Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, October 10, 2011

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-36




Rose walipokuwa ndani ya taksi alimwangalia Sweetie akiwa anazishikashika zile ndevu za bandia alizovalishwa, ilionyeshwa dhahiri kuwa zinamkera, akatabasamu, lakini bila kumwangalia Sweetie, kweli kwa zile ndevu usingeliweza kumtambua kama ndio yule yule Sweetie aliyekuwa akimjua yeye. Alimwangalia Sweetie alivyokuwa akihangaika, mara aangalie nje, mara ageuke kumwangalia yeye, ilimradi ilionyesha dhahiri kuwa akili yake ilikuwa ikijaribu kutambua jambo, na alihitaji msaada wa kuambiwa kuwa nini, na yupo wapi, huenda mazingira yote anayoyaona ni mageni kwake, huenda…na zile ndevu za bandia alizovikwa zilionekna kumkera kwasababuhata hivyo hakuelewa kwanini afanyiwe hivyo, hata Rose mwenyewe, hakuataka mambo hayo, lakini walisisitizwa na yule dakitari kuwa ni kwa usalama wa huyo mgonjwa nan i vyema wasitake kujua zaidi…,

Alimwangalia Sweetie alivyobadilika kwa zile ndevu, utafikiri kama sio yeye, alikuwa akiangalia huku na kule, kuonyesha kuwa alikuwa katika mshangao fulani, na kila alipojaribu kutaka kuuliza kitu, Rose alimuonyeshea ishara kuwa awe na subira kwanza, akamwambia kwa sauti; `tutaongea nyumbani, hapa sio mahali pazuri pa kuulizana maswali, najua una maswali mengi….tulia kwanza…’ na Sweetie akatikisa kichwa kuonyesha kuwa kaelewa, hakuwa mbishi, na hali hii ilimuonyesha dhahihiri kuwa huyu mtu akili yake sasa imetulia, na inaonyesha kuwa huyu mtu ni mpole na inaonyesha kuwa….Rose akawa anwaza mengi ya kumpamba huyu mtu, anayeitwa Sweetie, sijui jana lake hasa ni lipi…

Wakiwa ndani ya gari, Sweetie aliangalia huku na kule, na kila alipogeuza kichwa kumwangalia Rose, Rose alijifanya kama anaandika meseji kwenye simu, au anafanya jambo fulani, ilimradi kumpotezea Sweetie asiseme lolote mpaka wafike hotelini kwao, alijifanya haoni jinsi gani mwenzake anavyohangaika, na baadaye wakafika hotelini, na kuingia ndani. Rose akamwambia Sweetie akaoge kwanza , halafu anywe dawa. Alijua kabisa kabisa akinywa hizo dawa, atachukuliwa na usingizi, na akiamuka wataanza mazungumzo, Sweetie akaingia bafuni kuoga, na kumuacha Rose akiwa katulia kwenye sofa , na kabla hajakaa vyema, simu ya hapo chumbani ikalia…..Rose akaipokea, na kuambiwa kuwa kuna mgeni anataka kuonana naye.

‘Mgeni gani huyo, mwambie sijisikii vyema, nahitaji kupumzika, unajua kazi ya kumhudumia mgonwa sijapata muda wa kupumzika…tafadhali, huyo na yoyote atakayekuja kunitafuta mimi waambienii sipo, au ninaumwa…vyovyote, ilimradi nisipate masumbufu….’akasema Rose.

‘Tumemwambia hilo, na tunajua hilo, lakini mtu huyu, hataki hata kuondoka, amesisitiza kuwa katumwa na Mr Adam, kuwa aje kwako kuchukua ule mzigo, na hahitaji kusubiri zaidi…’akasema huyo mhudumu wa mapokezi.

‘Ngoja nakuja hukohuko…’Rose aliposikia jina la Adam, akakumbuka simu aliyopigiwa akiwa hospitalini, kuwa kuna mtu atakuja kumuona, na alitakiwa kumpa pesa…hakukubalina na hilo wazo kabisa, na moyoni alisema hampi hata senti moja, lakini ni bora kwanza akajua ni pesa za nini….huenda ni kwa ajilii ya kununulia madawa, huenda….na kila mara alipowaza ndipo alipozidi kuwa na hamu ya kuonana na huyo mtu. Akasogea karibu na mlango wa bafuni kusikilizia bafuni, akasikia maji yakiendelea kumwagika, akajua bado Sweetie anaoga….akamuita kuwa atoke mara moja afunge mlango kwani anatoka mara moja,na awe muangalifu mtu yoyote akimgongea asimfungulie….

