Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, December 7, 2011

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-59 hitimisho-3

‘Mimi sikuja hapa kwa ajili ya ule ugomvi wetu, yale yalikwishapita, na haki yako ulikwisha ipata, na kuja kwangu hapa sikujua kabisa kuwa nitakutana na wewe, kumbe huyu binti ni wa kwako, namfahamu sana, …’akaongea Inspketa akimwangalia Maua.
‘Ulimjulia wapi binti yangu, maana nyie maaskari hamna dogo, huyu ni mke wa mtu na nina hamu sana ya kusikia jambo lililokuafanya uje kwa binti yangu huyu ana kosa gani hadi umtafute, …?’akasema shangazi mtu akimwangalia huyo askari kwa macho ya mashaka.

‘Usiwe na shaka kabisa, binti yako nilionana naye huko nchi ya jirani katika shughuli zangu, nilikuwa huko kwa mkataba maalumu, na katika utendaji wangu ndipo nikakutana naye, ila kila muda unaopita naingiwa na wasiwasi kuhusiana na yeye, maana habari niliyoipta huko kwa mara ya mwisho ni kuwa Rose kaenda Ulaya kusoma, na hata siku za kesi hakuweza kuonekana, na cha ajabu hata mumewe alitoweka kiajabu, kitu ambacho kiliwafanya washukiwe kuwa wana uhusiano wa namna fulani, au kuna jambo ambalo wanalijua na linaweza kusaidia kulimaliza kabisa hilo kundi. Kundi hilo ni hatari hata kuloko wapiganaji wa msituni….’akasema Inspketa.

‘Kundi gani hilo maana sijakuelewa unaongea nini na binti yangu anahusikanaje na kundi hilo…?’akauliza shangazi mtu akiwa na wasiwasi kidogo.

‘Huko nchi ya jirani kuna makundi mengi yanayoipinga serikali, kuna makundi yaliyopo msituni, lakini kuna makundi yaliyokuwa yameandaliwa kitaalamu, kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu sana kuyajua,…haya yalijengwa na wataalamu wa Nyanja mbali mbali. Nikisema wataalamu nina maana kuwa ni watu wafanyakazi na nyazifa zao, kwa upande mmoja, lakini kumbe ni watu waliojifunza upiganaji kwa upande wa pili.

‘ Huyu mgunduzi wa makundi haya, ambaye ndiye mfadhili mkubwa alikuwa akiishi nchi za nje, alibuni njia hii mapema kabisa, akatuma wataalamu na silaha, na alichofanya ni kuwakuasanaya wale watu alioona wanafaa akawapika kisawasawa na pia kuwafunza vijana wengine toka vyuo vikuu, ambao walipomaliza masomo yao waliajiriwa na huku wanakujua jukumu lao jingine.

‘Kwa mfano binti yako alikuwa kaajiriwa katika hospitali mojawapo ya watu hawo, anaijua vyema sana, lakini hakujua nini kinachoendeela hapo, sizani hadi hatua ya mwisho kama alijua kuwa kuna watu kama hawo, kwani ilikuwa ni siri kubwa sana, na sisi tulipogundua hilo tukaamua kumfanya yeye kama chambo…’akasema inspekta huku kakunja nne kwenye kiti.

‘Maua alikuwa akitaka kuingilia yale maneno, lakini kila mara alipotaka kutamka kitu shangazi alimwahi na kumuonyesha ishara ya kutulia. Na inspekta bila kujua kuwa anamwaga mama kwenye kuku wengi akaanza kueelezea mambo yalivyotokea huko nchi jirani, akiwa kama mkufunzi na mtaalamu aliyepekwa kusaidia kuleta amani nchi ya jirani.


*******
Mkuu wa ile hoteli alijikuta akiingia kwenye mapigani ndani ya hoteli yake mwenyewe, kinyume na makubaliano na muajiri wake, ambaye alishapata taarifa kuwa bosi wake huyu ambaye ni mumiliki wa hiyo hoteli yupo njiani kuja hapo, aliona ni bora kuliingilia kati hilo tatizo na kuhakikisha kuwa bosi wake akija mambo yamekwishatulia, hakuwa na jinsi....

