Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, October 3, 2011

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-33
Wakati tupo na akina Maua na Maneno, mara tukapata taarifa kuwa huko nchi ya jirani kuna jambo limetokea, ni muhimu turejee huko haraka iwezekanavyo, kwahiyo tukatishe kidogo twende na labda tukirudii huku tutakuwa katika kuhitimisha. Karibuni sana.

Tukumbuke kuwa Sweetie alikutwa bafuni kazimia, na Rose akawa kachanganyikiwa kabisa, kwani jinsi livyomuona pale sakafuni, alikuwa kama mfu, ikabidi aanze kazi yake ya udakitari ya huduma ya kwanza, na alipoona imeshindikana, ikibidi atafute msaada na harakaharaka kwa kuonana na wahudumu wa hoteli ambapo kulikuwa na gari la dharura kama hiyo , na mara moja akakimbizwa hospitalini.

Wakati yupo hospitalini Rose alikuwa akiwaza ni nini hasa kimemtokea Sweetie wake, huenda ni kwasababu ya tukio la jana, …tukio la jana, ooh,. Alipofika hapo akatabasamu, na kuanza kupitisha kidole taratibu kwenye sehemu ya mbele ya mdomo wake, na alipohisi msisimuko akaondoa haraka, na kutamani kukasirika, lakini badala yake akatabasamu…mmh, hisia… halafu akatabasamu tena, na kuinuka pale alipokuwa amekaa, na kuwaza ina maana baada ya tukio la jana, hisia zake zimeanza kurudi, chuki kwa wanaume imeondoka…au kwasababu ya kupenda….mmh, kupenda, kumpenda nani…hapana sijapenda, sitaki kupenda, …mmh, lakini najidanganya…na hapo akawaza kwa tukio la jana, akianzia pale alipoamuka asubuhi.

Alipoamuka asubuhi, alijinyosha, na kuinua mikono juu, akinyosha na kutikisa sehemu za mabega huku mikono ikiwa juu, hadi shuka aliyokuwa kajifunika ikaondoka mwilini mwake, na kubakia mtupu…na baadaye mikono yake akaishusha taratibu hadi kugusa kwenye godoro, na mkono mmoja ukagusa kitu…na kumfanya ashituke,ooh, alishasahau kuwa hayupo kitandani pake, ….oh, …akainuka haraka, na kuvuta shuka kujifunika, alishasahau kuwa jana alilala kitandani kwa mgonjwa.
Haraka akageukia upande wa pili wa kitanda kumwangalia mgonjwa, …huku akiwaza nini alichokifanya jana, kafanya makosa,…kafanya makosa…kama dakitari alitakiwa kuzuia hisia zake, sasa nini kafanya…ooh, akatamani kujutia, lakini kwa upande mmoja wa akili yake akatamani tukio hilo lingepatikana tena, …..

Akilini alikuwa akijichambua na kujiuliza mara kwa mara je alichofanya ni makosa, je alifanya kwasababu mgonjwa alitaka , au alifanya kwasababu yeye alivutika na kutaka kufanya hivyo? Na je nini athari zake kwa mgonjwa, haimaanishi kuwa kalazimisha hisia za mgonjwa kabla ya muda wake? …Aalipofikia hapo kwenye kuwaza, akakurupuka haraka huku akitizama kitandani,.…mgonjwa hayupo…!

Sweetie hayupo, akatoka pale kitandani, na kwanza kabisa alichofanya ni kuangalia pale alipouficha ufungua wa mlango akaukuta upo pale pale, kwahiyo alikuwa na uhakika kuwa mgonjwa wake hajatoka nje, akatulia kidogo, halafu akavaa nguo zake haraka, na alipoona kimiya akakimbilia chooni,…hakuna mtu akafungua mlango wa bafuni, …mshituko….

Ndio muda ule alipomkuta Sweetie kalala sakafuni, bafuni..ule mlalo sio wa usalama, akamkimbilia pale chini na kuanza kutoa huduma ya kwanza…

Huduma ya kwanza haikusaidia kitu, mgonjwa alikuwa kazimia, na hali kama ile akiendelea nayoo inaweza ikamletea madhara, kwahiyo alichofanya ni kutoka mbio kwenda kuomba msaada kwa wenye hoteli, cha ajabu kulikuwa na simu, angeliitumia, lakini wazo hilo halikuwepo,akaamua kwenda mwenyewe kuwaona hawo wahudumu…

Mara akakumbuka kitu, kumbukumbu hiyo ilimtia wasiwasi kidogo, kwani alikuwa na uhakika kuwa, alifunga mlango usiku, lakini wakati anatoka kwenda kuomba msaada kwa wahudumu, hakufungua mlango kwa ufunguo, aliufungua , na ukafunguka bila kutumia ufunguo…hii inamaanisha nini…? Hiyi milango, hata ukifunga kwa ufunguo ukiwa ndani unaweza ukafungua bila kutumia ufunguo…! Haiwezekani, kwani alipofunga jana, aliujaribu kuufungua mlango, lakini haukuweza kufumnguka…akajiuliza akilini kwanini anawaza hivyo, kwanini, kwanini….

