Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, January 6, 2012

Akutukanaye hakuchagulii Tusi
Siku kadhaa nyuma nilikutana na tukio la ajabu, na jana usiku nikaona kwenye runinga watu waliochomewa nyumba kwasababu za imani za kichawi nikaamini kuwa hizi imani sasa zinazidi kukua badala ya kupungua. Na hutaamini tulidhania kuwa mambo hayo yapo kijijini tu, kumbe hata hapa Dar  yapo na yanazidi siku baada ya siku!

Siku hiyo niliwaona jamaa wakijaribu kumuua paka wakidai kuwa eti paka huyo ni mwanga. Hutaamini wakati wenzetu huko majuu wanapenda wanyama kama paka, huku kwetu hasa hapa Dar, paka anatambulika kama mwanga. Kuna watu kabisa hawataki hata kuwaona hawa paka. Nilipoona hawa jamaa wakimfukuza huyo paka kwa hasira nikashikwa na hamasa ya kutaka kujua dhumuni lao ni nini, na kujua ni nini hatima ya yule mnyama mdogo aitwaye paka, lakini kwa muda huo alipandikizwa jina la `mwanga'.

'Huyu paka lazima afe, maana kila siku anatuwangia...'wakasema wale jamaa huku wakiwa wameshika silaha zao,...wengine mawe, wengine magogo, ilimradi yote haya yalitakiwa kumalizikia kwenye mwili  mdogo wa paka ili hatimaye yake ageuke kuwa mfu. Wale jamaa wakawa wanatimua mbio kuelekea pale alisimama yule paka. Na yule paka alipohisi hatari akakimbilia kwenye jengo moja lisilo ishi watu na kujificha kwenye chumba kimojawapo.

'Leo ni mwisho wako mwanga mkubwa wewe, paka shume wewe...'wakasema wale jamaa wanne ambao waliingia kwenye lile jengo na kulizingira kuhakikisha kuwa huyo paka hapati mwanya wa kupitia. Wakapeana mbinu na kuanza kumchokonoa pale alipojificha na yule paka alipoona hivyo akajitokeza huku akihangaika huku na kule kuokoa maisha yake.

'Wewe mwanga leo ndio mwisho wako, wewe mchawi mkubwa, paka shume wewe, leo tutakomesha uchawi wako, wewe paka shume lazima uonje mauti...'yakatolewa majina mbalimbali ilimradi huyo paka aonekane hafai na anastahili kweli kufa, na kama wasemavyo wenzetu kuwa ukitaka kumuua mbwa, kwanza umuite huyo mbwa majina mabaya. Paka akawa keshaitwa majina yote mabaya...

Heka heka za kumtoa yule pala zikafikia mahali ambapo sasa ni shabaha iliyokuwa ikitafutwa, kwani alihsaitokea wazi, na kila aliyejaribu shabaha yake ilikuwa haimlengi yule paka, na yule paka kuona vile akawa kahamaki. Paka ni mnyama wa ajabu sana, huwa akizidiwa na kujua kuwa sehemu iliyobakia ni hapo uliposimama, hukurukia kwa ukali na usipoangalia anaweza akakutoa macho.

'Unaona anavyotoa macho ya kutisha,...mwanga mkubwa huyu...'akasema mmojawapo na kumrushia jiwe, lakini yule paka akaruka upande wa pili.

Yule paka akaanza kunguruma kwa hasira na kutoa meno yake, kwa nia ya kujihami, sasa akawa amewakabili, akionyesha kuwa yupo tayarii kufa na mtu. Hapo jamaa na ujasiri wao wote wakaanza kuogopa, na pale pale yule paka akaruka kwa hasira kuelekea pale waliposimama hawa jamaa.

'Ohh, yalaah....'mmojawapo ambaye alikuwa karibu na yule paka alikoswa koswa na makucha ya yule paka na alipoinama kujihami yule paka akaruka juu ya kichwa chake na kutokomea nje...

'Wewe mwoga sana, unaona umemuacha huyu mwanga ...kapenya upande wako...sasa tumemkosa atatuwangia usiku, nakumbuka siku moja nilimpiga huyu paka jiwe akanijia usiku kuniwangia...'akasema jamaa mmojawapo.

Walihangaika kumtafuta bila mafanikio.

Nilipokumbuka hili tukio nikakumbuka na taarifa iliyoonyeshwa kwenye runinga jana usiku, ikielezea jamaa waliochoma nyumba ya familia moja kwa imani hizi za kishirikina, kuwa familia hiyo ni wachawi, na hata kiongozi mmoja akatoa agizo kuwa viongozi wa maeneo hayo washughulikie hilo swala kwa watu wa namna hiyo wafichuliwe na hata ikiwezekana majina yao yaandikwe kwa siri.