‘Unatoka unakwenda wapi, .., mbona nimeshamaliza kuoga,….?’akauliza Sweetie toka bafuni.

‘Nina mgeni mapokezi, na nisingependa wageni waingie huku ndani, wewe funga mlango kwa tahadhari…’akasema Rose na wakati huo Sweetie alitoka, akiwa kajifunga taulo…, na alihakikisha kuwa Sweetie kafunga mlango kwa ndani ndipo akaondoka kwenda mapokezi. Alipofika mapokezi alimuona mtu mmoja kavaa mawani meusi, yaliyofunika sehemu kubwa ya uso wake, akahisi anaweza kuwa ndio yeye, na uvaaji wake huo, hakupendezewa naye, dio hawo watu asiowataka kukutana nao. Na hata kabla hajauliza mapokezi kuwa mgeni huyo yupo wapi yula jamaa akainuka na kumkabili Rose.

‘Mimi nimetumwa na Mr Adam, kuwa wewe una mzigo wangu, …na nina shida sana, …nina shida ya pesa, ndio maana nimeshindwa kuvumilia…najua bado upo kweye majonzi, lakini…lakini naomba univumilie, unipe hizo pesa niishie zangu, sitaki usumbufu zaidi…nilishafanya kazi aliyoiniagiza, sasa, sioni kwanini nisipate mzigo wangu…na …’akasema yule mtu kwa sauti ya chini.

‘Wewe unanifahamu mimi…?’akauliza Rose kwa hasira.

‘Sikiliza dada, mimi kukufahamu nakufahamu sana, …nimekufahamu vipi hiyo sio kazi yako, kwasababu sisi ni kama walinzi wenu tu, mnapofika hapa jijini, tunafanya hiyo kazi baadaye tunapata mshiko wetu, lakini kazi niliyopewa ilikuwa tofauti kidogo, na nimeshaifanya, iliyobakia ni kumalizana…sina zaidi…najua sasa hivi umepewa mlinzi mpya, na huyo jamaa uliye naye mwenye nduvu, sijawahi kumuona hapa jijini, sijui ni nani…hilo kwasasa, halinihusu, ninachotaka ni pesa…’ akasema yule mtu.

‘Kazi gani uliyonifanyia…, mbona sikuelewi, mimi sikujui na mumekubaliana wewe na huyo mtu wako, sijui anaitwa Mr .Nani, sijui…’akasema Rose na kabla hajamaliza yule mtu akasema `Mr Adam’

‘Sawa vyovyote aitwavyo, ila mimi sina pesa za kukupa, na kwa ufupi sina mzigo wowote wa kukupa, wasiliana na huyo Mr A…sijui nani…’ akajifanya hajui hilo jina na yule mtu akasema `Mr Adam’ na Rose akatikisa kichwa kukubali na kuendelea kusema `Ongea naye umwambia wazi kuwa mimi, nimesema sina pesa, mjuane jinsi ya kupeana hizo pesa zenu, msisnihusishe kwa kitu nisichokifahamu,

….hebu nikuulize, ulishawahi kufanya kazi yoyote na mimi, nilishwahi kutumwa kwako kukupa pesa, kama mnafanyiana hivyo, je leo iweje nitumwe mimi….hebu nikuulize tana kazi gani uliyoifanya mabayo inanihusu mimi…?’ akauliza Rose kwa kuwa na hamu ya kujua ni nini bosi wake anakifanya.
‘Dada yangu sina kawaida ya kuzipata pesa hizo kwa mtu mwingine, ili yeye ndio kaniagiza hivyo, …na hata hivyo ni kwasababau sina pesa kabisa, …na baya zaidi nimegundua kuwa …bosi kabadilika, nahisi huyu mtu sasa anataka kunidanganya, siku zote tunaaminiana , namfanyia kazi yake, bila matatizo,…tunalipana bila matatizo, lakini alipomleta huyo ambaye tunatakiwa kupata amri toka kwake…ok, sawa… leo hiii anajifanya haniamini tena, …’yule mtu alikuwa kama anaongea peke yake na alionekana kukerwa, au ana jambo muhimu linalohitaji pesa.

