Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, August 25, 2011

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli-19




`Sweetie wako…., una maana gani kuita jina hilo, Sweetie wako…?’ akauliza Maneno, huku akiwa kasimama mbele ya kochi alilokuwa kakalia Maua. Maua akacheka na kulaza kichwa kwenye kochi huku akiwa kafumba macho kama anawaza kitu kwa mbali, na huku kwa kuwaza hivyo anajiona kama yupo mahali fulani, na neno hilo au jina hilo ndilo linalompa faraja fulani. Aliwaza mbali sana, akiwa analikumbuka hilo jina na chanzo chake.

‘Mume wangu, hivi niwe nakuita nani kama nataka kukuita kwa sauti, ukiwa mbali, nikuite jina lako,Mhuja au nkuite mume wangu, au baba nanihino?’ alikumbuka siku moja alipokuja mgeni, na wakati huo mume wake yupo chumbani, mgeni huyo alikuwa baba mkwe wake alipita kuwasalimia mara moja, sasa akawa anajiuliza amuiteje mumewe kwa sauti. Kwasababu ilikuwa siku za mwanzoni mwanzoni mwa ndoa yao, aliogopa kumuita `mume wangu’ mbele ya mgeni, na kuinuka pale kumuacha mgeni peke yake akaona sio adabu…na bahati nzuri mumewe akatoka nje na kuwakuta baba yake akiongea na mkwewe. Na mgeni alipoondoka, ndipo Maua akamuuliza mumewe, awe anamuita jina gani kwa sauti.

‘Wewe ulitaka jina gani, mimi nitakuita Sweetie na wewe utaniita nani?’ akasema Mumewe
‘Sweetie, ….mmh, mbona jina hilo halifai kuitwa mbele za watu, hilo linafaa kuitana chumbani…” akasema Maua.

‘Chumbani au hadharani kwa mume na mke haina tofauti,mimi na wewe tumeshahalalishwa, hakuna cha kuoneana aibu, kwanza kuniita `mume wangu’ ingelitosha tu kabisa, maana hicho ndio cheo change halali mbele ya mungu na mimi nikikuita `mke wangu’ inakuwa imependeza zaidi, au sio lakini kwa kuonyesha kuwa nakupenda zaidi ya kupenda, na pendo la zati, lenye raha ya ajabu, basi mimi toka leo nitakuwa nakuita `Sweetie’ na wewe utatafuta jina la kuniita…’ akasema Mhuja na kuja kukaa karibu na mkewe, na mkewe akalaza kichwa chake mapajani mwa mumewe.

‘Hata mimi nitakuwa nakuita hivyohivyo…ingawaje jina lenyewe limekaa ki-kike-kike..’ akasema Maua, huku moyoni akimshukuru mungu kwa kumpa mume anayeonyesha kuwa kweli anampenda kizati, hatajaii kuwa kutakuwa na mabadiliko yoyote, akimuomba mungu amsaidie waishi hivyohivyo milele na milele, kwani akiwa karibu na mumewe huyo anajion kama wapo peponi. `Kweli ndoa ina raha yake na hasa mnapokutana wawili mnaopendana na mkajuana nini mwenzako anakitaka!’ akajikuta akiyasema yale maneno kwa sauti ya chini.

`Umenena kweli Sweetie…’ akasema Mhuja huku akichezea nywele za mkewe,
***********
Maua likuwa mbali sana akikumbuka chanz cha ina hilo na ndipo akamwambia Maneno ‘Unaniuliza kwanini nimetamka hilo jina Sweetie, wakati umenipiga marufuku nisiwe nazungumza au kukumbuka mambo yangu yaliyopita, jina hilo ni muhimu sana katika maisha yangu na nikilitamka hilo najisikia faraja sana, na namkumbuka sana mume wangu,…naogopa hata kutanguliza neno `marehemu’ ninapomtamka mume wangu, na sipendi watu wakitanguliza neno hilo, ila nashindwa kuwazuia tu, kwani namuona kama bado yupo hai…siuji kwanini nahisi hivyo…Sweetie ndilo jina lake nililokuwa nikimuita na yeye pia alikuwa akiniita hivyo hivyo….hatukujali kuitana hata mbele za watu, tangu siku ile tulipopeana majina hayo…mpaka watu wengine wakadhani andilo jina langu...’akasema Maua huku akiwa bado kafumba macho.

