Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, January 10, 2012

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-72 hitimisho 16




‘Hebu niambie mwenzangu, wifi yangu, ulijuaje kuwa Rose haitwi huko hospitalini..’ akauliza shangazi kwa kunong’ona ingawaje walishatoka sehemu ile alipolazwa mgonjwa baada ya kushauriwa na dakitari kuwa ni vyema wakabakia watu wawili tu mle ndani, na hivyo wakapangiana zamu ya wawiliwawili, kwa kuanzia wakakubaliana kuwa wabakie Rose na Maua maana wao hawakukubali kabisa kutoka mle ndani mpaka atakapozindukana mgonjwa wao.

'Haya mambo yaache tu, na namuomba mungu yaishe haraka iwezekanavyo, kabla sijaamua la kuamua,...maana ni hatari tupu,...usisikie waifi yangu. Maana kila mara nagundua mambo ambayo yananitia shinikizao la damu, na utakuta nayagundua kibahati bahati tu...na kwa njia isiyotegemewa,...'akatulia na kumwanglia mwenzake kwa muda halafu akaendelea kusema;

`Unajua wifi, sasa naamini kuwa mungu ananionyesha kitu, lakini mimi nimekuwa mgumu wa kutambua, na nahisi kuwa mwisho wake nitakuja kujuta...'akasema mama huku akionyesha uso wa mashaka.

'Mimi sijakuelewa maana unaongea tu kama cherahani ukikwepa swali langu...haya naomba unifafanulie vyema maana hapa hakuna mtu wa kutusumbua..hebu nipe kimarefu...'akasema shangazi.

'Wifi nakuomba usiyadodose sana haya mambo, kama ingelikuwa mimi ni wewe nisingetamani kabisa kuyasikia haya ninayokumbana nayo maana hayana wema, yanatishia amani, utaishi ukiwa na wasiwasi wa bure ...'akasema mama huku akishika kichwa.

'Hapo tu, penyewe umeshenitia wasiwasi, maana ulivyoongea hivyo, umeshaniweka kwenye wasiwasi mkubwa, na usiponiambia nitabakia nikiwaza sana, ni heri uniambie tu, kwasababu mimi sio mtoto mdogo kuwa nitaota usiku...'akasema shangazi.

Mama akainama kwa muda akitafakari na mwisho wake akaamua kupasua jipu kwa kusema;

'Sawa, kama upo tayari mimi sina shaka, ila mengine yaishie mimi na wewe, usije ukalogwa kuwaambia watoto, ...'akasema huku akionyesha kidole.
'Hivi wewe unaniona wa juzi au,...'akasema mama na kukiondoa kile kidole alichonyeshwa kwa kwa kuusukuma mkono pembeni.

'Wifi,tangu siku nyingi nilikuwa na shauku ya kujua chanzo cha utajiri wa mume wangu,...nilishindwa kuvumilia, na nikatamani nimjue vyema mume wangu na wapi anapopatia utajiri wake, maana upo muda nilitamani kuwa kama yeye...'akatulia halafu akatabasamu na kusema;

`Unakumbuka tukiwa shuleni, nilivyokuwa nikikuambia kuwa mimi mapenzi ni utajiri, kama mume sio tajiri kwangu ni kama kapuku tu, mapenzi kwangu ni pesa, kama mume hana pesa, sitaweza kumpenda...'akatulia na kutabasamu.

'Pesa ibilisi wifi...'akasema shangazi huku akitabasamu.

'Ndio pesa ni ibilisi kama watu wasemavyo, lakini sio kweli, kwangu mimi, pesa ni sabuni ya roho,...pesa ni kila kitu...unajua wifi pesa kama pesa haiwezi kuwa ibilisi , ibilisi ni watu wenyewe. Mimi nilimpenda sana mume wangu kwasababu ya utajiri wake, kwasababu pesa kwake sio shida, lakini sikujua chanzo ca hizo pesa, na mwanzoni sikujali sana...lakini baadaye..mmh'akasema huku akiangalia juu.

'Baadaye vipi, ulianza kudodosa dodosa nini,...?' akauliza shangazi na kabla hajajibiwa akasema `Sasa kwanini ukadododosa mambo yasiyokuhusu..?' akauliza shangazi alipoona mwenzake haongei kile alichokitaka.

'Hata kama ungelikuwa ni wewe ungelidodosa, kwani licha ya kuwa mume wangu ana pesa, na watu wanafikiri kuwa tunaishi maisha mazuri, lakini sio kweli maana masharti yake ni magumu sana, hata wakati mwingine unaona haina haja ya kuwa na hizo pesa....sipendi kufungwa, sipendi masharti ya namna hiyo yasiyo na maana, na hili limenifanya hata nikosane sana na mume wangu na zaidi sielewani kabisa na wakwe zangu..'akasema mama.