‘Nimekwama, nahitajiwa kodi ya pango,nyumbani mama mgonjwa, anahitajii pesa….na aanjua mtoto wake anafanya akzi ya maana, leo ….hapana, lazima niipate hiyo pesa, …nimeshamjua mbaya wangu, ni huyo jamaa, ngoja hilo nitalifanyia kazi, lakini ….’akasema yule mtu na kukatiza maneno alipoona mtu mmoja akiingia mlangoni, …watu wote mle ndani waligeuza macho kuangalia hapo mlangoni, kwani jamaa aliyeingia alionekana ni mtu wa mazoezi kweli, mwili ulivyokaa, halafu ni mrefu…, naye alivaa miwani mikubwa meusi, alipoingia alitizama huku na kule na macho yake yalipotua pale waliposimama Rose na yule mtu, akaonyosha mkono na kuonyesha ishara ya kuita. Rose hakujua kuwa anaitwa yeye au huyo mtu.

‘Noksi keshakuja, huyo jamaa lazimia nimuondoe, kabla hajaniondoa mimi, …sikiliza dada, nitakuja saa nne, na kwa vile nahitaji pesa, na jamaa hawa wananizungusha, basi tutaongea,. Nitakuambia kwanini nahitaji huo mzigo,…utagundua mengi kuhusu huyo bosi wako, sivyo kama unavyomjua wewe…ninachotaka kwako ni thamani ya nusu ya huo mzigo, sio mbaya kwangu…saa nne nitakuja usiniangushe, nimekwama ile mbaya....’akasema yule mtu kwa kunong’ona huku akiondoka kumfuta yule jamaa aliyekuwa naye anageuka kutoka nje.

Rose alibakia kashangaa, huku akijiuliza kuna nini kinanendelea, …akaingiwa na hamu ya kukutana na huyo mtu tena, hasa aliposikia hayo maneno kuwa `huyo bosi wako sivyo kama unavyomjua, haraka akasogea dirishani na kuangalia kwa nje, aliwaona wale jamaa wakiiingia ndani ya gari, na yule jamaa aliyekuwa akiongea naye, akawa kama hataki kuingi kwenye gari, lakini yule jamaa mwingine akamsukumiza ndani ya gari na kufunga mlango kwa nguvu, na ilionyesha dhahiri kuwa kuna kutokuelewana kwa hawa watu wawili, na haijulikani kuwa wapo pamoja, au kila mmoja ana mambo yake.

Rose alipogeuza kichwa kuangalia pale mapokezi, alikuwa watu karibu wote wanamwangalia yeye, akamsogelea yule jamaa aliyepo mapokezi na kumuulizia kuwa kuwa hawo watu ni akina nani, na yule jamaa wa mapokezi akamwambia hata yeye hawajui, vyema, kwani yeye ni mgeni kidogo, kaajiriwa hapo karibuni, lakini anamkumbuka sana huyo mmojawapo aliyekuwa akiongea naye kwani alishawahi kuja mwanzoni akitaka kuonana na yeye Rose,....

‘Alishawahi kuja kuniona tena alisema ananihitajikwa kazi gani, ..na kwanini hamkuniambia..?’ akauliza Rose.

‘Siku ile alikuja, akiwa na mfuko, akasema amleta mzigo wago, anataka kukupa na alikuwa na haraka, sana, na siku ile kulitokea jambo la ajabu humo ndani, haijawahi kutokea hivyo kabla, simu ilikuwa haifanyi kazi, na kulikuwa na tatizo la umeme, kulikuwa hakuna mawasiliano kabisa humu ndani,…kwasababu tulikuwa tukihangaika, kuangalia nini kimetokea, huyo jamaa alipokuja, tukawa tumemuamini na tukamwelekeza aje kwako bila kukupigia simu kwanza, tusamehe kwa hilo…lakini sasa inanipa wasiwasi…kuwa hawa watu wana lao jambo, angalia sana dada yangu , ina maana hamukuonana naye…?’ akasema yule mtu.

