Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, February 7, 2012

Ni nani anayechangia kuvunja ndoa mke au mume?

Nimeletewa habari hii, na nimefurahi sana kuwa huyu ni mmoja wa wapenzi wa blog hii kaamua kuniunga mkono kwa vitendo, namshukuru sana, nawaomba mchangie kwa wingi ili kumpa faraja, karibu sana tupo pamoja.


Ndugu mpendwa, nakusalimu kwa amani na upendo.

Mimi ni mmoja wa wapenzi wa blog yako, na huwa sikosi kuifungua karibu kila siku, na nikiikosa ninakuwa sina raha, na raha yangu huzidi zaidi pale ninapoona umeandika kitu , hasa kwenye visa vyako, vimekuwa kama kitu ambacho nikikikosa siwezi kuishi…umenipa limbwata la visa vyako…lol

Nimesikitika sana kuwa huna vitendea kazi au sehemu ya kujishikiza, ili uweze kutupa visa hivi ikiwezekana kia siku, maana hasa sisi tunaoishi nje, tunatamani kusoma habari za Kiswahili na hasa visa vyenye ukweli ndani yake, kama vya kwako, ambavyo ukivisoma ni sawa na mtu anayeangalia movie. Na kwanini usiweke matangazo,…mbona wenye mitandao wenine wanaweka, na utakuta mitandao yao haina mengine zaidi …sana-sana ni picha, udaku au umbeya.

Mimi leo nimeamua kukuandikia jambo moja linaloninyima raha,…kama halitifaa kuliweka hewani nirudishie, na kama litafaa lipitie vyema, kama nimekosea Kiswahili nirekebishe maana tumeloea Ulaya hata lugha sasa inatupiga chenga. Kwa ujumla nimekuwa nikipitia mitandao mingi, na mingi imekuwa haielezi ukweli kuhusu mwanamke na mwanaume, hasa NDOA, Naizungumzia ndoa, kwani mimi nipo ndani ya ndoa, nana bahati ya kuishi kwetu bongo kwenye manyayaso ya hali ya juu ya ndugu na mama mkwe na pia kuja kuishi Ulaya, ambapo maisha yetu sio mabaya, tunakula ….

Sasa ubaya upo wapi, najua wengi mtauliza, nakuwaza, Ubaya upo ndani ya ndoa yenyewe, ubaya upo kwenye kusikilizana, ubaya upo kwenye maisha ya mke na mume, mimi huku ni kama mfanyaakzi wa nyumbani, ninaweza kusema mimi ni mmoja wa wahanga wa ndoa,ingawaje nipo dunia ya sasa, ninaishi Ulaya na mume wangu, lakini maisha ninayoishi na mume wangu ni kama tupo ile dunia ya mababu zetu ambayo mke hana usemi. Mke ni kama bidhaa, yote nimevumilia sikujali kuwa nipo Ulaya, na kama ningeliamua kufanya lolote ningeliweza, lakini bado naiheshimu ndoa yangu.

Mimi hapa nipo kama mshumaa tu, siku yoyote unaweza ukazima, na ni bora niyasema haya ili watu wajifunze na waysikie, mwanga wa mshumaa huu usiishie kwangu tu, uwamulikie na wengine wanaoteseka kama mimi.

Najua wengi mtanilaumu kuwa natoa siri yangu ya ndoa, lakini nimeona ni heri kufanya hivyo, ili iwe chachu kwa wale wanaume wengine wenye tabia kama hizi waweze kubadilika, ila kwa mume wanu imeshindikana, imekuwa kama mbuzi kupigiwa gitaa. Hapa nilipo umri umeshapevuka, siwezi kusema niachane naye, nikatafute mume mwingine, nani atanioa mimi wakati sura imeshachujuka. Sitaweza kuwatelekeza watoto wangu kwa kuabdili wanaume, hapana, ila nahitaji mawazo yenu, ….

Kwanini naandika haya : Nimeamua kuyaaandika kwasababu kuna mtu aliuliza swali, je kati ya wanandoa wawili mke na mume ni nani anayechania kuvunja ndoa. Ndio sisi wanawake tunakuwa na kitu kinachoitwa kitchen party, je inatusaidiaje kudumisha ndoa zetu, huyu mtu aliuliza hivyo, nikashindwa kumuelewa kwani ndoa ni watu wawili, kama mke atajitahidi sana na mume bado haelewi hiyo ndoa, au hayo mafunzo ya kitchen party yatasaidia nini.