Akawa anawasiliana na Inspketa akiwa kwenye mitambo yake, kwani kundi hilo liliamua kuleta wapiganaji wake ili kujibu mashambulizi baada ya kusikia kuwa kuna watu wao wamenaswa humo ndani na hawo jamaa wakikamatwa siri kubwa itakuwa imefichuka. Kitu kilichogundulika ni kuwa kundi hilo lilimuhitaji Rose na mwanaume anayesadikiwa kuwa yupo naye,…na kitu ambacho kilihitajika ni kujua kwanini Rose na huyo mume wake walikuwa wakihitajika sana, na hawo watu, ndio maana binti yako anahitajika na mume wake.

Ndani ya hiyo hoteli kundi hilo lilipandikizwa watu wao, ambao kazi yao kubwa ilikuwa kuchunguza chumba baada chumba, kama watawakamata hawo watu wanaowatafuta. Ni wakati huo huo kundi letu la serikali la vijana waaminifu nalo lilishawaingiza wapiganaji, cha jabu vyumba vingi vilishachukuliwa, lakini haikutushinda kitu, licha ya kuwa asilimia kubwa ya vyumba humo ndani vilikwa vimeshikiliwa na wao.

Ndani ya chumba maalumu ambacho kilikuwa kikitafutwa ndipo walipokuwepo Rose na mtu wake, ambaye kwa Inspkta alimtambua kama mume wa Rose, na hapo alishaweka watu wake kwa ajili ya kumsaidia mkuu wa usalama wa hiyo hoteli baada ya kuwasiliana, na baadaye iliwashangaza kwani walipoingia humo chumbani, walimkuta Rose kalala, na mwenzake hayupo.
‘Rose vipi mumeo yupo wapi, maana anatafutwa na hawa majambazi..’akaulizwa Rose na Inspekta.

‘Sijui, nilipitiwa na usingizi baada ya kukesha naye usiku kucha, akiwa kazirai, nilihangaika naye bila matarajio lakini sikuwa na jinsi ya kufanya, kutokana na hali niliyoiona huko nje, …lakini alionyesha dalili njema, ndio maana sikuwa na wasiwasi sana..sijui kenda wapi mungu wangu...…’akasema Rose akiwa na wasiwasi akitaka kutoka nje,lakin wale maaskari walimuia, na msako mkali ukapita bila mafanikio ya kumuona huyo mume wake...

‘Huko nje mapigano yakazuka, kwani hawo jamaa hawakukubali kusalimu amri, na haikujuliakan wapi walipopata silaha kwa mara ya kwanza, na hili liligndulika baadaye kuwa miongoni mwa maaskari tuliowaamini walivujisha siri na alipoingia yule mumilikia wa hoteli baadaye, akawa anawasiliana na watu wa kwetu kinamna ambayo hatukuelewa mwanzoni, lakini hata hivyo ilitusaidia kumnasa mtu mmojawapo mkubwa aliyekuwa ndani ya serikali…hilo siwezi kuwaeelzea zaidi …

‘Jinsi silaha zilivyopenya ilitutatizo kidogo, lakini baadaye tulimnasa kijana wa kwetu ambaye alitumiwa na watu hawo, akapenyesha silaha na kuingia mikononi mwa hawo majangiri, na ilikuwa kazi kubwa sana, ikizingatiwa kuwa hawo jamaa waliiva kwa vita, sio mchezo, lakini tuliwashinda kwasababu walikuwa wachache na walizingirwa ndani ya jengo,na tukawshika mmoja baada ya mwingine, na walikaidi wapambana na mkono wa sheria…’akasema Inspekta.

‘Sasa huyo mume wa Rose alitowekaje, asionekane…?’akauliza shangazi.

‘Mwanzoni tulizania kuwa Rose anajua wapi alipo, lakini tulipofatilia mitambo yam le ndani tuligundua kuwa alizindukana wakati Rose kalala, na alionekana kama kuchanganyikiwa hivi , kwani alipoamuka aliangalia huku na kule na alipomuona Rose kalala karibu naye akamwangalia kwa makini, na bila kumwamsha akatoka mle ndani, …alipofika nje na kusikia milio ya bunduki alirudi na kuvaa koti refu na kofia, na kutoka bila hata mti kumjua…’akasema Inspekta .

‘Hapo sijapaelewa, atoke katika hali kama hiyo bila kujulikana, halafu akaenda wapi?’ akaluiza shangazi akiwa na hamu ya kusikia zaidi, kwani alikuwa kama anahadithiwa cinema fulani anayoipenda.