‘Sijawahi kuonana na mtu kama huyu, ndio mara yangu ya kwanza, …’akasema Rose na kumfanya yule jamaa wa mapokezi ashikwe na mshangao, lakini akijifanya ni kawaida…kwa kuficha ule mshangao, kwani aliona kuwa siku ile alifanya uzembe kumruhus mtu aingie kumuona mteja wao bila idhini ya huyo mteja…kama bosi wake akijua anweza akafukuzwa kazi…’samahani dada yangu, naomba unisamehe kwa hilo, na naomba lisifike kwa bosi…maana naweza kukosa ajira,’ ….na mara simu pale mapokezi ikaiita, na yule jamaa wa mapokezi akaipokea na alipokuwa akiongea akamwangalia Rose na kuonyesha uso wa wasi wasi .

Baadaye yule jamaa akamuita mlinzi mmojapo aliyekuwa akizungukazunguka humo ndani kuangalia usalama, na kumwambia…’Naomba umpeleke huyu dada chumbani kwa bosi anahitajika mara moja…’ Halafu akamgeukia Rose na kumwabia bosi wao anamuhitaji mara moja na kumsisistizia kuwa akiulizwa kuhusu hiyo siku amlinde…. Rose akauliza kwasababu gani anaitwa, yule mtu wa mapokezai akasema, hakuna wasiwasi. Yeye aende tu,….

Rose akafuatana na yule mlinzi hadi kwa huyo anayeitwa bosi,…walifika kwenye chumba kimojawapo kilichopo ghorofa ya tatu, kwani hoteli hiyo ilikuwa na ghorofa tatu,…yule mlizi alimuonyesha kwa kidole kuwa aingie chumba hicho …alionyeshea kwa kidole na kuondoka…Rose alifika kwenye huo mlango na kugonga, hakusikia sauti, akazungusha kitasa na mlango ukafunguka, na akatizama ndani, …akasikia sauti ya mtu akiongea na simu, akaingia hdai ndani bila kusubiri…alimkuta huyo jamaa, anaongea na simu huku anaanglia kwenye computa, na alipomuona Rose, keshaingia akakata simu na kuinuka pale alipokuwa kakaa na kuja kukaa kwenye meza kubwa iliyopangwa viti viwili...

‘Samahani mteja wetu tafdahli kaa kwenye kiti kidogo, hatuna maana mbaya kwako, lakini inabidi tufanye hivyo, kwa usalama wa hii hoteli…’akasema yule mtu na kutoa kitabu kwenye droo za hiyo meza, halafu akaandeela kusema,`Mimi ni mmoja wa wakuu wa ulinzi humu ndani, na shughulika na bili za wateja, …sasa tumeona kuwa kuwepo kwako humu ndani kunaleta wasi wasi kidogo, na usalama wa humu ni jambo muhimu sana, hatutaki kujiingiza kwenye matatizo ambayo tunayaona yapo dhahihiri, hatutaki kuingia katika matatizo na polisi….kwahiyo kwasababu za kiusalama, tunakuomba …sio kuwa tunakufukuza, lakini hatuna jinsi, kutokana masharti yaliyoainishwa kwenye mkataba wetu, natumai walikuonyesha wakati unaingia humu….samhani sana, kuwa uondoke, kwasababu, kuna vipengele tunaona vimekiukwa…tunakuomba ukatafute hoteli nyingine…’akasema yule jamaa.

‘Lakini kwanini mnifanyie hivi, …vipengele gani vimekiukwa, mbon siwaelewi, ….hata hivyo kesho naondoka, haina haja ya kutafuta hoteli nyingine, naomba mnivumilie kwa usiku wa leo tu… …’akasema Rose akiwa haelewi ni nini kibaya kafanya.