Nimefikiri sana, na kufanyia utafiti ukianzia kwangu mwenyewe na kugundua kuwa kati ya mwanaume na mwanamke anayechangia kwa kiasi kikubwa kubomoa ndoa,ni mwanaume ila nchi za kwetu,hasa nchi za dunia ya tatu(maskini,afrika)wanamwangalia mwanamke kama ndiye chanzo cha kuvunjika ndoa, hasa wakisema, eti wanawake wengi haweze kumtuliza mume, hawajitahidi kumshawishi mume atulie nyumbani na ndio maana wanatafuta nyumba ndogo n.k swali hapa ina maana mke pekee ndiye anatakiwa kufanya jitihada hizo?

Hebu tuziangalie jitihada za mwanamke hasa wa Kiafrika, na tujiulize mwanamume anataka jitihadi gani zaidi ya hizo, kwani,mwanamke wa kiafrika,anamoyo ule wa kuvumilia,maudhi pamoja na manyanyaso ya kila aina,anayofanyiwa na mume wk.Mfano,kupigwa, kuishi na mwanamume mlevi, kumvumilia mwanamume hata akichelewa kazini kwa visingizio mbali mbali,kuletewa watoto wa nje,au hata kuletewa nyumba ndogo au vimada nk.Lakini yote hayo,anayabeba ndani ya moyo wake,na anaona kuwa ni aibu ya ukoo,yeye kurudi kwao,kwa kisa,ameshindwa kuvumilia ndoa.

Wanawake wengine,hadi wanapata vilema vya maisha,kwenye ndoa zao na bado wapo kwenye ndoa wanavumilia na kuendelea na maisha kama kawaida.Wengine,wanawafumania waume zao,lakini,wanabakia na siri na kuwatetea waume wao,kuwa hakufanya jambo lolote baya na vitu kama hivyo, je uvu,milivu gani kama huo, upendo gani kama huo, uvuto upi mnaoutaka, kucheza sebene peke yake.

Hebu chukulia upande wa pili kwa mwanaume mfano mwanaume,akufumanie,itakuwaje, wewe uchelewe kurudi nyumbani itakuwaje, ….ukosee kufanya jambo fulani, na mengine mengi, mwanamke atakiona cha mtema kuni.
Kwa ujumlaNdoa,inaumiza sana kwa wanawake.Na vidonda vya ndoa au majeraha ya ndoa,ni mengi sana kwa mwanamke na hayaponyeki, kwani kila siku yanatoneshwa…

Kwa ujumla mwanamke wa Kiafrika anastahili kupewa heko, na hili nimejifunza nilipokuja kuishi huku Ulaya. Huku Ulaya mwanamke ana haki zake, hayanyanyaswi ovyo,na ole wako mwanamume umnyanyase mkeo halafu alifikishe hilo swala kwenye vyombo vya sheria….sio kwamba nawasifia kwa hili, lakini kwa kiasi kikubwa limemkomboa mwanamke na kujiona kumbe na yeye ni kimumbe kama mwanaume.

Mimi nimeishi maisha hayo ya taabu hata vile nipo Ulaya, nimekuwa nikiishi na mume wanu na kumfanyaia yote kama vile nipo nyumbani, lakini ….nasema lakini ni ule usemi usemao penye miti mingi hakuna wajenzi…imefikia mume wangu hawajabiki kwenye swala muhimu la ndoa yake, swala ambalo wengi wanatulaumu kuwa sisi sio wabunifu, hatujui mapenzi, lakini utajuaje kucheza mpira kama hujaingia uwanjani…hayo ni visingizio vyao na kusema ukweli kama hilo wao ndio wakulaumiwa, kwani walitakiwa kushirikiana na mkewe wakafundishana na kuelekezana sio kukimbilia vimada.

Uvumilivu una mwisho wake, na majeraha yakizidi sana mwisho wake yanaweza kugeuka kuwa kansa, ndio maana nimeandika hilo swala kwako, uliweke hadharani watu walijadili na wanaume wasema ukweli wao, ili sisi wanawake tujue ni nini hasa waanume wanakihitaji kutoka kwetu, ili tuwatimizie,… ili tukiwafanyia hivyo waweze kutulia majumbani kwao, ili mwisho wa siku ndoa ziwe na amani.

