na mimi...’akasema.

‘Nimeshakuambia kuhusu mimi usijali, kwani nyie hamtaki majirani kuja kuwasalimia. Kwanza naomba unijibu swali langu, hebu niambie kuhus maisha yako..?’ nikamuuliza tena.

‘Kuhusu maisha yangu yangu...hahaha...kwani maisha ni nini....hivi kweli ukiniangalia mimi nina maisha....hapana mimi najiona kama mti, kama mfu, aliyehai,au kama gogo ambalo kazi yake ni kusukumwa huku nakule, siijui dunia au raha ya dunia, labda hapo nitakapoweka ubavu wangu kwenye mkeka wangu usiku, angalau nipate usingizi ndio nasema ehu mungu wangu nimepona.....’akasema.

‘Mama yangu alifariki nikiwa mdogo, aliumwa ghfla tu, akafariki na mengi yakaongew , kuwa huenda mama huyu mdogo ambaye kwa muda huo alikuwa na mahusiana na baba ya kisiri huenda ndiye kamloga,...hayo ni maneno ya hapa kijijini,wala mimi siyaamini...najua mama alifariki kwa nguvu za mungu,inagawake kuondoka kwake ni pigo sana kwangu,lakini bado namshukuru mungu kuwa yeye kamchukua mja wake kwasababu anampenda zaidi yetu.

Alipofariki mama, kwasababu bado nilikuwa mdogo sana nikawa nalelewa na bibi, na maisha yangu na bibi yalikuwa ya raha, maana bibi anapenda wajukuu,...lakini huko kwa bibi hali haikuwa nzuri, njaa ilikuwa imezidi na misha ya kule yalikuwa magumu sababu ya njaa,na mifugo ikafa yote,na hata bibi naye hakudumu akafariki,...nikabakia yatima, bibi alikuwa ndiye mama ndiye baba.

Baba kwa muda huo alikuwa hatulii, yeye na kimwana wake, na hatimae wakafunga ndoa, na sikuwa na jinsi ikabidi nije kusihi nao,nilipofika tu, nilikaribishwa kwa fimbo.

‘Mara mtoto huyu mjeuri , mara mtoto huyu mvivu....kukawa hakukaliki, na hata baba alipoingili kati mama huyo alisema kuwa anataka anile na kuwa mke jasiri, anyejua kila kazi...

‘Kwahiyo nikaanza kufanyishwa kazi zote,kupika,kuteka maji,kwenda shamba hivyo hivyo,unafika shamba unapangiwa sehemu kubwa,unaambiwa kumaliza kwako ndio kupata uji, na uji wenyewe unahesabiwa vijiko,na wakati mwingine naenda shamba peke yangu, ni mbali kuna wanyamawakali , lakini huko nawakuta watu wengine tunalima nao na wao kwakunihurumia wananigawia uji au chochote walichokuja nacho,.....hata nilipoanza darasa la kwanza ,nilikuwa nimeshajua kazi zote....’akasema.

‘Kwahiyo ulipoanza kusoma kazi zikapungua...?’ nikauliza

‘Kazi zipungue au ndio ziliongezeka...nilitakiwa kuhakikisha kuwa nimefanya kila kitu, kufagia,kupika,kulisha mifugo kuteka maji, kabla sijakwenda shule asubuhi,....na nikirudi jioni niende shamba, kama kuna kilimo au palizi, ... sasa fikiri huo muda wa kuamka na kufanya hayo yote ,ili uwahi darasani....unaamuka usiku sana unawasha taa kama kunamafuta,unapika...huku ...hata sijui nikuelezeje, maana siku nyingine nakatazwa kwenda shule kwasababu sikumaliza moja ya majukumu yangu....’akasema.

‘Hata mtihani wa darsa lasaba niliufanya huku naumwa, huku natakiwa nifanye kazi, sijui hata niliuafanyeje,mungu mwenyewe ndiye anajua...nikafeli...na hapo ikawa gumzo kwa mama akisema unaona, alikuwa shuleni hasomi, kazi umalaya,kazi sijui nini...yaani nasingizwa mambo ambayo hata sijawahi kuyafanya na wala siyajui...’akasema huyo binti huku akihangaika kuosha vyombo. Nilitamani nimsadie lakininikaona nitakuwa nimezidisha.

‘Unajua nashangaa uliwezaje kufanya kazi zote wakati ulikuwa mdogo..?’ akaniuliza.

‘Nilifundishwa...kwa bibi nilikuwa najifunza kidogo kidogo maana bibi alikuwa mzee,kwahiyo wakati mwingine ananionyesha jinsi ya kupika....lakini nilipofika hapa kwa mama nilifundisha mengi kwa fimbo mgongoni, yaani upo unafagia, kwasaabbu ya utoto huwezi kupindisha mgongo,unapindishwa kwa fimbo, unapika chakula hakikuiva vyema, kitawekwa uchafu halafu unaambiwa ukile chote..au unaunguzwa na kaa la moto,nimejifunza hivyo hivyo,na nimekuwa nikijitahidi nisifanye makosa....maana fimbo ndio kumbusho langu...’akasema akishika mgongoni,kama vila anhisi kuchapwa.

‘Kwani baba muda wote hayupo nyumbani, au yeye anaishi wapi..?’ nikauliza.