‘Kesho ni mbali sana, kwa watu kama hawo , kabla sijaacha kazi serikalini, niliwahi kukumbana na kesi za watu hawa, nilifuatilia, nikagundua nyendo zao, nikawasilisha serikalini, kumbe baadhi ya wahusika ni watu wa humo humo serikalini, wakaanza kunifuatilia, mpaka nikaoenekana mbaya, nkaanza kufuatwafuatwa, na hata kutishiwa maisha,…nikaona hapana, ngoja niachane na hii kazi , nikajiuzulu, ndio nikawa nimeajiriwa kwenye hii hoteli, kwahiyo sio kwamba nabuni hilo, ninawajua hawa watu….’akasema yule mtu huku anachungulia chungulia kwenye komputa yake.

‘Hebu kidogo …’ akainuka na kuchungulia komputa yake, halafu akarudi na kukaa pale alipokuwa kaka mwanzoni, na kusema `Dada yangu, kuna watu wameingia leo hii kukutafuta wewe,…mmoja ndiye aliyekuulizia, lakini mwingine alikuja baadaye, …wote hawo wapo kundi moja, watu hawo wanapofika mahali hakuuishi kutokea…matatizo,…lazima jambo baya litatokea…, na mara nyingi ni mauaji,…nashindwa nikusaidieje, maana hata kama utakwenda polisi, sijui nani wa kumwamini…maana nchi hii ipo kwenye vita, kama unavyoona, watu wanatafuta madaraka…ni mapaka hali hii itakapotengamaa, ndipo labda, mabo haya yataisha…’akasema yule mtu huku akiwa anachungulia komputa yake, mpaka Rose akawa na hamu ya kujua nini anachochungulia mara kwa mara.

‘Ulipoingia hapa, ulipewa mkataba, …hapa tunaishi kwa mkataba, na hili nililiona kuwa ndilo jambo jema, la kuelewana na wateja wetu, na aktika mkataba wetu, kama uliusoma vyema, kuna kipengele cha usalama, kuwa kama mteja anauhusiano na wau wasioaminika na ikabainika hivyo, utatakiwa uondoke mara moja….’ Akainuka na kurejea kwenye kompuata yake na sasa akawa anongea kwa haraka na kwa ukakamavu kama askari ` Kutokana na hicho kipengele tunakuomba uondoke…na nakushauri uklitoka hapa jaribu kuwasiliana na polisi…huyo jamaa aliyekuhitaji wewe na baadaye akaja mwenzake, wote wawili sio watu wema, wanajulikana….sio watu wema…nashindwa kujua kwanini dada mrembo kama wewe uwe na mahusiano na hawo watu, na usijifanye huwajui, wasingekujua kukuulizia kama hawakuji….’akasema yule mtu akitoa karatasi ambayo ilionyesha kuwa ni bili ya Rose, kuwa kweli anatakiwa kuondoka hapo…!

‘Mimi siwezi kuondoka leo, nitaondoka kesho asubuhi na mapema, sina sababau ya kuendelea kukaa hapa, kwani mgonjwa wangu kesharuhusiwa, nitaondoka kesho asubhi na mapema, …’akasema Rose. Walibishana sana na yule mtu, mpaka , yule jamaa akapandwa na hasira, na kutaka kuchukua hatua zingine, lakini baadaye akaongea kwa unyenyekevu na kusema `Huyu jamaa aliyekufuata leo na mwenzake, ni watu wa hatari kabisa, kazi zao ni kutumwa na wakubwa kufanya mauaji, …na mara nyingi ukiwaona wakiongea na mtu, huyo mtu hatamaliza masaa, atakuwa maiti na kifo chake kinakuwa cha utata. Polisi wamejaribu kuwabana hawo watu, lakini hawajafanikiwa kupata ushahidi na mara nyingi wakikamatwa , baada ya siku mbili utawakuta wapo mitaani….sasa naogopa kuwa wewe au mwenzako ana tiketi ya kifo…naogopa kusema hivyo…nawajua sibahatishi…’akasema na kuinuka kufungua mlango ili Roe aondoke

‘Sasa mimi nitafanyaje, maana nipo na mgonjwa, na sasa usiku umeingia, na hapa ndipo nilipopaamini, kama hakuna uaminifu tena humu ndani..basi nitaondoka, na inaonyesha kuwa kumbe hoteli hii haina walinzi, hamujiamini…., kwa mfano kama hawo jamaa waliwahi kuja mara ya kwanza na kuruhusiwa kuja kuniona mimi bila hata taarrifa, ina maana kuwa mnaweza hata kumuingizia mtu jambazi…na kama ulivyosema hawo watu ni majambazi, huyo mmoja alikuja na kuruhusiwa kuniona, bila hata mimi kujua, na huku mnajifanya mpo makini…’akasema Rose.