‘Mhh, Maua, Maua…kwahiyo inavyoonyesha hapo ulipo upo na Sweetie wako kimawazo, ngoja niondoke, maana wewe na Sweetie wako hamuachani, …’ Akasema Maneno nab ado akiwa kasimama mbele ya Maua. Maua akafumbua macho na kumtizama Maneno kwa muda. Maneno alikuwa katizama dirishani na kuendelea kusema `Nimeshakuambia kuwa ili uishinde hiyo dhamira achana na mawazo hayo kwasababu hayo yapo nje ya uwezo wetu wa kibanadamu, tumeambiwa kuwa, mpende umpendaye, lakini ipo siku mtatengana naye, ama yeye au wewe, mmojawapo atatangulia, na penda uyapendayo,iwe mali au umasikini, lakini ipo siku utayaacha…kwahiyo licha ya udhaifu wetu, unyonge wetu wa kujipa moyo na kukubali hayo, lakini ndivyo hali halisi ilivyo…..’ akasema Maneno na kumsogelea Maua akamshika miguu yake miwili kwa mikono yake huku akimwangalia usoni.

‘Maua hata kama Mhuja kaondoka duniani, sio mwisho wa upendo, sio mwisho wa maisha, wapo watu wanakupenda sana kama alivyokuwa akikupenda Sweetie wako.Kwahiyo nakuomba uuachie mlango wa upendo wazi ili aweze kuja mtu mwingine,…’ akasema Maneno huku akimwangalia Maua usoni, na Maua akawa anamwangalia Maneno kwa macho ya kutahayari, kama vile haamini maneno kama hayo yangetoka mdomoni mwa mtu kama huyo. Huyu ndiye rafiki mkuu na alikuwa kama ndugu wa Mhuja, leo yeye anaoenekana kama kamsahau…hapana. Akatamani kuinuka na kukimbilia chumbani, Lakini baadaye akaguna na kukiri moyoni kuwa kuna ukweli ndani yake, hivi ataombeleza mpaka lini, mwaka na kitu sasa, na hata kama ataomboleza hadi mwisho wa maisha yake ndiyo itakuwa nini…akasogeza mikono yake na kuishika mikono ya Maneno kwenye viganja, na kusema;

‘Ahsante sana kwa kunijali shemeji, nimeamini kuwa wewe ni rafiki wa kweli…’ akatabasamu
Hii ilikuwa hatua kubwa sana kwa Maneno kuweza kumsogelea shemeji yake, hata kuweza kumgusa shemeji yake, ilikuwa ni kitu ambacho hakukitarajia kabisa, na siku aliyoweza hata kumkaribia ni baada ya kutoka naye kwenye mbuga za wanyama, aliona kuna mabadiliko makubwa sana na aligundua kuwa Maua anapenda sana wanyama, na akaona hiyo ndiyo itakuwa dawa nzuri ya kumrudisha kimawazo duniani. Alikuwa keshapanga safari nyingine ili kuweza kumsaidia zaidi shemeji yake, safari ya kwenda tena kwenye mbuga za wanyama. Na safari hii alikuwa kaipanga kuigharamia mwenyewe…na wakati.

Unajua Maua mimi na mhuja ni kama mtu na ndugu yake, ingawaje yeye anatokea milimani mimi natokea Pwani, lakini tulikuwa kama wanandugu waliozaliwa tumbo moja, nilimjali sana kama alivyonijali mimi, ndio maana hata akisafiri hana wasiwasi na mimi. Kuondoka kwake ni pigo kwangu pia mimi, kwani mambo yangu mengi yanakwama, alikuwa msaada mkubwa sana kihali na kimawazo, na nilimuahidi kuwa familia yake ni yangu, ingawaje mimi nimechelewa kuoa, lakini tulikuwa tukisema kuwa watoto wake ni wangu…na mke wake…aaaah’ malizia basi shemeji’ akasema Maneno kwa utani

‘Hiyo siwezi kumalizia, kuwa mke wake ni mke wako…haiji hata kama ni ndugu, hata kama ni mrafiki hiyo haiji, mke wake ni shemeji yako…hapo imekaa sawa’ akasema Maua.
‘Hapo imekaa sawa, nakubaliana na hilo, ila tuliahidiana kuwa hata kama ni miradi akiwa hayupo mimi naiendeelza, kwahiyo mimi nachukua jukumu hilo la kuendeleza kila kitu alicho kiacaha, ili uwe na amani, ….hilo nakuahidi shemeji, utaishi kwa amani hadi hapo utakapomupata mwenza utakaye mkubali moyoni mwako..’ akasema Maneno huku moyoni akitamani Maua aseme mwenza wangu ninayemkubali hayupo zaidi ya wewe…

‘Unajua Maua mimi ndiye niliyekujua kabla ya Mhuja, na aliniwahi kibahati –bahati…’ akasema Maneno.