‘Pale ilikuwa rahisi kwake kutoka, maana mtu kutoka mle walipokuwa wamefichwa ilikuwa ni rahisi, kwasababu hakuna aliyekuwa akijali,mtu anayetoka , ila kuna kauzembe kalifanyika kidogo, walinzi wetu walikuwa wakihakikisha kuwa hakuna mtu anayeweza kuingia, na kwahiyo alipotoka, walihisi kuwa ni mimi, niliingia na kutoka kwa njia hiyo, na alipotoka akatoweka kinamna, na hakuonekana hadi aliporejea wiki liyopita wakati nikiwa huko na wakamkamata, sikuwa na jinsi ya kufanya, kwasababu na mimi nilikuwa nahitajika huku nyumbani,….’akasema Inspekta.

‘Na huyo Rose walimfanyaje, maana hujaniambia vyema kuhusu yeye..’akauliza shangazi na kumwangalia Maua. Na inspekta naye akamwangalia Maua na kutabasamu akasema;

‘Binti yako ni mjanja sana, kwa kipindi kifupi nilichofahamiana naye , niligundua kuwa ni mtu jasiri licha ya fani yake ya udakitari, lakini ni mtu anayeweza kupambana kama askari…unajua hapa nilipo ninashindwa kuamini, kwani hapa kabadilika kuliko maelezo, kiasi kwamba nawaona kama watu wawili tofauti, sijui…’akasema Insepkta huku akimwangalia vyema Maua na kumlinganisha na yule binti aliyekuwa naye akiwa na nywele kama za mzungu.

‘Wewe mwenyewe umekiri kuwa yeye ni jasiri, na uajsiri hasa wa kupambana na watu inabidi ujiabdili kutegemeana na watu, haya nieleze ilikuwaje baada ya hapo?’ akasema shsngazi mtu.

‘Zaidi ya hapo askari wakalivamia lile jengo na kuwakamata wote waliohusika, hutaamini kuwa mumiliki wa hiyo hoteli alikuwa mshirika wa karibu wa huyo mkuu wa hilo kundi, …alipofika uwanja wa ndege vijana wetu walimuona wakawa wanamfuatilia, bila yeye kujua, na hakufika moja kwa moja hotelini kwake, alifikia hoteli nyingine, ambayo kumbwa na mumilikiw ake anahusika pia, humo waliweka kambi ya muda, ilikuja kugunduliak silaha nyingi kwenye hiyo hoteli.

‘Huyo mumiliki alipotoka hapo alikuwa kajibadili sura, na kuingia hotelini kwake kama mtalii tu, na alipofika kwenye chumba alichopewa, akaanza shughuli zake za kuwasilina na wenzake, huku akitoa amri za mapigano, kazi ikaanza, lakini kwa vila tulishajiandaa, haikutupa shida kabisa,na tukaja kumnasa kirahisi, ila alikaidi na kwenye mapigano na kupoteza uhai….’akasema Inspekta huku akiangalia saa.

‘Na kwa Rose ilikuwaje, maana hujaniambia kuhusu yeye..?’akauliza shangazi.

‘Ina maana hajakuambia mwenyewe, nini kilitokea, …?’ akasema inspekta na simu yake ikawa inaita, …akaipokea na kusikiliza kwa makini, halafu akamwangalia Maua.

‘Hali ya mume wako ni mbaya sana, wamemtoa kule jela alipokuwa kaweka na sasa hivi kalazwa hospitali ya serikali, ….’akasema Inspekta, `Na kuna kitu wamekigundua, kuwa huyo mume wako aliwahi kulazwa tena hapo akiwa na tatizo la kichwa, tatizo hilo limeongezewa alipokuwa huko jela, kama ilivyo kawaida ilibidi watumie njia za ziada kupata taarifa walizozitaka, ingawaje haikufanikiwa kwani wakati wanahangaika naye akapoteza fahamu na hakuweza kuzindukana kwa muda wote waliokuwa naye, ikaonenakan haina haja ya kuendelea kukaa na mtu kama huyo, wakati ahwana vifaa zaidi …ndio wameamua kumtoa hospitali ya jeshi na kumpeleka hospitali ya serikali.
‘Mara ya kwanza alipolazwa walijua kuwa alitokea wapi na jina lake mnalijau kuwa ni nani? ‘akauliza shangazi.