Hili likamganda akilini, ina maana basi wahudumu walifika mapema wakafungua mlango, na walipoona wamelala, hawakukumbuka kufunga tena, …hapana kwa sheria za pale, kama chumba kina mtu, mhudumu hawezi kufungua, hadi amgongee mwenye chumba….au walipoingia kwake wakakuta hakuna mtu, walitaka kuahkikisha kuwa yeye kalala wapi, …hapna hiyo sio taratibu njema na kama wamefnaya hivyo ni makosa, lazima atawaulizia, …lazima awaulizie, kwasababu wangelisababisha mgonjwa wake kutoka nje na kukimbia…! Akanona aachane na hayo mawazo kwasababu hayasaidii kitu, kwani mgonjwa hakutoka, na badala yake kazimia bafuni…..

Rose akaanza kumwaza Sweetie na kusema ‘Jamani huyu Sweetie mbona hali imembadilika haraka hivi, na hali yake ni mbaya sana, sijawahi kumuona akiwa katika hali kama hiyo kabla, hali… hali ile ya mwanzo ina nafuu…’ halafu akawa anawaza akilini akilinganisha hali ya mwanzoni na hali aliyomkuta nayo sasa na kusema ‘Hali ya mwanzoni haikuwambaya hivi ingawaje nilimkuta keshahudumiwa na nikakabidhiwa kuwa huo ni mzigo wangu….’ Oooh, ni mzigo wangu na kweli umekuwa mzigo wangu…

Rose aliendelea kuwaza , mara akae mara asimame, ilimradi alikuwa akijaribu kutafuta nia ya kupoteza muda na kundoa hisia mbaya zilizokuwa zimeanza kujijenga kichwani, akajaribu kukumbuka jinsi alivyoanza kulalamika kuwa kichwa kinamuuma, na hii sio mara ya kwanza ya kulalamika kuhusu kichwa, ikitokea anampa dawa ya kutuliza maumivu, na kinaweza kupona mara moja, au kikachukua muda, lakini haikuwahi kutokea kama ilivyotokea leo…ilifika hatua akawa anajilaumu, kuwa huenda ni kwasababau ya tukio la jana, huenda walichofanya jana kimesababisha shinikizo la damu….haiwezekani kabisa, hilo akaliondoa akilini, haiwezekani kabisa…..

Akageuka upande ule wa chumba cha wagonjwa mahututi na kuwaangalia wataalamu wanavyohangaika, na kukumbuka kazi yake hiyo, hapo alijiona anakosa kuwajibika, ilitakiwa naye awe anahangaika nao., lakini aliambiwa asubiri…hakutaka kubishana nao, …cha muhimu ni kuhakikisha wanayaokoa maisha ya huyo mgonjwa, wao hawakumurhusu yeye kuingia, eti kwasababu sio mfanyakazi wa hapo, hata pale alipojitambulisha kuwa hata yeye ni dakitari.

Baadaye kitambo akaja dakitari aliyekuwa akimhudumia Sweetie wake, na kumuomba Rose wafuatane hadi chumba hicho cha wagonjwa mahututi. Alimkuta Sweetie akiwa na vyombo vya kumsaidia kupumua.
‘Docta tumekuita, samahani kuwa mwanzoni tulikuzuia, lakini kwa hali ya mgonjwa ilivyo, tumeona uje , labda kwa vile unamjua toka huko ulipokuwa ukimitibia mwanzoni unaweza ukatusaidia , maana hali yake ni kutatanisha kabisa….inavyoonekana kapatwa na kitu kama mshituko, na kichwani, tuna mashaka napo, je aliwahi kugongwa kichwani,…?’ Akauliza yule dakitari.

‘Hilo tuliwahi kuligundua wakati tulipompokea kwa mara ya kwanza…lakini…hebu nimwangalie…’ akasema Rose.

