Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, October 24, 2011

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-41



Adamu alabakia ameduwaa bila kusema kitu . akataka kutamaka neno, lakini mdomo ukawa haufunguki, moyo ukawa unamwenda mbio, katika hisia za ajabu, huku macho kayakodoa kuangalia mlangoni. Alijaribu kukumbuka jinsi gani hali kama hii imeanza kumtokea lini, kwani kwa ujasiri wake aliojijengea hasa baada yay ale mafunzo aliyopewa, angeliweza kujizuia na kupambana na hisa zozote ….lakini sio vile akikutana na huyu …..amegundua kuwa hali kama hii imekuwa ikimtokea mara tu anapokutana naye, na hali hii ilimuandama kipindi kile cha ujanani, na alipokumbuka hivyo, akabenua mdomo na kutabasamu, halafu aaksogea mlangoni na kunyosha mkono wa kukaribisha, hakutaka uwe mkono tu, alitamani angemkumbatia…lakini akajua kuwa sio vyema…huenda ….
‘Vipi docta mbona unakuwa kama mtu aliyeona mzuka fulani,…vipi kwani hukutarajia kuniona lmimi tena, kwanini uwe hivyo, kwanini umeduwaa kiasi hicho…’ akauliza huyo mgeni aliyesimama mlangoni.
‘Sijui nikuambieje,…’akasema huku akitoa tabasamu lake lote. `Hali kama hii ilikuwa inanipata kipindi kile cha ujanani, wakati damu inachemka, kipindi ambacho nilikuwa natafuta ….sasa umri kama huu nateseka kiasi hiki…kwakweli inanipa jakamoyo la aina yake…kwa ujumla moyo wangu umekuwa kama mtu aliyekuwa na kiu mara ghafla maji yakaonekana…lakini maji hayapo mkononi mwangu, natamani niyanywe na kiu ni kali sana, …sijui mtu kama wewe ungelifanyaje…’ akasema Adam huku akiwa bado katabasamu.
‘Mhh, Adamu, kwanini upate shida, mimi kama ningelikuwa wewe, nisingelisumbuka, kwani maji siku hizo yapo mengi madukani, ya kila aina…ningelienda dukani kutafuta maji mengine , nikanywa kiu ingelikwisha….lakini maswala mengine ni ya kujitakia, kwanini ujitese moyo wako na kitu kisichowezekana, na kwa ujumla Docta sina muda mwingi, nimekuja mara moja na natakiwa ni rudi mjini…kama ulivyoshituka kuniona ndivyo ilivyo kuwa sikutakiwa kuonekana leo hii hapa, nilitakiwa niwe huko mjini mpaka kieleweke, mpaka uchunguzi utakapokamilika,…ila, nimeona sio jambo jema kuhini ahadi, ahadi ni deni… kwahiyo nimeruhusiwa kwa masharti ya muda maalumu, …’ akasema huyo mgeni
‘Najua hilo …na inglikuwa mimi ndio wewe, ningelifanya hilo mapema sana…kwa ujumla nimeshangaa sana kukuona hapa leo, kwani nilivyosikia ni kuwa wamekushuku kuwa wewe ulihusika, au unajua chochote na kifo cha yule mtu aliyeuwawa kwenye hiyo hoteli uliyokuwa umepanga, …ni swala la muda tu, lakini hata hivyo swala la mauaji sio la kuchezea, unaweza ukaozea jela ndio maana kwa kukujali nikakutumia wakili…’akasema Adam.