‘Ushaanza visa vyako, ulinijuaje hata mimi nisikujue…’ akauliza Maua
‘Mimi nitakukumbusha ilivyokuwa, unakumbuka siku moja kwenye supermaketi moja ambayo ni ya kwanza kufunguliwa pale Kariakoo, uliwahi kudondosha vitu ulivyonunua na ukavunja chupa ya chai…?’ akauliza Maneno, na kumfanya Maua acheke, kwani ilikuwa kitambo sana, na tukio hilo lilimkaa sana kichwani, akasema `Kwanini nisikumbuke tukio kama hilo…’
‘Ni nani yule aliyekusaidi akuokota vifaa vyako na kuviweka kwenye kapu, na ulipojaribu kuichukua ile chupa ukaikata na kipande cha ile chupa ya chai, na akatoa kitambaa chake kukufuta kidole chako..? akauliza Maneno, na hapo akatoa leso ikiwa na doa dogo la damu, kumuonyesha Maua. Na maua kumbukumbu ikamjia lakini hakumbuki kabisa kuwa alikuwa huyu shemeji yake, na ndipo Maneno akaanza kumhadithia jinsi alivyomjua.

***
‘Maneno mwenetu sasa umeshakua lakini unatupa wasiwasi sana, wadogo zako wote wameshaoa, lakini wewe siui ndio huo usomi wako, hutaki hata kutuletea mwanamke wa kudanganyia, una nini mwanetu..’ akamuulizia mjomba wake.

‘Mjomba mbona leo unanigeuka, ulishatuambia kuwa uhuni ni mbaya, hasa uzinzi, na ulituasa kuwa hutaki katika familia yetu watu wapate watoto bila ndoa, na mimi nafuata masharti yako, nataka nioe kihalali na wewe uwe mhusika mkuu…hilo ndio lengo langu, lakini sijampata nimtakaye…’ akasema Maneno huku akimkumbuka binti mmoja ambaye anamuona mara kwa mara akiwa anatoka kazini, binti huyu anaonekana anasoma, lakini sio shule za sekondari, huenda anasomea kozi fulani.
Akawa anmfuatilia kwa karibu sana, hadi akagundua kuwa ni mtoto mwenye adabu sana, licha uzuri aliojaliwa nao, lakini kiliongezeka kitu kingine kikubwa cha heshima na adabu. Aliahidi kuwa huyo ndiye anayemfaa kuwa mke wake... Akamwambia shangazi yake ajaribu kumsaidia kwa kumchunguza kwa makini, lakini alimuomba sana asije akamwambia kuwa analengo gani, kwani kama watagundua badaye kuwa hafai wasije wakamuumiza kiakili.

Kweli shangazi yake alifanya kazi hiyo, lakini kabla hajaimaliza akapata safari ya kwenda mikoani, kwahiyo hilo zoezi likasimamishwa kwa muda. Lakini yeye mwenyewe hakuchoka kumfuatilia, ila cha ajabu kila mara anapotaka kukutana naye angalau kumsalimia anakutana na kikwazo fulani, moyoni akasema hana haraka sana naye, siku itafika tu kama anamfaa atahakikisha anampata kuwa mkewe…hakupenda kufanya makosa kwa kumpata mtu wa maisha yake.

Shangazi yake akarudi, na akapewa maagizo kuwa sasa anaweza kumuunganishia maana , muda wa Maneno ni mdogo sana, na kila anapopata muda kama huo, anakuwa hafanikiwi, kinazuka kikwazo fulani, kwahiyo akamuomba shangazi yake ahakikishe anakutana naye, na ipangwe siku waonane na Maneno…`shangazi mimi kama nilivyowaahidi nitafuta mila na desturi zenu moja baada ya jingine,sitapeleka mambo kisasa-sasa…’ akamwambia shangazi yake.

Shangazi yake alipofika kwa huyo binti alikuta sura mpya, akauliza hakupata jibu la kumfurahisha, wanasema huyo mtu alikuwa mpangaji, na ameondoka, na hakuna anayejua kahamia wapi…ikabidi arudi kumfahamisha Maneno, na Maneno hakuamini akaenda mwenyewe na kupata jibu hilohilo,akauliza kila mtu anayeishi kwenye nyumba hiyo, lakini hakuna aliyeweza kujua wapi alipohamia, ikawa pigo kwa Maneno. Shangazii yake akamwambia kuwa asijali, inawezekana hakuwa bahati yako,tutapata mwingine bora zaidi yake. Lakini kwa Maneno ikawa haiwezekani, hakuona anayefanana naye, hakuna ambaye atachukua nfasi hiyo.

