Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, September 19, 2011

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-28




Adamu akiwa amechoka huku kakasirika alimfuta yule polisi aliyekuja kumfungulia pale rumande, akafika mapokezi,akamkuta wakili wake kasimama pembeni,…hawakuongea kitu, yeye alifuta maagizo ya maaskari, leo alikuwa kama goigoi, kila anachoambiwa anafanya, aliambiwa na polisi aweke saini yake kwenye kitabu, na baadaye alikabidhiwa vifaa vyake…alivipokea harakaharaka na hakuwa na haja ya kuvikagua kuwa vipo sawa, alichokuwa anatamani ni kuondoka eneo lile na kufika nyumbani kwake, ambapo angeoga na kupata angalau usingizi, maana hizo mbu alizokutana nazo jana yake humo mahabusu hatazisahau,…achilia mbali ile hali ya hewa mle ndani, … alimlaani sana aliyekuwa mke wake kwa kitendo alichomfanyia, …

‘Na bado utafungwa sana mpaka ukome ubishi…’ ilikuwa kauli ya aliyekuwa mke wake akiwa kaongozana na hawo maaskari wakati alipokuja kukamatwa, …alikuwakafungwa mabandeji mengi usoni na mkononi, kama ushahidi…hakumbuki kuwa alimuumiza kiasi kile…alionyesha uso wa dharau na kebehi na hakuwa na lepe la huruma, angalau kumtetea ili asiweke rumande, …akachukuliwa juu kwa juu hadi kituo cha polisi na hapo alijikuta akiambiwa kuwa kakamatwa kwa kosa la kupiga na kujeruhi, na shitaka hilo limeletwa na mkewe ambaye kweli imethibitika hivyo kwa vipimo vya dakitari, na ushahid halisi wa muatahirika…

‘Lakini mbona hata yeye kanijeruhi, ina maana hamunioni,….au kwa vile yeye ni mwanamke, …hamuoni hali niliyo nayo….’ Akajitetea Adamu.

‘Kama uliumizwa ungelikuja kutoa taarifa, lakini wewe inonyesha kuwa ulitumia ubabe na yeye alikuwa naithidi kujitetea, ndio maana hata wewe uliumia….’ Akasema yule askari!
‘Naomba niwasiliane na wakili wangu, maana siwezi kulala humu ndani, kwa ujumla yeye huyo alikuwa mke wangu, na tuliachana,…alifika kwangu na kuanza kuleta furugu, …na baadaye tukashindana hadi kufikia hatua ya kupigana…’ akajitetea Adam, lakini polisi walimuuliza kwanini alipoona hivyo hakuiarifu polisi, na badala yake akaamua kuchukua sheria mikononi mwake, yeye anaielewa vyema sheria, kwahiyo hana cha kujitetea.

‘Kitu kinachotutisha sasa hivi ni kuwa maeneo yetu kwa ujumla kumekuwa na kesi nyingi za kuzalilishwa wanawake, wanaume wanawapiga wanawake wao kwa kusingizia kuwa waligombana kidogo, na hilo limefanyiw auchunguzi wa kina na kuonekana kweli wanaume ni wakatili kwa wanawake, sasa sisi kama walinda usalama hatutalifumbia macho hili swala, hii ni shutuma kwetiu kuwa hatutendi haki, ….na leo tumethibitisha jinsi gani ulivyokosa huruma unampiga mwanamke kiasi kileswall…hili swala lazima likomeshwe na wewe atakuwa mfano kwa wengine….’ Akasema mkuu wa kile kituo
Hata vile alivyojaribu kujitetea haikusaidia na baya zaidi kila akimpigia simu wakili wake , simu ilikuwa haipatikani, ikabidi aandike ujumbe,na yeye akaswekwa ndani.