‘Kwa kunijali au kwa kujali maslahi yenu, mimi nisingependa kuwaingilia mipango yenu, lakini mnanisikitisha sana pale mnapowaumiza watu wasio husika kabisa…na hata kuwaua watu wasio na hatia, …nini mnachokitaka katika dunia hii, kuwa mtaishi milele…hakuna atakaye ishi milele, …mwisho wa kuuwa wengine ni kuishia kuuliwa tu…nini kinachotafutwa hapa…sielewi kabisa, ..eti utajiri, ni nani aliyekufa na utajiri wake, hakuna…hata mkilimbikiza mailioni ya mapesa hata mkiwa matajiri wa kupindukia, lakini ipo siku mtaondoka, ipo siku mtakufa kama hawo mliowaua, tumeona wagonjwa wangapi wanakuja kutibiwa matajiri wana kila kitu wanakuja na mapesa yao na kuomba kuwa tuwasaidie wasife, lakini wapi…muda wao unafika wanaondoka, huku tukiwa tumefanya kila aina ya juhudi, pesa zao, utajiri wao haukusaidia kitu…’ akaongea huku machozi yakimtoka.
‘Adamu , inaniuma sana, sikutarajia mtu kama wewe, …sikutarajia kabisa,….kuwa unajihusisha nan a mambo kama haya…inaniuma sana…kwahiyo..nimekuja kuwapa mapesa yenu, ili msiendelee kuniandama, msisendelee kuziandama roho za watu wasio na hatia…manachotaka ni nini , ni pesa, haya pesa zeni hizi hapa…..’akasema yule mgeni akiwa kavaa mawani meusi kuficha macho yaliyokuwa yalkitoa machozi, na Adamu aliyaona yale machozi, yakitiririka hadi chini kidevuni, na yeye hisia za huruma zikamteka, kitu ambacho humjia kwa muda mfupi, lakini akiwa hayupo kwenye uwanja wa mapambano, yeye kwake alijua kuwa yupo uwanja wa mapambano, anapambana na wale wasiotaka wengine wapate maisha bora….akamsogelea mgeni wake na kumshika mkono na kumsindikiza hadi kwenye kiti na yeye hapo hapo akaona hisia za machozi zikimlenga lenga.
Hisia hizo zilipomteka moyo wake, akageuka na kuangalia dirishani na taswira za kimaisha zikapitiliza dirishani na kwenda mbali kabisa…, hali ile ilimtia uchungu sana, na hata yeye alishajiuliza mara nyingi, ni kwanini akajishirikisha na hawa watu, nini lichokuw akikitaka, ni pesa, ni utajiri…hapana ni zaidi ya hayo, ni uchungu wa kile alichokiona, ….uchungu wa jinsi gani watu waliopewa madaraka, wanavyofanya, ….wanavyokula mali ya wanyonge, bila huruma, …nia na lengo lake ni kuhakikisha amewaondoa hawo na ikibidi haki itawale na mali ya wanyonge ibakie mikononi mwao,…aliona kuwa hakuna jinsi nyingine, ….ila hiyo ianayokwenda nayo, ….ilikuwa kama mchezo tu, na hatimaye akawa ndani kabisa ya bahari ambapo alipotoka ni mbali na anapokwenda ni mbali, haoni wapi aelekee, ila alichojali ni upepo unavyomtuma ….sasa je afanyaje, akajitosa na kuanza kuogelea.
*********
Alipoanza ajira alikuwa na ndoto ya kuwa dakitari mkubwa sana, kutokana na akili yake ilivyokuwa kubwa shuleni, tangu alipoanza darasa la kwanza hadi chuo kikuu alikuwa anafanya vizuri katika mitihani yake,na hata walimu wake walimuweka katika kundi la wanafunzi wenye vipaji maalumu. Akafaulu hadi chuo kikuu, katika nyanja ya udakitari, na hata alipomaliza chuo kikuu alijiona hajafikia pale alipopataka, akaomba kwenda kusoma nje, kwani alikuwa na sifa zote…., lakini kwa upendeleo uliokuwepo hakuweza kwenda kusoma nje, nafasi yake ilichukuliwa na watoto wa wakubwa ambao alikuwa akiwazidi sana kimasomo, …alafanya kila juhudi lakini hakufanikiwa hana pesa, hana refa …hana…hapo akaanza kuvunjika moyo, lakini bado ndoto yake yakuwa mmoja wa madakitari bingwa haikumuondoka kichwani.