‘Waliwahi kuja tena humu ndani..haiwezekani, kabisa, hilo nakataa…?’ akuliza huyo jamaa kwa mshangao.

‘Aliwahi kuja, na siku hiyo kulikuwa na matatizo ya umeme na mawasiliano, kama unabisha nenda kawaulize huko chini, watakuthibitishia hilo……na kwahiyo naondoka naenda kutoa taarifa hii polisi kuwa kumbe kuna watu mnawajua, wanakua mnawaruhusu kuona wateja, bila kuali usalama wao…’akasema Rose.

‘Aisee…kumbe ndio wao….kwasababu haiwezekani siku ile, umeme ukatike, mawasilano yakatwe…walikuwa na lao jambo, lakini sikumbuki kutokea maujai…labda walikuwa na mambo yao mengine…..’akasema yule mtu, na Rose alijaribu kutafakari kuwa siku ile kulikuwa na jambo gani lilitokea lakini hakuweza kugundua kabisa kichwani mwake, au walitumia jina lake kuingia humo….!, mwishowe alimaua kutokuliwazia zaidi, kwani mambo mengi yametokea hapo katikakati na hakuwa na akili yakugundua zaidi, kuwa kweli walikuwa wanakua kwake, kwa ulinzi kama walivyodai, au kuliko na jambo jingine…akawa kasimama mlangoni na kumwambia yule bosi wa ulinzi ;

‘Kwahiyo kama nikiondoka hapa nakwena moja kwa moja polisi kuwaambia nini kinachoendelea humu hotelini…, maana sitakuwa na usalama…huenda kuna njama mumeisuka wewe na hawo watu kuwa nitoke humu, wanikute huko nje… niuawae…’akasema Rose, na yule jamaa akakuna kichwa.

‘Ok, dada, naona umenishinda, lakini sio kwamba nasema hivyo kwa kuwa nashirikiana na hawo watu, ila sitaki matatizo na polisi, sitaki matatizo na makundi mabaya kama hayo, ….Sikiliza kwa vile kesho mnaondoka asubuhi na mapema, basi ngoja na mimi nitumie ujuzi wangu wa ulizi na uslama, na hapa najitolea mwenyewe kukulinda, na itakugharimu, kama utakubalana nami, niatbeba dhamana ya kukulinda…., nitawapatia chumba kingine chenye usalama, sio safi kama hicho mnachokaa, lakini usalama wake ni mkubwa,….’ Akatulia na kuangalia komputa yake, ..

‘Hapo mtakapokaa hakuna mtu anayeweza kuja kuwadhuru, hilo nawahakikishia, ila msitoke kabisa humo hadi kesho yake mkiondoka,….ukikiuka hayo mimi sitalaumiwa,…na baada ya kesho mimi sina dhamana na nyie, na ukumbuke kuwa hiyo ni kazi ya ziada kwangu, kwahiyo inabidi unilipe, na malipo hayo utanipa kesho ukilipia bili yako, hayo utabidi unipe mwenyewe mkononi, kama umekubaliana na hilo, twende nikakuhamishe mara moja….’akasema yule bosi na Rose akakubalian na hilo wazo, wakatoka mle na kurudi chumbani kwake, na walimkuta Sweetie kapitiwa na usingizi, walimuarifu kuwa wanahama chumba…

‘Mbona mnapenda sana mambo ya kuhamahama, huko hospitalini ilikuwa hivyiohivyo, mara huku mara kule, kuna nini kinaendelea,…mnanifanya nijihisi vinginevyo, ….kwanza hapa kwenyewe sikujui …sikumbuki kabisa kufika hapa kabla, nawaombeni, mniambieni nipo wapi…hapa ni wapi?’akalalamika Sweetie.