Docta Adamu alilaani jinsi siku yake ilivyogeuka kutoka kwenye msisimuko wa kukutana na mtu aliyemuhitaji sana na mipango yote aliyokuwa ameipanga, imegauka kuwa kashifa, kuzalilika na hadi kuumbuliwa kwa kuwekwa ndani, alitahayari sana…akiwa anawaza kiundani jinsi siku yake ilivyoiharibiwa, alijipweteka chini , sakafuni , chumba kilikuwa hakina godoro, kina sehemu imetengenezwa kwa udongo wa saruji kama benchi la kukalia, na hapo ndipo alitakiwa kuweka ubavu wake, …aliwaona wengine wakiwa wamejilaza…

Alimuomba yule mkuu wa kituo, ajidhamini mwenyewe, lakini haikusikilizwa….mkuu wa kituo akawa keshaondoka, na wale askari waliobakia walikuwa hawana mamlaka yoyote ya kumtoa mle mle ndani, wakawa wanamsikiliza tu …. Alijipweteka chini ya sakafu manana pale kwenye sehemu ya kukaa kama benchi, wapo wenzake walishawahi na wamelala, akainamisha kichwa chini, kwa kukiweka kwenye magoti huku anawaza mengi, hakuamini kuwa ipo siku atazalilika kiasi kile, akiwa kainamisha kichwa chake kwenye magoti ndipo mawazo ya siku nzima ilivyokuwa yakamjia…

Alikumbuka jinsi alivyohangaika siku nzima baada ya kupokea barua toka kwa wafadhili kuwa hiyo ni barua ya onyo la mwisho kwa Rose, kwa kutokutii barua ambayo ilikuwa kama makubaliano,…kwamba akubali kuwa atalipaje hilo deni, alilolidhamini, ….ingawaje kulikuwa na masharti mengine, lakini yote yalikuwa yametokana na hilo deni…kilichotakiwa ni yeye kukubali kwa maandishi , kwa kuandika baruia nyingine inayokuabaliana na hilo, halafu afike kwenye kikao cha makubaliano, …lakini yote hakufanya…ikaonekana kuwa kafanya dharau.

Docta Adamu alipoipata hiyo barua aliona kuwa sasa mambo yamekuwa mabaya kinyume kabisa na alivyokuwa katarajia, na ilivyo hangeliweza kumtetea zaidi Docta Rose kama yeye mwenyewe hatajitetea, kwahiyo alimpigia Rose simu, ili wakutane wapange jinsi ya kukabilaiana na hilo tatizo…alishangaa jinsi alivyojibiwa, mwanzoni Rose alionyesha kutokujali, akaleta hata ukaidi….hapo Docta Adam, akaona asipofanya jambo, lazima Rose atakufukuzwa kazi, na itakuwa mbaya kwake,….kwani anaweza akamkosa kabisa, na hata hivyo alikuwa anatakiwa kulipa fadhila zake kwa Rose, kwani kama isingekuwa yeye ……

Kwahiyo akafanya jambo moja la hatari kidogo, lakini alijua mwisho wa siku ataeleweka tu…kwahiyo baadaye jambo hilo lilipofanikiwa akampigia simu Rose na kumtajia kuwa anajua wapi Sweetie wake alipo, akasikia Rose akisema atakuja,…Hiyo kauli ilimpa matumaini makubwa kuwa kwa vyovyote Rose atakuja tu. Kwahiyo akahakikisha nyumba ipo safi hasa varandani akaweka vivutio mbalimbali, akiwa na nia ya kumshawishi Rose kuwa nampenda na kumjali, akanunua Ua la ghrama la waridi na akaliandika ‘Rose I love you’ na yale maandishi yaliwekewa kitu kama taa, kwahiyo humeremeta kwenye lile ua na kutengeneza taswira nzuri ya kuvutia, na pia alinunua zawadi nyingi tu na mwisho akanunua pete ya dhahabu, hiyo ni maalumu kwa kuomba uchumba…..