Rose akaingia kazini, akisaidiana na hawo madakitari wengine, lakini haikusaidia kitu, ilionekana kabisa imeshindikana, na ina maana mgonjwa ni wa kusubiria tu…lakini lazima juhudi nyingine zifanyike….

‘Haiwezzekani, inabidi tumuhamishe hapa apelekwe hospitali kubwa yenye vyombo zaidi ….’ Akapendekeza dakitari wa hapo na wote wakakubaliana na hilo wazo, kwahiyo ikawa kazi ya kutafuta usafari wa haraka na mgonjwa akaingizwa kwenye gari na kukimbizwa kwenye hospitali kubwa, ambayo haikuwa mbali sana na hapo.

Njia Rose kila alipokuwa akimwangalia yule mgonjwa, alikuwa hajisikii vyema, machozi yalishamuanza kumlengalenga, alijipa moyo, lakini kwa utaalamu wake na uzoefu wake, hali aliyokuwa nayo huyo mgonjwa, ilikuwa ni kuhesabu masaa, lakini yeye kama dakitari hakuliweka hilo mbele, alijipa matumaini kuwa wakifika kwenye sehemu yenye vifaa zaidi , mambo yanaweza yakabadilika, …alijaribu kuondoa wazo la kuwa imeshindikana, kwani kazi yao ni kuhakikisha kuwa mgonjwa anapona, hadi dakika ya mwisho, kama akifa ni jambo jingine. Akajipa moyo.

Wakati anajipa moyo akakumbuka jinsi jana yake ilivyokuwa, hali ya mgonjwa haikuwa mbaya kiasi kile, hata pale mgonjwa alivyoanza kulalamika kuhusu kichwa, haikuwa ni hali ya kutisha sana. Alikumbuka alipomchunguza, aligundua ni kichwa cha kawaida, …lakini kama walivyogundua hawo madakiati kuna athari kichwani, ….lakini hiyo athari, haingemfanya awe katika hali kama hiyo, ingelitokea kama hivyo…lakini. Akakumbuka maneno ya yule mtaalamu wao kuwa alisema mgonjwa huyo ana athari kwenye kichwa, labda ndio hilo tatizo limeanza kuleta shida, lakini kwa kumbukumbu zake yule mtaalamu alisema hali kama hiyo itatokea pale akipata jambo la mshituko, …au kugongwa tena kichwani….!

‘Kugongwa tena kichwani, ….’ Akayarudia hayo maneno, na hapo likamjia wazo kuwa huenda kwa vile kichwa kilikuwa kikimuuma sana, wakati anaoga, alishikwa na kizunguzungu, akadondoka na kugonga kichwa kwenye ukuta…inawezekana kabisa…alikumbuka mtaalamu wao aligundua kuwa tatizo kubwa, limetokana na kugongwa kichwani, au kudondokea kichwa, na mtaaalmu wao alikuwa kapendeekzaa kuwa hilo tatizo linahitaji upasuaji, kwani hata kama atakuwa kapona, ikitokea tataizo la mshituko, hali kama hiyo itakuwa ianmreeja mara kwa mara.

‘Ok, hilo lazima nilifanyie jitihada, Itabidi apelekwe India, na kama ni hivyo, inabidi nisilipe deni la hospitali kwanza, au nilipie sehemu ya deni….lakini hata nikilipa deni lote bado nahisi pesa itatosha tu…’ Akapiga mahesabu akaona kuwa kama atauza zile dhahabu zilizobakia ataweza kuyamudu yote hayo, deni, matibabu na hata kujisomesha, …na hapo akawa anaomba mungu tu hali iliyopo isiwe mbaya zaidi ..akafumba macho na kuanza kuomba, na machozi yakawa yanamtoka kwa wingi.

Kwa vile alikuwa kakaa karibu na mgonjwa, alisogeza mkono wake taratibu na kumshika mgonjwa mkono wake, …alijikuta akipatwa na mshituko wa mwaka, …mkono wa mgonjwa ulikuwa baridi kama mfu…ina maana mgonjwa alishakata roho muda mrefu,… hapana haiwezekani, akasogeza kidole kwenye sehemu inayosikika mapigo ya moyo, ….kimiya….keshakufa, Sweetie hayupo tena duniani….

‘Keshakufa ….ooh, mungu wangu..’ alaijikuta akianza kuishiwa na nguvu, na akamshikilia kiganja yule mgonjwa na kuanza kumuombea, alimuombea kuwa aende safari njema huko ahera, na amsamehe sana kwa kutokuweza kutimiza lengo lake la kumtibia, nia ilikuwepo, lakini mambo ayamekwenda haraka isivyo tegemewa….