'Mahsarti gani hayo, mbona huyasemi, lakini Ukitaka cha mvunguni sharti uiname,wewe umempenda mume , lazima upende na mambo yake, haya hebu niambie vyema ni mambo gani hayo maana sasa unanitamanisha
kuyasikiliza, na je yanahusuiana vipi na watiti hawa wasio na hatia.

'Siwezi kukuambia hayo masharti, sio muhimu kwako, ila ninachoweza kukuambia ni kuwa Pesa za mume wangu kwa kiasi kikubwa zimefungamana na imani za
kishirikina...'akasema na kugeuka nyuma kuhakikisha kuwa hakuna matu anayewasikiliza.

'Eti nini, mungu wangu, mbona unanitisha...ushirikina gani huo?'akasema shangazi.

'Nilikuambia tangu mwanzo kuwa ingelikuwa mimi ni wewe nisingelipenda kabisa kusikiliza kabisa hayo unayotaka kuyasikia..,na ...hata naogopa hata kukuambia mambo mengine, ....lakini shauri lako kama unataka kusikia mimi sina shida, niendelee au tuyaishie hapa....'akauliza mama

'Endelea bwana, sio kwamba ninaogopa bali nawahofia hawa watoto, je wanafungamana na mambo hayo ya kishirikina na utajiri wenu..?' akasema shangazi.

'Kama wengelikuwa ni damu halali ya mume wangu,natumai tusingelikuwa nao hivi sasa duniani, na kama siku ile usingelikuja mapema, nadhani sasa hivi ningelikuwa naongea mengine...ndio maana nikimwangalia Maua moyo wangu unan
iuma sana...'akasema mama na machozi yakimlengalenga machoni. Na hapo kumbukumbu za nyuma zikamrejea, hasa siku hiyo alipotoka kiliniki na kumkuta mumewe akiongea na mzee mmmoja.

****
'Huyo mkeo ni mja mzito na kama ulivyoambiwa toka awali, tunahitaji damu ya mtoto mchanga, ili kafara letu lifanikiwe, na kama ni mapacha, lazima wote wauwawe maana ni nuksi katka biashara yetu...'akasikia huyo mzee akiongea

'Lakini mke wangu hajaniambia kuwa ana mapacha, licha ya kuwa tumbo lake ni kubwa, lakini hakuwahi kuambiwa hivyo huko kiliniki, leo akirui kiliniki ataniambia kwani nilimuambia akapime kuhakikisha kuwa ni mapacha au la...'akasema mume wake.

'Hivi wewe huna macho, unaona tumbo la mkeo lilivyo kubwa, ile mimba ni ya mapacha, wewe utaona, sasa kama ni mapacha ni bora ujiandae ama wewe ufe, au mke, au hawo watoto mchague wenyewe, ili kuondo hilo nuksi, na hali hiyo imeshaanza kujionyesha kwenye mizimu yetu, unaona biashara zinavyoyumba, hayo yote yameshaonekana na kiujumla chnzo ni wewe na mkeo...'akasema yule mzee.

Kipindi hicho mama ndio karudi na wakati anataka kufungua mlango aingie ndani ndipo akasikia mazungumzo hayo . Alipoikia kauli hiyo toka kwa huyo mzee, akasita kuufungua ule mlango na kuegesha sikio kusikia nini wanachozungumza. Na sura ya huyo mzee ilikuwa ngeni sana kwake.

Mama aliposikia hayo mazungumzo mwili mzima ulisisimuka, akijua sasa amekwisha kwani huko alipotoka vipimo vilionyesha kuwa ana mapacha, na siku za kujifungua zinakaribia, na hapo alikuwa kashika karatasi inaoyoonyesha jinsi mapacha hawo walivyo tumboni.

Ile furaha aliyokuwa nayo baada ya kupewa hivyo vipimo na yule dakitari iliyeyuka na kujaa huzuni na chuki, na kuanza kujuta kwanini hakuitoa hiyo mimba mapema, alikumbuka jinsi mume wake alivyokuwa na mashaka siku alipomuambia kuwa ni mja mzito;

'Unasema una mimba yangu, mbona imekuwa haraka hivyo...?" alisema mume wake huku akishindwa kuficha hisia za kutoamini kauli ya mkewe

'Kwani kuna ajabu gani hapo, au ndio huniamini,sema niskie kuwa umeshindwa kuniamini, nijue moja...'akasema mama huku akionyesha mbwembwe za kujivunga. Na mumewe akaliposikia hivyo akamsogelea na kumkumbatia, na mama akaendeleakuongea kwa kusema;

'Kumbuka tumeanza lini mchezo huo wa mapenzi hata kabla hujanitamkia kuwa unataka kunioa, sasa kipi cha ajabu, ukumbuke mchumba wangu wa huko nyumbani nilimbania kwa kumuahidi kuwa mpaka tuoane ndio tukutane kimwili,lakini wewe nikawa nakukabidhi kila kitu, nikijua kuwa wewe ndiye ninayekupenda, sasa nashangaa ukionyesha uso wa mshangao, au kama hutaki hii mimba nikaitoe....'akasema mama.