Na siku moja Maneno akiwa anapita kwenye supermarket moja hapo Kariakoo, akiwa na nia ya kununua baadhi ya vifaa,na akiwa kasimama kwenye fremu moja iliyopangwa vitu , akavutiwa na sura ya amsichana aliyesimama upande wa pili wa hiyo fremu, sio kuvutiwa tu, ila moyo wake ulishikwa na mshituko, oooh, sio yule binti kweli…sio Maua kweli, kwani alikuwa keshamjua hata jina lake. Akaacha kuchagua vitu na kuanza kumfuatilia nyuma huyo binti, ili apate nafasi ya kumuongelesha, na huku akisema kimoyomoyo, kama ndio yeye, basi leo kitaeleweka, lazima aongee naye na ajue wapi walipohamia, ili kila akipata nafasi amtembelee, na aliomba sana awe hana mtu aliyemuwahi. `Lakini binti mzuri kama huyu sidhani kama hajawahiwa…hata kama kawahiwa, ujanja ni kupata sio kuwahi..…

Wakati anamfuatilia mara yule binti kwa bahati mbaya akawa kama kajikwaa akiwa kabeba kapu la vifaa alivyokuwa kanunua, siunajua tena viatu alivyokuwa kavaa huyu binti vilikuwa na visigino virefu vilivyo, ukikosea unaweza ukaaumbuka, basi yule binti akajikuta analiachia lile kapu kujihami, na kumbe kwenye lile kapu kulikua na chupa ya chai, iakw aya kwanza kutoka na ikawa imechomoka kwenye boksi lake ambali lilikuwa hakijafungwa vyema na kudondokea sakafuni,…yule binti kwa kiwewe akaifunua ile chupa harakaharaka kuikagua kuwa ipo nzima na wakati anaitingisha tingiosha vichupa vilivyokuwep ndani vikamwangika, sakafuni, na sijui ni kwasababu ya uwoga,akawa anavizoa kwa mkono ili kuvirudidhia kwenye ile chupa, ingawaje ilikuwa ni ajali tu..

Maneno alishafika karibu yake, yeye akakimbilia kuokota vitu vingine na kuvirudiha kwenye lile kapu, na alipogeuka akamuona Maua kashika kidole kinavuja damu, harakaharaka akatia leso yake na kukifunga kile kidole,ili damu isivuje, na wakti huo wahudumu walishafika kutoa msaada.
‘Vipi umeumia binti, pole sana, ni ajali tu usiwe na wasi wasi tutaangali atutakavyosaidiana , hebu tuone kama umeumia tukakupake dawa…’wakasema wale wahudumu na mara akaja mama mmoja ambaye alionekana ni shangazi wa Maua kujua nini kimetokea na walipojielezea, wakachukuana na kuelekea sehemu ya malipo, na Maneno akawa nafuatilia nyuma, wakati huo kesharudishiwa kitambaa chake, na kila akitafuta upenyo aongee na hiyo huyo binti akawa haipati kwani shangazi yake alikuwa naye sawia.

Na mara Maneno akasikia naitwa kwa nyuma alipgeuka akakuta ni rafiki yake Mhuja, akampungia mkono kuwa anakuja, halafu akageuka kumwangalia ndege wake wa fahari, lakini alijikuta anaangaliana namhudum wa pale sokoni. Akatizama huku na kule hakumuona Maua wala shangazi yake, ikalaani bahati yake hiyo maana haui wapi wanaishi sasa na hakupata hata nafasi ya kuongea naye , kwahiyo ikawa umetoka tena.

‘Duuh, nina bahati mbaya sana ….aah, ndege wangu mrembo kaondoka…’ akajikuta akilaani na rafiki yak akaja na wakaondoka, hakusema lolote, na wala hakumuhadithia rafiki yake Mhuja, kwani hilo swala alitaka liwe siri na aje kumshitukizia rafiki yake huyo.

‘Vipi mbaona upo hivyo, unaonekana huna raha, kuna nini kimetokea?’ akamuuliza Mhuja.
‘Hakuna kitu,kuna ndege nilikuwa namfuatilia, ili ikiwezekana nimweke kwenye kiota changu , lakini karuka….yaani siju nitamata wapi maana msitu ni mnene ajabu…’ akasema Maneno.
‘Wewe na mfumbo yako ya Pwani bwana hata sikuelewi, ndege , au mtu…kama ni ndege mtu wapo wengi, utapata mwingine, ipo siku, na …hili liwe shindano, ni nani atawahi kuoa, ukishinda wewe nitakupa zawadi na nikishinda mimi utanipa zawadi. Sijui tupange zawadi gani..?