‘Hilo ndilo tunataka kuongea na binti yako, najua wanajuana walikutana wapi, kwani uchunguzi uliofanyika haujagundua wapi huyu mtu alitokea, kwani kipindi kingi alichokuwa kalazwa, alikuwa hana kumbukumbu, …na cha ajabu hata Rose hakuwahi kuandikisha jina sahihi la mume wake, alitumia jina la `Sweetie…’ jina moja tu, kitu ambacho madakitari waliompokea sasa hivi wanashindwa kuelewa kwanini wenzao hawakuwa na kumbukumbu za kutosha za huyo mgonjwa, na hivyo basi Rose ni muhimu kuwepo huko kujibu maswali yote hayo, kwasababu hata docta Adam, ametoweka, haijulikanai kaenda wapi..kuna mambo huko…lakini atapatikana tu…’akasema Inspecta.

‘Nini, eti, `Sweetie…’akasema Maua kwa kushangaa huku akingalia juu na baadaye akatabasamu..

‘Sio ndivyo ulivyoandikisha, hayo majina yenu ya kimapenzi mnayatumia hata mahali pasipohusika, kwani huyo mumeo jina lake halisi ni nani..?’akauliza Inspecta na kabla Maua hajajibu kitu, shangzi akaingilia na kati na kusema;

‘Naona hayo tutayaongea baadaye…kwanza tumalizane na moja kabla ya kuingilia maswala mengine ya majina, nilikuwa na wasiwasi na taarifa yako, una uhakika kweli unamfahamu binti yangu vyema…?’ akauliza shangazi mtu.

‘Kwanini unaniuliza swali kama hilo wakati nimekwisha kuambia kuwa nilikutana naye nchi ya jirani, Rose hebu niambie hatukukutana huko nchi ya jirani..?’

‘Nchi ya jirani ipi hiyo…?’ akauliza Maua.

‘Nina maana Uganda, kwani wewe umewahi kufanya hiyo kazi yako nchi ngapi, mimi ninamaanisha nchi tuliyokutana na wewe, hizo nyingine ulizowahi kufanya kazi sina umuhimu nazo, inaoenakana umefanya kazi sehemu nyingi eeeh, lakini kwangu sio muhimu sana…mimi namaanisha Uganda, wakati upo huko na docta Adam, …na…’ akakatizwa na simu , ikabidi atoke tena nje kuongea, aliporudi alisimama na kuwaangalia hawo watu wawili kwa makini, bila kusema neno.

Shangazi naye akamwamgalia Inspekta akiwa na lengo la kutaka kumwambia ukweli, lakini kabla hajasema neno simu ya Inspeta ikaita tena, na Inspekta akatoa tafadhali na kuelekea nje,akijua hiyo simu ni ya kikazi na ni muhimu sana,hakutaka kusikilizia hapo akatoka nje na kuwaacha Maua na shangazi yake wakiangaliana.

‘Shangazi mbona mimi sielewi, au kuna kitu kinaendeela hapa mimi sikijui, huko nchi ya jirani niliwahi kufika lini, na kama tunakwenda huko, mimi inanihusu nini, msinichanganye na mambo yenu, mimi huko siendi kabisa, kwanza nitamuelezaje Maneno,..’ akasema Maua kwa sauti ya chini chini, na alipoona shangazi yake hamjibu kitu akasema `Huyo polisi akija hapa nitamwambia kabisa mimi sio Rose, kama kuna mhalifu anaitwa Rose, anamfananisha na mimi, akamtafute huko huko, mimi na polisi mbali mbali, kwanza hapa natamani kutapika,..’akasema Maua huku akishika mdomo.

‘Na hilo ndilo linalonifanya mimi na wewe twende huko huko, ukamuone huyo Rose anayemfananisha na wewe,…hebu jiulize mpaka polisi anakufananisha na huyo mtu, huoni kuwa..., wewe subiri kwanza, kwani kuna mengi huyajui na ulishaanza kuniuliza maswali mengi kuhusiana na hilo jina Rose, sasa kama unataka kupata jibu la swali lako hilo ni bora twende hiyo safari,…ila nina wasiwasi na huyo mgonjwa, ni nani huyo, nahisi kitu, huyo anayeumwa kama sikosei atakuwa ni …..