Humutaamini kuwa wengine tunamaliza miezi zaidi ya mitatu hatuwajui waume zetu, waume zetu huku Ulaya wanasingizia kuwa wanachoka kwenye kubeba maboksi, je ni kweli hili au ni kisngizio cha mume wangu tu, au na wenzangu wanafanyiwa hivyo hivyo, …je huko wanaposhinda na hata kulala na machangudoa hawachoki, au wanatufanya sisi ni wajinga tu hatjui nini wanachokifanya, je hii ni ndoa kweli, je na sisi tukiamua kutoka nje ya ndoa waatsemaje, na kwa hilo ni nani atalaumiwa, lakini tunaogopa kuja kuwaacha watoto wetu mayatima kwa kuugua magonjwa mabaya.

Samahani sana kama nitakuwa nimewakwaza wengine kwa hayo niliyoyaongea lakini kama ilivyo kawaida ukweli huuma, …

Mimi mwenye majeraha ya ndoa Mama Wawili.


Ni mimi: emu-three nikiwaletea habari hii kama nilivyotumiwa:

5 comments :

Anonymous said...

Naomba,nichangie kwa kidogo tu.Kwanza,naanza kwa kujiuliza.Nini maana ya ndoa?Kwanini,umeoa/kuolewa.Wajibu wako kwenye ndoa ni upi,namaanisha kwa mwanamme/mwanamke.Tuje,kwenye imani zt,hasa yangu ya kikristu.Kabla ya kufunga ndoa kwanza,huwa wanandoa watarajiwa,wanafunzwa au wanafanya semina ya ndoa.Cjui kwa imani ya kiislamu.Napenda kuchangia kuwa,kwa asilimia kubwa,anayevunja ndoa ni mwanamme mwenyewe,nasema hivi,mwanamme ni kichwa cha familia,yeye ndiye shina au chipuko la familia.Shina,likiwa bovu na matawi yt ni mabovu.Mwanaume kwa kulijua hilo na mfumo dume,aliokulia nao,kuanzia kwenye ukoo wao hadi kufikia kuwa na familia yk,ndiyo unaosababisha ndoa kuvunjika.Wanawake wa karne hii,cyo wa karne ya jana.Nani kwa sasa,atakayekubali kunyanyaswa,kupigwa nk.Nawalaumu sana,wanaume,ndiyo chanzo cha kuzagaa hovyo watoto wa mitaani,nk.Kama,mwanaume,angelijua thamani ya ndoa yk au maana ya ndoa,natumaini,ndoa zingegeuka kuwa paradiso.Nina mfano,wa marehemu dada yangu.Amefariki kwa ukimwi,tena aliyemletea ndani ya nyumba ni marehemu mumewe.Lkn,pamoja na tabia ya marehemu shem wt,ilikuwa mbaya,lkn mkewe,alikuwa anamtetea kwa kila jambo.Ilikuwa ukitaka kukosana na marehemu dada,umseme vibaya mumewe,hadi anakufa,alikuwa anakataa kuwa ni mumewe ndiye,aliyempatia huo ugonjwa na alikuwa akikataa kuwa anaumwa huo ugonjwa.Mimi,nakubali kuwa,matatizo ya kwenye ndoa,wanaosababisha ni wenyewe wanaume,japo kuna wanawake wengine nao ni vichwa ngumu.Niko na mifano mingi.Ngoja,nione kwa wengine,watasemaje.

Swahili na Waswahili said...

Duuhh Mhhhh ndugu yangu mama 2,Pole sana tena sana,yaani nimesoma hapa mpk nimejiuliza maswali mengi sana,Kwanza kuchoka kwa sababu ya box ni muongo huyo mumeo na mengi afanyao,kwani maisha ya Ulaya bila kusaidiana na mumeo ni shida kubwa sana,kama angekuwa hayupo sawa,jee mama 2 wewe unafanya kazi au kusoma kwa sasa?kama upo tuu ndani na matatizo hayo utazidi kudidimia,Pia kuvunja ndoa kama mwenyewe ulivyosema si jambo zuri kwani utakapokwenda pia hupajui.Unajua haya Maisha ya watu 2 tuliyokutana ukubwani yanamatatizo sana,kwani kila mtu kalelewa kwao na itikadi/malezi yao,kamwe hatuwezi kuwa sawa kwa kila kitu,lakini tunahitaji kuvumiliana kama binaadam,lakini Vikwazo visizidi sana,inatakiwa umwambie ukweli kama nini na nini wewe hupendezewi,na maisha na yeye yanakuwa magumu sana.Kwani kama huna mtu wa kukupa faraja na Amani yeye ni wakwanza kwa yote hayo.Umeuliza kama wote wanapata/wanaishi kama wewe,jibu,hapana mimi ninawaona ukiacha Waafrika yaani Waswahili wengi tuu hapa nilipo wanawasaidia wake zao sana tuu ktk malezi na mambo mengine.Duuhh kwanza wewe ni Mwanamke haswa Mungu akuepushe na hayo yote ili muwe na mawasiliano mema na shemjeji,Yaani nimeona huu ujumbe niusambaze zaidi ili na wengine waweze kukusaidia Mawazo.Naami ipo siku atabadilika,lakini umwambie na umuweke wazii kwani tusije tukakupoteza,kwani Mawazo ni Ugonjwa mbaya sana.Sipendi mtu aninyayase au kunyanyasika.@ emu wa 3 Ndugu wa mimi Ahsante sana kwa Shule hii,Pamoja sana ndugu yangu ipo siku tutafika tuu.