‘Zawadi ni zawadi tu, haina haja ya kupanga, mimi naahidi nitakupa bonge la zawadi…’ akasema Maneno akijua kuwa ipo siku atampata huyo binti, na atakuwa kamshinda rafiki yake. Na siku zikaenda hakuwahi kabisa kukutana na huyo binti,alitafuta Dar nzima, kila kona, lakini hakumuoma Maua na wala familia yao, inakuwa kama vile walikuja mara moja na kurudi huko mbali kusikojulikana, na hata pale walipokuwa wamepanga awali walidai kuwa hawajui hawo wapangaji walihamia wapi. Maneno akakata tamaa, na ikawa malengo kumtafuat mtu mwingine, lakini kila aliyempata ikawa analinganisha na mrembo huyo aliyeyeyuka, anakuta hamfai. Masiku na mwaka ukakatika.

Siku moja Maneno akiwa karudi toka safari za mikoani, rafiki yake alimjia na kumpa taarifa kuwa keshapata mtu anayetaka kumtambulisha kama mchumba…! Maneno akaruka kwa furaha na kusherehekea utafikiri mchumba huyo ni wa kwake yeye. Akamuuliza Mhuja `Ni yule yule msichana uliyesema mlikutana naye kituo cha basi, uliyemuokotea kitabu chake cha kumbukumbu…?’
‘Ndiye huyo, tatizo lako kila nikikualika uje tukamuona, unakuwa hukamatiki, lakini nilifanya utafiti wa kina na sina wasiwasi naye, hata wewe mwenyewe ukibahatika kumuona, utanisifia…nakuhakikishia hilo…sasa kwa ujumla nimeshalifikisha kwa wazazi na wao wamelipokea kwa mikono miwili, iliyobakia ni taratibu za kawaida, …’

‘Safi sana rafiki yangu, ina maana sasa umeniwahi, kwahiyo utanidai zawadi, au sio, lakini usihakikishe moja kwa moja, naweza nikampata wangu chapu chapu nikakufunga mabao…huwezi jua’ akasema Maneno.

‘Yote ni heri, kiukweli umri wetu ni wa kuoa, haihitaji kuchelewa zaidi, tatizo linakuwa ni nani anayefaa, kwani wakuoa wapo wengi, lakini swali kubwa ni nani atayekubalika moyoni, ni nani mke mwema, …’ akasema Mhuja.

‘Kama ilivyo kwa wanawake kuiuliza je ni nani mume mwema….ni kazi kubwa hiyo…’ akasema Maneno, na kuongezea kusema `Kwakeli rafiki yangu nimefurahi sana kusikia habari hii..unajua ssiku ile uliponielezea, wakati nina mafikara ya ule mzigo uliopotea, nilikuwa sikuelewi, maana mimi pale nilijua kazi sasa basi, kwahiyo nilikuitikia tu, kumbe mambo yameiva, sawa, tutakuwa pamoja, …hata ikibidi kuomba ruhusa, ingawaje nafasi hii niliyo nayo sitaki kuichezea, siunajua tena safari ndio inatufanya tusihi hapa mjini, mshahara mdogo, lakini ukipata marupurupu ya safari ukayabanabana unafany ajambo la maendeleo..’ akasema Maneno.

‘Ni kweli, mimi na familia yangu tumejipanga vyema, hutaamini kuwa hatukuhitaji hata michango ya watu, hilo swala lilipofika kwa wazee, huyu kaahidi ng’ombe, yule mbuzi, yule mchele, ….yaani mwisho wa siku kila kitu kimekamilika,…tukaona haina haja ya kuitisha vikao, kuwasumbua watu, cha muhimu ni kuwapa kadi za mualiko tu…kwahiyo siku ikifika utapata kadi yako , maana sasa tunachofanya ni zile taratibu za awali, kuna kupeleka barua, …’ akasema Mhuja kwa furaha.
‘Mhuja wewe tumetoka mbali, shule na sasa tupo kazini sehemu moja, na siwezi kukutupa kwa hiko, mimi nitakupa mchango wangu kwa ajili ya maandalizi yako binafsi, na ….usfikiri nimesahau ile ilikuwa ahadi ya kweli, kuwa atakayewahi kuoa,lazima apewe zawadi,…lakini zawadi hiyo nitakupa baada ya ndoa, maana mimi badi nafukuzia, naweza nikakuwahi…’ akasema Maneno akimuwaza yule binti aliyemuona ambaye sasa kayeyuka kama barafu, lakini bado alikuwa na matumaini labda ipo siku atakutana naye tu.