Alipotamka kutoa mimba, mume wake aliruka na kumsukama pembeni akasema kwa hasira,;
'Eti nini, utoe mimba, Hapana, hapana, wewe usije kufanya hivyo, ukifanya hivyo, utaniangamiza hata mimi mwenyewe, kuna mambo ndanii ya familia hayaruhusu kabisa mamboo hayo, ni bora azaliwe na ....'hakumalizia haya maneno simu ya mumewe ikasikika kulia na kukatiza hayo mazungumzo.

********

Mama aliposikia hayo mazungumzo ya mumewe na huyo mzee akajua kweli ndio maana mume wake alikuwa ana mashaka, ina maana katika familia yao lazima kuwe na kafara la damu ya mtoto mchanga ili kuwezesha matakwa ya mizimu yao ...

Hapo mama akahisi kizungu zungu, alichofanya ni kuificha ile karatasi ndani ya nguo zake za ndani kabla hajapoteza fahamu , kwani baadaye alidondoka na kupoteza fahamu ,alipozindukana alijikuta yupo kitandani akiwa kasimamiwa na dakitari na mumewe.

'Vipi mke wangu unajiskiaje?' akauliza mume wake.

'Kwani kumetokea nini?" akauliza mama kwa mshangao mshangao.

'Tumekukuta mlangoni ukiwa umezirai na mimi haraka nikamuita dakitari, tukakuingiza ndani na dakitari anasema ni kwasababu ya mimba, ....'akasema mum wake.

'Na yule mzee yupo wapi? 'akauliza mama kwa wasiwasi.

'Mzee gani huyo...?' akasema mume wake kwa mshangao.

'Wewe hukuwa ukiongea na mgani humo ndani, mtu wa makamo...?' akauliza mama kwa mshangao.

'Hapana, muda wote nilikuwa peke yangu, naona umeota...'akasema mume wake na kumuacha mkewe hoi, kwani ana uhakika alimuona mzee mmoja akiongea na mume wake,

Ikawa mara kwa mara anamfuma mumewe akiongea na huyo mzee, lakini hakuwahi kukutana ana kwa ana na huyo mzee, na cha ajabu huyo mzee hutoweka kiaina, kwani hata pale mama alipomsubiria kwa nje ili akitoka amuone hakuwahi kumuona akitoa nje, na hali hii ilimfanya aishi kwa mashaka kwani alihisi kuwa mzee huyo yupo humo ndani au sijui kajificha wapi, ambapo hapaonekani.

Mara nyingine mumewe, alikuwa akitoka kitandani na kumuacha mkewe akiwa kalala,na mkewe alipofuatilia kwa nyuma, alimuona mumewe akiongea na huyo mzee, hasa kipindi cha usiku na kitu alichokuja kugudua ni kuwa mara nyingi akitokea huyo mzee wa ajabu,lazima kuna tukio la ajabu litatokea, kama sio mtu kuuwawa kiajabu basi unaweza ukaona ngombe au kondoo amechinjwa na yote hayo alijua ni kwasabbu ya kutafuta utajiri.

Siku aliyokata tamaa na maisha na mumewe ni pale aliposikia mazunguzo na katika kuongea kwao,akasikia huyo mzee akisema kuwa yeye ni mkosi katika hiyo familia na inabidi auwawe au mtoto wao auwawe maana inaonekana wazi kuwa mkewe kamuleta damu ambayo siyo ya familia kwahiyo lazima mkosi huo uondolewe, na hauwezi kuondolewa bila ya damu ya mtu...na mtu huyo si mwingine na huyo huyo binti....

NB Je ilitokeaje baadaye



Ni mimi: emu-three

3 comments :

AMMY K said...

mmmh si mchezo. ni noma.

Rachel Siwa said...

Eeeehhh ndugu yangu weee Mungu akubariki sana kwa kazi za mikono yako,yaani wee acha tuu,mimi penda sana ndugu wa mimi,Pamoja daima!

Yasinta Ngonyani said...

Duh! haya mambo ya ushirikiana ni kazi kwelikweli. Yaani umekatisha hapa nilikuwa nataka kujua itatokea nini? Yaani watu mpaka leo bado wanaamini mambo kama haya ukiofanya hivi basi utakuwa tajiri? na huyo mzee atakuwa nini? NASUBIRI KWA HAMU KUJUA HAYA MASWALI YANGU.