Kitu kilichoniuma sana, ni kuona watoto wa ile familia wakiwa wameongozaan na wazazi wao ambao wanashukiwa kuwa ni wachawi, nikajiuliza je ina maana na hawa watoto pia ni wachawi? au kwasababu ya ule usemi kuwa mtoto wa nyoka ni nyoka? Kwa kweli inasikitisha kwasababu watoto wale watakulia katika mazingira ya hisia za kuogopa,na sijui kama kweli wataweza kusoma kwa raha na wenzao.

Mawazo ya matukio haya yalinifanya nijikute nimeshafika mwisho wa safari yangu na leo nilijikuta nimefika ofisini mapema zaidi, na kama ningelikuwa na lile jembe(komputa) ningeliweza kuandika kisa chetu na hata kufikia tamati kama ingeliwezekana, lakini nilikumbuka kuwa jana niliambiwa nikabidhi kila kitu likiwemo hilo jembe, ...kwani leo ndio siku ya mwisho wangu katika ofisi hii. Nilikubali nakusema `sawa yote maisha..' niliomba nipewe hilo jembe, angalau nitafute `flash' niweze kunakili kazi zangu nilizokuwa nimehifadhia hapo, nikaambulia kicheko, na kuambiwa `unaona huyu jamaa anavyotumia vifaa vya kampuni kuweka mambo yake binafsi, ndio maana anatuulia komputa zetu...'

Wapendwa nia yangu sio kuyasema haya yangu na ofisi yangu, lakini najua katika mitulinga hii ya utumwani baadhi wanaweza kukutana na madhila mbali mbali, hata kusingiziwa mabaya,...usijali lugha zao kwani kwa kawaida akutukanaye huwa hachagu tusi, kwa ushauri wangu ni kuwa unapokutana na majambo kama haya usihamanike, cha muhimu ni kuwajibika katika majukumu yako hadi hatua ya mwisho, timiza wajibu wako katika kazi ulizokabidhiwa. Kumbuka kuwa wema hauozi, na ubaya haulipi katu, na mtoa riziki ni mungu peke yake.

Nawatakia Ijumaa njema na mungu akipenda tutawasiliana zaidi kama nimepata sehemu nyingine ya kujishikiza na nitajitahidi kukiendeleza kisa chetu, ila mkiona kimiya mjue sijapata jembe, na kwenye internet cafe kuna matatizo yake, nyingi zina matatizo na hata wale walionishauri kuwa ninunue modermu, bado nitashindwa kwasababu sina jembe...hata hivyo sijakata tamaa.

TUPO PAMOJA

i: emu-three

6 comments :

samira said...

pole sana m3 mtoaji riziki ni mungu yote haya mungu ndo kapanga inshallah utapata pa kustirika tu
mtoaji ni mungu
tupo pamoja

emu-three said...

Nashukuru sana Samira kwa kunipa moyo mwenyezimungu akujaze heri

Pam said...

pole sana m3,ni kweli riziki haivutwi kwa kamba lkn mlango ukifungwa hata dirishani waweza kupenya.. kila la kheri.

Subira said...

Mimi ushauri wangu ni huu, usiwategemee watu kabisa kuhusu rizki yako, weka ndani ya nafsi yako huku ukiamini kwa dhati kabisa ni Allah peke yake ndio mwenye kujua rizki yako utaipata wapi na kwa njia gani. Hii ni mitihani yake tu inakupata na Inshaallah itapita. Cha msingi na cha muhimu unapoamka kusali Alfajiri uwe unafanya nyiradi za majina ya Mungu ya kuombea riziki kama vile Ya Latwifu na ya Razak, na Ya rahmani. Pia uanze na kustaghafiru mara 100.

Ukitaka majibu ya haraka zaidi, fanya dua hii

weka nia
Soma surat fatiha
Msalie Mtume SAW x 11 kisha uendelee kila siku kwa idadi hiyo waweza kusaidiana na watu kutimiza hiyo idadi.

J2- Lailaha Illa lah x 10000
23- Lailaha illa lah x 11000
J4 - Lailaha illa lah x 12000
J5 - x 13000
Alhamisi 14000
Ijumaa x 16000
Jmosi 17000

AMMY K said...

maskini pole sana em3 mungu atakuwezesha inshaallah. riziki hutoa mungu mwanadamu katu hawezi kukupa hiyo riziki. mtegemee yeye. sina uwezo lakini laiti ningekuwa nao wa kutosha. ningekununulia jembe. umetufunza na kutuelimisha sana kwa kweli. kama utataka michango yetu. tujulishe. tupo nyuma yako ucjali.

Subira said...

Samahani nimekosea namba ya kufanya uradi. Nilikua naandika huku mtoto akinisumbua ni hivi

J2 = 11,000
J3 = 12,000
J4 = 13,000
J5 = 14,000
ALH = 15,000
IJUM = 16,000
J1 = 17,000

believe mimi mkiwa 2 au 3 haiwezi hata kuchukua 2 hours kwa siku.