Basi wakaachana na siku moja wakawa wapo pamoja tena, Maneno siku hiyo alikuwa kapumzika nyumbani kwake na kama walivyo kawaida yao, siku Maneno yupo nyumbani hana safari wanajikuta wapo pamoja kama mapacha, wakijadili hili na lile, walishazoeana tangu wakiwa shuleni, wakawa wote chuoni, na sasa wamejaliwa kufanya kazi sehemu moja,…na siku hiyo Mhuja alikuwa na jambo zito la kumwambia mwenzake;

‘Maneno naona leo upo huna safari za kikazi maana tangu nikuambie nimepata mchumba, umekuwa mtu wa safari kiasi kwamba, hata siku moja sijawahi kukutambulisha kwa huyo mchumba wangu, na sijui kama utamjuaje na wewe miguu yako haitulii. Unajua sikutaraji aitakuwa hivyo, wewe ni zaidi ya ndugu yangu, lakini hili swala langu limkuwa la kivyangu na familia yangu, inakuwa kama nimekutenga, sasa leo nataka ushiriki kwenye safari ya kupeleka barua…, leo hata kama ipo safari itaahirishwa tu…’ akasema Mhuja.

‘Kiukweli, Ipo safari, lakini sio mapema sana,…siunakumbuka kipindi hiki mizigo mingi sana,…bishara yetu imekubali, siunaona mwenyewe kwenye mahesabu huko…na safari hii wasiponipa bonsai, tutaelewana vibaya…. Unajua wakati mwingine nawaonea wivu nyie wahasibu, nyie muda mwingi mpo ofisini, na mnasafiri mara moja moja sio kama sisi, lakini najua hivi karibuni utaanza kusafiri, maana wewe utahusika kwenye ufunguzi wa matawi mapya huko Bukoba na Mwanza, kwenda kuwasimika wahasibu wa kanda za ziwa…’ akaongea huku bado akiwaza mengi akilini, lakini kwa vile yeye ni mtu wa maneno mengi, alijifanya hana kitu moyoni, akasema tena ‘Mimi ni mtu wa masoko na mauzo, na unajua masoko na wateja vitu hivyo katika ofisi yetu havipatikani kwa kukaa ofisini kama nyie wahasibu, …lakini tupo pamoja ndugu yangu, usijali sana, hata mimi inaniuma sana, ila leo nitawasindikiza watu wanaopeleka barua,ili angalau nimuone huyo mrembo wetu, ulisema jina lake nani vile..

‘Anaitwa Maua..’ akasema Mhuja

‘Wee,…mamama… unasema anaitwa nani, …?’ akauliza kwa mshangao, halafu akaficha ule mshangao wake akasema kwa utulivu `Umesema anaitwa Maua, ooooh, jina zuri, lakini mbona imetokea sawa na mtu ninayemfahamu…isije ikawa ndio huyo mtu ninayemfahamu, lakini yeye alishahama hili jiji..anaishi wapi sijui, kwani huyo Maua wanaishi wapi na familia yao…?’akauliza Maneno na kabla hajajibiwa wakafika watu wa msafara wa kwenda kwa binti, mchumba wa Mhuja. Hawakupata nafasi ya kuongea tena, maana walikuwepo wageni maalumu na muda ulikuwa mchache, na msafara wa kupeleka barua ukaondoka, bila ya Mhuja.

Wakafikisha ile barua, na waliwakuta wanaume tu, wakauliza vipi mbona hakuna wanawake, wakaambiwa wanawake hawakubahatika kuwepo kwasababu kuna shughuli nyingine ya kifamilia na wao kama wahusika wakuu walitakiwa kuondoka, lakini kwa sababau ya hiyo barua waliona wagawane majukumu, ila wao baada ya hilo tukio wataondoka kueleeka huko kwenye hiyo shughuli. Waliendelea kusema kuwa kwasababu ni barua tu, itapokelewa, na siku nyingine wataikuta familia nzima na watapata nfasi ya kumjua kila mtu muhimu kwenye familia. Na baadaye Maneno akaondoka kuwahi safari ya kikazi hakurudi haraka, na aliporudi safari yake hiyo alikuta mambo mengi yamekamilika, na siku ya harusi imeshafikia, kwani harusi hiyo haikutakiwa kuchelewesha kwa makubaliano ya familia hizo mbili.