‘Tumefika, mshusheni huyo mgonjwa….’ Wakasikia madakitari wenzake wakiamuarisha, lakini yeye moyoni alishajua kuwa uhai haupo tena kwa huyo mgonjwa, wanapoteza muda tu, na ….
Sweetie alichukuliwa na kuingizwa kwenye hiyo hospitali na wakati anatolewa kwenye gari, Rose akamsogelea na kumshika usoni, akisema moyoni; `kwaheri Sweetie, nilikupenda sana, na nilikuwa tayari kukupigania hadi hatua ya mwisho, na kama haukuwa na mke, nilikuwa tayari niwe mkeo, na hata kama unaye, huenda alishaolewa, basi …mimi nilishafunga azima ya kuwa nawe…na hata kama unaye mke na yupo anakusubiri, bado ningelikuwa rafiki yako, au ….’

‘Samahani,…sogea pembeni, tunamchukua mgonjwa, …hatakiwi kucheleweshwa …’ akaambiwa Rose, na mgonjwa alipoingizwa chumba cha wagonjwa mahututi, yule dakitari kabla hajafunga mlango akamgeukia Rose na kumuuliza `Wewe ndio mkewe…?’ akauliza yule daktari.

‘Ndi…ndi..ooh, aaah…ni…’ Rose akashikwa na kigugumizi na kuanza kulia.

‘Usilie, keshafika mahala pake, hapa tuna kila kitu siku hizi ,… atapona tu, usikatae tamaa, mumeo mtakuwa naye muda si mrefu, kaa, tulia, swali, omba….’aksema yule dakitari.

Na kweli Rose akaingia kwenye maombi, alikuwa san asana anamuombea huyo mgonjwa ambaye kwake sasa alishamuona kuwa ni marahemu,asamehewe madhambi yake, na alazwe mahala pema, peponi, lakini kwa nafsi nyingine, akawa anajipa matumaini kuwa huenda alimuangalia kwa mashaka, huenda ni kwa vile alichanganyikiwa…huenda bado yupo hai…huenda…huenda.

Wakati anawaza hayo akakumbuka kuwa kutokana na hali ilivyo, huenda asiweze kufika huko nyumbani kwake mapema, na hata kazini atachelewa kutokana na ruhusa aliyoomba, akaona ni vyema ampigie simu docta Adam, kumfahamisha na kama ikiwezekana, awaambie wafadhili kuwa pesa zao zipo tayari, lakini yeye hataweza kufika huko mapema kapatwa na dharura….

‘Umepatwa na dharura, dharura gani….?’ Akauliza Adam kwa ukali, na kabla Rose hajijibu akamwambiia `Wewe Rose, unataka kusema nini, kwanza umepatia wapi hizo hela, …?’ Akauliza kwa mdhaha, na hata kabla Rose hajajibu akasema `Ohooo, ni zile dhahabu bandia, umeamua kuwaingiza watu mjini, au sio…Rose angalia sana utafungwa, …shauri lako, …’ akatulia kwa muda halafu akakohoa kidogo na kusema tena….

‘Rose na kwa swala la wafadhili, mimi siwezi kuongea nao tena kuhusu wewe, ukumbuke sasa wanashughulika na wewe moja kwa moja sio kwa kupitia kwangu tenai,hata hivyo nitakuaminije tena, wakati muda wote wewe unakuwa kinyume namimi, hata kama nikiamua kufanya hivyo, nitakuwa najiweka pabaya sana, kwani najua mwisho wa siku utanitosa….kwanza huyo Sweetie wako ambaye unatanua naye huko, nasikia hali yake sio ya kupona…’akasema Docta Adam.

‘Nanii kakumbia hilo, ...?’ akauliza Rose kwa mshangao kwasababu kuondoka kwake huko n Sweetie, hakutaka kabisa bosi wake ajue, kwani alifanya kama kutoroka toka kwake. Sasa anashngaa kusikia kuwa Bosi wake anaua kuwa anaye huku na baya zaidi anajua kila kinachoendelea huku mjini, kwanini anaamua kufanya hivyo, ni kwa sababu kuwa kweli anafuatilia usalama wake, hapana, lazima kuna jambo jingine…akawa anawaza na kuwazua bila kujua ni kwanini….