Subira said...

Pole dada yangu, yaani mwanamke wa kiafrika popote pale alipo hana tofauti na mwanamke mwenziwe, haijalishi yuko mjini au kijijini, haijalishi kama mumewe msomi au hajasoma hata darasa moja au ameishia darasa la 7. Jamani wanaume vitendo vyao vinachokesha sana, wakati mwingine unajiuliza si bora basi wangejikalia tu wakauza udaga badala ya kupoteza muda kwenda shule. Maana hiyo elimu waliyoipata bado haijawasaidia kuwakomboa wao wala familia zao. Mfano mwanaume anateyetembea na wanawake hovyo wakati yuko ndani ya ndoa mpaka anafikia kuambukizwa maradhi na kisha kwenda kumuambukiza mkewe nyumbani, huyu mwanaume elimu yake inamsaidia nini? Faida yake ya kwenda shule iko wapi? Kwanini anashindwa kuelewa mpaka karne hii kila kitu kiko wazi, majarida, matangazo mabararani kwenye vyombo vya habari kuwa ukimwi unaambukizwa kwa kufanya ngono zembe? Kwanini anashindwa kuelewa kuwa ukimwi hauna dawa? Kwanini anashindwa kumlinda mkewe na maambukizo? Kwanini anashindwa kutumia upeo wake mdogo kuelewa tu kuwa wakipata ukimwi yeye na mkewe watoto wao watabaki yatima na watapata tabu? Ni utamu wa aina gani huo unaomfanya mtu awe tayari kuhatarisha maisha yake na kuutoa uhai wake na wa mwenziwe? Kwanini wanaume wanakuwa wakatili na selfish kwa watoto wao kufikia kiwango cha kuwaondolea hao watoto mama zao vipenzi kwa maradhi yanayoweza kuepukika? Kwanini?

Kama elimu imeshindwa je tujaribu nini? Dini? Mbona hiyo nayo imeshindwa kuwapa hofu ya Mungu? Maana unaweza jificha vichochoroni huko na kufanya mambo yako lakini unasahau kuwa pamoja na kuwa mkeo hakuoni lakini Mungu anakuona! Duh hatari sana, wako wanaume na elimu zao wanaamini eti majuu hakuna ukimwi. Poleni wanawake mnaokumbana na haya maswahiba.

Ushauri kwa dada mtoa mada, wewe concentrate na kujiendeleza kielimu, kwani elimu haina mwisho, ukishapata elimu ya kutosha na kuweza kusimama mwenyewe ukijitegemea utaona mabadiliko, wanaume wanaogopa mwanamke mwenye confidence ambaye anasimama mwenyewe kwa miguu yake, heshima yako itarudi ndani ya nyumba. Pili usitolerate hizo abused behaviour zake, mwambie wazi if you lift your finger I will report you, asijekutia kilema cha uzeeni bure, maana na baridi ya ulaya mtu akuvunje mfupa si anataka kukutia kilema!

Yasinta Ngonyani said...

Nimesoma habari hii kwa majonzi makubwa sana yaani kusikia kuwa bado watu wanafanya hivyo kwa kweli inasikitisha sana. Pole sana mama wawili. Ndoa, ndio ni kiapo kuwa tutatunzani,na kupendana wakati wa raha na shida. Najiuliza je kweli pale unapoitikia unajua maana yake ni nini? Na kama ulimpenda mwenzio sasa kwa nini iwe hivyo? Naamini wewe mama wawili ni mkristo tena ni yule aliyelelewa hapo zamani maana unaonyesha imani, upendo na uvumilivu haswa. Nina mengi sana ya kusema na kukushauri kwa kweli hii habari imenisikitisha sana na pia najisikia mpaka siwezi kuandika hapa..nami nasema kama da.Rachel hapo juu ngoja niichukue hii habri na kuweka pale pangu ili wengi waseme pia. em3 ahsante kwa kukubali kuiweka habri hii hapa.