Kabla hajasema kitu Inspketa akarudi na kusema,

‘Kesho nahitajika kwenda huko nchi ya jirani, licha ya kuwaomba kuwa mke wangu ni mgonjwa, lakini wamesema hiyo safai ni muhimu sana lazima niwemo, kuna mambo ya kwenda kumalizia, sasa nikaongea na wakuu zangu kuwa kuna watu wawili nawahitaji sana kutoa ushahidi muhimu sana, nia kubwa ni nyie muwepo kwenye hiyo safari, nikawaomba viti viwili kwenye ndege yetu kwa ajili yenu,mnasemaje….?’ Akasema Inspekta akiwa na uhakika kuwa ombi lake litakubaliwa.

‘Kwanini tuwemo, mbona mimi bado sijaelewa…?’Maua akaanza kujitetea, lakini shangazi akamkatiza na kusema `Tutafurahi kuwepo kwenye hiyo safari, kwasababu ni ya dharura na ni muhimu tukamuona huyo mgonjwa ili tuone tutamsaidiaje umesema jina lake anaitwa Sweetie..hahaha, mambo ya mapenzi hayo wanayapeleka hadi kusipofaa, kwanini msiandikisha jina lake..?’ akasema shangazi huku akijifanya kumwangalia Maua,alishaona kuwa ni vyema hali hiyo ikabakia kama ilivyo hadi atakapohakikisha hicho anachohisi kuwa ndicho

‘Shangazi huyo mgonjwa ni…?’akataka kuuliza Maua kwa hasira, na shangazi akamfinya na kumfanya Maua anyamaze kimiya, kwani hiyo ni ishara ya shangzi yake anapomkataza kitu. Na inspekta aliona lile tendo tendo akawaangalia kwa jicho la kujiiba, halafu akageuka kuondoka, na alipofika mlangoni akasema;

‘Basi jiandaeni,na kwa vile hiyo ni safari ya dharura, kinachotakiwa ni kibali cha dharura, na hilo nitalifanyia kazi mwenyewe, nitawapigia simu baadaye mnipe majina na kumbukumbu zenu kamili, ili niweze kuzijaza kwenye hicho kibali cha dharura, nataka ikiwezekana tukayamalize haya mambo kabisa, ili hata binti yako akirudi huko asiwe katika mashaka mashaka, na bado sijaongea naye, kuna mambo nahitaji kutoka kwake, na hayo nahitai kuongea naye peke yake, lakini sio leo, kwasasa hivi nahitajika haraka ofisini, jiandaeni kwa safari, mtachukuliwa kesho, kama mpo tayari lakini…’ akawaangalia kwa makini kwa muda.

‘Sawa tutawasiliana afande…’akasema shangazi mtu akimwangalia binti yake.

‘Na mjue tutasafiri na ndege ya jeshi,…’akaongezea Inspekta, akimwangalia Maua tumboni, moyoni akisema mimba yake bado ndogo haiwezi kusumbua.

‘Hamna shida mimi mwenyewe niliwahi kupitia jeshi kwa mujibu wa sheria, nikapitia mgambo, na huko niliwahi kupewa kazi maalumu, kwahiyo safari kama hizo niliwahi kuwepo…usijali na huyu nitamlinda mwenyewe…’akasema shangazi na Maua akamwangalia shangazi yake kwa uso wa kutahayari.

‘Namba yangu ya simu hii hapa…’akawapa kadi na kuondoka na kabla hajatoka mlangoni gari la Maneno likaingia….

NB. Najua bado kuna sintofahamu nyingi kuhusiana na hiki kisa, lakini hitimisho hili ambalo lina sehemu nyingi, litamaliza mengi kati ya sitofahamu hizo, naombeni tena, kama kuna sehemu tumeruka, hazikueleweka, tuambizane, ili kisa hiki kiishe vyema, nawashukuru sana wale ambao wamenidokeza wapi tumesahau au nini kinatakiwa kiongezwe au kifanyike.., na hilo ndilo lango langu, Tuweni pamoja.

Ni mimi: emu-three

3 comments :

Yasinta Ngonyani said...

Naona kama unatupeleka huku na huku ila tupo pamoja ndugu yangu..

AMMY K a.k.a mimi said...

daah siku nyingi sikuiingia humu cause ya kuumwa ila tupo pamoja cijaona uliporuka naona mambo bambam.

Subira said...

Wala hakuna chasintofahamu wala mkoroganyo, hivi ndivyo hadithi za flashback zinavoandikwa. Hongera sana endelea hivyo hivyo utafika mbali sana! Lazima uwaweke wasomaji kwenye suspense!

Subira