‘Lazima atakubali tu, hii ni kete yangu muhimu ….’ Akajipa moyo wakati anaweka mambo safi.
Baada ya maandalizi yote hayo na kuhakikisha kuwa vinywaji maalumu vipo, akachagua mziki maalumu , mziki wa wa taratibu ambao mara nyingi alimsikia Rose akiuimba na hata kuusikia kwake akimtembelea, na alishamwambi akuwa anaupenda sana huo mziki! Baada ya kuhakikishja kuwa kila kitu kipo tayari akakaa kwenye kochi huku akivuta muda kumsubiria mtu muhimu kwake, …muda ukapita mpaka akaona kuwa huenda Rose kaghairi, …alipoona hivyo akatoka hadi chumba alichokuwa kamweka mtu wake maalumu kwake…chambo chake…alijua kabisa akimtumia huyo, lazima Rose atakuja tu, na sasa aliona amtumie kwa kumpigia Rose simu, halafu akiitikia tu anamuunganishia na mtu wake…

‘Wewe muhuni, Sweetie wako anataka muongee…’ akasema huku anafungua chumba alichokuwa kamweka huyo jamaa, lakini kwa mshangao alikuta chumba kipo kitupu, akashituka, nani kamfungulia huyu jamaa, akazunguka huku na kule bila kuamini kuwa chambo chake alichokuwa kaikiweka kwnye ndoana, kimechomoka….je atawezaje kumnasa huyo mtu muhimu kwake….! Akakarudi chumbani kwake huku akiwa na imani kuwa Rose atakuja tu, akatulia huku anawaza afanye nini zaidi kama Rose ataamua kutokufika na huku keshafanya maandalizi makubwa kama yale, akainua simu kutaka kumpigia Rose, lakini akaona avute subira kwanza kwani muda bado upo….na akajilaza kwenye kocho lake na kujikuta akipitiwa na usingizi…

Ndani ya usingizi akawa anaota anazozana na aliyekuwa mke wake huku Rose yupo pembeni anawacheka kwa dharau na kuwaona wajinga, akisema anashangaa kumuoa mume kama yeye kumuoa mke mshamba …mke ambaye hajui kuiishi na mume, ndio maana anazalilishwa kiasi hicho….kwa hasira akamwendea mke wake na kutaka kumpiga, lakini kabla hajamfikia mara akazindukana toka usingizini na kusikia kelele nyingi hook nje…ikabidi akurupuke haraka na kwenda kufungua mlango kuona kuna nini…
Zilikuwa sauti za watu wakiwa wanaangalia ugomvi wa wanawake wawili, na hamu ikamjia kujua ni akina ani hawo wanawake, aliposogea…akasikia sauti….sauti , ile anajua kokote kule, ni sauti kali ya aliyekuwa mke wake…akasogea karibu kuona kuwa anagombana na nani….oooh, alipofika pale alishituka, ….akawa haamini, yule aliyelala chini huku kakanywagwa kwa mguu, na sio kukanyagwa tu, anatimbwa kwa nguvu…alikuwa ni ….akawa hana uhakika vyema, akasukuma watu na kupita mbele….ooh, alikuwa ni Rose, ….

Kwa haraka akawasukuma watu na kwenda kumuokoa Docta Rose….Hakuamini kuwa huyo mwanamke angelikua tena kwenye anga zake kwani walishamalizana na kumlipa fidia nyingi sana, na hata wakati walishapeana talaka, sasa iweje aje tena wakati yeye sio mume wake tena, huyu ana lake jambo….akamsogela pale aliposimama, alikuwa hajamuona.

Rose alikuwa chini na hakuonyesha dalili zozote za kupigana, ilionekana kuwa hakutaka kuibisha mashambulizi, hata kama alikuwa akitimbwa kwa mguu kama mtu anayekanyaga gunia. Docta Adamu akatoa sauri ya ukali, na alijua akitoa sauti yake tu aliyekuwa mke wake atasalimu amri, na kweli alipolisema ` Wewe mwanamke unaleta fujo gani hapa kwangu,….’ Aliyekuwa mke wake alisinyaa na kuacha kile kitendo alichokuwa akikifanya cha kumtimba mwenzake kwa mguu na akamgeukia akiwa anaonyesha uso wa hasira chuki na sasa akiwa tayari kumgeukia yeye kwa mapigano….