‘Wewe usijali, utakuja kuyajua baaadaye, sasa hivi tuondoke hapa, unajua sasa hivi dunia imebadilika,…na hapa kwetu bado tupo kwenye uwanja wa vita, hakuna usalama kabisa…’akasema yule bosi wa ulinzi.

‘Hapa kwenu,…na mimi pia, au…?’ akauliza Sweetie, halafu akanyamza huku akitafakari kitu, akamwangalia Rose kwa makini akitaka maelezo…lakini Rose alijifanya hamuoni, hakutaka kuongea naye chochote mapaka muda muafaka, hasa kuhusiana na kumbukumbu zake, alitaka watulie waongee bila bughudha, lakini kwa hali ilivyo hapo, wasingeliweza kuongea lolote….. Hata hivyo kila alipomwangalia Sweetie alihisi kuwa bado hajatulia vyema, kama ni kumbukumbu zitakuwa zimerejea kiasi tu…bado ubongo unahitajika kutulizwa…. mara nyingi amekuwa akimwangalia kwa kujificha, na wakati mwingine macho yao yanakutana, kuonyesha kuwa hata Sweetie, alikuwa akimwangalia kwa kujiibaiba.

Dawa anazotumia Sweetie zilikuwa akizinywa anapitiwa na usingizi na hicho ndicho kilichomsaida Rose, na kwahiyo walipofika kwenye hicho chumba walichohamishiwa, alipma dawa Sweetie na haikupita muda, Sweetie akawa ndani ya usingizi, yeye akajilaza kitanda cha pili yake kwani humo ndani kulikuwa na vitanda viwili, na alipofika saa nne za usiku, akili yake ikawa hautulii, licha ya kuwa walikanywa na huyo bosi wa ulinzi kuwa wasitoke, yeye akawa na hamu ya kujua nini yule mtu alitaka kumwambia, …akatoka nje..,baada ya kuhakikisha kuwa mlango kaufunga vyema na Sweetie kalala.

Chumba walichohamishiwa kilikuwa ni sehemu ambazo zinatumika na utawala, ni vyumba vya wafanyakzi hata nje kuliandikwa kuwa ni sehemu ya utawala, hakuruhusiwi mtu kuingia kama hahusiki. Rose akatoka mle chumbani akiwa amevaa nguo za Sweetie na koti refu, na kuvaa kofia, kiasi kwamba usingelijua kuwa na mwanamke…alitoka mle chumbani na kuingia kwenye korido, na kukutana na watu mbalimbali waliokuwa wakitoka na kuingia kwenye vyumba vyao, na ilionekana siku hiyo kuwa na watu wengi zaidi. Na hii ilimpa nafasi Rose kufikia kile chumba alichokuwa kikaa mwanzoni bila kuhisiwa lolote.

Alipofika pale kwenye chumba walichokuwa wamepanga mwanzoni, akaangalia huku na kule kuhakikisha kuwa hakuna matu anayemtizama, …aliwaza, je huyu jamaa akija atawaulizia watu mapokezi, aua atakuja moja kwa moja huku chumbani, ….alibahatisha kuwa huenda akaja mopa kwa moja huku chumbani, …akafungua ule mlango, ….na wakati anafungua alisikia sauti za ving’ora vya polisi huko nje, kuonyesha kuwa kuna polisi wamekuja au wanapita, hakujali hilo, alijua kuwa huenda ni moa ya kazi zao…akafungua kitasa cha kile chumba na mara mlango ukafunguka…alikumbuka wakati wanatoka na yule bosi mlinzi aliufunga ule mlango kwa funguo, akasita kidogo kuwa huenda kuna mtu mpya kaingia humo…

Hisia zikamtuma aingie ndani, ..lakini nywele zilikuwa zikimsismuka, kiasi kwamba aliogopa, na kuna wakati alitaka kuondoka, lakini akakumbuka yale maneno ya yule mtu akisema; utagundua mengi kuhusu huyo bosi wako, sivyo kama unavyomjua wewe…