‘Nani kaniambia,…hahaha…Rose, Rose… hivi wewe huJui kuwa mimi najulikana karibu nchi nzima, kila hospitali utakayoingia kuna watu wananijua, na kwa usalama wa wafdanyakazi wangu wao hunipa taarifa….ulipofika hapo tu, kuna mtu kanipa taarifa, na huyo mgonjwa anaishii tu kwasababu anatumia hivyo vyomvo vya kupumilia na haviwezi kutumika kwa muda mwingi, …nasikitika sana kukuambia hili, ila ni ili ujiweke tayari kupokea hiyo taarifa…pole sana…’ akasema Docta Adam.

‘Sawa yote ni mapenzi ya mungu, na huenda miujiza yake ikatokea pia…’ akasema Rose na kukata simu
**********
Docta Adam alipopokea simu toka mjini aliingiwa sana na hamu ya kusikia nini atakachoambiwa, licha ya kuwa alishawasiliana na hao jamaa zake kuchunguza nyendo za mtu wake, na akawa na shauku kujua nini hasa kilichompeleka Rose mjini. Jamaa yake huyo alimwambia kuwa Rose alifika mjini na kukutana na mmoja wa jamaa zake wa karibu wanaoishi mjini. Jamaa yake huyo wa karibu anafanya biashara ya uwakala wa madini. Adamu akakumbuka kuwa Rose alimwambia kuwa kauziwa madeni bandia, na alihis kuwa Rose naye alikuwa anatapatapa kutaka kumbambika mtu, kwa vile maji yamemfika shingoni….

Lakini cha kumvutia sana Adamu ni kusikia kuwa Rose ameonekana akiwa na jamaa mmoja,..aliposikia hivyo akashituka, alijua kuwa Rose yupo mjini, lakini kuwa na jamaa mmoja, hilo likamtia wasi wasi na kuulizia jamaa huyo ni nani, aliambiwa kuwa jamaa huyo ni mgeni kabisa machoni mwao, na hapo Adam akazidi kuingiwa na hamasa na kuulizia kutaka kujua jamaa huyo anafananaje, alipotajiwa sifa za huyo jamaa, akajikuta akishikwa na kigugumizi, na hisia zake zikawa zimeshamjua kuwa ni nani….

‘Ina maana huyu mshenzi katoroka hapa, kumbe alikimbilia huko mjini, inawezekana jamaa huyo ana mipango maalumu, kwanza alitorokaje wakati nilimfungia kwa ndani, ni nani alimfungulia mlango?...

‘Unawaonaje huko, wapowapo vipi…?’ akauliza Adamu akiwa kajawa na donge la wivu.
‘Wameonekana kama wapenzi, na wengi wanajua kuwa ni mtu na mkewe, kwasababu wameonekana wakitanua kwenye hoteli kubwa ya kitalii hapa mjini..na kufanya `shooping’ hapa na pale…’ akaambiwa na kauli hii ilimtia hasira sana Docta huyu, na chuki alizokuwa kazificha zikaanza kumuandama, alikuwa kishikilia ile simu na kuiminya utafikiri ndiyo yenye makosa, na kama isingekuwa bado anaongea na huyo mtu angeshaibamiza chini hiyo simu kwa hasira. Kichwani akawa analaani, `ina maana huyu dada kaamua kujirusha na huyo jamaa akijitia anamlinda, akijitia kuwa anamuuguza kumbe wana mapenzi yao ya siri, weli kaamua kaniacha njia panda, lakini sitakubali. Kwanza namlinda kwa kila hali angelishafukuzwa kazi, lakini hathamini juhudi zangu, na kesho tu anahitajiwa kikaoni na kikao hicho kama nijuavyo ni cha kufukuzwa kazi vinginevyo awe na hela za watu….’ Akapumua kwa nguvu.

‘Huyo jamaa ni tahira…namfahamu,…ina maana ndiye anajirusha na Rose, …Rose nay eye bwana, sijui anajiweka wapi, …hajui kabisa anajivunjia hadhi yake, ok, huyo jamaa ana matatizo ya akili, …sijui kafikaje huko mjini…una uhakika sifa ulizonitajia kuhusu huyo mtu, ndio hizo…?’ akauliza Adam.

‘Ndio hivyo hivyo bosi…mbona haonekani kuwa kichaa…yupo safi kabisa…’ akasema huyo mtu, na kitambo kikapita bila Adamu kusema kitu, hadi jamaa akaingiwa na wasi wasi kuwa huenda bosi kaibwaga simu chini na hataki kuonga tena, lakini alikuwa akisikia muhemo upande wa pili kuonyesha kuwa bosi bado yupo hewani, na labda alikuwa akiwaza nini cha kufanya. Jamaa huyo alipoona kimiya kinazidi, akaamua kuulizia.