Anonymous said...

Mimi ni mwaume, tena rijali, nina mke na watoto. Napinga kauli kuwa waanume `ndivyo walivyo' sio wote wenye tabia hiyo.

Mimi ninavyoishi na mke wangu watu wanasema nimepewa limbwata, maana ukinikuta nyumbani, napika nafanya kila kitu ambacho mke wangu anakifanya, tunasaidiana, na hili kwa wenzangu limekuwa gumzo, jamaa kapewa kitu, sio bure.

Kwanza labda nisema watu wengi wanaingia kwenye ndoa kama kutimiza wajibu, kwa kuwa wengine wana wake, na mimi nioe. kwa vile mume anatakiwa kuoa, lakini nini maana ya ndoa, na msingi na msharti yake wengi hawajui.
Kwanza kuona ni `nusu ya dini'
Kuona ni kukamilisha `imani' yaani kabla hujaoa, imani yako ipo nusu, hii ina maana kwamba mke anakuja kukuwezessha wewe ukamilike kiimani. mke anakuja kukupa msaada, na sio anakuja kuwa mtumishi, au bidhaa fulani.

Ndoa ina misingi yake, na mojawapo ni kujaliana, kusaidiana na kupendana,. Hapa unapata mwenza wa kusaidiana, halafu kuna `mawada' yaani raha, lakini pia kuna matokea yake ni kujaliwa watoto nk.

Ukichunguza hiyo msingi kujaliana maana mshirikiane, huwezi kumjali mwenzako kama humthamini, utamjalije wakati umemfanya kibarua, umemfanya bidhaa, umemfanya sio kitu kwako. Hapo utakuwa hujui ndoa na kama nia yako ni kupata mfanyakazi wa ndani , kwanini ujidanganye na kutanagza ndoa, ...nenda shule kwanza ukajifunze nini maana ya ndoa, sio kukurupuka tu.

Mawada, au raha ya ndoa ni pale mnaposikilizana, mkakidhina haja zenu, kama mtu hamjali mwenzake, hiyo raha itatoka wapi, kama hakuna maelewano vipi mtatoshelezana, kwahiyo ukiangalia misingi mikubwa ya ndoa, utakuta inazama kwenye `kusaidiana, kuheshimiana, kupendana, ...' ni kwa ujumla, huwezi ukafanya mwenyewe, mke atachoka, utamchoka...

Sasa hebu nikuuliza wewe uliyeleta hoja, je huko ulaya unaishi kama mama wa nyumbani au na wewe unabeba maboksi, nitashangaa kuwa unaishi huko majuu, halafu unakaa nyumbani tu, wakati upo sehemu ambayo ina uwazi wa kujiendeleza,

Au jamaa kakufungia ndani kama mtumwa, kama ni hivyo, ongea, toa dukuduku lako kwa wahusika, andika maombi ya kusoma kwa makundi yakutetea haki za wanawake, usijifunge, wakati upo sehemu inayothamini wanawake....ajabu kabisa

Hata hivyo kama jamaa kaubana vipi, zipo njia nyingi za kujiendeleza, kuna mitandao, kuna kusoma kwa kupitia mitandao, na hiyo nayo hakuruhusu, duuh, jamaa huyo ni mtu gani huyo....

Mimi nakushauri sana soma maana kama upo huko halafu unarudi bongo bila ganda la elimu, utaendeelea
a kuwa mtumwa, na kuja kujijutia hiyo nafasi uliyoipata.

Nakushauri tena, jitahidi sana kutafuta elimu, kwani hiyo ni fursa adimu, mchombeze jamaa, usome, ukipata ganda lako la elimu, hata usipolifanyia kazi huko, lakini ukirudi huku litakusaidia sana.

Kama unafanya kazi, tumia mshahara wako kujiendeleza, na nikuuliza hawo watoto wawili mliwapataje, maana umesema hata haki ya ndoa huipati...mmh, jamani, mimi nasikia huko Ulaya waafrika wanasifika sana, kuwa ni marijali, sasa inakwuaje, mbona unatutia wasiwasi na huyo mume wako, asije akawa sio riziki, samahani kusema hivi, ila inakera, insikitisha.
mmh, sijui mungu akuepushie na hilo.

Nakushukuru emu3, kama utaiweka hii hoja yangu , najua wewe huna tabia ya kuzitia kapuni hoja za watu. Ni hayo tu