Akaufungua ule mlango na kuingia ndani, kulikuwa giza, kwasababau taa ilikuwa imezimwa, akasogelea sehemu ya kuwashia taa, na akahisi kakanyaga chupa au kiyoo, kilichovunjika, …hakujali akawasha taa yam le ndani, ….wakati huo mlango wa kila chumba alikuwa hajaufunga kabisa, kwahiyo alikuwa akisikia nini kinachoendelea huko nje, na kilichotawala zaidi ni kelele za ving’ora vya polisi….akajiuliza kuna nini humo, ….je kama kuna polisi huyo jamaa kweli anaweza kuja…, kama ni miongoni mwa wahalifu akisikia polsi hataweza kuja…akawa anajiluza maswali mengi na akageuka nyuma kuangalia mle chumbani…akahisi moyo ukimlipuka, …akahisi nywele zikimsisimuka, pale kwenye sofa kubwa la kupumzikia kulikuwa na mtu kakaa, unamuona kichwa, na kichwa kimekuwa kama kimeegemea uapnde, kwasabaabu ya ukubwa wa sofa siyo rahisi kuona kiwiliwili chote…ndiyo yeye huyo jamaa, kofia lake lilionekana wazi….

Bila kusema kitu, Rose akasogelea karibu na lile sofa…kwani pali alipokuwa kasimama, anakuwa nyuma ya sofa, kwahiyo sio rahisi kumuona huyo mtu upande wa mbeleni, anamuona kwa nyuma, tena kichwani tu, ….akasogea kwa mbele, .. wakati anasogea akahisi ubaridi ukitokea dirishani, akageuza uso kwa haraka kutizama dirishani, akaona kiyoo cha dirisha kimevunjika,…kumetokea nini….kwa haraka akageuza uso sasa kumwangalia yule jamaa kwani alishamuelekea…alichelewa, …ingawaje lishaufikisha mkono kuziba mdomo usitowe yowe, lakini alishachelewa, sauti ikawa imeshamtoka na yowe likasikika, …na kabla hajatoa yowe jingine, mara mlango ukafunguliwa, …polisi…

NB: Mwenyewe nilisisimukwa nilipofika hapa, lakini tusubiri sehemu ijayo, tujue nini kilitokea, kwanini Rose alitoa yowe….na polisi hawoooo….mimi sijui zaidi tusubiri sehemu ijayo…tukiombeana heri…kwani mambo bado hayajawa sawa….! Swali je mumeipenda sehemu hii, kama mumeipenda mimi ninawapenda nyie zaidi, ndio maana najitahidi vyovyote iwavyo niweze kuwa nanyi katika kisa hiki….ingawaje ni kwa shida kubwa…..



Ni mimi: emu-three

8 comments :

Precious said...

mmmmmhhhhhhhhh...nimesisimka pia mpk naogopa maskini Rose kwa nini hakutulia kule2 ss anajitafutia matatizo.....Pole M3 kila kitu kitakuwa sawa kwa uwezo wa Allah.

samira said...

m3 roho yangu iko juu hadi basi
jamani rose angetoa izo hela jela inanukia
hii inatufundisha kumuamini mtu rose alimuamini sana docta adam
kumbe jambazi sugu
m3 mungu akulinde na hapo kazini patulie

Pam said...

Moyo wangu jamani nipepeeni naona cpati hewa ya kutosha!!! m3 ni aje wapenda kuturusha roho mh sasa Rose jamani kwann kwann kwann aaah...

Anonymous said...

Hebu Kula 5, wewe mkali,vp kuhusu ule mpango wa kutoa vitabu umefikia wapi?

ROGER-UK

Yasinta Ngonyani said...

Kweli inasisimua na. Sasa wewe Rose kwa nini usingetulia hapa ulipokuwa jamani...mimi binafsi nimeipenda sehehemu hii au niseme nimependa na napenda kila kitu unachoandika. Naungana na Roger-UK inabindi utoe kitabu ndugu yangu...ingawa sasa hivi mambo yapo kama yalivyo lakini fikiria hili. Twasubiri kinachoendelea......

Anonymous said...

Hapo,sasa.Tunasubiri kwa hamu,kijua kinachoendelea.

Anonymous said...

kama nilikua naangalia movie sio mchezo.

ROGER-UK

Godwin Habib Meghji said...

Ninasubiria kitabu, kwa sababu kuna sehemu kama 10 hivi nimezikosa.