Alikuja kuajiriwa kwenye hospitali za serikali na kuanza kupambana na maisha, alitumia muda mwingi kujisomesha zaidi ili afikie hatua ya juu, na kweli baada ya muda akarudi chuoni kusoma zaidi na hatimaye akafikia hatua ya udakitari bingwa, lakini kilichomkwaza zaidi ni kuwa kipato alichokuwa akikipata kilikuwa hakilingani kabisa na ujuzi wake, na hasa ukilinganisha na wenzake waliokuwa wamekwenda kusoma nje….akaona atafute mbinu nyingine,….
Katika kuhangaika huku na kule akakutana na wenzake aliosoma nao ambao walibahatika kwenda nje walimshauri atafute hospitali za watu binafsi na kufanya kazi kwa muda wa ziada, wao wapo tayari kumuunganishia kwa hilo, hasa huko wanapofanyia. Basi akawa anafanya hivyo, …anahangaika mchna kutwa katika hospitali za serikali, na ikifika muda wa kuondoka, anakimbilia hospitali za watu binafsi kufanya masaa machache yaliyobakia , hata ikibidi hadi usiku wa manane, na hali hii ilimchosha sana, kwani alikuwa hana muda wa kupumzika.
Siku moja, akakutana na rafiki yake wa siku nyingi , akamshauri kuwa kuna hospitali inafunguliwa na mmoja wa wahusika wakubwa wa hiyo hospitali ni baba yake , na yeye ndiye alitarajiwa kuwa mkuu wa hiyo hospitali, lakini yeye hapendi kabisa kufanya kazi hapa nchini, ndoto yake ilikuwa kwenda kufanya kazi nje ya nchi na keshafanikiwa, …alisema kuwa wazazi wake wamekua juu kwa hasira, kwani wao juhudi zao zilikuwa kwake, walishamuandaa kuchukua nfasi hiyo, sasa amewasaliti…aliwaambia kuwa atawatafutia mtu anayefaa, kwa kazi hiyo, ndio maana amekua kukutna naye, kama yupo tayari, masharti ni kuwa aachana na kazi serikalini ….na kukubalina na msharti machache, na pia kuna mafunzo machache anatakiwa kuyapitia, kama yupo tayari yeye atamuunganishia…!
Adamu alishawaza sana kuachana na kazi za hospitali za serikalini, lakini hakujua aende wapi, kwani kila alipojaribu walikuwa wakimtaka,lakini sio kwa wadhifa kama huu aliopewa na huyu rafiki yake, kuwa anakwenda kuwa dakiari mkuu wa hospitali, …na hospitali yenyewe sio ndogo …Adamu akakubali kwa furaha, na kweli alipokutanishwa na baba wa huyo jamaa, alikubalika, lakini kwanza akubaliane na msharti yao, na mojawapo ni kupelekwa semina maalumu, na pili kupitia mafunzo ya uaskari…hapo akagwaya, lakini akasema potelea mbali, …lazima apambane na maisha.
Kwanza kabisa aliingizwa kwenye semina, semina hiyo ni kumjenga mtu kiakili, alionyeshwa mambo yanayotendeka nchini, akakutana na mambo ambayo hakuamini kuwa yapo nchini kwao…akapikwa ipasavyo….na akaona kweli ipo haja ya kupambana, ipo haja ya kutumia utaalamu wake kuhakikisha naye anakuwa katika hali itakayorejesha yale aliyoyaona kwenye himaya ya wananchi…lakini haikuwa rahisi hivyo…
Siku kabla hajakabidhiwa majukumu akakutana na huyo baba aliyemuunganishia na huyu baba akamkalisha chini,na kumuusia kama mwanae alimwambia;
‘Mwanangu dunia hii haina haki,…utashangaa kwanini haya yapo, ni kwasababu hali ilivyo, kila mtu anavutia kwake, ndio tuseme sera ya ubepari ndivyo ilivyo, kuwa ili ufanikiwe ni lazima utafute njia ya kupata zaidi na ili upate zaidi lazima utumie juhudi za ziada, na kwa nchi yetu hii juhudi za ziada zimebanwa, kinachotakiwa ni kupambana, ….na huwezi kupambana ukiwa umelegea, unatakiwa kujiandaa kwa kila hali, ujijenge kikakamavu….’akatulia yule mzee akimwangalia huyo kijana mbele yake, halafua akaendelea kusema.