Kilichofuta baadaye ikawa vurugu ,…kwa Adam hakuona ajabu kwani alishamjua huyu mke wake kuwa ni mpenzi wa shari, hakanyiki kwa kuongea hata siku moja, utaongea mpaka utachoka na mwishowe anakudharau tu. Hili alijifunza katika miaka yao mitano ya ndoa, ambayo ilitawaliwa na vuruga karibu kila siku. Alikumbuka baada ya kumuona, haikuchukua muda, siku za mwanzoni tu, walianza kukorofishana na mkewe huyu na ugomvi wakati mwingine ulikuwa wa mambo madogo madogo ambayo hayakuhitaji kugombana, na hata pale alipojaribu kumrekebisha mkewe kwa hekima aliambulia matusi, akashangaa, na kujiuliza huyu mtu yukoje, kosa kafanya yeye, na akielekezwa anakuja juu, na mwishowe anakimbili matusi, akajaribu kuvumilia.

Siku kadhaa, akagundua mambo yaliyomkatisha tamaa kabisa, hayo yalivuka mpaka, alianza kwa kuambiwa na watu, akawa haamini, na baadaye mwenyewe kwa macho yake akashuhudia, alimfumania moja kwa moja mkewe akiwa na mwanaume mwingine, ndani ya chumba na kitanda chao…siku hiyo alitamanani kuua, …alishindwa hata achukue hatua gani…kwa hasira akaanza kumpiga mkewe,baada ya yule mwanaume kukimbia, ha hapo ndipo alipogundua kuwa mkewe kupigwa kwake ni jambo la kawaida, na ukimsema kwa maneno hawezi kukuelewa, na kupiga inabidi ujitahidi kweli maana mkewe aslikuwa kama vile bondia ….


‘Hebu kama mwanaume kweli niguse, …’ hiyo ilikuwa kauli yake ya mara kwa mara ambayo Adamu hakupendwezwa nayo kabisa….hakuwa na nia ya kupigana….
Tabia ambazo Adamu zilimkera kutoka kwa mke wake huyo zilipozidi Adamu akaona kwanza aonane na aliyekuwa mashenga wake, alikuwa rafiki wake wa karibu na akaona sio jambo jema kulipeleka hili swala mbele, ngoja kwanaza alifikishe kwa huyu mshenga wake. Mshega wake alikuwa akimjua huyo mwanamke vyema, na alikumbuka siku alipomuomba kusaidia hiyo kazi ya ushenga, alishauriwa na huyo mshenga kuwa awe makini kweli, kwani familia ya huyo mke anaijua vyema, …
‘Rafiki yangu tabia haziwezi kuwa sawa, ila kwa uzoefu wangu, familia ile ina tabia ambayo kama huijui utateseka sana,…siwezi kuilamu kama familia, na kila familia ina uzaifu wake ila ile imezidi, nakwambia hilo kwasababu nimelishuhudia hilo kwa dada za huyo mkeo, walioolewa mapema, lakini wameolewa na watu ambao tabia zao zinaendana, ….hutaamini kuwa kuna watu wasipopigana katika ndoa hawaoni raha, na ugomvi wanautafuta kwa visingizio vidogo, kwao ni moja ya mapenzi, unaamini hilo docta?’ rafiki yake huyo alimuuliza kama vile mzaha...
‘Hili kwangu siamini, hakuna haja ya kupigana kwa mke na mume, kwani mumeshakuwa kitu kimoja, ni sawa na kusema mkono huu umpige mkono….’ Akasema Adamu akionyesha kwa vitendo, halafu akaendeela kusema `Kama mnapigana ina maana hampendani, mimi yule binti nimempenda, tangu siku ile alipokuja akiwa anaumwa, nikamtibia tukaanza kujenga urafiki na nimemuona kama nikimuoa tutaweza kuishi naye,…hilo lisikutie shaka, akifika kwangu kwanza lazima asome zaidi…nitamwelka sawa, hakuna linaloshindikana ukiwa na nia na maelewano..’ akasema Docta Adam.
‘Sawa kupenda bwana ni kitu cha ajabu sana kwani ukipenda hata chongo utaita kengeza, mimi sitaki kukukatisha tamaa ila nakupa ushauri tu, maana ni vyema, ukitaka kumpata mwenza, usichukulie juu ju tu, kwani huyo utakaye muoa anakuwa sehemu ya maisha yako, mchunguze vyema,toka asili yake , ….lakini nyie wasomi wa siku hizi hamuangalii hilo , ukishapenda mambo mbele kwa mbele, …..sawa, mimi nitakusaidia kwa hilo, ila ushauri wangu mkubwa ni kuwa kama unaoa kwenye ile familia uwe jasiri ….na kama nilivyokuambia wapo watu wengine wamejijengea katabia kuwa kupigana ni sehemu ya mapenzi,… ‘ akashika kidevu huko akimwangalia Adam kwa makini.
‘Nakusikiliza mzoeufu…’ akasema Adam.
‘Kweli hilo nikwambialo lipo, nyie simnakaa tu ofisini, sisi tunajichanganya, tupo na jamii wakati wote, wapo watu urafiki haukamiliki mpaka mkong’oto….usije ukaogopa kutumia nguvu kidogo…na ukilemaa kwa hiyo familia utapigwa wewe mwenyewe….hahaha…hujasikia wanawake wanawatwanga wanaume zao, basi hiyo famili ukiwa legelege utatwanga kisawasawa….nisikutishe, maana vyema ukaingia uwanjani kuucheza mpira umkimjua mwenza wako, sio kuingia kichwa kichwa, au kuwa shabiki, shabiki anajifanay kujua sana, lakini mwambie acheze huo mpira, utaishia kwenye ugoko…hahaha….sawa ushenga nitakufanyia safi kabisa…’ akakubali rafiki yake huyo wa kimila.