‘Baba hashindi nyumbani , yeye anafanya kazi za uvuvi huko kijiji cha ziwani,hurudi usiku au siku nyingine harudi kabisa, kwahiyo mimi nashinda na mama na wadogo zangu , yaani watoto wa mama huyu ninayeishi naye....siku baba akiwepo aah,mama atajitumakila kazi, lakini akiondoka, mguu juu....mimi kabarua nipo nitafanya..’akasema.

‘Kwani hawo wadogo zako hawakusaidii kazi.....?’ akauliza.

‘Mhh, wao bado wadogo hawaruhusiwi kufanya kazi...’akasema huku akibenua mdomo.

‘Lakini wewe umesema ulianzia kufanyishwa kazi ukiwa bado mdogo, na wao kwanini hawafundishwi hizo kazi.?’ Nikadadisi.

’Wewe jua tu kuwa wao bado wadogo,....mengine siyajui,mimi ninachojua ni kufanya kazi, maana sina la heri,hata ninavyojituma, lazima kutakuwa na kasoro...unaona hizi alama mkononi,haya ni makovu ya kumwa meno,kuchomwa moto ... achilia mbali huko mwilini, kuna michirizi ya fimbo, kama nimejichora, yaani ndio maana naomba mungu kufike usiku nipate kuulaza huu ubavu. Na wakati mwingine namuota mama, nananipa faraja...’akasema huku akishika ubavu wake na machozi ya kimlenga lenga.

‘Pole sana, ipo siku utaaachana na shida hii,nakuhakikishia...?’ nikamwambia.

‘Hizo ni ndoto ambazo hata sizifikirii..maana mwenye maaumiz ni mama, kwa kila jambo, aliwahi kuja kijana mmoja akataka kunioa mama akamtolea nje,na baba anamsikiliza mama husemi kitu kuhusu mama, kwahiyo maisha yangu yapo mkonono mwa mama, sijui nini mama atasema kuhusu maisha yangu ya baadaye,mungu ndiye anayejua.

Nilitaka kumwambi hapo hapo kuwa mimi nitaka awe mchumba wangu , lakini nikakumbuka msharti ya mjomba kuwa nisije nikaungumza neon kama hilo, mapaka niwaone wote halafu tukae kikaokidogo cha kuwaathimini, kwani mwisho wa siku wataniambi sifa au ubaya wa kila mmojawapo,ili niweze kuchuja.

‘Sikiliza.... nahitaji muda wa kuongea na wewe,sijui lini nitakupata,mimi nataka kukusadia uondokane na haya maisha, kwa njia yoyote ile,lakininahitaji kwanza wewe mwenyewe ukubali, pili ujiamini,kuwa mama yako huyo sio kila kitu na wewe unahitaji maisha yako ya kujitegemea....unanielewa..’nikamwambia kumpa ujasiri.

‘Wewe unaongea tu kwasababu ni mwanaume,hujui ni maisha gani niliyo nayo,humjui mama yangu, mtu hata chakula ananihesabia vijiko, ugali nahesabiwa matonge, nikikata nyama natakiwa kupeleka idadi ya vipande...wewe unamuelewa mama au unamsikia, olewangu nikutwe naonja mboga, ikiiva natakiwa kumuita aje anoje yeye....sijui kama unanielewa,na naomba uondoke maana ndio mida yake ya kurudi,nikionekana nimesiamam na mwanaume,nitakoma siku hiyo....’akasema huku akiangalia njia ambayo huenda ndipo mama yake anapotokea.

‘Sawa naondoka lakini nakuhitaji kuongea na wewe, nitajitahidi kutafuta kila mbinu tuongee vyema, usijali, mimi sina malengo mabaya na wewe vyovyote utakavyopenda mimi nitakusaidia...’nikamwambia huku nikiondoka, nilijaribu kumpa pesa lakini alikataa kata kata..
Na nilipgeuka nyuma nikamuona mama mmoja kibonge akiwa anakuja,na aliponiona akaniangalia kwa jicho la hasira, ......

NB Je huyo mama ni nani, na ilikuwaje? Tuwepo sehemu ijayo.

WAZO LA LEO: Ugumu wa maisha aujuaye ni mwenye maisha hayo,ni kama siri yakata aijuaye ni mtungi.


Ni mimi: emu-three

5 comments :

Anonymous said...

Kuna kitu kimoja nataka kujua, hivi visa hasa hiki ni vya kweli au umejitungia tu, maana kinafanana na tukio lililotokea kabisa.

Rachel Siwa said...

Yaaani na hizi picha zilizofuatana zinanikosha sana tuu Ndugu Wa mimi!!!Huu ni moto wa kuotea mbali, hakika utafika unapotaka, kwa mapenzi ya Mola!!Pamoja ndugu yangu!

emuthree said...

Tupo pamoja ndugu wa mimi Rachel na mwenzangu usiye na jina, mungu awabariki sana kwa kunipa moyo. Tupo pamoja

Precious said...

M3 una zaidi ya kipaji kwa kweli maana mikasa yako yote ndio maisha yetu kila siku miongoni mwetu.. Ipo siku Mungu atashusha baraka zaidi kwa kazi ya mikono yako, itajulikana na watu wengi wenye kuelewa umaana wa kipaji ulichonacho na kukitumia ipasavyo. Mungu azidi kukubariki.

emuthree said...

Nashukuru Precious mungu akubariki sana.Tupo pamoja