‘Mimi ujana wangu niliupotezea katika kulitumikia taifa, nilifanya kazi kama punda, lakini mwisho wa siku unarejea nyumbani, ukiwa na mdeni, huna mbele wala nyuma, ukigeuka unawaona wenzako wanajenga mahekalu…unajiuliza wanapata wapi hizo pesa…mpaka nafikia makamo, sijaweza hata kununua baiskeli, nikasema hapana lazima kuna kitu hakipo sawa, nikafanya utafiti, ndip nikagundua kuwa kuna hujuma, sio kweli nchi yetu kuwa ni masikini kiasi hicho…kama ni masikini mbona hawo wanajenga mahekalu…’akasimama yule mzee na kumsogelea yule kijana mbele yake na kumshika begani.
‘Mwanzoni niliwaza kuwa ile hali ni ya muda mfupo, labda baadaye hali itatengamaa, hasa kipindi kile walipofukuzwa wageni wote hapa nchini na yule jamaa aliyeitwa nduli…lakini badala yake, wajanja wakamiliki zile mali na kuzifanya zao, …mjanja kuwahi…na waliowahi wakaweza kutenegneza maisha yao wao na familia zao, wengine tukabakia kumezea mate, kuwa labda ipo siku hali itakuwa nzuri, …labda, labda, umri unakwisha, …aah, nikasema haiwezekani, tukakutana na wenzangu tuakasema hapana lazima lifanyioke jambao, kwasababu watu wenye nafasi wamezuia kila kitu, kwanini…na kila kinachopatikana kinaishia mikononi mwao kwanini, aaah, tukasema hapana, saa lazima na sisi tujipenyeze tuwe nawo sambamba, tule sahani moja…vinginevyo tutabakia masikini, …’ Yule mzee akamwangali akwa muda yule kijana, kuhakikisha kuwa kweli kaelewa anachomwambia.
‘Kwahiyo sasa ili ijipenyeze kwao, ni lazima uwe nao, uende nao sambamba, lakini hata hivyo kuwa nao sambamba sio kazi rahisi, wengi wao hawapendi kwasababu wameshajenga hulka ya uchoyo wanataka wapate wao wenyewe, ndio maana unaoana kuna makundi makundi, ambayo mengine yameamua kujitenga na hata kuingia msituni, sisi hatutaki kuingia msituni, tuna maujuzi yetu, tutatumia ujuzi wetu kama sehemu ya mapambano, ili tuweze kubanana hapa hapa, sio kwa kwenda msituni, haow wa msituni, wanatumia ujuzi wao wa uaskari, sisi tutatumia uuzi wetu wa kitaaluma, …siri kubwa ni kuwa huku na kule…unauma huku unapulizia, …ndio maana ya ile semina. ..’akasema yule mzee na kuinuka kuondoka akujua kuwa kijana kaiva, na kweli toka siku ile Adamu akaanza kubadilika.
Baadaye akakabidhiwa hospitali hiyo rasmi, akiwa keshakuwa jasirii kama askari mwenye kila kitu, kazi ni kuingia uwanja ni, na kusimama mstari wa mbele wa mapambano…yeye alikuwa na kipaji, yeye alikuwa na taaluma adimu, alikuwa keshamsoma binadamu ndani na nje, na alishajua jinsi gani ya kumbadili binadamu toka alivyo kisura, kihisia na ….na kumtengeneza amtakavyo, na mwisho wa siku anamtumia kama roboti….