Kweli yale yale aliyoambiwa na huyo rafiki yake, ndiyo aliyokutana nayo, akaona bora akutane na rafiki yake huyo mzoefu …akamwendea siku moja ili watoke kuongea kidogo, alijua kwa uzoefu wake huenda anaweza kumsaidia na kuondokana na hilo tatizo, …wakaanza kuongea na baadaye Adamu akampa hiyo taarifa, na huyo jamaa alipopata hiyo taarifa hakushangaa sana, akasema `sinilikuambia, mambo mengine hayahitaji kwenda shule, tabia ni tabia, ….lakini usikate tamaa, ngoja mimi nitalifanyia kazi, kwanza nitaongea na shemeji nione ana tatizo gani, na ikibidi itabidi wewe uwepo, lakini kwanza ngoja niongee naye faragha, nitakuWa namtembelea shemeji, niongee naye, wewe ukiwa mzigoni, kapige mzigo wako ukirudi tutaongea…’Docta Adam akaona hilo ni jambo jema, huenda mambo yakawa shwari.

Aliporudi siku hiyo alimkuta mkewe kanuna, akamuuliza kisa nini, akaambulia maneno, ya kashifa na kuambiwa; `Hivi wewe umeshindwa kuishi na mkeo, umeshindwa kumlea mke mpaka unahitaji msaada wa wanaume wenzako, wewe mwanaume wa namana gani….sawa kama hilo ndilo unalitaka hakuna shaka, …’ akaambiwa.

‘Lakini mke wangu ninachotaka ni kuyaweka mambo sawa, na nia kubwa ni kuona kama kuna jambo unahitaji, tusaidiane , na huenda hutaki kunaiambi mimi, nikaoana nimtumie huyu mtu anayewajua vyema, kwani nimekuulizia nimetafiti sioni ufumbuzi, kwahiyo huyo mshenga anakujua vyema tangu ukiwa mtoto hadi ukawa msichana, nikaona labda atanisaidia kwa hilo….kama nimekosea naomba unisamehe, naomba tuyajadili haya wenyewe basi, …unaonaje mke wangu?’ Akasema Adam.