Siku ya harusi ikafika na hapo walikuwepo wanafamilia wote, ndugu jamaa, na majirani, akiwemo Maneno, ambaye alikuwa mmoja wa wapambe, hakuwa mpambe mkuu, kutokana na majukumu yake, alikuwa msaidizi wa `mpambe mkuu wa bwana harusi’ kama itakuwa nilazima, lakini muda wote akili ya Maneno ilikuwa ukiwaza mengi kumjua huyo Maua. Alikuwa akijiuliza, ni yuleyule Maua anayemjua yeye au ni majina tu yanafana, na kila mara alijipa moyo kwa kusema kimoyomoyo kuwa sio yeye, mbona hajabahatika kumuona angalau yule shangazi yake anayemfahamu kwa sura akiwemo kwenye hizo pilika pilika. Mbona hakuna hata sura anayoifahamu, aliyowahi kuiona siku alizokuwa akimfuatilia huyo Maua, ina maana kweli chelewachelewa imemkuta mwana sio wa kwake tena…haiwezekani

‘Kama atakuwa yeye sijui nitachukua hatua gani, nashindwa hata kuelezea,…’ Akawaza huku akikuna kuna kichwa, halafu akaendelea kuwaza kwa kusema ’ Kama atakuwa ni yeye kwakweli nitateseka sana, lakini hata hivyo siwezi kumweleza rafiki yangu lolote, maana namjali sana rafiki yangu, nitajifanya sijui lolote…’ akajisemea moyoni. Huku akiwa anawaangalia watu walivyo na shauku ya harusi hiyo, huku akiwazia kuwa anatamani ingelikuwa ni yeye `mtarajiwa’ na hapo anasubiri kukutaa na Maua anayemfahamu…’Lakini kila kitu na wakati wake, najua Maua wangu yupo ananisubiri, atakuwa sio yeye bwana…’ akajipa moyo.

Ikawa ndio kila mtu anajiandaa kueleeka huko kwenye harusi na mara simu ikaja kuwa Maneno anahitajika haraka kwenda ofisini kuna mzigo umefika na yeye anatakiwa kwenda kuukagua,karibu apasuke kwa hasira, lakini hakuwa na jinsi kwani kazi ya watu ni dhamana kubwa,ikabidi amwelezee rafiki yake kuwa imetokea hiyo dharura, na kwa vile rafiki yake anajua , akamwambia asijali aende akawajibika, kama atamaliza haraka asiache kufika, alimwambia hata ukimaliza usiku wewe njoo tu, wakaishia kucheka, na kuagana kwa kupeana kila-laheri kwa shughuli njema. Akaondoka akiwaacha wenzake wakimwaga kwenye magari kuondoka, na bahati mbaya hakuweza kurudi kabisa kuhudhuria hiyo harusi. Na kesho yake akasafiri kwani mzigo uliofika ulikuwa na kasoro, kwahiyo yeye kama mhusika mkuu alitakiwa kwenda kufuatilia kwanini imekuwa hivyo. Alirudi baada ya siku tatu…

Maneno alimpigia simu rafiki yake kumpa hongera na kumuomba amsamehe kwa kutokuwepo kwenye harusi, ingawaje wote walijua kuwa ni sababau ya majukumu ya kikazi kwani wote wanafanya kazi kwenye kampuni moja, na kila mmoja anajua nini kinachoendelea, kwahiyo wasingeliweza kulaumiana, hata siku nyingine Mhuja humuonea sana huruma rafiki yake jinsi gani anavyopigika kwenye kazi, kwani katika nafasi yake ya kazi anakuwa hana ratiba yak wake binafsi, inaweza ikavunjwa wakati wowote, anaweza kuitwa hata usiku wa manane kama kuna mzigo ulioingia usiku huo. Rafiki yake huyo akamwambia anakuja mara moja kumuona shemeji yake…na kimoyomoyo akawa anasema `na kutoa ile zawadi niliyokuahidi.

‘Hata kama mpo fungate, mimi lazima nimuone shemeji yangu…’ akasema Maneno
‘Wewe ndio mimi, usijali, njoo haraka, tunakusubiri, kwani kama kuna mtu nilyemsimulia kuwa kukosekaa kwakwe kwenye harusi yetu ni pengo kubwa sana ni wewe…sijui kwanini imetokea hivyo, lakini yote ni heri, hatuwezi kulazimisha kile kisichowezekana….njoo haraka maana tulikuwa tunatoka mara moja, lakini tutakusubiri…’ na baada ya muda Maneno akawasili. Alipofika alimkuta Mhuja yupo varandani anaangalia runinga, binti harusi alikuwa ndani, na Maneno akawa kasimama mlangoni huku anatabasamu, alikuwa akitabasamu kwani anajua anadaiwa zawadi, na zawadi ilikuwa `surprise’…ya kushutukizia.

‘Kwanza nimuone shemeji….’ Akanong’ona Maneno
‘Kwanza naitaka zawadi uliyoahidi…’ akasema Mhuja kwa sauti ile ya kung’ona...