Taaluma ikafanya kazi yake na jambo kubwa alilojifunza na usiri katika kazi yao…na akweli aliweza kudumu katika kazi hiyo ya udakitari bila mtu yoyote kumhisi kuwa ana mambo mengine ya ziada, na utaalamu huu ilikuwa siri yake na wanachama walioaminika…akiwa kwenye mafunzo ya uaskari, alionekana kujua vyema matumizi ya silaha na hata kuwa mlenga shabaha mzuri, na kwa ile hamasa aliyokuwa nayo Adamu katika taaluma hiyo, akajikuta anapenda sana kuingia kwenye mapambano, na hata akawa miongoni mwa viongozi wa kificho katika kupambana kisilaha pale inapobidi. Kawaida huonekana dakitari, lakini akiwa uwanja wa mapambano huwezi kuamini kuwa ndiyo yule yule aliyekuwa akaokoa maisha ya watu kwa kutumia mikasi na madawa.
Kwa aijili hiyo wakati mwingine anaitwa mjini kwenda kuingia kwenye mapambano yasiyo rasmi, au kutekeleza jukumo liloshindikana na anapokuwa huko, hafiki kwa sura yke ya kawaida…na kwa mtindo huo hakuna aliyeweza kumjua, kwani alikuwa akijibdilisha sura kama kinyonga….
Siku zilivyoZIDI kwenda ndivyo alivyozidi kuvutiwa na kuhamsaka na kazi hiyo ya ziada, lakini hata hivyo alijikuta akiwa katika maisha ya hatarishi, na hata alipo-oa, hakuweza kuifaidi ndoa yake ipasavyo kwani wakati mwingine alihitajika usiku, na hapo hakuwa na jinsi , ila kudanganya kuwa anakwenda hospitalini kuna dharura, kumbe anakwenda uwanja wa mapambano ,au kwenda kutekeleza ukumu fulani ambalo lilihitaji utaalamu wake. Na baya zaidi akampata mke ambaye hawakuelewana kabisa, na kuishia katika kugombana mara kwa mara,…
Hata alipooa, kwasababu za usalama hakutakiwa kumwelezea mkewe chochote kuhusiana na kazi yake hiyo ya ziada, au kumuonyesja dalili zozote, hata itokee nini…, kwani moja ya masharti ya kazi zao ni kutokumwambia yoyote asiyekuwa mwanachama, hata kama ni familia yako, …kwahiyo alihakikisha mkewe hajui lolote,…baadaye mkewe alianza kumchunguza chunguza, na hili akaambiwa na wanachama kuwa mkewe ni hatari, keshagundua kitu, na amewahi kutumiwa na maadui atafute baadhi ya siri, kwahiyo awe macho naye….
Kabla hajaambiwa hivyo yeye mwenyewe alishachoka na tabia za mkewe, kwani alishagundua kuwa anajihusisha na wanaume kisiri…hili Adamu aliligundua mapema, lakini alitakiwa asichukue hatua yoyote haraka. Baadaye wanachama wakamshauri atafute mbinu aachane na mkewe haraka iwezekanavyo, kwani kuna uchunguzi kuwa anamahusiano na mmoja wa maadui zao, na pale alipomfumania na mshenga wake, ikawa ni nafasi mojawapo ya kumuacha, lakini aikaonekana kwanza wamtumie kama chambo katika kufaniklisha mambo yao…chambo hiyo ilipofanikiwa, huyo mke akaachwa, bila kujua nini kilichokuwa kinaendeela ndani ya nyumba hiyo.