‘Mimi sina la kujadili, ..una uhakika kuwa huyo mshenga ananijua vyema mimi, na je huyo mshenga unamjua vyema wewe, au unamsikia tu…wewe ni mwanaume sio, unatakiwa upambane kiume, kama umeshindwa na kutafuta wanaume wengine wakusaidie sawa…mimi nipo tayari, nishakuambia sawa….sihitaji muda wa kuongea, kwanza nina mambo kibao ya kufanya….’ Mkewe akasema na kundoka na kumuacha Docta Adamu haelewi afanye nini tena, na hata alipojaribu kumfuata mke wake huko jikoni ili waongee wakaishia kuzozana na hata kukawa hakuna usalama kabisa.

Hakuweza kuonana na mshenga wake karibuni na hata alipomtafuta na kukutana naye majibu aliyopata yakawa hayana muamala mwema, akaona sasa huyo sio msaada mwema kwake, afanyeje, …akajarabu kutumia ujuzi wake wa kidakitari kwa kumuita mkewe aje kazini kwake amuhoji kama mgonjwa, na siku hiyo aliabika kweli, kwani mwenzake alianza kupayuka humo ofisini na hata watu wakaja wakizania kuna ugomvi….

Docta Adam akaanza kukonda kwa mawazo, hakuamini kuwa ndoa inaweza kumtesa mtu kiasi hicho, akafikia hatua ya kuomba ushauri kwa wataalamu, madakitari wa ushauri nasaha, lakini mkewe wake alimwambi yeye sio mgonjwa, na hatafika hospitalini labda awe anaumwa, na yeye anauhakika kuwa haumwi. Ikabidi Docta Adamu awe anapata ushauri mwenyewe na kujaribu kuutumia kwa mkewe, lakini yote hayo kwa mkewe yalionekana kama mume legelege…alifikia kumuita hivyo, `wewe ni mume legelege…’ hakuelewa hilo neneo legelege lilikuwa na maana gani kwake.

Basi siku moja akakutana na huyo mshenga wake na mshenga wake alimwambia yale yale aliyozoea kumwambia, akamwambia hivi;

‘Huyo unatakiwa uwe mkali kweli, kwani kupigwa, au kupigana wao wanaiona kama sehemu ya mapenzi, hutaamini hilo , kama nilivyokuambia kuwa dada zao wapo hivyo hivyo, kuna dada yake mmoja kaolewa na jamaa bondia, wao wakikorofishana wanavyaa kibondia na kuanza kupigana kiukweli hasa, na mwisho wa siku kila mmoja hasira zimekwisha siku zinakwenda…na huyo mdogo wake naona yupo hivyo hivyo, …’ akaambiwa, lakini kwa Adamu hilo halikumuingia akilini kabisa, na hata hivyo alimuoma rafiki yake huyo kama kabadilika sivyo kama vile alivyokuwa akiongea naye mwanzoni, akaona labda nay eye kachemsha, kwani mkewe hana subira ya maneno, anaweza kukutoa nishai ukabaki kushangaa.

Siku moja alirudi nyumbani kwake , na wakati anataka kuingia nyumbani kwake akashangaa anaitwa na mzee mmoja jirani yao, yule mzee akamwambi ana maongezi naye kidogo, …lakini Adam alikuwa na haraka sana, akamwambia yule mzee kuwa kwa muda ule haitawezekana kwani kaja kwa haraka kuna wagonjwa wengi kazini kwake, na amerudi mara moja kuonana na mkewe. Na kweli ilikuwa hivyo kuwa aje mara aonane na mkewe, kwani aliondoka asubuhi bila kuacha chochote, akiwa na nia kuwa akifika ofisini atapata kiasi na kurudi nyumbani haraka, na ndivyo ilivyokuwa, na wakati anafungua mlango baada ya kubisha hodi kwa muda bila kujibiwa, ndipo huyo mzee akatokea… mkewe alikuwa hayupo, na hakujua kaenda wapi mapema yote ile…!