Oooh, sijui kipi kitatangulia na nini kiliajiri tuwepo karibuni

NB:Samahani kwa kuadimika kwa siku mbili, ni mambo yaliyokuwa nje ya uwezo wangu, lakini tupo pamoja, na nilipata bahati ya kuhojiwa na Blog ya Tanzania Blog awards, kama unataka kunijua vyema, basi tembelea hapo usome; http://www.tanzanianblogawards.com/2011/08/mwanablogger-wa-week-hii-emu-three.html



Ni mimi: emu-three

7 comments :

Anonymous said...

Hadi raha ndani ya moyo, hivi nikuulize unwazaje hadi iwe hivo...i love u very much

Pam said...

najaribu kuwaza kwa sauti Sweet wa kwa Dr ndo mume wa Maua utanisahihisha M3 kama cko kwenye wazo sahihi... Maneno anataka kula vya rafiki yake huku akitumia mbinu ya kufariji, iko vzr haya tusubiri Maua ataingia kwenye tundu la faraja??

Rachel Siwa said...

Ndugu wamimi wewe ni kiboko, Hongera sana kwa kazi hii,ngoja nikuswalike swali kidogo,ni muda gani uwa unaandika hii kitu ni asubuhi,mchana au usiku wenzio wakilala wewe ndio unapata wakati mzuri wa kuandika? Hiki ni kipaji ndugu yangu si chakuwinda na manati. Natamani nikuone punga hata mkono mwanakwetu.Kila la kheri ndugu yangu, Pamaja!!!ngoja nizame huko kwa mahojiano.

Precious said...

Thanks nimefarijika leo but pole kwa majukumu M3 maana kila baada ya 30mnts nilikuwa nachungulia bado nakutana na episode 18 nikawa naugua mwenyewe.......by the way nimesoma mahojiano yako kule tanzaniablogsaward big up kwa maelezo yako ingawa me natamani kukufahamu zaidi kwa sura.

Pam said...

nami nilizama kwenye mahojiano itakuwa njema ukitualika mashabiki wako idd hii ili tukuone mana mpaka uje uweke picha yako hapa itachukuwa muda mrefu... joke!!

emu-three said...

Pam na Anyn. Msipungue uzito mambo bado yanakuja, tuendelee kuwemo, mambo ndio bado kabisa. Na nddugu yangu wa Swahili na waswahili, tupo pamoja, na ama kwa jibu la swali lako ni kuwa naandika hivi visa wakaati gani , jibu ni kuwa naandika asubuhi sana kabla ya kazi. Ninachofanya ni kuamuka asubuhi sana, kiasi cha saa 11 kasorobo alifajiri , ili niwahi usafiri , na inabidi tufanye hivyo maeneo tunayosihi , kwasababu ya usafiri na foleni, kwahiyo kwa muda huo nitafika kazini saa moja kasoro, saa moja na robo, nikifika hapo kama nimefika mapema, basi naanza kuandika, mapaka saaa mbili na nusu nakuwa nimemaliza, na natumia muda mchache kupitia pitia.
Wakati mwingine naazima laptop ya kazini naaondoka nayo nyumbani, huko naandika kwenye Macrosoft word, na nikifik akesho yake naipiti akidogo halafu naiingiza kwenye blog kwa kucopy and paste…na wakati mwingine nakwenda internet café, naandika moja kwa moja kwenye blog. Na hata hapa ofisini kuna muda naandika moja kwa moja kwenye blog, lakini hii unakuta ina makosa mengi, ambayo sikupata muda wa kuyapitia ninachofanya nikuandiak kwenye Macrosofy words, ili nipate muda mzuri wa kupitia pitia. Kwa sura moja ambayo naibandika kila siku natumia muda mchache sana kuiandika, …
Precious , tupo pamoja, kama ulivyo wewe, natumai hilo siyo jina lako kamili, name navutika zaidi kukuona moa kwa moja na kujua kwanini umejiita hilo jina..lakini kama unahamu kiasi hicho basi wewe ingia nyuma ya pazia ukitumia Skype, kwa kutafuta jina `emu-three’ basitutwasiliana live …unasemaje?
Kama alivyosema Pam, KWA MOYO MKUNJUFU NAWAALIKA SANA KWENYE IDD, TUOMBE MOLA ATUPE UZIMA,NATAMANI KAMA NINGEKUWA NA LAPTOP YENYE INTERNET,, NIKAWAUNGANISHA MOJA KWA MOJA. I LOVE YOU ALL,

Yasinta Ngonyani said...

Hakika umebarikiwa kipaji..na naamini siku moja utakuwa mkubwa sana kwa uandishi. Kweli kupenda ni kitu cha ajabu sana... Haya sasa hapo kazi ipo tunataka kuja na kuona hata kamkono..ha ha ha kaazi kwelikweli...pamoja daima