Alimpomuajiri Rose awe msaidizi wake wengi hawakilipendelea hilo, walitaka mtu wanayemjua, waliataka mtu atakayepitia mafunzo yao, na walimuona Rose hafai, bila kutoa sababu maalumu. Adamu aling’ang’ania kuwa yeye alimuhitaji huyo kwasababu kaiva kitaaluma hata akiondoka kuwajibika sehemu nyingine huyo ataweza kufanya kazi yake bila wasiwasi. Wfadhili wale walikubali shingo upande na kutoa agiza kuwa wao watakuwa nyuma yao wakiangalia utendaji wake…
Siku zikapita na Adamu alikuwa anaishi bila mke, wakamshauri atafute mke, …na kipindi hicho Adamu alikuwa anamuwaza Rose awe ndio mke wake, akampendekeza mbele ya wanachama kuwa kama atampata Rose kuwa mkewe atafurahi sana, hapo akakutana na pingamizi kubwa sana, kuwa anataka kugeuza huo mradi sehemu ya mapenzi, ….
‘Kijana unajua tupo kwenye uwanja wa vita,…tumekuona siku nyingi kuwa huyo ulimuajiri kwasababu ya mapenzi, sio kama tulivyotka sisi…sasa umeanza kulidhihirisha hili mapema, tunakuasa tena, …hakikisha unakuwa katika njia tuliyokuagiza, vinginevyo, tutakuwa hatuna jinsi, …na unajua kiapo chetu, ni kiapo cha uaskari, kama unarudi nyuma, …unajua nini kitakachofanyika…sisi hatukukatilii huyo Rose awe mkeo, lakini kwa jinsi ulivyo kwake, tuna wasiwasi unaweza ukatoa siri kwake, …’akaambiwa.
‘Mimi naomba hilo mniachie, nitahakikisha anakuwa katika msitari wangu, ipo siku mtaniunga mkono…’akasema Adam, na kweli wakamuachia ahangaike na Rose wake, wakijua kabisa hataweza kufanikiwa kwa hilo, muda ukapita bila kukubaliwa na Rose awe mkewe, na hata wanachma walikuja kumwambia kuwa Ros hamfai, kwasababu kubwa kuwa akiwa karibu naye ataweza kushindwa baadhi ya majukumu, wanahitaji mtu baki ambaye atakuwa mbali na yeye… hilo hawakumwambia moja kwa moja Adamu, ilikuwa siri ya kundi, na walijua moja kwa moa kuwa Rose hataweza kumkubalia Adam , awe mkewe kwa jinsi walivyomuona, kwahiyo hawakufanya juhudi yoyote ya kumsaidia kwani wangelitaka wangafanya hivyo na Rose asingelikuwa na ubishi, anglikubali tu…
*************
Rose alikuwa alifungua mkoba wake akatoa bulungutu la pesa, na kumkabidhi Docta Adam, Docta Adam akawa kasimama anaziangalia zile pesa, na baadaye akamwangalia Rose usoni, akatabasamu na kugeuka bila kuzishika zile pesa aliangalia nje kwa muda halafu akaelekea kwenye kiti chake na kutoa kitabu cha stakabadhi na kabla hajakifungua mlango ukagongwa, akainuka haraka na kueleeka pale mlangoni, na waliokuwa wamesimama ni yule mkuu wa uadhamini na docta moya aliyeletwa kushika nafasi ya Rose.
‘Ohh, tena mumerudi wakati muafaka, karibu waheshimiwa…’akasema Adam. Na wao awakingia na kujikuta wakishngaa walipomuona Rose, na mbele yake zipo pesa.
‘Ohh, Docta umerudi, ..mbona tulisikia kuwa umeshikiliwa na maskari huko mjini, hebu tuambie ilikuwaje maana tumekusubiri kwenye kikao mara zaidi ya nne huonekani…’akauliza mwenyekiti wa wadhamini.
‘Ina maana uumbe wangu hamkuupata kwa Docta Adam?’ akauliza Rose.