Yule mzee akamwambia ` sitaki kukupotezea muda wako, najua wewe una kazi nyingi, na kazi hizo nyingi zina madhara yake, wenzako wanakuchora, na wameshakujua hivyo…. ila ninachokushauri kuwa uwe mwangalifu na hawo marafiki zako, wanakugeuka,…’

‘Mzee una maana gani kusema hivyo marafiki zangu ni akaina nani wanaonigeuka’ akauliza Adam.
‘Hilo siwezi kukuambia ni akina nani, nitakuwa mmbea, ila chunguza,…utagundua mwenyewe…nenda kazini kwako Docta, utawaumiza wagonjwa wako….’ yule mzee akaondoka na kumuacha Adamu akiwaza, na kwa vile alikuwa na haraka akaacha pesa sehemu ambayo ana uhakika mkewe ataikuta na kuacha ujume, alishangaa mkewe hata simu kaacha humo humo ndani, kwani alikuwa akipiga inaita haipokelewi, na alipofika hapo akaikuta ipo kitandani.

Basi siku nyingine akakutana na huyo mshenga wake , na siku hiyo aliamua kurudi nyumbani mapema kama nia ya kubadili tabia na nyendo zake ili kuona mambo yanakwenda vyema, ilikuwa sio siku ya kazi nyingi…na wakati kapumzika mara mshenga wake akafika na kupiga hodi…`shemeji upo, nahitaji chai shemeji….’ Na alipofungua malngo akamkuta Adam kajaa sebuleni.

‘Oooh , leo upo Docta, nilifika mara moja kumuona shemeji, kuhusiana na lile jambo uliloniomba, nimeonega naye sana, naona sasa kama anakuja kuja…..ila nazidi kukusisitizia kuwa uwe mkali, wake wa namna hiyo wanahitaji ukali, sio ulegelege….

‘Ulegelege, una maana gani, kwasababu neno hilo nimelisikia tena…lakini mimi sijaamini hivyo kuwa kupiga ni sehemu ya utatuzi wa matatizo ndani ya ndoa, kama unamaanisha hivyo, ila nataka tu uelewe kuwe imefikia hapo, nimesema wee, nimejaribu kutumia utaalamu wangu wa kidakitari kumkanya na kumuelezea, lakini hasikii, inafikia hata kinidharau kuwa eti mimi sio mwanaume, nikirudi kazini nakimbilia kulala, …imenishangaza sana,… kweli kutokana na kazi yangu ipo siku nachoka, lakini sio kila siku na nilipoliguindua hilo nikajibadilisha ili ntwende sawa, kwani najua umuhimu wa mambo hayo kwenye ndoa,na najua nini nifanye , lakini haijasaidia kitu…tatizo kubwa, yeye akiamua lake kaamua…yaani nashindwa nifanyeje, maana huko kazini mambo ni mchakamchaka, ukirudi nyumbani umechoka ile kuchoka, na nilitaraji kuwa ukiwa na mweza utapata kitulizo, kumbe ukirudi unakutana na karaha, sijui wapi nimekosea je wewe ulipoongea naye umegundua nini…?.’ Aksema Adam.

‘Unajua ukiongea naye hana matatizo ila…nilichogundua ni wewe kuwa labda kutokana na majukumu unakuwa huwajibiki…sio kuwajibika kwa kutokupenda, lakini…ni waibu wa kiume…unanielewa vyema…uwajibike kiume….sasa mtu kama huyu hawezi kujua hilo kuwa umechoka, una kazi nyingi…na nilivyomdadisi kuhusiana na hilo anaishia kusema kuwa mbona wengine hawapo hivyo, wana kazi zao wanawajibika…analinganisha na wengine, …kuwa mkali, wajibika sana, punguza kufanya kazii sana, kwani ni lazima kila kazi ufanye wewe bwana tusidanganyane, usikwepo majukunu yako…..’ akawambia yule mshenga wake, na huongea kama utani, lakini alikuwa na maana yake!

Adamu akaanza kubadili ratiba yake, na kwa kufnya hivyo ndio akagundua mengi, alikuwa hana tabia ya kurudi nyumbani bila taarifa, akawa sasa muda wowote anafika nyumbani, na ndipo siku moja alifika ghafla na kukutana na jambo lililo mkatisha tamaa na kukumbuka maneno ya yule mzee kuwa kumbe marafiki zake wengine ndio wanaomgeuka, ….!