‘Sasa bosi tufanyeje, …’ Adamu akasikia jamaa akimuuliza karibu mara tatu bila ya yeye kutoa jibu. Alikuwa anataka kutoa jibu, lakini alijua kabisa jibu hilo linaweza kumfanya akajijutia maisha yake yaote, na hasa kama hatakuwa muangalifu, lakini kama hatachukua hatua sasa, ina maana kile chote alichokitegemea hatakipata tena. Sasa lipi jema, kukaa kimiya na kupoteza au kupambana kiume…Hapo wazo likamjia kichwani kuwa wakati ni sasa, akisubiri sana atamkuta mwana sio wake…atamkuta Rose sio wake tena na chanzo ni huyo jamaa…jamaa tahira, kwasababu yake huyo yote yametokea, asingelitokea yeye sasa hivi huenda waneglikuwa wanaishi na Rose, ina maana kuwepo kwake huyo jamaa ndio kikwazo, sasa kwanini asikiondoe hicho kikwazo…na muda wa kukiondoa ndio huo, nafasi ipo nje nje, nini anasubiri…kinachosuburiwa ni kauli yake tu.

‘Sasa rafiki yangu, naomba unisaidia kitu, naomba sana huyo mtu asionekane tena,fanyani mfanyalo, huyo mtu apotee kabisa, ….’ Akamwambia huyo jamaa aliyempigia simu. Huku akikunja uso kwa chuki na hasira.

‘Mimi nakusikiliza wewe tu,….kwanza bosi nakumbuka umeniambia kuwa huyo jamaa ana matatizo kichwani, kama ni hivyo, mbona kazi itakluwa rahisi kwetu, …’ akasema huyo jamaa.

‘Usijali kila kitu kitakuwa tayari nikisia matokea…’akasema Docta Adam na kukata simu.

NB: Kama nilivyowaambia kuwa bado tunasubiria kupewa hiyo barua, kwahiyo najiiba iba, nikiwahi. Mungu yupo, na yeye ndiye mgawaji wa riziki!

Ni mimi: emu-three

4 comments :

Anonymous said...

Naona wengi tunependa kusoma kimiya-kimiya, hasa mimi, ila leo nimeguswa sana. Nikaona niongee kidogo, kwa kutoa maoni haya;
1. Huyu ndugu yetu keshasema kuwa ajira yake imefikia kikomo,na hali ya ajira ilivyo Bongo ni kwa kujuana, sisi wengi wetu tupo maofisini, cha muhimu kama mtu akisikia kuwa kwao wanahitaji mhasibu , basi tumfahamishe jamaa yetu huyu.
2. Kazi zake ni nzuri, namuonea huruma sana, kwani anatufurahisha lakini yeye anapata nini mwisho wa siku, ...kaweka hata ajira yake rehani, maana waajiri wakikuona unafanya mambo yasiyo stahili na kazi yako wanakujengea fitina. Sasa mimi nashauri kuwa kama kuna watu wapo kwenye sehemu wanachapa vitabu, au wanajua taratibu, basi tumsaidie jamaa yetu huyu, ili na yeye apate cha kuanzia.
3.Namuomba emu-three, asikate tamaa, kwani hayo ndio maisha, na kama kuna mtu ana nafasi ambayo huyu jamaa anaweza kufanya mambo yake, ...basi tumualike, ....
Ni hayo tu emu-three, samahani sana siku nyingi nipo nawe ninachofanya ni kuprinti kazi zako na kuzisomea nyumbani, sasa kimiya kimekuwa kingi, ndipo nilipotafiti nikagundua hili.
Ni hayo tu emu-three tupo pamoja

emu-three said...

Nashukuru sana kwa wewe uliyetoa hayo maoni. Kwa ujumla yamenipa faraja kubwa kuwa kuna watu wananijali kivitendo. Mungu awabariki sana!

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli wengi wanasoma kimya kimya na kutoka bila kuacha maoni. lakini usijisikie unyonge unafanya kazi nzuri sana. Na pole sana kwa yote..Maombi yetu yapo nawe.

Precious said...

Tuko pamoja M3 kimaombi na kuhangaika pia kama tukisikia nafasi yoyote. MUNGU MKUBWA SANA.