‘Ujumbe haukutakiwa kupitia kwa docta Adam, ina maana hukusoma ile barua tuliyokuandikia maana ilielezea kila kitu, sisi tuliona kabisa umedharau, maana wewe ni msomi, kila kitu kimejieezea kisheria, …hii ilidhihirisha kabisa kuwa nafasi hiyo uliyopewa ilikuwa haikufai, …lakini haina shida tumeshalitatua hilo, nafikiri umeshapata taarifa kwa huyo uliyetka taarifa zako zipitie kwake, na…umeshampa barua yake?’akauliza huyu mkuu wa wadhamini.
‘Hpana ndio mefika na alikuwa akinikabidhi pesa alizokuwa akidaiwa..’akasema Adamu.
‘Haiwezekani, umepata wapi pesa hizo, oooh, safi sana, kama umeweza kuzipata hizo pesa, tutaangalia jinsi gani ya kukuweka katika nafasi nyingine, lakini sio hiyo uliyokuwa nayo mwanzoni, hilo tutaliongea abadaye, kwa sasa tumekuja kwa mambo mengine, sijui mumemalizana, …maana tunahitaji nafasi ya kuongea , na Rose hastahili kuwemo katika maongezi yetu…’akasema yule mkuu wa wadhamini.
‘Mimi naondoka, sina muda mwingi, naomba stakabadhi yangu ya malipo, na ninachotaka kusema nikuwatakia mafanikio mema, maana sidhani kuwa nitarejea hapa kama mfanyakazi wenu, natumai nikija tena nitakuja kwa ajili ya makabidhiano, …nawashukuru sana kwa yote …na kama niliwakosea nawaomba mnisamehe kwasaabbu nilifnay hivyo kwa nia njema kabisa, na huwezi kumuhadithia mtu akakuelewa, …unakutana na mtu kazidiwa hana pesa, na yupo mkononi mwako, utamuacha afe kwasabau hajalipia.., hapo mimi sielewi, ndio maana naona labda nimeingia uwanja usionifaa…nawashukuru sana….’akasema Rose na kuchukua stakabadhi yake na kuondoka,..
‘Lakini Rose nilikuwa na mazunguzmo na wewe, usiondoke kwana naomba unisibiri nje…’akasema Adam.
‘Mazunguzmo na wewe yamekatika ….sina mazunguzmo na wewe natumai umelielewa hili…naomba, na akuomba uwaambie watu wako kuwa, sitaku kufuatwa fuatwa , nimeshamalizana na nyinyi, …kama nyie ni miungu wa hapa duniani, haya endeleeni kinifuatafuta, lakini ipo siku,…’akasema na kundoka, huku mwenyekiti wa kamati ya wadhamini akicheka na kusema;
‘Nilijua kuwa huyu sio mke wa kuoa, Adamu, unatakiwa uwe jasiri, usikubali mapenzi yakulangai, mapenzi ni sumu katika uwanja wa mapambano, hili ulishaambiwa mara kadhaa, muda wa mapenzi ni wakati upon a mkeo nyumbani, lakini kama mpo uwanaj wa mapambano, huruma, haitakiwi, je itakwuaje kama umepewa amri ya kutekeleza jukumu na mkeo yupo karibu yako anakuambia usifanye….?’ Akauiliza yule mwenyekiti.
‘Jamani hilo swala la mimi na Rose nilishasema mniachie mwenyewe, sawa naona tuongee, maana, mumeshanifukuzia ndege wangu, sijui nitafanyaje ili nimpate…sijui …’akasema Adam.
‘Utampata ndege mzuri kuliko huyo, hawo ndege wapo wengi, na kila siku wanazaliwa wazuri zaidi, usikubali kutekwa moyo wako na kufanywa dhaifi kwa kitu mapenzi, huo ni udhaifu usiofaa, ukishindwa tuambie tutakutafutia, wewe tumekulea mwenyewe, hatushindwi kukutafutia mke , tena mke ambay hutaamini, …..ngoja tumalizane na hili, suijali..’akasema yule mkuu wa udhamini, na wakaingia kwenye majadiliano na mabo yao ya kiakzi hata walipomaliza ilikuwa imeshafika jioni.