Siku hiyo lifika nyumbani ghafla, na alipofika akakuta mlango upo wazi, na hili alishamuonya mkewe kuwa mwangalifu , asizoee kuacha milango wazi, sasa siku hiyo alikuta kuanzia getini kupoi wazi, mlango wa ndani wazi…..akaingia bila hodi na ghfla akasimama mlangoni, aliona viatu vya kiume vimevuliwa nje ya mlango wa chumbani…akavitizama kwa uangalifu, akawaza ni nani kaleta viatu hapo, hakutaka wazo la kuwa mkewe ana mtu ndani limwingie moja kwa moja akilini, lakini dalili zote zilionyesha hivyo!

Kila dakika iliyopita ilikuwa kama mtu anajazwa hasira kifuani, na ndani ya mwili wake na kumfanya asisimukwe kwqa hasira na alichofanya nikuchukua panga toka jikoni na taratibu akasukuma mlango wa chumbani…..lolololo…

‘Nahisi kuna mtu kaingia vile…’ alisikia sauti ya mkewe ikiuliza …

‘Wewe unaanza visa, nilikuambia ufunge mlango na funguo,..ulifanya hivyo, au unanitega, ili nifumaniwe… na isije ikawa ni rafiki yangu amekuja, maana kama ni yeye utanifanya nihame mji, na sijui nitauweka wapi uso wangu,….lakini hii ni moja ya kazi aliyonipa ni kazi nyeti sana, hapa najaribu kukuweka sawa, au sio, sogea huku basi…hahaha…wewe kweli ni mrembo kwanini usimpagawishe mumeo akasahau machungu unayompa, …mbona mimi unanipagawisha mpaka nimemsahau mke wangu…’ akasikia sauti ambayo hakuamini kabisa kuwa ingekuwa hivyo…hakuamini, na hapo akaamini ule usemi usemao kikulacho kinguoni mwako…!

NB, Natumai wikiend ilikuwa njema, tuwepo kwenye sehemu ifuatayo, ili tumue huyu Docta Adam, katokea wapi ….TUPO PAMOJA


Ni mimi: emu-three

5 comments :

Anonymous said...

Tobaaaaaaaa! kweli si kila aliye karibu ni rafiki yako, we mshenga hata aibu huna????? umetumwa kujua nini tatizo linalomfanya mke awe hivyo wewe umefunua hadi vya uvunguni?????? Du! pole doct Adam ila nawe hukutaka kusikia ulivyoambiwa mwanzo kuhusu huyo mke na njia uliyotaka kuitumia kwa Rose si sawa siku zote mapenzi huja yenyewe hayalazimishwi. Jane

Simon Kitururu said...

Kazi nzuri Mkuu!
Nipo hapa kijiweni ingawa sijasema kitu hapa kijiweni kwa muda!
Tuko pamoja!

Anonymous said...

Nahisi kama nina upungufu wa kitu ambacho nimekosa kwa siku kama mbili hivi!!!! Jamani naomba ningekuwa na uwezo ningetatua hili tatizo linalokukabili ili tuwe tunapata vitu vipya kila siku. Lakini naamini hata kama siwezi kufanya kitu basi Mungu atafungua njia upande mwingine. Jane

Yasinta Ngonyani said...

Pole Doc. Adamu...sasa hapa sijui wanaume au wanawake ndo wasaliti?...ama kweli kikulacho ki nguoni mwako..unayemwamini kumbe siye...kaaazi kwelikweli!!!

emuthree said...

Jamani wapendwa wangu msinione kimiya ni ile mitihani na hapa natumia simu ya kiganyani kuandika hii meseji,angalau mjue kuwa tupo pamoja. Kesho mungu akipenda nikafika kwa ofisi mapema kabla hawajafika wajamaa nitavizia computa yenye neti ! Mungu yupo ipo siku. Na dua zenu ni muhimu sana