Ilikuwa wakati Adamu anafunga mlango wa ofisi yake na muda huo pilikapilika zilishapungua,…sehemu iliyoonekana watu ni sehemu ya kulaza wagonjwa. Adamu kichwa kizima kilikuwa kimejaa hasira, akawa anafunga mlango wake, huku akimuwaza kiongozi wa wadhamini kwa kauli zake chafu, ambazo zimemuuashiria kuwa huenda hathaminiki tena na huyo aliyeletwa kushika nafasi ya Rose anandaliwa rasmi kuchukua nafasi yake….eti kafanya makosa mengi ambayo yanaweza kuwafichua na huenda wakaingia kwenye migogoro na serikali, kwahiyo lazima wajiandae, …ili kama atashikwa na kufungwa kuwa na mtu atakayeshika nafasi yake, kwanini ashikwe na kufungwa, kwanini wahisi hivyo……akajipa moyo kuwa hata kama watamundoa kwenye hiyo nafasi yake , bado anahisa, bado anauwezo wa kufungua hospitali yake mwenyewe…labda huko kufungwa, lakini kwa kosa gani….
Na mara wazo jingine likamjia kichwani, akawa sasa anamuwaza Rose, ina maana yeye na Rose ndio basi, hatakubali kwa hilo, akawaza jinsi gani atakuatana naye aili amthibitishie kuwa kweli anampenda na kwa kumuonyesha hilo atamwambia kuwa anaacha kazi na kufungua hospitali yao watakayoiendesha wao wawili, lakini je atakubali, na je bado yupo au keshaondoka mjini, … huenda atakuwa hajaondoka yupo nyumbani kwake, …akazmiria kwenda kwake kukutana na yeye, akafanya haraka haraka kuondoka, na kabla hajafunga mlango vizuri akasikia hatua za viatu zikimkaribia….
‘Ni nani huyu anakua kunisumbua muda kama huu..’akajisema moyoni, huku akihisi nywele zikimsisimuka, kwanza alizania kuwa huenda ni mlinzi,…kama ni mlinzi anakua kufanya nini…akasikilizia huku anafunga mlango, hakuwa na haja ya kugeuka kuangalia ni nani, lakini kitu kilichomshanagza ni hile hali ya mwili kusisimuka kama vile kuna hatari inamkaribia, …akahisi hali isiyo ya kawaida, …huyo sio mlinzi ni nani, atakuwa anakuja nyuma yake, akageuka haraka kuangalia,….na karibu azimie kwa mshituko alioupata…
NB, Unaweza kukisia ni nani huyo aliyemjia muda kama huo na kwanini shitake kiasi cha kutaka kuzimia

Ni mimi: emu-three

4 comments :

samira said...

m3 kutuweka roho juu mi naona ni sweetie huyo katokea

Rachel Siwa said...

Duhhhh kweli akuafaaye kwa dhiki, kazi yako yauhakika ndugu yangu, Mungu yu pamoja nawe, Pamoja ndugu wa mimi!!!

mimi said...

duuh kazi kweli docta adam kapatikana sasa. me nahisi ni yule jamaa aliyempa rose dhahabu. poa emu-three nakuombea upate kijiwe kizuri ili usettle ili uweze kutupatia vitu vitamu zaidi.

emuthree said...

Nawashukuru sana kwa dua zenu, kwani nazihitaji sana, kwanli kuchapo mambo yanakuwa magumu, kwa ule usemi akufukazaye hakuambii toka...Huwa najiuliza kwanini mgenii anakuja kwako na kuanza kukutawala? Hivi huko nje inafanyika hivyo hivyo...sizani, ....ni kwasababu hakuna wakutujali.